Ramadhan Special Thread
Assalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh

Ili Muislamu aendelee kuwa katika utiifu wa Allah basi hana budi kuwa karibu na mambo ambayo yatamuweka karibu na Allah ikiwemo kusoma mawaidha mbali mbali na kusikiliza darsa mbali mbali na kusoma qur'an pamoja na kujua maana yake pia maana kwa kufanya hivyo ndio uzingatiaji wa aya zake hufikia malengo

Ikiwa Ramadhani ikiisha na mambo haya hayapatikani basi ni rahisi sana kwa mja kurejea tena katika maisha yake ya awali,kwakuwa imani ina sifa ya kupanda na kushuka,ni kwa kujiweka karibu tu na mambo hayo niliyo taja hapo juu itamsaidia mja kuendelea kuwa katika imani

Kwa Muktadha huu mimi binafsi ningependa uzi huu uwe ni sehemu ya kupeana mawili matatu juu ya uislamu wetu na kuzidi kuhuisha imani zetu,yani isiishie kwenye ramadhani tu! Bali tupate faida nyenginezo pia

Uzi huu uwe ni jukwaa la kukumbushana juu ya mambo ya dini yetu pia

Ntaanza tukumbushane mambo ya fiqh/sheria za kiislamu,ntachukua elimu hii kutoka mtandao wa Alhidaaya.com kwakuwa wanaruhusu kushare materials

Hii itatukumbusha baadhi yetu na kuwafundisha wageni katika uislamu waijue sheria yao ya dini katika kuyaendea maswala mbali mbali ya kiibada

Karibuni sana
 
001-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara:Taarifu Ya Twahara Na Umuhimu Wake


Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara:



001-Taarifu Ya Twahara Na Umuhimu Wake





Alhidaaya.com





Maana Ya Twahara Katika Lugha Ya Kawaida:





Ni usafi na kuondosha uchafu au takataka za kihisia (kugusika) kama najsi ya mkojo au kinginecho, na za kidhahania kama kasoro (mapungufu) na maasi.



Kutwaharisha ni kusafisha, nako ni kupaweka mahala maalumu katika hali ya usafi. [Al-Libaab Sharhul Kitaab (1/10) na Ad-Durru Al-Mukhtaar (1/79)].



Ama kisharia (kitaaluma):



Ni kuondosha kinachozuia kuswali kama hadathi au najsi kwa kutumia maji (au kinginecho), au kuondosha hukmu yake kwa mchanga. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (1/12)].





Hukmu ya twahara:



Kutwaharisha najsi na kuiondosha ni jambo la wajibu ikiwa mtu atakumbuka na ataweza. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Anasema:

((وَثِيَابَكَ فَطَهِّر))

((Na nguo zako zitwaharishe)) [Al-Muddath-thir (74:4)]



Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala):

((أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ))

((Ya kwamba itakaseni Nyumba Yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kutufu na wanaojitenga humo kwa ‘ibaadah, na wanaoinama na kusujudu)). [Al Baqarah (2:125)]



Ama kujitwaharisha na hadathi, hilo ni lazima ili ruhusa ya kuswali ipatikane kwa neno lake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

(( لَا تُقْبَلُ صَلَاةُ بغير طهور))



((Swalaah haikubaliwi bila ya wudhuu). [Swahiyh Muslim 224]





Umuhimu Wake:





1- Twahara ni sharti ya kusihi kwa sala ya mja. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((لَا تُقْبَلُ صَلَاةُ مَنْ أَحْدَثَ حَتَّى يَتَوَضَّأَ ))

((Haikubaliwi Swalaah ya mtu mwenye hadathi mpaka atawadhe)). [Imepasishwa na Al Bukhaariy (135), Muslim (225].



Kuswali na twahara ni kumtukuza Allaah. Na hadathi na janaba – ingawa si najsi zenye kuonekana – lakini hata hivyo ni najsi za kidhahania zenye kukifanya kilichoingiwa navyo kuonekana kichafu. Hivyo basi, kuwepo kwake huteteresha utukuzo kwa Allaah, na huenda kinyume na msingi wa usafi.





2- Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Amewasifu wenye kujitwaharisha. Anasema:



((إِنَّ اللّهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ))

((Hakika Allaah Anawapenda wenye kutubia mara kwa mara na Anawapenda wenye kujitwaharisha)). [Al Baqarah 2:222]



Akawasifu watu wa Masjid Qubaa kwa Neno Lake:



((فِيهِ رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُواْ وَاللّهُ يُحِبُّ الْمُطَّهِّرِينَ))

((Ndani yake kuna watu wanaopenda kujitwaharisha, na Allaah Anawapenda wenye kujitwaharisha)). [At Tawbah 9:108]





3- Kutojali au kutotilia maanani kujitakasa na najsi, ni moja kati ya sababu za kuadhibiwa watu makaburini. Imepokelewa na Ibn 'Abbaas akisema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipita kwenye makaburi mawili akasema:



(( إِنَّهُمَا لَيُعَذَّبَانِ وَمَا يُعَذَّبَانِ فِي كَبِيرٍ، أَمَّا هذا فَكَانَ لَا يَسْتَنزه مِنْ بَوْلِهِ، ))

((Kwa hakika wawili (hawa) wanaadhibiwa, na hawaadhibiwi kwa jambo kubwa. (la kuwashinda kutekeleza au kujiepusha nalo). Ama huyu, alikuwa hajitakasi na mkojo wake)). [Abu Daawuud (20), An Nasaaiy (31-69), na Ibn Maajah (347) kwa Sanad Swahiyh].
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara:



002-Aina Za Twahara



Alhidaaya.com





Maulamaa wanaigawanya twahara ya kisharia katika vigawanyo viwili:

1- Twahara halisi, nayo ni kuondosha uchafu (najsi) unaokuwepo katika mwili, nguo na mahala.





2-Twahara ya kihukmu, nayo ni kujitwaharisha kutokana na hadathi. Twahara hii inahusiana na mwili tu, na iko aina tatu:

-Twahara kubwa, nayo ni kuoga.

-Twahara ndogo, nayo ni kutawadha.

-Na badala ya viwili hivyo vinaposhindikana, nayo ni kutayamamu.





Kwanza: Twahara Halisi



Makusudio Ya Najsi:



Najsi ni kinyume cha twahara. Ni jina la kitu chenye kuonekana kichafu kisharia. Ni lazima Muislamu ajiepushe nacho na akioshe kile kilichompata katika kitu hicho.



Aina Za Najsi:



Vitu ambavyo dalili za kisharia zimethibitisha kuwa ni najsi ni:



1, 2- Kinyesi na mkojo wa mwanadamu



Viwili hivi ni najsi kwa Ijma’a ya Maulamaa.



Dalili ya kinyesi kuwa ni najsi ni neno lake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

(( إذَا وَطِئَ أَحَدكُمْ بِنَعْلِهِ الْأَذَى فَإِنَّ التُّرَابَ لَهُ طَهُورٌ ))

((Akikanyaga mmoja wenu kinyesi kwa kiatu chake, basi udongo ndio kitwaharisho chake)). [Abuu Daawuud (385) kwa Sanad Swahiyh].

Pia zinadulisha unajsi wake Hadiyth zote zenye kuamuru kustanji ambazo zitakuja karibuni.



Ama mkojo, ni kwa Hadiyth ya Anas kwamba bedui mmoja alikojoa ndani ya masjid na baadhi ya watu wakamnyanyukia kutaka kumpiga. Hapo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:

((دعوه لا تزرموه))

((Mwacheni msimkatishe)).



Akasema: “Alipomaliza, aliagiza ndoo ya maji akaimimina juu yake”. [Imepasishwa na Al-Bukhaariy (6025) na Muslim (284)].





3, 4- Madhii na wadii



Madhii ni maji mepesi mno yenye kunatanata yanayotoka wakati wa matamanio ya kimwili kama kuchezeana, au mtu anapokumbuka tendo la kujimai au kuwa na hamu nalo. Maji haya hayachupi au kufuatiwa na mchoko, na mtu anaweza asiyahisi yanapomtoka. Humtoka mwanamume na mwanamke, lakini wanawake ni zaidi. [Angalia Fat-hul Baariy (1/379), na Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (1/599)].



Nayo ni najsi kwa Ijma’a ya Maulamaa. [Angalia Al-Majmuu cha An-Nawawiy (2/6) na Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (1/168)].



Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru kuuosha utupu maji hayo yanapotoka.



Katika Swahiyh Mbili panaelezwa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia aliyemuuliza kuhusu madhii:

((يغسل ذكره ويتوضأ))

((Aoshe dhakari yake na atawadhe)). [Imepasishwa na Al-Bukhaariy (269) na Muslim (303)]

Ama wadii, haya ni maji mazito meupe yanayotoka baada ya kukojoa. Ni najsi kwa Ijma’a ya Maulamaa.



Imepokelewa na Ibn 'Abbaas akisema: "Manii, wadii na madhii. Ama manii, ni yale ambayo yakitoka, ni kuoga. Ama wadii na madhii (yakitoka), basi osha dhakari yako – au nyuchi zako – na tawadha wudhuu wako wa Swalaah". [Sunan Al-Bayhaqiy (1/115). Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahiyh Sunan Abuu Daawuud (190)].



5- Damu ya hedhi



Ni kwa Hadiyth ya Asmaa binti Abuu Bakr (Radwiya Allaahu 'anhuma), amesema: "Alikuja mwanamke mmoja kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Afanyaje mmoja wetu nguo yake ikiingia damu ya hedhi?” Akasema Rasuli:

((تحته ثم تقرصه بالماء ثم تنضحه، ثم تصلي فيه))

((Ataipikicha, kisha ataikwangua kwa ncha ya kidole na maji, halafu ataisuuza, na kisha ataswalia)). [Imepasishwa na Al-Bukhaariy (227) na Muslim (291].





6- Kinyesi cha mnyama asiyeliwa

Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah ibn Mas'uud, amesema: Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitaka kwenda haja kubwa akaniambia:

((ائتني بثلاثة أحجار))

((Niletee vijiwe vikubwa vitatu)).

Nilimpatia viwili na kinyesi cha (punda). Akachukua vijiwe viwili akakitupa kinyesi na kuniambia:

((هي رِجْسٌ ))

((Hicho ni najsi)). [Swahiyh Al-Bukhaariy (156), At-Tirmidhiy (17), An-Nasaaiy (42), na Ibn Khuzaymah ambaye ameongeza (punda wake].



Kitendo hiki kinaonyesha kwamba kinyesi cha mnyama asiyeliwa ni najsi.





7- Mate ya mbwa





Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:



(( طُهُورُ إِنَاءِ أحَدِكُمْ إِذَا وَلَغَ فِيهِ الكَلْبُ أنْ يَغْسِلَهُ سَبْعَ مَرَّاتٍ أُولاَهُنَّ بِالتُّرَابِ.))

((Utwaharisho wa chombo cha mmoja wenu mbwa akikitia ulimi ni kukiosha mara saba, ya kwanza kati yake kwa udongo)). [Swahiyh Muslim (279)].



Hadiyth hii inaonyesha kwamba mate ya mbwa ni najsi.







8- Nyama ya nguruwe



Ni najsi kwa Ijma’a ya Maulamaa kwa kuelezewa wazi katika neno Lake Subhaanah:



((قُلْ لَا أَجِدُ فِي مَا أُوحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَىٰ طَاعِمٍ يَطْعَمُهُ إِلَّا أَنْ يَكُونَ مَيْتَةً أَوْ دَمًا مَسْفُوحًا أَوْ لَحْمَ خِنْزِيرٍ فَإِنَّهُ رِجْسٌ ))

(( Sema: Sioni katika yale niliyofunuliwa mimi kitu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayomwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hayo ni uchafu )). [Al An-Aam (6:145].





9- Nyamafu



Naye ni mnyama aliyejifia mwenyewe bila kuchinjwa chinjo la kisharia. Ni najsi kwa Ijma’a ya Wanazuoni kwa neno lake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam:

(( إِذَا دُبِغَ الإِهَابُ؛ فَقَدْ طَهُرَ))

((Ngozi ya nyamafu ikisafishwa na kukaushwa kwa madawa, basi imetwaharika)). [Swahiyh Muslim (366)].



Haviingii katika hukmu hii:



(a) Maiti ya samaki na nzige.



Viwili hivi ni twahara kwa neno lake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):



((أُحِلَّتْ لَنَا مَيْتَتَانِ وَدَمَانِ: أما الميتتان فالحوت وَالْجَرَادُ ، وأما َالدمان فالْكَبِدُ ، وَالطِّحَالُ ))

((Tumehalalishiwa mfu mbili na damu mbili. Ama mfu mbili, ni samaki na nzige. Ama damu mbili, ni ini na wengu)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (3218, 3314) na Ahmad (2/97) kwa Sanad Swahiyh].





(b) Mfu wa mnyama asiye na damu ya kuchuruzika



Ni kama nzi, nyuki, sisimizi, chawa na kadhalika kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):



(( إذا وقع الذباب في إناء أحدكم فليغمسه كله أو ليطرحه، فإن في أحد جناحيه داء وفي الآخر شفاء))

((Akiangukia nzi katika chombo cha mmoja wenu, basi amzamishe wote au amtupe, kwani katika bawa lake moja kuna ugonjwa na katika jingine kuna ponya)).[Swahiyh Al-Bukhaariy (3320)].





(c) Mifupa ya mfu, pembe zake, kucha zake, manyoya yake na magoya yake.



Hivi vyote asili yake ni twahara. Al-Bukhaariy katika Swahiyh yake (1/342) ameeleza: “Amesema Az-Zuhriy - kuhusu mifupa ya mzoga wa mnyama kama vile tembo na wengineo - : Niliwakuta watu katika Maulamaa waliotangulia wakichana nywele na kujitia mafuta kwa vitu hivyo, nao hawaoni ubaya wowote kwa hilo”.

Hammaad amesema: “Hakuna ubaya kwa ugoya wa mfu”.





10- Kilichokatwa toka kwa mnyama aliye hai



Kilichokatwa toka kwa mnyama hai kina hukmu ya nyamafu kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((ما قطع من البهيمة وهي حية فهو ميتة))

((Kilichokatwa kwa mnyama akiwa hai, basi ni nyamafu)).[Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (1480), Abu Daawuud (2858) na Ibn Maajah (3216)].



11- Makombo ya maji ya wanyama mwitu na wanyama wasioliwa.



Unajsi wake unagusiwa na kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoulizwa kuhusu maji ya jangwani (nyikani), na yale yanayonywewa mara kwa mara na wanyama mwitu na wanyama wasioshambulia akasema:

((إِذَا كَانَ الْمَاءُ قُلَّتَيْنِ؛ لَمْ يَحْمِلِ الْخَبَثَ))

((Maji yakiwa kullatayni, hayabebi uchafu (najsi)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (63), An Nasaaiy (1/46), na At-Timidhiy (67). Ipo katika Swahiyh Al-Jaami’i (758)].

Ama mabaki ya paka na mfano wake, hayo ni twahara kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

(( إِنَّهَا لَيْسَتْ بِنَجَسٍ ، إِنَّهَا مِنَ الطَّوَّافِينَ عَلَيْكُمْ وَالطَّوَّافَاتِ ))

((Yeye si najsi, bali ni katika waume na wake wanaowazungukieni)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (5/303) na Aswhaab As-Sunan. Angalia Al-Irwaa (173)].





12- Nyama ya mnyama asiyeliwa



Hii ni kwa Hadiyth ya Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: "Tuliipata nyama ya punda – yaani siku ya Khaybar – na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akanadi:

((إن الله ورسوله ينهاكم عن لحوم الحمر فإنها رجس، أو نجس))

((Hakika Allaah na Rasuli Wake Anakukatazeni nyama ya punda. Ni uchafu, au najsi)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1940) na Ahmad (3/121). Ipo kwenye Al-Bukhaariy bila ya neno: (فإنها رجس)]



Na kwa Hadiyth ya Salamah bin Al Akwa'a, amesema:

“Ilipoingia jioni ya siku Khaybar imekombolewa, waliwasha mioto mingi. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:

((ما هذه النار على أي شيئ توقدون))

((Moto huu ni wa nini? Mnauwashia kwa jambo gani?))

Wakasema: "Kwa ajili ya nyama". Akauliza:

((Ya mnyama gani?)).

Wakasema: “Nyama ya punda wa mjini”. Akasema:

((Imwageni na vivunjeni)).

Akasema mtu mmoja: “Ee Rasuli wa Allaah! Je, tuimwage na tuvioshe”? Akasema:

((Au hilo)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1802)].



Katika Hadiyth hizi mbili, kuna dalili kwamba nyama ya punda wa mjini (kienyeji) ni najsi kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ya kwanza:

((Ni uchafu, au najsi)), na katika Hadiyth ya pili kwa kukivunja chombo kwanza, kisha kuruhusu kutumika kwa kukiosha mara ya pili.
 
Allahumma Aamiin

20250326_230732.jpg
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara:



003-Je Manii Ni Twahara Au Najsi?



Alhidaaya.com





Wanazuoni wamehitilafiana juu ya suala hili kwa kauli mbili:



Kauli ya kwanza:



Inasema kwamba manii ni najsi. Kauli hii ameisema Abu Haniyfah na Maalik, nayo ni riwaya iliyopokelewa toka kwa Ahmad. Wamelitolea dalili hilo kwa Hadiyth ya 'Aaishah alipoulizwa kuhusu manii yaliyoingia kwenye nguo akasema: "Nilikuwa nikiyaosha kwenye nguo ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kisha anatoka moja kwa moja kwenda kuswali huku athari ya doa la maji ikiwa katika nguo yake". [Imepasishwa na Al-Bukhaariy (230) na Muslim (289)].

Na kuosha hakuwi ila kwa kitu najsi.





Kauli ya pili:



Wenye kauli hii wamesema kuwa manii ni twahara. Kati ya waliolisema hilo ni Ash-Shaafi'i na Daawuud. Hii ni riwaya Swahiyh zaidi kati ya riwaya mbili zilizopokelewa toka kwa Ahmad. Wamelitolea dalili hilo kwa Hadiyth ya 'Aaishah kuhusu manii, aliposema: "Nilikuwa nikiyakwangua kuyatoa kweye nguo ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)”. [Hadiyth Swahiyh: Muslim (288)].



Na kwa Hadiyth yake nyingine kwamba mgeni alishukia kwa 'Aaishah na akawa anaiosha nguo yake. 'Aaishah akamwambia: "Ilikuwa inakutosha tu ikiwa utayaona, uoshe mahala pake, na ikiwa hukuyaona, unyunyizie maji kuzungukia hapo. Na bila shaka umeniona nikiyakwangua kwa umakini kwenye nguo ya Nabiy wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na yeye akaiswalia". [Hadiyth Swahiyh: Muslim (288)].



Na kutosheka kuyakwangua, kunaonyesha kuwa manii ni twahara.



Wenye kusema kuwa manii ni najsi, wamejibu kuwa kukwangua hakuonyeshi kuwa manii ni twahara, bali kunaonyesha namna ya kuyatwaharisha kama vinavyotwaharishwa viatu kwa kuvipangusa katika mchanga.



Hili linajibiwa kwa kusema kuwa 'Aaishah alipoyakwangua manii mara moja na kuyaosha mara nyingine, hilo halihukumii kuwa ni najsi, kwani nguo inaoshwa kwa kuingia makamasi, mate au uchafu. Na hivi ndivyo walivyosema baadhi ya Maswahaba kama vile Sa'ad bin Abiy Waqqaasw, Ibn 'Abbaas na wengineo. Wamesema:

"Manii ni kama makamasi na mate, jisafishe uyaondoshe japokuwa kwa kijiti." [Majmuu Al-Fataawaa (21/605)].



Na kwa hili, inadhihiri kuwa kitendo cha 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa), kinaingia katika mlango wa kujichagulia namna ya kusafisha. [Sharhu Muslim].



Hukmu ya kuwa manii ni twahara inapata nguvu tunapojua kwamba Maswahaba walikuwa wakiota wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na manii hayo yalikuwa yakiingia katika miili na nguo za baadhi yao. Na lau kama yangelikuwa ni najsi, basi ingelikuwa ni lazima kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) awaamrishe wayasafishe kama alivyowaamrisha wastanji. Na kwa kuwa hakuna yeyote aliyelinukuu hili, inajulikana kwa yakini kuwa kuyaondosha hakukuwa ni jambo la lazima. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi. [Majmuu Al-Fataawaa (21/604)].
 
Naam ndugu zangu hili ni darsa la fiqh linaendelea,hiki kitabu kizur sana alhidaaya walitoa sababu nzur sana kwa nini walikichagua kama mrejea wa kujifunza fiqh,kina dalili mbali mbali na kimepitishwa na wajuzi wa hadith

Sikutaka tu kuweka utangulizi hapa wa kitabu lkn wametoa maelezo mazuri sana,kwahiyo tujikumbushe kuhusu fiqh kwa tunao jua hakika hutakosa jambo jipya la kujifunza

Uislamu ni elimu,na ibada hazifanywi vizur bila elimu ya kutosha

Tuendelee kufuatilia darsa kwani kujifunza elimu ya dini nayo ni ibada
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



004-Je, Pombe Ni Najsi?





Alhidaaya.com







Wanazuoni wamehitilafiana juu ya hukmu ya pombe katika kauli mbili:



Kauli ya kwanza:



Pombe ni najsi.

Huu ni mwelekeo wa Jamhuri ya Maulamaa wakiwemo Maimamu wanne. Shaykh wa Uislamu yupo katika kundi hili. Na hoja yao ni Neno Lake Subhaanah:



((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالأَنصَابُ وَالأَزْلاَمُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ))

((Enyi walioamini! Bila shaka ulevi, kamari, kuabudu masanamu na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya shaytwaan. Basi jiepusheni navyo ili mpate kufanikiwa)). [Al Maaidah 5:90].

Wanasema kwamba uchafu "rijsu" ni najsi, na kwa hivyo, wamehukumu kuwa pombe yenyewe ni najsi ya kihisia.



Kauli ya pili:



Pombe ni twahara.

Rai hii wameisema akina Rab-y'a, Al-Layth, Al-Muzany na watangu wema wengineo. Na imetiliwa nguvu na Ash-Shawkaany, As Swan-’aaniy, Ahmad Shaakir na Al-Albaaniy (Allaah Awarehemu). Kauli hii ndio yenye nguvu kwa dalili zifuatazo:



1- Ni kwamba katika Aayah hakuna dalili juu ya unajsi wa pombe. Na hii ni kwa njia zifuatazo:



(a) Ni kwamba neno uchafu "rijsu", ni katika visawe, kwani linabeba maana tofauti. [Angalia kitabu cha An-Nihaaya cha Ibn Al-Athyr pamoja na Lisaan Al-‘Arab, Mukhtaar As-Swihaah na Tafsiyr mbalimbali]. Kati ya maana hizo ni kitu kichafu, kitu kilichoharamishwa, kitu kibaya, adhabu, laana, ukafiri, shari, dhambi, najsi na kadhalika.



(b) Ni kwamba "sisi hatujakuta" au kugundua kauli ya mwanasalafi yeyote aliyefasiri "Ar-Rijsu" katika Aayah hii kwa maana ya najsi, bali Ibn 'Abbaas amesema kuwa "Ar-Rijsu" ni hasira, wakati Ibn Zayd amesema kwamba "Ar-Rijsu” ni shari.



(c) Kwamba neno "rijsu", mbali na Aayah hii, limekuja katika Kitabu cha Allaah katika pahala patatu, na hakuna pahala popote kati yake ambapo "rijsu" ina maana ya najsi. Katika Neno Lake Subhaanah:

((كَذَلِكَ يَجْعَلُ اللّهُ الرِّجْسَ عَلَى الَّذِينَ لاَ يُؤْمِنُون))

Hivyo ndivyo Allaah Anavojaalia unajisi (na adhabu) juu ya wale wasioamini. [Al-An’aam: 125]

…neno "Ar-Rijsu" hapa, maana yake ni adhabu.

Na katika neno Lake Subhaanah kuhusu wanafiki:

إِنَّهُمْ رِجْسٌ ۖ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ

hakika wao ni najsi, na makazi yao ni Jahannam. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyachuma. [At-Tawbah: 95]



..makusudio ni kuwa vitendo vyao ni vichafu, yaani vibaya.



Na katika Neno Lake Subhaanah:

((فَاجْتَنِبُوا الرِّجْسَ مِنَ الْأَوْثَانِ))

Basi jiepusheni na uchafu wa (kuabudu) masanamu [Al-Hajj: 30]



..masanamu yameitwa uchafu kwa vile yenyewe ndio sababu ya makamio na adhabu, na wala makusudio sio najsi ya kukamatika, kwani mawe yenyewe na masanamu si najsi.

(d) Na ilipotuka katika Aayah kuwa pombe ipo sanjari na masanamu na upigaji ramli, hilo limekuwa ni kielelezo chenye kuengua maana ya uchafu kupelekea katika unajsi usio wa kisharia. Na ndivyo hivyo hivyo katika Kauli Yake Subhaanah:

((إِنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَسٌ ))

((Hakika washirikina ni najsi)). [At Tawbah (9:28)]



..zilipokuja dalili sahihi zinazothibitisha kuwa miili ya washirikina si najsi.





(e) Kwamba kuharamishwa pombe, hakuwajibishi kuwa ni najsi, kwani tunaona ni haramu kuvaa hariri na dhahabu ingawa vyenyewe ni twahara ikiwa ni udharura wa kisharia na kwa makubaliano ya wote.



(f) Kwamba neno "Ar-Rijsu" katika Aayah limeainishwa (muqayyad) kuwekwa ndani ya (kazi ya shaytwaan). Kwa hiyo ni uchafu wa kivitendo, kwa maana ya kuwa ni kitu kibaya au kilichoharamishwa au dhambi, na wala si uchafu wa kiini cha kitu wa kuvifanya vitu hivi kuwa ni najsi.



2- Na kati ya vinavyotolewa ushahidi juu ya utwahara wa pombe ni aliyoyasema Anas katika kisa cha kuharamishwa pombe. Anasema: "…Na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamrisha mwenye kunadi atangaze: Jueni kwamba pombe imeharamishwa,…". Akasema: "Nikatoka nikaimwaga, ikatiririka katika barabara za Madiynah” [Swahiyh Al-Bukhaariy (2332), na Muslim (1980)].





3- Na katika kisa cha mtu aliyekuwa na mapipa mawili ya pombe



((…Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Hakika Allaah Aliyeharamisha kuinywa, Ameharamisha kuiuza)). Mtu yule akayafungulia mapipa mawili mpaka vikamalizika vilivyomo ndani yake…).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa ‘ikhraaj” na Muslim, na Maalik (1543)].



Na lau kama tembo ingelikuwa najsi, basi Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) angeliamrisha kumwagia maji juu ya ardhi ili kuitwaharisha kama alivyoamrisha kumwagia maji juu ya mkojo wa bedui, na angeliwaamuru kujikinga nayo.



4- Kwamba asili yake ni twahara, na hanukui kuhusu utwahara huo ila mnukuzi sahihi. Na kwa kuwa hakuna dalili yoyote inayothibitisha unajsi wake, pombe inabakia katika asili
 
Katika hadithi iliyopokelewa na ummu habiba mkewe na Mtume rehma na amani ziwe juu yake

Amesema Mtume "Maneno yote anayoongea mwanadamu ni dhidi yake isipokuwa anapo mtaja Allah na kumkumbuka Allah,anapoamrisha mema na kukataza mabaya na annapoelekeza mambo ya kheri"

Kwahiyo haya maneno tunayo ongea ni hoja dhidi yetu dhidi ya siku ya kiama kwa maana mengi tunayoongea itakuwa ni sababu ya kututia matatizoni

Kwahiyo tuwe makini na kauli zetu
 
MSAADA WA ALLAH HUPATIKANA KWA SUBIRA NA KUSWALI

Ndugu zangu katika imani Allah ameshatufahamisha kwenye qur'an kwamba tutake msaada kwa kusubiri na kuswali

Kama alivyotueleza katika al baqara 153

2:153 - Enyi mlio amini! Takeni msaada kwa subira na Sala. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri.

Kwahiyo ndugu zangu katika imani endapo umepatwa na changamoto yoyote katika maisha basi kwanza swali rakaa mbili kisha fanya subira hakika Allah yupo pamoja na wanao subiri

Mtume swallallahu alaih wassallamu alipopata changamoto yoyote ile kwanza alikimbilia msikitini na kuswali rakaa mbili,inasemwa siku moja Mtume alipoona upepo mkali alikimbilia msikitini huku anaburuza joho lake

Na Mtume anasema manabii wote walikuwa wanaswali mara tu wanapopata mtihani wowote ule

Kwahiyo ndugu hiyo ni njia ya kutatua shida zetu

Amka usiku wa manane swali rakaa mbili na mlilie Allah kwa shida zako kisha kuwa na subira
 
Inasemwa Wema walio tangulia huko nyuma walikuwa wanajitayarisha miezi sita kabla ya Ramadhani na kisha baada ya kufunga Ramadhani wanaendelea kuishi na yale mema ya Ramadhani kwa miezi mingine sita

Nasi pia tuwe katika twaa hiyo ili siku zote nyoyo zetu zimuelekee Allah

Ndio maana mimi binafsi hata baada ya Ramadhani kadri ya atakavyonijalia Allah nitakuwa napost humu katika uzi huu ili tuhuishe imani zetu,Nayafanya haya kwa kutaka radhi za Allah
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



005-Je Damu Ni Najsi?



Alhidaaya.com







Damu ina vigawanyo:



1- Damu ya hedhi:



Damu hii ni najsi kwa makubaliano ya Maulamaa. Dalili ya unajsi wake imekwisha elezewa nyuma.





2- Damu ya mwanadamu



[Tafsiyr Al-Qurtubiy (2/221), Al-Majmuu (2/511), Al-Muhalla (1/102),Al-Kaafiy (1/110), As-Sayl Al-Jarraar na Bidaayat Al-Mujtahid (1/31), Ash Sharh Al-Mumtani-’i (1/376), As Silsilat As-Swahiyhah , na Tamaam Al-Minna (uk.50)].



Ni damu iliyosababisha mahitalifiano juu ya hukmu yake. Lililo mashuhuri kwa wafuasi wa madhehebu ya kifiqhi ni kwamba damu ni najsi, lakini hawana dalili. Isipokuwa damu imeharamishwa kwa matni ya Qur-aan katika neno Lake Aliyetukuka:



((قُل لاَّ أَجِدُ فِي مَا أُوْحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَى طَاعِمٍ يَطْعَمُهُ إِلاَّ أَن يَكُونَ مَيْتَةً أَوْ دَمًا مَّسْفُوحًا أَوْ لَحْمَ خِنزِيرٍ فَإِنَّهُ رِجْسٌ ))

(( Sema: Sioni katika yale niliyofunuliwa mimi kitu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayomwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu)).[Al An-‘aam (6:145)].



Kwa hiyo, kutokana na kuharamishwa kwake, wao wameichukulia kwamba ni najsi - kama walivyofanya katika pombe - na yaliyomo ndani yake hayafichikani. Lakini amenukuu zaidi ya Mwanachuoni mmoja katika Maulamaa kuwa wanakubaliana wote kwamba damu ni najsi. Maelezo zaidi yatakuja katika hilo.



Ni wakati ambapo kundi la waliokuja baadaye akiwemo Ash-Shawkaany, Siddiyq Khaan, Al-Albaaniy, Ibn ‛Uthaymiyn (Allaah Awarehemu) wameelekea kusema kuwa damu ni twahara kwa kutothibiti Ijma’a kwa upande wao. Wao wametoa dalili vilevile kwa haya yafuatayo:



1- Asili ya vitu ni twahara mpaka iwepo dalili kuthibitisha unajsi wake. Na sisi hatujui kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru kuosha damu nyingine zaidi ya hedhi ingawa mtu hupatwa mara nyingi na majeraha na mfano wake. Na lau kama damu ni najsi, basi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angelibainisha, kwa sababu hali ya mambo inahitajia hilo.



2- Ni kwamba Waislamu waliendelea kuswali na majeraha yao, na waliweza kuchuruzikwa na damu nyingi ambayo si ya kusameheka. Na wala haikupokelewa toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba aliamuru kuiosha, au kupokelewa kuwa wao walikuwa wakijilinda kwa hadhari isiwapate.



Amesema Al-Hasan: "Waislamu bado wanaswali wakiwa na majeraha yao". [Isnadi yake ni Swahiyh. Ameisimulia Al-Bukhaariy ikiwa ni “Mu’allaq” (1/336). Ibn Abiy Shaybah ameiunga kwa Sanad Swahiyh kama ilivyo katika Al-Fat-h (1/337)].



Na katika kisa cha Swahaba Muanswaar aliyekuwa akiswali usiku, ni kuwa mpagani alimpiga mshale, naye akauchomoa. Akampiga mwingine hadi ikafika mitatu. Kisha alirukuu, akasujudu na akaendelea na Swalaah yake na huku akivuja damu. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy ameifanya ni “Mu’allaq” (1/336), na Ahmad na wengineo wameseama ni “Mawsuwl”iunga, nayo ni Hadiyth Swahiyh].



Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) amesema: [Tamaam Al-Minnah (51,52)].

"Nayo iko katika hukmu ya Hadiyth Marfu’u, kwa vile kwa kawaida haiyumkiniki Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asilijue hilo. Na lau kama damu nyingi ingelikuwa inabatilisha Swalaah, basi Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angebainisha hilo, kwani haifai kuchelewesha taarifa wakati ule inapohitajika kama inavyojulikana katika taaluma ya "usuul". Na kama tutachukulia kwamba hilo lilifichikana kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi halifichikani kwa Allaah Ambaye hakifichikani Kwake chochote kikiwa ardhini au mbinguni. Na lau kama (damu) ingelikuwa inabatilisha au ni najsi, basi Rasuli angeliteremshiwa wahyi kama inavyojulikana kwa kila mtu".

Na katika kisa cha kuuawa ‘Umar bin Al-Khatw-twaab (Allaah Amridhie): "Umar aliswali, na huku jeraha lake linachuruzika damu". [Hadiyth Swahiyh. Maalik ameifanyia “ikhraaj”, na Al-Bayhaqiy kutoka kwake (1/357) na wengineo kwa Sanad Swahiyh].



3- Ni kwa Hadiyth ya 'Aaishah katika kisa cha kufa kwa Sa'ad bin Mu’aadh. Alisema: " Sa'ad bin Mu’aadh alipojeruhiwa siku ya Khandaq baada ya kupigwa mshale kwenye mshipa wa damu mkononi na mtu mmoja, Rasuli alimjengea hema Msikitini ili apate kumtizama kwa ukaribu. Na mara ghafla usiku, jeraha lake lilipasuka na damu ikachuruzika kwa wingi. Wakasema: Enyi wenyeji wa nyumba! Nini hiki kinatujia toka kwenu? Wakatazama. Wakashtuka kuona jeraha la Sa'ad limepasuka na damu inafoka, naye akafariki hapo hapo. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (3100) kwa ufupi, na Atw-Twabaraaniy katika kitabu cha Al-Kabiyr (6/7)].



Ninasema (Abuu Maalik): "Na wala haikupokelewa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru maji yamwagiwe juu yake na hasa pakizingatiwa kwamba yuko Msikitini kama alivyoamuru kumwagia maji juu ya mkojo wa bedui.



4- Kwamba Ibn Rushdi wakati alipotaja hitilafu za Maulamaa kwa upande wa damu ya samaki, alieleza kwamba sababu ya kuhitalifiana kwao ni kuhitilafiana kwa upande wa maiti yake. Mwenye kuzingatia kwamba maiti yake inaingia ndani ya ujumuishi wa kuharamishwa, basi na damu yake ataizingatia hivyo hivyo. Na asiyezingatia hivyo, basi ataitoa damu yake kwa kipimo cha maiti yake.



Na tunasema: "Wao wanasema kuwa maiti ya mwanadamu ni twahara, na kwa hivyo damu yake iwe hivyo hivyo kwa mujibu wa kaida yao".



Na kwa ajili hiyo, Ibnu Rushdi alisema baada yake: "Na matni ya Hadiyth ishaonyesha kwamba damu ya hedhi ni najsi. Ama damu nyingine, basi hiyo iko katika uasili uliokubaliwa na wenye kuzozana ya kwamba ni twahara. Na haitoki kwenye utwahara, ila kwa matni ya kusimamishia hoja".



Na ikiwa mtu atauliza: "Kwa nini damu ya hedhi isifanywe kipimo, na damu hii ni najsi?”

Tunasema: "Hiki ni kipimo kisichoendana, kwani damu ya hedhi ni damu ya maumbile ya asili kwa wanawake. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((ان هذا شيئ كتبه الله على بنات آدم))

((Hakika hiki ni kitu ambacho Allaah Amekiandika kwa mabinti wa Aadam (wanawake)).[Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (294) na Muslim (1211)].

Na akasema kuhusu istihaadhwah:

((انه دم عرق))

((Hakika hiyo ni damu ya mshipa (asili)). [Hadiyth Swahiyh, Al-Bukhaariy (327) na Muslim (333)].



Kisha damu ya hedhi ni damu nzito ya mvundo na harufu kali. Inafanana na mkojo na kinyesi, si damu yenye kutoka katika zisizo njia mbili.





3- Damu ya mnyama mwenye kuliwa



Mjadala kuhusu damu hii ni kama mjadala kuhusu damu ya mwanadamu kwa upande wa kutokuwepo dalili juu ya unajsi wake. Kwa hivyo inaambatana na utwahara wa asili.

Kusema kuwa ni twahara kunaungwa mkono vilevile na:



Yaliyoelezewa na Ibn Masu’ud, amesema: "Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali mbele ya Al-Ka’abah, na Abuu Jahli na marafiki zake wamekaa. Wakaambizana: “Ni nani kati yenu anaweza kwenda kwa ngamia wa akina fulani, kisha akusanye vinyesi, damu, na matumbo yao, halafu aje amsubiri mpaka atakaposujudu, amwagie mabegani mwake”? Mwovu wao akachomoka haraka, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposujudu, alim-mwagia kati ya mabega yake, na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi sallam) alitulia tuli katika sijdah, na wao wanacheka.[Hadiyth Swahiyh, Al-Bukhaariy (240) na Muslim (1794)].



Na lau kama damu ya ngamia ingelikuwa ni najsi, basi Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angeliitenga kando nguo yake, au angeikatisha Swalaah yake.



Aidha, imethibiti kwa njia sahihi kwamba Ibnu Mas-’oud aliswali na tumboni mwake kuna kinyesi na damu ya ngamia aliowachinja, lakini hakutawadha. [Isnadi yake ni Swahiyh. Muswannaf ‘Abdul Razzaaq (1/25), na Ibn Abiy Shaybah (1/392)].

Athar hii inaweza kuleta mvutano katika kutolea ushahidi juu ya utwahara wa damu ya mnyama, kwa vile Ibnu Mas-’oud hakuwa akiona kwamba utwahara wa mwili na nguo ni sharti ya kusihi Swalaah, bali anaona kuwa ni jambo linalopendeza (mustahab).



Ninasema (Abuu Maalik): “Lau kama imethibiti kwa Ijma’a kwamba damu ni najsi, basi hatutaziangalia dalili za waliofuatia baadaye. Na kama haikuthibiti, basi asili ni utwahara, na sisi hatuhitajii dalili hizo. Na lililodhihiri kwangu - baada ya kuchagua kauli (isemayo kuwa) damu ni twahara kwa kipindi cha miaka kumi - ni kwamba Ijma’a katika suala imethibiti. Ijma’a hii imenukuliwa na Maulamaa wengi na hakikuthibiti chenye kuitengua. Na nukuu ya juu zaidi kati ya hizo ni yale yaliyonukuliwa toka kwa Imaam Ahmad, kisha yale aliyoyanukuu Ibn Hazm, kinyume na yule aliyedhani kwamba madhehebu yake yanasema kwamba damu ni twahara!! Na kati ya niliyoyafahamu katika hilo ni:



Ibnu Al-Qayyim katika Ighaathat Al Lahafaan (1/420) amesema:



“Ahmad aliulizwa: Je, damu na usaha kwako ni sawa"? Akasema: "Hapana, watu hawakuhitilafiana kuhusu damu".



Na alisema mara moja: "Usaha kwangu ni afadhali kuliko damu".



Na imenukuliwa toka kwa Ibnu Hazm katika Maraatib Al Ijma’a: "Maulamaa wamekubaliana kwamba damu ni najsi ".



Vile vile Al-Haafidh katika Al Fat-h (1/420) amekunukuu kukubaliana huko.



Na Ibnu ‘Abdul-Barri katika At-Tamhiyd (22/230) anasema:



"Na hukmu ya kila damu ni kama damu ya hedhi, isipokuwa damu kidogo husamehewa kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameweka sharti ya unajsi wa damu kuwa iwe ni yenye kuchuruzika, na hapo inakuwa ni uchafu, na uchafu ni najsi. Na hii ni Ijma’a ya Waislamu kwamba damu yenye kuchuruzika ni uchafu na najsi..".



Na Ibnu Al-Araby katika Ahkaam Al-Qur-aan (1/79) anasema:



"Maulamaa wamekubaliana kwamba damu ni haramu na ni najsi kwa kinacholiwa na haitumiwi kwa manufaa yoyote. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameiainisha hapa kwa kuifanya ni damu ya aina yoyote ile (mutwlaq), na katika Suwrat Al-An 'Aam Ameiainisha kwa kuiwekea mpaka (muqayyad) ile tu ya kuchuruzika. Na Maulamaa kwa Ijma’a hapa, wameichukulia damu yoyote wakaiacha iliyoainishwa".



Na An-Nawawy katika Al-Majmu’u (2/576) amesema:

"Na dalili juu ya unajsi wa damu zinatiliana nguvu zenyewe kwa zenyewe, na mimi sijui kama kuna hitilafu yoyote toka kwa Muislamu yeyote ila tu yale aliyoyaelezea mtunzi wa Al-Haawiy toka kwa baadhi ya Maulamaa wa tawhiyd. Amesema kuwa ni twahara, lakini maneno ya Maulamaa wa tawhidi hayachukuliwi katika Ijma’a au mahitalifiano…".



Ninasema (Abuu Maalik): “Ninalolipa nguvu na uzito ni kuwa damu ni najsi kwa kuthibiti Ijma’a mpaka inukuliwe toka kwa Imaam mwingine atakayempiku Imaam Ahmad – (Allaah Amrehemu) – kwa kusema kuwa damu ni twahara. Na Allaah Ndiye Mjuzi
 
Kuombeana Dua za kheri kwa siri (bila ya mwenye kuombewa Dua kujua) ni jambo zuri mnooo. Nawakumbusha na kujikumbusha hili ndugu zangu Waislam.

20250326_230406.jpg
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



006- Je, Matapishi Ya Mwanadamu Ni Najsi?



Alhidaaya.com









Tumetangulia kusema mara nyingi kwamba asili ya vitu vyote ni twahara, na kwamba havihamishwi toka kwenye asili yake ila kwa kinukuo sahihi cha kutolea hoja kisichopingana na kile chenye kutiliwa nguvu au kuwa sawa nacho. Na ikiwa tutalipata hilo, basi ni vizuri. Na kama hatukulipata, basi itatulazimu tusimame msimamo wa kumpinga anayedai kuwa ni najsi. Kwani kudai huku kunamaanisha kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amewajibisha kwa Waja Wake kuviosha vitu hivyo vinavyodaiwa kuwa ni najsi, na kwamba kuwepo kwake kunazuia kuswali navyo. Basi ni ipi dalili ya hilo?!

Matapishi na mfano wake, hakuna kilichothibiti kwa njia sahihi chenye kuyahamisha toka kwenye utwahara wake wa asili.



Kuna kauli ya ‘Ammaar iliyopokelewa kuhusu matapishi akisema: "Wewe utaosha nguo yako iliyoingiwa na mkojo, kinyesi, matapishi, damu na manii".



Lakini kauli hii ni dhaifu haitolewi hoja. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.



Na imethibiti toka kwa Abu Ad-Dardaai akisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitapika, akafungua na akatawadha. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (2381), At-Tirmidhiy (87), Ahmad (6/443) na wengineo].



Katika Hadiyth hii, hakuna kiashirio chochote chenye kuonyesha kuwa matapishi ni najsi, na wala hakuna dalili juu ya ulazima wa kutawadha akitapika mtu, na wala haionyeshi kuwa wudhuu unatenguka kwayo, bali lengo lake ni kusunisha mtu atawadhe anapotapika. Kwani kwa kitendo tu cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hakuonyeshi kuwa ni wajibu.



Pamoja na hayo, si kila chenye kutengua wudhuu kinahesabiwa kuwa ni najsi. Ibnu Hazmi amelikhitari hili, na pia Shaykh wa Uislamu katika
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



007- Nini Hukmu Ya Majimaji Yanayotoka Kwenye

Utupu Wa Mwanamke Au Unyevunyevu Wa Utupu Wake?



Alhidaaya.com









Maulamaa wana mielekeo miwili kuhusu unyevunyevu wa utupu wa mwanamke: [Al-Mughny (2/88), na Al-Majmu'u (1/570)].



Mwelekeo wa kwanza:



Ni najsi, kwa kuwa yako ndani ya utupu, si maji ya uzazi na yanafanana na madhii. Wametolea dalili kwa Hadiyth ya Zayd bin Khaalid kwamba alimuuliza 'Uthmaan bin ‘Affaan (Allaah Amridhie) akisema: "Nieleze, (nini hukmu) mtu anapomwingilia mkewe na wala hakumwaga manii? Akasema 'Uthmaan: "Atatawadha kama anavyotawadha kwa ajili ya Swalaah, na ataiosha dhakari yake". 'Uthmaan akasema: "Nimeyasikia toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)". [Isnadi Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (292), na Muslim (347), lakini imekuwa Mansuwkh]

.

Na Hadiyth ya Ubayy bin Ka-'ab kwamba alisema: "Ee Rasuli wa Allaah! Inakuwa vipi mtu akimwingilia mkewe bila kumwaga? Akasema:



(يغسل ما مس المرأة منه ثم يتوضأ ويصلي)

((Ataiosha sehemu aliyomgusa nayo mwanamke, kisha atatawadha, na ataswali)). [Isnadi Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (293), na Muslim (346), lakini imekuwa Mansuwkh].



Wamesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuamrisha kuiosha sehemu iliyogusana na utupu wa mwanamke, ni dalili juu ya unajsi wa unyevu wa utupu wa mwanamke”.



“Mimi ninapinga (Abuu Maalik) kwa kusema kuwa Hadiyth hizo mbili zimenasikhiwa na Hadiyth nyingine zenye kuamrisha kuoga kama itakavyokuja katika sehemu yake inshaAllaah”. [Angalia kwenye Kitabu cha Fat-hul Baary (1/473)].



Na pia kuna uwezekano wa kuwa amri ya kuosha ni kutokana na madhii yanayomtoka mwanamume au mwanamke.



Vile vile, wametolea ushahidi juu ya unajsi wa (majimaji hayo) kwa kuwa yanatoka katika moja ya njia mbili. Na kaida inasema:

"Chenye kutoka katika njia mbili, basi ni najsi isipokuwa manii".





Mwelekeo wa pili:



Ni kwamba majimaji ya utupu ni twahara. [Angalia kwenye Jaami'i Ahkaamu An-Nasaaiy (1/68) cha Shaykh wetu Mustwafa bin Al-'Adawy Allaah Amhifadhi].



Mwelekeo huu unatolewa dalili kwa haya yafuatayo:



1- Kwamba 'Aaishah - Allaah Amridhie,- alikuwa akiyakwangua manii kutoka katika nguo ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yakiwa yametokana na kukutana kimwili, kwani Rasuli kamwe hakuota kuwa anaingilia. [Hivi ndivyo alivyosema katika Al-Mughny (2/88). Na Shaykh wetu amesema: "Hili linahitajia matni toka katika Qur-aan au Hadiyth, na wala hatukuikuta matni katika mfano wa hili"].

Anapoingilia, hukutana na umajimaji wa utupu. Na kwa vile sisi, lau kama tungelihukumia unajsi wa utupu wa mwanamke, basi tungelihukmu unajsi wa manii yake, kwani manii hayo yanatokea kwenye utupu wake, na kwa hivyo yananajsika kwa unyevunyevu wake.





2- Kwamba majimaji haya ni jambo ambalo liko wazi, nayo huwatoka sana wanawake. Na hakuna shaka kwamba jambo hili lilikuwepo kwa wanawake katika enzi za Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyo kwa wanawake wa zama zetu hizi. Na wala haikupokelewa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaamrisha kuosha, au kutawadha kutokana na hali hiyo.



3- Kwamba sehemu ya kutokea majimaji haya, si sehemu ya kutokea mkojo ambao ni najsi.



4- Kwamba kauli ya Maulamaa isemayo: "Kila chenye kutoka kwenye njia mbili ni najsi isipokuwa manii", si kauli iliyopokelewa toka kwa Rasuli Al Ma’aswuwm (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na wala kauli hii haijafanyiwa Ijma’a ya Ummah. Bali imepokelewa kwamba baadhi ya vinavyotoka kwenye njia mbili havitengui wudhuu, mfano wa damu ya istihaadhwah ambayo tutakuja kuielezea mbeleni.



Ninasema (Abuu Maalik): “Ninaloliona mimi lenye nguvu, ni kwa ufafanuzi huu:

"Ikiwa majimaji haya yanamtoka mwanamke wakati wa kuchezeana na mumewe, au wakati anapokuwa na hamu ya kujamiiana na mfano wa hili hasa, basi hayo ni madhii. Na mimi nimejua kwamba madhii ni najsi ambayo ni lazima ioshwe, na pia inatengua wudhuu.



Ama ikiwa majimaji haya yanatoka kwenye utupu wa mwanamke takriban nyakati zote, na yanazidi wakati wa ujauzito, au wakati anapofanya kazi kwa bidii, au anapotembea mwendo mrefu, basi majimaji hayo ni twahara kiasili kwa kutokuwepo dalili juu ya unajsi wake. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



008-Najsi Zinazosamehewa



Alhidaaya.com





Kuna kauli mbalimbali za Maulamaa kuhusu aina na kiasi cha najsi ambayo inaweza kuingia katika nguo, au mahala, au mwilini na inakuwa ni yenye kusamehewa. Isipokuwa kidhibiti cha najsi zinazosamehewa ni udharura, kuenea kwa wingi, kuwa ni vigumu kujikinga nayo, na kuwepo tabu na uzito mkubwa katika kuiondosha. [Al-Fiqh Al-Islaamiy wa Adillatuhu (169 – 177)].
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



009-Namna Ya Kuzitwaharisha Aina Za Najsi Zilizobainishwa na Hadiyth



Alhidaaya.com







1- Kuitwaharisha nguo yenye damu ya hedhi



Inakuwa ni kwa kuikwangua na kuigandua, kisha kuisugua kwa ncha za vidole ili iachiane na itoke, kisha utaiosha kwa maji. Ni kutokana na Hadiyth ya Asmaa binti Abu Bakr, amesema: "Mwanamke mmoja alikuja kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Mmoja wetu nguo yake ikiingiwa na damu ya hedhi, afanyaje"? Akasema Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):



تحته, ثم تقرصه بالماء ثم تنضحه, ثم تصلي فيه

((Ataipikicha, kisha ataikwangua kwa ncha za vidole na maji, kisha atainyunyizia maji, na halafu ataswalia)).

[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy na Muslim (291)].



Na kwa Hadiyth ya 'Aaishah, amesema: " Mmoja wetu alikuwa akipatwa na hedhi, huikwangua damu kwenye nguo yake wakati anapotwaharika, kisha huiosha, na hunyunyizia maji sehemu iliyobaki, halafu huswali nayo". [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (308), na Ibn Maajah (630)].



Na kama mwanamke atapenda kutumia kijiti au kinginecho ili kuondosha damu, au kuosha nguo kwa maji na sabuni na mfano wake katika madawa ya kusafishia, basi itakuwa ni bora zaidi.



Hii ni kwa Hadiyth ya Ummu Qays binti Muhswan, amesema: "Nilimuuliza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu damu ya hedhi iliyoingia kwenye nguo, naye akasema:



((حكيه بضلع، واغسليه بماء وسدر))



((Ikwangue kwa ujiti, na uioshe kwa maji na mkunazi)). [Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (363), An-Nasaaiy (1/195) na Ibn Maajah (628)].







2- Kuitwaharisha nguo yenye mkojo wa mtoto mchanga

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:



((يغسل من بول الجارية, ويرش من بول الغلام))



((Huoshwa ikiingia mkojo wa mtoto wa kike, na hurashiwa maji ikiingia mkojo wa mtoto wa kiume)). [Hadiyth Swahiyh “Lighayrih”. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (376), An Nasaaiy (1/158), na Ibn Maajah (526). Kuna Hadiyth kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine].







3- Kuitwaharisha nguo yenye madhii



Na kwa vile madhii yanakithiri sana kutoka na kuwa uzito kwa wengi, Allaah Mwekaji wa sharia, Ametuhafifishia namna ya kuyatwaharisha. Inatosha kuinyunyizia nguo maji sehemu iliyoingia madhii kutokana na Hadiyth ya Sahl bin Hunayf kwamba yeye alikuwa akipata tabu na uzito kutokana na madhii. Akamuuliza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Ni vipi kwa yale yanayoingia katika nguo yangu? Akasema:



((يكفيك أن تأخذ كفا من ماء فتنضح به ثوبك حيث ترى أنه قد أصاب منه))



((Inakutosha kuchukua teko la maji, ukanyunyizia kwalo nguo yako pale unapoona yameingia)). [Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (210), At-Tirmidhiy, na Ibn Maajah (506)].





4- Kuitwaharisha ncha ya nguo ya mwanamke (inayoburuzika)



Inaponajsika sehemu ya nguo ya mwanamke inayoburuzika, basi hutwaharika kwa kugusana na ardhi iliyo twahara. Mwanamke mmoja alimuuliza mke wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Ummu Salamah akimwambia: "Mimi ni mwanamke ninayerefusha ncha za nguo yangu na ninatembea sehemu chafu". Ummu Salamah akamwambia: Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:



((يطهره ما بعده))



((Huitwaharisha (ardhi) iliyo baada yake)). ] Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (383), At-Tirmidhiy (143) na Ibn Maajah (531).]







5- Kuitwaharisha soli ya viatu



Imepokelewa na Abuu Sa’iyd Allaah Amridhie kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((اذا جاء أحدكم المسجد فليقلب نعليه ولينظرفيهما، فان رأى خبثا فليمسحه بالأرض، ثم ليصل بهما))



((Anapokuja mmoja wenu Msikitini, basi avipindue viatu vyake na aangalie vina nini. Ikiwa ataona najsi, basi aipanguse kwa ardhi, kisha aswali navyo)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (646)].





6- Kukitwaharisha chombo mbwa akikitia ulimi

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:



((طهور اناء أحدكم اذا ولغ فيه الكلب أن يغسله سبع مرات أولاهن بالتراب))



((Kukitwaharisha chombo cha mmoja wenu mbwa akitia ulimi wake ndani, ni akioshe mara saba, ya kwanza yake kwa udongo)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (279) na Abuu Daawuud (71)].





7- Kuitwaharisha ngozi ya nyamafu

Ni kwa kusafishwa na kukaushwa kwa madawa. Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):



((اذا دبغ الاهاب فقد طهر))

((Ngozi ya nyamafu ikisafishwa na kukaushwa kwa madawa, basi imetwaharika)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim na wengineo].





8- Kuitwaharisha ardhi iliyoingia mkojo na mfano wake



Ni kwa kumiminia maji juu yake kama alivyomrisha ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwagia maji juu ya mkojo wa bedui Msikitini. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (219) na Muslim (283)].



Bila shaka aliamuru hilo kwa ajili ya kuharakia usafi. Na kama si hivyo, lau kama angeliacha mpaka ukakauka na athari ya najsi ikaondoka, basi (ardhi) ingekuwa imetwaharika.







9- Kukitwaharisha kisima au samli inapoingia ndani yake najsi



Ni kwa kuichota na kuiondosha najsi pamoja na sehemu za pambizoni mwake, na iliyosalia inabakia twahara. Ni kwa Hadiyth ya Ibnu ‘Abbaas kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu panya aliyeangukia katika samli akasema:

((ألقوها، وما حولها فاطرحوه، وكلوا سمنكم))

((Mtupeni, na sehemu za pambizoni mwake ziondosheni, na samli yenu itumieni)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (Wanyawa wa kuchinjwa mlango wa 34)].
 
Back
Top Bottom