Ramadhan Special Thread
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



037-Muda Wa Kupukusa



Alhidaaya.com





Sharia imeweka muda wa siku tatu na masiku yake kupukusa juu ya khufu mbili kwa msafiri, na siku moja na usiku wake kwa mkazi. Haya ndiyo yaliyokubaliwa na Jamhuri ya Maulamaa wa Hanafi, Hanbali, Dhwaahir na Ash-Shaafi’iy katika madhehebu mapya na Adh-Dhwaahiriyyah. [Al-Mabsuwtw (1/98), Al-Ummu (1/34), Al-Mughniy (1/209) na Al-Muhalla (2/80)].



Dalili ya hayo ni haya yafuatayo:



1- Ni Hadiyth ya ‘Aliy (Allaah Amridhie) aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameweka muda wa siku tatu na masiku yake kwa msafiri, na siku moja na usiku wake kwa mkazi”.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (276) na An-Nasaaiy (1/84)].



2- Ni Hadiyth ya ‘Ouf bin Maalik Al-Ashja’iy aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru kupukusa juu ya khufu mbili katika Vita vya Tabuk siku tatu na masiku yake kwa msafiri, na siku moja na usiku wake kwa mkazi”.[Hadiyth Swahiyh.: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (6/27) kwa Sanad Swahiyh, nayo ina ushahidi toka Hadiyth ya Abu Bakrah iliyoko kwa Ibn Maajah (556) na wengineo].



3- Hadiyth ya Swafwan bin ‘Assal, amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akituamrisha tunapokuwa safarini, tusizivue khufu zetu siku tatu na masiku yake ila kwa janaba, lakini si kwa kwenda haja kubwa, au ndogo, au kulala”. [Hadiyth Hasan: Imetajwa hivi karibuni].



Maalik amekwenda kinyume na haya (nayo ni kauli ya zamani ya Ash-Shaafi’iy). Yeye anaona kwamba hakuna muda wake maalumu, bali mtu anaweza kupukusa juu ya khufu zake madhali hakuzivua au kupatwa na janaba!! Na ndivyo hivi hivi alivyosema Al-Layth. [Al-Mudawwanah (1/41) na Bidaayat Al-Mujtahid (1/24)].



Wao wametoa hoja kwa Hadiyth ambazo ni Dhwa’iyf. Kati ya Hadiyth hizo ni:



1- Iliyopokelewa toka kwa Ubayya bin ‘Ammaarah, amesema: “Nilisema: Ee Rasuli wa Allaah! Je, nipukuse juu ya khufu mbili? Akasema: Ndiyo. Nikasema: Siku moja? Akasema: Siku moja. Nikasema: Na siku mbili je? Akasema; Na siku mbili. Nikasema: Na siku tatu je? Akasema: Na siku uzitakazo”.[Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (157), At-Tirmidhiy na Ibn Maajah (553).]



2- Yaliyopokelewa toka kwa Khuzaymah bin Thaabit, amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuwekea siku tatu, na lau kama tungelimtaka atuongezee, basi angetuongezea”.[Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (1/280)]. Yaani kupukusa juu ya khufu mbili kwa msafiri. Na hili lau kama lingekuwa sahihi, basi haliwezi kuwa hoja, kwani ni dhana tu ya Swahaba, na sisi tusingelichukulia.



3- Yaliyopokelewa toka kwa Anas bin Maalik kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((إذا توضأ أحدكم ولبس خفيه فليصل فيهما، وليمسح عليهما، ثم لا يخلعهما إن شاء إلا من جنابة))

((Anapotawadha mmoja wenu akazivaa khufu zake, basi aswali nazo na apukuse juu yake, kisha asizivue muda autakao, isipokuwa kwa janaba)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (1/280), Atw-Twahaawiy (1/48) na Ad-Daara Qutwniy (72).



Hadiyth zote hizi ni dhwa’iyf na hazifai kwa ushahidi.



4- Ni athar iliyopokelewa toka kwa ‘Aamir akisema: “Nilitoka Sham kuelekea Madiynah. Niliondoka siku ya ijumaa na nikaingia Madiynah siku ya ijumaa. Kisha niliingia kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab akaniuliza: Ni lini uliziivaa khufu zako? Nikajibu: Siku ya ijumaa. Akauliza: Je, ulizivua? Nikajibu: Hapana. Akasema: Umefanya sawa”.



Hii pia ni dhwa’iyf. Al-Bayhaqiy amesema: “Tumepokea toka kwa ‘Umar kuhusu wakati. Basi inawezekana kuwa ima alirejea katika kauli hiyo wakati ilipomfikia toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au iwe kauli yake iliyowafikiana na Sunnah Swahiyh iliyo mashuhuri zaidi. Na kwa ajili hiyo, Ibn Hazm amesema katika kitabu cha Al-Muhalla (2/93): “ Haiswihi kwa Swahaba yeyote kukhalifu muda uliowekwa isipokuwa Ibn ‘Umar peke yake”.
 
Naomba nitoe ufafanuzi kidogo khufu ni kama kiatu cha ngozi mfano wa soksi ambazo ndio zinazungumziwa hapa

Kwahiyo ukizivaa hizo hauna haja ya kuzivua bali unapaka maji juu yake kama vile unatia udhu

Na baadhi ya watu naona wakivaa soksi wakitia udhu wanafuta tu juu yake,naona wamechukua kama hukumu ya khufu
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



038-Muda Wa Kupukusa Unapoanzia



Alhidaaya.com





Imejulikana kwamba muda wa kupukusa kwa mkazi ni siku moja na usiku wake, na kwa msafiri ni siku tatu na masiku yake. Basi ni wakati gani muda huo unaanza kuhesabiwa? Katika hili, Wanachuoni wana kauli tofauti:



Ya kwanza



Unaanza pale anapopata hadathi ya kwanza baada ya kuzivaa. Hii ni kauli ya Sufyaan Ath-Thawriy, Ash-Shaafi’iy, Abu Haniyfa na wenzake. Na hili li wazi katika madhehebu ya Hanbali. [Al-Mabsuwtw (1/99), Al-Majmu’i(1/470), Al-Mughniy (1/291) na Al-Awsatw (1/443)].



Wamesema kuwa kipindi cha baada ya hadathi, ni wakati unaoruhusiwa kupukusa.



Ya pili



Unaanza kuanzia wakati wa kuzivaa. Ni kauli ya Al-Hasan Al-Baswriy. [Al-Ikliyl Sharh Manaar As-Sabiyl cha Shaykh Wahiyd ‘Abdu Ssalaam (1/136)].



Ya tatu



Atapukusa Swalaah tano, yaani Swalaah 15 kwa msafiri (3X5), na wala asipukuse zaidi ya hivyo. Ni madhehebu ya Ash-Sha’abiy, Is-haaq, Abu Thawr na wengineo. [Al-Mughniy (1/291), Al-Majmu’u (1/466) na Al-Awsatw (1/444)].



Ya nne



Unaanza pale inapojuzu kwake kupukusa baada ya hadathi, sawasawa ikiwa alipukusa au hajapukusa na wala hakutawadha kwa namna ambayo lau kama atapukusa baada ya kupita sehemu ya muda, itambidi apukuse ule muda uliosalia basi. Haya ni madhehebu ya Ibn Hazm. Yeye ameyajadili madhehebu mengi. [Al-Muhalla cha Ibn Hazm (2/95 na kurasa zinazofuatia)].



Ya tano



Unaanza tokea pukuso la kwanza baada ya hadathi. [Masaail Ahmad cha Abu Daawuud (10) na Al-Muhallaa (2/95)].



Ni kauli ya Ahmad bin Hanbali na Al-Awzaa’iy. Pia ni kauli iliyoungwa mkono na An-Nawawiy, Ibn Al-Mundhir na Ibn ‘Uthaymiyn. Na hii ndio kauli yenye nguvu zaidi kutokana na maana bayana ya neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((يمسح المسافر)) و ((يمسح المقيم))

((Msafiri hupukusa)) na ((Mkazi hupukusa)).



Na haiwezekani kuthibitishwa kwamba mtu anapukusa, ila kwa kitendo cha kupukusa. Na haijuzu kuipiga pande maana hii bayana bila dalili au ushahidi. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.



Na kwa haya, ikiwa mtu ametawadha wakati wa Swalaah ya adhuhuri na akavaa khufu zake saa sita kwa mfano, kisha akabakia na utwahara wake hadi saa tisa alasiri, kisha wudhuu ukamtenguka na wala hakutawadha mpaka saa kumi (baada ya Swalaah ya alasiri) na akapukusa, basi atapukusa mpaka saa kumi alasiri ya kesho yake ikiwa ni mkazi, na mpaka siku ya nne ikiwa ni msafiri.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



039-Mkazi Akipukusa Kisha Akasafiri



Alhidaaya.com





Aliyepukusa khufu zake naye ni mkazi kwa muda wa chini ya siku na usiku wake kisha akasafiri, basi Maulamaa wana kauli mbili:



Ya kwanza:



Ni haki yake kupukusa mpaka akamilishe siku tatu na masiku yake kwa kujumlisha na ule muda aliopukusa kabla ya kusafiri. Haya ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Abu Haniyfah na wenzake, na riwaya iliyopokelewa toka kwa Ahmad. Ibn Hazm pia amesema hivyo. [Ikhtilaaf Al’ulamaa cha Al- Maruuziy (uk.31), Al-Mughniy (1/299) na Al-Muhalla (2/109)].



Ya pili:



Ni haki yake kupukusa mpaka akamilishe siku moja na usiku wake, kisha itampasa aoshe miguu yake anapotawadha. Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Is-Haaq. [Al-Ummu (1/35), Ikhtilaaf Al’ulamaa (uk.31) na Al-Awsatw (1/446)].



Yenye nguvu ni kuwa ni haki yake kupukusa mpaka akamilishe siku tatu na masiku yake kwa vile mtu huyu inapomalizika siku na usiku wake na yeye ni msafiri, basi ana haki ya kuutimiza muda kutokana na uwazi wa maana ya Hadiyth:

((يمسح المسافر ثلاثة أيام ولياليهن))

((Msafiri hupukusa siku tatu na masiku yake)).
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



040-Msafiri Akipukusa Kisha Akawasili Mjini Kwake



Alhidaaya.com





Ikiwa msafiri atapukusa juu ya khufu zake siku moja na usiku wake au zaidi kisha akawasili kwake, ni lazima azivue khufu zake, aoshe miguu yake anapotawadha, kisha atakuwa na hali ile ile ya mkazi.



Na ikiwa msafiri amepukusa kwa muda wa chini ya siku na usiku wake, basi inajuzu kwake anapowasili mjini akamilishe muda uliosalia wa siku moja na usiku wake, kisha ni lazima azivue.



Ibn Al-Mundhir amenukulu Ijma’a ya kila Mwanachuoni anayezungumzia kwa kuainisha kuhusu muda wa kupukusa. [Al-Awsatw (1/446)].
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



041-Mlango Wa Twahara: Masharti Ya Kupukusa



Alhidaaya.com





Ili kupukusa juu ya khufu mbili kuweze kujuzu, ni sharti mtu azivae akiwa twahara. Imepokelewa toka kwa Al-Mughyrah bin Shu’ubah amesema: “Nilikuwa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika safari usiku mmoja. Nilimmiminia maji toka katika chombo, naye akaosha uso wake na mikono yake, na akapaka kichwa chake. Kisha niliinama mzima mzima ili nizivue khufu zake naye akanambia:

((دعهما، فإني أدخلتهما طاهرتين))

((Ziwache, kwani mimi nimezivaa nailhali miguu ni twahara)).

Kisha akapukusa juu yake. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (206) na Muslim (232)].



Hadiyth hii imeufanya utwahara kuwa ni sharti ya kujuzu kupukusa kabla ya kuzivaa khufu mbili. Na jambo lenye kufungamanishwa na sharti, halijuzu ila kwa kuwepo sharti hilo. Na wudhuu ndio utwahara wa kisharia uliochukuliwa na Jamhuri ya Maulamaa. [Fat-h Al-Baariy (1/370)].



Faida



Mwenye kutawadha, kisha akaosha mguu wake mmoja halafu akauvisha khufu, kisha akauosha mguu wake mwingine halafu akauvika khufu, basi wudhuu wake unapotenguka, haitojuzu kwake kupukusa kwa sababu alivaa khufu moja kabla ya kukamilisha wudhuu wake. Lakini kama aliivua ya kwanza kisha akaivaa, basi itajuzu kupukusa. Haya yamesemwa na Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad. [Al-Muwattwa (1/46), Al-Ummu (1/33) na Al-Mughniy (1/282)].



Ama Abu Haniyfah na Ahmad (katika moja ya riwaya mbili), Ibn Hazm, Ibn Al-Mundhir na Shaykh wa Uislamu, wao wanaona kwamba inajuzu kwake kupukusa juu ya khufu hizo kwa mazingatio ya ukweli kuwa alizivaa katika miguu yake yote miwili hali ya kuwa ni twahara. [Al-Mabsuwtw (1/99), Al-Awsatw (1/442), Majmu’u Al-Fataawaa (21/209) na Al-Muhalla (1/100)].



Ninasema:



“Kusema kuwa inajuzu, hakuna tatizo lolote mpaka itakapoonyesha dalili kwamba utwahara haugawanyiki, na hivyo kupelekea kwenye kuzuia. Na kwa kiakiba tu na tahadhari, ni vizuri kuingiza miguu miwili katika khufu baada ya kumaliza kutawadha. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



042-Je, Khufu Iliyotoboka Hupukuswa?



Alhidaaya.com





Mafuqahaa wengi wameshurutisha kwamba ili kupukusa juu ya khufu mbili kujuzu, ni lazima ziwe ni zenye kusitiri mahala palipolazimu kuoshwa katika wudhuu. Kwa ajili hiyo, wamekataza kupukusa juu ya khufu iliyotoboka, kwani huonekana kupitia khufu hiyo, mahala pa viungo vinavyolazimu kuoshwa. Na kuosha na kupukusa havikutani pamoja, na kwa hivyo hukmu ya kuosha inapewa uzito zaidi.



Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Ahmad. [Al-Ummu (1/28), Masaail Ahmad cha Ibn Haani (1/18) na Al-Mughniy (1/287)].



Na Maalik na Abuu Haniyfah wamesema kuwa inajuzu kupukusa juu ya khufu iliyotoboka madhali inaweza kutembelewa na jina lake bado lipo. Na hivi ndivyo alivyosema Ath-Thawriy, Is-Haaq, Abu Thawr, Ibn Hazm, Ibn Al-Mundhir na Ibn Taymiyah. [Al-Mudawwanah (1/44), Al-Mabsuwtw (1/100), Al-Awsatw (1/449), Al-Muhalla (2/100) na Majmuu Al-Fataawaa (21/173)].



Haya ndiyo sahihi, kwani ruksa ya kupukusa juu ya khufu mbili ni ruksa jumuishi; kinaingia kila kiitwacho khufu kwa mujibu wa uhalisia ulivyo, na haiwezekani kuibagua khufu fulani ikaachwa nyingine ila kwa dalili. Na lau kama kutoboka kunazuia kupukusa, basi Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angelibainisha hilo na hasa tukizingatia kwamba Maswahaba wengi walikuwa ni masikini katika enzi yake. Khufu za wengi wao zilikuwa hazikosi matobo.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



043-Mahala Pa Kupukusa Na Sifa Yake



Alhidaaya.com





Linalo ruhusika kisharia, ni kuzipukusa khufu mara moja tu nje (juu) na sio ndani (chini ya unyayo). Hii ni kwa Hadiyth ya ‘Aliy bin Abi Twaalib aliyesema: “ Lau kama dini ingelikuwa ni kwa rai, basi kupukusa chini ya khufu ingelikuwa ni bora kuliko juu yake. Na hakika nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akipukusa juu ya khufu zake mbili”.[Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (162), Ad-Daara Qutwniy (73) na Al-Bayhaqiy (2/111). Tazama Al-Irwaa (103)].



Na haya ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Al-Awzaa’iy, Ahmad, Abuu Haniyfay na wenzake. Na haya ndio sahihi. [Ikhtilaaf Al-‘Ulamaa (uk.30), Masaail Ahmad cha Ibn Haaniy (1/21), Al-Awsatw (1/453) na Al-Muhalla (2/111)].



Maalik na Ash-Shaafi’iy wamesema: “Hupukusa juu yake na chini yake. Na kama atapukusa juu tu, basi itamtosheleza. [Nihaayat Al-Muhtaaj (1/191), Al-Mudawwanah (1/39) na Al-Khurshiy (1/177)].



Hili limetolewa dalili kwa Hadiyth ya Al-Mughyrah bin Shu’ubah aliyesema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha, kisha akapukusa chini na juu ya khufu zake. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (165), At Tirmidhy (97), Ibn Maajah (550) na Ahmad (4/251). Ahmad, Al-Bukhaary, Abuu Haatim, Ad-Daara Qutwniy na Ibn Hajar wamesema ina dosari].



Hii ni kauli dhwa’iyf, lakini lililo na uthibitisho toka kwa Al-Mughyrah ni kauli yake isemayo: “Nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akipukusa juu ya khufu zake mbili”.[Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (161), At Tirmidhy (98) na wengineo].



Hivyo basi, haifai kupukusa isipokuwa juu ya khufu mbili tu. Na kama atapukusa chini tu akaacha juu, basi kupukusa huko hakutatosheleza. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



044-Yanayotengua Kupukusa



Alhidaaya.com





Imetangulia katika Hadiyth iliyoelezewa na Swafwan bin ‘Assal akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi waalihi wa sallam), alikuwa akituamuru tunapokuwa safarini, tusizivue khufu zetu siku tatu na masiku yake ila kwa janaba, lakini si kwa kwenda haja kubwa, au ndogo, au kulala”.



Kwa Hadiyth hii, imejulikana kuwa haifai kupukusa juu ya khufu mbili linapotokea moja kati ya mambo yafuatayo:



1- Janaba na mengineyo yenye kuwajibisha kuoga kama vile kujitwaharisha na hedhi au nifasi.



2- Kumalizika muda wa kupukusa.



3- Kuivua khufu na kupata hadathi kabla ya kuivaa.



Endapo ataivua khufu yake - ijapokuwa kabla ya kumalizika muda – kisha akapata hadathi, basi haitojuzu kuivaa na kupukusa, kwani anakuwa hakuivaa wakati huo akiwa na twahara.



Kwa hivyo, kama litatokea lolote kati ya mambo haya matatu, haitojuzu kupukusa juu ya khufu mbili, bali linalopasa kwake anapopata hadathi, ni kutawadha na kuosha miguu yake miwili, kisha anaweza kuzivaa khufu zake na kupukusa juu yake kama ilivyotangulia.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



045-Uzindushi: Kubatilika Upukusaji Hakumaanishi Kutenguka Wudhuu



Alhidaaya.com





Mtu ambaye alikuwa anapukusa juu ya khufu zake mbili kisha akazivua bila ya kupata hadathi, Maulamaa wana kauli nne juu ya hukmu yake:



Ya kwanza:



Itampasa atawadhe upya. Haya ni madhehebu ya An-Nakh’iy, Al-Awzaa’iy, Ahmad, Is-haaq na Ash-Shaafi’iy katika madhehebu yake ya zamani. [Ikhtilaaful ‘Ulamaa (uk. 31), Masaail Ahmad cha Ibn Haaniy (1/19) na Al-Majmu’u (1/557)].



Wanasema kuwa sababu ya hilo ni kuwa kupukusa panachukua mahala pa kuosha. Na kwa ajili hiyo, anapokiondosha kinachopukuswa, basi utwahara katika miguu miwili hubatilika, na matokeo yake ni kubatilika katika viungo vyote kwa sababu havigawanyiki.



Ya pili:



Itampasa aoshe miguu yake basi. Haya ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Abuu Haniyfah na wenzake na Abu Thawr. Pia ni kauli mpya ya Ash-Shaafi’iy. [Ikhtilaaful ‘Ulamaa (uk. 31), na Al-Awsatw (1/458)].



Ya tatu:



Ni lazima aoshe miguu yake miwili baada tu ya kuzivua khufu. Ikiwa atachelewa, basi atatawadha upya. Haya ni madhehebu ya Maalik na Al-Layth. [Al-Mudawwanah (1/41)].

Ya nne:



Hawajibiki kutawadha wala kuosha miguu. Hii ni riwaya iliyopokelewa toka kwa An-Nakh’iy. Haya haya yamesemwa na Al-Hasan Al-Baswriy, ‘Atwaa na Ibn Hazm. Aidha, yamekhitariwa na An-Nawawiy, Ibn Al-Mundhir na Ibn Taymiyah. [Al-Muhalla (1/105), Al-Awsatw (1/460), Al-Majmu’u (1/558) na Al-Ikhtiyaaraat (uk.15)].



Haya ndiyo madhehebu sahihi. Hii ni kwa vile, mtu huyu akiwa na khufu zake, kwa mujibu wa Hadiyth iliyothibiti, anakuwa na utwahara kamili. Na hilo haliwezi kutanguka anapozivua khufu zake isipokuwa kama kutapatikana dalili toka katika Hadiyth au Ijma’a. Na wanaosema kuwa itamlazimu kutawadha tena au kuosha miguu miwili, hao hawana hoja. Kauli hii inatiliwa nguvu na yale yaliyothibiti toka kwa Abu Dhwabyaan kwamba yeye alimwona ‘Aliy (Allaah Amridhie) akikojoa kwa kusimama, kisha akaomba aletewe maji, akatawadha na kupukusa juu ya viatu vyake. Halafu akaingia Msikitini, akavivua viatu vyake, kisha akaswali. [Isnad yake ni Swahiyh: Imetolewa na Al-Bayhaqiy (1/288) na At-Twahaawiy (1/58). Tazama Tamaam Al-Minnah (uk115)].



Kisha imefanyiwa kipimo kwa mtu aliyepaka maji kichwani kisha akazinyoa nywele. Bila shaka wao hawasemi kuwa itapasa kupaka maji tena kichwani au kutawadha tena!! Na hii ndiyo sawa hasa katika suala hili. Anapozivua khufu zake bila ya kupata hadathi, basi anaweza kuswali Swalaah zozote azitakazo mpaka pale wudhuu wake utakapotenguka. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



046-Kupaka Juu Ya Soksi Na Viatu



Alhidaaya.com





1- Kupaka Juu Ya Soksi



Soksi ni kile anachokivaa mtu miguuni sawasawa zikiwa zimetengenezwa kwa sufi au pamba au katani au mfano wa hivyo.



Maulamaa wana kauli tatu kuhusu hukmu ya kupukusa juu ya soksi:



Ya kwanza:



Haijuzu kupukusa juu yake ila tu kama zitafunikwa na viatu vya ngozi.



Haya ni madhehebu ya Abuu Haniyfah (ambaye baadaye aliachana na msimamo huu), Maalik na Ash-Shaafi'iy. [Al-Mabsuwtw (1/102), Al-Mudawwanah (1/40), Al-Ummu (1/33) na Al-Awsatw (1/465)].



Wao wanasema kuwa sababu ni kuwa soksi haiitwi khufu, na kwa hivyo haichukui hukmu yake, na wala hakuna Hadiyth yoyote inayothibitisha kupukusa juu ya soksi!!



Ya pili:



Inajuzu kupukusa juu ya soksi lakini kwa sharti ziwe nzito na zenye kusitiri mahala penye kulazimu kuoshwa.



Haya ni madhehebu ya Al-Hasan, Ibn Al-Musayyib na Ahmad. Pia Mafuqahaa wa Hanafi, Shaafi'iy na Hanbali. [Masaail Ahmad ya Ibn Haaniy (1/21), Al-Awsatw (1/464), Al-Majmu'u (1/540) na Fat-h Al-Qadiyr (1/157)].



Ya tatu:



Inajuzu kupukusa kwa hali yoyote hata kama ni nyepesi.



Ni madhehebu ya Ibn Hazm na Ibn Taymiyah kama inavyojulikana. Kauli hii pia imekhitariwa na Ibn 'Uthaymiyn na Al-'Allaamah Ash-Shanqiytwiy nayo ndiyo yenye nguvu. [Al-Muhalla (2/86), Al-Masaail Al-Maardiyniya (uk.58), Majmuu Al-Fataawaa (21/184), Al-Mumt'i (1/190) na Adhwaau Al-Bayaan (2/18,19) ambayo ina utafiti murua kabisa].



Maulamaa wenye kauli mbili za mwisho wamejuzisha kupukusa juu ya soksi kwa dalili zifuatazo:



1- Ni Hadiyth ya Al-Mughiyrah bin Shu'ubah aliyesema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha, akapukusa juu ya soksi zake na viatu vyake. [Al-Albaaniy amesema ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (159), At-Tirmidhiy (99) na Ahmad (4/252), naye ndiye mzungumzaji. Angalia katika Al-Irwaa (101)].



2- Imepokelewa toka kwa Al-Azraq bin Qays akisema: "Nilimwona Anas bin Maalik ametengukwa na wudhuu, akaosha uso wake, mikono yake miwili na akapukusa juu ya soksi zake za sufi. Nikamuuliza: Je, wapukusa juu yake? Akasema: Hakika hizi ni khufu mbili, lakini ni za sufi". [Ahmad Shaakir amesema kuwa ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ad-Duwlaabiy katika Al-Kunaa (1/181)].



Anas Allaah Amridhie akaeleza hapa kuwa khufu si lazima iwe ni ya ngozi tu, bali ni zaidi ya hivyo, naye ni Swahaba anayeijua vyema lugha.



3- Ni kwamba kuna Maswahaba 11 waliozungumzia kuhusu kujuzu kupukusa juu ya soksi mbili. Kati yao ni 'Umar na mwanawe ‘Abdullaah, 'Aliy, Ibn Mas'uud, Anas na wengineo. Na hakuna yeyote katika enzi yao aliyekwenda kinyume, na hilo likawa limekubaliwa na wote.



Kisha Jamhuri ya Maulamaa ikaja kupiga marufuku kupukusa juu ya soksi nyepesi kwa vile hazisitiri mahala panapolazimu kuoshwa. Tumekwisha eleza nyuma kuwa hili si sharti – kwa mujibu wa utafiti – kwa kuchukulia kipimo cha khufu iliyotoboka. Na kwa vile siku hizi zinazovaliwa zaidi ni soksi nyepesi, tutaona kwamba kushurutisha mfano wa masharti kama haya, kunakwenda kinyume na makusudio ya sharia iliyotufanyia ukunjufu kwa kuwabana watu na kuwatia uzito. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.



Faida



Inaingia katika maana ya soksi bendeji, plasta na matambara anayofungwa mtu mguuni kwa udhuru, kwani hizo ni vigumu kuzifungua. Yeye atapaka tu juu yake kama alivyolikhitari hilo Shaykh wa Uislamu.



Na hukmu za kupukusa juu ya soksi mbili ni hukmu zile zile za kupukusa juu ya khufu mbili.



Anapovaa Soksi Juu Ya Nyingine



Hili lina hali mbalimbali:



1- Akitawadha kisha akavaa soksi juu ya nyingine (mbili), basi atapukusa soksi ya juu tu endapo kama atatengukwa na wudhuu.



Na haya ni madhehebu ya Hanafiy. Na ni kauli yenye nguvu kwa Maalik na Hanbali. Aidha ni kauli ya zamani ya Ash-Shaafi'iy aliyetofautiana nao katika kauli yake mpya. [Haashiyat Ibn 'Aabidiyn (1/179), Jawaahir Al-Ikliyl (1/24) na Rawdhat At-Twaalibiyn (1/127). Mengi wameyazungumzia hapa kuhusu khufu, lakini hukmu ni moja].



2- Akitawadha akavaa soksi juu ya nyingine, kisha akapukusa juu yake, halafu akaivua ya juu baada ya kupukusa, basi inajuzu kwake kuukamilisha muda kwa kuzipukusa soksi za ndani, kwa kuwa cha msingi hapa ni kuwa yeye alizivaa miguu yake ikiwa twahara.



3- Akitawadha akavaa soksi, kisha akaivaa nyingine juu yake kabla ya kutengukwa na wudhuu, basi atapukusa juu ya soksi zozote azitakazo (za ndani au za nje. [Mahanbali wamelielezea hili katika Kash-Shaaf Al-Qina'a (1/117-118)].



4- Akitawadha akaivaa soksi moja, akapukusa juu yake kisha akaivaa nyingine hali ya kuwa ana twahara, itajuzu kwake kupukusa ya juu, kwa vile kimsingi ameiingiza miguu yake ikiwa ni twahara. Na kama alitengukwa na wudhuu kisha akaivaa nyingine, haitojuzu kwake kupukusa ya juu, bali itajuzu ya chini. [Imeelezwa katika Kash-Shaaf Al-Qina'a (1/117-118) kwamba hapukusi. Amesema: "Kwa vile khufu iliyopukuswa ni badala ya kuosha ile iliyo chini yake. Na badali haijuzu kuwa na badali nyingine, bali atapukusa ya chini kwa vile ruhusa imefungamana nayo!!].



2- Kupaka Juu Ya Viatu



Imetangulia katika Hadiyth ya Al-Mughiyrah bin Shu'ubah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha, akapukusa juu ya soksi zake na viatu vyake. [Tumeitaja nyuma kidogo]



Hadiyth hii tukisema kuwa ni Swahiyh, inaweza kubeba mambo mawili:



1- Ni kuwa alivaa viatu na soksi na akapukusa juu yake, na hukmu ya viwili hivyo ni moja kama ilivyotangulia katika kuvaa soksi juu ya soksi au khufu juu ya khufu.



2- Ni kuwa Al-Mughiyrah alimwona Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akipukusa mara juu ya soksi na mara nyingine juu ya viatu. Na hii inakuwa ni dalili kuwa inajuzu kupukusa juu ya viatu ijapokuwa bila ya soksi. Na hili ingawa liko mbali kidogo, lakini linaweza kutolewa dalili juu ya kujuzu hilo kutokana na yaliyotangulia katika Hadiyth ya Abuu Dhwabyaan kwamba "Aliy bin Abi Twaalib alitawadha, akapukusa juu ya viatu vyake, kisha akaingia Msikitini, akavua viatu vyake, kisha akaswali…" Na hapa hakutaja soksi. [Tumeitaja nyuma kidogo]



Na pengine kujuzu kupukusa juu ya viatu kunatilika nguvu vile vile kwa kutoshurutishwa kuwa chenye kupukuswa kiwe ni chenye kusitiri mahala pa lazima kuoshwa. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
 
Naam leo ni siku ya Ijumaa,basi ni sunna kukata kucha zako,kuoga na kwa mwanaume kupaka mafuta mazuri au perfume unukie vizur kabisa tayar kwa kwenda msikitini

Ni bora uwahi kwenda msikitini na mara baada ya kuingia tu swali rakaa mbili au au nyingine zozote utakazo jaaliwa,kisha kaa safu za mbele kabisa zina fadhila kubwa

Ni isomwapo hutuba inapaswa kutulia na kuisikiliza na sio kulala,utakuta mtu anaangalia mpira dakika 90 na pengine za nyongeza jumla 120 lkn anashindwa kusikiliza hutuba ya dakika 30 au 20

Isomwapo hutuba haitakiwi kushughulishwa na chochote hata ikiwa kuhesabu tasbih,pale uwe hadhir kusikiliza hutba,ndio maana baada ya kuanza kusomwa hutba tu hata malaika wanaacha kuandika orodha ya watu walio wahi msikitini na kuanza kusikiliza hutuba

Ila kwa masikitiko makubwa nimeshuhudia mtu hutuba inasomwa anashughulishwa na simu yake kwa kuingia mtandaoni na kuperuzi,ndio maana tunatakiwa tusome walau tujue mambo ya muhimu katika ibada zetu,nimeshuhudia ijumaa iliyopita wakati wa hutuba mtu anapokea simu na kujibu nipo msikitini inna lilah wainna ilaih rajiuu

Hakika hawa wamepuuza na wanakosa fadhila za ijumaa

Ijumaa Mubarak
 
Ikiwa unataka kupata notification wa uzi huu ni rahisi tu,comment neno subhanallah au alhamdulillah au hata weka nukta basi utakuwa umejiunga katika uzi huu na utapata status

Au waeza endelea kuusoma unapo ubahatisha hewani,kazi kwako

Darsa inaendelea
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



047-Tatu: Kupaka Juu Ya Kinachofunika Kichwa



Alhidaaya.com





1- Kupaka Juu Ya Kilemba Katika Wudhuu



Inajuzu kupukusa juu ya kilemba – badala ya kupukusa kichwa – wakati wa kutawadha kwa hali yoyote. Na haya ni madhehebu ya Ahmad, Is-haaq, Abu Thawr, Al-Awzaa'iy, Ibn Hazm na Ibn Taymiyah. Nayo ni kauli ya Abu Bakr, 'Umar, Anas na Maswahaba wengineo (Radhwiya Allaahu ‘anhum). [Masaail Abuu Daawuud (8), Al-Mughniy (1/300), Al-Majuu'u (1/406), Al-Awsatw (1/468), Al-Muhalla (2/58) na Majmu'u Al-Fataawaa (21/184)].



Na bila shaka, hilo limethibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).



Imepokelewa toka kwa 'Amri bin Umayyah Adh-Dhumariy akisema: "Nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akipukusa juu ya khufu mbili na kilemba". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaji” na Al-Bukhaariy (205)].



Kauli kama hiyo hiyo imepokelewa toka kwa Al-Mughiyrah bin Shu'ubah. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaji” na Al-Muslim (275)].



Pia imepokelewa toka kwa Bilaal akisema: "Nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akipukusa juu ya khufu mbili na khimaar”.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaji” na Muslim (285)].



Khimaar hapa ni kile chenye kufunika kichwa, na makusudio ni kilemba.



Na kwa upande mwingine, Abuu Haniyfah na wenziwe, Maalik na Ash-Shaafi'iy, wameelekea kwingine wakisema kuwa mwenye kutawadha hapukusi juu ya kilemba tu, bali hupukusa juu yake pamoja na utosi, na utosi unakuwa ni fardhi na kilemba ni Sunnah (ziada) kwa kujengea juu ya kujuzisha kwao kupaka sehemu tu ya kichwa!! [Haashiyat Ibn 'Aabidiyn (1/181), Haashiyat Ad-Dusuwqiy (1/164) na Al-Majmu'u (1/407)].



Lakini pamoja na hivyo, Ash-Shaafi'iy anasema: “Ikiwa Hadiyth ya kupukusa juu ya kilemba ni Swahiyh, basi hiyo ndiyo kauli yangu”. Na bila shaka yoyote Hadiyth hiyo ni Swahiyh, kwa hiyo ndiyo kauli yake.



Wenye kupinga kupukusa juu ya kilemba wametoa hoja kwa Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdillaah aliyesema: "Nilimwona Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akikivuta nyuma kilemba chake na akapukusa juu ya utosi wake". [Sikuipata na wala haipo katika kitabu chochote kati ya vitabu vya Hadiyth nilivyonavyo. Na Ibn Al-Mundhir ameitaja bila ya Isnaad (1/469)].



Sijaipata Sanad yoyote ya Hadiyth hii!!



Na kwa Hadiyth ya Al-Mughiyrah akisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipukusa juu ya kilemba chake, na juu ya utosi na khufu zake mbili". [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa katika mlango wa wudhuu].



Ninasema: "Kauli yenye nguvu ni kuwa inajuzu kwa hali yoyote kupukusa juu ya kilemba kwa kuthibiti kuelezewa hilo toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwa kufanywa hilo na Makhalifa wawili waliokuja baada yake, na kukosa uzito hoja iliyotolewa na wenye kulipinga hilo. [Angalia hoja zao na zilivyojibiwa katika "Al-Muhalla" (2/61)]. Lakini pamoja na hivyo, ni bora kupukusa sehemu ya utosi pamoja na kilemba ili kuepuka mahitilafiano. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.



2- Kupukusa Mwanamke Juu Ya Ushungi / Mtandio



Shaykh wa Uislam anasema: "Ikiwa mwanamke atahofia baridi au mfano wa baridi, basi atapukusa juu ya ushungi wake, kwani Ummu Salamah alikuwa akipukusa juu ya ushungi wake. Lakini akipukusa ushungi, anatakiwa apukuse baadhi ya nywele zake. Na ikiwa hakuhitajia hilo, basi hapa kuna mvutano baina ya Maulamaa.” [Majmu'u Al-Fataawaa (21/218)].



Ninasema: "Katika riwaya, [Al-Mudawwanah (1/42), Al-Ummu (1/26), Al-Badaai-'i (1/5) na Al-Mughniy (1/305)]…..Hanafiy, Maalik, Ash-Shaafi'iy na Hanbali, wameelekea mwelekeo wa kusema kuwa haijuzu kutokana na yale yaliyopokelewa toka kwa 'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) kwamba yeye aliingiza mkono wake chini ya ushungi wake na akapukusa kichwa chake, akasema: "Hivi ndivyo alivyoniamuru Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)". [Sijapata kuiona bali ameitaja Al-Kaasaaniy katika Al-Badaai-'i (1/5), nami sijaiona katika kitabu chochote cha Hadiyth!!]



Wamesema: "Na kwa vile hicho ni kivazi cha kichwani kwa mwanamke na hakuna uzito katika kukiondosha, haijuzu kupukusa juu yake."



Al-Hasan Al-Baswriy amechukua msimamo wa kuwa inajuzu kupukusa juu ya ushungi. Hayo hayo wameyasema Mahanbal, - lakini wameshurutisha kuwa ni lazima mitandio au shungi ziwe zimezungushiwa chini ya koo!! – kwa kuchukulia kipimo cha kilemba, kwani khimaar kikawaida huvaliwa kichwani.



Ninasema: “Ingelikuwa Hadiyth ya 'Aaishah ni Swahiyh, basi ingelimaliza mjadala katika kuzuia kupukusa juu ya ushungi. Na kama si hivyo, basi kipimo kitachukuliwa juu ya kilemba. Na ili kuondosha wasiwasi, ni vyema mwanamke apukuse juu ya ushungi wake pamoja ncha ya utosi wake. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.”



3- Kupukusa Juu Ya Kofia Katika Wudhuu



Jamhuri ya Maulamaa imeshikilia mwelekeo wa kuwa haijuzu wakati wa kutawadha kupukusa juu ya kofia badala ya kichwa, kwani fardhi ni kupukusa kichwa. Lakini hilo limeachiliwa katika kilemba kutokana na uzito wa kukivua kwa Jamhuri ya Maulamaa, au kwa matni ya Ahmad.



Ibn Hazm, Ibn Taymiyah na watafiti kati ya wadau wa taaluma hii, wameshikilia mwelekeo wa kujuzu kupukusa juu ya kofia.

[Al-Muhalla (2/58) na Majmu'u Al-Fataawaa (21/ 184-187, 214)].



Hii ni kwa vile, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipopukusa juu ya kilemba, sisi tumejua kwa hilo kuwa si fardhi kugusanisha maji na kichwa, bali inajuzu kupukusa juu ya kitu chochote kilichovaliwa kichwani hata kama hakisitiri mahala pa lazima kuoshwa na wala haikuwa ni uzito kukivua. Na hili ndilo sawa, na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.



Faida



- Si Sharti Kuwa Na Twahara Wakati Wa Kuvaa Chenye Kufunika Kichwa Ili Ijuzu Kupukusa Juu Yake.



Hili halipimiwi na kupukusa juu ya khufu mbili, kwa vile hakuna sababu ya kuvikutanisha viwili hivyo, bali Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameelezea ulazima wa twahara wakati wa kuvaa khufu mbili na wala hakulielezea hilo kwa upande wa kilemba na ushungi. Na lau kama ingelikuwa ni lazima, basi angelibainisha. [Al-Muhalla (2/64)]



Ninasema: “Hii ni kwa vile, khufu mbili ni badala ya kilicho fardhi kukiosha. Ama kichwa, fardhi yake ni kupukusa, na kilicho juu ya kichwa, huchukua hukmu yake. Kwa hiyo vimekuwa ni vitu viwili tofauti. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.



- Hakuna Wakati Wala Muda Maalumu Wa Kupukusa Juu Ya Chenye Kufunika Kichwa

Ni kwa kutofaa kipimo cha kupukusa juu ya khufu mbili. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipukusa juu ya kilemba na khimaar na wala hakulipangia hilo wakati. Na hili limepokelewa toka kwa 'Umar bin Al-Khattwaab (Allah Amridhie). [Al-Muhalla (2/65)]
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



048-Nne: Kupaka Juu Ya “Al Jabiyrah”



Alhidaaya.com





"Al Jabiyrah" ni majiti mawili ambayo huungiwa kwayo mifupa iliyovunjika ili ishikamane. Na katika maisha yetu ya leo, plasta ya jasi (piopi) hutumiwa badala yake.



Na mtu ambaye katika kiungo chake kimoja cha wudhuu kutakuwa na "jabiyrah" (piopi) kama mikono miwili au miguu miwili, basi inajuzu kwake kupukusa kwa mujibu wa rai ya Jamhuri ya Maulamaa wakiwemo Maimamu wanne na wengineo. [Sharh Fat-h Al-Qadiyr (1/140), Al-Mudawwanah (1/23), Al-Mughniy (1/203) na Al-Majmu'u (2/327)].



Wao wametolea dalili yafuatayo:



1- Hadiyth ya Jaabir kwa yule aliyepatwa na mpasuko usoni, na kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Hakika inamtosheleza tu kufunga jeraha lake kwa kitambaa, kisha akapukusa juu yake)). Na hii ni Hadiyth Dhwa’iyf. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (236) na wengineo. Angalia Al-Irwaa (105)].



2- Ni kauli ya Ibn 'Umar: "Mwenye jeraha lililofungwa, atatawadha na atapukusa juu ya bendeji, na ataosha pembezoni mwa bendeji".[Isnadi yake ni Swahiyh: Imekharijiwa na Ibn Abi Shaybah (1/126) na Al-Bayhaqiy (1/228)].



Na hajulikani Swahaba yeyote aliyekwenda kinyume na Ibn 'Umar.



3- Ni kuchukulia kipimo cha kupukusa juu ya khufu mbili, kwani kupukusa juu ya khufu mbili kunajuzu bila ya dharura, basi vipi kwa upande wa "jabiyrah" (piopi) ambayo ni dharura? Hivyo inachukua uzito zaidi.



Na Ibn Hazm ameshikilia msimamo wa kuwa mwenye kufungwa "jabiyrah", basi halazimiki kupukusa juu yake na kwamba hukmu ya mahali hapo inaondoka. [Al-Muhallaa (2/74)].



Ninasema: "Hii ni kwa vile Ibn Hazm amezichukulia Hadiyth za kupukusa juu ya bendeji, plasta n.k kuwa ni Dhwa’iyf na wala haoni Qiyaas kuwa ni hujjah!! Na Hadiyth hizi hazifai kama alivyosema. Ama Qiyaas, bila shaka itakuwa ni hujjah endapo kama nguzo na sharti zake zitakuwepo. Lakini inaweza kusemwa kuwa Qiyaas hapa hakifai kutokana na kutofautiana tanzu na asili. Ni Qiyaas waajib (kupukusa juu ya piopii kwa Jamhuri ya Maulamaa) juu ya mubaah (kupukusa juu ya khufu mbili). Na hapa basi, madhehebu ya Ibn Hazm yanang'aa. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.



Faida



1- Kupukusa juu ya "jabiyrah" (piopi) kunatosheleza, sawasawa katika wudhuu au katika kuoga, kwa vile "jabiyrah" (piopi) ni jambo lisilo na budi, na kwa hivyo hakuna tofauti ndani yake kati ya hadathi ndogo na hadathi kubwa. Ni kinyume na kupukusa juu ya khufu mbili, kwani hili limeruhusiwa (kwa atakaye).



2- Si lazima kufungwa "jabiyrah" wakati mtu ana twahara wala hakuna muda maalumu wa kupukusa juu yake.



Hii ni kwa vile, hilo linakwenda kinyume na makusudio ya sharia katika kuruhusu kupukusa kati ya kuondosha uzito na tabu. Aidha, kufungwa (piopi) ni hali ya kulazimika ambayo huja ghafla bila kutegemewa kinyume na khufu mbili. Mbali ya hivyo, hakuna matni au Ijma’a.

Hivyo basi, hakuna muda maalumu wa kupukusa juu ya "al-Jabiyrah". Lakini wakati wowote atakapoliondosha au kiungo kikapona, basi haitojuzu kupukusa.



3- Bendeji na plasta za kitiba (hospitali) zilizofungwa katika kiungo cha wudhuu, zina hukmu ya "al-Jabiyrah" (piopi) kama lilivyohakikiwa hilo na Shaykh wa Uislamu. [Majmuu Al-Fataawaa (21/185)].
 
Mashaallah wallah kusoma raha, hakika hii dini ni nyepesi sana ila kwa kutoijua kwetu tunajikuta tunaitia uzito

Allah azidi kutufahamisha

Naam tutakuja sasa kuangalia hukumu za kuoga,ambazo ni muhimu sana

Haya maswala ya tohara ndio msingi mkubwa wa ibada zetu,ukifeli hapa hata ibada zako zinafeli

Darsa itaendelea hapo baadae inshallah
 
Screenshot_20250404_143121_Quran Swahili.jpg
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



049-Kuoga



Alhidaaya.com





Kilugha maana yake ni kuchuruzika maji juu ya kitu. Ama kisharia, ni kumiminisha maji yaliyo twahara katika mwili wote kwa njia maalumu. [Kash-Shaaf Al-Qinai (1/158)].



Yenye Kupasisha Kuoga



1- Ni kutokwa na manii mtu akiwa macho au usingizini



Ni kwa Neno Lake (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

((وإن كنتم جنبا فاطهروا))

((Na mkiwa na janaba, basi ogeni)). [Al-Maaidah (5:6)].



Na Neno Lake (Subhaanahu wa Ta’aalaa):



(( يا أ يها الذين لا تقربوا الصلاة وأنتم سكارى حتى تعلموا ما تقولون ولا جنبا إلا عابري سبيل حتى تغتسلوا))

((Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah hali mmelewa, mpaka muyajue mnayoyasema, wala hali mna janaba – isipokuwa mmo safarini – mpaka mkoge)). [An-Nisaa (4:43)].



Na imepokelewa toka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriy toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba amesema:

(( إنما الماء من الماء))

((Hakika maji ni kutokana na maji)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (343) na Abuu Daawuud (214)].



Yaani kuoga (kwa maji), sababu yake ni kumwaga (maji), nayo ni manii.



Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia 'Aliy:

((إذا فضخت الماء فاغتسل))

((Ukimwaga maji, basi oga)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (206), An Nasaaiy (193) na Ahmad (1/247). Asili yake ni kutoka Swahiyh Mbili.



Na katika tamko jingine:

((إذا حذفت))

((Utakapokatia))



Na hayawi kwa sifa hii ila yanapotoka kwa matamanio kama Alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

((خلق من ماء دافق))

((Ameumbwa kutokana na maji yenye kuchupa)). [At Twaariq (86:6)].



Na imepokelewa toka kwa Ummu Salamah (Allaah Amridhie) akisema:

"Alikuja Ummu Sulaym, naye ni mke wa Abu Twalha, kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika Allaah Haonei haki hayaa. Je, inampasa mwanamke kuoga kama ameota? Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

((نعم، إذا رأت الماء))

((Naam, kama akiyaona maji)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (282) na Muslim (313)].



Kauli hii inafahamisha kuwa si lazima manii yatoke kwa matamanio na kuchupa wakati wa kuota ndipo ipase kuoga, bali itambidi kuoga anapoyaona manii katika nguo yake. Na kama hakuyaona, basi hapaswi kuoga hata kama atakumbuka kuwa aliota. Hii ni kutokana na Hadiyth ya Mama wa Waumini 'Aaishah (Allaah Amridhie) aliyesema:

"Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu mtu anayekuta ubichi ubichi na wala hakumbuki kama aliota. Akasema:

((يغتسل))

((Ataoga))



Na kuhusu mtu anayeona kwamba aliota lakini hakukuta ubichi bichi, akasema:

((لا غسل عليه))

((Hapaswi kuoga)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhy (113) na Abuu Daawuud (233)].



Zindushi Mbili



(a) Katika yote yaliyotangulia, mwanamke ni kama mwanamume, sawa kwa sawa.



(b) Yeyote mwenye kuchuruzikwa na manii bila ya matamanio kutokana na ugonjwa, au baridi au mfano wa hayo, basi hana lazima kuoga kwa mujibu wa kauli mbili zilizo sahihi zaidi za Maulamaa. Na haya ndiyo madhehebu ya Jamhuri kinyume na Ash-Shaafi'iy na Ibn Hazm.



Na Maulamaa kwa sauti moja wamesema kuwa ni lazima kuoga mtu anapotokwa na manii kwa matamanio wakati yu macho, na anapotokwa na manii akiota usingizini. [Al-Majmuu (1/139), Bidaayat Al-Mujtahid (1/58) na As-Sayl Al-Jarraar (1/104)].



Isipokuwa yale yaliyopokelewa toka kwa Ibraahiym An-Nakh'iy kwamba yeye alikuwa haoni kuwa inampasa mwanamke kuoga anapoota na kujimwagia.



2- Kukutana tupu mbili ijapokuwa bila ya kumwaga manii



Kinapozama kichwa cha dhakari ya mwanamume katika utupu wa mwanamke, basi inawalazimu wote wawili kuoga ni sawa ikiwa wamemwaga manii au hawakumwaga. Hii ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyoipokea toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

(( إذا جلس بين شعبها الأربع، ثم جهدها فقد وجب الغسل)) (وإن لم ينزل))

((Anapokaa kati ya tanzu zake nne, kisha akamtoa jasho, basi ni lazima kuoga)) ((hata kama hakumwaga)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (291) na Muslim (348) na ziada ni yake yeye].



Na imepokelewa toka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Allaah Amridhie) kwamba mtu mmoja alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu mtu anayemwingilia mkewe kisha akaishiliwa nguvu, je, ni lazima waoge? – nailhali Mama wa Waumini 'Aaishah yuko hapo amekaa - Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

(( إني لأفعل ذلك أنا وهذه ثم نغتسل ))

((Hakika mimi nafanya hilo na huyu, kisha tunaoga)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (350)]



Amesema An-Nawawiy: "Na hili halina mvutano hivi leo. Lilikuwa na mvutano kwa baadhi ya Maswahaba na waliokuja baada yao. Kisha ikafungika Ijma’a’ juu ya tuliyoyataja."



Ninasema: “Ama hitilafu ya Maswahaba katika suala hili, miongoni mwake ni Hadiyth ya Zayd bin Khaalid ambapo yeye alimuuliza 'Uthmaan bin 'Affaan akimwambia: "Unasemaje endapo mtu atamwingilia mkewe na wala hakumwaga manii"? 'Uthmaan akamwambia: "Atatawadha kama anavyotawadha kwa ajili ya Swalaah na ataosha dhakari yake". Akasema 'Uthmaan: "Nimelisikia hilo toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na nikaliulizia hilo kwa ‘Aliy bin Abi Twaalib, Az-Zubayr bin Al-'Awwaam, Twalha bin 'Ubayd Allaah na Ubay bin Ka'ab, nao wakamwamuru hilo". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (292) na Muslim (347)].



Daawuud Adh-Dhwaahiriy ameelekea msimamo wa kutolazimu kuoga kama mtu hakumwaga kwa Hadiyth:

((Hakika maji ni kutokana na maji)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (348). Imeshatajwa nyuma.]



Na Hadiyth ya Abu Sa'iyd kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia mtu fulani:

(( إذا أعجلت ـ أو قطحت – فعليك الوضوء))

((Ukiingilia bila kumwaga, basi yakupasa kutawadha)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (180) na Muslim (345)].



Ama Maswahaba hawa, bila shaka imethibiti kutoka kwao kuwa waliachana na kauli ya kutokupasa kuoga. [Angalia athar kutoka kwao katika kitabu cha Jaami'u Ahkaamin Nisaa cha Shaykh wetu (Allaah Amhifadhi) (1/89,90)].



Ama kauli ya Daawuud, bila shaka imekwenda kinyume na Jamhuri ya Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Mafuqahaa wa Taabi-'iyna na waliokuja baada yao. Hawa wanaona kwamba Hadiyth ya ((Maji ni kutokana na maji)) na yaliyo katika maana yake, ilikuwa ni mwanzoni mwa Uislamu kisha ikanasikhiwa.



At-Tirmidhiy amesema (1/185):

"Na hivi ndivyo alivyopokea zaidi ya mtu mmoja katika Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwemo Ubay bin Ka'ab na Raafi'i bin Khudayj. [Hadiyth ya Ubayya ni Swahiyh kwa njia zake kama alivyoibainisha Shaykh wetu Abu ‘Umayr Al-Athariy- Allaah Amstareheshe katika maisha yake- katika Shifaau Al'ayyi Bitahqiyq Musnad Ash-Shaafi'iy (100)].



Na hili ndilo linalofanywa na Maulamaa wengi zaidi kuwa mtu anapomwingilia mkewe katika tupu, inawabidi wote wawili kuoga hata kama hajamwaga manii”.



Faida [Zimetolewa toka kwenye kitabu changu cha Fiqhu As Sunnah Lin Nisaa (uk 46)].



1- Dhakari ya mwanamume ikigusa uchi wa mwanamke bila kuingizwa ndani, basi haiwapasi kuoga kwa makubaliano ya Maulamaa. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (1/204)].



Ibraahiym An-Nakh'iy aliulizwa kuhusu mtu anayemwingilia mkewe sehemu isiyokuwa tupu (farji) kisha akamwaga. Alijibu akisema:

"Atakoga yeye, lakini mkewe hakogi bali ataosha sehemu iliyochafuka". [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdu Rrazzaaq (971). Angalia athar mfano wake kutoka baadhi ya watangu wema katika Jaami Ahkaam An-Nisaa (1/95)].



2- Mtu akimwingilia mkewe, akaingiza sehemu ndogo tu ya kichwa cha dhakari, kisha manii yake yakaingia katika utupu wa mkewe, na mkewe hakumwaga, basi haimpasi mke kuoga.

Amesema An-Nawawiy: "Anapoingiziwa mwanamke manii katika utupu wake wa mbele au wa nyuma kisha manii hayo yakatoka, basi hapaswi kuoga. Hili ndilo sahihi lililopitishwa na Jamhuri." [Al-Majmu’u (2/151). Tazama Al-Muhalla (2/7)].



3- Mtu anapomwingilia mkewe kisha mkewe akakoga, halafu baadaye yakamtoka manii ya mumewe toka kwenye utupu wake, basi hapaswi kuoga tena. Lakini je, itamlazimu kutawadha?



Kwa mujibu wa kauli ya Jamhuri, itamlazimu kutawadha kwa vile maji hayo yametoka kupitia moja ya njia mbili ingawa ni twahara. [Al-Majmu’u (2/151)



Ibn Hazm amesema:

"Wudhuu utampasa kutokana na hadathi yake yeye na wala si kutokana na hadathi ya mwingine. Na kutoka manii ya mumewe toka kwenye utupu wake hakuzingatiwi kuwa yeye ndiye anayemwaga, wala haizingatiwi kuwa ni hadathi yake yeye. Kwa hivyo, hakogi wala hatawadhi." [Al-Majmu’u (2/151).



Ninasema: “Ama kaida ya kutawadha kwa kila chenye kutoka katika moja ya njia mbili, kaida hii haikubaliki kama ilivyotangulia, kwani mapitio ya manii kwa mwanamke, siyo mapitio ya mkojo. Hivyo basi madhehebu ya Ibn Hazm yanakuwa na nguvu zaidi. Lakini pamoja na hivyo, pachukuliwe tahadhari kuwa manii haya yanaweza kuchanganyika na madhii ya mwanamke. Hivyo la akiba zaidi atawadhe, na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.



4- Mume akimwingilia mkewe mdogo ambaye bado hajaanza kuingia hedhini, au mtoto mdogo ambaye hajabaleghe akamwingilia mwanamke, basi inamlazimu mwanamke kuoga vile vile kama alivyosema Imam Ahmad:

"Hebu nielezeni! Je, 'Aaishah, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akimwingilia, alikuwa hakogi?! [Al-Mughniy (1/206)].



5- Mume anapomtaka mkewe kufanya mapenzi, basi haitakikani kumkatalia hilo kwa kisingizio cha kutokuwepo maji ya kukogea.



Shaykh wa Uislamu katika "Al-Fataawaa" 21/454" anasema:

"Haitakikani kwa mwanamke kumkatalia mumewe tendo la ndoa. Amwachie amwingilie. Na ikiwa ataweza kuoga, basi akoge, na kama hakuweza, atatayammamu na kuswali".



3, 4 – Hedhi na nifasi



Mambo haya mawili ni sababu mbili zenye kuwajibisha kukoga. Na kwa vile kukoga kunatokana na sababu ambapo hakufanyiki ila baada ya kukatika kwake na kumalizana nayo, inabidi kukoga baada ya kukatika hedhi na nifasi.



Imepokelewa na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Faatwimah binti Abi Hubaysh:

((إذا أقبلت الحيضة فدعي الصلاة، وإذا أدبرت فاغتسلي وصلي))

((Hedhi ikija basi acha Swalaah, na ikiondoka basi oga na uswali)). [Hadiyth Swahiyh: Takhriyj yake itakuja katika mlango wa hedhi].



Na nifasi ni kama hedhi kwa Ijma’a. Kisha imethibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiielezea nifasi kama hedhi na hedhi kama nifasi.



Hukmu za hedhi na nifasi zitakuja kuelezewa kwa uchambuzi InshaAllaah.



5- Kafiri anaposilimu



Maulamaa wana kauli tatu kwa upande wa hukmu ya kuoga wakati kafiri anaposilimu:



Kwanza:



Ni lazima aoge kwa hali yoyote. Haya ni madhehebu ya Maalik, Ahmad, Abu Thawr na Ibn Hazm. Pia Ibn Al-Mundhir na Al-Khattwaabiy wamelikhitari. [Mawaahib Al-Jaliyl (1/311), Al-Mughniy (1/152), Al-Majmu’u, (2/175) na Al-Muhalla (2/4)].



Dalili zao ni:



1- Hadiyth ya Qays bin ‘Aaswim aliyesema kwamba aliposilimu, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru akoge kwa maji na mkunazi. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (355), At-Tirmidhiy (605) na An-Nasaaiy (1/109). Tazama “Al-Mishkaat” (543)]. Na asili ya amri hii ni ulazima.



2- Ni yale yaliyomo katika Hadiyth ya Abu Hurayrah katika kusilimu Thumaamah bin Uthaal kutokana na kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Nendeni naye hadi katika bustani ya Bani fulani, kisha mwamrisheni akoge)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (2/304) na Ibn Khuzaymah (252). Na asili yake ni kutoka Swahiyh Mbili, lakini hakuna amri ya kuoga. Angalia vilevile Al-Irwaa (128)].



3- Kisa cha kusilimu Usayd bin Hudhayr. Kisa hiki kinaeleza kwamba Usayd aliwauliza Mus’ab bin ‘Umayr na As’ad bin Zuraarah: “Mnafanya vipi mkitaka kuingia katika Dini hii?” Wakajibu: “Unaoga unatwaharika, halafu unazitwaharisha nguo zako mbili, kisha unashuhudia shahada ya haki, halafu unaswali…” Hadiyth. [Isnadi yake ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twabary katika kitabu cha At Taariykh (1/ 560), na Ibn Hishaam katika As Siyrah (2/285)].



Pili:



Inapendeza (imesuniwa) kafiri akoge, isipokuwa tu kama alikuwa na janaba kabla ya kusilimu, hapo italazimu akoge. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Abu Haniyfah. [Al-Majmu’u (1/174), Al-Ummu (1/38) na Ibn ‘Aaabidyn (1/167)].



Tatu:



Si lazima kukoga kwa hali yoyote. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah. [Al-Mabsuwtw na Sharh Fat-h Al-Qadiyr (1/59)].



Hawa wametoa dalili zao katika haya yafuatayo:



1. Neno Lake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

(( قل للذين كفروا إن ينتهوا يغفر لهم ما قد سلف ))

((Waambie waliokufuru, ikiwa wataacha (ukafiri), watasamehewa yaliyopita)). [Al-Anfaal (8:38)]



2. Hadiyth ya ‘Amru bin Al-‘Aasw ikiwa Marfu’u:

((Uislamu unapomosha yaliyopita)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (121) kutoka kwa Hadiyth ya ‘Amri bin Al ‘Aasiy].



Katika kutolea ushahidi wa Aayah na Hadiyth, kuna mlahadha. Ni kuwa yanayokusudiwa katika Aayah na Hadiyth ni kughufiriwa madhambi. Maulamaa wamekubaliana wote kuwa anayesilimu lau kama alikuwa na deni au kisasi, basi hayo hayafutiki kwa kusilimu kwake, na hasa kwa vile kuwa kulazimika kuoga si uchukulifu au ukalifisho kwa yaliyomlazimu katika ukafiri, bali ni ulazimisho wa sharti katika masharti ya Swalaah katika Uislamu, kwani yeye ana janaba. Na Swalaah haisihi mtu akiwa na janaba. Naye havuliki na janaba hiyo kwa kuwa ameingia katika Uislamu. [Al-Majmu’u (2/174)].



3. Wamesema:

“Watu wengi walisilimu wakiwa na wake na watoto lakini Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwaamrisha kuoga kwa njia ya lazima. Na lau ingelikuwa ni wajibu, basi angeliwaamrisha hilo”.



Na hapa kuna mlahadha:



Lililo dhahiri ni wajibu kuoga, kwani kuamrishwa baadhi, kuna maana kuwa wao washafikishiwa amri. Ama kudai kuwa wengineo hawakuamrishwa, hilo halifai kwa kushikilia tu, kwani ukomo wake ni wao tu kutokuwa na habari nalo, nako si kutojua kwa sababu ya kutojulikana. [Nayl Al-Awtwaar (1/281)].



Kwa hivyo, lenye nguvu zaidi ni kuwa inamlazimu kafiri – sawasawa akiwa kafiri wa asili au aliyeritadi – aoge kwa hali yoyote anaposilimu. Na linalotuhisisha kwamba kuoga wakati wa kuingia katika Uislamu lilikuwa ni jambo linalojulikana vizuri na Maswahaba, ni yale yaliyomo ndani ya kisa cha kusilimu mama wa Abu Hurayrah. Kisa kinaeleza kuwa mama huyo alioga na akavaa deraya yake.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (2491) na Ahmad (7911)].

Pia kisa kilichotangulia cha kusilimu Usayd bin Hudhayr. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.



6- Swalaah ya Ijumaa



Kukoga siku ya ijumaa ni jambo la lazima, na mwenye kuacha, basi anapata dhambi kwa mujibu wa kauli mbili sahihi zaidi za Maulamaa. Haya yamesemwa na Abuu Hurayrah, 'Ammaar bin Yaasir, Abuu Sa'iyd Al-Khudriy na Al-Hasan. Haya yamekuja pia katika riwaya iliyopokelewa toka kwa Maalik na Ahmad. Aidha, ni madhehebu ya Ibn Hazm. [Al-Muhalla (2/12) na Al-Awsatw (4/43)].



Dalili za hili ni:



1- Hadiyth ya Abuu Sa'iyd Al-Khudriy kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) amesema:

((غسل يوم الجمعة واجب على كل محتلم)(

((Kukoga siku ya ijumaa ni wajibu kwa kila aliyebaleghe)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (2491) na Ahmad (7911)].



2- Hadiyth ya Ibn 'Umar kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) amesema:

((من جاء منكم إلى الجمعة فليغتسل))

((Anayekwenda ijumaa kati yenu, basi aoge)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2/6) na Muslim (844)].



3- Hadiyth ya Abuu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) amesema:

((حق على كل مسلم أن يغتسل في كل سبعة أيام يوما، يغسل رأسه وجسده))

((Haki iliyo juu ya kila Muislamu, ni kuoga siku moja katika kila siku saba. Aoshe kichwa chake na mwili wake)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2/318) na Muslim (849)].



4- Hadiyth ya Thawbaan kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) amesema:

((حق على كل مسلم السواك، وغسل يوم الجمعة، وأن يمس من طيب أهله إن كان))

((Haki iliyo juu ya kila Muislamu ni mswaki, kuoga siku ya ijumaa na ajipake mafuta uzuri ya ahli wake kama yapo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (4/34). Tizama "Asw-Swahiyhah" (1796)].



5- Hadiyth ya Hafswa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) amesema:

((على كل محتلم رواح الجمعة، وعلى من راح الجمعة أن يغتسل))

((Kila aliyebaleghe ni lazima aende ijumaa, na mwenye kwenda ijumaa ni lazima akoge)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (338), An-Nasaaiy (3/89) na Ahmad (3/65)].



6- Imepokelewa toka kwa Ibn 'Umar, amesema:

"Tuliamrishwa kukoga siku ya ijumaa, na tusitawadhe (ili kuondosha janaba) kutokana na kujamii".[Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Bakr Al-Muruuziy katika "Ijumaa na fadhila zake”].



Wamesema:

“Na kuyafanya kuwa si wajibu wala si haki kwa mfano wa dalili hizi zilizotajwa hapo juu, hayo aliyoyaelezea Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) ya kwamba ni haki ya Allaahu (Subhaanahuu Wata'alaa) kwa kila Muislamu na kwamba ni wajibu kwa kila aliyeota (aliyebaleghe), basi hili ni jambo ambalo ngozi husisimka kwalo!! [Mfano wake katika Al-Muhalla].



Nayo Jamhuri ya Maulamaa wakiwemo Ibn Mas'uud na Ibn 'Abbaas ambao ni katika Maswahaba, msimamo wao ni kuwa kukoga siku ya ijumaa ni jambo mustahabbu na wala si lazima. Na kati ya dalili muhimu walizozitoa ni:



1- Hadiyth Marfu’u ya Samurah bin Jun-dub:

((من توضأ يوم الجمعة فبها ونعمت، ومن اعتسل فالغسل أفضل))

((Mwenye kutawadha siku ya ijumaa, basi hilo ni jambo zuri, na mwenye kukoga, basi kukoga ni jambo bora)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (354), An-Nasaaiy (3/94), At-Tirmidhiy (497) na wengineo. Hadiyth hii ina njia ambazo nimezitafiti kwa kina na kuzizungumzia katika Allam-'at Fiy Aadaab Wa Ahkaam Al-Jum-'ah. Al-'Allaamah Al Al-Baaniy amesema ni Hadiyth Hasan].



Haya ni maneno yaliyo wazi zaidi katika dalili yao ijapokuwa Hadiyth ni Dhwa’iyf kwa kauli yenye nguvu.



2- Hadiyth Marfu’u ya Abuu Hurayrah:

((من توضأ فأحسن الوضوء ثم أتى الجمعة فاستمع وأنصت، غفر له ما بينه وبين الخمعة وزيادة ثلاثة أيام .....))

((Mwenye kutawadha, akatawadha ipasavyo, kisha akenda ijumaa, akasikiliza na akanyamaza, hughufiriwa yaliyo baina yake na kati ya ijumaa pamoja na nyongeza ya siku tatu…..)).[Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (857), At-Tirmidhiy (498) na wengineo].



Wamesema:

“Lau kama kuoga kwa ajili ya ijumaa kungelikuwa ni lazima, basi Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) asingelitaja wudhuu peke yake”.



Al-Haafidh ameijibu kauli hii katika "Al-Fat-h" (2/422) kwa kusema:

" Kukoga hakujakanushwa, kwani Hadiyth imekuja kwa njia nyingine katika Asw-Swahiyh kwa tamko "Mwenye kukoga". Kwa hiyo inawezekana kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) ametaja wudhuu kwa yule ambaye alikwishaoga kabla ya kwenda, na akahitajia kutawadha tena".



Ninasema:

"Wao wana dalili nyinginezo nilizozitafiti kwa kina na kuzijadili moja baada ya nyingine katika Kitabu changu cha "اللمعة في آداب وأحكام الجمعة". Na hitimisho la suala ni kuwa wenye kusema kwamba kukoga ni wajibu, dalili zao zina nguvu zaidi, Sanad zake ni Swahiyh zaidi na kuzitumia ni salama zaidi”.



7- Kufa



Ni moja kati ya sababu zenye kuwajibisha kukoga, lakini si kwa maiti mwenyewe, bali ni kwa Muislamu aliyeko kwa maiti. Uchambuzi wake utakuja katika mlango wake wa "Kitaab Al janaaiz'
 
Back
Top Bottom