Ramadhan Special Thread
Talha bin Ubaidullah r.a amesimulia kuwa Rasulillah swallallahu alaih wasallam amesema " Hakika ninaijua Kalimah ambayo kama itasomwa na mtu anayekata roho,itakuwa ni sababu ya kufarijika (kupata raha) kwa roho yake mpaka itoke mwilini mwake,na itakuwa ni nuru kwake siku ya kiama (kalimah hiyo ni Laa ilaha illallah)


Anas radhiallahu anhu amesimulia katika hadith ndefu kwamba Rasulillah swallallahu alaih wasallam amesema " Atatolewa kutoka motoni kila mtu ambaye ametamka Lailaaha illallahu,na moyoni mwake kuna wema (imani) ambao ni sawa na uzito wa chembe ya shairi.

Baada ya hao ,atatolewa kutoka motoni kila mtu ambaye ametamka Lailaaha illallahu na moyoni mwake kuna wema (imani) ambayo ni sawa na uzito wa chembe ya ngano. Baada ya hayo atatolewa kutoka motoni ambaye ametamka Lailaaha illallahu,na moyoni mwake kuna wema sawa na uzito wa chembe ya vumbi

Hapa tunaona kwamba hakika kalimah itawaokoa watu kutoka motoni baada ya kupata adhabu yao,kwa maana hakuna muislamu ambaye aliamini juu ya Mungu mmoja japo imani yake ndogo kiasi gani ambaye atakaa motoni milele

Watakao kaa motoni milele ni wale wote ambao hawamuamini Mungu Mmoja,na wanasema Allah ana mtoto na mambo kama hayo,wanasema Allah ana nafsi tatu na mfano wa watu hao na wale wote wanao mshirikisha kwa namna moja au nyingine


Miqdad ibn Aswad r.a amesimulia ; Nimemsikia Rasulullah s.a.w anasema " Haitabaki nyumba yoyote duniani ,iliyotengenezwa kwa tope (udongo) au ngozi ya ngamia isipokuwa Allah ataingiza humo Kalimah ya Uislamu,kwa heshima kubwa na mapenzi au kwa utiifu na unyenyekevu,au Allah atawatukuza wao kwa kuwaafanya kuwa ni miongoni mwa watu wa Kalimah,au kuwadhalilisha wao kwa kuwafanya waishi wakiwa chini ya Uislamu
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



079-Yaliyoharamishwa Kwa Mwenye Hedhi Na Nifasi



Alhidaaya.com





1- Kuswali



Maulamaa wote wamekubaliana kwamba ni haramu kwa mwenye hedhi au nifasi kuswali, sawasawa ikiwa ni Swalaah ya faradhi au ya Sunnah. Wamekubaliana kwamba ufaradhi wa Swalaah huporomoka, na kuwa hatozilipa atakapotwaharika. [Al-Majmu’u ya An-Nawawiy (2/351) na Al-Muhallaa (2/175) ya Ibn Hazm].



Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd akisema, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( أليس إذا حاضت لم تصل ولم تصم؟ فذلك نقصان دينها))

((Je, si anapopata hedhi haswali wala hafungi? Basi hilo ni upungufu wa Dini yake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1951), Muslim (80) na wengineo].



Na imepokelewa na Mu'aadhah kwamba mwanamke mmoja alimwambia ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha):

"Je, inamtosheleza mmoja wetu Swalaah yake anapotwaharika?" Akamjibu: "Je, wewe ni Mharuriyah? Sisi tulikuwa tukiingia hedhini tukiwa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hakuwa akituamrisha, au akasema: Hatuiswali". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (321) na Muslim (uk. 265)].



“Mharuriyah”, ni sifa ya mwenye kufuata madhehebu ya Khawaariji. Baadhi yao walikuwa wakiwajibisha kulipa Swalaah kwa mwenye hedhi.



Faida



1- Mwanamke akiingia hedhini muda mfupi kabla ya kuingia Swalaah ya alasiri kwa mfano, na hakuwa ameswali adhuhuri, je itamlazimu alipe Swalaah ya adhuhuri baada ya kutwaharika?



Ikiwa kwa mfano itamjia muda mfupi kabla ya alasiri na hakuwa ameswali adhuhuri, basi atailipa Swalaah hiyo ambayo ilimwajibikia kabla ya kupata hedhi wakati anapotwaharika. Hii ndio rai ya Jamhuri ya Maulamaa. Sababu ni kuwa Swalaah ilikuwa imemwajibikia, na ni lazima ailipe madhali wakati wake uliingia hali ya kuwa yuko twahara kwa kiasi cha rakaa.



Hii ni kwa Neno Lake Allaah Mtukufu:

((إنَّ الصَّلاةَ كَانَتْ عَلَى المُؤْمِنِينَ كِتَاباً مَّوْقُوتا))

((Hakika Swalaah ina wakati wake maalumu kwa Waumini)). [An-Nisaa (4:103)]



Kuna kauli nyingineyo isemayo kwamba haimlazimu kuilipa adhuhuri. Wenye kusema hivi wanatoa dalili inayoashiria kuwa wanawake wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), walikuwa wakipata hedhi nyakati zote, lakini haikupokelewa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru mwanamke yeyote kuswali Swalaah iliyompita kabla ya kupata hedhi anapotwaharika.



Shaykh wa Uislamu anasema katika Al-Fataawaa (23/235):

"Dalili yenye nguvu zaidi ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Maalik isemayo kuwa halazimiwi na chochote, kwani kulipa kunapasa kwa jambo jipya, na hapa hakuna lolote linalompasa kulipa, mbali na kuwa alichelewesha ucheleweshaji usio wa kuzembea. Ama aliyelala hata kama hakuzembea, basi analolifanya si kulipa, bali huo ni wakati wa Swalaah yake wakati anapoamka na akakumbuka."



2- Anapotwaharika mwenye hedhi muda mfupi kabla ya alasiri kwa mfano, kisha baada ya kuoga wakati wa alasiri ukawa umeshaingia, je, ni lazima aswali adhuhuri?



Anapotwaharika na hedhi na nifasi kabla ya kuingia magharibi, itamlazimu aswali adhuhuri na alasiri za siku hiyo. Vile vile, anapotwaharika kabla ya kuchomoza alfajiri, itamlazimu aswali magharibi na ‘ishaa za usiku huo kwa vile wakati wa Swalaah ya pili ndio wakati wa Swalaah ya kwanza katika hali ya udhuru. Katika Al-Fataawa 2/334, Shaykh wa Uislamu anasema:



"Na kwa haya, ndivyo yalivyo madhehebu ya Jamhuri ya Maulamaa kama Maalik, Ash-Shaafi'iy na Ahmad, na kwamba mwenye hedhi anapotwaharika mwishoni mwa mchana, atazisali adhuhuri na alasiri. Na anapotwaharika mwishoni mwa usiku, ataswali magharibi pamoja na ‘ishaa. Na hivi ndivyo ilivyonukuliwa toka kwa ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf, Abu Hurayrah na Ibn 'Abbaas, kwa vile wakati ni mmoja kati ya Swalaah mbili katika hali ya udhuru. Hivyo basi, akitwaharika mwishoni mwa mchana, wakati wa adhuhuri hubakia na ataiswali kabla ya alasiri. Na akitwaharika mwishoni mwa usiku, basi wakati wa magharibi hubakia katika hali ya udhuru na ataiswali kabla ya ‘isha. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.



2- Kufunga



Imekubalika kwa Ijma’a ya Maulamaa kuwa mwenye hedhi na nifasi hafungi, lakini atazilipa siku za Ramadhwaan. ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) amesema:

"Hilo lilikuwa likitupata (hedhi) na tunaamrishwa kulipa swawm, lakini hatuamrishwi kulipa Swalaah". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (265) na Abu Daawuud (263)].



Faida



1- Mwenye hedhi akitwaharika kabla ya alfajiri na hakuoga, je, atafunga?



Ikiwa mwenye hedhi atatwaharika kabla ya alfajiri na akanuia kufunga, basi Swawm yake ni sahihi, kwani kusihi kwa swawm yake hakutegemei kuoga, kinyume na Swalaah. Na hii ni kauli ya Jamhuri. [Fat-h Al-Baariy (1/192)]



2- Akitwaharika mwenye hedhi kabla ya kuchwa jua, je, atajizuia kula muda uliobakia?



Si lazima ajizuie kula mchana uliobakia, kwani alikwishafungua tokea mwanzo, lakini siku hiyo atailipa. Imepokelewa toka kwa Ibn Jaryj akisema: "Nilimwambia 'Atwaa: Mwanamke akiingia hedhini, kisha akatwaharika sehemu ya mchana, je atakamilisha? Akasema: Hapana, bali atalipa". [Isnadi yake ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdur Raaziq katika Al-Musannaf (1292) kwa Sanad Swahiyh].



3- Kumwingilia (kumjimai)



Maulamaa wote wamekubaliana kwamba haijuzu kumwingilia mwanamke mwenye hedhi katika utupu. [Al-Muhalla (2/162), Majmu’u Al-Fataawaa (21/624) na Tafsiyr At-Twabariy (4/378)]



Allaah Mtukufu Ameliharamisha hilo katika Kauli Yake:

((فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي المَحِيضِ))

((Basi waepukeni wanawake katika hedhi)). [Al-Baqarah (2:222)]



Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

(( اصنعوا كل شيئ إلا النكاح))

((Fanyeni kila kitu isipokuwa kujimai)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (203), Abu Daawuud, An-Nasaaiy, At-Tirmidhiy na Ibn Maajah].



Shaykh wa Uislamu katika Al-Fataawaa (21/624) anasema:

"Kumwingilia mwenye nifasi ni kama kumwingilia mwenye hedhi, na hilo ni haramu kwa makubaliano ya Maimam.



Faida



1- Ikiwa Muislamu ataitakidi kuwa ni halali kumwingilia mwanamke mwenye hedhi katika utupu wake, basi atakuwa ni kafiri aliyeritadi. Na lau kama mtu atalifanya hilo bila kuitakidi kuwa ni halali; ima kwa kusahau au kutojua kuwepo hedhi, au hajui kuwa hilo ni haramu, au akalazimishwa, basi hana makosa, na wala hatoi kafara. Na ikiwa atamwingilia kwa kukusudia akijua kwamba mkewe yuko mwezini na kuwa hilo ni haramu na bila kulazimishwa, basi atakuwa ametenda dhambi kubwa, na ni lazima atubie. [An-Nawawiy katika Sharh Muslim (3/204).



Na je, atawajibika kutoa kafara kwa kufanya hivyo?



Jamhuri ya Maulamaa – kinyume na Ahmad – wanasema kuwa hapaswi kutoa kafara.



Ninasema: "Hili ndilo sahihi. Ama Hadiyth ya Ibn 'Abbaas aliyoipokea toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa anasema kuhusiana na mtu anayemwingilia mkewe akiwa hedhini kwamba ((Anatoa swadaqah dinari moja au nusu dinari)), basi Hadiyth hii ni Dhwa’iyf kwa kauli yenye nguvu, nayo imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (264), An Nasaaiy (1/153), na Ibn Maajah (640).. Na kuchukua mali ya Muislamu ni haramu kiasili, na si halali kuitwaa mali hiyo ila kwa matni.



2- Kinachokatazwa kustarehe na mwenye hedhi ni tupu yake basi. Mume anaruhusiwa kumchezea popote atakapo isipokuwa kuingiza dhakari yake katika utupu. [Ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Ahmad na Is-haaq. Pia Muhammad bin Al-Hasan na Atw-Twahaawiy katika Mahanafi, na baadhi ya wafuasi wa Maalik. Vile vile ni moja ya kauli mbili za Ash-Shaafi'iy. Aidha, limeungwa mkono na Ibn Al-Mundhir na An-Nawawiy (Fa-th Al-Baariy) (1/404). Ni madhehebu ya Ibn Hazm vile vile].



Na dalili ya hilo ni Hadiyth ya Anas. Anasema kwamba iliposhuka Kauli Yake Allaah Mtukufu:

((فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي المَحِيضِ))

((Basi waepukeni wanawake katika hedhi)), hapo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

((اصنعوا كل شيئ إلا النكاح))

((Fanyeni kila kitu isipokuwa kujimai)). [Tumeitaja milango iliyopita].



Na imepokelewa toka kwa baadhi ya wakeze Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakisema:

"Alikuwa anapotaka kitu kwa mwenye hedhi, hutupia nguo juu ya utupu wake". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (272) kwa Sanad Swahiyh].



Ninasema: "Lenye kutilia nguvu zaidi kauli hii ni Hadiyth ya Masruuq. Alimwambia Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha): "Ninataka kukuuliza jambo lakini naona hayaa. Akasema: Mimi ni mama yako, na wewe ni mwanangu. Akasema: Ni jambo lipi ambalo mtu anaweza kulifanya kwa mkewe akiwa hedhini? Akasema: Anaweza kufanya mambo yote, isipokuwa utupu wake". [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Atw-Twabariy katika ((At-Tafsiyr)) (4/378) kwa Sanad Swahiyh, nayo ina njia kadhaa].



Na hakuna shaka kuwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) ndio mjuzi zaidi wa hukmu ya suala hili, kwa kuwa yeye ndiye mke wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.



Tanbihi



Kauli nyingine ya Maulamaa inasema kuwa linalojuzu kwa mwanamume kustarehe na mkewe wakati wa hedhi ni kila kitu, isipokuwa sehemu iliyopo kati ya kitovu na magoti. Kauli hii ina dalili zake, lakini kauli ya kwanza ndiyo yenye nguvu zaidi. Na Allaah Mtukufu Ndiye Ajuaye Zaidi.m [Haya ni madhehebu ya Maulamaa wengi. Angalia kwenye Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/140) na kurasa zinazofuatia ukipenda].



3- Mwanamke anapotwaharika hedhi, haijuzu kwa mumewe kumwingilia mpaka aoge. Allaah Mtukufu Anasema:

((ولا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّى يَطْهُرْنَ فَإذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّهُ))

((Wala msiwakurubie mpaka watwaharike, na wanapotwaharika, basi waingilieni pale Alipowaamrisheni Allaah)). [Al-Baqarah (2:222)]



Mujaahid anasema: "Wanawake wana twahara mbili; twahara ya Kauli Yake Allaah Mtukufu:



((حَتَّى يَطْهُرْنَ))

Yaani wanapooga, na hawi halali kwa mumewe mpaka aoge.

Anasema:

((فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّهُ))

Pale damu inapotoka, na kama hakumwingilia pale Alipoamrisha Allaah, basi si katika wenye kutubia wala wenye kujitwaharisha". [Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdur-Raaziq (1272) na Al-Bayhaqiy (1/310) kwa Sanad Swahiyh hadi kwa Mujaahid].



Maulamaa wote wamekubaliana kwamba mwanamke haingiliwi na mumewe – hata kama damu imekatika – mpaka aoge, kinyume na Ibn Hazm.



· Ikiwa mke wa Muislamu ni Ahlul-Kitaab, je atalazimishwa kuoga?



Atalazimishwa kuoga, na mumewe haruhusiwi kumkurubia mpaka baada ya kuoga, kwani Aayah haimbagui mwanamke Muislamu au asiye Muislamu. [Tafsiyr ya Al-Qurtubiy (3/90)].



4- Ni lazima mwanamke mwenye hedhi amgomee mumewe akitaka kumwingilia, lakini kama atazidiwa nguvu, basi habebi jukumu, bali ataomba maghfirah kwa Allaah Mtukufu. [Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/180)]



4- Kutufu



Kwa Ijma’a ya Maulamaa, ni haramu kwa mwenye hedhi kutufu. Na dalili ya hili ni Hadiyth ya Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) kwamba alipopata hedhi wakati wa kufanya ‘amali za Hijjah, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:

(( إفعلي ما يفعل الحاج غير أن لا تطوفي بالبيت حتى تطهري))

((Fanya ayafanyayo mwenye kuhiji, lakini usitufu Nyumba (Ka'bah) mpaka utwaharike)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1650)].



Maelezo zaidi yatakuja kuhusiana na hili katika mlango wa Hajji Insha Allaah.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



080-Mambo Yanayoruhusiwa Kwa Mwenye Hedhi



Alhidaaya.com





1- Kusoma nyiradi na Qur-aan



Kama ilivyotangulia nyuma, inajuzu kwa mwenye hedhi au janaba kufanya hivyo kwa kauli yenye nguvu zaidi. Haya ni madhehebu ya Abu Haniyfah, na mashuhuri katika madhehebu ya Ash-Shaaf'iy na Ahmad. [Yamenukuliwa haya na Shaykh wa Uislamu katika Al-Fataawaa (21/459)]



Ibn Hazm katika Al-Muhallaa (1/77, 78) anasema:

"Kusoma Qur-aan, kusujudu kwenye Aayah ya sajdah, kuugusa Msahafu na kufanya nyiradi, hayo ni matendo ya kheri, yaliyosuniwa na yenye thawabu. Basi mwenye kudai kwamba hayo hayafai, basi alete dalili".



2- Kusujudu kama atasikia Aayah ya sajdah



Hakuna ubaya mwanamke mwenye hedhi kusujudu anaposikia Aayah ya sajdah, kwani sajdah si Swalaah, na wala si lazima awe na twahara.



Imethibiti katika Swahiyh Al-Bukhaariy (4862) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma Suwrat An-Najm, akasujudu yeye, kisha wakasujudu pamoja naye Waislamu, washirikina, majini na wanaadamu.



Ni mbali kusema kuwa wote walikuwa na wudhuu, kisha sajdah ya kisomo si Swalaah. Az-Zuhriy na Qataadah wamesema hayo hayo kama ilivyo katika Muswannaf wa ‘Abdur-Raaziq. [Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/174) kwa maana yake]



3- Kugusa Msahafu



Hatuijui dalili yoyote ya wazi inayomzuia mwenye hedhi kugusa Msahafu ijapokuwa Maulamaa wengi wanasema kuwa haijuzu kwa mwenye hedhi kugusa Msahafu. Na haya yashaelezewa kwa urefu nyuma.



4- Mume kusoma Qur-aan akiwa kwenye paja la mkewe mwenye hedhi



Ni kwa Hadiyth ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) aliyesema:

"Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiisoma Qur-aan na kichwa chake kipo kwenye paja langu nami niko hedhini" [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (7549) na Muslim (uk. 246) na wengineo].



5- Kuhudhuria Swalaah za ‘Iyd Mbili



Hili halina ubaya, bali ni jambo mustahabu kwa wenye hedhi watoke ili kuhudhuria Swalaah ya ‘Iyd, lakini watakaa kando ya uwanja wa Swalaah.

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((يخرج العواتق وذوات الخدور والحيض وليشهدن الخير ودعوة المؤمنين، ويعتزل الحيض المصلى))

((Watoke wazee wakongwe, waliotawishwa na wenye hedhi, ili waishuhudie kheri na du’aa za Waumini, lakini wenye hedhi wawe kando ya uwanja wa Swalaah)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy katika sehemu tofauti, kati yake ni nambari (324)].



6- Kuingia Msikitini



Suala hili lina mvutano mkubwa kati ya Maulamaa, nalo limeshachambuliwa hapo kabla. [Ni mwisho wa Mlango wa Kuoga]



Tunachoweza kusema ni kuwa sisi hatujagundua dalili yoyote sahihi na ya wazi inayomzuia mwenye hedhi kuingia Msikitini. Na asili ya jambo lolote ni uhalali mpaka liwepo la kuliharamisha. Lakini pamoja na hayo, kila mmoja aendelee kufanya istikhaarah kwa Allaahu Ta'alaa kuhusu suala hili.



7- Kulishana na kunyweshana na mumewe



Imepokelewa toka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) akisema:

"Nilikuwa nikinywa huku niko hedhini, kisha nampa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye anaweka kinywa chake mahala nilipoweka kinywa changu, kisha anakunywa. Na ninang'ata mnofu wa nyama nikiwa hedhini, kisha ninampa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye anaweka kinywa chake mahala pa kinywa changu.” [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (300), Abuu Daawuud (259), An Nasaaiy (1/59) na Ibn Maajah].



8- Kumtumikia mumewe



Ni kama kumwosha kichwa au kumchana nywele. Imepokelewa na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) akisema:

"Nilikuwa nikimchana Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nywele nami niko hedhini". [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (295) na Muslim (297)].



9- Kulala na mumewe ndani ya shuka moja



Imepokelewa toka kwa Mama wa Waumini Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anha) akisema:

"Wakati nikiwa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tumelala katika shuka, nilipata hedhi, kisha nilijichomoa nikachukua nguo yangu ya hedhi. Akaniuliza: Je, umepata hedhi? Nikamjibu: Ndio, halafu akaniita nikalala naye ndani ya qatifa". [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (298) na Muslim (296)].



Katika Sharh Muslim (1/954) An-Nawawiy anasema: "Inajuzu kulala na mwenye hedhi katika blanketi moja."
 
NASAHA ZA IJUMAA

Naam ndugu zangu katika imani alhamdulillah tumefikiwa na siku bora kabisa katika wiki,na leo ni eid,maana ijumaa ni sikukuu kwa waislamu,kama hali inaruhusu kifedha ipambe siku ya ijumaa hapo nyumbani kwa pilau,biliani nakadhalika,ili iwe ni siku tofauti na nyingine

Naam ndugu zangu hakika pepo imezungukwa na mambo yenye karaha sana,yaani ili uipate pepo basi wallah utakaraika sana

Mfano kuswali swala tano,wallah ni uzito mkubwa isipokuwa kwa wenyenyekevu, anasema Allah mtukufu "TAKENI MSAADA KWA KUSUBIRI NA KUSWALI HAKIKA JAMBO HILO NI GUMU ISIPOKUWA KWA WENYENYEKEVU"

Ebu fikiria unaacha usingizi wako alfajir na kisha waenda kuswali wallah ni karaha sana,haya mchana umeshughulishwa na mambo yako mara adhana hiyo,unaacha unachofanya waenda kuswali,al asir,maghari mpaka isha hivyo hivyo

Au kuamka usiku kuswali swala za usiku,tahajjud,watu wanakoroma lkn wewe una msabihi na kumtukuza Allah

Hela ni zako na mwenyewe wazihitaji lkn waambiwa uzitoe kwa ajili ya Allah,usaidie maskini na mayatima,wakati wewe mwenyewe bado unazihitaji

Unaambiwa uwatendee watu wema hata kama wao hawakutendei wema,unaambiwa usamehe hata kama walio kukosea hawajakuomba msamaha,hakika ni mambo magumu sana

Kwahiyo pepo haipatikani kirahisi rahisi huna budu upate karaha na ugumu,kwahiyo kama hupendi karaha na ugumu sahau kuhusu pepo

Kinyume chake,moto umeumbwa na mambo ya kufurahisha na kuvutia, kuzini kunaleta starehe si ndio,kunywa pombe,kwenda kwenye maclub na makasino hakika kunavutia maana maisha ya usiku kwa wanao penda starehe yana raha sana

Kwahiyo ndugu zangu katika imani ikiwa unataka pepo basi kuwa tayar kwa mambo yenye karaha,magumu na yenye uzito mkubwa

Au

Laa wataka moto basi endelea na mambo yenye kufurahisha na rahisi rahisi,ila tambua mwisho mwema ni kwa wacha mungu



Ijumaa Mubarak!
 
Naam bado tupo katika hadith ambazo zinazungumzia Kalimah Tayibar ya Laailaaha illallahu

Umar r.a amesimulia kuwa Nabii swallallahu alaih wasallam amesema " Ewe Ibn Khattab nenda ukawatangazie watu kuwa hakika hawataingia jannah ila waumini"


Abu Laila r.a amesimulia kuwa Nabii swallallahi alaih wasallam alisema "Ole wako ewe Abu Sufyan! Nimekujieni na mafanikio ya dunia hii na akhera hivyo ukubalini Uislamu Mutasalimika"

Anas radhiallahu anhu anayesimulia " Nimemsikia Nabii anasema " itakapo fika siku ya kiama,nitapewa nafasi ya kuombea,kwa hivyo nitasema, Ewe Mola wangu! Waingizi peponi/jannah wale ambao nyoyoni mwao wana imani ya chembe ya Hardali (Allah Subhanahu Wataala atakubali uombezi wangu) kwa hivyo wataingia jannah. Kisha nitasema "Muingize Jannah yule ambaye moyoni mwake ana chembe ndogo zaidi (ya imani)

Chembe ya hardal inasemwa udogo wake ni sawa na uchukue gramu 1 kisha uigawanye mara 10,000 halafu kisha uchukue moja ya saba au moja ya nne ya mgawanyo huo


Abu Said Khudri r.a amepokea kutoka kwa Nabii s.a.w katika hadith Qudus anasema "Wakati wa jannah/peponi watakapo kuwa wameshaingizwa peponi na watu wa motoni wameshaingizwa motoni, Allah atasema "Mtoeni kutoka motoni yule ambaye moyo wake ana imani sawa na uzito wa chembe ya Hardal. Kwahiyo watatolewa kutoka motoni wakiwa wamepigwa weusi kutokana na moto,watatiwa watatupwa kwenye mto wa uhai,ambamo watatoka wakiwa wamechipuka upya,kama mbegu inavyo chipuka ukingoni mwa mto wenye maji mengi (.mkubwa) . Jee hujaiona vipi inavyotoka ikiwa imepiga rangi ya manjano na imeviringika

Kwa wasio fahamu hadith Qudus ni maneno yenyewe ya Allah anamwambia Mtume


Abu Umamah r.a amesimulia kuwa,mtu mmoja alimuuliza Rasululah swallallahu alih wasallam . Akasema Ewe Rasulullah nini Imani? Akajibu "Pale matendo yako mema yanapo kufurahisha na matendo yako mabaya yakakuhuzunisha,basi wewe ni muumini"


Abass bin Abdul Muttalib r.a Nimemsikia Rasulullahi akisema "Kwa hakika ameonja ladha nzuri ya Imani,yule atakaye ridhia kuwa Allah ni Mola wale na Uislamu ni Dini yake na Muhammad swallallahu alaih wasallam kuwa ni Mjumbe wa Allah"

Maelezo: ina maana ya kuwa yeyote anayemuabudu Allah na akaishi kulingana na Uislamu pamoja na utiifu kamili kwa Rasulullah swallallahu alaih wasallam pamoja na mapenzi makubwa kwa Allah na Rasillah kwa hakika ameonja utamu wa Imani


Anas r.a amesimulia kuwa Nabii swallallahu alaih wasallam amesema " Mtu atakaye kuwa na mambo matatu ameonja utamu wa Imani. Awe Allah na Mtume wake wanapendeza zaidi kwake kuliko kingine chochote kile asiyekuwa wawili hao,ampende mtu asimpende isipokuwa kwa ajili ya Allah,na achukue kurudi katika Ukafikiri kama anavyochukia kutupwa motoni


Darsa itendelea inshallah na tutaifikia milango yote kikubwa endelea kufuatilia uzi
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



081-Damu Ya Nifasi



Alhidaaya.com





Ni damu inayomtoka mwanamke kwa sababu ya kujifungua.



1- Muda wake



Hakuna uchache wa muda wa kutoka kwake. Maulamaa wote wamekubaliana kuwa wakati wowote mwanamke anapoona utwahara – hata kabla ya kumalizika siku arobaini – basi ataoga, ataswali na mumewe anaweza kumwingilia. [Imenukuliwa na At-Tirmidhiy katika As-Sunan (1/429)]



Ama upeo wa juu zaidi wa muda anaosubiri mwanamke endapo damu ya nifasi itaendelea, Jamhuri ya Maulamaa wanaona kuwa ni siku arobaini, kisha ataoga na kuswali. Hili wamelitolea dalili kwa Hadiyth ya Mama wa Waumini Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anha) aliyesema:

"Wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam), wanawake wenye nifasi walikuwa wakikaa siku arobaini au masiku arobaini baada ya nifasi". [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (307), At-Tirmidhiy (139) na Ibn Maajah (648). Wametofautiana katika kuifanya Hadiyth Hasan, lakini kauli yenye nguvu ni kuwa ni Hadiyth Dhwa’iyf. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi. Lakini pamoja na hivyo, inafanyiwa kazi].



2- Maulamaa wote wamekubaliana kuwa nifasi ni kama hedhi katika yote yaliyohalalishwa, yaliyoharamishwa, yaliyo makruhu na yaliyo manduwb. [Nayl Al-Awtwaar ya Ash-Shawkaaniy (1/386)]



3- Nifasi inatofautiana na hedhi kwa kuwa eda haihesabiwi, kwani eda humalizika kwa kujifungua kabla ya kutoka damu ya nifasi. [Al-Mughniy ya Ibn Qudaamah (1/350)]
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



082-Damu Ya Istihaadhwah



Alhidaaya.com





Ni damu inayomtoka mwanamke katika nyakati zisizo za hedhi au nifasi, na wala haina uhusiano nazo. Ni damu isiyo ya kikawaida au kimaumbile, bali inatokana na mshipa uliokatika wenye kutoa damu nyekundu isiyokatika ila baada ya kupona. [Huitwa kuvuja damu]



Hukmu Yake



Mwanamke anapotokwa na damu hii, anabakia kuwa twahara, na damu haimzuii kuswali au kufunga kwa mujibu wa Ijma’a ya Maulamaa. Ikiwa damu hii itatoka katika wakati usio wa hedhi au nifasi bila kuwa na uhusiano navyo, basi hakuna tatizo.



Ikiwa damu hii haikatiki, nini mwanamke atafanya?



Tunasema:

“Mwanamke huyu haepukani na moja kati ya hali nne:



1- Ima atakuwa anaingia hedhini kawaida na anakijua kipimo cha hedhi yake. Huyu ataangalia kipimo hicho, kisha ataoga na ataswali. Na damu itakayoendelea baada ya hapo, itakuwa ni damu ya istihaadhwah na wala si ya hedhi.



Imepokelewa na Mama wa Waumini 'Aaishah akisema: "Ummu Habiybah alimuuliza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu damu. Mama wa Waumini 'Aaishah akamwambia: Nimeona beseni lake limejaa damu. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

(( امكثي قدر ما كانت تحبسك حيضتك ثم اغتسلي وصلي))

((Kaa kitambo cha hedhi inavyokuzuia, kisha oga na uswali)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (uk. 264), Abuu Daawuud (279), na An-Nasaaiy (1/119)].



2- Ima atakuwa haijui hedhi yake, lakini anaweza kupambanua kati ya damu ya hedhi na damu ya istihaadhwah. Hapo ataisubiri damu yake ya hedhi, ataacha kuswali, kisha ataoga na kuswali baada ya kumalizika hedhi yake.



Imepokelewa na Mama wa Waumini 'Aaishah akisema:

"Alikuja Faatwimah binti Abu Hubaysh kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Mimi ni mwanamke nipataye damu ya istihaadhwah na wala sitwahariki, je, niache kuswali? Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi waalihi wa sallam) akamwambia:

(( لا، إنما ذلك عرق، وليس بحيض، فإذا أقبلت حيضتك فدعي الصلاة، وإذا أدبرت فاغسلي عنك الدم ثم صلي)).

((Hapana, huo ni mshipa, na wala si hedhi, na ikija hedhi yako basi acha Swalaah, na ikimalizika, jitwaharishe kisha swali)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al Bukhaariy (228) Muslim (uk. 262) na wengineo].



3- Ima atakuwa ndio mwanzo wa kupata hedhi na hawezi kupambanua kati ya damu ya hedhi na damu nyingineyo. Huyu ataiangalia hali ya wanawake wengi inavyokuwa. Na kama hali ya wanawake wengi anaoishi nao ni kudumu hedhi yao kwa muda wa siku sita au saba kila mwezi kwa mfano, basi atasubiri pale inapoanza hedhi yake, kisha atahesabu siku sita au saba na kuzifanya ndio siku za hedhi yake, kisha baada ya hapo ataoga. Na damu itakayoendelea baada ya hapo, ataizingatia kuwa ni damu ya istihaadhwah.



Imepokelewa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Himnah binti Jahsh:

((إنما هذه ركضة من ركضات الشيطان، فتحيضي ستة أو سبعة في علم الله ثم اغتسلي، حتى إذا رأيت أنك قد طهرت واستنقيت فصلي أربعا وعشرين ليلة أو ثلاثا وعشرين وأيامهن، وصومي، فإن ذلك يجزيك، وكذلك فافعلي في كل شهر، كما تحيض النساء وكما يطهرن لميقات حيضهن وطهرن)).

((Hakika hii ni adha katika adha na masumbufu ya shaytwaan. Basi kaa na hedhi yako, siku sita au saba kwa mujibu wa Hukmu ya Allaah, kisha oga. Mpaka utakapoona umetwaharika na umetakasika kabisa, basi swali siku ishirini na tatu au ishirini na nne, na ufunge, hilo litakutosheleza. Fanya hivyo hivyo kila mwezi kama wanavyopata wanawake hedhi na kutwaharika katika nyakati zao)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (287), Ash-Shaafi'iy katika Al-Ummu (1/51), Ibn Maajah (622) na At-Tirmidhiy katika mlango wa 95 wa twahara, na Sanad yake ni Layyin. Katika Al-Irwaa (205), Al-Albaaniy amesema ni Hadiyth Hasan]



4- Ima awe mwanamke amesahau ada yake kwa kiasi chake na wakati wake wa kuja, na hawezi kupambanua kati ya damu ya hedhi na istihaadhwah. [Maulamaa wanamwita mwanamke huyu "mbabaikaji"]



Maulamaa wamezungumza kauli kadhaa kuhusiana na mwanamke huyu. Kauli iliyo dhahiri zaidi ni kuwa mwanamke huyu anakuwa ni kama yule mwanamke anayeanza kupata hedhi ambaye hukmu yake ishaelezwa katika hali ya tatu iliyotangulia. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



083-Hukmu Zinazohusiana Na Mwanamke Mwenye Istihaadhwah



Alhidaaya.com





1- Hukmu yake ni kama mwanamke aliye twahara, hakatazwi lolote katika yale aliyokatazwa mwenye hedhi.



2- Anaruhusiwa kuswali, kufunga, kusoma Qur-aan, kugusa Msahafu, kusujudu sajdah ya kisomo, na sajdah ya kumshukuru Allaah, na mengineyo anayoruhusiwa aliye twahara. Na hii ni kwa Ijma’a’ ya Maulamaa.



3- Halazimiki kutawadha kila Swalaah madhali hakutengukwa na wudhuu, kwani kauli yenye nguvu inaashiria kuwa habari zote zinazogusia hilo ni dhwa’iyf. [Zirejelee katika kitabu cha Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/230) na yanayofuatia]



Lakini lililobora pamoja na hivyo, ni kutawadha au kuoga kwa kila Swalaah kutokana na Hadiyth ya Mama wa Waumini 'Aaishah kwamba Mama wa Waumini Ummu Habiybah alipatwa na damu ya istihaadhwah kwa muda wa miaka saba. Akamuuliza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu hilo, na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamrisha akoge akimwambia:

(( هذا عرق))

((Huu ni mshipa)), na akawa anaoga kwa kila Swalaah. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (327), Muslim (262) na wengineo].



4-Mumewe anaweza kumwingilia madhali si wakati wa hedhi hata kama damu inamtoka. Hii ndiyo kauli ya Maulamaa wengi. [Al Majmu’u (2/372), na Al-Mughny (1/339)]



5-Inajuzu kukaa ‘itikaaf Msikitini. Imepokelewa na ‘Aaishah akisema:

“Mmoja katika wakeze wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alikaa naye ‘itikaaf. Alikuwa akitokwa na damu na unjano na beseni liko chini yake huku akiswali”. [Al-Bukhaary]



An-Nawawy katika Sharhu Muslim (1/631) ameinukulu Ijma’a ikisema kwamba mwenye istihaadhwah katika ‘itikaaf, ni kama mwanamke yeyote mwingine mwenye twahara.
 
Naam alhamdulillah tumeamaliza darsa letu la Twahara

Naamini tumejifunza mengi sana

Mengine yanafuata
 
NAAM TUJIFUNZE KUPITIA MASWALI NA MAJIBU

Alhidaaya.com


SWALI

Assalam aleikum ndugu zangu.nashukuru sana kwa kunipatia jibu swala langu lilotangulia.Sasa niko na swali: jee kumwangalia na kumlea mwanaharamu wa mumeo inafaa?yaani yule baba kuchukuwa responsibility ya yule mtoto wake wa nje ni dhambi,is it like entertaining what he did in his past?ama si dhambi?kisha huyo mtoto ni wa kike ana ndugu yake kwa mama mwengine wa kiume .








JIBU:
BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa ba’ad:

Kwanza tutambue kuwa mtoto aliyesababishwa na zinaa hana dhambi yoyote ile, bali dhambi ni kwa baba na mama waliyemzaa. Kwa hiyo asiwe ni mtoto wa kudharauliwa au kutupiliwa mbali, au kuonewa kwa aina yoyote au kupewa jina hilo 'mtoto wa haramu'.

Na kumlea mtoto huyo ndivyo inavyompasa mtu baada ya kusababisha kuzaliwa kwake kutokana na kitendo cha zinaa. Na mke kumlea mtoto wa mumewe ikiwa ni mtoto wa zinaa au aliyezaliwa katika ndoa ni jambo jema ambalo litampatia mke huyo thawabu kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى na pia itakuwa ni sababu ya kupata ridha na mapenzi zaidi ya mume.

Na thawabu zitakuwa zaidi pindi atakapomlea mtoto huyo kwa malezi mema yenye mafunzo ya dini hadi akue ili atambue jema na baya na aweze naye kujiepusha na mabaya kama hayo aliyoyatenda baba yake.

Na haina maana kwamba kumlea huyo mtoto ni kama kutia nguvu jambo la zinaa bali unafanya wajibu unaokupasa kufanya kumlea mtoto asiye na dhambi yoyote.




Na Allah Anajua zaidi.
 
Abu Umamah r.a amesimulia kuwa Rasulullah swallallahu alaih wasallam amesema " Yule anayependa kwa ajili ya Allah tu na akachukia kwa ajili ya Allah tu, na akatoa kwa ajili ya Allah tu na akazuia kwa ajili ya Allah tu,kwa hakika amekamilisha Imani yake


Ibni Abass r.a amesimulia kuwa Nabii s.a.w alimuuliza Abu Dhari "Ewe Abu Dhari tawi gani la Imani lililo madhubuti zaidi? Akajibu " Allah na Mtume wake ndio wanajua zaidi. Akasema " Kufanya urafiki kwa ajili ya Allah tu na kupenda kwa ajili ya Allah tu,na kuchukia kwa ajili ya Allah tu"

Maelezo: Ina maana ya kuwa miongoni mwa matawi ya imani lulilo kubwa zaidi na madhubuti ni kuwa katika matendo ya mtu,kama itakuwa ni kufanya au kuvunja suluhu,kwa kupenda au kuchukia ,mtu awe anaangalia radhi za Allah tu,na kutenda kulingana na maamrisho ya Allah aliwacha kando matamanio ya nafsi yake


Anas bin Malik r.a anasema kuwa Rasulullah amesema "Bishara njema ,kwa yule aliyeniamini na akaniona (mara moja) na bishara njema mara saba zaidi,kwa yule ambaye ameniamini na hakuniona


Anas bin Malik r.a amesimulia kuwa Rasulillah swallallahu alaih wasallam alisema "Ninatamani kama ningekutana na ndugu zangu. Na Masahaba wakasema: "Je sisi sio ndugu zako?" Akajibu "Nyinyi ni Masahaba zangu,lakini ndugu zangu ni wale ambao wataniamini bila ya kuniona
 
Swalah Za Sunnah Zote Ni Zipi?
Maswali: Swalah-Sunnah


SWALI:



Assalamu Aleykum, namshuku ALLAAH alie wapa fahamu ndungu zetu wa alhidaaya kutuelimisha. pia salaamu nyingi zimfikie mtume wetu (s.a.w.) pia nawashukuru sana ndugu zangu kwa iman alhidaaya naomba mutuvumilie namalipo yenu kwa ALLAAH na ALLAAH AWAZIDISHIE ELMU zaidi na zaidi na sasa namshukuru ALLAAH elmu yangu naipata kwa alhidaaya na ninawaamini sana.



bismillah swali yangu.

nimesikia mawaidha kuhusu swala za sunnah sasa nahitaji munielekeze jee imethibiti kutoka kwa mtume S.A.W nakama ninayo yasema haijathibiti naomba munipe swala sote za sunnah. huyo shekh anasema kuna hadith ya mtume S.A.W. INASEMAATAKAE SWALI SWALA YANJONGEZA KILA SIKU RAKA 12 BASI M.MUNGU ATAHARAMISHA NYAMA YAKE KUTOKANA NA MOTO WA JAHANNAM.


KATIKA SWALA yaalfajir- kuna sunnah muwakala na jua ikitoka una swali swala ya sunnah ya sharuq unaandikiwa unaandikiwa thawabu ya hajj na umra, kabla na baada ya jua kutoka kwa urefu wa mkuki kuna swala ya sunnah baina ya hapo na dhuhri kuna sunna ya dhuha raka 2 mpaka 8 na kuna swala kabla ya dhuhri raka 4 na ukisha swali dhuhri kuna swala sunnah baadiya raka 4, kabla ya kuswali al asir kuna sunnah raka 4 , swala ya maghrib kuna swala ya sunnah raka 2 na unaweza kuongeza halafu mtume s.a.w alikuwa akiswali raka 4 baada ya isha alafu akilala alafu witri.









JIBU:


Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.




Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Atutakabalie hizo du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelimishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn



Tunamshukuru muulizaji kwa Swali lake hili zuri ambalo litampatia mja thawabu za kujichumia kwa ajili ya Akhera yake na kila atakayefuata na kutekelezo hizo Swalah za Sunnah.


Hadiyth uliyotaja haihusiani na kuswali Swalah za Sunnah za idadi ya Rakaa kumi na mbili kwa siku. Kwani hiyo ni kauli iliyokuja katika kuswali Sunnah za kabla na baada ya Swalah ya Adhuhuri pekee kama ifuatavyo:


عن أم حبيبة رضي الله عنها قالت: سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول: ((من صلى أربع ركعات قبل الظهر و أربعا بعدها حرم الله على النار)) أبو داود, الترمذي, النسائي ,ابن ماجه, أحمد والحاكم

Kutoka kwa Ummu Habiybah (Radhiya Allaahu 'anhaa) ambaye amesema: "Nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Atakayeswali Rakaa nne kabla ya Swalah ya Adhuhuri na nne baada yake, Allaah Atamupeusha na moto)) [Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Ibn Maajah, Ahmad na Al-Haakim]




Ama fadhila za kuswali Rakaa kumi na mbili kwa siku imekuja usimulizi ufuatao:


((مَا مِنْ عبْدٍ مُسْلِم يُصَلِّي للَّه ِتَعَالى كُلَّ يَوْمٍ ثِنْتَيْ عشْرةَرَكْعَةً تَطوعاً غَيْرَ الفرِيضَةِ ،إِلاَّ بَنَى اللَّه لهُ بَيْتاً فيالجَنَّةِ ، أَوْ : إِلاَّ بُنِي لَهُ بيتٌ فيالجنَّةِ)) رواه مسلم



((Atakaye Swali Rakaa 12 zisizo za fardhi kwa siku atajengewa nyumba peponi)) [Muslim]


Swalah za Sunnah zote ni kama zifuatavyo:



- Sunnah zilizosisitizwa na zisizosisitizwa kama ilivyoelezewa katika ratiba ifuatayo:


NYAKATI ZA

SWALAH



*MUAKKADAH (ZILOSISITIZWA)

GHAYR MUAKKADAH (ZISOSISITIZWA)

KABLA

BAADA

KABLA

BAADA

ALFAJIRI

**2

Soma Suratul-Kafiruun na Ikhlaasw

-

-

-




ADHUHURI



4

2

-

-

ALASIRI



-

-

4

-

MAGHARIBI



-

2

Soma Suratul-Kafiruun na Ikhlaasw

2

-

'ISHAA



-

2

2

-





FADHILA ZAKE:



((مَا مِنْ عبْدٍ مُسْلِم يُصَلِّي للَّهِتَعَالى كُلَّ يَوْمٍ ثِنْتَيْ عشْرةَرَكْعَةً تَطوعاً غَيْرَ الفرِيضَةِ ،إِلاَّ بَنَى اللَّه لهُ بَيْتاً فيالجَنَّةِ ، أَوْ : إِلاَّ بُنِي لَهُ بيتٌ فيالجنَّةِ)) رواه مسلم




* ((Atakayeswali Rakaa 12 zisizo za fardhi kwa siku atajengewa nyumba peponi)) [Muslim]




(( ركْعتا الفجْرِ خيْرٌ مِنَ الدُّنياومَا فِيها )) رواه مسلم.



** ((Rakaa mbili (za Sunnah) kabla ya Alfajir ni kheri kuliko duniya na yaliyomo ndani yake) [Muslim]



((ما من عبد يسجد لله سجدة إلاكتب الله له بها حسنة ومحا عنه بها سيئة ورفع له بها درجة فاستكثروا منالسجود)) رواه ابن ماجه



((Mja yeyote atakayesujudu sajda moja ataandikiwa wema mmoja, na atafutiwa baya moja, na atapandishwa daraja yake, kwa hiyo zidisheni kusujudu)) [Ibn Maajah]


Tunakuwekea hapa aina za Swalah za Sunnah zikiwa na maelezo yake mafupi kisha tunakuwekea viungo ambavyo utapata maelezo zaidi kwa kila Swalah:




- Swalaatul-Witr


Rakaa tatu baada ya Swalah ya 'Ishaa au wakati wowote usiku kabla ya kuingia Alfajiri


Swalah Ya Witr Inaswaliwa Vipi Na Vipi Kutia Nia?




- Qiyaamul-Layl (Tahajjud) hii pamoja na Swalatut-Taraawiyh katika mwezi wa Ramadhaan.


Ni Swalah inayoswalia ima Rakaa mbili au nne au sita au nane na kumalizia na Swalatul Witr.


Wakati Wa Swalah Ya Tahajjud Na Vipi Kuswali




- Swalaatud-Dhwuhaa


Inaswaliwa baada ya jua kutoka hadi kama nusu saa kabla ya Swalah ya Adhuhuri nayo ni ima Rakaa mbili, au nne, au sita au nane.


Swalah Ya Dhwuhaa - Rakaa Zake, Fadhila Zake na Wakati Wake


Swalah Ya Shuruuq Ni Sawa Na Swalah ya Dhwuhaa?





- Swalaatul-Istikhaarah


Inaswaliwa unapotaka kufanya jambo ukawa hujui kama litakuletea kheri au shari, hivyo unamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akuongoze katika hili jambo yaani Akuamulie Yeye.


Kwa Nini Tuswali Istikhaarah Na Iswaliwe Kwa Ajili Ya Nini?




-








Tunatumai kwa maelezo hayo yote utakuwa umepata mafunzo kamili yanayohusu Swalah zote za Sunnah anzoweza kuswali Muislamu katika maisha yake kila siku.


Ama Swalah nyingine za Sunnah ni zile zinazoswaliwa kwa msimu wake, mfano Swalaatul-'Iydayn (Swalah za 'Iyd mbili), Swalaatul-Kusuuf (Swalah ya kupatwa jua au mwezi) Swalaatul-Istisqaa (Swalah ya kuomba mvua) na Swalatul-Janaazah ambazo ni fardhwu kifaaya (fardhi inayotosheleza ikiwa itaswaliwa na Waislamu wengine).







Na Allaah Anajua zaidi
 
Maswali: Swalah-Sunnah


Swalaah Ya Witr Inaswaliwa Vipi Na Vipi Kutia Niyyah?

www.alhidaaya.com






SWALI:



nategamea muko katika hali ya afya njema na ramadhan karim mimi nina suala langu kuhusu salaa ya witri .witri inasaliwa rakaa moja ,tatu ,tano,ambazo rakaa zisizogawika kwa mbili ama sivyo na wengine wanasema utakaposali rakaa tatu haifai kusali kama sala ya magharibi yaani usalii rakaa mbili ukae atahiyat ikisha umalize rakaa ya mwisho utoe salamu na wengine wanasema usali rakaa zote tatu moja kwa moja ya mwisho ndio utoe salamu yaani usikasali rakaa mbili ikisha ukae atahiyat ikisha umalize rakaa moja kwa ufupi yaani usisali kama sala ya magharib kwa hiyo naomba jibu kutoka kwa wanalhidaaya

na utakaposali unatia nia gani ya witri? nadhani nitapata jibu kutoka kwenu inshaalah a/a







JIBU:



AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.



Witr ni kuswali Rakaa moja, au tatu, au tano, au saba, au tisa au kumi na moja. Swalaah hii huswaliwa usiku baada ya Swalaah ya 'Ishaa ikiwa ni kabla ya kulala au baada ya kulala na kuamka kabla ya Alfajiri.



Mafunzo ya Sunnah yanatufundisha kuwa Rakaa zozote utakazojaaliwa kuswali, basi umalizie na Rakaa moja au tatu za Witr ambazo huswaliwa hivi:



Kuswali Rakaa mbili kwanza kisha utoe salaam. Kisha unamalizia na Rakaa moja na kutoa salaam.



Au kuswali Rakaa zote tatu kwa tashahhud (kikao) moja ya mwisho tu na kutoa salaam.



Haifai kuswali Rakaa tatu zote pamoja kwa kuleta Tashahhud mbili kama vile Swalaah ya Magharibi, bali ni kuitofautisha na Swalaah ya Magharibi kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((… ولا تشبهوا بصلاة المغرب))

((… wala msiishabihishe (hiyo witr) na Swalah ya Magharibi)) [Al-Haakim, Al-Bayhaqiy, Ibn Hibbaan, Ad-Daraaqutniy?]



Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi ya jinsi kuswali Qiyaamul-Layl



Suwrah Gani Kusoma Katika Swalaah Ya Witr



Hii ni kuhusu Swalaah ya Tahajjud ambayo ni sawa na Swalah ya taraawiyh au kwa jina lingine ni Qiyaamul-Layl.



Wakati Wa Swalaah Ya Tahajjud Na Vipi Kuiswali



Vile vile soma Faatawa zifuatazo za mas-ala mbali mbali kuhusu Swalah ya taraawiyh au Qiyaamul-Layl.



Qiyaamul-Layl, Witr, Laylatul-Qadr Na I'tikaaf



Jibu kuhusu Kutia Niyyah:



Niyyah ya ‘ibaadah yoyote haitamkwi, bali huwekwa moyoni. Na hayo ndio mafunzo sahihi ya Sunnah. Kutamka niyyah ni bid'ah. Unapojitayarisha kwenda kuswali Taraawiyh au Swalaah yoyote nyingine kwa kufanya wudhuu, na kutoka kwenda Msikitini, huwa tayari umeshatia niyyah moyoni kwa lile unaloliendea, hivyo inatosheleza kuwa nia yako imeingia moyoni.



Na Allaah Anajua zaidi
 
Maswali: Swalah-Sunnah



Wakati Wa Swalaah Ya Tahajjud Na Vipi Kuswali

www.alhidaaya.com







SWALI:



Swala ya Tahajjud inaswaliwa vipi? Na wakati gani?
Je unaweza kutumia saa yake ikuamshe ili upate kuswali au mpaka uamke mwenyewe?





JIBU:



AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.





Swalaah ya Tahajjud ni Swalaah inayoswaliwa usiku ambayo pia kwa jina lengine ni Qiyaamul-Layl (kusimama kuswali usiku). Nayo huswaliwa wakati wowote baada ya Swalah ya 'Ishaa mpaka karibu na Alfajiri.



Ama ikiwa mtu anataka kupata fadhila zilizotajwa kuswali katika thuluthi ya usiku kama ilivyo katika Hadiythi ifuatayo:





عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ، مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba du’aa Nimuitike? Nani Ananiomba jambo Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, Muslim]





basi wakati huu wa Thuluthi ya mwisho ni kugawa sehemu tatu kuanzia Swalaah ya Magharibi mpaka Swalaah ya Alfajiri. Sehemu ya tatu ndio Thuluthiy-Llayl (thuluthi ya usiku) ya mwisho



Na huswaliwa ifuatavyo:



1-Idadi ya Swalaah za Sunnah za usiku:



Jumla ya Swalaah za usiku za Sunnah ni Raka'ah kumi na moja kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba: “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali usiku Raka'ah kumi na akitoa salaam baada ya kila Raka'ah mbili kisha akiswali Witr Raka'ah moja.” [Muslim]



Na akasema vile vile: ”Hajapata Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuzidisha katika Ramadhwaan wala miezi mingine zaidi ya Raka'ah kumi na moja, akiswali nne, wala usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha akiswali nne wala usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha akiswali tatu.” [Al-Bukhaariy na Muslim]



b-Namna zinavyoswaliwa Swalaah za usiku:





Unatoa salaam kila baada ya Raka'ah mbili kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:



((Swalaah ya usiku ni (raka’ah) mbili mbili na ukiogopa kukukuta asubuhi basi Swali Witr [Raka'ah] moja)) [Al-Bukhaariy]





c-Suwrah za kusoma katika Swalash ya usiku:





Hakuna Suwrah maaluum ya kusomwa katika Swalaah za usiku, bali ni vizuri sana kusoma Suwra ndefu kwa dalili ya Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) iliyotangulia juu kwamba: “Wala usiniulize uzuri wake.” akikusudia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Swalaah kwa utulivu kabisa kwa kusoma mara nyingine Suwrah ndefu, Rukuu ndefu, sujuwd ndefu na kadhalika.



Pia kutokana na Hadiyth inayojata fadhila za kusoma Aayah nyingi katika Swalaah za usiku:




عبدالله بن عمرو عن النبي صلى الله عليه وسلم ((من قام بعشرِ آياتٍ لم يُكتبْ من الغافلينَ ، ومن قام بمئةِ آيةٍ كُتبَ من القانتينَ ومن قام بألفِ آيةٍ كُتبَ من المُقَنْطِرينَ)) صحيح أبي داود



Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amr (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayesimama usiku kuswali na akasoma Aayah kumi, hatoandikiwa kuwa miongoni mwa walioghafilika, na atakayesimama kuswali akasoma Aayah mia, ataandikiwa ni miongoni mwa watiifu, na atakayesimama kuswali akasoma Aayah elfu, ataandikwa miongoni mwa wenye mirundi (ya thawabu).’ [Abuu Daawuwd, Al-Albaaniy ameisahihisha: Swahiyh Abiy Daawuwd (1398), Swahiyh Al-Jaami’ (6439)]



Maana ya mirundi ni: Mirundi ya thawabu.





Ama katika Raka'ah tatu za mwisho imethibitika kuwa alikuwa akisoma Suwrah zifuatazo:





Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba: “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika Raka'ah ya mwanzo ya (Swalaah) Witr “Sabbihisma Rabikal-A'alaa” na Raka'ah ya pili “Qul-Yaa-Ayyuhal-Kaafiruwn” na Raka'ah ya tatu “Qul- Huwa-Allaahu Ahad pamoja na Qul-A'uwdhu mbili (Al Falaq na An Naas)” [At Tirmidhiy]





Raka'ah hizi tatu za mwisho vile vile ziswaliwe mbili kwanza kisha umalizie na moja pekee, na katika hiyo raka’ah ya mwisho bada ya kuinuka katika ruku'u usome du'aa ya Qunuwt.



Au pia unaweza kuziswali zote tatu kwa Tashahhud moja ya mwisho na kisha kutoa salaam, yaani bila kusoma At-Tahiyaat kwenye raka’a ya pili, na ‘Ulamaa wamesema kusema kuunga raka’ah tatu kwa pamoja ni kuitofautisha na Swalash ya Maghrib ambayo unakaa At-Tahiyaat kwenye raka’ah ya pili.



Swali kuhusu kuweka saa au kuamka mwenyewe, jibu ni kwamba hakuna shuruti ya kuweka saa, vyovyote utakavyoamka kuswali ni sawa fadhila zake ni zile zile.



Na Allaah Anajua zaidi
 
Naam ndugu zangu katika imani baada ya kusoma darsa la Tohara,sasa tunaingia katika darsa la Swala

Kwahiyo kazi kwako,elimu ipo hapa hapa jf kupitia huu uzi

Tutasoma kupitia kitabu cha Swala ya Mtume,tunaanza Utangulizi

Karibuni sana
 
Utangulizi Wa Mfasiri



Alhidaaya.com



BismiLLaahir-Rahmaanir-Rahiym





Hakika shukurani ni Zake Allaah (Subhaanahuu wa Ta’aalaa), tunamshukuru Yeye, na kumtaka msaada, na tunamuomba Yeye msamaha. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atulinde na shari za nafsi zetu na ubaya wa matendo yetu. Anayeongozwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) hakuna wa kumpoteza, na anayepotezwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) basi hakuna wa kumuongoza.



Na nashuhudia kuwa hakuna apasaye kuabudiwa ila Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), Ni Mmoja tu Asiye na mshirika. Na nashuhudia kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mja Wake na ni Mjumbe Wake. Swalah na Salaam za Allaah zimshukie yeye, jamaa zake, Swahaba zake, na wote waliotangulia kwa wema hadi siku ya mwisho.



Ama ba’ad,



Namshukuru tena Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kuniwezesha kukamilisha kazi hii kwa Lugha ya Kiswahili, kazi ambayo naamini sana kuwa itawanufaisha sana Waislam wazungumzaji wa lugha hii na kuweza kuwasaidia kupata mafunzo sahihi ya 'Ibaadah hii adhimu ambayo itakuwa ni jambo la kwanza kabisa kwa mja kuulizwa kwalo siku ya Hesabu.



Umuhimu wa kitabu hiki ni mkubwa sana, haswa kwa kuwa ni kitabu kilichoelezea ‘Ibaadah hii ya Swalah kwa mapana na marefu na kwa dalili sahihi zilizothibiti kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni kitabu kwa mwenye kutaka kujua ilivyokuwa Swalah ya kipenzi chetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallaam) kama alivyosema: (Swalini kama mlivyoniona nikiswali) [Al-Bukhaariy]. Basi anapaswa kuwa nacho kwenye nyumba yake.



Hiki ni kitabu cha Swalah kilichoenea na kuuzika kwa wingi sana labda kuliko vitabu vyote vya Swalah vilivyowahi kuandikwa. Ni kitabu chenye mauzo makubwa katika nchi za Kiarabu kwa mujibu wa wachapishaji wa kitabu hicho. Hali kadhalika kimetafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na kimeuzwa na kinaendelea kuuzika kwa wingi katika nchi za Ulaya na haswa Uingereza. Nimeonelea manufaa hayo yasiwaenee tu wenye kuzungumza Kiarabu na Kiingereza pekee, bali na jamii yetu ya wazungumzao Kiswahili.



Swalah ina fadhila kubwa sana, hivyo kukosa kuswali ni kosa kubwa. Swalah ni 'amali ya kwanza itakayokaguliwa Siku ya Qiyaamah na ndio ufunguo wa Jannah. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:



’Amali ya mwanzo atakayoulizwa Muislamu Siku ya Qiyaamah kuwa kaitekeleza–na kaitekeleza vilivyo–ni Swalah. Ikiwa aliitekeleza vilivyo basi kunatarajiwa atafaulu. Ikiwa hakuitekeleza au kaitekeleza, lakini sivyo ndivyo, basi itatazamwa Swalah za Sunnah, kama alizitekeleza vilivyo. Ama ikiwa hana hata Sunnah au kaitekeleza sivyo ndivyo, basi keshapata khasara’ [Ahmad, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaaiy na Ibn Maajah].



Amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Funguo za kufungulia milango ya Jannah ni Swalah” [Muslim].



Ubaya wa kuacha Swalah ni mkubwa sana kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:



فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلاَةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ ۖ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا

Wakafuata baada yao waovu, walipoteza Swalaah na wakafuata matamanio; basi watakutana na adhabu motoni. [Maryam: 59].



Na kadhalika Anasema tena Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) kwa kutaja habari za wasioswali pindi watakapoulizwa sababu yao ya kuwepo motoni:



مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ﴿٤٢﴾ قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ﴿٤٣﴾

(Watawauliza): Nini kilichokuingizeni katika motoni? Watasema: Hatukuwa miongoni mwa wanaoswali. [Al-Muddaththir: 42 -43].



Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kizuizi kilichoko baina ya mtu na ukafiri ni Swalah” [Muslim].



Kadhalika akaeleza ubaya wa mtu kutokuswali na kumfananisha na kafiri: “Tofauti baina yetu Waislamu na wasio Waislamu ni Swalah” [Abu Daawuud, an-Nasaaiy na Ibn Maajah].



Baada ya kujua masuala hayo muhimu kutoka katika Kitaab na Sunnah, ndivyo vilevile tutaona umuhimu wa kuijua ‘Ibaadah hiyo vilivyo ili tuweze kuitekeleza ipasavyo. Na kwa mintarafu hiyo, tutaona kuna ulazima wa kupata mafunzo hayo kutoka katika chanzo kilichokamilika kwa dalili thaabit kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake. Na ndio nikakichagua kitabu hiki kukitafsiri ili kumuwezesha Muislam mwenye kusoma Kiswahili anufaike na aweze kuinoa na kuiboresha Swalah yake ili aweze kufikia makusudio yaliyotajwa katika Aayah na Hadiyth mbalimbali nilizotanguliza hapo juu, na pia ili aweze kuepukana na sifa na adhabu nilizotangulia kutaja.



Nisiwe mbakhili wa fadhila na mchache wa shukurani kwa wale waliotoa mchango wao mkubwa kabisa katika kazi hii tukufu. Nawaombea wote malipo kamili kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) yanayotokana na kazi hii, bila kukosa thawaab za wale wote watakaonufaika kutokana na ‘amali hii.



Shukurani zangu za dhati na du’aa zangu ni kwa dada yangu Ummu Iyyaad ambaye kwa juhudi zake zisizo mithali kazi hii imeweza kukamilika na pia ushirikiano wake mkuu wa dhati. Pia Al-Akh 'Abdullaah Mu'awiyyah na Al-Akh Fayswal ‘Abdul-‘Aziyz, kwa kujitolea wakati mkubwa kuipitia kazi hii. Pamoja na ndugu yangu mpenzi Sa’iyd Baawaziyr kwa kupitia vilevile na kuchangia maoni mbalimbali. Bila kusahau mchango mkubwa wa upitiaji na mawazo wa Al-Akh Muhammad Faraj As-Sa’ay. Hali kadhalika Al-Ukht Ummu ‘Abdir-Rahmaan kwa mchango wake.



Na shukurani nyingi kwa tashji’i kubwa na uvumilivu wa hali ya juu kutoka kwa mke wangu Ummu ‘Abdillaah ambaye amenisaidia kwa kiasi kikubwa na amenipa fursa ya kutosha ya kushughulika na majukumu haya matukufu bila kuchoshwa wala kuvunjika moyo. Namuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amlipe yeye na wote duniani na Akhera. Aamiyn





Abu ‘Abdillaah Muhammad Baawaziyr



Swafar 1429 H – Februari 2008 M
 
Historia Fupi Ya Shaykh Al-Albaaniy




(Historia hii fupi ya Shaykh nimeitoa katika kitabu nilichoandika kuhusu maisha ya Shaykh kiitwacho Shaykh Al-Albaaniy – Mwanachuoni Wa Karne Ambacho kinapatikana katika tovuti ya www.alhidaaya.com na karibuni kitachapishwa in shaa Allaah)


Abu ‘Abdillaah Muhammad Saalim Sa’iyd Baawaziyr



Al-Imaam, Al- Muhadith, Shaykh Muhammad Naaswirud-Diyn Al-Albaaniy

1332 H-1420 H – 1914 M-1999 M



Jina Lake: Muhammad Naaswir-ud-Diyn bin Nuuh An-Najaatiy

Nasaba Yake: Al-Albaaniy (Kajulikana kwa jina la Al-Albaaniy kwa sababu asili yake ni mtu wa Albania)

Kun-Yah Yake: Abu ‘Abdir-Rahmaan (Baba ya ‘Abdur-Rahmaan’)

Wake Zake: Alioa wake wanne; watatu wa mwanzo walimzalia watoto, na wa nne ‘Ummu Al-Fadhwl’ hakujaaliwa kuzaa, na ndiye aliyeishi naye hadi alipofariki dunia.

Watoto Wake: Aliruzukiwa watoto 13; 7 wa kiume na 6 wa kike. Wa kiume ni: ‘Abdur-Rahmaan, ‘Abdul-Latwiyf, ‘Abdur-Razzaaq, ‘Abdul-Muswawwir, ‘Abdul-Muhaymin, Muhammad na ‘Abdul-A’alaa. Wa kike ni: Aniysah, Aasiyah, Salaamah, Hassaanah, Sakiynah na HibatuLlaah.



Mwanachuoni Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn bin Nuuh An-Najaatiy Al-Albaaniy ni mmoja kati ya Ma’ulamaa wakubwa wa Kiislam katika zama hizi. Anahesabika kuwa ni Mwanachuoni wa Hadiyth maarufu kabisa katika fani ya elimu ya Jarh na Ta’adiyl.[1]

Shaykh Al-Albaaniy vilevile ni hoja katika elimu ya Mustwalahul-Hadiyth.[2] Na Wanachuoni wamemsifu na kuelezea kwamba kwa elimu yake hiyo, karejesha kumbukumbu za zama za kina Imaam Ibn Hajr Al-‘Asqalaaniy, Ibn Kathiyr na Wanachuoni wengine wakubwa wa fani hiyo.



Alikuwa na kumbukumbuku ya hali ya juu katika kuhifadhi vitu kichwani na mengine mengi. Kumbukumbu inayotukumbusha wema waliotangulia kama kina Ibn ‘Abbaas, Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliofuatia kama Imaam Al-Bukhaariy, Imaam Ash-Shaafi’y, Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah, Imaam Ibn Kathiyr, Imaam An-Nawawiy na wengine (Allaah Awarehemu wote).







Kuzaliwa Na Kukua Kwake





Alizaliwa mwaka 1332 H – 1914 M katika mji wa Ashkodera ambao kwa wakati huo ulikuwa mji mkuu wa Albania huko Ulaya Mashariki na ukoo wake ulikuwa maskini. Baba yake aliyeitwa Shaykh Nuuh An-Najaatiy alihitimu katika chuo cha Shari’ah huko Istanbul, Uturuki, na kurejea kwao akiwa Mwanachuoni. Lakini baada ya mfalme Ahmad Zogo kutwaa madaraka ya nchi na kuendesha utawala wa nchi hiyo kikomunisti ikabidi baba yake (Shaykh Al-Albaaniy) ahamie Damascus, Syria. Wakati huo Shaykh Al-Albaaniy alikuwa na umri wa miaka tisa.



Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy alianza masomo yake ya awali katika madrasah ya Al-Is’aaf Al-Khayriyah hapo Damascus na kuendelea hadi alipomaliza na kuwa msimamizi wa chuo hicho hadi yalipoanza mapinduzi dhidi ya Ufaransa nchini humo. Madrasah hiyo ikakumbwa na maafa ya moto yaliyosababishwa na vurugu na machafuko katika vita hivyo. Baba yake akaamua kumuachisha masomo na akaanza kumsomesha yeye mwenyewe. Alimwekea ratiba kali ya masomo ambayo ni; Qur-aan, Tajwiyd, Swarf, Fiqh (ya Kihanafi, yaliyokuwa madhehebu ya baba yake aliyekuwa Mwanachuoni mkubwa wa madhehebu hayo). Shaykh Al-Albaaniy alijifunza pia masomo mbalimbali ya Dini na lugha kutoka kwa Wanachuoni wakubwa na Mashaykh waliokuwa marafiki wa baba yake kama vile Shaykh Sa’iyd Al-Burhaaniy ambaye alimsomesha masomo ya balaaghah na lugha.







Kujifunza Kwake Elimu Ya Hadiyth





Alitunukiwa shahada ya juu ya elimu ya Hadiyth kutoka kwa Shaykh Raaghib At-Twabbaakh, Mwanachuoni mkubwa wa Halab katika wakati huo. Hapo ni wakati alipokutanishwa naye kupitia Shaykh Muhammad Al-Mubaarak ambaye alimjulisha Shaykh At-Twabbaakh umahiri wa kijana huyo (Al-Albaaniy) katika elimu ya Hadiyth. Baada ya Shaykh At-Twabbaakh kumjaribu na kuthibitisha hilo mwenyewe, akamtunuku shahada (Ijaazah). Shahada hiyo si pekee, bali pia alipata kwa Wanachuoni wengine wakubwa wa Hadiyth kama Shaykh Bahjatul Baytaar (ambaye isnaad yake inafika hadi kwa Imaam Ahmad bin Hanbal).[3]



Aliingia kwenye fani ya Hadiyth akiwa na umri wa miaka ishirini. Aliathirika sana na tafiti mbalimbali za Muhammad Rashiyd Ridhwaa, Mwanachuoni wa Misr wakati huo. Tafiti hizo zilikuwa katika jarida la Al-Mannaar. Anasema Imaam Al-Albaaniy: “Nilichokimulika mwanzo miongoni mwa vitabu, ni vile vya visa vya lugha ya kiarabu, kama vile; Adhw-Dhwaahir, ‘Antarah, Maalik as-Sayf na vinginevyo kama hivyo. Kisha nikazama katika vitabu vya visa vya kijasusi vilivyotarjumiwa katika lugha ya Kiarabu. Siku moja nikapita katika vibanda vya kuuza vitabu na macho yangu yakaangaza kwenye jarida moja liitwalo Al-Mannaar na katika kupekuapekua ndani yake nikakutana na makala ya kitafiti ya Rashiyd Ridhwaa akikielezea kitabu cha ‘Ihyaa ‘Uluum ad-Diyn’ cha Abu Haamid al-Ghazaaliy, akitaja mazuri yaliyomo ndani ya kitabu hicho na kasoro zake. Kwa mara ya kwanza nikakutana na aina kama hii ya uchambuzi wa kielimu. Nilivutika sana na uchambuzi sampuli hiyo na ukanifanya nisome toleo zima la makala hiyo. Kisha nikawa nafuatilizia maudhui za uchambuzi wa Hadiyth wa Mwanachuoni Al-Haafidh Al-‘Iraaqiy alioufanya kwa Hadiyth zilizomo ndani ya kitabu ‘Ihyaa ‘Uluum ad-Diyn’. Sikutosheka hadi ikabidi nimuombe muuza duka aniazime jarida hilo kwa kuwa sikuwa na uwezo wa fedha wa kulinunua!



Hapo ndipo ilipoanza safari ndefu ya kusoma vitabu mbalimbali. Nikatoa nakala ya maudhui hiyo iliyofanyiwa uchambuzi wa kina katika jarida hilo”



Shaykh Al-Albaaniy alijifunza pia kwa baba yake elimu ya kutengeneza saa hadi akawa fundi mzuri maarufu kwa kazi hiyo. Ikawa ndiyo kazi iliyompatia rizki yake. Alikuwa fundi na hapo hapo mtafutaji elimu. Hali hiyo ikaendelea hivyo hadi alipoamua kutenga siku mbili tu za kufanya kazi ya kutengeneza saa, na siku zote zilizobaki zikawa ni za kutafuta elimu. Elimu hiyo alikuwa akiichukulia katika maktaba kubwa ya mji huo wa Damascus iliyoitwa Adhw-Dhwaahiriyah ambapo alikuwa akitumia siku nzima kusoma na kutafiti. Alishughulishwa mno na kusoma hadi akawa anasahau hata kula. Kilichokuwa kinakatisha utafiti na masomo yake ni vipindi vya Swalah tu. Mwishowe, wahusika wa maktaba hiyo wakamuamini na kuamua kumpa funguo zake awe anatumia maktaba wakati wa ziada, na akawa daima ni mtu wa mwisho kutoka na kufunga mwenyewe.



Hadiyth za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) zilikuwa zina athari kubwa sana katika maisha ya Shaykh kielimu na kiutendaji. Zikamuelekeza katika Manhaj (Njia, mwenendo) Sahihi; ambao ni kuchukua kutoka kwa Allaah (Qur-aan) na Mtume Wake (Sunnah) tu. Akipata usaidizi wa ufahamu wa vyanzo hivyo viwili vikuu kutoka kwa Maimaaam Wanachuoni katika wema waliotangulia (As-Salafu as-Swaalih) bila kuwa na ta’aswub (kasumba) ya kumshabikia yeyote miongoni mwao au kumponda yeyote, bali msimamo wake ulikuwa ni kuchukua haki popote ipatikanapo na kutoka kwa yeyote.



Kwa sababu hiyo, aliyaacha na kuyaweka pembeni madhehebu ya Kihanafi aliyokulia nayo na aliyosomeshwa na baba yake. Baba yake (Allaah Amrehemu), alikuwa akivutana naye sana juu ya masuala hayo ya kimadhehebu, kwani baba yake alikuwa ameshikilia kwa nguvu sana msimamo wa Kihanafi na hataki kusikia mingine hata iliyokuwa sahihi katika masuala mengine. Shaykh alijaribu sana kumfahamisha baba yake kuwa anapaswa kufanyia kazi Hadiyth za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) endapo itathibiti usahihi wake, na kuacha ya wengine wote kama hayawafikiani na maneno ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم).







Wanafunzi Wake Maarufu



Wanafunzi wake ni wengi sana na walio maarufu katika Mashaykh ni hawa ambao baadhi yao wako hai hadi leo:

Shaykh Muqbil bin Haadiy Al-Waadi’iy (Yemen)

Dkt. ‘Umar Sulaymaan Al-Ashqar (Jordan)

Shaykh Saalim Al-Hilaaliy (Palestina)

Shaykh Hamdiy ‘Abdul-Majiyd

Shaykh Muhammad ‘Iyd ‘Abbaasy

Shaykh Muhammad Ibraahiym Shaqrah (Jordan)

Shaykh ‘Aliy Khushshaan

Shaykh Muhammad Jamiyl Zaynuu (Saudi Arabia)

Shaykh ‘Abdur-Rahmaan ‘Abdus-Swamad







Vitabu Vyake



Maktaba za Kiislam zimeneemeka kwa vitabu vingi vya Shaykh hususan vile vikubwa vyenye mijalada mingi vya ‘Silsilatul Ahaadiyth Asw-Swahiyhah’ na ‘Silsilat al-Ahaadiyth adhw-Dhwa’iyfah wal-Mawdhuw’ah’ na kitabu chake cha Swalah kiitwacho ‘Swiftatus Swalaatin Nabbiy’[4] ambacho kimepokelewa kwa nguvu sana na wasomaji pande zote za ulimwengu, haswa vijana. Ni mojawapo ya vitabu vizuri na muhimu sana katika mafunzo ya Swalah kama ilivyoswaliwa na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم).



Kadhaalika, Shaykh ana vitabu maarufu sana vya Hadiyth vyenye kuvifanyia sharh, tahkiki, na hata kubainisha yale ya sahihi na ya dhaifu ndani ya vitabu hivyo, kama alivyofanya kwenye vitabu Sunan At-Tirmidhy, Sunan Ibn Maajah, Sunan Abi Daawuud n.k. Vilevile ana mijalada mingi ya vitabu kama tutakavyoona hapo chini kwenye orodha fupi. Vilevile ameweza kutoa vitabu vya kufafanua na kusahihisha vitabu maarufu vya Wanachuoni wakubwa wa karibuni kama vitabu ‘Tamaamul-Minnah Fiyt-Ta’aliyq ‘Alaa Fiqhis-Sunnah’ kilichokuwa ni masahihisho ya Hadiyth zisizo sahihi katika kitabu cha Shaykh Sayyid Saabiq kitwacho ‘Fiqhus-Sunnah’, na ana kitabu cha ‘Ghaayatul-Maraam Fiy Takhriyj Ahaadiyth Al-Halaal wal Haraam’ ambacho ni usahihisho wa Hadiyth zilizomo katika kitabu cha Dr. Yuusuf Al-Qaraadhwaawiy kiitwacho ‘Al-Halaal Wal Haraam Fiyl Islaam’.



Kazi zake za uandishi kuhusu masuala ya Hadiyth zinazidi zaidi ya mia.



Baadhi Ya Vitabu Vyake Vilivyoenea Sana Ni:



1- Silsilatul Ahaadiyth Asw-Swahiyhah (Mijalada 1-11)



2- Silsilatul Ahaadiyth Adhw-Dhwa’iyfah wal Mawdhuw’ah (Mijalada 1-14)



3- Al-Irwaa Al-Ghaliyl (Mijadala 1-9)



4- At-Targhiyb wa At-Tarhiyb (Mijalada 1-4)



5- Swahiyh wa Dhwa’iyf Sunan Abi Daawuud (Mijalada 1-4)



6- Swahiyh wa Dhwa’iyf Sunan At-Tirmidhiy (Mijalada 1-4)



7- Swahiyh wa Dhwa’iyf Sunan Ibn Maajah (Mijalada 1-4)



8- Mukhtaswar Swahiyh Al-Bukhaariy



9- Mukhtaswar Swahiyh Muslim



10- Sharhu Al-‘Aqiydah Atw-Twahaawiyah



11- Ahkaam Al-Janaaiz



12- At-Tawaswul: Anwa’uhu wa Ahkaamuhu



13- Kitaabu As-Sunnah



14- Swalaatu At-Taarawiyh (Qiyaamu Ramadhwaan)



15- Tamaamul-Minnah Fiyt-Ta’aliyq ‘Alaa Fiqhis-Sunnah



16- Ghaayatul-Maraam Fiy Takhriyj Ahaadiyth Al-Halaal wal-Haraam



17- Adaabu Az-Zafaaf[5]



18- Swifatu Asw-Swalaatin-Nabiy[6]















Fadhila Na Mema Yake







Shaykh Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) alikuwa ni mwenye kufuata mwenendo wa wema waliotangulia (Salafus-Swaalih), akifuata mwenendo wao na tabia zao, na yakawa macho yake yanafuata kilichosemwa na Allaah (سبحانه وتعالى) na Mtume Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).



Alikuwa hastahi katika haki, akiitangaza haki katika vitabu na mihadhara yake. Hii ni sifa ya nadra sana kuipata katika ulimwengu wa leo, ambao wengi hawapendi kusema haki kwa kuchelea kuwaudhi wengine au kupoteza kukubalika. Shaykh alikuwa akijirudi pindi alipokutana na dalili sahihi inayokwenda kinyume na kauli yake, na aliacha kauli yake na kufuata dalili hiyo iliyosihi bila kuangalia imetoka kwa nani. Kuna baadhi ya Hadiyth alizokuwa akiitakidi kuwa sahihi kwa elimu yake, na baadaye zikambainikia au akatanababishwa kuwa si sahihi, akawa anajirudi haraka na kukubali na kuzitaja katika vitabu vyake.















Elimu Yake Na Athari Yake Kwa Watu







Shaykh alikuwa katika daraja ya Al-Haafidh (Mwanachuoni wa Hadiyth aliyehifadhi Hadiyth laki moja (100,000) pamoja na mnyororo wa wapokezi wake na ‘mutuun’ zake (maneno ya kila Hadiyth). Hayo yanaelezwa na Shaykh ‘Ashiysh aliyemuuliza suala hilo na Shaykh akakataa kumjibu kwa unyenyekevu na kutotaka kujifakharisha, alichojibu baada ya kukazaniwa sana swali hilo, alijibu kwa Aayah hii: ((Na neema yoyote mliyonayo inatoka kwa Allaah)) [An-Nahl: 56].[7]







Katika wasia wake Shaykh alitoa hadiya maktaba yake ya vitabu na kazi zake za uandishi kukitunuku Chuo Kikuu Cha Madiynah Al-Munawarah kama alivyosema katika wasia wake: “Nimeiachia maktaba yangu – vyote vilivyomo, vikiwa ni vilivyochapishwa tayari, au nakala, au kazi nilizoziandaa kuchapishwa; kwa maandishi ya mkono wangu, au ya mwengine aliyeniandikia – kwa kuipa maktaba ya Jaami’atul-Islaamiyah (Chuo Cha Kiislam) kilichopo katika mji wa Madiynah. Kwa sababu ni kumbukumbu nzuri kwa chuo hicho wakati nilipokuwa huko nikifundisha, kwa kulingania kwake kwa msingi wa Kitaab (Qur-aan) na Sunnah kwa kufuata mwenendo (Manhaj) wa wema waliotangulia (Salafus-Swaalih)”.[8]







Alikuwa mtu wa kawaida sana, mnyenyekevu asiye na makuu na asiyetofautishwa na watu wengine ila kwa vitendo na maongezi yake ya kielimu.







Katika kipindi cha maisha yake, alifanya tafiti nyingi na kuzichambua taqriban silsilah 30,000 za wasimulizi wa Hadiyth (isnaad), akiwa ametumia kiasi cha miaka 60 ya umri wake kusoma na kupitia vitabu vya Sunnah na kuwa karibu navyo kwa muda wote huo, na mawasiliano ya nyanja hiyo, na pia kuwa karibu na Ma’ulamaa wa elimu hiyo.[9]















Sifa Njema Walizotoa Ma’ulamaa Kwa Mujaddid Wa Zama Hizi Shaykh Muhammad Naaswir-Ud-Diyn Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu)







Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz Bin Baaz [Aliyekuwa Mufti Wa Saudi Arabia] (Allaah Amrehemu)







Sikumuona mtaalamu wa Hadiyth za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) katika enzi yetu ya leo chini ya qubah la mbingu kama Mwanachuoni mkubwa Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy. Aliulizwa kuhusu Hadiyth ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) isemayo:



((Allaah Hutuma kwa Ummah huu Mwanachuoni katika kila miaka mia mtu wa kupiga msasa mambo ya dini Yake)).[10] Aliulizwa ni nani mpiga msasa wa karne hii? Akajibu: Ninadhani Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy, ndiye mpiga msasa wa zama hizi. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.











Mwanachuoni Shaykh Muhammad Ibn Swaalih Al-‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu)







Yale niliyoyajua kuhusu Shaykh na ambayo ni kidogo wakati nilipokuwa nakutana naye, ni kuwa yeye ana shime ya hali ya juu ya kutumia Sunnah na kupiga vita bid’ah; sawasawa katika ‘Aqiydah au matendo. Ama kwa kusoma kwangu vitabu vyake, hakika nimemjua vyema kwa hayo. Ana elimu kubwa ya Hadiyth kwa upande wa Riwaayah na Diraayah. Allaah Amewanufaisha watu wengi kutokana na yale aliyoyaandika kwa upande wa elimu, mfumo na mwelekeo katika taaluma ya Hadiyth. Hii ni faida kubwa sana kwa Waislam. Himdi ni za Allaah. Ama kwa upande wa uhakiki wake wa kitaaluma katika fani ya Hadiyth, basi hayo hayasemeki.











Mwanachuoni Mfasiri Shaykh Muhammad Al-Amiyn Ash-Shanqiytwiy (Allaah Amrehemu)







Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz Al-Haddaah anasema:



“Hakika Mwanachuoni mkubwa Ash-Shanqiytwy anamtukuza Shaykh Al-Albaaniy utukuzo wa kushangaza. Anapomuona anapita nailhali yeye yuko katika darsa yake katika Msikiti wa Madiynah, kasha husimamisha darsa lake, husimama na kumsalimia kwa ajili ya kumuheshimu”.











Shaykh ‘Abdul-Muhsin Al-’Abaadiy (Allaah Amhifadhi)







Bila shaka Shaykh Al-Albaaniy, alikuwa ni katika Ma’ulamaa wa kipekee walioumaliza umri wao katika kuitumikia Sunnah, kuitungia vitabu, kulingania kwa Allaah Mtukufu, kuinusuru ‘Aqiydah ya kisalafiya, kuipiga vita bid'ah, na kutetea Sunnah ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم). Yeye ni katika Ma’ulamaa wazuri wenye sifa za kipekee. Sifa zake zimeshuhudiwa na watu maalumu na wa kawaida. Hakuna shaka kwamba kumpoteza Mwanachuoni kama huyu, ni katika misiba mikubwa inayowapata Waislamu. Allaah Amlipe kheri nyingi kutokana na juhudi zake kubwa na Amweke katika Pepo Yake pana.











Mufti Wa Zamani Wa Saudia Mwanachuoni Shaykh Muhammad Bin Ibraahiym Aal Shaykh (Allaah Amrehemu)







Amesema kuhusu Shaykh Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu): “Yeye ni mwana Sunnah, mpiganiaji haki, na mwenye kupambana na watu wasiofuata haki”.











Mwanachuoni Shaykh Muqbil Al-Waadi'iy (Allaah Amrehemu)







Hakika katika taaluma ya Hadiyth, hakuna mtu kama Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy. Na Allaah Amenufaisha kwa elimu yake na vitabu vyake mara nyingi zaidi kuliko yale wanayoyafanya wale wenye hamasa na Uislam pasi na elimu ya kutosha, na wasio na msimamo. Ninaloliamini na ambalo ni deni kwangu mbele ya Allaah ni kuwa, Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy, ni katika waipigao msasa Dini na wanasadikishwa na neno la Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم):



((Allaah Hutuma kwa Ummah huu mwanzoni mwa kila miaka mia mtu wa kupiga msasa mambo ya Dini Yake)).[11]











Mwanachuoni Wa Hadiyth India, Shaykh ‘Abdus-Swamad Sharafud-Diyn (Allaah Amrehemu)







Katika moja ya barua walizokuwa wakiandikiana na Shaykh Al-Albaaniy katika masuala ya kitafiti ya Hadiyth, alikiri kuwa Shaykh Al-Albaaniy alikuwa Mwanachuoni mkubwa wa Hadiyth.











Waziri Wa Masuala Ya Kiislamu, Al-Awqaaf, Ulinganio Na Uongozi Shaykh Swaalih Bin ‘Abdil-‘Aziyz Bin Muhammad Aali Shaykh







Alisema: “Shukrani ni za Allaah kwa hukumu Zake na uwezo Wake ((Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea)).[12] Hakuna shaka kwamba kumpoteza Mwanachuoni Mkubwa Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn Al-Albaaniy, ni msiba. Yeye ni katika Wanachuoni wakubwa wa Ummah na mabingwa wa Hadiyth. Kwa Ma’ulamaa hao (Shaykh Al-Albaaniy), Allaah Mtukufu Ameilinda Dini hii na Akaieneza Sunnah kupitia kwao…”















Kipindi Cha Mwisho Cha Maisha Yake Na Kifo Chake







Shaykh (Allaah Amrehemu) hakutulia kutafuta elimu hadi umri wa miaka 86, akisoma, akifundisha, akielimisha, akiandika vitabu, akiandika barua kwa Wanachuoni wenzake kuwapongeza, kuwanasihi, kuwakosoa makosa ya vitabuni mwao au fatwa zao. Hadi umri huo hakuwa akiacha kutafiti masuala ya Hadiyth, akipangua sahihi na dhaifu na za kutungwa, aliweza kugawa vitabu vingi vikubwa vya Hadiyth kama vya Maimaam Abu, Dawuud, Ibn Maajah, At-Tirmidhy, An-Nasaaiy na wengineo, akaweza kuvigawa Sahihi zake na Dhaifu zake na kuwasaidia kuwarahisishia wenye elimu na wanafunzi katika uandishi na tafiti zao.







Shaykh anakumbukwa sana kwa kazi hiyo iliyosaidia Ummah leo hii, na kuuamsha kujua Hadiyth sahihi na dhaifu na pia kuwafanya wengi wawe karibu na kuifuatilizia elimu ya Hadiyth na sayansi yake. Aliyafanya yote hayo – kwa sababu moyo wake ulikuwa umefungamana nayo hayo kwa mapenzi ya juu – na hakuacha hadi taqriban miezi miwili ya mwisho ya maisha yake, alipokuwa dhaifu akiugua kitandani. Pamoja na magonjwa mazito yaliyomdhoofisha sana na kutotoka kitandani, hakuacha kusoma wala hakupoteza kumbukumbu zake, akiwa anamjua kila aliyekwenda kumtazama, akimuita kila mmoja kwa jina lake! Hadi Allaah (سبحانه وتعالى) Alipoirejesha roho yake na akamfisha katika nyakati za mwisho za Alasiri, siku ya Jumamosi, tarehe 22 katika mwezi wa Jumaadah Al-Aakhirah, mwaka 1420 H sawa na 10-02-1999 M huko ‘Ammaan, Jordan.



Wanachuoni, watafuta elimu, wanafunzi, na watu wa kawaida wote waliathirika sana na kifo cha Shaykh. Taarifa za kifo chake zilipowafikia Waislam, majonzi yalienea pote na wengi kuhisi kuwa ile elimu na yule ‘Mujaddid’ (Mkarabati wa Dini) wa zama hayupo nao tena. Mwaka huo ulikuwa ni mwaka wa huzuni, kwa kutanguliwa na kifo cha Mwanachuoni mkubwa wa zama hizo hizo ambaye alikuwa Mufti wa Saudia wa wakati huo, Shaykh Al-‘Alaamah ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdullaah bin Baaz, na baada yao kufuatiwa na kifo cha Mwanachuoni Shaykh Muhammad bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn, Mashaykh wengine wakubwa waliofariki katika mwaka huo ni, Shaykh Swaalih bin 'Aliy Ghaswuun, Shaykh 'Aliy Twantwawiy, Dkt. Mustwafaa Az-Zarqaa, Shaykh Mana'a Al-Qahtwaan na Shaykh 'Atwiyah bin Muhammad Saalim (Allaah Awarehemu wote hao na Awaweke katika pepo Yake Tukufu).







Abu ‘Abdillaah (1432 H – 2011 M)












[1] Ni fani ya Hadiyth inayohusiana na uaminifu wa wasimulizi wa Hadiyth na inakusanya habari zao zinazothibitisha uaminifu au udhaifu wa hao wasimulizi.

[2] Sayansi ya Hadiyth

[3] Hayaatul Al-Albaaniy, Muhammad Ash-Shaybaaniy. Al-Albaaniy mwenyewe anayaeleza hayo pia kwenye vitabu vyake ‘Mukhtaswar Al-’Uluww’ na ‘Tahdhiyrus-Saajid’.

[4] Kitabu hiki kimeshatafsiriwa na mwandishi kwa lugha ya Kiswahili na kinapatikana maeneo mbalimbali kwa jina “Sifa Ya Swalah Ya Mtume ”.

[5] Kitabu hiki kilishatafsiriwa na mwandishi wa Historia hii ya Shaykh na kinapatikana kwa jina “Adabu Za Ndoa Katika Sunnah Iliyotwaharika.” Chapa za mwanzo kimetawanywa bure na shukurani zote ni Zake Allaah.

[6] Kitabu hiki kimeshatafsiriwa na mwandishi kwa jina “Sifa Ya Swalah Ya Mtume” na chapa za mwanzo zimetawanywa bure na himidi zote Anastahiki Allaah.

[7] Shaykh Husayn Al-’Awaaishah, Swafahaat Baydhwaa Min Hayaati Shaykhina Al-Albaaniy, uk. 40.

[8] Samiyr bin Amiyn Az-Zuhayriy, Muhadith Al-’Aswr, uk.78.

[9] Abu Hudhayfah: 20 Points Regarding Shaykh al-Albaanee

[10] Imepokewa na Abu Daawuud, na imeelezewa kuwa ni sahihi na Al-’Iraaqiy na wengineo.

[11] Imepokewa na Abu Daawuud, na imeelezewa kuwa ni sahihi na Al-’Iraaqiy na wengineo.

[12] Al-Baqarah:
 
Naam ndugu zangu tumeona hapo Sheikh Albaany pamoja na kuwa na umri wa miaka 86 bado hakuacha kusoma au kutafuta elimu,je vipi kuhusu sisi tunajitihada gani?

Azimia kujifunza mambo ya dini yatakufaa wewe binafsi na ambao utakutana nao ukawapa au kuwafahamisha kile ulichojifunza na utakuwa mwenye kupata thawabu toka kwa Allah

Kama ambavyo mimi napata thawabu kwa kushare haya mambo ya kheri

Penda kusoma kuna faida kubwa!
 
بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ



UTANGULIZI WA KITABU





Sifa njema zote ni za Allaah Aliyefanya Swalah kuwa ni fardhi kwa waja Wake na kuwaamrisha kuitekeleza ipasavyo; Aliyeambatanisha kufaulu na furaha kutokana na unyenyekevu katika Swalah; Aliyefanya kuwa ni kigezo cha Iymaan na kufr; na aliyeifanya ni kizuizi cha mambo machafu na vitendo viovu.



Swalah na Salaam zimshukie Mtume Muhammad ambaye Amefunuliwa na maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى):



وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ

((Nasi Tumekuteremshia wewe Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao, wapate kufikiri))

Na ambaye ametekeleza kikamilifu kazi hii. Swalah ilikuwa ni jambo muhimu kabisa aliyowaeleza watu kwa kauli na vitendo, hata aliwahi kuswali mara moja katika minbar akisimama, akirukuu na kusujudu, kisha akasema: ((Nimefanya hivi ili mnifuate na mjifunze Swalah yangu)). Ametuwajibisha tumfuate anavyoswali kwa kusema: ((Swalini kama mlivyoniona nikiswali)). Amebashiria pia kuwa atakayeswali kama anavyoswali, atakuwa katika ahadi ya Allaah kwamba Atamuingiza katika Pepo, akisema: ((Swalah tano ambazo Allaah (عزوجل) Amezifaradhisha. Atakayefanya wudhuu wake vizuri, akaziswali kwa wakati wake, na kutimiza rukuu zake, sujudu zake na unyenyekevu, ana dhamana kutoka kwa Allaah kwamba Atamsamehe, lakini asiyetekeleza hana dhamana kutoka kwa Allaah, Akipenda Atamsamehe au Akipenda Atamuadhibu))



Swalah na amani pia ziwafikie jamaa zake na Maswahaba zake Waswalihina waliotuletea ‘Ibaadah yake (صلى الله عليه وآله وسلم), na Swalah, kauli na vitendo vyake na wakavifanya hivyo kuwa ni madhehebu na mfano bora kwao wa kufuata; na wale watakaofuata nyayo zao hadi siku ya Qiyaama.



Nilipomaliza kusoma kitabu cha Swalah katika At-Targhiyb wat-Tarhiyb cha Al-Haafidhw Al-Mundhiry (رحمه الله) na kuwafundisha ndugu zetu miaka minne iliyopita, ilidhihirika kwetu umuhimu wa nafasi ya Swalah katika Uislamu; na thawabu, neema na fadhila zinazowasubiri watakaoitekeleza na kuiswali sawa sawa; na kwamba yote inatofautiana, kutegemea ukaribu wa Swalah ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم). Hii ndivyo ilivyoashiriwa katika usemi wake: ((Hakika mja huswali Swalah ambayo haandikiwi kitu ila sehemu ya kumi, au ya tisa, ya nane, ya saba, ya sita, ya tano, robo, thuluthi au nusu yake)). Hivyo nikawakumbusha ndugu kwamba haiwezekani kutekeleza Swalah ipasavyo au hata kuikaribia ila tutambue maelezo ya sifa ya Swalah ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), ikijumuisha namna ya kuiswali, mfumo wake, du'aa na adkhkaar zake, kisha tufanye jitihada kutumia elimu hiyo katika utekelezaji kwa makini, hapo ndipo tutaweza kuwa na tamaa kwamba Swalah zetu zitatuzuia na mambo machafu na vitendo viovu na ndipo tutaandikiwa thawabu na baraka zilizotajwa katika usimulizi mbali mbali.



Lakini, maelezo kwa urefu juu ya vipengele vyote hivi vya Swalah sio wepesi kutekelezwa na watu wengi siku hizi, hata Maulamaa wengi kwa sababu ya kujihusisha na kujiwekea mipaka ya madhehebu fulani. Lakini kwa yeyote mwenye kujali na kusaidia katika ukusanyanji na utafiti wa Sunnah zilizotakasika, atajua kwamba katika kila madhehebu kuna Sunnah ambazo hazipatikani katika madhehebu mengine; juu ya hivyo, katika kila dhehebu kuna usemi na vitendo ambavyo havipatikani dalili za usahihi wake kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم). Mengi hayo hupatikana katika usemi tu wa Maulamaa waliofuatia, wengi wao tunaona kwamba wanahusisha haya kwa Mtume. Ndio maana Maulamaa wa Hadiyth (Allaah Awalipe wote vyema) wametoa vitabu vya Takhriyj kuhusu vitabu maarufu vya Maulamaa waliofuatia, wakielezea daraja ya kila Hadiyth iliyotolewa humo: mfano kama ni 'Swahiyh' au 'Dhaifu', au 'Imezushwa'. Mifano ya vitabu hivi vya Takhriyj ni: 'Al-‘Inaayah fiy Ma'rifah Al-Ahaadiyth Al-Hidaayah na At-Twuruq wal-Wasaail fiy Takhriyj Ahaadiyth Khulaaswah Ad-Dalaail cha Shaykh 'Abdul-Qaadir bin Muhammad Al-Qurayshiy Al-Hanafiy; Naswb Ar-Raaayah li Ahaadiyth Al-Hidaayah cha Haafidwh Zayla'iy, na mukhtasari yake ya Ad-Diraayah cha Haafidhw Ibn Hajr Al-Asqalaaniy ambaye pia ameandika Talkhiys Al-Habiyr fiy Takhriyj Ahaadiyth Ar-Raafi'iy Al-Kabiyr; kuna vingi vingenvyo, kuvitaja vyote vitazidisha urefu wa maelezo.




















[1] Suratun-Nahl: 16: 44

[2] Al-Bukhaariy na Muslim – itafuatia baadaye kikamilifu

[3] Al-Bukhaariy na Ahmad

[4] Maalik, Abu Daawuud, An-Nasaaiy na Ibn Hibbaan. Hadiyth Swahiyh iliyobainishiwa kuwa Swahiyh na Maimamu wengi. Nimeitoa takhriyj yake katika Swahiyh Abi Daawuud (451, 1276)

[5] Swahiyh – Imekusanywa na Ibn Al-Mubaarak katika Az-Zuhd (10/21/1-2), Abu Daawuud na An-Nasaaiy ikiwa na isnaad nzuri; Nimetoa takhriyj yake katika Swahiyh Abi Daawuud (761).



[6] Abul-Hasanaat Al-Laknawiy kasema katika An-Naafi' Al-Kabiyr Liman Yutwaali' Al-Jaami' As-Swaghiyr (Uk. 122.3) baada ya kuvikadiri vitabu vya Fiqh ya Hanafiy na kutaja vipi vya kutegemea na vipi visitegemewe: "Yote hayo tuliyosema kuhusu daraja zinazohusika za ukusanyaji huu unahusiana na yaliyomo katika mas-ala ya Fiqhi; lakini ama yaliyomo kuhusu Hadiyth za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), hazihusiki kwani vitabu vingi ambavo Mafuqahaa wanatagemea vimejaa uzushi wa Hadiyth, achilia mbali hukmu za Maulamaa. Ni dhahiri kwetu kutokana na uchambuzi mpana kwamba ingawa waandishi wake walikuwa ni mahodari lakini hawakuwa makini katika kunukuu usimulizi".



Si Maulamaa wa Hadiyth wala hawakutoa hizi Hadiyth kutoka kwa wakusanyaji wa Hadiyth".

Ash-Shawkaaniy pia alitaja Hadiyth hii katika Al-Fawaaid Al-Majmuu'ah Fil Ahaadiyth Al-Mawdhwuu'ah ikiwa na maneno yaliyofanana, kisha akasema (Uk. 54): "Hii imezushwa bila shaka – sijaipata hata katika mkusanyo wa Hadiyth za Uzushi! Bali imekuwa ni maarufu baina ya wanafunzi wa Fiqh katika mji wa San'aa katika karne yetu, na wengi wameanza kuitekeleza. Sijui nani aliyewazushia. Allaah Awahizi waongo".



[7] Maneno ya Imaam An-Nawawiy (رحمه الله) katika Al-Majmuu' Sharh Al-Muhadhdhab (1/60) yanaweza kujumuishwa kama ifuatavyo: "Maulamaa watafiti wa Hadiyth na wengineo wamesema kwamba ikiwa Hadiyth ni dhaifu, haitotajwa kuwa: 'Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)kasema/katenda/kaamrisha/kakataza….' Au ibara yoyote nyingine inayotaja uhakika, bali itasemwa: 'Imeripotiwa/imenukuliwa/imesimuliwa kutoka kwa…' au ibara zingine zinazodokeza shaka. Wanasema kuwa ibara za uhakika huwa ni Swahiyh na Hadiyth Hasan na ibara zenye shaka huwa ni nyinginezo. Hii ni kwa sababu ibara zinazotaja uhakika zina maana kwamba yanayofuatia ni Swahiyh, hivyo zinatumika kwa hali ya Usahihi pekee, au sivyo itakuwa ni kumzulia (صلى الله عليه وآله وسلم).



Jambo hili limepuuzwa na Mafuqahaa wengi wa zama zetu, bali Maulamaa wengi wa nidhamu yoyote, isipokuwa Muhaddithiyn wenye ujuzi. Huu ni uzembe wa kuchukiza kabisa, kwani mara nyingi hutaja Hadiyth Swahiyh: 'Imeripotiwa kutoka kwake kwamba…' Na kuhusu Hadiyth dhaifu: 'Amesema' na: 'Fulani na Fulani ameripoti...' Hivi sio sawa kabisa".



Laknawiy akaendelea kusema: "Kutegemea Hadiyth hii ambayo inapatikana katika vitabu vya uradi na du’aa ni uzushi, nimeandika insha fupi ya kitaalamu na dalili inayoitwa 'Kuwakanusha Ndugu Kutokana Na Uzushi Wa Ijumaa Ya Mwisho Ya Ramadhaan'. Humo nimetoa nukta ambazo zitamulika akili na zitazibua masikio, hivyo isome, kwani ni ya thamani katika maudhui hii na ni ya ubora wa hali ya juu.



Marudio ya Hadiyth za uongo kama hizo katika vitabu vya Fiqhi vimeharibu uaminifu wa Hadiyth nyinginezo ambazo hazikunukuliwa kutoka katika vitabu vya Hadiyth vinvayotegemewa. Maneno ya 'Aliy Al-Qaariy yameashiria haya. Muislamu lazima apokee Hadiyth kutoka kwa watu ambao ni wataalamu katika fani hii, kama usemi wa zamani wa Kiarabu unavyosema: "Watu wa Makkah wanajua njia za milima yao vizuri" na "Mwenye kumiliki anajua vyema vilivyomo nyumbani mwake".



[8] Tanbihi ya Mchapishaji

Katika mlango huu, kuna kazi ya mwalimu wetu pia mwandishi wa Irwaa' Al-Ghaliyl Fiy Takhriyj Manaar As-Sabiyl katika Mijalada 9, na Ghaayah Al-Maraam fiy Takhriyj Ahaadiyth Al-Halaal wal-Haraam, takhriyj ya Ahaadiyth zinazopatikana katika kitabu cha Dkt. Yuusuf Qaradhwaawiy 'Halali Na Haramu Katika Uislamu' (ambacho kina Hadiyth nyingi dhaifu).
 
Sababu Za Kuandika Kitabu Hiki Na Baadhi Ya Vipengele Vyake





Kwa vile sijapata kuona kitabu chenye maarifa mengi kuhusu maudhui hii, nimehisi imeniwajibikia kutoa kitabu ambacho kitakusanya sifa nyingi za Swalah ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa ajili ya manufaa ya ndugu zangu Waislamu wapendao kufuata uongofu wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) katika ibada zao, hadi iwe wepesi kwa yeyote mwenye kumpenda kweli Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) aweze kutumia kitabu hiki kutimiza amri yake: ((Swalini Kama Mlivyoniona nikiswali)).



Hivyo nikaianza kazi hii ngumu, na kufanya utafiti wa Hadiyth zinazohusika kutoka vyanzo mbali mbali za Hadiyth hadi kitabu hiki kilichokuwa sasa mikononi mwako kuwa ni matokeo yake yote. Nikajiwekea masharti nafsini mwangu kwamba nitaziweka Hadiyth zilizokuwa na isnaad Swahiyh pekee kutokana na kanuni za msingi na sheria ya Sayansi ya Hadiyth. Nimepuuza Hadiyth yoyote ambayo imetegemewa na msimulizi asiyejulikana au dhaifu ikiwa imehusianina na maelekezo ya nje, adhkhaar, ubora n.k. wa Swalah. Hii ni kwa sababu naamini kwamba Hadiyth Swahiyh[1] zinatosheleza, na hakuna haja ya zilizo dhaifu kwani zilizo dhaifu hazizidishi kitu isipokuwa dhana (makisio, mashaka) na makisio yasiyo sahihi ni kama Anavyosema Allaah (سبحانه و تعالى):



وَإِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئًا



((Na dhana haisaidii chochote mbele ya haki))[2]



Na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kasema: ((Tahadharini na dhana kwani dhana ni kauli ya uongo))[3]



Kwa hiyo hatuwezi kumuabudu Allaah kwa kufuata Hadiyth zisizo Swahiyh, bali Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ametukataza akisema: ((Jiepusheni na kusema yanayonihusu isipokuwa muyajuayo))[4]. Kwa vile ametukaza kusimulia masimulizi dhaifu, basi pia haipasi kuzitekeleza.



Nimekigawa hiki kitabu katika sehemu mbili; kubwa na ndogo, matini kuu na matini ya kisaidizi/matini ndogo.



Matini kuu imejumuisha matini ya Hadiyth au ibara ilivyochukuliwa humo, pamoja na maneno yanayolingana kuunga pamoja ili kukifanya kitabu chepesi tokea mwanzo hadi mwisho. Nimekuwa makini kuibakisha matini ya kila Hadiyth kama ilivyopatikana katika vitabu vya Sunnah; ambako Hadiyth ilikuwa na meneno tofauti na nimechagua maelezo yaliyo bora kabisa yanayowafikiana na ufasaha, wepesi n.k.. Lakini nimekusanya maneno mengine pamoja; hivyo: "(katika usemi kadha na kadhaa…..)" au "(katika usimulizi kadhaa na kadhaa …)". Sikumtaja Swahaba aliyesimulia Hadiyth ila kwa nadra tu nimefanya hivyo, wala sikumtaja Imaam gani wa Hadiyth aliyekusanya Hadiyth, ili kufanya wepesi usomaji na marejeo.



Ama matini ya kisaidizi/ndogo ni maelezo kutokana na matini kuu. Humo nimefuatilia Hadiyth kutoka asili yake nikifumbua maelezo mbali mbali na njia za usimulizi. Pamoja nayo, nimetoa maelezo katika isnaad zao na usimulizi unaotilia nguvu, pamoja na tanbihi Swahiyh na zenye kutezwa kwa wasimulizi, ikiwa ni Swahiyh au dhaifu kutokana na hukumu za Sayansi ya Hadiyth. Aghlabu njia ya usimulizi moja huwa na nyongeza ya maneno ambayo hayapatikani katika njia nyingine, hivyo nimezitia hizi katika Hadiyth ya asili zilizotajwa katika matini kuu kila ilipowezekana bila ya kuharibu ufasaha, nikiweka nyongeza katika mabano ya mraba […]. bila ya kutaja chanzo gani kilichonacho nyongeza hiyo. Hii imefanywa ikiwa Hadiyth asili yake imetoka kwa Swahaba mmoja, au sivyo nimeitoa peke yake; mfano katika Du'aa za kufungulia n.k. Nyongeza hii ya maneno ziada ni manufaa makubwa ambayo hutoyapata katika vitavu vingi – Sifa njema zote ni za Allaah Ambaye Kwa Neema Zake Mema hutimia.



Kisha, nikataja katika matini ya kisaidizi/matini ndogo Madhehebu ya Maulamaa kuhusu Hadiyth tulizozitoa na dalili zake kila moja pamoja na hoja zake na kubainisha uzito wake na udhaifu wake. Kisha tukachagua rai iliyo sahihi ambayo tumeiweka katika matini kuu. Pia katika matini ya kisaidizi tumetoa baadhi ya mas-ala ambayo hakuna matini katika Sunnah, lakini imehitaji Ijtihaad, na haikuja chini ya maudhui ya kitabu hiki.



Kwa vile kuchapishwa kitabu kuwekwa matini kuu na matini ya kisaidizi haiwezekani sasa kwa sababu mbali mbali, tumeamua kukichapisha kikiwa na matini kuu ya kitabu (pamoja na tanbihi fupi) kwa uwezo wa Allaah, na kukiita 'Swiffatus-Swalat 'An-Nabiyy' (صلى الله عليه وآله وسلم)Min At-Takbiyr ilaa At-Tasliym Kaannaka Taraaha' (Sifa ya Swalah ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) Kuanzia Takbiyra Ya Mwanzo hadi Kumalizika kwa Salaam Kama Kwamba Unaiona)"





Namuomba Allaah Ajaalie kazi hii iwe khaswa kwa ajili Yake, na iwasaidie ndugu zangu katika Iymaan kunufaika nayo kwani Yeye ni Mwenye Kusikia Aliye Karibu.











[1] Istilahi ya 'Hadiyth Swahiyh' inajumuisha Swahiyh na Hasan mbele ya macho ya Muhaddithiyn, ikiwa ni Hadiyth Swahiyh lidhaatihi au Swahiyh lighayrihi, au Hasan lidhaatihi au Hasan lighayrihi.



[2] An-Najm: 53: 28

[3] Al-Bukhaariy Na Muslim

[4] Swahiyh – imekusanywa na At-Tirmidhiy, Ahmad na Ibn Abi Shaybah.
 
Back
Top Bottom