Ibilisi alisema kwa kumwambia Allah subhanahu wataala: "Nina apa kwa utukufu wako na kwa nguvu zako nitaendelea kuwapotosha waja wako kwa kadri roho zao bado zimo kwenye kiwiliwili chao (kwa maana; maadamu bado wapo hai nitaendelea kuwapotosha na hutapata wenye kukushukuru wewe)".
Akasema Allah rabbul izza: Nina apa kwa utukufu wangu na kwa nguvu zangu, nitaendelea kuwasamehe (waja wangu) mradi tu wataniomba msamaha wangu.
-------------------
Kuna nyakati huwa zinamfika binaadamu na kumsahau Allah. Katika kumsahau Mola wake binadamu huwa anafanya madhambi na wakati mwengine huwa anafikia kufanya kufru. Unapofika wakati anataka kurudi kwa Allah huwa anajihisi haya kwa madhambi aliyoyafanya. Anajiona haya hata kutaja jina la Mola wake.
Hakika ya Allah yeye alishasema: "Yeye ni arrahmani arrahiim". Yeye ni mwingi wa rehema mwenye kurehemu. Ni mwenye kusamehe na kwake hilo lipo.
Mmoja katika watu alifika kwenye Kaaba na akisema; Ya Allah nimekukosea mimi, lakini naona aibu kukuelekea wewe kwa dhambi nilizofanya. Lakini ni nani nitakayemuomba zaidi ya wewe? Ninataka msamaha kutoka kwako ewe Mola wangu.
Mmoja katika watu qaumu ya Nabii Musa Alayhi ssalaam alikuwa ni mwenye kuabudu sanamu. Katika ibada zake alikuwa ni mwenye kusema; Ewe sanamu niponye, ewe sanamu niruzuku mimi, ewe sanamu nisamehe.
Siku hiyo ulimi wake uliteleza katika kufanya ibada yake. Alupotaka kutamka ya swanamu ukatamka ya Swamad, Allah subhanahu wataala akajibu kwa kuitikia "labbayka yaa abdi" (nipo hapa ewe mje mja wangu).
Nabii Musa Alayhi ssalaam akasema; "Ewe Mola wangu! Unajibu kwa kumwitikia wito wake wakati huyo mtu anaabudu usiyekuwa wewe?" Allah subhanahu wataala akamjibu akamwambia "Ewe Musa! Kuna Asswamad (tegemeo wa kila kitu ambaye hategemei chochote) mwengine zaidi yangu?"
Hivyo, tusikate tamaa kumuomba Allah msamaha. Allah ni mwenye huruma sana, tena sana. Halikadhalika, tusiwakatishe tamaa watu ambao wanataka kurudi kwa Allah subhanahu wataala.