Ramadhan Special Thread
Amemuota Aliyefariki Anayemdai Kuwa Anawambia Atoe Sadaka Pesa Zake
Maswali: Taqwa - Tazkiyyah
SWALI:



ASSALAMU ALYKUM WARAHMATULLAH WABARAKATUH.

Kuna mtu fulani nilimkopa kiasi cha fedha lakini sikumbuki kiwango lakini hazizidi 5000Tsh. Kwa bahati yule mtu amefariki muda mrefu tena ina fika miaka sita au saba kama sikosei lakini lile deni limenikaa kila nikilifikia sijui nilipeke kwao au vipi. Kwa ule wasi wasi nilonao wa deni la watu nilimuota aliyefariki akiniambia kuwa pesa zake nimtolee sadaqa, kutokana na hali hii sasa jee nimtolee sadaka au nizipeleke kwao halafu niwaelezee jinsi nilivyoota naomba ushauri wenu inshallah ili nipate kutoka kwenye khofu hii. Wabillahi tawfiq.



JIBU:





Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.





Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndoto.





Ndoto zipo aina nyingi ambazo mwanaadamu huota kwa sababu moja au nyingine. Zipo ndoto ambazo huwa tunaota kwa sababu ya kulifikiria jambo wakati wa asubuhi au mchana au kitu kukuingia sana rohoni au kutamani kitu. Au pia huletwa na shetani ili kukutia wasiwasi katika mambo yako mengi.



Kwa aliyefariki anayekudai ilikuwa akuelezee hayo kuwa umtolee sadaka kabla ya kuaga dunia au atie katika wasiya wake kabla ya kuaga dunia kwake. Pindi anapokufa huwa mali si yake tena bali ya warithi wake. Hivyo, jambo ambalo unafaa kufanya ni kulipeleka deni hilo unalodaiwa na aliyefariki kwa warithi wake kama vile wazazi wake, au mkewe au watoto. Kama hao tuliowataja pia nao wameaga basi kwa nduguze na wala usiwaelezee ndoto yako.



Na Allaah Anajua zaidi
 
Ameombewa Du’aa Na Majirani Makafiri Wakati Wa Kukata Roho, Je Itaathiri Imani Yake?
Maswali: Taqwa - Tazkiyyah
SWALI:



Assalam Aleikum ndugu waislam, natoa shukrani zangu kwa kazi yenu nzuri mwenyezi mungu atawaji mema.Mimi nina swali linanipa dhiki sana nalo ni hili, mimi nilikuwa nimeolewa na mume wangu wa kwanza ambae alifariki miaka mitatu ya liopita na katika kifo chake kulikuwa hakuna mtu bali ni mimi na yeye hakuwa mgonjwa aliamka na pumu siku hiyo niliona ni pumu zake za kawaida lakini sivo nilivodhani ilikuwa ni mauti,nilipiga kelele jirani yangu tunaishi nyumba moja akatokea na mume wake walipoona ile hali wakaamua kuomba kwa dini yao kwani walijua yuko kwenye sakaratmaut nahawakunijulisha chochote kama mume wangu yuwatuacha ilinimpe maneno mema ingawa nilikua nikisema kwa kelele laillailallah bali haikuwa inavotakikana.Naomba munifamishe ikiwa nilimkosea aliyefariki kutompa shahada na wale jirani ambao siisilamu yale maombi yao yatamtia aliyefariki dhambini.Shukran



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa swali lako kuhusu kubabaika kwako wakati mumeo anakata roho.

Hakika hakuna kitakachomdhuru aliyefariki ikiwa hakupata taathira yoyote ile wakati majirani zako wasiokuwa Waislamu walikuwa wanaomba. Ataathirka tu mbele ya Allaah Aliyetukuka ikiwa mumeo aliweza kuyashika na kutamka yale yaliyokuwa yakisemwa na hao majirani zake.

Sisi kama Waislamu tunatakiwa tuwe makini wakati jamaa zetu wapendwa ni wagonjwa au wanakata roho ili katika utulivu huo tuweze kuwaelekeza.

Tunaomba kuwa shahada uliyokuwa ukiitoa kwa mayowe japokuwa inatakiwa iwe polepole imesibu kumfikia mumeo naye akatamka.



Na Allaah Anajua zaidi
 
Ametubia Baada Ya Kuzini Na Mwanamke Je Kumsaidia Na Mzazi Wake Atakuwa Anaharibu Toba Yake?
Maswali: Taqwa - Tazkiyyah
SWALI



Asalam allaykum,

Ama baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu na kumuombea mema mtume wetu Muhammad salallah allaih wasalam, naomba taaluma juu ya swala hili lifuatalo

Imetokea mtu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi (kuzini) na mwanamke ambaye sio muislam. Mwanamme akaamua kuishi nchi nyengine tafauti ambayo anaishi mwanamke. Mwanamme alishatubu wala hana nia tena ya kurudia uovu huu. Siku kadhaa zimepita, mwanamme amesikia hali ya yule mwanamke na mzee wake sio nzuri kiuchumi (umaskini). Katika hali, je mwanamme atapata dhambi au ataharibu toba yake iwapo ataamua kumsaidia huyu mwanamke na mzee wake kiuchumi (kifedha), lakini sio kwa nia ya kimapenzi ila ni kwa huruma ya umasikini wao.



JIBU:



Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.



Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu kumsaidia aliyezini naye.

Tunamtakia kila la kheri mtu huyo aliyetubia baada ya kuzini na tunamuombea kwa Allaah Aliyetukuka asirudie tena tendo hilo ovu.



Msaada unatakikana kwa Muislamu yeyote yule mwenye kuhitajia. Na ikiwa wako Waislamu wenye kuhitajia ni muhimu sana kuwasaidia.

Ama ikiwa huyo mtu anataka kumsaidia huyo mwanamke aliyezini naye

Pamoja na mama yake kwa sababu ya ule uhusiano wao na kujuana kwao, hiyo inaweza kupelekea kuendelea kuunganisha mahusano yao na kuzidi kuwaweka karibu na ukaribu huo ukapelekea wao kwa njia moja au nyingine kurudi au kukaribia maharamisho na makatazo ambayo Shari'ah haiwataki wao kuwa nayo. Kadhalika hali hiyo ya kusaidiana inaweza kuibua upya mapenzi kutokana na msaada huo haswa kwa upande wa mwanamke na kumfanya yeye bado akawa ana hisia na huyo mwanaume kwa kuona jinsi alivyo na huruma na kuwasaidia.



Katika hali kama hiyo pamoja na kuwa msaada ni jambo muhimu kwa wanaadamu lakini linaweza kuwarejesha tena kwenye maasi kwa njia moja au nyingine, hivyo ni bora kuepuka hilo na inshaAllaah watapata msaada kwa njia nyingine kwa uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).

Kuna kanuni inayosema, 'Kuzuia madhara kunatangulizwa kuliko kuleta maslaha'.



Na swali la kujiuliza, msaada kama huo anautoa kwa Waislam wenzake na wasio na uwezo au ni kwa huyo tu mwanamke asiye Muislamu kwa sababu ya historia yao?



Ajitahidi huyo mwanaume kusaidia mambo ya kheri na Waislamu wenye matatizo yao kwanza maadam ana uwezo wa kusaidia, na ikibidi sana kuwasaidia hao ima kwa hali yao kuzidi kuwa mbaya, basi asisaidie kwa njia ya moja kwa moja yeye, bali msaada ufikishwe na mtu mwengine na pia uambatane na nasaha za kurudi katika dini ya Allaah kweli na afundishwe Uislam na pia ajulishwe umuhimu wa kujilinda na maasi na kuwa mbali na ya haraam na awapelekee vitabu vya dini na mawaidha mbalimbali ya kuujua Uislam. Kwa upande mwengine kufanya hivyo pia kunaweza kuwavuta katika Uislamu na wakasalimika na kupata uongofu inshaAllaah.



Na Allaah Anajua zaidi
 
Ana Uzito Kufuata Maamrisho Ya Allaah, Vipi Anaweza Kurekebisha Iymaan Yake
Maswali: Taqwa - Tazkiyyah
SWALI:

Asalam Aleykum,

Natumaini wote Mwenyezi Mungu amewajali afya njema kabisa.

Nipo katika mtihani mkubwa sana wa kujenga imani yangu. Katika kitu ambacho huwa naomba kila sk ni kuwa na Imani iliyokamili na yenye kumtumikia ALLAH ipasavyo. Tatizo linalonipata ni uzito wa moyo wangu katika kufata amari za Mwenyezi Mungu ikiwemo SWALA TANO na nguzo zinginezo. Nimejaribu kujifunza kusoma Kiarabu (Lugha Tukufu ya Qur-an) kupitia mtandao wa quranitukufu na alhamdulillah kidogo napata kuelewa.

Swali langu: Tafadhali naomba uniambie namna ambayo ni rahisi kubadilisha imani yangu kwani nahitaji sana kurudi katika Maamrisho ya Mwenyezi MUNGU.

Natumaini nitapata jibu.asante.



JIBU:



Sifa zote njema zamstahikia Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Rehma na amani zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.



Shukran kwa swali lako.

Kwa kweli hakuna kitu chenye kuitwa namna rahisi ya kubadilisha Iymaan. Kama ulivyosema kuna uzito wa moyo katika kufuata amri za Allaah hasa hasa Swalah tano na hii inathibitisha kuwa bado unahitaji kazi kubwa kuifanya ili kuweza kwa msaada wa Allaah kufikia kuwa na Iymaan yenye kupenda kutekeleza amri za Allaah, na hilo si jepesi kwani Allaah Anasema:



“Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kusali; na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu, Ambao wana yakini kuwa hakika watakutana na Mola wao Mlezi na ya kuwa hakika watarejea Kwake” Al-Baqarah: 45-46



Unachotakiwa kujifunza sio lugha tu bali Iymaan na yakini kuwa hakika unahitaji kutekeleza amri za Aliyekuumba na kuwa na yakini kuwa utakutana Naye na Kwake Yeye utarejea na kuwa hapa duniani ni pahala pa kupita na salama ya mwanaadamu ni kutekeleza aliyoamrishwa na Mola wake.



Unachohitaji ni kumpenda Mola na Mtume Wake jambo ambalo litaweza kukusaidia kukufikisha pahala pa kupenda kutekeleza armi Zake Mola. Kupenda kitabu Chake ni jambo litalokupelekea kupenda kukisoma na kutekeleza unachokisoma; kuwapenda wenye kumpenda Allaah na Mtumewe ni jambo litalokusaidia kuweza kufikia kuwa tayari kuwasikiliza na kupenda kukaa nao na kuwa karibu nao wakati mwingi.

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate manufaa zaidi:



Swalah, Umuhimu Wake, Fadhila Na Hukmu Ya Mwenye Kuacha

Imani Yangu Inapungua Nakhofu Kupotoka Nifanyeje?

Anaomba Toba Kisha Anarudia Tena Kufanya Kosa Kila Mara. Vipi Aweze Kuimarika Bila Kurudi Makosani?

Nataka Kutubu Lakini Shaytwaan Kanivaa Nifanye Nini?

Nataka Kutubia...Lakini!!

Na Allaah Anajua zaidi
 
Imani Yangu Inapungua Nakhofu Kupotoka Nifanyeje?
Maswali: Taqwa - Tazkiyyah


SWALI:



asalam aleikum.

swali langu ni najiona siku zinavyo zidi kenda najiona imani yangu inapungua nakuwa mzito wakufanya ibada na kusoma quraan, nina ogopa nisije nikaendelea hivihivi. naombeni mnisaidie nifanye nini? niweze kurudi katika msimamo mzuri wa dini.

na alaah awajaalia kila la kheri kwa kazi mnayo fanya ya kuelimisha watu





JIBU:



Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.



Tunapenda kujulisha kwamba mja anapotambua kuwa imani yake inakuwa dhaifu na anapotaka kujua njia za kujikurubisha na Mola wake ni dalili ya uongofu na kupendwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Kwani wangapi wanakuwa katika hali kama hiyo lakini hawatambui wala kujali bali kuacha nafsi zao ziendelee kuridhisha matamanio yake.



Hivyo inakupasa kwanza kumshukuru Mola wako Mtukufu kwa kukutanabahisha kabla ya kutumbukia kabisa katika upotofu.



Pili fanya yafuatayo ili usalimike na urudishe hali yako katika usalama na taqwa:



Mlaani shaytwani kwa kusema kila mara (A’uddhu BiLLahi minashaytwaanir-Rajiym)
Jieke katika wudhuu kila mara
Soma sana Qur-aan pamoja na maana yake.
Soma nyiradi za asubuhi na jioni kila siku BILA YA KUACHA nazo zinapatikana katika kiungo kifuatacho:


Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)



027-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Za Asubuhi Na Jioni





Sikiliza sana mawaidha yaliyomo Alhidaaya, chagua mawaidha ya mbali mbali yanayohusu kujikurubisha kwa Allah,
na yatakayokupa khofu ya adhabu zake.
Jieupushe na mambo yote ya upuuzi bali tumia wakati wako wote katika dhikr, kutafuta elimu na ibada.
Jeipushe na marafiki wabaya.
Omba sana du’aa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akusaidie kukurudisha katika iymaan na taqwa.
Fanya sana Istighfaar.
Kumbuka mauti kila mara na kwamba haya maisha na ya starehe ndogo tu, na kwamba maisha ya Akhera ndiyo ya milele.


Tunatumai kwamba utayatekeleza hayo tuliyokuarifu, na tunaomba kuwa yakufae, na Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Azidi Kukuongoza Akutoe katika kiza unachokaribia kuingia na Akuweke katika nuru na Akujaalie uwe katika waja Wake Wema.



Na Allaah Anajua zaidi
 
Anaomba Toba Kisha Anarudia Tena Kufanya Kosa Kila Mara. Vipi Aweze Kuimarika Bila Kurudi Makosani?
Maswali: Taqwa - Tazkiyyah


SWALI:



assalaam alykum swala ni mambo gani ambayo natakiwa kufanya ila nisirudie kosa baada ya kutubu, kwani huwa najitahidi kutubu huwenda isipite hata miezi mitatu hurirejea kosa lile lile nililotubu najitahidi kujizuia kwa kubadilsha mazingara lakini bado shetani hunizidi nguvu naomba msaada kuhusiana na hili









JIBU







Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kurudia katika kosa baada ya kutubia.



Yapo mambo mengi ambayo unaweza kufanya ili kujitenga na maasiya na makosa hayo ambayo unayarudia.



Hakika ni maumbile ya mwanaadamu kurudia kosa baada ya muda. Hata hivyo, inatakiwa ufanye juhudi nyingi za kuweza kutorudia lakini ukikosa inabidi urudi utake msamaha kwake. Ikiwa utaweza kutimiza yale masharti ya kusamehewa basi InshaAllaah Allaah Aliyetukuka Atakusamehe. Jaribu sana utimize masharti yafuatayo:



Kuacha maasiya.
Kujuta katika kufanya hayo maasiya.
Kuazimia kutorudia makosa hayo.
Ukiwa umemkosea mwanaadamu mwenzako basi uombe msamaha kutoka kwake.


Baada ya kurudia kosa basi utarudia mfumo huo ulio juu katika kuomba msamaha. Ama mambo ambayo yanaweza kukusaidia ili kukupatia kinga ili usirudie makosa hayo kwa kiasi ulicho nacho sasa ni kama yafuatayo:



Kuifanya Qur-aan kuwa rafiki yako wa karibu sana. Na haitakiwi kuisoma peke yake bali unatakiwa uisome pamoja na kufahamu na kujua maana yake. Na baada ya kujua maana yake kufanya juhudi kutekeleza yaliyo ndani kwa kiasi kikubwa sana.
Kuifahamu Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kujaribu sana kufuata yale tuliyofundishwa ndani yake.
Kuyafahamu majina ya Allaah Aliyetukuka na kujua maana ya kila jina pamoja na sifa Zake.
Kuleta adhkaar za asubuhi na jioni pamoja na adhkaar nyingine ambazo zinapatikana katika viungo vifuatavyo:



Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)



027-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Za Asubuhi Na Jioni







Kufanya urafiki na watu walio Waumini ili kuweza kusaidiana katika kufanya mema na kuacha mabaya.


Kufanya hayo kutatusaidia sana katika kujiepusha na makosa ambayo unayarudia rudia kila wakati.



Na Allaah Anajua zaidi
 
Nataka Kutubu Lakini Shaytwaan Kanivaa Nifanye Nini?



Alhidaaya.com





Swali:



Asalaam aleykum,



In shaa Allaah natuwai wote wazima na alhamdulilah kwa kuttuelimisha,mimi ni msichana wa miaka 23 naomba nasiha zenu In shaa Allaah mutaweza kunisaidia,mie siswali,na na[enda kuwa karibu na watu waovu,na najua kuwa nafaanya makosa nimejaribu kuacha lakini narudia tena, napenda kuangalia mambo yasio na maana, naomba munisaidie natamani kutubu kuwa kama wasichana walioshika dini, hijab, abaya yote navaa lakini matendo yangu yote kinyume na msichana wa kiislamu,naombeni munisaidie ndugu zangu wa kiislam, In shaa Allaah Allaah atawalipa, shukran.




Jibu:



AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.





Kwanza tambua kuwa hiyo ni neema kwako kutoka kwa Rabb wako kwamba Amekupa uongofu wa kutambua makosa yako kwa hiyo jambo la kwanza linalokupasa ni kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kukuzindua ukatambua kuwa uko makosani kabla ya adhabu Yake au mauti kukufika. Vile vile kupata uongofu katika umri kama huo pia ni jambo la kumshukuru Allaah kwani wengi huendelea na maasi na kuendelea kuchuma madhambi hadi wanafikia katika umri mkubwa. Yote hayo ni neema kutoka kwa Mola wako unapasa umshukuru sana kila wakati.





Pili jua kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anawapenda sana waja Wake wanaofanya makosa kisha wakarudi Kwake kama Anavyosema:

اِنَّ اللّهَ یُحِبُّ التَّوَّابِینَ وَیُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِینَ

Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha. [Al-Baqarah:222]





Kwa hiyo wewe ni miongoni mwa hao ambao (Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anawapenda, kwani wangapi wanafanya maovu lakini wamo tu na kuendelea na maovu hawashtuki wala hawajuti wala hawataki kurudisha nafsi zao katika Kumucha Allaah, lakini wewe ni kinyume.





Tafuta muda wa kusoma mada katika viungo vifuatavyo ambavyo viko katika tovuti hii ya Alhidaaya ili ujue jinsi ya kuomba Tawbah na pia utambue faida zake na uweze kurudisha nafsi na moyo wako katika hali ya kukuridhisha mwenyewe na kumridhisha Mola Wako ili uweze kufuzu duniani na Aakhirah In shaa Allaah.





Mahitajio Ya Nafsi



Tawbah



Nilipotoka Lakini Nimetubu Je Allaah Atapokea Du'aa Zangu? Vipi Kumkwepa Shaytwaan?

Nataka Kutubia...Lakini!!



Ana Tabia Za Maasi Anashindwa Kujizuia Nazo





Tatizo ulilonalo ni kwamba Shaytwaan amekuganda ili uendelee kufanya maovu na usibanduke. Na wewe inaonyesha umesalimu amri kwake na hutumii njia tulizofundishwa na Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salaam) za kumfukuza na kumuepuka. Nazo ni kujikinga na Shaytwaan kama utakavyoona hapa chini. Kwa hiyo baada ya kuomba Tawbah kama utakavyojifunza katika mada hizo tulizokutajia, kisha fuata yafuatayo:



1. Kaa na wudhuu kila mara.

2. Jikinge na Shaytwaan kwa kusema ‘Audhu Billahi Minash-shaytwaanir-rajiym’ kila mara unapohisi kutaka kufanya jambo ovu.

3. Tekeleza Swaalah Zako tano kwa wakati wake kwani Swaalah humuepusha mtu na maasi na maovu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

اتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ ۗ

Soma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) uliyoletewa Wahy katika Kitabu na simamisha Swalaah, hakika Swalaah inazuia machafu na munkari. [Al-‘Ankabuut: 45]

4. Mkumbuke sana Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kusoma Qur-aan kila siku japo ukurasa mmoja.



5. Vile vile soma nyiradi za kila siku za asubuhi na jioni ambazo zimo humu katika site ya Alhidaaya katika kitabu cha Hiswnul-Muslim katika kiungo kifuatacho:



027-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Za Asubuhi Na Jioni



6. Jitenge na marafiki waovu na ambatana na marafiki wema. Jaribu kuwakwepa marafiki zako waovu na anza kutafuta marafiki wacha Mungu wenye kupenda Dini yao. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Amesisitiza kuwa na marafiki wa Dini.



7. Kumbuka mauti kila mara.



8. Kumbuka pepo na kutarajia neema na raha zake.



9. Wakati wako wa faragha soma vitabu vya dini upate elimu kwani utakapokuwa na elimu ya dini utajua maovu na utakuwa na khofu ya kujikinga nayo na utajua mema na kutarajia ujira mzuri.



10. Jitahidi sana kujiweka katika hali ya kuwa na kazi, usikae bure hata wakati mmoja, jishughulishe kila mara kwa kusoma, kusikiliza maiwadha, Qur-aan na hata kutazama video za mawaidha badala ya hizo chafu na utajikuta DAIMA huna muda wa kushawishika na upuuzi wowote na maovu.



11. Kama kuna eneo linasomesha Darsa jaribu kujiungana kuhudhuria kila mara.



Umesema kwamba mavazi yako ni ya Kiislamu ila tu hufuati yanayompasa Muislamu kufanya, basi jitahidi kuendelea kujisitiri kwa mavazi ya hijaab ya kisheria na ujiepushe na maasi ili yalete maana na dhamiri khaswa yasije yakakukupeleka katika sifa ya unafiki. Allaah Akuepushe na sifa hiyo chafu.





Tunatumai kuwa In shaa Allaah baada ya kufuata maelezo na mafunzo yote hayo utaweza kujirekebisha na kujirudisha hali yako katika ucha wa Allaah ili upate kuiokoa nafsi yako na ghadhabu za Rabb wako upate Ridhaa Yake na uwe miongoni mwa waja Wake Alioridhika nao na upate kufuzu duniani na Aakhirah In shaa Allaah.





Na Allaah Anajua zaidi
 
Anasumbuliwa Na Khofu Aliyonayo
Anaishi Nchi Zenye Maasi Anajizuia Anaomba Toba Lakini Anasumbuliwa Na Khofu Aliyonayo
Maswali: Taqwa - Tazkiyyah


SWALI:



Asalamu aleikum swali langu ni juu ya mimi kijana wa umri 28 na sina mke nafuata dini yangu alhamdulilah lakini shida niko nayo ni kuwa nchi hii holland kuna maasi nyenge sana kwenye tv, internet na pia njiani najaribu sana kujizuia na pia kufunga naafila pia lakini mara kwa mara naingia maasi ya fahisha lakini siyo zina naomba toba kila mara lakini baada ya muda tena vili vili na toba tena, lakini sasa naogopa kwa sababu imekuwa kama kawaida na ina nisumbua kwa ibada naona kwamba hii ni tabia ya kimunafiiq.

Naomba advice yenu kidugu inshaallah.



JIBU:



Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.



Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuingia katika maasiya.

Hakika ni kuwa mara nyingi watu hufanya makosa kwa kuamua kuhama nchi zao na kukimbilia Ulaya. Nchi ambazo kabla hatujakwenda tunajua dhahiri kuwa maasiya ni mengi na hakuna nidhamu kabisa ya kimaadili mbali na kuwa wameendelea kimada. Tunakuja kujipata mashakani baada ya muda wa kuishi huko na hatuna njia ya kujitoa.



Kuna njia nyingi ya kujiepusha na maasiya kabla hujatumbukia ndani yake na hasa hali uliyo nayo. Njia ni kama zifuatazo:



1. Kuoa, nayo ni amri kutoka kwa Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hii ndio njia nzuri kabisa ya kukuwezesha kujizuilia na maasiya hayo. Hivyo, nasaha yetu ni kuwa ikiwa una uwezo wa kumueka mke basi fanya hima utekeleze hilo.



2. Kufanya usuhuba mkubwa na Kitabu cha Allaah Aliyetukuka na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwani kufanya hivyo kutakupatia kinga. Unatakiwa usome, uelewe na ujue maana ya unayosoma na kujitahidi sana kufuata kimatendo unayosoma.



3. Kusoma visa vya Maswahaba na watangu wema wa zamani na sasa jinsi walivyoepukana na maasiya katika maisha yao.



4. Kufunga, japokuwa unasema unafunga lakini inaonyesha unahitaji kufanya bidii kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia kuwa kufanya hivyo ni kinga.



5. Kufanya urafiki na marafiki wema na wazuri na hata kuishi nao katika nyumba moja, kwani Muislamu ni kioo kwa Muislamu mwenziwe. Ukiwa na marafiki hao watakusaidia sana katika kujiepusha na maasiya.



6. Jaribu kujishughulisha na mazoezi na michezo inayokubalika kisheria, Unaweza kwa wakati wa faragha kufanya zoezi la kukimbia, au kwenda gym, ilimradi ujishughulishe.



7. Kujifungamanisha na Msikiti au Markazi ya Kiislamu hata kama iko mbali kidogo kwani hapo mtakuwa mnatapa darsa ya kuwaepusha na maradhi na ugonjwa wa maasiya.



8. Kukumbuka mauti na kuwa utakutana na Mola wako Mlezi.



Ama kuhusu kukosea na kurudia tena maasiya ni ada ya mwanaadamu na Allaah Aliyetukuka Anampenda Anayefanya makosa sio kwa makusudi anayerudi haraka kutaka msamaha. Na mara nyingine zinakuwa ni pepesi za Shaytwaan hivyo unatakiwa usome Adhkaar na asubuhi na jioni kila siku na nyinginezo ambazo zinapatikana katika kitabu hiki ndani ya Alhidaaya:



Hiswnul Muslim



Na Allaah Anajua zaidi
 
UJUMBE WA LEO :
Utajiri sio kuwa na Mali bali ni kuwa na nafsi yenye kukinai/kuridhika

- Nabii swalla aallahu alayhi wa aliih wa sallam
 
Baadhi ya post za zamani...

JE MTOTO ALIYEZALIWA NJE YA NDOA ANAFAA KUITWA KWA UBINI WA BABA


Kwa mujibu wa imani ya kiislamu mtoto ambaye amezaliwa nje ya ndoa hatambuliki Kwa mujibu wa Sheria kama mtoto wa Baba husika.

Kwasababu kizazi au uzao WA familia unatakiwa upatikane ndani ya ndoa ya kisheria au ndoa iliyofungwa Kwa misingi ya Dini,na nje ya hapo huyo ni mtoto wa zinaa ambaye kisheria anatambulika kama mtoto wa mama aliye mzaa Tu.

Ingawa kikawaida atafahamika kama mtoto wa Baba Fulani lkn kidini huyo Baba hatambuliki na hivyo kuna haki Fulani ambazo Baba hawezi kumfanyia mtoto wake.

Moja wapo ni huyo mtoto hafai kuitwa Jina la ubini WA Baba yake,Hilo Jambo ni haramu Sana na Mungu ameshalikemea tayari, ingawa Kwa bahati mbaya Sana Kwa kutojua wengi wamewapa majina ya ubini wao hao watoto wa nje ya ndoa.

Na lingine ni kumuozesha kwenye ndoa, Baba Hana haki ya kumuozesha binti yake WA nje ya ndoa Kwa mumewe kwani ndoa hiyo ni batili na haifai kabisa.

Lingine huyo mtoto hawezi kumrithi Baba yake kwasababu kisheria huyo mtoto sio WA huyo Baba,Bali Baba anaweza kumpa sehemu ya Mali huyo mtoto,lkn mara Tu huyo Baba anapokufa basi huyo mtoto Hana haki ya Kurithi chochote.

Lakini sio vibaya huyo Baba kumhudumia huyo kijana Kwa malezi na mahitaji mbali mbali maadam Tu yeye ndiye sababu ya kuja Hicho kiumbe hapa duniani.

Na mtoto ambaye Hana Baba kisheria anaweza kuitwa Kwa jina la mama yake, Kwa mfano ETUGRUL BEY ASHA au Kwa jina la ubini Kwa upande wa mama yake.

Kubwa ni kutambua uzao mzuri ambao hata kizazi chako kinaweza pata haki stahiki ni kizazi ambacho kinatokana na ndoa takatifu ambayo IPO Kwa mujibu wa Sheria.

Na hata wale ambao wanafunga ndoa za kiserikali basi watambue kidini Hicho kizazi Chao hakitambuliki na Sheria za Dini Kwa maana Baba Hana watoto hapo Ila watoto ni WA mama.
 
Baadhi ya post za zamani....

KISA JUU YA KUMWAMINI ALLAH

Kutoka kwa Shuaib amesema Mtume swalallahu alayh wassalam

Kulikuwa na Mfalme ambaye alikuwa na mchawi wake, ikafikia kipindi yule mchawi akamwambia mfalme,hakika sasa nimekuwa mzee nitafutie kijana wa kumfundisha uchawi.

Mfalme akamtafuta kijana mmoja awe anaenda kwa mchawi kujifunza uchawi, wakati kijana akiwa njiani kwenda kwa mchawi alikuwa anakutana na mtawa mmoja anasiikiliza mazungumzo yake kisha anaenda kwa mchawi,kijana akawa anavutiwa sana na yale mazungumzo ya mtawa mpaka akawa anachelewa kwenda kwa mchawi na hivyo kuchapwa.

Akaja kulalamika kwa mtawa, basi mtawa akamwambia mwambie mchawi kuwa watu wako wanakushughulisha ndio maana unachelewa, na ukiogopa watu wako nao waambie kuwa mchawi anakuchelewesha.

Siku Moja wakati kijana anaenda kule kwa mchawi njiani kuna kiumbe kikubwa sana kiliingia barabarani na watu wakawa wanaogopa kupita.

Yule kijana akasema leo nataka nione maneno gani ni ya kweli kati ya mchawi na yule mtawa. Basi akachukua jiwe na kusema Ewe Allah ikiwa vitendo vya mtawa vinakupendeza zaidi kuliko vya yule mchawi basi muue kiumbe hiki, kijana akarusha jiwe na kile kiumbe kikafa.

Yule kijana akawa na uwezo wa kuponyesha vipofu wa kuzaliwa, na watu wenye Maradhi ya ngozi na mengineyo, kuna mshauri mmoja wa mfalme alikuwa kipofu aliposikia habari za kijana yule basi, alitafuta zawadi na kumletea kijana yule na kumwambia basi niponye ntakupa zawadi hizi, kijana akajibu mimi sio mponyaji ila anayeponya ni Allah, ikiwa unataka kuponywa basi mkubali Allah na umuamini kisha atakuponya.

Basi yule bwana akakubali na kuponywa, akarejea kwa mfalme,baada ya mfalme kumuona akamuuliza nani amekuponya upofu wako? Akajibu ni Allah. Mfalme akasema kwahiyo una Mungu mwingine badala yangu? Akajibu Allah ndio Mungu wako na Mungu wangu, basi akateswa mpaka akamtaja yule kijana.

Mfalme akasema kijana aletwe, nae akaulizwa inamaana umejifunza uchawi mpaka umefikia kiwango cha kuponya watu upofu na maradhi mengine? Kijana akajibu anayeponya ni Allah,naye akateswa mpaka akamtaja Mtawa, hapo awali baada ya tukio lile la kumwambia Allah kama unapendezewa na vitendo vya mtawa kuliko mchawi basi muue kiumbe hichi. Alienda kumpa habari mtawa, na mtawa akasema hakika leo umenishinda hata mimi ila hivi karibuni utapata majaribu lakini usije kunitaja.

Lakini kutokana na mateso ikabidi tu amtaje mtawa, basi mtawa aliletwa mbele ya mfalme akaambiwa ikane imani yako la sivyo atauwawa, mtawa akakataa basi mfalme akaagiza msumeno na kumkata mtawa vipande viwili.

Kisha mshauri wa mfalme akaambiwa aikane imani yake nae akakataa, naye akakatwa na msumeno, kisha mfalme akamwambia kijana aikane imani yake akakataa.

Mfalme akasema mchukueni huyu kijana nendeni nae juu ya kilele cha mlima, akikataa kuikana imani yake basi mrusheni kutoka huko, walipofika kileleni akasema Ewe Allah naomba uniokoe kwa namna yoyote unayopenda, basi mlima ukatingishika na wale watu wa mfalme wakaanguka na kujifia, kisha kijana akarudi kwa mfalme.

Mfalme akauliza imekuaje kuhusu watu wangu, akajibu Allah ameniokoa. Mfalme akaagiza watu wake waende na kijana katikati ya bahari, akikataa kuikana imani yake basi wamtumbukize baharini, akasema Ewe Allah naomba uniokoe kwa namna yoyote unayotaka, basi boti zikazama na wale watu wakafa, kisha kijana akarudi kwa mfalme.

Mfalme akauliza kama awali akajibiwa Allah ameniokoa, sasa kijana akamwambia huwezi kuniua ila mpaka utumize sharti langu, mfalme akasema sharti gani hilo?

Akamwambia wakusanye watu katika ardhi yenye mwinuko kisha nifunge kwenye mti halafu chukua mshale na useme kwa uwezo wa Allah mola wa huyu kijana nitakuua!

Basi akaachia mshale na kumpiga yule kijana katika paji la uso na yule kijana akanyanyua mikono yake na kugusa pale alipopigwa na kufa.

Watu wakaanza kupaza Sauti na kusema Tunamwamini Allah mola wa huyo kijana, basi mfalme akaamuru uchimbwe mtaro mkubwa pembeni ya barabara, kisha ndani ya mtaro pakawashwa moto, kisha mfalme akasema yoyote ambaye haikani imani yake atatumbukizwa mtaroni.

Watu wakawa radhi kuingizwa mtaroni kuliko kuikana imani yao juu ya Allah, basi kulikuwa na mwanamke mmoja ana mtoto mdogo, akawa anasita kuingia mtaroni, yule mtoto mdogo Kabisa akamwambia Mama usiogope kuwa miongoni mwa wenye subira imani yako ni ya kweli, basi akajirusha na kuwa miongoni mwa mashahidi walioingia peponi.

(sahihi Muslim, hadith no. 7148)
 
Dalili Ya Tawhiyd Kwa Wenye Akili Ni Kutafakari Uumbaji Wa Allaah ('Azza wa Jalla)



www.alhidaaya.com





Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):



إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana; bila shaka ni Aayaat (ishara, zingatio) kwa wenye akili.





الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾

Ambao wanamdhukuru Allaah kwa kusimama na kwa kukaa na kwa kulala ubavuni mwao na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): “Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu ni Wako tukinge na adhabu ya moto.” [Al-'Imraan: 190-191]











Aayah hizo mbili tukufu ni Aayah ambazo zinaonyesha dalili ya Tawhiyd kwa watu wanaotafakari uumbaji wa Allaah ('Azza wa Jalla) ambao wanadhihirisha imani zao kwa matendo yao ya kumdhukuru Rabb wao kwa du'aa na adkhaar kila wakati na popote walipo.





Na hakika mwenye kutafakari uumbaji wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), ndio waliokusudiwa kuwa ni wenye akili. Nao hukaa na kutafakari uumbaji wa mbingu jinsi ulivyo ukubwa wake na umbali wake, na uumbaji wa ulimwengu mzima pamoja na viliomo ndani yake; vikiwemo nyota mbali mbali zinazozunguka angani, bahari, milima, mabonde, chemchemu za maji, mito, majangwa, miti, mimea, maua yenye rangi na harufu mbali mbali, matunda ya kila aina kwa rangi na ladha mbali mbali ambayo yote yanatokana na maji (mvua) hiyo hiyo ya aina moja tu, wanyama wa kila aina wa angani, ardhini na baharini, madini, na mengi mengineyo ambayo hayahesabiki. Wenye akili hutafakari pia uumbaji wa mwili wao na hutafakari pia sababu na lengo la kuumbwa kwao pamoja na uumbaji wa ulimwengu mzima.





Juu ya hivyo hutafakari kuhusu mabadiliko ya mfuatano wa mbingu na ardhi na wakati pia; mfano siku za majira ya baridi kuwa fupi na siku za majira ya joto kuwa refu, kugeuka mchana, usiku na kupambazuka kwa Alfajiri, yote hayo ni kwa amri na uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Mwenye Hikma zote na ndio maana Anasema:



لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾

…bila shaka ni Aayaat (ishara, zingatio) kwa wenye akili.





Wanaokusudiwa hapo ni Waumini wenye mawazo ya kutafakari sana kuhusu ukweli wa uumbaji wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na si wale wasioamini ambao wao ni kama vipofu wasiokuwa na mawazo kabisa ya kufikiri uumbaji wa Rabb wao ambao wanaishi na kunufaika nao. Uumbjai ambao unaonekana kila mahali walipo, mchana na usiku, na hata kama wanajua kuwa ni uumbaji wa Allaah ('Azza wa Jalla) Ambaye ni Muumba Mwenye Nguvu na Uwezo wote, lakini wanakanusha haki, bali wanapuuza. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anataja kupuuza kwao katika kauli Zake:



وَكَأَيِّن مِّنْ آيَةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يَمُرُّونَ عَلَيْهَا وَهُمْ عَنْهَا مُعْرِضُونَ ﴿١٠٥﴾

Na Aayah (ishara, dalili) ngapi katika mbingu na ardhi wanazipitia na huku wao wanazipuuza.







وَمَا يُؤْمِنُ أَكْثَرُهُم بِاللَّـهِ إِلَّا وَهُم مُّشْرِكُونَ ﴿١٠٦﴾

Na wengi kati yao hawamwamini Allaah isipokuwa wao ni wenye kufanya shirki. [Yuwsuf: 105-106]













Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Kawaelezea Waumini wanaotafakari, kuwa wao wanamdhukuru Rabb wao kila wakati, popote walipo na vyovyote walivyo na wanashuhudia Utukufu Wake na Uwezo Wake na Rahma zake. Kisha humtukuza Rabb wao na kutambua kwa kukiri kuwa hakika Allaah ('Azza wa Jalla) Hakuviumba vyote hivyo bila ya sababu bali Kaviumba kwa haki ili awalipe wanaotenda maovu adhabu wanazostahiki na Awalipe wanaofanya mema mazuri wanayostahiki. Kisha wanamalizia kumuomba Rabb wao Awaepushe na adhabu ya moto:





الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾

Ambao wanamdhukuru Allaah kwa kusimama na kwa kukaa na kwa kulala ubavuni mwao na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): “Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu ni Wako tukinge na adhabu ya moto.” [Al-'Imraan:191]









Hali ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ilivyokuwa wakati zimeteremshwa Aayah hizi ni kama ilivyoelezewa katika Hadiyth:







روي أن عائشة أم المؤمنين رضي الله عنها سئلت عن أعجب ما رأته من رسول الله صلى الله عليه وسلم فبكت ثم قالت: كان كل أمره عجباً، أتاني في ليلتي التي يكون فيها عندي، فاضطجع بجنبي حتى مس جلدي جلده، ثم قال: ((ياعائشة ألا تأذنين لي أن أتعبد ربي عز وجل؟)) فقلت: يارسول الله: والله إني لأحب قربك وأحب هواك- أي أحب ألاّ تفارقني وأحب مايسرك مما تهواه- قالت: فقام إلى قربة من ماء في البيت فتوضأ ولم يكثر صب الماء، ثم قام يصلي ويتهجد فبكى في صلاته حتى بل لحيته، ثم سجد فبكى حتى بلّ الأرض، ثم اضطجع على جنبه فبكى، حتى إذا أتى بلال يؤذنه بصلاة الفجر، رآه يبكي فقال يارسول الله: مايبكيك وقد غفر الله لك ماتقدم من ذنبك وماتأخر؟ فقال له: ((ويحك يابلال، ومايمنعني أن أبكي وقد أنزل الله عليّ في هذه الليلة هذه الآيات : (إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاخْتِلاَفِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لآيَاتٍ لِّأُوْلِي الألْبَابِ... ) ثم قال: ((ويل لمن قرأها ولم يتفكر فيها)).



Imesimuliwa kwamba Mama wa Waumini 'Aishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) aliulizwa kuhusu jambo la ajabu alilolishuhudia kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alilia kwanza kisha akasema: "Mambo yake yote yalikuwa ya ajabu. Usiku mmoja alikuja karibu na mimi mpaka ngozi yake ikagusa ngozi yangu na akasema, ((Huniaachi nimuabudu Rabb wangu?)) Nikasema: "Ee Rasuli wa Allaah, Wa-Allaahi, hakika mimi napenda ukaribu wako kwangu (uwe karibu yangu), na pia napenda mahaba yako, kwamba napenda usiwe mbali na mimi, na napenda yale yanayokufurahisha". Akasema ('Aishah): Akainuka na kutumia kiroba cha maji na akafanya wudhuu wala hakutumia maji mengi. Kisha akasimama akaswali akalia mpaka ndevu zake zikawa zimerowa. Kisha akasujudu na kulia mpaka akaifanya ardhi irowe. Kisha akalala kwa upande wa kulia mpaka akaja Bilaal kumjulisha Adhaan ya Alfajiri, akamuuliza: Ee Rasuli wa Allaah! Jambo gani linakuliza na hali Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amekwishakufutia madhambi yako yaliyotangulia na yanayokuja?" Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ee Bilaal, na nini kinizuie mimi kulia wakati usiku huu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameniteremshia Aayah hizi?"



إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana; bila shaka ni Aayaat (ishara, zingatio) kwa wenye akili.





الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾

Ambao wanamdhukuru Allaah kwa kusimama na kwa kukaa na kwa kulala ubavuni mwao na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): “Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu ni Wako tukinge na adhabu ya moto.”





رَبَّنَا إِنَّكَ مَن تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ ﴿١٩٢﴾

“Rabb wetu, hakika Umuingizaye motoni, kwa yakini Umemhizi. Na madhalimu hawana yeyote mwenye kuwanusuru.”





رَّبَّنَا إِنَّنَا سَمِعْنَا مُنَادِيًا يُنَادِي لِلْإِيمَانِ أَنْ آمِنُوا بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا ۚ رَبَّنَا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَكَفِّرْ عَنَّا سَيِّئَاتِنَا وَتَوَفَّنَا مَعَ الْأَبْرَارِ ﴿١٩٣﴾

“Rabb wetu, hakika sisi tumemsikia mwitaji anaita kwenye iymaan kwamba ‘mwaminini Rabb wenu’ basi tukaamini. Rabb wetu, Tughufurie madhambi yetu na Tufutie makosa yetu na Tufishe pamoja na Waumini wema.”





رَبَّنَا وَآتِنَا مَا وَعَدتَّنَا عَلَىٰ رُسُلِكَ وَلَا تُخْزِنَا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ إِنَّكَ لَا تُخْلِفُ الْمِيعَادَ ﴿١٩٤﴾

“Rabb wetu na Tupe Uliyotuahidi kupitia Rusuli Wako, wala Usituhizi Siku ya Qiyaamah; hakika Wewe Huendi kinyume na miadi.”





فَاسْتَجَابَ لَهُمْ رَبُّهُمْ أَنِّي لَا أُضِيعُ عَمَلَ عَامِلٍ مِّنكُم مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ ۖ بَعْضُكُم مِّن بَعْضٍ ۖ فَالَّذِينَ هَاجَرُوا وَأُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَأُوذُوا فِي سَبِيلِي وَقَاتَلُوا وَقُتِلُوا لَأُكَفِّرَنَّ عَنْهُمْ سَيِّئَاتِهِمْ وَلَأُدْخِلَنَّهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ثَوَابًا مِّنْ عِندِ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عِندَهُ حُسْنُ الثَّوَابِ ﴿١٩٥﴾

Basi Rabb wao Akawaitikia “Hakika Mimi Sipotezi ‘amali za mtendaji yeyote yule miongoni mwenu akiwa mwanamume au mwanamke, nyinyi kwa nyinyi. Basi wale waliohajiri na wakatolewa majumbani mwao na wakaudhiwa katika njia Yangu, wakapigana na wakauliwa; bila shaka Nitawafutia makosa yao na bila shaka Nitawaingiza Jannaat zipitazo chini yake mito, ni thawabu kutoka kwa Allaah. Na kwa Allaah kuna thawabu nzuri kabisa.”





لَا يَغُرَّنَّكَ تَقَلُّبُ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي الْبِلَادِ ﴿١٩٦﴾

Isikudanganye kabisa kutangatanga kwa wale waliokufuru katika nchi.



مَتَاعٌ قَلِيلٌ ثُمَّ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۚ وَبِئْسَ الْمِهَادُ ﴿١٩٧﴾

Ni starehe ndogo, kisha makazi yao ni Jahannam. Na ni mahala pabaya mno pa kupumzikia.





لَـٰكِنِ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ لَهُمْ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا نُزُلًا مِّنْ عِندِ اللَّـهِ ۗ وَمَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ لِّلْأَبْرَارِ ﴿١٩٨﴾

Lakini wale waliomcha Rabb wao watapata Jannaat zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo, mapokezi kutoka kwa Allaah. Na vilioko kwa Allaah ni khayr kabisa kwa ajili ya wema watiifu.





وَإِنَّ مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ لَمَن يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْكُمْ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْهِمْ خَاشِعِينَ لِلَّـهِ لَا يَشْتَرُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ ثَمَنًا قَلِيلًا ۗ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ أَجْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ ﴿١٩٩﴾

Na miongoni mwa Ahlil-Kitaabi wamo wanaomwamini Allaah na yaliyoteremshwa kwenu, na yaliyoteremshwa kwao, wananyenyekea kwa Allaah hawabadilishi Aayaat za Allaah kwa thamani ndogo. Hao watapata ujira wao kwa Rabb wao. Hakika Allaah ni Mwepesi wa kuhesabu.





يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٢٠٠﴾

Enyi walioamini! Subirini na zidini kuvuta subira na bakieni imara na mcheni Allaah ili mpate kufaulu. [Aal-‘Imraan: 190-200]









Kisha akasema: ((Ole wake, yule anayezisoma lakini hatafakari kwayo))



Unapoamka usiku kwa ajili ya kuswali, ni Sunnah kuzisoma Aayah hizo kwani ilikuwa ni ada ya Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuzisoma Aayah hizi anapoamka usiku kuswali. Na sisi tunapaswa tufuate Sunnah hii tukufu.





Ndugu Waislamu, hizo ndizo Aayah ambazo zilimliza Nabiy wetu mpenzi (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa aalihi wa sallam) akawa hakuweza kulala usiku huo akawa anazisoma na huku analia tu. Hakika ni Aayah tukufu mno zinazosisimua mwili na kushitua nyoyo za wenye akili. Basi tujiulize:



Je, tutakuwa katika wale wanaomdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kila wakati na popote tulipo?



Je, tutafikiria Uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wa kuumba vitu vyote vilivyo ulimwenguni na katika uumbaji wa nafsi zetu pia na kufikiria Ufalme na Utukufu wake? Lau kama tutatafakari tunaposoma au kusikia Aayah hizi basi na sisi tutalia kwa khofu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), lakini labda nyoyo zetu zimekuwa ngumu, kwa hivyo inatupasa tumuombe Allaah ('Azza wa Jalla) Atuajaalie Nuru ya Qur-aan katika nyoyo zetu itujaze imani na khofu ya Rabb wetu. Aamiyn.







اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ قَلْبٍ لاَ يَخْشَعُ وَمِنْ دُعَاءٍ لاَ يُسْمَعُ وَمِنْ نَفْسٍ لاَ تَشْبَعُ وَمِنْ عِلْمٍ لاَ يَنْفَعُ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَؤُلآءِ الأَرْبَعِ



Allaahumma inniy a’uwdhu bika min-qalbin-laa yakh-sha’u, wamin du’aain-laa yasma’u, wamin nafsin-laa tashba’u, wamin ilmin-laa yanfa’u, a’uwdhu bika min haaulail-arba’i



Ee Allaah, hakika mimi najikinga moyo usionyenyekea na du’aa isiyosikizwa na nafsi isiyoshiba na elimu isiyonufaisha, najikinga Kwako dhidi ya haya manne.



[Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Swahiyh An-Nasaaiy, Swahiyh Al-Jaami’ (1297)]



Aamiyn
 
Mambo Yanayosababisha Katika Kumpwekesha Allaah (Tawhiyd) Kwenye 'Ibaadah



Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy (Rahimahu Allaahu)



Alhidaaya.com







Inasikitisha kuona kuwa hadi wakati huu, bado wapo Waislamu wenye itikadi isiyokuwa sahihi na wenye kusema maneno ambayo huenda yakawatia katika shirki.

Watu wa aina hiyo wengi wao niyyah zao ni nzuri, na ni katika watu wamchao Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aala) sana, wanaswali na kufunga na kutimiza nguzo zote tano za kiislamu. Lakini itikadi zao hizo pamoja na kuvuka kwao mipaka katika kuwasifia na kuwatukuza watu wema au Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Rusul wa Allaah ('Alayhis Salaam Ajmaiyn), huwafanya kutoa kauli zinazoweza kuwatia katika shirki na kuwatoa katika Tawhyid ambayo juu yake Dini hii tukufu imesimama.

Allaah Anasema:



وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾

Na Luqmaan alipomwambia mwanawe huku akimuwaidhi: “Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah, hakika shirki ni dhulma kubwa mno!” [Luqmaan: 13]



Na Akasema:



إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا ﴿١١٦﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali. [An-Nisaa: 116]



Kabla ya kuendelea mbele, ni bora tufafanue kidogo nini maana ya Tawhiyd:

Tawhiyd - ambayo kinyume chake ni Shirki; maana yake ni: "kupwekesha" au kuelekeza ‘ibaadah zote mahali pamoja tu. Nako ni kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Tawhiyd inakanusha aina yoyote ya kumshirikisha Allaah.



Dini ya Kiislamu ndiyo dini pekee ulimwenguni inayohubiri Tawhiyd. Kwasababu dini nyengine zote zinamnasibisha Allaah na washirika wengine.

Ma’ulamaa wameigawa elimu hii ya Tawhiyd sehemu tatu, nazo ni:

Tawhiyd Ar-Rubuubiyyah
Tawhyid Al-Uluuhiyyah
Tawhiyd Al-Asmaa Was-Swifaat


1. Tawhiyd Ar-Rubuubiyyah



Nayo ni kuamini kwamba Allaah. Allaah Ndiye aliyeumba kila kitu bila ya msaidizi. Itikadi hiyo pekee haimuingizi mtu Peponi, kwasababu washirikina wa Makkah wote walikuwa wakiamini kwamba Allaah ndiye Aliyeumba kila kitu bila ya msaidizi.

Allaah Anasema:

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ﴿٣١﴾

Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini. Au nani anayemiliki kusikia na kuona; na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu, na anayemtoa mfu kutoka aliye uhai; na nani anayeendesha mambo (yote)?” Watasema: “Ni Allaah”; basi sema: “Je basi hamuwi na taqwa?” [Yuwnus: 31]



Hata Ibliys aliyelaaniwa na Allaah, alikuwa anayo Tawhiyd hii.



Allaah Anasema:

قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ﴿٣٦﴾

Akasema: “Rabb wangu! Nipe muhula mpaka Siku watakayofufuliwa.” [Al-Hijr: 36]



Kutokana na Aayah zilizotangulia, utaona kuwa Maquraysh waliokuwa wakiabudu masanamu, pamoja na Ibliys wao, walikuwa wakiamini kuwa Allaah ndiye Rabb wao, na ndiye aliyeumba na ndiye Mwenye kumiliki kila kitu. Lakini imani yao hiyo hakuwasaidia kitu, kwa sababu ya kutoamini sehemu nyingine za Tawhiyd.



Kwa hivyo, hata kama utaamini kwamba Allaah Ndiye aliyeumba na ndiye mwenye kumiliki kila kitu, lakini ikiwa hujaamini sehemu ya pili na ya tatu ya Tawhiyd, basi iymaan yako hiyo haitokusaidia kitu.



2. Tawhyid Al-Uluuhiyyah



Nayo ni kuamini kwamba ‘ibaadah zote lazima zielekezwe kwake tu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).



‘Ibaadah kama vile kuswali, kuhijji, kuomba du’aa, kuchinja, kuweka nadhiri, kuhukumu n.k., zote hizo pamoja na niyyah ya mtu katika kutenda tendo lolote lile la kidunia au la kiakhera lazima zielekezwe kwake tu (Subhaanahu wa Ta’ala), na asiingizwe mshirika wa aina yeyote ndani yake.



Allaah Anasema:

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾

Sema: “Hakika Swalaah yangu, na kuchinja kafara na ‘ibaadah zangu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu.” [Al-An’aam: 162]





3. Tawhiyd Al-Asmaa Was-Swifaat



Nayo ni kuamini na kukubali kila kilichoandikwa katika Qur-aan Tukufu na katika Hadiyth zilizo sahihi za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zikielezea sifa tukufu za Allaah au majina Yake matukufu, bila ya kukisia kisia, wala kuchelewesha, wala kubadilisha maana yake.



Kwa mfano unapokutana na kauli ya Allaah isemayo:

يَدُ اللَّـهِ فَوْقَ أَيْدِيهِمْ ۚ

Mkono wa Allaah Uko juu ya mikono yao… [Al-Fat-h: 10]



Kubadilisha neno mkono tukasema nguvu, tutakuwa tumebadilisha maana.



Na Shaytwaan anapojaribu kutaka kukuchezea kwa kutaka ufananishe au ugeuze maana ya sifa, au majina ya Allaah kumbuka kauli Yake (Subhaanahu wa Ta’ala):



لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ

Hakuna chochote kinachofanana Naye… [Ash-Shuwraa: 11]



Shirki



Shirki katika lugha ya Kiarabu maana yake ni Ushirika. Nako ni kumjaalia mmoja au zaidi, awe na sehemu kubwa au ndogo, katika jambo lolote lile aloshirikiana na mwenziwe au wenziwe.



Kumshirikisha Allaah katika kuamini kwamba anaye mshirikia katika kuumba chochote kile (Tawhiyd Ar-Rubuubiyyah) au kuamini kwamba yuko mwenye uwezo au sifa kama Zake (Tawhiyd Al-Asmaa Was-Swifaat), au kuamini kwamba ‘ibaadah ya aina yoyote ile, inaweza ikaelekezwa au kupitia kwa mwengine asiyekuwa Allaah (Tawhyid Al-Uluuhiyyah), basi huko ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini yetu tukufu ya Tawhiyd na kumkadhibisha Allaah, na kwa sababu hii, dhambi yake haisameheki [kwa ukubwa wake].



Allaah Anasema:



شَهِدَ اللَّـهُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ

Allaah Ameshuhudia kwamba hapana muabudiwa wa haki ila Yeye… [Aal-‘Imraan: 18]



Na Anasema:

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ

Basi jua kwamba laa ilaaha illa-Allaah, hapana muabudiwa wa haki ila Allaah… [Muhammad: 19]





Tofauti Baina Ya Shirki Na Kufru



Shirki inahitilafiana na kufru. Kwani kuna shirki nyengine hazikupeleki kwenye kufru, kama vile Shirki ndogo (Ash-Shirkul-Asghar) au Shirki iliyojificha (Ash-Shirkul-Khafiy).

Pia kutenda au kutamka neno la shirki bila kujua, hakumpeleki mtu katika kufru. Isipokuwa mara tu baada ya kutambua, inampasa Muislam akiache kitendo hicho haraka sana. Dalili ya maneno haya ni Hadiyth zifuatazo:



Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), aliulizwa juu ya watu ambao wanapokuwa mbele ya wenzao hujionyesha kuwa ni watu wema na wanapokuwa peke yao hufanya kinyume na hayo. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwakufurisha watu wa aina hiyo, bali alisema: “Ninachokuogopeeni sana ni Shirki ndogo”. Maswahaabah wakauliza: "Ni nini hii Shirki ndogo, ewe RAsuli wa Allaah?" Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Riyaa (kujionyesha). [Imepokewa na Imaam Ahmad]





Dalili nyengine ni pale Swahaabah mmoja alipomwambia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Kama alivyotaka Allaah na ulivyotaka. Maa shaa Llaahu wa shi-ita.” Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Umenigeuza kuwa mshirika wa Allaah? Sema: 'Alivyotaka Allaah peke Yake' Qul Maa shaa-Llaahu wahdahu”. [Imepokewa na Imaam Ahmad, Addarmy na Ibni Maajah]





Zipo dalili nyingi juu ya maudhui haya, lakini hapa nitamaliza kwa kutoa dalili ifuatayo:



Siku moja Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwasikia baadhi ya watu wakisema: "Njooni tuombe, tuelekeze du’aa zetu kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).” Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipowasikia, akawaambia: “Nani huyu mnafiki? Du’aa hazielekezwi kwangu, bali zinaelekezwa kwa Allaah”. [Imepokewa na Imaan Ahmad na At-Twabaraaniy]





Ingawaje maneno yaliyotamkwa hapo juu na baadhi ya Maswahaabah, yalikuwa na dalili ya shirki ndani yake; lakini Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwahukumu waliotenda au kutamka maneno hayo kuwa ni makafiri. Bali aliwasahihisha itikadi yao, na hii ni kwasababu ya kutokujua

kwao kosa lao, kisha akawafahamisha hatari ya makosa hayo.



Kwa hivyo mwenye itikadi kama hiyo ya kumuomba Rasuli katika Rusul ya Allaah ('Alayhis Salaam Ajmaiyn) au Waliy katika Mawaliy wa Allaah n.k., hatuhumiwi kuwa ni kafiri. Isipokuwa mtendaji au msemaji wa kauli kama hizi ikiwa anafanya inadi na kushikilia, pamoja na kuendelea kutenda au kutamka maneno mfano wa haya kwa inadi na kutakabari tu, basi hapo ndipo anapokuwa katika hatari ya kuingia katika kufru.





Je, Inajuzu Kumuomba Rasuli (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)?



Suala sasa linakuja: "Jee inajuzu kuelekeza du’aa yako kumuomba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?"



Jawabu: "Haijuzu".



Kwa sababu Rasuli mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amebainisha aliposema: “Du’aa ndiyo ‘ibaadah”. [Imepokewa na Imaam Ahmad na Imaam At-Tirmidhiy]







Nini ‘Ibaadah?



Anasema Ibnu Qayyim Al-Jawziyyah (Rahimahu Allaah): "’Ibaadah ni jina lililokusanya kila Anachokipenda Allaah na kuridhika nacho ikiwa ni kitendo au kauli, zilizojificha au zilizodhihirika.”



Kwa hivyo kitendo chochote kinachokukaribisha kwa Allaah kama vile kuswali, kufunga, kuhijji, kutoa Zakkah, kutoa Swadaqah, kusoma Qur-aan, kuomba du’aa n.k. ni ‘ibaadah.

Ushahidi kwamba du’aa ni ‘ibaadah unatokana na kauli yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyotajwa hapo juu; aliposema katika Hadiyth sahihi iliyosimuliwa na Imaam Ahmad pamoja na Imaam At-Tirmidhiy: “Du’aa ndiyo ‘ibaadah”.



Kwa hivyo atakayemuomba yeyote asiyekuwa Allaah iwapo ni Malaika mtukufu, au Rasuli katika Rusul ya Allaah ('Alayhis Salaam), au Waliy katika mawaliy wa Allaah au jinni au kiumbe chochote kile kihai au kilichokufa, atakuwa amekwisha fanya kitendo cha ushirikina.

Allaah Anasema:



وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ﴿١٠٦﴾

Na wala usiombe badala ya Allaah visivyokufaa wala visivyokudhuru. Na ukifanya, basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.



وَإِن يَمْسَسْكَ اللَّـهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ ۖ وَإِن يُرِدْكَ بِخَيْرٍ فَلَا رَادَّ لِفَضْلِهِ ۚ يُصِيبُ بِهِ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ ۚ وَهُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿١٠٧﴾

Na Allaah Akikugusisha dhara, basi hakuna wa kuiondosha isipokuwa Yeye. Na Akikutakia kheri, basi hakuna wa kurudisha fadhila Zake, Anasababisha kumfikia kwayo (fadhila Yake) Amtakaye katika waja Wake. Naye ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Yuwnus: 106-107]



Na Anasema:

قُلْ إِنِّي لَا أَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا رَشَدًا﴿٢١﴾

Sema: “Hakika mimi sikumilikieni dhara na wala uongofu.” [Al-Jinn: 21]



Na pia Anasema:



قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي نَفْعًا وَلَا ضَرًّا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۚ وَلَوْ كُنتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ ۚ إِنْ أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿١٨٨﴾

Sema: “Siimilikii nafsi yangu manufaa yoyote wala dhara yoyote isipokuwa Apendavyo Allaah. Na lau ningekuwa najua ya ghayb, bila shaka ningelijikithirishia ya khayr, na wala lisingelinigusa ovu. Mimi si chochote isipokuwa ni mwonyaji na mbashiriaji kwa watu wanaoamini.” [Al-‘Aaraaf: 188]



Ukizichunguza Aayah nyingi, utaona kwamba Allaah Anamwambia Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): sema, waambie, wafahamishe, wajuulishe kwamba hakuna awezae kudhuru au kunufaisha isipokuwa Allaah, na kwamba hapana ajuae ghayb isipokuwa Allaah tu. Lakini kinachosikitisha ni kwamba bado wapo wasiotaka kufahamu wala kuambiwa.



Inafaa mtu ajiulize suali hili: "Je Rasuli mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kudai au kutufundisha kwamba du’aa zielekezwe kwake?"



Bila shaka hakupata hata siku moja kudai hayo, bali kauli zake zote ni dalili ya kuyakanusha hayo. Ndiyo maana siku ile Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipopanda mnyama pamoja na Ibni ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamwambia:



“Ewe kijana, mimi ninakufundisha maneno: Muhifadhi Allaah naye atakuhifadhi, muhifadhi Allaah siku zote atakuwa na wewe, ukiomba du’aa umuombe Allaah ukitaka msaada umuombe Allaah na ujue ya kwamba Ummah wote ukikusanyika ili wakunufaishe na kitu basi hawawezi kukunufaisha ila kwa kile ambacho Allaah ameshakuandikia, na wakikusanyika ili wakudhuru kwa jambo, basi hawawezi kukudhuru ila kwa kile ambacho Allaah keshakuandikia; kalamu zimekwishanyanyuliwa na wino umekwishakauka juu ya karatasi”. [Imepokewa na At-Tirmidhiy]



Hakumwambia Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba: "Ukiomba du’aa niombe mimi, na ukitaka msaada niombe mimi." Bali alimwelekeza kule kule kwa Mwenye Nguvu, Mwenye Uwezo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).



Anasema Imaam Ibn Qayyim Al-Jawziyyah (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake kiitwacho Zaad al-Maad, ukurasa wa tatu:



"Ninashuhudia kwamba Rasuli Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameletwa na Rabb wake kama Rasuli mingine, akiwa kiongozi wa wamchao Allaah ni rahmah kwa walimwengu. Akawaongoza watu katika njia iliyo sahihi na iliyonyooka. Allaah akawafaradhishia waja wake kumtii Rasuli huyu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kumuheshimu, kumpenda na akajaalia njia ya kuelekea kwenye Jannah yake ni moja tu, nayo ni kufuata njia yake Rasuli huyu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).



Akajaalia kudhalilika na kudharaulika kumfikie kila atakayekwenda kinyume na Rasuli huyu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).



Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Na akajaalia kudhalilika na kudharaulika kwa kila atakayekwenda kinyume na amri yangu na atakayejifananisha na kundi keshakuwa pamoja nao”. [Imepokewa na Imaam Ahmad]



Kwa hivyo watadhalilika waliomuasi na wataheshimika watakaomtwii na kumfuata Rasuli huyu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).



Allaah Anasema:

وَلَا تَهِنُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَنتُمُ الْأَعْلَوْنَ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٣٩﴾

Na wala msilegee na wala msihuzunike na ilhali nyinyi mko juu mkiwa ni Waumini. [Aali-‘Imraan: 139]



Na Akasema:

وَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَلَـٰكِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَا يَعْلَمُونَ﴿٨﴾

Na hali utukufu ni wa Allaah na wa Rasuli Wake na wa Waumini, lakini wanafiki hawajui. [Al-Munafiquun: 8]





Kutosheleza Na Kufuata



Anaendelea kuelezea Imaam Ibnu Qayyim Al-Jawziyyah katika kitabu chake hicho akisema: Allaah Anasema:



Na Akasema:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَسْبُكَ اللَّـهُ وَمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ﴿٦٤﴾

Ee Nabiy! Anakutosheleza Allaah na anayekufuata miongoni wa Waumini. [Al-Anfaal: 62]

Anaendelea kueleza Ibnul-Qayyim kwamba; katika Aayah hizi Allaahh Anamjuulisha Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba Allaah pekee anamtosheleza yeye pamoja na waliomfuata, na kwamba hawahitajii msaada wa yeyote mwengine isipokuwa wake Subhaanahu wa Ta’ala.



Katika Aayah nyengine Akasema:





الَّذِينَ قَالَ لَهُمُ النَّاسُ إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّـهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ ﴿١٧٣﴾

Wale walioambiwa na watu: “Hakika watu wamejumuika dhidi yenu, basi waogopeni.” Lakini iliwawazidishia iymaan wakasema: “Hasbuna-Allaah! (Allaah Anatutosheleza) Mzuri Alioje Mdhamini Anayetegemewa kwa yote.” [Aal-‘Imraan: 173]





Ukiichunguza Aayah hii utaona kuwa Waislamu hawakusema "Anatutosheleza Allaah na Rasuli wake". Bali walisema: "Allaah Anatutosha. Naye ni mlinzi bora kabisa".



Na ukiichunguza kauli ya Allaah (Subaahanahu wa Ta’aalaa) katika Suuratut-Tawbah: 59 Aliposema:



وَلَوْ أَنَّهُمْ رَضُوا مَا آتَاهُمُ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّـهُ سَيُؤْتِينَا اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ وَرَسُولُهُ إِنَّا إِلَى اللَّـهِ رَاغِبُونَ﴿٥٩﴾

Na lau wangeliridhiya yale Aliyowapa Allaah na Rasuli Wake, na wakasema: “Anatutosheleza Allaah, karibuni Allaah Atatupa katika fadhila Zake na Rasuli Wake (pia); hakika sisi kwa Allaah tuna raghba.” [At-Tawbah: 59]



Tazama jinsi Allaah Alivyomnasibisha Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika ‘kutoa’. Akatumia neno (Allaah Atatupa katika fadhila zake na Rasuli wake) kama katika kauli nyengine aliposema:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ

Na lolote analokupeni Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. [Al-Hashr: 7]



Lakini katika neno ‘kutosha’, utaona kwamba amejinasibisha Yeye peke yake Subhaanahu wa Ta’ala. Hakusema: ‘Anatutoshea Allaah na Rasuli wake’ bali amesema: ‘Anatutoshea Allaah’. Akakamilisha kwa kauli yake: ‘Hakika sisi tunaelekea kwa Allaah’. Akajaalia ‘kuelekea’ kuwe kwake tu, kama Alivyosema katika Suuratun-Nashrah:

فَإِذَا فَرَغْتَ فَانصَبْ ﴿٧﴾

Basi utakapopata faragha fanya juhudi katika ‘ibaadah.





وَإِلَىٰ رَبِّكَ فَارْغَب ﴿٨﴾

Na kwa Rabb wako elemea kwa raghba (kutakabaliwa). [Ash-Sharh: 7-8]



Kwa hivyo, kutegemea, kutosheleza, kuelekea ni kwake Allaah tu peke yake. Pia kusujudu, kuweka nadhiri, kuapa, yote haya yanaelekezwa kwake tu Subhaanahu wa Ta’ala. Ushahidi wa haya ni kauli yake Allaaah (Subhaanahu wa Ta’alaa):

أَلَيْسَ اللَّـهُ بِكَافٍ عَبْدَهُ ۖ

Je, kwani Allaah si Mwenye kumtosheleza mja Wake? [Az-Zumar: 36]



Kwa hayo tunatambua kuwa, kumshirikisha Allaah katika ‘ibaadah zake zozote zile, na kiumbe chochote kile baada ya kuzijua dalili zilizotangulia na zilizowazi kabisa, ni jambo lililo baatwil na la ufisadi.



Kwa ufupi, Allaah Anatutaka tumtegemee Yeye tu na Kumuomba Yeye tu, pamoja na kuelekeza ‘ibaadah zetu zote kwake Yeye tu, na Anatutaka tumfuate Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndipo utakapopatikana ushindi na utukufu na kusaidiwa na Allaah pamoja na maisha mema hapa duniani na Aakhera.



Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliapa akasema:

“Hatoamini mmoja wetu mpaka mapenzi yake kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yawe makubwa kupita mapenzi ya nafsi yake, na ya watoto wake na ampende Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko watu wote”.



Na Allaah Akaapa Akasema:



فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٦٥﴾

Basi Naapa kwa Rabb wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasipate katika nyoyo zao karaha katika yale uliyohukumu na wajisalimishe, kwa kujisalimisha kikamilifu. [An-Nisaa: 65]



Katika Aayah hii, Allaah Anatukataza kufuatwa amri isiyokuwa Yake Subhaanahu wa Ta’ala au ya Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).



Muislamu hana hiari ya kuchagua, kufuata au kutofuata baada ya kuijua hukumu ya Allaah au ya Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Bali Muislamu, lengo lake lote pamoja na mapenzi yake yote, yawe katika kufuata amri za Allaah na za Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).



Mwisho wa maneno ya Ibnul-Qayyim (Rahimahu Allaah).



Wasiylah

Nini maana ya Wasiylah?

Majibu:

Wasiylah katika lugha ya Kiarabu, maana yake ni njia au sababu inayoweza kukufikisha utakapo.

Na asili yake ni kauli yake Mwenyezi Mungu katika Qur-aan aliposema:



يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَابْتَغُوا إِلَيْهِ الْوَسِيلَةَ وَجَاهِدُوا فِي سَبِيلِهِ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣٥﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah na tafuteni njia za kumkurubia; na fanyeni jihaad katika njia Yake ili mpate kufaulu. [Al-Maaidah: 35]



Na katika Hadiythul-Qudusy Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:



“Hatojikurubisha kwangu mja wangu kwa jambo nilipendalo kuliko yale niliyomfaradhishia. Na mja wangu angali anaendelea kujikurubisha kwangu kwa ‘ibaadah za Sunnah mpaka nimpende...” [Imepokewa na Al-Bukhaariy]



Ama katika lugha ya Dini (katika Fiq-hi), neno 'Wasiylah' pia huwa na maana ya ‘amali njema anayoitanguliza mja kwa Rabb wake, kabla hajaomba du’aa au pamoja na du’aa ili du’aa yake ikubaliwe.



Katika kujisogeza huku kwa Rabb wao, baadhi ya Waislamu wakavumbua njia zisizo za kishari’ah ambazo badala ya kuwasogeza karibu na Rabb wao, huwa zinawabaidisha Naye. Kuna Wasiylah inayompeleka mtu katika shirki, na nyengine inampeleka mtu katika uzushi (bida’ah).





Mambo Yanayowababaisha Watu



Kujikurubisha Kwa Jaha (Heshima) Ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)



Kwanza kabisa; nini maana ya Jaha:



Jaha, katika lugha ya Kiarabu maana yake ni hishima. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema juu ya Nabii ‘Iysa ('Alayhis Salaam):



إِذْ قَالَتِ الْمَلَائِكَةُ يَا مَرْيَمُ إِنَّ اللَّـهَ يُبَشِّرُكِ بِكَلِمَةٍ مِّنْهُ اسْمُهُ الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ وَجِيهًا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَمِنَ الْمُقَرَّبِينَ ﴿٤٥﴾

Na pale Malaika waliposema: “Ee Maryam! Hakika Allaah Anakubashiria Neno (la Kun!) kutoka Kwake (umzae mtoto), jina lake ni Al-Masiyhu ‘Iysaa mwana wa Maryam, mwenye taadhima katika dunia na Aakhirah na ni miongoni mwa waliokurubishwa (kwa Allaah). [Aali ‘Imraan: 45]



Na juu ya Nabii Muusa ('Alayhis Salaam), Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) Anasema:



يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ آذَوْا مُوسَىٰ فَبَرَّأَهُ اللَّـهُ مِمَّا قَالُوا ۚ وَكَانَ عِندَ اللَّـهِ وَجِيهًا ﴿٦٩﴾

Enyi walioamini! Msiwe kama wale waliomuudhi Muwsaa, lakini Allaah Akamtoa tuhumani kutokana na yale waliyoyasema. Na alikuwa mbele ya Allaah mwenye kuheshimika. [Al-Ahzaab: 69]



Bila shaka (Jaha) hishima ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mbele ya Rabb wake ni kubwa kabisa. Lakini kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) akukubalie jambo lako kwa hishima ya Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) badala ya kumuomba akukubalie kwa nguvu Zake Allaah au kwa uwezo Wake au kwa ukarimu Wake n.k. huku ni kuyakimbia yale majina na sifa Zake tukufu Subhaanahu wa Ta’ala.







Kujikurubisha Kwa Baraka Za Mawalii



Nako ni kujisogeza kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa njia ya kwenda makaburini (makaburi ya mawalii) au njia zilizo kama hizo.



Hapana anayepinga kuwepo kwa Mawalii wa Allaah (Subhaanahu wa ta’aalaa), pamoja na makarama yao pale walipokuwa hai. Qur-aan na Sunnah zimezungumzia juu ya yote hayo. Lakini kwenda makaburini na kuwaomba maiti hao ili kupitia kwao uweze kuondolewa shida zako na Rabb wako, jambo hilo halijuzu kabisa na pana hatari ya kukuingiza katika kumshirikisha Allaah (Subhaahu wa Ta’aalaa) na kiumbe.





Kujisogeza Kwa Du’aa Iitwayo ‘Wasiylah’



Kuna baadhi ya watu hujisogeza kwa kusoma ‘Wasiylah’ - nayo ni du’aa maarufu iitwayo Asw-Swalaatu-Nnaariyah. Husomwa mara 4,444 ili kuondoa shida au dhiki. Inasemekana kwamba mmoja katika watu wema alioteshwa na kufundishwa du’aa hii.

Swalah yenyewe inasomwa hivi:



"Allahumma swalliy swalaatan kaamilah, wa sallim salaaman taammah ‘alaa Sayyidina Muhammad, alladhiy tanhallu bihil ‘uqad, watanfarij bihil kurab, watanqadhiy bihil hawaaij...” mpaka mwisho wake.



Maana yake ni: "Rabb wangu Swali Swalah iliyokamilika na umsalimie salaam iliyotimia Bwana wetu Muhammad, ambaye kwake yeye fundo zinafunguka na dhiki zinaondoka na haja zinatimia…” mpaka mwisho wa du’aa.



Ukiichunguza Swalah hii, utaona kwamba badala ya kuelekeza du’aa kwa Mwenyezi Mungu, inaelekezwa kwa Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kumpa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Hasa pale inaposemwa ‘kwake yeye fundo zinafunguka na dhiki zinaondoka’, na huku ni kumpa kiumbe sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).



Baadhi ya Ma’ulamaa wamesema laiti pale paliposemwa, alladhiy tanhallu bihil ‘uqad na maana yake ni ‘kwake yeye fundo zinafunguka’ pangesemwa tanhallu bihal ‘uqad; hapo maana yake inabadilika na kuwa ‘kwa kumswalia na kumsalimia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndiyo dhiki na shida zinaondoka’; na kwa vile kumswalia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ‘ibaadah ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametuamrisha.



Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:



إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾

Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini mswalieni na msalimieni kwa mamkizi ya amani na kwa tasliymaa. [Al-Ahzaab: 56]



Na kwa vile inajuzu kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa ‘ibaadah iliyo sahihi, kwa hivyo inajuzu kujikurubisha Kwa kumswalia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).



Ama kuielekeza du’aa yako kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) moja kwa moja au kumpa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sifa katika sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), hiyo haijuzu.







Kujisogeza Kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Kwa Amali Njema



Inajuzu kujisogeza kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) (Kutawassal) kwa ‘amali njema. Kwa mfano, mtu aseme:



"Ee Rabb wangu siku moja nilifanya jambo fulani jema, na sikulifanya jambo hilo ila kwa ajili ya kutaka ridhaa yako tu, kwa hivyo kwa ajili ya kitendo changu kile chema nakuomba unikubalie du’aa yangu hii".



Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitufundisha hayo katika Hadiyth iliyopokewa kutoka kwa Al-Bukhaariy na Muslim. Hadiyth hiyo imo katika kitabu cha Imaam An-Nawawiy kiitwacho Riyaadhus-Swaalihiyn (Hadiyth nambari 13) juu ya wale watu watatu walioingia pangoni kisha jiwe kubwa sana likaanguka na kuifunga njia yao ya kutokea. Kila mmoja wao aliomba kwa ‘amali njema yake na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akawafungulia njia yao.







Toba Ya Aadam ('Alayhis Salaam)

Kuhusu usemi wa baadhi ya watu kw

amba Nabii Aadam ('Alayhis Salaam) alipotubu aliomba asamehewe kwa Jaha ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hadiyth zilizoegemewa katika kuithibitisha hoja hii ni zile ambazo Ma’ulamaa wa Hadiyth wamezitaja kuwa ni maudhui (za uongo na hazina msingi wowote).





Qur-aan imekweshatujulisha juu ya du’aa aliyoiomba Aadam ('Alayhis Salaam). Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:



فَدَلَّاهُمَا بِغُرُورٍ ۚ فَلَمَّا ذَاقَا الشَّجَرَةَ بَدَتْ لَهُمَا سَوْآتُهُمَا وَطَفِقَا يَخْصِفَانِ عَلَيْهِمَا مِن وَرَقِ الْجَنَّةِ ۖ وَنَادَاهُمَا رَبُّهُمَا أَلَمْ أَنْهَكُمَا عَن تِلْكُمَا الشَّجَرَةِ وَأَقُل لَّكُمَا إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمَا عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿٢٢﴾

Basi akawachota (wote wawili) kwa ghururi. Walipoonja mti ule zikawafichukia sehemu zao za siri; na wakaanza kujibandika majani ya Jannah. Na Rabb wao Akawaita: “Je, kwani Mimi Sikukukatazeni mti huo na kukuambieni kwamba shaytwaan ni adui bayana kwenu?”



قَالَا رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٢٣﴾

Wakasema: “Rabb wetu! Tumedhulumu nafsi zetu, na basi Usipotughufuria na Ukaturehemu; bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” [Al-‘Aaraf: 22-23]



Natumai inafahamika hapa kwamba; Aadam na mkewe ('Alayhimas Salaam) waliomba toba moja kwa moja kwa Rabb wao bila kupitia njia nyingine.







Hadiyth Ya Kipofu



Kipofu mmoja alimwendea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: "Niombee du’aa ili Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) anijaalie niweze kuona.” Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Ukitaka nitakuombea na kama ukitaka subiri, kwani hiyo ni khayr kwako”. Yule kipofu akasema: "Bora niombee ili nipone". Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuamrisha atawadhe vizuri na aswali raka’ah mbili kisha aombe ifuatavyo: ”Rabb wangu mimi nakuomba na ninaelekea kwako pamoja na Rasuli wako, Rasuli wa Rahmah, Ee Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mimi naelekea Kwa Rabb wangu pamoja nawe katika haja yangu hii ili ikubaliwe. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) mkubalie du’aa yake kwa ajili yangu.)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy na Ahmad]. Hadiyth inaendelea: "Baada ya kuomba du’aa hii mtu yule akapona".





Jawabu



Baadhi ya watu imewakanganya Hadiyth hii, wakaona kwamba labda inajuzu kuomba kwa baraka au kwa Jaha ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hasa kwa vile kipofu yule alitumia neno: "Atawassal ilayka binabiyyika Muhammad, nabiyyi rahma". Maana yake ni: "Ninajisogeza kwako pamoja na Rasuli wako Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Rasuli wa Rahmah".



Ukiichunguza, utaona kwamba; tawassul hii imepangika kwa mambo mengi, na haiwi sahihi ila baada ya kupatikana kwa mambo hayo, na baadhi ya mambo hayo hayawezi kupatikana hivi sasa baada ya kufa kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mambo yenyewe ni haya yafuatayo:





a. Iwapo wakati huu mtu ataomba aseme:



"Ee Rasuli wa Allaah, muombe Rabb wako anikidhie haja yangu".

Kauli yake hiyo itakuwa ni batwili na ya upotevu. Kwasababu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hamsikii wala hamuoni na wala hatoweza kumuombea kama alivyoombewa kipofu yule.





b. Iwapo mmoja wetu atasema:





"Rabb wangu ninakuomba na ninaelekea kwako pamoja na Rasuli wako.”

Mtu huyo atakuwa muongo, maana Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hayupo ili aelekee naye na aombe du’aa pamoja naye. Kwasababu maneno hayo husemwa na aliyesimama na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mfano wa yule kipofu.

Kwa hivyo tawassul hiyo haifai, kwasababu ya kukosekana kwa nguzo muhimu, nayo ni du’aa ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa muombaji wa wasiylah.





Hadiyth Ya Kuomba Mvua





Hadiyth ifuatayo pia imewakanganya baadhi ya watu. Hadiyth hiyo inasema hivi:



’Umar bin Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu), alikuwa akimuomba Al-‘Abbaas Ammi yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati wa ukame na mvua ilikuwa ikinyesha.

Hadiyth inaendelea:

‘Umar bin Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa wakati wa ukame akimuomba Al’Abbaas Ibn ‘Abdul-Muttwalib na kusema:



"Rabb wetu tulikuwa tukikuomba kupitia kwa Rasuli wetu na ukituletea mvua, na sasa tunakuomba kwa njia ya Ammi yake ili utuletee mvua - Walikuwa wakinyeshewa mvua". [Imepokewa na Al-Bukhaariy]



Wamebabaika kwa kudhani kuwa kwa vile ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alisema:



"Sisi tulikuwa tukikuomba kupitia kwa Rasuli wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ukituletea mvua". Wakaona kuwa huu ni ushahidi kwamba ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akitawassal kwa jaha ya ‘Ammi yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa hivyo, haina lazima sisi kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Na kwa vile hapo mwanzoni ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akitawassal kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa nini basi na sisi tusiuombe kwa njia ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?





Jibu:



Kule kutawassal kwa Maswahaba wakati wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kulikuwa ni kwa kumuomba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awaombee du’aa. Naye Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba, na du’aa yake ilikuwa ikikubaliwa. Hadiyth hiyo kwa ukamilifu inasema hivi:



"Siku moja Mabedui walimuendea Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtaka awaombee du’aa ili mvua inyeshe, maana hata wanyama wao walikuwa wakifa kwa ukame. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akanyanyua mikono yake juu na kuomba, kabla ya kuishusha chini, mvua kali ilinyesha."





Shaykh Abuu Bakar Al-Jazairiy katika kuisherehesha Hadiyth hii katika kitabu chake kiitwacho “Itikadi ya Muislam” Aqiydatul-Muumin alisema:



Maswahaabah hawakuwa wakiomba kwa kuelekeza du’aa zao kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe, au kwa dhati yake au kwa jaha yake kama wanavyofikiria.





Kwa sababu ingelikuwa ni hivyo basi ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) asingemuomba Al-‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ili awaombee du’aa. Bali angeomba kwa Jaha ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikuwa amezikwa pale pale msikitini, karibu yake.



Lakini alielewa kuwa hivyo si sawa na sivyo alivyofundishwa na Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ndiyo maana baada ya kufa kwake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akaona ni vizuri kumtaka ‘Ammi yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awaombee, na alikuwa akiwaombea na kukubaliwa du’aa yao.





Na hii ni dalili kuwa inakubaliwa kumtanguliza mtu mwema ili aombe du’aa na wengine waitikie. Lakini haikubaliwi kumtanguliza maiti au asiyekuwepo na kusema: "Rabb wetu tunatawassal kwako kwa jaha ya fulani".





Maana huyo atakayetangulizwa anatakiwa awepo na anyanyue mikono yake juu na kuomba, wakati maiti au asiyekuwepo hawezi kufanya hivyo."



Mwisho wa maneno ya Shaykh Abu Bakar Al-Jazairiy.



Tunamaliza kwa kauli yake Subhaanahu wa Ta’ala katika Suuratul-‘Imraan, aayah ya 79 Aliposema:



مَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُؤْتِيَهُ اللَّـهُ الْكِتَابَ وَالْحُكْمَ وَالنُّبُوَّةَ ثُمَّ يَقُولَ لِلنَّاسِ كُونُوا عِبَادًا لِّي مِن دُونِ اللَّـهِ وَلَـٰكِن كُونُوا رَبَّانِيِّينَ بِمَا كُنتُمْ تُعَلِّمُونَ الْكِتَابَ وَبِمَا كُنتُمْ تَدْرُسُونَ ﴿٧٩﴾

Ni mustahili kwa mtu kwamba Allaah Amempa Kitabu na Al-Hukma na Unabii kisha awaambie watu: “Kuweni wenye kuniabudu mimi badala ya Allaah” Bali (atawaambia): “Kuweni Wanachuoni waswalihina kwa yale mliyokuwa mkiyafundisha ya Kitabu na kwa yale mliyokuwa
 
Maswali: Fiqhi


Nguzo Waajib Na Sunnah Katika Swalaah



Alhidaaya.com





Swali:



Ni vitendo gani katika Swalah ni Sunnah na vipi ni Fardhi? Nitashukuru mkinieleza kwa Salaa za rakaa mbili, tatu na nne.

Jazzakallahu Khayr



Jibu:



AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.



Maelezo bayana kuhusu swali lako na tutaja kuhusu yaliyo Sunnah katika Swalaah kwa sababu ni mengi ambayo yamegawanywa katika Sunnah za maneno (As-Sunnan Al-Qawliyyah) na Sunnah za vitendo (As-Sunnan Al-Fi'iliyyah) hadi baadhi ya ‘Ulamaa wanasema hizo Sunnah zinazidi 50.



Nguzo za Swalaah ni 14. Nguzo ni zile ambazo ukiswali na ukaziacha kwa makusudi Swalaah yako inabatilika, na ikiwa umeacha kwa kusahau, Swalaah yako pia itakuwa haikukamilika hadi urejee kitendo chenyewe au urejee rakaa na kisha mwishoni utoe Sajdatus-Sahw (Sajdah ya kusahau). Lakini ukiwa umesahau nguzo ya Takbiyratul-Ihraam, basi Swalaah yako basi itakubidi uiswali Swalah upya tokea mwanzo.





Nguzo Za Swalaah:





1. Kusimama katika Swalaah za fardh kwa yule mwenye uwezo. (Wanachuoni wengine wamesema nguzo ya kwanza ni Niyyah kabla ya Kusimama). Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ﴿٢٣٨﴾

Na simameni mbele ya Allaah katika hali ya utiifu [Al-Baqarah: 238]



Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:



"Swali hali ya kuwa umesimama, ukitoweza kwa kukaa na ukitoweza basi kwa kulala ubavu" [al-Bukhaariy na Abuu Daawuwd].





2. Takbiyratul-Ihraam (Takbira ya kuhirimia) kwa tamko la “Allaahu Akbar” kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Ufunguo wa Swalaah ni kuzitwaharisha, na kuifunga ni Takbiyra, na kuifungua ni kutoa Salaam" [Abuu Daawuwd na at-Tirmidhiy].





3. Kusoma Suwrah-Al-Faatihah katika kila rakaa. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hapana Swalaah kwa ambaye hakusoma Suwrah Al- Faatihah" [al-Bukhaariy].



4. Kurukuu.



5. Utulivu (Twumaaninah) katika Rukuu



6. I'itidaal (hapa inaingia na kunyanyuka kutoka katika Rukuu hadi anaponyooka mtu).



7. Utulivu katika I'Itidaal.



8. Kusujudu.



9. Utulivu katika kusujudu. Kutulia wakati wa kurukuu, kusujudu, kusimama, kukaa baina ya sijdah mbili kwa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Kisha rukuu mpaka utulizane hali ya kurukuu, kisha nyanyuka mpaka ulingane sawa hali ya kusimama, kisha sujudu mpaka utulizane na hali umesujudu, kisha nyanyuka mpaka utulizane hali ya kuwa umekaa" [al-Bukhaariy]



10. Kikao baina ya Sijda mbili.



11. Utulivu katika kikao baina ya Sijda mbili.



12. Tashahhud ya mwisho.



13. Kikao katika Tashahhud ya mwisho.



14. Salaam (Kutoa Salaam) ya kwanza.





Utahakikisha unafuatanisha yote hayo kama utaratibu ulivyopangika.





Waajib Za Swalaah:



Ni lile ambalo ni wajibu kulifanya au kusema, inaondoka kwa kusahau na kulazimisha mwenye kuswali kusujudu sijdah mbili za kusahau. Yeyote mwenye kuacha kwa kusudi Swalaah yake inabatilika ikiwa anajua uwajibu wake.

Istwilahi hii inatumika kwa madhehebu ya Hanafi na Hanbali ila ma-Hanafi hawaoni kuwa mwenye kuacha wajibu kwa kusudi inabatilisha Swalaah yake bali yeye amefanya madhambi anayostahiki adhabu. Ama ma-Maaliki na ma-Shaafi'y hawana kigawanyo hichi cha Waajib kwao ila wao wana nguzo na Sunnah kwa ujumla wake.



Hapa tutaweka yale yaliyotajwa ambayo yanaelekea kuwa na nguvu zaidi.



Kwanza kabla hatujataja mambo yenyewe, tunapaswa kujua kuwa mambo ya Waajib ni yale ambayo vilevile atakapoacha mtu kwa makusudi hubatilika Swalaah yake, na atakapoacha kwa kusahau inamtosheleza yeye kusujudu Sijda mbili za kusahau (Sujuwdus-Sahw).





Mambo ya Waajib ambayo yametajwa katika kitabu cha 'Swahiyhu Fiqhis-Sunnah' kwa dalili mbalimbali za Aayah na Hadiyth ni 9 kama yafuatayo:



1. Du'aa ya ufunguzi wa Swalaah (Du'aa al-Istiftaah).



2. Kusema:



أَعـوذُ بِاللهِ مِنَ الشَّيْـطانِ الرَّجيـم

A’uwdhu biLLaahi minash-shaytwaanir-rajiym



kabla ya kusoma

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

Na kabla ya Suwrah Al-Faatihah.





3. Kusema baada ya Suwrah Al-Faatihah:



آمين

Aamiyn



4. Takbiyrah za kuhama baina ya kitendo na kitendo.



5. Kusema:



سَمِـعَ اللهُ لِمَـنْ حَمِـدَه

Sami’a Allaahu liman hamidah



6. Kusema katika I'itidaal.





رَبَّنـا وَلَكَ الحَمْـدُ

Rabbanaa walakal-hamdu,



7. Kusema:



سُبْـحانَ رَبِّـيَ الْعَظـيم

Subhaana Rabbiyal ’Adhwiym



Wa kurukuu na kusema:



سُبْـحانَ رَبِّـيَ الأَعْلـى

Subhaana Rabbiyal A’-laa



Wakati wa kusujudu.





8. Tashahhud ya kwanza.



9. Kikao cha Tashahhud ya kwanza.





Wanachuoni wengine wametaja mambo ya Waajib ni 8 kama yafuatayo:





1. Takbiyrah nyingine zote isiyo ile ya Ihraam.



2. Kusema



سَمِـعَ اللهُ لِمَـنْ حَمِـدَه

Sami’a Allaahu liman hamidah



kwa Imaam na mwenye kuswali peke.





3. Kusema:



رَبَّنـا وَلَكَ الحَمْـدُ

Rabbanaa walakal-hamdu,





4. Kusema:





سُبْـحانَ رَبِّـيَ الْعَظـيم

Subhaana Rabbiyal ’Adhwiym





Mara moja kwenye kurukuu.





5. Kusema



سُبْـحانَ رَبِّـيَ الأَعْلـى

Subhaana Rabbiyal A’-laa



kwenye kusujudu.





6. Kusema:



اللّهُـمَّ اغْفِـرْ لي

Allaahummaghfir liy



Kwenye kikao baina ta Sijda mbili.



7. Tashahhud ya mwanzo.



8. Kikao katika Tashahhud ya mwanzo.



Hizi ndizo maarufu zaidi kwa wanachuoni wengine.





Sunnah Za Swalaah



Hizi ni kauli na vitendo zinazopendeza kuletwa katika Swalaah. Mwenye kufanya hayo hupata thawabu wala Swalaah haibatiliki kwa kuachwa hata kwa kusudi. Wala sijdah ya kusahau hailetwi. Hapa tuna vigawanyo viwili vya Sunnah katika Swalaah; Sunnah za kauli na Sunnah za vitendo.





Sunnah Za Kauli:



1. Kisomo baada ya al-Faatihah.



2. Adhkaar nyinginezo katika Rukuu.



3. Adhkaar baada ya kusimama kutoka katika Rukuu na baada ya kusema ‘Rabbana Lakal Hamd’.



4. Adhkaar nyinginezo katika Sujuud.



5. Du’aa baina ya Sijdah mbili.



6. Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Tashahhud ya kwanza na ya pili.



7. Du’aa baada ya Tashahhud ya kwanza na ya pili.



8. Salaam ya pili.



9. Adhkhaar na du’aa mbalimbali baada ya Swalaah.





Sunnah Za Vitendo:



1. Kuweka Sutrah (kizuizi mbele ya sehemu unayoswalia) katika Swalaah.



2. Kunyanyua mikono wakati wa Takbiyratul Ihraam, na wakati wa kurukuu na na wakayi wa kunyanyuka kwayo na wakati wa kuinuka kutoka katika Tashahhud ya kwanza. Na kadhalika wakati unapoinama na kuinuka.



3. Kuweka mkono wa kuume juu ya mkono wa kushoto juu ya kifua unaposimama kuswali.



4. Kutazama mahali pa kusujudu.



5. Kulingana sawa mgongo unaporukuu na kutonyanyua kichwa au kukiinamisha sana, na kuweka viganja kwenye magoti mawili na huku umeviachanisha vidole vya mikono na kuachanisha viwiko visiguse mbavu au tumbo lako.



6. Kuteremka katika Sijdah kwa mikono miwili kabla ya magoti.



7. Kuimakinisha paji la uso, pua na mikono (viganja viwili) kwenye ardhi pamoja na kupanua mikono isiguse mbavu zako; kuwe na uwazi wa kuweza kupita kinyama kidogo. Na viganja vyako viwe usawa wa mabega au masikio wakati uko katika kusujudu na viwiko vikiwa vimenyanyuliwa juu na vidole vya mikono vikiwa vinaelekea Qiblah. Matumbo ya vidole vya miguu yakiwa ardhini visigino vikielekea juu na hali vidole vya miguu vikielekea Qiblah.



8. Kulilalisha guu la kushoto na kulisimamisha la kulia wakati wa kikao baina Sijdah mbili.



9. Kurefusha kikao baina ya Sijdah mbili.



10. Kikao cha mapumziko baada ya kukamilisha rakaa ya kwanza na ya tatu.



11. Kutegemea ardhi kwa mikono wakati mtu anaponyanyuka kutoka kusujudu na kwenda kwenye rakaa nyingine.



12. Kukaa kikao cha Iftiraash (Kusimamisha mguu wa kulia na kukalia mguu wa kushoto) katika Tashahhud ya mwanzo. Na kukaa kikao cha Tawarruk (kusimamisha mguu wa kulia na kuipitisha mguu wa kushoto chini ya muundi wa mguu wa kulia na huku kikalio chako kimekaa juu ya ardhi).



13. Kuashiria kwa kidole cha shahada katika Tashahhud kuanzia mwanzo hadi mwisho bila kukishusha na huku unasoma na ukikitazama.



[Abu Maalik Kamaal Saalim, Swahiyh Fiqhus Sunnah, Mj. 1].





Na Allaah Anajua zaidi
 
Maswali: Fiqhi


Maiti Kukamuliwa – Ameusia Asikurubishwe Na Moto



Alhidaaya.com





Swali:



Assalamu alaikum warahmatullahi,



Hivi majuzi niliandika wasia wangu kama alivyo amrisha Allaah na Nabiy wake. Katika wasia wangu niliandika kuwa maiti yangu isikurubishwe moto hata pale nitakapo kuwa nimekwa chumbani katika kuoshwa na kukafiniwa. Watu wangu wakaniuliza jee pale tutakapo kukamua, tukufukize vipi? Sasa suala langu Mashekhe wangu liko hapa. Huku kukamuliwa, je ni mila, au ni madhehebu au ni sunnah?





Jibu:



AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.



Vitabu mbalimbali maarufu vya Fiqhi kama Al-Mulakhkhasw al-Fiqhiy cha Shaykh Dkt. Swaalih Fawzaan aal-Fawzaan, na pia Swahiyh Fiqhis Sunnah cha Shaykh Abuu Maalik Kamaal Sayyid Saalim.



Vitabu hivi ambavyo tumevitaja na vyenginevyo vinatueleza njia ambayo inafaa kufuatwa ili kumtayarisha Muislamu aliyekufa kwa mazishi. Katika moja wa njia hiyo ni kukamuliwa maiti ili kukamilisha tendo la kuoshwa, kuswaliwa na kisha kuzikwa. Waislamu na hasa wanazuoni hawakubaliani katika jambo la batili. Lakini fahamu kuwa kukamuliwa huko si kukamuliwa kama wanavyofanya baadhi ya watu au vitabu vinavyosema kuwa anakamuliwa kwa nguvu, na hadi wengine wanamkunja maiti na kuminya tumbo lake na kulikamua kwa nguvu hasa. Hayo ni makosa. Lililo sahihi ni kumkamua kwa upole, ni kama unalipapasa tumbo lake na kulibonyeza kwa upole na utaratibu na kama kipo choo kitatoka na kama hakipo basi hakipo wala hakuna haja yoyote ya kumbana, kumminya, na kumpinda kama wengine wanavyofanya kutokana na mafundisho ya baadhi ya Mashaykh na vitabu.



Muislamu aliye hai anafaa kujisafisha na kuondoa uchafu kwa juhudi yake kubwa. Lakini pindi anapofariki huwa hawezi kujitwahirisha wala kujisafisha hivyo inafaa walio hai wamkirimu kwa kumsafisha na kumtayarisha kwa ajili ya mazishi. Katika kumsafisha ni kumtoa uchafu ulio ndani ya matumbo. Na inafaa tufahamu kuwa kukamuliwa huko kunafanywa kwa taratibu ili asiumizwe kwa njia yoyote ile.



Ama kutumiwa kwa moto si jambo lenye kupendeza wakati wowote ule, lakini kwa kama kuna harufu au kunachelewa hilo, basi kunaweza kuchomwa udi au kupulizwa vinukiavyo ili kuondoa harufu mbaya iliyo katika chumba anachooshewa maiti.



Kwa faida zaidi ya mas-alah ya maiti, ingia kwenye viungo vifuatavyo:



Yampasayo Maiti



Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti





Na Allaah Anajua zaidi.
 
Mume Kupokea Maiti Ya Mkewe Kaburini Akiwa Ametoka Kwenye Kitendo Cha Ndoa Kabla Ya Kufariki Mkewe



Alhidaaya.com



Swali:



Asalam Alaykum warahmatulah swali langu linahusu kupokea mayti ndani ya kaburi je mume aliyefiwa na mke anaruhusiwa kupokea maiti hiyo iwapo alishiriki tendo la ndoa na mkewe muda mfupi kabla ya kufa kwa mkewe?





Jibu:



AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.



Kwa hakika jambo hilo limekatazwa kama zinavyoonyesha Ahaadiyth zifuatazo:



Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anasimulia kuwa, "Tulikuwa pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati bint yake anazikwa. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa anavujwa na machozi yakimiminika kwenye mashavu yake na akauliza, "Je, kuna kati yenu aliyefanya kitendo cha ndoa na mkewe usiku? Abu Twalhah akajibu, “Mimi sikufanya Ee Mjumbe wa Allaah.” Kisha Nabiy ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuamrisha ashuke ndani ya kaburi lake (la binti yake Nabiy) na kumzika." [Al-Bukhaariy].



Naye Imaam Ahmad katika riwaya nyingine kasimulia wka maneno yaliyo tofauti kidogo hivi: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: "Mtu aliyefanya tendo la ndoa na mkewe, hapaswi kuingia kwenye kaburi lake."



‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakuingia kwenye kaburi la mkewe.



Kwa hiyo wataingia wale Mahaarim wake au watu wowote wengine.





Na Allaah Anajua zaidi
 
Shari’ah Inasemaje Kuhusu Mke Kuzikwa Bila Mume Aliye Safarini Kujulishwa



Alhidaaya.com



Swali:



Mm niliwahi kufunga ndoa na mtoto wa Baba yangu mdogo, faida ya ndoa hiyo nilipata watoto 3, kutokana na maisha nilianza kusafili mpaka leo hii, kwa bahati mbaya mungu alipanga kumchukua kiiumbe chake yani ni mke wangu, baada ya kufaliki malehemu alizikwa bila kufahamishwa mm mume wa mke. Je shelia inasemaje kwa swala hili.





Jibu:



AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.



Inafaa mume ajulishwe pindi mkewe anapoaga dunia ikiwa yuko mbali au karibu. Na vile vile mke anafaa ajulishwe pindi mumewe anapofariki.



Kutojulishwa huko kwaweza kuwa kunatokana na kusahamu kwa sababu ya mshtuko kwa kuondokewa na kipenzi chao au hawakuwa na mawasiliano nawe kwa kuwa ulikuwa safari. Inabidi tuwe na dhana nzuri baina yetu. Ama kule kuzikwa kwa mkeo kutakuwa ni sawa kwani Muislamu anapoaga dunia anafaa azikwe haraka asiwe ni mwenye kucheleweshwa.



Ni nasaha zetu kwako uwasamehe hao waliokosa kukuarifu kwa kuwapatia udhuru.





Na Allaah Anajua zaidi
 
Siku Za Kiislamu Zinaanzia Saa Ngapi?



Alhidaaya.com





Swali:



Siku kwa waislam inaanza na kwisha saa ngapi?





Jibu:



AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.



Siku za Kiislamu zinaanza kuhesabika jua linapozama yaani wakati wa Magharibi hivyo kama mfano leo ni siku ya Alkhamiys na Magharibi inapoingia, basi usiku huo huitwa tena Laylatul-Jumu'ah (Usiku wa Ijumaa) na hali kadhalika kwa masiku mengine.



Na si saa sita ya usiku kama ilivyo hali ya siku au tarehe za ki-Gregorian ambayo ni marekebisho ya tarehe zilizokuwa zikijulikana zamani kama tarehe za ki-Julian ambazo ndizo zinazotumika katika ulimwengu leo hii. Nazo hujulikana zaidi kwa wengi kama tarehe za kikristo au tarehe za kizungu!



Kubadilika huko kwa siku za Kiislam wakati wa Magharibi, ni kwa sababu tarehe za Kiislam hufuata mwezi na hazifuati jua kama ilivyo hali ya tarehe nyinginezo. Na ndio maana Waislamu huanza kuswali Swalaah ya taaarawiyh usiku huo huo wa kuandama mwezi kabla ya kuanza Swawm kwa vile usiku huo umeshaingia kuwa ni wa mwezi wa Ramadhwaan.





Na Allaah Anajua zaidi
 
Vipi Kutia Niyah Ya Ibaada?
Maswali: Fiqhi







SWALI:

tunatakiwa tufunge sunna mbali mbali kamav vile sunna za jumatatu na alkhamis hususa kwale mabarubaru ili kupunguza matamanio ya nafsi pamoja na kumcha Allah.Je katika funga kama hizo za jumatatu na alkhamis tunatakiwa tunuie vipi? Naomba nia yake kwa matmshi ya kwiswahili










JIBU:

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa ba’ad:

Niya ni muhimi katika kitendo chochote cha ibada na hakuna ikhtilaaf baina ya Maulamaa kuhusu hili. Na hii ni rai ya Maalik, Ahmad ibn Hanbal na Abu Daawuud kwa kutoa dalili ya Aayah:

((وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ))

((Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Allaah kwa kumtakasia Dini)) [Al-Bayyinah: 5]



Kumaubudu Allaah سبحانه وتعالى Pekee kwa ikhlaas ni kitendo katika moyo, nacho ndio nia na amri katika Aayah hiyo inaonyesha kuwa ni fardhi.

Vile vile katika Sunnah Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema katika Haidiyth iliyopokelewa na 'Umar ibnul-Khatwaab رضي الله عنه

((إِنَّما الأَعْمَالُ بالنِّيَّاتِ وإنَّما لكُلِّ امْرِىءٍ ما نَوَى)) البخاري و مسلم



((Vitendo vinategemea (vinalipwa kwa) nia na kila mtu atapata kwa mujibu wa kile alichokusudia))

[Al-Bukhaariy na Muslim]

Lakini inapasa kutambua kwamba niya ya ibada yoyote kama ni kujitia tohara, wudhuu, tayammum, Swalah, Swawm, kutoa Zakaah na kadhalika haitamkwi kwa sauti bali huwekwa moyoni. Niya inaunganika na elimu. Ikiwa mtu anajua anachotaka kufanya basi tayari niya yake imeshaingia moyoni.

Kuitamka kwa sauti itakuwa sio kufuata mwendo wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم au Maswahaba zake, kwa hiyo kuitamka kwa sauti itakuwa ni Bid'ah (uzushi). Na kama ingelikuwa ni jambo lililokuwepo katika sheria basi Mtume صلى الله عليه وآله وسلم angeliwafundisha Maswahaba zake na mafunzo hayo yangelitufikia sisi pia kwani Niya ni jambo ambalo lina uhusiano na kila ibada ya Ummah huu; mchana na usiku kwa hiyo ingelikuwa ni muhimu kutaja kwa sauti asingeliacha kutoa mafunzo.

Kutamka Niya kwa sauti ni jambo lisokuwa na mantiki, kwani mtu anapotaka kufanya jambo la kawaida huwa hasemi kwa sauti kuwa "mimi nataka kufanya jambo fulani", bali hutia niya yake moyoni na kujitayarisha kwa kila njia na wakati maalum hadi atimize jambo lake. Kwa mfano mtu anapotaka kutoka nyumbani kwake na tuseme yuko peke yake, basi hatosema kwa sauti kuwa 'Mimi natoka kwenda kwa fulani" Au "natoka kwenda mahali fulani" Na Allaah سبحانه وتعالى ni Mwenye mifano bora.

Tutatumbue kuwa jambo hili limejulikana sana kutokana na mafunzo yasiyo sahihi tuliyoyapata kutoka kwa wazazi wetu au waalimu kwamba Niya hutajwa kwa sauti. Kama mfano tunapotaka kuswali mtu hutia Niya kwa sauti kwa kusema: "Nawaytu Fardha Swalaat Adh-Dhuhr Arba'a Rakaat LiLLaahi Ta'ala……" na kadhalika. Na kwa wengi wetu tunapoambiwa kinyume na hivyo hushangaa na hata kwa wengine huwa ni vigumu kukubali mafunzo sahihi. Kuna baadhi ya sehemu hadi sasa, wanaona wasipokwenda msikitini mwezi wa Ramadhaan kunuizwa na Imaam (Nawaytu Swawma Ghadin...) basi wanaamini kuwa kesho hawana Swawm kwa kukosa kunuizwa siku hiyo!! Huo ni ujahili wa dini, na ni jambo ambalo linatakiwa liachwe lisizidi kupoteza wengi maskini wasio na elimu ya dini yao.

Basi inampasa Muislamu aliyezoea kuweka niya kwa sauti ajirekebishe na kuweka niya moyoni katika ibada zake zote, kutokana na mafunzo haya sahihi tunayoyaeleza pamoja na dalili zake.

Na Allaah Anajua zaidi
 
Wakristo Wanauliza Kwanini Wanaume Wanaruhusiwa Kuoa Wake Wengi Na Wanawake Hawaruhusiwi?



Alhidaaya.com





Swali:


Swali hili nanukuu kutoka kwa wakristo wauliza kuwa sisi waislamu imeruhusiwa kisheria mwanaume wa kiislamu kuowa mke zaidi ya mmoja. Je, inaswihi mwanaume kufunga ndowa na wanawake 2-3 kwa siku moja? Natanguliza shukran zangu kwenu katika ujenzi wa Ummah.



Wabillah Tawfiiq




Jibu:



AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.


Hakika Muislamu anaruhusiwa kufunga ndoa sio tu siku moja bali wakati mmoja kwa wanawake wawili hadi wanne bila pingamizi wala tatizo lolote lile. Pia waeleze Wakristo waliokuuliza kuwa swali hilo pia ni sawa kwao nao wanaruhusiwa kufanya hivyo bila ya kuwa na pingamizi kutoka katika Biblia.


Hilo la kuoa wake wengi limepatikana kwa Manabii na wateule wa Allaah walioelezewa katika Biblia mfano wa Ibrahimu, Yakobo, Muwsaa, Suleimani na wengineo. Hakika ni kuwa Suleimani alikuwa na wake mia saba.



Ndoa imetajwa na kuhimizwa katika Biblia lakini hakuna hata msitari mmoja ambao unasema uke wenza haufai katika hii dunia. Bali Biblia inaashiria kuwa watu walio bora kama Manabii na Rusuli walikuwa na wake zaidi ya mmoja.



Katika kuwa katika uke wenza yapo masharti ambayo yanafaa kutimizwa. Biblia inatueleza hilo: "Ikiwa mwanamme fulani ana wake wawili naye anampenda mmoja kuliko mwingine. Nao wanawake hao wamemzalia watoto wa kiume, na mtoto wa kwanza kuzaliwa ni wa yule mama asiyempenda" (Kumbukumbu la Sheria 21: 15).


Biblia inatueleza kuwa Ibrahimu (Abramu) alikuwa na wake watatu kama tunavyoelezwa: "…na Sarai mkewe Abramu…" (Mwanzo 11: 31).



Tena: "Kisha, Sarai akampa Abramu Hagari, mtumwa wake wa kike, Mmisri, awe mke wake" (Mwanzo 16: 3).



Na pia: "Abrahamu alioa mke mwingine, jina lake Ketura" (Mwanzo 25: 1). Naye Ya'quub (Yakobo) alikuwa na wake wanne kama tunavyoarifiwa na Biblia: "Kisha Yakobo akamwambia Labani, 'Muda wangu umetimia, kwa hiyo nipe mke wangu'. … Lakini jioni, Labani akamchukua Lea, binti yake mkubwa, na kumpeleka kwa Yakobo. Yakobo akalala naye" (Mwanzo 29: 21 – 23).



Pia: "Na Yakobo alipomtimizia Lea siku zake saba, Labani akampa Raheli, binti yake mdogo awe mke wake" (Mwanzo 29: 28).


Tena: "Kwa hiyo Raheli akampa Yakobo mtumishi wake, Bilha, awe mkewe, naye akalala naye" (Mwanzo 30: 4).



Pia: "Lea alipoona ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mtumishi wake wa kike, na kumpa Yakobo ili awe mkewe" (Mwanzo 30: 9).



Biblia inatufahamisha tena kuwa kumbe anayefaa kuwa na mke mmoja ni askofu kumaanisha asiyekuwa askofu anaweza kuwa na zaidi ya mmoja. Hebu tusome: "Basi, askofu anapaswa kuwa mtu asiye na lawama; anapaswa awe na mke mmoja tu, awe mwenye kiasi, nidhamu na utaratibu" (1 Timotheo 3: 2). Hatujui kwa nini maaskofu wa Kikatoliki hawaruhusiwi kuoa kabisa?


Mwengine anayefaa kuwa na mke mmoja ni mzee wa Kanisa kama tunavyoarifiwa: "Mzee wa Kanisa anapaswa kuwa mtu asiye na hatia; aliye na mke mmoja tu, na watoto wake wanapaswa kuwa waumini" (Tito 1: 6).



Lakini pia inatakiwa katika Uislamu wanawake wanapoolewa wafanyiwe ihsani, watendewe wema na uadilifu. Hawafai kuwadhulumu na ikiwa huwezi kufanya hivyo unatakiwa uoe mwanamke mmoja pekee.



Ingia katika viuongo vifuatavyo kupata maelezo zaidi na hikma za wanaume kuruhusiwa kuoa zaidi wa mke mmoja:



Wanaume Kuoa Wake Wanne Na Wanawake Kuolewa Na Mume Mmoja



Hikma Ya Ruhusa Ya Ukewenza





Na Allaah Anajua zaidi
 
Back
Top Bottom