Naomba tuisomeni hii makala kwa umakini kisha tuangalie ni jinsio gani tutavyoweza kunufaika na mchango wa mtaalamu huyu.
Na Maura Mwingira
WAKATI wowote unapotekeleza mipango yako ya kuwasaidia wananchi wanyonge na maskini, usihesabu wangapi umeshawafikia, bali ni wangapi hujawafikia.
Kisha, jiwekee malengo, mwezi huu unataka uwafikie wangapi, miezi sita ijayo wangapi na miaka mitatu ijayo wangapi. Utaratibu huu ndio utakaowezesha kufanikisha yale unayotaka kuyafanya au kuwafanyia watu. Hivi ndivyo tufanyavyo sisi, tunahesabu wangapi hatujawafikia ndio tunaowafanyia kazi.?
Hayo ni maneno ya mwanauchumi maarufu duniani, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel na mwanzilishi wa Benki ya Watu Maskini maarufu, Grammen Bank, Profesa Yunus Mohammed, alipokutana na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam takriban wiki tatu zilizopita.
Mwanauchumi huyo aliyekuwa nchini kwa mwaliko wa Rais Kikwete aliweza pia kufichua mambo mengi yanayohusiana na uwezeshaji wa watu maskini.
Akizungumza kwa taratibu na kwa lugha fasaha ambayo haikuhitaji mtu aliyekuwa akimsikiliza, kuwa msomi au mtaalam wa fani ya uchumi, ilikuwa rahisi kutambua kile ambacho msomi huyo alikuwa akitaka kukisema.
Profesa Yunus, kwa alitumia mifano ya wazi na inayohusu maisha ya kila siku ya mwanadamu. Kwa tafakuri ya haraka, ilikuwa rahisi kutambua kwamba lugha ile nyepesi na iliyoeleweka kwa urahisi ya msomi huyo ndiyo iliyomwezesha kuwasiliana na watu na kufanya kile alichofanya na anachoendelea kukifanya.
Nilipopata taarifa za kuwasili kwa mchumi huyu nchini, nilijawa na mshawasha hasa wa kutaka kumwona, kwa kuwa nimekuwa nikimsoma kwenye vitabu au vyombo vya habari.
Binafsi, nilikuwa mmoja wa Watanzania waliotaka na hatimaye kubahatika kumwona msomi huyo ambaye ametokea kuheshimiwa na wakubwa wa mataifa yote tajiri na maskini, hasa kwa uwezo wake kuwafanya mamia ya watu maskini nchini Bangladesh na hasa wanawake kuondokana na umaskini.
Siku ya siku ilipofika, mchumi huyo aliwasili katika Ikulu, kwa hakika nilishikwa na butwaa kidogo, kwani picha niliyokuwa nayo kichwani mwangu haikuwa ya yule aliyekuwa ameketi mbele yangu.
Nilikuwa na picha ya mtu ambaye kutokana na umaarufu wake angekuwa amevalia suti ya bei mbaya, mkoba wa nguvu na wapambe kadhaa.
Kumbe wapi, aliyekuwa ameketi mbele yangu akimsubiri mwenyeji wake (Rais) alikuwa mtu rahisi kabisa, hakuwa amevaa suti, bali vazi lake maridadi la asili ya kwao, Bangladesh .
Hakuwa na mkoba wa bei mbaya wala wapambe kibao, ila alisindikizwa na watu wawili tu ambao baadaye waligundulika kuwa walikuwa wenyeji wake hapa Tanzania.
Nje ya urahisi huo, Profesa Yunus alikuwa nchini kwa lengo la kubadilishana mawazo na mwenyeji wake, Rais Kikwete, kuhusu kitu gani ambacho anadhani na kwa uzoefu wake, Tanzania ingeweza kufanya ili kuharakisha mchakato wa kuwapunguzia ugumu wa maisha watu wake walio wengi, hususan wale wanaoishi katika maisha ya umaskini ili waweze kuondokana na hali hiyo.
Katika mazungumzo yao, profesa huyo alimweleza Rais Kikwete kwamba, katika nchi anakotoka, kiwango cha umaskini ni cha kutisha na idadi ya watu maskini ni kubwa mno ikilinganishwa na Tanzania.
Akasema kuwa amepata taarifa ya idadi ya watu maskini katika Tanzania, kuwa ni asilimia 39, sawa na kama familia milioni 2.5.
Akaeleza kuwa familia hizo ni chache mno ikilinganishwa na kwao, Bangladesh.
"Hawa mnaweza kabisa kuwaondoa katika umaskini, labda tatizo lenu ni kwamba familia hizi zimetawanyika sana kwa kuwa nchi yenu ni kubwa ambayo Bangladesh inaweza kuingia mara sita.
Kwa tathmini yangu, ninyi katika Tanzania mnayo kazi ndogo sana ya kuwaondoa watu wenu katika umaskini kwa sababu, kwanza idadi ya watu maskini mliyo nayo ni ndogo sana ikilinganishwa na kule ninakotoka."
Katika ushauri wake, profesa huyu akaeleza kuwa tofauti na ilivyo Bangladesh, Tanzania inazo rasilimali nyingi, watu wenye kujituma, serikali madhubuti kinachotakiwa ni kuongeza ubunifu kidogo tu, basi!
"Familia milioni 2.5 ni idadi ndogo sana, mnaweza kuwafikia hawa, ni kweli kwamba wamesambaa nchi nzima, lakini mnaweza, ndiyo inawezekana, kinachotakiwa ni uamuzi tu."
Akasisitiza kuwa licha ya kwamba Tanzania inazo rasilimali nyingi, kuwapo kwa fursa za mikopo nafuu kwa watu wa kawaida, ndio hasa kutakakoweza kuongeza chachu ya watu kuondokana na umaskini.
Anasema benki nchini lazima ziondokane na ile dhana kwamba watu maskini hawalipi... "Sisi tumedhihirisha kuwa watu maskini au wa kipato cha chini wanalipa mikopo. Katika benki yetu ulipaji wa mikopo ni asilimia 98 na tunakusudia kufikia asilimia 100, na nina hakika tutafika huko tunakotaka."
Anatoa mfano kwamba yeye na wenzake walipoamua kuanzisha Grameen Bank, wala hawakuanza na mtaji mkubwa.
Anaeleza kuwa walianza na mtaji mdogo lakini leo hii benki yake inao mtaji mkubwa, ambao unatokana na amana za hao maskini ambao mabenki ya biashara yanasema hawalipi.
"Wanachohitaji watu hawa maskini, wala si kiasi kikubwa cha fedha, ni mkopo mdogo tu wenye masharti nafuu sana au usio na masharti, ili waweze kuongeza tija katika kazi zao ambazo wamekuwa wakizifanya siku zote," anaeleza na kuongeza:
"?Mama anayefuma kikapu kimoja na kukiuza, anahitaji nyongeza ya fedha katika mtaji wake mdogo ili afume vikapu 10 badala ya kimoja cha awali, aviuze na kujipatia kipato, ndicho anachohitaji mtu maskini, nafasi na fursa kujipatia mkopo."
Profesa huyo akamweleza Rais Kikwete kwamba, kila mtu ni mjasiriamali hata yule ombaomba wa mitaani, tofauti iliyopo ni kwamba watu wengine walipata mapema fursa za kuwa kama walivyo (wajasiriamali) na wengine hawakupata fursa hiyo.
Licha ya wanawake wale maskini wa Bangladesh kuwezeshwa kwa mitaji na hivyo kuongeza kiwango cha uzalishaji wa bidhaa zao, lakini pia anasema profesa huyo kwamba hali ya maisha ya wanawake hao na familia yao imebadilika na kubwa bora zaidi.
"Wale wanawake ambao tuliwatoa kwenye umaskini, leo wana hali bora sana ya maisha, wanazalisha bidhaa zao kwa ufanisi zaidi, wanauza, wanatunza familia zao, watoto wao wamesoma sana kuliko wazazi wao, wana ujuzi wa fani na taaluma mbalimbali.
"Hata ongezeko la watu limepungua kwa sababu sasa akina mama hawa wana shughuli zinazowafanya wajishughulishe na kuwe bize, hawana tena muda wa kupoteza au kufanya kazi ya kuongeza familia."
Kauli hiyo ilimkuna na kumchekesha kila mmoja akiwamo Rais Kikwete.
"Wazazi wao hawajui kusoma wala kuandika, lakini watoto wao, sasa wanapata fursa ya kusoma, na cha kufurahisha zaidi hata umri wa kuishi kwa wanawake umeongezea. Hii yote ni kwa sababu ya uwezeshaji tulioufanya," anaeleza.
Ubunifu huo wa Profesa Yunus wa kuwaondoa wananchi katika umaskini, hauishii kwa wanawake, bali unamfikisha kwenye kundi jingine la kijamii, ombaomba.
"Kama nilivyosema, Rais kila mtu ni mjasiriamali amezaliwa hivyo, kinacho tutofautisha ni kwamba wengine waliipata fursa hiyo mapema na wengine wakachelewa. Hata hao ombaomba wanaweza kuwa wajasiriamali wazuri sana, hilo tumelifanya kwetu na sasa wao ni mfano mzuri.
Anasimulia profesa huyo kwamba waliwakusanya ombaomba kama 100,000 hivi wakakaa nao na kuanza kuwahoji sababu zilizowafanya kuwa katika hali hiyo ya kuombaomba.
"Ombaomba wale kila mmoja alikuwa na simulizi za kusikitisha sana, wapo walioiingia kwenye shughuli ya kuomba kwa sababu ya mazingira wanayoishi. Wengine wanasema kazi hiyo imo ndani ya ukoo wao, alianza babu wa babu akaja baba sasa na yeye na kizazi chake ni kama wameirithi," anasimulia.
Ombaomba hao, Profesa Yunaus anasema kuwa baada ya kuwahoji waliamua kumpatia kila moja wao kitu cha kuuza ili badala ya kwenda kuomba, basi auze na kujipatia fedha yake mwenyewe, tena tukawaelekeza wapite katika nyumba zile zile na kuwauzia wale ambao awali walikuwa wakiomba.
"Huwezi kuamini, kati yao ni 10,000 tu ndio wamebaki wakiendelea na kazi ya kuomba, lakini kati ya hao wako ambao wanafanya biashara ndogo ndogo na wakati mwingine wanakuwa ombaomba. Lakini, wapo wengine ambao wao wameamua kubaki ombaomba kwani ni wataalam wa kazi hiyo na hawapendi kubadilika," anasema.
"Wanaume walipokeaje hatua yako hiyo ya kuwasaidia wanawake maskini, Je, ulipata changamoto gani ningependa kufahamu," akauliza Rais Kikwete."Eehe, Rais haikuwa kazi rahisi, alijibu profesa huyo na kuendelea: "Wanaume, kumbe walichukia, hawakutaka wake zao wawezeshwe, lakini sasa, wanaume wamebadilika sana kwani wamebaini kwamba faida ya uwezeshwaji ule unarudi nyumbani na kuendeleza familia.
Lakini, mwanzoni ilikuwa kazi kweli, sisi kwa upande wetu hatukukata tamaa, tuliamua kuendelea,? anasimulia profesa huyo na kisha kucheka.
Profesa huyo anaongeza kwamba tatizo la wanaume kutopenda wake zao au wanawake kwa ujumla kumiliki kipato chao si la wanaume wa nchi zinazoendelea tu, tatizo hili lipo pia katika nchi zilizoendelea.
Anatoa mfano kwamba alialikwa kwenye mkutano wa nchi tajiri na zenye viwanda, maarufu, G8 uliomalizika hivi karibuni huko Ujerumani.
Anasema kuwa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, katika mazungumzo hayo, alimweleza (Profesa Yunus) kwamba pingamizi alilolipata kutoka kwa wanaume wa Ujerumani, pale alipobainisha mpango mkakati wake wa kuwawezesha wanawake wa nchi hiyo ni kubwa mno.
Akasema kuwa Merkel alipopata uwaziri kwa mara ya kwanza katika miaka ya 1980, na kuanza kuainisha mikakati ya kuwainua kiuchumi wanawake, wanaume wa Ujerumani walikuja juu kweli.
Anamnukuu Kansela Merkel akisema: ? Wanaume wa Ujerumani walifadhaika sana, unajua wanaume wa Kijerumani wanachotaka ni chakula cha moto mezani, ilikuwa kazi sana kubadilisha fikra na mitazamo yao.?
Profesa Yunus alisema anakerwa na kitu kinachoitwa wataalam, akiongeza kwamba wengi wanaoletwa katika nchi au kusimamia mradi fulani, kwa namna moja au nyingine, ni watumiaji wa fedha ambazo zingetakiwa zitumike kuwasaidia watu maskini.
"Utasikia tunakuletea consultants (mshauri) wa nini huyu? Hivi mama huyu ambaye miaka nenda rudi amekuwa akitengeneza vyungu vyake leo unamletea mtaalam, eti amfundishe anamfundisha nini asichojua, huyu mama anachohitaji ni kuongezewa mtaji, kwangu mimi masuala haya ya consultant ni matumizi mabaya ya fedha tu.
Mtaalam huyo anatoa ushauri kwamba, linapofikia suala la kuwasaidia watu maskini, halipaswi kuwa wa serikali peke yake, anasema ni mchakato unaotakiwa kumshirikisha kila mtu na hasa wale walionacho.
Anafafanua kuwa wale walionacho lazima wawe tayari kuchangia huduma za kijamii au kufanya biashara ya kijamii ili serikali itumie nguvu zake katika kuwasaidia wale wasionacho.
"Mnaweza kufanya biashara ya kijamii, hapa ninamaanisha nini? Maana yangu ni kwamba wale wenye uwezo walipie zile huduma muhimu kama vile afya, maji, elimu na nyinginezo. Kwa kufanya hivyo, watasaidia kuipunguzia kazi serikali na hivyo kujielekeza kuwasaidia watu maskini.
Anasisitiza kwamba hili la kuchangia ni lazima lifanyike, wafanyabiashara nao lazima waonyeshe mchango wao, kwa mfano, mtu anaweza kujenga hospitali yake na kuwatoza watu kwa huduma wanayoipata.
Lakini, kwa fedha ile ile wanayotoa watu wenye uwezo, akatoa huduma hiyo hiyo kwa watu wasio na chochote, hapa huyu atakuwa anafanya biashara sawa, lakini upande mwingine atakuwa anamsaidia mtu maskini asife kwa sababu tu hana fedha,? anaeleza mchumi huyo.
Anaongeza kuwa hili likifanyika kwa ufanisi, mfano huu unaweza pia kusambazwa katika maeneo mengine ya nchi.
Rais Kikwete akamweleza: "Afadhali hilo la uchangiaji, umelisema wewe, maana sisi hapa tumeanzisha utaratibu wa watu kuchangia elimu ya juu, lakini hizo kelele tunazopigiwa ni ajabu ya Mungu.
Tunachosema ni kwamba wale walionacho wachangie ili wengine wasionacho waweze kugharamiwa na serikali, lakini wapi watu hawataki kabisa kuelewa. Natamani kauli yako hii ungeisema hadharani.?
Rais Kikwete pia akamweleza mgeni wake kwamba madhumuni hasa ya kumwalika kubadilishana mawazo na kuchota hekima, busara na maarifa yake.
Akasema kwamba serikali yake imeanza taratibu za kuwawezesha wajasiriamali wadogo kwa kuwapatia mikopo ya kuendeshea shughuli zao.
Lakini akasema ingawa serikali yake imeanza hatua hizo, bado anadhani michango kutoka kwa wataalamu mbalimbali kama Profesa Yunus inahitajika ili kuboresha mchakato huo.
Anakubaliana na profesa huyo kwamba mabenki na taasisi nyingine za fedha hazina sababu ya kuogopa kumkopesha mjasiriamali mdogo kwa kuwa wameonyesha uadilifu katika ulipaji wa mikopo hiyo.
Akasema anafarijika kwa kusema angalau hivi sasa kumekuwa na mwamko kidogo kutoka baadhi ya mabenki nchini ambayo yameanza kukiri kwamba watu wa kipato cha chini nao wanalipa mikopo tena kwa wakati.
Profesa Yunus akahitimisha mazungumzo na Rais Kikwete kwa kuahidi kwamba yuko tayari wakati wowote, kufika Tanzania na kushirikiana na serikali ili kuratibu mipango mbalimbali itakayoharakisha mchakato wa kuwaondoa wananchi katika umaskini.
Akasema anashukuru serikali kwa heshima kubwa ya kutambuliwa hasa na Rais Kikwete na serikali kwa ujumla kwamba anaweza kuchangia katika maendeleo ya wananchi wa Tanzania.
*Maura Mwingira ni Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais.
Source : mwananchi