Kufukiza Ubani Wakati Wa Kuomba Duaa Inafaa?



Alhidaaya.com







SWALI:



Asalam Alaykum,

Kuna uhalali/faida/hasara gani wa kutumia ubani kuweka kwenye moto wakati wa kuomba duah au kurehemu ndugu zetu waliotutangulia katika haki?

Wabillah tawfiq



JIBU:





AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.





Kufukiza ubani katika moto wakati wa kusoma du’aa haina uhalali wala faida yoyote. Na hii imekuwa ni ada ya baadhi ya ndugu zetu hasa wanaosoma Maulidi na Khitmah kwa kuamini kuwa du'aa inapanda juu na moshi wake. Yote haya ni mambo ya kijahili yasiyokubalika katika Shariy’ah ya Kiislamu.





Inayopatikana ni hasara kubwa kwani ni kwenda kinyume na Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).



Chetezo cha moto wakati wa ‘aibadah na du’aa imechukuliwa kutoka kwa Mafursi (Iran) ambao walikuwa wanaabudu jua na moto. Walipoingia katika Uislamu waliingia na baadhi ya desturi zao mbaya zinazokwenda kinyume na Uislamu. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametusisitiza sana tusifuate ada na desturi za makafiri au kujifananisha nao kwani tutakuwa sawa na wao kama alivyosema:

((مَنْ تَشَبَّهَ بِقَوْمٍ فَهُوَ مِنْهُمْ))

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Atakayejifananisha na watu basi yeye ni miongoni mwao". [Abuu Daawuwd na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Abiy Daawuwd (3401)]





Leo pia utakuta wanawake Waislamu wanaoishi India wanavaa sare kama Mabaniyani huku matumbo yao yapo wazi kabisa jambo ambalo linakataliwa na kwenda kinyume na Dini hii ya Kiislamu. Au vijana wa kiume kusuka nywele, kuvaa hereni, mikufu au kuchonga nyusi kwa kuwaiga makafiri wanamuziki na wachezaji mipira, na vijana wa kike kuvaa masuruali kama wanaume n.k.





Na Allaah Anajua zaidi
 
Kufupisha Thanaa (Kumtukuza Allaah) Na Kumswalia

Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم), Maamkizi Ya Kiislaam



Alhidaaya.com



SWALI:



Asalaam alaykum,kwanza poleni kwa shughuli nzito za kuisaidia dini kwa hali na mali ALLAAH atawalipa. Nilikua nauliza kuhusu haya masuala ya mfano mtu akiandika kitabu au msg nk.mfano anaandika Allaah s.w badala ya Allaah subhanahu wataala au anaandika Rasul S.A.W badala ya Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam na kadhalika. Sasa nilikua nataka fatwa kama haifai kuandika kwa ufupi basi nlikua naomba dalili na hoja na kama inafaa pia unipe dalili.kwa haya nawatakia kila la kheri.





JIBU:



AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho





Haifai kabisa kufupisha thanaa kwa maana kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kuandika (s.w.t). Au kufupisha Jalla Jalaahu kwa kuandika (J.J). Vile vile haifai kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuandika (s.a.w) au (s).





Pia, haifai hata kufupisha katika kuwataja Swahaba ‘Radhwiya Allaahu ‘anhu’ (Radhi za Allaah ziwe juu yake) kwa kuandika (R.A.) badala yake.





Hali kadhalika kuongeza neno 'Ta'aalaa' kwenye Salaam kwa kusema 'Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaahi Ta'aalaa wa Barakaatuh', si jambo tulilofundishwa katika Salaam na hivyo ni bora mtu kuliepuka katika Salaam.





Wengine huona tabu kuandika kirefu na hivyo hufupisha maamkizi haya katika mawasiliano ya barua, maandikiano ya simu za mkononi (text messages) ambayo ndio yameenea sana katika zama zetu hizi, barua pepe (e-mail) kwa kuandika ima A.A, au A.A.W, au A.A.W.W.B. Wamekosa kutambua kwamba wanakosa fadhila kubwa za kuamkiana kikamilifu, jambo ambalo halimchukui mtu hata dakika moja kuandika kirefu 'Assalaamu 'Alaykum' au Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh'.





Kufupisha thanaa kwa Allaah au kumswalia Nabiy ni dalili ya kutokuonyesha heshima mbele ya Allaah na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Dalili ya mapenzi kwao ni mtu kutokudharau au kutokuona uvivu kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) au kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ikiwa kwa kutamka au kuandika.





Watu wengine huwa wanafanya hivyo na wakijulishwa kutokufaa kufanya hivyo, hutoa hoja kuwa makatazo ni katika matamshi na si katika maandishi! Na hoja nyingine ni kuwa vitabu vingi vya 'ulamaa kumeandikwa kwa ufupi kumswalia Nabiy kama hivi (ص) Lakini watu hao ima kwa kutokuwa na maarifa ya kutosha na Taariykh na kutazama nyakati za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba ikiwa waliwahi kutumia njia hizo katika maandishi au la, wao hujikuta wanafanya kwa mazoea na kuiga! Tunajua sote kuwa Nabiy alishawahi kutuma barua kadhaa kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi na wafalme, na pia Swahaba kama Makhalifa walikuwa wakiwaandikia Ma-Gavana na wateule wao katika majimbo mbalimbali na hakuna popote pale utaona walikuwa wakifupisha Salaam au kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).





Ama suala la Mashaykh kuchapisha au kuchapishiwa vitabu vyao kwa kufupishwa hivyo na mashirika ya uchapishaji, haina maana kuwa ni sahihi wao kufanya hivyo. Ima hawajalipitia vyema na kulitafiti suala hilo, au hazijawafikia hoja kuhusiana na kutokufaa kufanya hivyo. Kwa hiyo kufanya kwao hivyo sio hoja ya kufaa jambo hilo.





Itambulikane kwamba maamkizi ya Kiislamu ni ‘Ibaadah kwani ni maamrisho kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama Anavyosema:



يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ بُيُوتِكُمْ حَتَّىٰ تَسْتَأْنِسُوا وَتُسَلِّمُوا عَلَىٰ أَهْلِهَا ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿٢٧﴾

Enyi walioamini! Msiingie nyumba zisizokuwa nyumba zenu mpaka muombe ruhusa na muwatolee salamu wenyewe. Hivyo ni bora kwenu ili mpate kukumbuka. [An-Nuwr: 27]





Pia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipohamia Madiynah, mafunzo ya maamkizi ya Salaam yalikuwa ni katika mafunzo ya mwanzo kabisa kuwapa Swahaba alipoyatoa katika khutbah zake za mwanzo huko. Mafunzo haya pia yanabainisha kuwa kuamkia kwa maamkizi ya Kiislamu ni jambo litakalomuingiza Muislamu katika makaazi ya Pepo:

((ايها الناس ،أفشوا السلام، وأطعموا الطعام، وصلّوا بالليل والناس نيام تدخلوا الجنة بسلام)) رواه الترمذي، حديث صحيح

"Enyi watu, toeni (amkianeni kwa) salaam, na lisheni chakula, na Swalini watu wakiwa wamelala (Tahajjud), mtaingia Peponi kwa amani." [At-Tirmidhiy – Hadiyth Swahiyh]





Na Salaam hizo ili mtu apate daraja kubwa na ukamilifu wa thawabu, ni sharti iwe imetimia kwa ukamilifu wake kama ilivyofundishwa katika Hadiyth ifuatayo:

عن عمران بن حصين رضي الله عنهما قال :جاء رجل الى النبي صلى الله عليه وسلم فقال :"السلام عليكم" فرد عليه السلام ثم جلس فقال النبي صلى الله عليه وسلم: ((عشر)) ثم جاء رجل اخر فقال: "السلام عليكم ورحمة الله" فرد عليه فجلس فقال: ((عشرون)) ثم جاء رجل اخر فقال: "السلام عليكم ورحمة الله وبركاته" فرد عليه فقال ((ثلاثون)) رواه ابو داود والترمذي و قال حديث حسن

'Imraan bin Huswayn (Radhwiya Allaahu 'anhuma) amesimulia: "Mtu mmoja alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuamkia: "Assalaamu 'Alaykum" (Nabiy) akamrudishia (Salaam) kisha yule mtu akaketi. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Kumi)) [Kwa maana amepata thawabu kumi]. Kisha akaja mtu mwengine, akasema: "Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaah" Naye akamrudishia, kisha yule mtu akaketi, Nabiy akasema: ((Ishirini)). Kisha akaja mtu mwingine akasema: "Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh". Naye akamrudishia kisha akasema ((Thelathini)) [Imesimuliwa na Abuu Daawuud na At-Trimidhiy na akasema Hadiyth Hasan]





Ama kuhusu Fatwa za Wanavyuoni zipo nyingi na miongoni mwazo ni kama zifuatazo:





Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin Baaz (Rahimahu Allaah):



Kama ilivyoamrishwa kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye Swalaah katika Tashahhud, na imeamrishwa katika kutoa khutbah, kuomba Du’aa na kuomba maghfira, baada ya Adhaan, wakati wa kuingia na kutoka Msikitini, na wakati wa kumtaja katika hali nyinginezo, hivyo basi ni muhimu zaidi kufanya hivyo katika kumtaja jina lake katika kitabu, barua, makala n.k. Hivyo basi imeamrishwa kuandika Swalah na Salaam kwa ukamilifu ili kutimiza amri ya Allaah Aliyotuamrisha na ili msomaji apate kukumbuka kutaja kumswalia Nabiy anapoisoma. Hivyo tusiandike Swalah na Salaam kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kifupi kama kuandika (S) au (S.A.W.) n.k. au mfumo wowote ambao watu wanatumia kwa sababu inakwenda kinyume na maamrisho ya Allaah na Kitabu Chake Anaposema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾

Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini mswalieni na msalimieni kwa mamkizi ya amani na kwa tasliymaa. [Al-Ahzaab: 56]





Kamati Kuu Ya Kudumu Ya Kutoa Fatwa Saudi Arabia ikiongozwa na Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Baaz:



Wametoa fatwa ifuatayo watu walipoulizwa kuhusu kufupisha kumswalia Nabiy(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Sunnah ni kuandika ibara kikamilifu (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kwani hivyo ni kama du’aa, na du’aa ni ‘Ibaadah (ikiwa kuandika) kama ilivyo katika kutamka. Hivyo kufupisha kutumia herufi (Swaad ص) au herufi kama (Swaad-Laam-‘Ayn-Miym) sio du’aa wala ibada ikiwa imetajwa katika kutamka au maandishi. Kwa sababu kufupisha huko hakukutumiliwa na karne tatu za mwanzo ambazo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amezishuhudia ubora wake.”

[Fataawaa Al-Lajnat Ad-Daa'imah #18770 (12/208-209)]





Al-Fayruuz ‘Abaadiy:



"Haipasi kutumia alama au vifupisho kuhusiana na Salaam kwa wanavyofanya baadhi ya wavivu na watu wajinga na pia baadhi ya wanafunzi wa elimu wanaoandika ‘Swaad-Laam-‘Ayn-Miym’ badala ya ‘Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam." [Katika Kitabu chake Asw-Swalaatu wal-Bushr, kama iliyvonukuliwa katika Mu'jam Al-Manaahiy Al-Lafdhwiyyah (Uk .351)





Ahmad Shaakir:



"Ni mila za upumbavu za karne za sasa kwamba watu wanafupisha kuandika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam". Ufafanuzi [Musnad Imaam Ahmad (#5088, 9/105)]





WasiyuLLaah Al-'Abbaas:



Hairuhusiwi kufupisha Salaam kwa ujumla katika maandishi kama ilivokuwa hairuhusiwi kufupisha Swalah na Salaam kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa wa sallam). [Jibu aliloandika Shaykh kwa mkono, Faili Namba: AAWA004, tarehe 24.06.1423]





Kadhalika si watu wote wanaoelewa vifupisho hivyo, na unapoandika hivyo utakuwa unamchanganya na kumshughulisha mtu yule kwa mambo kama hayo. Leo hii tunaona watu wengi wakisoma vitabu vya Kiswahili na hata tafsiri za Qur-aan za Kiswahili vilivyofupishwa sifa hizo, huwa wanazisoma hivyo hivyo kwa ufupi kama zilivyoandikwa! Mtu anapokutana na jina la Allaah na kusema ‘es dabliuu ti’ kwa sababu kumeandikwa kwenye kitabu (s.w.t.), au anaposoma jina la Nabiy na kisha anasema ‘es ei dabliuu’ kwa sababu kumeandikwa (s.a.w.) kwenye vitabu hivyo!! Hivyo ni uvurugaji na pia kumkosea Allaah na Nabiy Wake kwa kuwapa sifa za ajabu zisizowahusu, na makosa hayo huwarejea wale walioandika kuliko yule mwenye kusoma kwa kutokujua!



Hivyo basi haifai kufupisha kwani ni kujikosesha thawabu na fadhila zinazopatikana katika kutaja thanaa za Allaah na kumswalia Nabiy na pia kutoa Salaam kwa ukamilifu, na pia ikiwa mtu atafikiwa na ufafanuzi huu na akaendelea kuifanya hayo, basi ni alama ya kiburi na huenda asikose tu thawabu za kuandika, bali huenda akapata na dhambi za kuifanyia haki kiburi na ujeuri.





Na Allaah Anajua zaidi
 
Kufupisha Thanaa: Ufafanuzi Wa Kiburi Na Mas-ala Ya

Bid’ah Katika Jibu La “Hukmu Ya Kufupisha Thanaa”



Alhidaaya.com





SWALI:



Baada ya kusoma jibu katika kiungo kifuatacho:



Hukmu Ya Kufupisha Kumtukuza Allaah Na Kumswalia Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam Na Maamkizi Ya Kiislam



Nakubaliana ni vizuri kuandika kirefu. Ispokuwa Rasul hakukataza wala hakusherehesha kuhusu kufupisha ila kwenye salaam nayo wapata thawabu hata kidogo. Lakini nanukuu kipande cha mwisho cha fatwa hiyo:



"Hivyo basi haifai kufupisha kwani ni kujikosesha thawabu na fadhila zinazopatikana katika kumtukuza na kumhimidi Allaah na kumswalia Mtume na pia kutoa Salaam kwa ukamilifu, na pia ikiwa mtu atafikiwa na ufafanuzi huu na akaendelea kuifanya hayo, basi ni alama ya kiburi na huenda asikose tu thawabu za kuandika, bali huenda akapata na dhambi za kufanyia kiburi haki".



Nakbaliana na karibu na maelezo yote na ushahidi uliotolewa. Lakini ushahidi uliotolewa kwa hadith wote umetolewa kuhusu hukumu ya salaam. Fatwa zilizotolwa ni kuhusu Nabiy Swalla Allaahu 'alaiyhi wa salaam hakulifanya. Je mangapi mtume hakuyafanya na halali kuyafanya sasa. Mfano, Sasa tuko kwenye karne ya 21 mambo mengi hayakuwapo wakati wa Rasul Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam mfano mdogo vipando. Wakati ule walikuwa wakipanda Ngamia na farasi huchukua muda mrefu na sasa twatumia Ndege nayo watu hutumia muda mfupi. Hata vita ya sasa haipiganwi na mapanga tena yapiganwah na mabomu kutumia satalite. Na mengi mengineyo yote haya twakubali ni Elmu aliyotupa Allaahu Subhaanahu wa Ta'aalaa na ni halali kuyatumia. Sasa wasiwasi wangu ni huu wa fatwa hii ya kumtia mtu Alama ya Kibri Imetoka Wapi Kama Ilivyo Katika maneno hayo hapa juu "na pia ikiwa mtu atafikiwa na ufafanuzi huu na akaendelea kuifanya hayo, basi ni alama ya kiburi"




Nakumbusha kuwa si pingi hiyo Fatwa ninacho kuwa na wasiwasi nacho nihukmu ya kupewa mtu kuwa na Kibri. Ikiwa hilo jambo limepitishwa (fatwa) na viongozi waliopo sasa je wakipita hao wakija wengine wakisema yafaa itakuwaje.Tukumbuke mwenye sifa hiyo ni Allaahu Subhaanahu wa Ta'aalaa Peke Yake.





Wabillahi Tawfiq.




JIBU:



AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho



Tuanze kwanza kukujibu kuhusu suala la kiburi katika majibu tuliyoyaweka.





Baada ya kubainika kwa hoja zilizotolewa kwenye majibu hayo ya 'ulamaa ambao wamechambua mas-ala kwa hoja zenye kufahamika na zenye egemezo na Sunnah, kisha mtu akayasoma na kuendelea kufanya kinyume, basi hiyo ni dalili ya kiburi, kwani kiburi ndugu yetu ni kukataa haki. Na haki ni kuwa tayari yashatolewa maelezo kuhusu ubaya wa kumkatia Allaah na Nabiy Wake heshima zao na utukufu wao na hali wewe ni Muislamu ambaye unadai unawapenda na kuwaheshimu. Bila shaka si heshima kumkatia Rabb wako au Nabiy wako hadhi zao wanazostahiki na kufanya hivyo baada ya kukumbushwa, basi itakuwa ni alama ya kiburi ila kwa yule aliyesahau ambaye atasamehewa na shari'ah.



Na kusema kiburi ni nafuu kuliko kumwambia mtu kuwa: 'Wewe unamchukia Allaah au unamchukia Mtume kwa sababu unawavunjia heshima'! Au kumtuhumu mtu kuwa hampendi Allaah au Nabiy kwa kuwakatakata hivyo! Au kumwambia mtu: “Hakika wewe una dharau kwa Rabb wako na Nabiy Wako!” Na yote hayo yanaweza kusemwa na watu lakini sisi tumechagua neno muwafaqah ambalo tunahisi ni mahali pake na wala hatujahalalisha haramu hapo au kuharamisha halali kama ulivyofahamu wewe katika maelezo yako.



Na vizuri ufahamu kuwa hatujamtia mtu alama ya kiburi bali tumesema ikiwa mtu ataendelea kufanya hayo kinyume kwa kumkata heshima Allaah na Nabiy Wake na baada ya kubainishiwa madhara na kukosa fadhila kwa kufanya hivyo, basi itakuwa ni alama ya kiburi; yaani kwa kukataa kwake haki. Na hakuna asiyefahamu au asiyekubali kuwa katika hayo mawili ya kufupisha na kukata na kurefusha heshima hizo, kuwa ya pili ya kurefusha ni bora na yenye thawabu. Sasa kwa mwenye akili, atawezaje kuliacha lililo bora na thawabu na kulifuata lisilo bora wala lenye thawabu?

أَتَسْتَبْدِلُونَ الَّذِي هُوَ أَدْنَىٰ بِالَّذِي هُوَ خَيْرٌ ۚ

... Kubadilisha yaliyo duni kwa yaliyo bora? [Al-Baqarah: 61]







Ama kuhusu nukta yako nyigine ya pili, tunatakiwa tufahamu nini maana sahihi ya bid'ah kwanza na ndio utata ulionao utaweza kuondoka:



Bid'ah katika istilahi ya kisheria ina maana njia iliyoanzishwa katika dini, inayoshabihiana na ile njia ya kisheria (lakini kwa hakika si hivyo, yaani inakwenda kinyume na sheria), hivyo wanazua bid'ah kwa kusudi ya kuwa na ada ya kujikurubisha kwa Allaah Aliyetukuka (hii ni kuwa haiwatoshelezi yale yaliyokuja katika sheria na hivyo wanataka kuongeza juu yake kama kwamba wanakamilisha yaliyopungua)”. [Imaam Abu Ishaaq ash-Shaatwiby, al-I’tiswaam, Mj.1, uk. 37]



Naye Shaykh Abdulla Saleh Farsy amesema, “Bidaa iliyokusudiwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kukatazwa ni kutiwa katika Dini – na kuitakidiwa kuwa ni Ibada jambo ambalo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakusema litiwe katika Dini wala hakulifanya, na hali ya kuwa anao uweza wa kulifanya”. [Bid-a, Dibaji].



Imaam Maalik amesema: “Yeyote atakayeanzisha katika Uislamu bid'ah akiona kuwa ni nzuri amedai ya kuwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amefanya khiyana katika kufikisha risala, kwani Allaah Amesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu. [Al-Maaidah:3]





Na kwa yule ambaye hakuwa na dini siku hiyo basi hatakuwa na dini leo” [al-I’tiswaam, Mj.1, uk. 49 ya Imaam ash-Shaatwiby]




Imaam Ahmad amesema: “Misingi ya Sunnah kwetu sisi ni kushikamana na yale waliyokuwa nayo Swahaba wa Nabiy, kuwafuata na kuacha bid'ah kwani kila bid'ah ni upotevu” [Ibn Ya’la al-Fara’, Twabaqaatul Hanaabilah, Mj. 1, uk.241]



Ibn Rajab naye anasema: “Maana ya bid'ah ni yale yaliyoanzishwa ambayo hayana asili katika sheria yenye kuwafikiana nayo, na ama yale ambayo yana asili katika sheria basi sio bid'ah, japokuwa ni bid'ah kilugha (kumaanisha kuwa kwa matumizi ya lugha ya Kiarabu inafahamika hivyo lakini kisheria inakuwa ni kinyume na hayo matumizi ya kilugha)” [Jaamiul ‘Uluum wal hikam, uk. 233]



Katika maelezo hayo yameweka mipaka ya kwamba bid'ah sehemu yake ni katika dini na wala si katika mambo ya kidunia, na hiyo ni kuwa "ni njia iliyoanzishwa". Na dalili katika hili ni kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):





"Mwenye kuzua katika dini yetu hii lisilokuwamo humo litakataliwa" [Al Bukhaariy na Muslim]





Na katika baadhi ya riwaya nyengine:





"Yeyote atakayezua katika hili jambo letu – na makusudio pia (jambo letu la dini) lisilokuwamo humo, litakataliwa". [Al Bukhaariy, Muslim, Abu Dawuud na Ibn Maajah] Yaani itakataliwa kutoka kwa mwenye kufanya kama zinavyorudishwa hela mbaya kwa mwenyewe.



Hivyo bid’ah haiwi isipokuwa katika dini. Na hapa wengi tunakosea kwa kudhania ya kwamba bid’ah inaingia katika mambo ya ada. Vitu vya kawaida haviingii katika bid'ah. Haiyumkiniki kusemwa kuwa: jambo hili katika mambo ya kimaisha ni bid'ah kwa sababu ma-Salaf miongoni mwa Swahaba na Tabiina hawakufanya. Inawezekana kuwa ni jambo jipya lakini haichukuliwi kuwa ni bid'ah kisheria na kama si hivyo basi tungechukua mengi ambayo tuko nayo leo kuwa ni bid’ah: kama hivi vipaza sauti, mazulia (carpets), hii meza, na hivi viti ambavyo tunakalia, vyote havikuwepo kwa wale Waislamu wa mwanzo na havikufanywa na Maswahaba. Je, hizi zinachukuliwa kuwa bid'ah?





Na hivyo hukosea wengi katika watu katika jambo hili mpaka wanapoona, kwa sikitiko, minbar yenye zaidi ya vidaraja vitatu wanasema: ‘Hii ni bid’ah’. Hapana! haiingii bid'ah katika jambo hili. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akihutubu mwanzoni juu ya kigogo cha mtende lakini watu walipokuwa wengi aliambiwa, “Je, hatukufanyii kitu ambacho utasimama kwayo mpaka watu wakuone?” Wakaja na fundi seremala ambaye alikuwa Mrumi na kumtengezea minbar yenye vidaraja vitatu na lau jambo hili lingehitajia zaidi ya vidaraja vitatu wangefanya. Mambo haya hayaingii katika bid'ah. Na hizi ni katika ada ambazo kwamba zinatofautiana kwa kutofautiana kwa watu, mazingira na hali. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akila kufuatia ada za kaumu yake na hasa yenye kuafikiana na maumbile yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), maumbile ya usahali (wepesi), unyenyekevu na kujinyima. Hivyo haichukuliwi kuwa kula juu ya meza au kula kwa kijiko kuwa ni bid'ah katika dini.



Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho na usome ‘Hoja Ya Tisa Ya Watetezi Wa Maulidi’ ambayo imefafanuliwa zaidi kuhusu mas-ala haya na hasa uliyoyataja ya kuwa Nabiy (Swalla-Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipanda ngamia sasa vipi sisi tupande gari, ndege n.k.





Hoja Za Wanaosherehekea Mawlid Na Majibu Yake



Tunadhani tutakuwa tumefafanua kiasi cha kufahamika vizuri inshaAllaah





Na Allaah Anajua zaidi
 
Mawaidha: Umuhimu wa Kuwa na Tabia Njema

Tabia njema ni hazina isiyochakaa. Mtu mwenye tabia nzuri hupendwa na watu, huheshimiwa, na huacha alama njema kila mahali anapopita. Haijalishi elimu, mali au cheo, bila tabia njema, vyote havina thamani ya kweli.

Kwa nini tabia njema ni muhimu:
1. Huleta heshima – Watu huthamini na kuamini mtu mwema.
2. Huonyesha maadili ya familia na imani yako.
3. Hujenga mahusiano mazuri kazini, shuleni, na jamii kwa ujumla.
4. Huleta baraka – Mwenyezi Mungu hupenda wenye tabia njema.
5. Huleta amani ya ndani – Mtu mwema hulala kwa utulivu bila kujilaumu.

Mifano ya tabia njema:
  • Kusema ukweli
  • Kusaidia wengine
  • Kuvumilia na kusamehe
  • Kuwa na adabu kwa wakubwa na wadogo
  • Kujizuia na hasira au maneno mabaya

Hitimisho:
Tabia njema si udhaifu, ni nguvu ya kweli. Mtu anaweza kusahau sura yako, lakini hatasahau jinsi ulivyomtendea.
 
Maswali: Bid'ah - Uzushi


Kuhudhuria Mwaliko Unaochanganyika Mazuri, Maovu na Bid-ah Inafaa?



Alhidaaya.com





SWALI:



Assalaam ‘Alaykum Warahmatullah.



Naumba kuuliza suala ambalo linanitatiza siku nyingi bila ya kupata ufumbuzi. Jee mfano umepata mualiko siku mbili, moja inafanywa vizuri na siku ya pili huchanganya na yasiokuwemo. Jee nini wajibu wetu kwa sisi waalikwa?



Mara nyengine hutokea haya ndani ya familia, maziko yetu, harusi zetu zote huwa na mitazamo kama hii ya kuchanganya mambo, hivyo nini haki zetu juu ya kushiriki jambo hili?





Jazaka Allah Khayra





JIBU:



AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho





Hakika hili ni tatizo kubwa ambalo linatukabili katika jamii yetu kuchanganya yaliyo mazuri na mabaya. Inastaajabisha unapoona leo kunafanywa mambo yanayolingana na Sharia na siku ifuatayo hata utashangaa huku unauliza je, hawa ni wale wale au ni wengine?





Mwanzo katika hayo ikiwa wewe ni jamaa na wale wanaofanya harusi au matanga uwe ni mwenye kuwaelezea namna nzuri ya kutekeleza hayo katika Dini yetu. Kufuata kwao au kutofuata ni juu yao lakini wewe jitoe katika dhimma hiyo ya kueleza na kuwanasihi. Ikiwa watasikiliza itakuwa kheri na ikiwa hawakuchukua nasaha basi dhambi ni kwao.





Unalopaswa kufanya ni kuwa ikiwa harusi au mwaliko mwengine wowote kwa shughuli unakwenda sambamba na Uislamu utakwenda kuitikia mwaliko huo lakini ikiwa siku ya pili watafanya yao ya upuuzi na kinyume cha Dini utawaelezea tena na hutakwenda katika mwaliko huo. Hii ni kwa mujibu wa Aayah inayosema:

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚوَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٢﴾

Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. Na Mcheni Allaah; hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu. [Al-Maaidah: 2].



Kwa maelezo zaidi ingia katika kiungo kifuatacho:



Kuchangia Na Kushiriki Shughuli Za Bid-ah Ni Dhambi?





Na Allaah Anajua zaidi
 
Kujengea Kaburi Inajuzu?



Alhidaaya.com





SWALI:



Ahsante Kwa Nasaha Za Wiki Lakini Nina Swali



Je Kaburi Lina Faa Kujengewa Kama Ipo Dalili Yeyote Naomba Mnijuze Ahsante





JIBU:



AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho





Haifai kujengea kaburi kwa dalili ya Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

نْ جَابِرٍ (رضي الله عنه) قَالَ: نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ يُجَصَّصَ الْقَبْرُ وَأَنْ يُقْعَدَ عَلَيْهِ وَأَنْ يُبْنَى عَلَيْهِ. مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kaburi kutiwa chokaa (liwe imara), kuketiwa juu yake na kujengewa. [Muslim]





Bonyeza viungo vifuatavyo upate faida zaidi:



129 - Hadiyth Ya 129: Haifai Kutia Chokaa Makaburi Au Kujengea Au Kukalia

Kujengea Makaburi



Na Allaah Anajua zaidi
 
Kumbukumbu Ya Kifo (Death Anniversary) Nini Hukmu Yake?



Alhidaaya.com







SWALI:





Assalam alaikum warahmatullahi wabarakatuh



Shukrani sana kwa kazi mnayo ifanya kwakutuelimisha, Allah Awajaze kheri (Allahumma Amin)



swali langu, ni kwamba, nilifiliwa na baba yangu, nikasema(moyoni bila kutamka kwa watu) kuwa nikiwa bado hai na ikafikia ile tariki aliyofia baba yangu, (yani kila mwaka), nitakuwa nikifunga siku 3(yani siku ya kabla, na siku ile aliyozikwa, na siku ya baada yake)mfano, kafariki tarehe 28(kwahio nitafunga toka tarehe 27,28 na 29)ili iwe ni siku maalum zakumuombea dua .



Nilifaanikiwa kufanya hivyo mara chache, ila badae sikurudi kutekeleza hayo kwakuwa, kuna mara ilikuwa inafkia sina udhu(niko katika HEDHI),hadi ikafkia nikaacha kabisa kufanya hivyo. sasa naulizia, je hiyo ni nadhiri? na kama sikuitekeleza kama nilivyosema je napata dhambi?



Naombeni jibu kwa swali hilo -haya kila lakheri na watakieni





JIBU:





AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.





Kwanza ni dhambi katika Uislamu kuweka kumbukumbu ya kifo inayojulikana kama ni ‘death anniversary’. Hili ni jambo la kuiga makafiri ambalo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekemea. Kwa hiyo kulitenda ni miongoni mwa madhambi makubwa unapaswa ujiepushe nalo kabisa.





Shariy’ah ya Kiislamu kuhusu mtu anapoweka nadhiri kwa ajili ya jambo lisilofaa basi anatakiwa asitekeleze hiyo nadhiri bali ajiepushe na hilo jambo. Dalili ni Hadiyth ifuatayo ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):



عَنْ أبي طريفٍ عَدِيَّ بْنَ حَاتِمٍ الطَّائي (رضي الله عنه) قال: سَمِعْتُ رسول اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم) يَقُولُ: ((مَنْ حَلَفَ عَلَى يَمِينٍ ثُمَّ رَأَى أَتْقَى لِلَّهِ مِنْهَا فَلْيَأْتِ التَّقْوَى)) رواه مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abu Twariyf ‘Adiyy bin Haatim (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nimesikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

((Atakayeapa yamini [kufanya jambo] kisha akaona linalomridhisha zaidi Allaah kuliko aliloliapia, basi amche Allaah kwa kufanya linalomridhisha Allaah)) [Muslim]





Kwa hiyo ukipenda kumfanyia wema mzazi wako aliyefariki unaweza kumfanyia mambo yaliyothibiti kutendwa. Nayo yanapatikana pamoja na dalili zake katika viungo vifuatavyo:





Bonyeza kiungo kifuatacho kwa faida zaidi:



‘Amali Za Kuwatendea Wazazi Waliofariki Waendelee Kupokea Thawabu





Hayo ndiyo pekee yatakayomfaa mzazi aliyefariki. Ama mengineyo yanayotendwa katika jamii kama khitmah, matanga na arubaini ya kifo, yote haya hayakuthibiti kwa hiyo kutekelezwa kwake hayamnufaishi lolote maiti bali mtendaji anaingia katika dhambi na khasara ya kupoteza mali na wakati wake kwa amali isiyokuwa na thamani yoyote mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama alivyosimulia Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa):

من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد البخاري

Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika Dini yetu) basi kitarudishwa [Al-Bukhaariy]



Na Allaah Anajua zaidi
 
Kumsomea Khitmah Maiti, Kumchinjia Na Kumuombea Duaa Kwa Pamoja



Alhidaaya.com





SWALI:



Assalaam alaykum.



Naomba kuuliza:



1. Ikiwa hairuhusiwi kumfanyia khitima aliyefariki, je, inaruhusiwa kuchinja mnyama au kutoa sadaka kwa ajili ya kumuombea dua aliyefariki? Yaani nikakusudia mathalani kufanya sadaka ya chakula/ kichinjo kwa makusudio kuwa thawabu za sadaka hiyo iwe ni dua kwa aliyefariki.

2. Ikiwa sadaka hiyo inruhusiwa, je ni sahihi kuwakusanya waislamu kwa ajili ya dua na sadaka hiyo?



Naomba mjibu In shaa Allaah niweze kuelimika.



Wabillah Tawfiq.





JIBU:


AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho





Kwa ujumla, ikiwa mtu anataka kumfanyia mzazi wake aliyekwishafariki vitendo ambavyo vitamfikia thawabu zake, ni lazima atende vitendo ambavyo vimepatikana dalili zake katika Sunnah. Kufanya kinyume na hivyo ni kupoteza mtu muda wake, mali yake kwa jambo ambalo halina thamani mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

(( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

"Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika dini yetu) basi kitarudishwa". [Al-Bukhaariy]





Shaykh Al-Fawzaan alipoulizwa kuhusu vitendo gani vyema ambavyo aliye hai anaweza kumfanyia maiti alijibu:



"Maiti anaweza kunufaika kwa vitendo vya walio hai ambavyo vinatokana na dalili sahihi inayodhihirisha kuruhusiwa kama; kumuombea du'aa, kumuombea maghfira, kumfanyia sadaka, kumfanyia Hajj na 'Umrah, kumlipia madeni yake na kumtekelezea mirathi yake ya Kiislam. Vitendo vyote hivyo vimethibiti kisheria. Na baadhi ya Maulamaa wameunganisha na hayo pia vitendo vyote vengine vya ibada ambavyo Muislamu hutenda kwa ajili ya Muislamu mwengine ambaye yu hai au amefariki. Lakini, iliyo sahihi ni kujiweka katika mipaka ya yale yaliyoruhusiwa yakiwa na dalili sahihi, kwani hivyo itakuwa ni kutokana na maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaposema:

وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ ﴿٣٩﴾

Na kwamba insani hatopata (jazaa) isipokuwa yale aliyoyafanyia juhudi. [An-Najm: 39]





[Shaykh ibn Fawzaan - Al-Muntwaqaa min Fataawa Shaykh ibn Fawzaan – Mjalada 2, Uk. 161, Fatwa Namba 139]





Mas-alah Ya Kuchinja



Kwa vile haikupatikana dalili kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja kwa ajili ya maiti yeyote kwa nia ya kumfikia thawabu, hivyo kitendo hicho hakipasi kumtendea maiti.





Mas-alah Ya Kuomba Du'aa Pamoja



Aghlabu ya watu hukusanyika katika shughuli kama hizo na nyinginezo na huomba du'aa kwa sauti pamoja, jambo ambalo halikupatikana dalili katika mafunzo ya dini yetu.





Muislamu anaweza kumuombea du'aa mzazi wake akiwa pekee na hii ni dalili kutoka katika Hadiyth ifuatayo:



((إذا مات ابن آدم انقطع عمله إلا من ثلاث: صدقة جارية، أو علم ينتفع به، أو ولد صالح يدعو له)) رواه النسائي و الترمذي

"Anapokufa binaadamu hukatika vitendo vyake (vyema) isipokuwa (vitendo) vitatu; sadaka inayoendelea, elimu inayoendelea kunufaisha au mtoto mwema anayemuombea." [An-Nasaaiy na At-Trimidhiy]



Hii kwa maana amuombee yeye mwenyewe peke yake na sio kujumuisha watu kumuombea kwani Hadiyth iko wazi kuwa ni 'mtoto mwema anayemuombea'.





Kuhusu Khitmah



Nalo ni jambo lisilokuwa na dalili katika mafunzo ya dini yetu, kwani hakuwahi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumsomea khitma mtu yeyote katika maisha yake. Watoto wake na Swahaba walifariki katika uhai wake na hakuna hata masimulizi yoyote yale kuwa alikusanya watu kuwasomea Khitma; alifiwa na wanawe, ‘ami zake, baba, mama na hata marafiki zake Swahaba, lakini hakuwahi kuwafanyia Khitmah. Pia alipofariki yeye, wapenzi wake kama kina Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan na hata binamu yake ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhum), hawakuwahi kumfanyia jambo kama hilo au hata lenye kufanana na hilo! Nao walikuwa wanampenda sana na pia kuwa na uchungu naye kuliko sisi. Hivyo kutenda ibada hiyo ni kuzusha katika dini jambo ambalo amelikemea sana Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwani alikuwa akitanguliza maonyo katika khutba zake:



(( إن خير الكلام كلام الله وخير الهدي هدي محمد صلى الله علي وسلم وشر الأمور محدثاتها وكل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة وكل ضلالة في النار)) أخرجه مسلم في صحيحه

"Maneno bora ni Kitabu cha Allaah (Qur-aan) na uongofu mbora kabisa ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na jambo la shari kabisa ni uzushi, na kila jambo jipya (katika dini) ni bid'ah (uzushi) na kila bid'ah ni motoni)". [Muslim katika swahiyh yake





Bonyeza hapa usome kuhusu mas-alah ya Khitmah na hukmu yake:





KHITMAH: Kutokufaa Na Madhara Yake







Na Allaah Anajua zaidi
 
Kumsomea Maiti Qur-aan Nini Hukmu Yake?



Alhidaaya.com







SWALI:



Nini hukmu ya mwenye kusoma Al-Faatihah au chochote katika Qur-aan kuwasomea Maiti?





JIBU:



AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.





Hili ni jambo la kuzushwa. Hakulifanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam) wala Maswahaba zake (Ridhwaanu Allaahi ‘alayhim), hawakuwa wakiwasomea Maiti (Suwrat) Al-Faatihah, au Aayatul-Kursiy, au Al-Mu’awwidhatayn (Suwraah Al-Falaq na An-Naas), au Al-Ikhlaasw, au chochote katika Qur-aan.





Amesema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Mwenye kuzusha katika jambo letu (Dini yetu) hili ambalo halimo, basi hurudishwa (halipokelewi).”[Al-Bukhaariy na Muslim]





Na amesema Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Hakika Allaah Kazuia tawbah ya mwenye kufanya bid’ah mpaka aache bid’ah yake.”





Inapasa (aache hilo na afanye) tawbah kwa kitendo hicho.





Na Allaah Anajua zaidi
 
Maswali: Bid'ah - Uzushi


Kumsomea Maiti Surat Yaasiyn Anapooshwa, Au Akishazikwa Pamoja Na Du'aa Inafaa?



Alhidaaya.com





SWALI LA KWANZA:



Assalaamu alaikum warrahmatullahi wabarakatu.

Swala langu ni hili:Maiti akishazikwa inafaa asomewe sura-Yasin pamoja na dhikiri au kumuombea dua tu na watu waondoke?


Jazaakumullahu kheiran.





SWALI LA PILI:



Assalamu alekum,



Tunashukuru kututoa kizani na hasa mambo ya bidaa ambayo wengi tulikuwa hatujui tunafuata tu.



Swali langu ni je, maiti anapokata roho au anapokoshwa na kukafiniwa inafaa kumsomea Yaasiyn? Na pia pale akishazikwa watu hubakia kaburini kumsoema Yasin na duaa kwa pamoja, je kuna dalili yoyote kuhusu jambo hili?





JIBU:



AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.





Imekuwa ni ada katika jamii yetu kumsomea mtu anapokata roho au pale anapooshwa au akishazikwa Suwrah Yaasiyn na du'aa kwa pamoja. Tutambue kwamba ibada yoyote inayotendwa lazima ipatikane dalili, bila ya kwayo, huwa ni kitendo kisichokuwa na thamani mbele ya Allaah, wala hakimfai maiti kwa lolote lile!





Suwrah Yaasiyn hasa imekuwa maarufu kusomewa maiti. Maiti anapokata roho au akishafariki, na wengi wakiitumia dalili ya Hadiyth hii ambayo sio sahihi:



"Someni Yaasiyn kwa maiti wenu" [Abu Daawuud]





("Maiti wenu' hapo wengine wamefahamu kuwa ni wale wanaokata roho, na wengine wamefahamu kuwa ni wale tayari waliokwishakufa) Ndio maana utakuta mtu anapotaka kukata roho watu hukimbilia kumsomea Yaasiyn, na wengine baada ya kumzika humsomea maiti wao Yaasiyn kwa ufahamu wao wa Hadiyth hiyo ambayo ni dhaifu. Imaam An-Nawawiy, Ibn Hajar, Adh-Dhahabiy, Ibn Al-Qattwaan, Al-Albaaniy na wengineo wamesema Hadiyth hiyo ni dhaifu.



Anapofariki mja hakuna tena limfaalo ila mambo matatu kama ilivyo dalili katika Hadiyth:



"Anapofariki mwanaadamu ‘amali zake zote hukatika isipokuwa kwa mambo matatu: Sadaka yenye kuendelea, elimu yenye manufaa na mtoto mwema mwenye kumuombea du’aa (mzazi/wazazi anapofariki)". [Muslim kutoka kwa Abu Hurayrah].





Na katika Suwrah Yaasiyn yenyewe kuna ushahidi kwamba Qur-aan ni kwa ajili ya kuwaonya walio hai na sio waliokwishafariki. Sasa vipi iwe kinyume chake?



Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):



وَمَا عَلَّمْنَاهُ الشِّعْرَ وَمَا يَنبَغِي لَهُ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ وَقُرْآنٌ مُّبِينٌ ﴿٦٩﴾لِّيُنذِرَ مَن كَانَ حَيًّا وَيَحِقَّ الْقَوْلُ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴿٧٠﴾

Na hatukumfunza (Nabiy Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) mashairi, na wala haipasi kwake, hii si chochote isipokuwa ni ukumbusho na Qur-aan bayana. Ili imuonye yule aliyekuwa hai na neno lihakikike juu ya makafiri. [Yaasiyn: 69-70]





Pia kumsomea du'aa kwa pamoja sio jambo lilotendeka katika Sunnah, achilia mbali kumsomea maiti, hata kukusanyika kusoma du'aa pamoja kwa ajili ya jambo lolote lile haina dalili.





Hadiyth mbalimbali ambazo ima ni dhaifu au za kutungwa inazotumiwa sana na watu kuonyesha au kuthibitisha fadhila za Suwrah Yaasiyn ni hizi zifuatazo:



Kutoka kwa Anas Bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu): "Atakayeingia makaburini na akasoma Suwrah Yaasiyn atawafanyia wepesi (maiti) siku ya masiku, na ataandikiwa mema idadi ya walio humo makubirini." Imesimuliwa na As-Sakhaawiy . Imechambuliwa kuwa ni Hadiyth ya kutungwa kutoka katika kitabu cha 'Silsilatul Ahaadiyth Dhwa'iyfah' /1246



kutoka kwa Anas Bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu): "Kila kitu kina moyo, na moyo wa Qur-aan ni Suwrah Yaasiyn, atakayesoma Yaasiyn ataandikiwa thawabu za kusoma Qur-aan yote mara kumi." Imesimuliwa na Adh-Dhahabiy. -Imechambuliwa kuwa ni Hadiyth dhaifu kutoka katika kitabu 'At Targhiyb wat-Tarhiyb' /885



"Atakayesoma Yaasiyn kwa kutaka Ridhaa ya Allaah ataghufuriwa madhambi yaliyomtangulia, basi isomeni kwa maiti wenu." Hadiyth dhaifu kutoka katika kitabu 'Aj Jami'i Asw-Swaghyr'/5785.



"Atakayesoma Yaasiyn katikati ya mchana atakidhiwa haja yake" - Hadiyth dhaifu kutoka katika kitabu 'Mishkaat Al-Maswaabiyh'/2118.





Naye Imaam Ad-Daaraqutwniy kasema hakuna katika fadhila za Surah Yaasin Hadiyth yoyote iliyosihi.





Bali lililo sahihi kusomewa anayekaribia kufa ni kauli ya "Laa Illaaha Illa Allaah". Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):



"Yule atakayekuwa neno lake la mwisho ni Laa ilaaha illa Allaah ataingia Peponi". (Ahmad na Abu Daawuud).



Bonyeza viungo vifuatavyo ambavyo vinatoa maelezo zaidi kuhusu mas-ala ya Suwrah Yaasiyn na kumsomea maiti Qur-aan:





Kumsomea Khitmah Maiti, Kumchinjia Na Kumuombea Duaa Kwa Pamoja



Kumsomea Qur-aan Maiti Akishazikwa



Fadhila Za Surat Yaasiyn Na Al-An'aam





Na Allaah Anajua zaidi
 
Maswali: Bid'ah - Uzushi


Kupangusa Uso Baada Ya Kusoma Du’aa Inafaa?



Alhidaaya.com





SWALI:



Assalam aleikum

ningependa munifahamishe kuhusu mtu kufuta uso wake akimaliza dua wakati anaposema Amin, je kuna hadith yoyote ama kithibitisho kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alikuwa akifanya hivyo? Jaza yenu iko kwa Allaah subhanahuu wa Ta'aalaa kwa kazi munayo fanya, Shukran





JIBU:



AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho



Kupangusa uso baada ya kuomba du’aa si kitendo cha Sunnah, na Hadiyth nyingi zilizopokelewa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aailihi wa sallam) alipokuwa akiomba du’aa zake hakuwa akipangusa uso wake baada ya du’aa. Na hata katika Khutbah ya Ijumaa au Swalaah ya Istisqaa haikuthibiti kwamba alipangusa mikono yake usoni. Hadiyth moja au mbili zilizosimuliwa kuhusu kitendo hiki zimechambuliwa kuwa ni Hadiyth dhaifu, na 'ulaamaa wamekubaliana kwamba kitendo hiki hakipo katika Shari’ah.



Na hata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akimaliza Swalaah zake na kutoa salaam, hakuwa kamwe akipangusa uso wake kama ilivyo ada ya Waislamu wengi hivi leo wanavyofanya na hawajui kwanini wanafanya hivyo na hata ukimuuliza mtu anashindwa kukupa jibu, na wengine wanajibu kuwa wamejikuta wakikuwa na kuona ikifanywa hivyo na wao wanafanya. Muislamu anapaswa kufanya matendo yake yote ya ‘Ibaadah kwa dalili na si kwa kubahatisha au kuiga bila dalili.



Na Allaah Anajua zaidi
 
Maswali: Bid'ah - Uzushi


Kupiga Makofi Katika Mihadhara, Kongamano Na Sherehe



Alhidaaya.com



SWALI:



Nini hukumu ya kupiga makofi wanaume wanapokuwa wanapongeza mtu au kushangilia jambo kama tunavoona ktk mihadhara, makongomano, semina, mijadala na midahalo ya dini? Hili limekuwa jambo la kawaida hata ktk TV za Kiislamu tunazoona.





JIBU:



AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho



Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

وَمَا كَانَ صَلَاتُهُمْ عِندَ الْبَيْتِ إِلَّا مُكَاءً وَتَصْدِيَةً ۚ

Na haikuwa Swalaah zao (makafiri) kwenye Nyumba (Al-Ka’bah) isipokuwa ni miruzi na kupiga makofi. [Al-Anfaal: 35].

قال الرسول صلى الله عليه وسلم: (مَنْ نَابَهُ شَيْءٌ فِي صَلَاتِهِ فَلْيُسَبِّحْ فَإِنَّهُ إِذَا سَبَّحَ الْتُفِتَ،، و إِنَّمَا التَّصْفِيقُ لِلنِّسَاءِ). رواه البخاري (684) ومسلم (421)

"Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayetanabahi kitu katika Swalah yake, alete tasbiyh [Aseme Subhaana-Allaah] kwani anapoitamka, humvutia mtu atanabahi, na hakika kupiga makofi ni kwa ajili ya wanawake))." [Al-Bukhaariy (684), Muslim (421),]



Imeulizwa kuhusu tafsiyr ya:

وَمَا كَانَ صَلَاتُهُمْ عِندَ الْبَيْتِ إِلَّا مُكَاءً وَتَصْدِيَةً ۚ

Na haikuwa Swalaah zao (makafiri) kwenye Nyumba (Al-Ka’bah) isipokuwa ni miruzi na kupiga makofi. [Al-Anfaal: 35]





Imaam ‘Abdul-’Aziyz bin Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:



Hiyo ni Swalaah ya watu wa jaahiliyyah yaani makafiri wa ki-Quraysh na waliyokuwa wakifanya ya miruzi na kupiga makofi. Ikawa ada yao kupiga makofi kwa mikono na kupigia miruzi wakaharamishwa Waislamu vitendo kama vyao. Kwa hiyo haimpasi Muislamu apige miruzi au makofi katika ‘ibaadah zao wala katika Masjidul-Haraam wala katika vitendo vyake vinginevyo, bali kupiga makofi ni kwa ajili ya wanawake. Ama mwanamme aseme anapotanabahisha jambo; alete tasbiyh katika Swalaah: Subhaana-Allaah! Subhaana-Allaah! Wala asitumie miruzi, bali atamke maneno yanaohitajika bila ya miruzi.





Swali:



Nini Hukmu Ya Watu Kupiga Makofi Katika Sherehe, Matukio Na Mihadharah Na Makongamano?



Kupiga makofi ni katika vitendo vya ujaahiliyyah na hukmu ya chini kabisa ni jambo ka kuchukiza na lililo dhahiri kabisa katika dalili ni kuharamishwa kwake kwa sababu Waislamu wamekatazwa kuigiza makafiri, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika kuwaelezea makafiri wa Makkah:

وَمَا كَانَ صَلَاتُهُمْ عِندَ الْبَيْتِ إِلَّا مُكَاءً وَتَصْدِيَةً ۚ

Na haikuwa Swalaah zao (makafiri) kwenye Nyumba (Al-Ka’bah) isipokuwa ni miruzi na kupiga makofi. [Al-Anfaal: 35].





Wanavyuoni wamesema: ‘Al-Mukaa’ ni Miruzi na ‘At-Taswdiyah’ ni kupiga makofi. Na Sunnah kwa Muumini ni kwamba anapoona au kusikia jambo linalompendeza au linalomchukiza aseme: “Subhaana-Allaah” au aseme: “Allaahu Akbar” kama ilivyothibiti kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth nyingi. Na imeruhusiwa wanawake kupiga makofi hasa wanapotanabahisa kitu katika Swalaah au wanapokuwa na wanaume pale Imaam anaposahau kitu katika Swalaah basi inaruhusiwa atanabahishe kwa kupiga kofi. Ama wanaume anapokosea Imaam, wao wanatakiwa walete tasbiyh kama ilivyotibiti katika Sunnah kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na kwa hayo, inatambulikana kwamba wanaume kupiga makofi ni katika kuigiza makafiri na kuwaiga wanawake; na yote hayo yamekatazwa.





Na Allaah Ndiye Mwenye kuleta Tawfiyq.





Kwa faida, Ash-Shawakaan amesema katika ‘Niyl Al-Awtwaar’: (kuhusu kauli ya Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):



"Hakika kupiga makofi ni kwa ajili ya wanawake."



Inamaanisha kwamba imekatazwa kwa wanaume kabisa kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayejishabihisha na watu basi yeye ni miongoni mwao)).



Na Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika: ‘Al-Iqtidhwaa’ (1/83):



Hadiyth hii, inaonyesha na kuthibitisha kuwa, hali ya chini kabisa ni kuharamishwa kushabihiana nao japokuwa dhahiri yake ni hukmu kuwa ni kufru kushabihiana nao kama katika kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَإِنَّهُ مِنْهُمْ ۗ

Na yeyote atakayewafanya marafiki wao wandani; basi hakika yeye ni miongoni mwao.[Al-Maaidah: 51].



Na akasema pia kuhusu Hadiyth hii katika ‘Al-Iqtidhwaa’ (1/81):



"Sababu ya kuharamishwa huku ni kushabihiana (kujifananisha) nao."





Na Fatwa ya ‘Allaamah Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah) chini, inatilia nguvu yaliyotanguliwa kuelezwa:





Swali:



Fadhwilat Shaykh, Allaah Akuhifadhini: Nafanya kazi ya udaktari na nnapohudhuria vikao au makongamano ya udaktari, wanaume husimama kumpigia makofi mtoa mada. Ninapowaambia kwamba hakika kupiga makofi haifai kwenu bali ni kwa wanawake tu, husema: Hukmu hiyo imekusudiwa katika Swalaah pekee. Je, maneno haya ni sahihi?





Akajibu ‘Allaamah Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah):



Hapana! Si sahihi. Wanaume hawatakiwi kupiga makofi katika Swalaah wala kwengineko. Kupiga makofi ni kwa ajili ya wanawake na si kwa wanaume katika Swalaah au kwengineko. Hivyo ni kwa upande mmoja. Ama kwa upande mwengine, ni kwamba kuna kujifananisha na makafiri. Hiyo ni ada ya makafiri hatukuwa tukiijua wala Waislamu hawakuwa wakiijua (wakifanya) au hapakuwepo wanaume kupiga makofi isipokuwa ilipotujia mila na desturi za kikafiri katika sherehe zao na katika mikusanyiko yao. Na kupiga makofi pia ni katika mambo ya kijaahiliyyah:

وَمَا كَانَ صَلَاتُهُمْ عِندَ الْبَيْتِ إِلَّا مُكَاءً وَتَصْدِيَةً ۚ

Na haikuwa Swalaah zao (makafiri) kwenye Nyumba (Al-Ka’bah) isipokuwa ni miruzi na kupiga makofi. [Al-Anfaal: 35]





Wanavyuoni wamesema: ‘Al-Mukaa’ ni Miruzi na ‘At-Taswdiyah’ ni kupiga makofi. Kwa hiyo kupiga makofi ni katika kitendo cha kafiri. Na sasa (siku hizi) Subhaana-Allaah Wanapiga makofi na kupiga miruzi katika sherehe kama kitendo cha jaahiliyyah.”





Na Allaah Anajua zaidi
 
Maswali: Bid'ah - Uzushi


Kusema ‘Swadaqa-Allaahul-‘Adhwiym’ Baada Ya Kumaliza Kusoma Qur-aan

Au Kutaja Aayah; Inafaa?



Alhidaaya.com



SWALI:



Tumesikia kwamba mtu anapomaliza kusoma Qur-an kusema ‘Sadakallaahu l adhim’ ni bid’a, Je ni kweli? Tunaomba jibu la ufafanuzi kwa dalili.





JIBU:





AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.






Hakika Muislamu anapaswa kutambua kwamba vitendo vyote vya ibada lazima kupatikane dalili. Pindi isipothibiti dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah, basi kitendo hicho hakifai kama alivyotuonya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):


(( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika dini yetu) basi kitarudishwa)) [Al-Bukhaariy]



Swali hilo limeshaulizwa kwa 'Ulamaa wetu wakubwa na wakalijibu vizuri kabisa kwa maelezo bayana. Tunaweka hapa majibu yao kama ifuatavyo:





Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Baaz (Rahimahu-Allaah):



Sifa zote Njema ni za Allaah.

Sijui (sijapata) dalili yoyote ya ada ya watu kusema: “Swadaqa-Allaahul-‘Adhiwym” wanapomaliza kusoma Qur-aan. Kwa hiyo isifanywe kuwa ni ada. Hakika anayeamini kuwa ni Sunnah kufanya hivyo, basi katika Shari’ah ya Kiislamu ni bid’ah. Kwa hiyo haipasi kutamkwa wala kufanywa ni mazoea au ada.





Ama kuhusu maana ya Aayah: (Akatoa hoja kama hiyo ya Shaykh Ibn ‘Uthaymin Rahimahu-Allaah akaendelea):

قُلْ صَدَقَ اللَّـهُ ۗ

Sema: Allaah Amesema kweli. [Aal-‘Imraan 3:95]





Hii Aayah haizungumzii masuala haya. Bali Allaah Alimuamrisha Nabiy Wake kuwafafanulia watu kwamba Allaah Amesema kweli kwa kile Alichosema ndani ya Vitabu Vyake, Tawraat n.k., na kuwa Amesema kweli kwa yote yale Aliyoyasema kwa waja Wake ndani ya Tawraat, Injiyl na Vitabu vingine vilivyoteremshwa.





Na Allaah Amesadikisha yote Aliyoyasema katika Qur-aan kwa waja Wake. Lakini hivyo si dalili kwamba inapendekezeka kusema “Swadaqa-Allaahul-‘Adhwiym” baada ya kusoma Quraan au baada ya kusoma Aayah au Suwrah, kwani haikuripotiwa au kujulikana kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum).





Ibn Mas’uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipomsomea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Suwrah An-Nisaa mpaka alipofikia:



فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِن كُلِّ أُمَّةٍ بِشَهِيدٍ وَجِئْنَا بِكَ عَلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ شَهِيدًا ﴿٤١﴾

Basi itakuwaje Tutakapoleta kutoka kila Ummah shahidi, na Tukakuleta (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa shahidi juu ya hawa? (yaani dhidi ya Ummah wake) [An-Nisaa: 41]





Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

Hasbuka! (Inatosha, simama hapo).” Ibn Mas’uud akasema: “Nikamtazama na kuona machozi yamejaa machoni mwake.” yaani alikuwa akilia kwa sababu ya kutajwa jinsi hali ngumu itakavyokuwa Siku hiyo ya kufufuliwa [kama ilivyo Aayah hiyo].




La muhimu ni kwamba hakuna dalili katika Shari’ah kuongezea maneno ya “Swadaqa-Allaahul-‘Adhwiym” anapomaliza mtu kusoma Qur-aan, kwani haikuamrishwa hivyo kuwa ni kufuata mfano wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Lakini mtu akitamka hivyo mara moja moja bila ya kukusudia, haina neno kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasadikisha ukweli katika mambo yote. Lakini kufanya kuwa ni ada, desturi, au mazoea kila anapomaliza mtu kusoma Qur-aan kama wanavyofanya aghlabu ya watu siku hizi, ni kwamba hakuna dalili kama ilivyotajwa juu”



Kitaab Majmuu’ Fataawa wa Maqaalaat Mutanawwi’ah li Samaahat al-Shaykh al-‘Allaamah ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Baaz (Rahimahu Allaah), mj. 9, uk. 342.





Shaykh Muhammad bin Swaalih bin ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah):



“Sifa Njema zote ni za Allaah. Aghlabu ya watu wana tabia ya kumalizia kusoma Qur-aan kwa kutamka: ‘Swadaqa-Allaahul-‘Adhwiym’ (Amesadikisha Allaah Mtukufu). Lakini hiyo hakuna dalili katika Uislamu kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakufanya wala haikuwa ni ada (desturi) ya Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum), na pia haikutambulikana miongoni mwa Taabi’iyn (Waliowafuata Swahaba). Ada hii imeanzia nyakati zilizofuatia kwa sababu baadhi ya wasomaji Qur-aan waliipenda Aayah inayosema:

قُلْ صَدَقَ اللَّـهُ ۗ

Sema: Allaah Amesema kweli. [Aal-‘Imraan 3:95]





Lakini kuipenda huko kunapasa kukanushwa kwa sababu ingelikuwa ni jambo zuri, basi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba wake na Taabi’iyn ambao ni wa karne za mwanzo zilizo bora kabisa za Ummah wasingelipuuza kufanya hivyo. Aayah hiyo ((Sema Allaah Amesema)) haimaanishi kwamba maneno hayo yatamkwe baada ya kumaliza kusoma Qur-aan. Ingelikuwa inapasa hivyo, basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Angelisema: “Unapomaliza kusoma, sema: Allaah Amesadikisha” kama vile Alivyosema:



فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ﴿٩٨﴾

Unaposoma Qur-aan basi (kwanza) omba kinga kwa Allaah dhidi ya shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa. [An-Nahl: 98]



Aayah wanayoitumia Ahlul-bid’ah (wazushi) kuipa nguvu kauli yao ya ‘Swadaqa-Allaahul-‘Adhwiym’ baada ya kusoma Qur-aan imeteremshwa hasa kwa muktadha ya kuthibitisha yaliyotajwa kwamba chakula chote kilikuwa ni halali kwa Bani Israaiyl (Wana wa Israayiyl), isipokuwa kile alichokifanya haramu mwenyewe (Israaiyl; yaani Nabii Ya’quub [‘Alayhis-Salaam]).

كُلُّ الطَّعَامِ كَانَ حِلًّا لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ إِلَّا مَا حَرَّمَ إِسْرَائِيلُ عَلَىٰ نَفْسِهِ مِن قَبْلِ أَن تُنَزَّلَ التَّوْرَاةُ ۗ

Kila chakula kilikuwa halali kwa wana wa Israaiyl, isipokuwa kile alichojiharamishia Israaiyl (Ya’quwb) mwenyewe kabla ya kuteremshwa Tawraat. [Aal-‘Imraan: 93]





ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akasema:



..فَأْتُوا بِالتَّوْرَاةِ فَاتْلُوهَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٩٣﴾فَمَنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٩٤﴾قُلْ صَدَقَ اللَّـهُ ۗ فَاتَّبِعُوا مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٩٥﴾

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Basi leteni Tawraat kisha muisome mkiwa wakweli.Na yeyote atakayemtungia Allaah uongo baada ya hayo; basi hao ndio madhalimu. Sema: Allaah Amesema kweli. Basi fuateni millah (Dini) ya Ibraahiym aliyejiengua na upotofu akaelemea Dini ya haki na hakuwa miongoni mwa washirikina. [Aal-‘Imraan 3:93-95





Ingelikuwa Aayah hiyo imemaanisha kwamba maneno hayo yatamkwe baada ya kusoma Qur-aan, basi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) angelikuwa wa kwanza kutambua na kutekeleza hivyo. Lakini kwa vile hali haikuwa hivyo, nasi tunajua kwamba hivyo sivyo ilivyokusudiwa.





Kwa kuhitimisha, tunasema kwamba kusema: “Swadaqa-Allaahul-‘Adhwiym” baada ya kusoma Qur-aan ni bid’ah (uzushi) na hivyo Muislamu hapaswi kutamka hayo.





Lakini itambulike kwamba kuamini kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amesadikisha (Amesema kweli) ni wajibu. Na yeyote asiyeamini au akatilia shaka ukweli Aliosema Allaah basi yeye ni kafiri anayetoka nje ya Uislamu. Tunajikinga na Allaah kutokana na hilo.





Ikiwa mtu atasema katika hali ya kawaida: “Swadaqa-Allaah” (Allaah Amesema kweli), mfano imezungumzwa jambo na ikathibitishwa kauli Aliyoisema Allaah, hapo inaruhusiwa, kwa sababu hivyo ni kama ilivyothibiti katika Sunnah kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akihutubia na Al-Hasan na Al-Husayn wakaja, naye akataremka kutoka katika minbar akawabeba na kuwaweka mbele yake kisha akasema: "Hakika Allaah Amesadikisha". Na baada ya hapo akataja kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):



إِنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ..﴿١٥﴾

Hakika mali zenu na watoto wenu ni jaribio. [At-Taghaabun: 15]





Mwisho wa kauli ya ibn ‘Uthaymin (Rahimahu-Allaah) iliyorekodiwa kutoka: ‘Izaalat as-sitaar ‘an al-jawaab al-mukhtaar Ibn ‘Uthaymiyn, 79-80).





Hivyo, hapo kwenye fatwa ya Shaykh juu tunaona hata ilivyothibiti kwenye Hadiyth ni kuwa Nabiy alisema kabla ya kutaja Aayah na si baada ya kutaja Aayah au kumaliza kusoma Qur-aan kama ilivyozoeleka kwa wasomaji Qur-aan wengi na wahadhiri wenye kutoa mawaidha. Kwa hiyo, hawezi mtu kutumia Hadiyth hiyo kama ni dalili au hoja ya kufanya hivyo.





Na Allaah Anajua zaidi
 
Kusherehekea Anniversary Inafaa Kwa Waislamu?



www.alhidaaya.com





SWALI



Assalam alykum.... nilikuwa nataka kuulizaa swali juu ya Annivasary....

je waislamu inafaa kusherekea annivassary? ama haifai? shukran





JIBU:



AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.





Uislamu ni Dini yenye kutuongoza katika mfumo mzima wa maisha hapa duniani. Kwa ajili hiyo, lolote tufanyalo ni lazima liambatane na Shariy’ah ya Uislamu.



Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakuta watu wa Madiynah wakisherehekea siku kuu zao. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia kuwa wao wamebadilishiwa hizo sikukuu zao kwa siku mbili kuu zilizo bora kabisa, nazo ‘Iyd al-Fitwr na Al-Adhw-haa.



Ama sherehe ya anniversary hata ya Nabiy mwenyewe (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haipo katika siku za sherehe.



Ama hizi anniversaries ambazo tunasherehekea ni katika ada na desturi za makafiri na mushrikina. Na kwa hilo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza katika Hadiyth:



عن إبن عمر ((من تشبه بقوم فهو منهم)) ابن حبان - صحيح

Kutoka kwa Ibn 'Umar ((Mwenye kujifananisha na watu naye ni kama wao)) [Ibn Hibbaan ikiwa swahiyh]



Na zimezuka anniversaries nyenginezo mbali na ya ndoa ambayo ndio iliyoanzishwa mwanzo na makafiri. Kumezuka mpaka anniversary za kifo. Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho upate faida ziyada:



Hukmu Ya Kumbukumbu Ya Kifo (Death Anniversary)


Kwa hiyo, haifai kusherehekea anniversary ya tukio lolote lile.



Na Allaah Anajua zaidi
 
Maswali: Bid'ah - Uzushi
SWALI:

asalam alaikum warahma tullahi wabarakatum. suali langu hivi jee ni vibaya mtoto kufanyiwa birthday bila musik ni ya watoto tu wenzao kula na kunywa tu, na jee nivibaya kupuliza au kuuzima mshumaa wa happy birthday ni kuwa eti anauabudu moto? inshallah mtanipa jibu muafaka.







JIBU:

AlhamduliLLah, Waswalaatu Was-salaam 'alaa Rasuli-Llah صلى الله عليه وآله وسلم Amma ba'ad,



Tunamshukuru ndugu yetu kwa kuuliza swali hili muhimu ambalo lenye kuhusu jambo ambalo Waislamu wengi wanalitenda wakati jambo lenyewe halina msingi wa mafundisho ya dini, bali ni katika mambo ya kuigiza makafiri.

Amesema Allaah سبحانه وتعالى

((وَلَن تَرْضَى عَنكَ الْيَهُودُ وَلاَ النَّصَارَى حَتَّى تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ))

((Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao)) Al-Baqarah:120

Miongoni mwa mila zao makafiri ni hizo za kuwasha mishumaa na kupuliza, na kuweka muziki na kadhalika, yote hayo ni mafundisho ya baatil yasiyompasa Muislamu kuyafuata bali ni kufuata mwendo wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم pamoja na Wema Waliotangulia (Salaf Swaalih) ambao haijathibitika kuwa walikuwa wakishereheka siku zao za kuzaliwa abadan.

Kwa hiyo haifai kabisa kusherehekea kwa aina yeyote hata kama ni kualika watoto wenzake kukusanyika kula na kunywa tu, kwani kufanya hivi itakuwa ni mafundisho kwa wengine kuwa jambo hili linafaa kwa vile eti halina muziki au hupulizi mishumaa. Na kusita kwako kufanya hivyo itakuwa ni mafundisho ya wenzako na kizazi chako kuendelea kujiepusha na mila hizi na kila atakayewacha kufanya kwa mafundisho yako basi utapata thawabu zako kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى .

Ili kupata maelezo zaidi kuhusu upotofu wa jambo hili tafadhali soma makala muhimu sana iliyokuweko katika ALHIDAAYA katika kiungo kifuatacho yanayohusiana na maudhuu hii, upate kuona madhara yake na uweze kujiepusha na mambo haya yasio na maana katika dini yetu bali ni ya kumuingiza mtu katika kufuru ya kuigiza makafiri.

Bonyeza hapa:

Historia Ya Keki Na Mishumaa Katika Kuadhimisha Siku Ya Kuzaliwa (Birthday)

Na Allaah Anajua Zaidi.
 
Umuhimu wa Subira katika Uislamu

Subira (صبر) ni miongoni mwa tabia tukufu kabisa katika Uislamu. Ni uvumilivu wa moyo mbele ya matatizo, majaribu, na changamoto za maisha — kwa kutokata tamaa na kubaki imara kwa kumtegemea Allah.

📖 Qur'an inasema:
"Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye subira."
(Surat Al-Baqarah, 2:153)

Umuhimu wake:
1. Ni alama ya imani ya kweli – Muislamu wa kweli hujua maisha si ya raha muda wote.
2. Huvuta rehema na msaada wa Allah.
3. Husaidia kudhibiti hasira na maamuzi ya haraka.
4. Huimarisha moyo katika ibada na toba.
5. Ni njia ya kupata thawabu kubwa – Majaribu yanapovumiliwa kwa subira, Allah hutoa malipo yasiyo na kipimo.

Aina za subira:
  • Subira katika kutekeleza ibada.
  • Subira dhidi ya maasi na vishawishi.
  • Subira katika majaribu na misiba.

Mtume Muhammad (s.a.w) alisema:
"Ajabu ya hali ya muumini! Kila hali ni kheri kwake – akipatwa na neema hushukuru, na hiyo ni kheri; akipatwa na shida huvumilia, na hiyo pia ni kheri."
(Muslim)

Hitimisho:
Subira si udhaifu, bali ni nguvu ya kiroho na akhlaq inayomletea muumini utulivu, heshima, na mafanikio ya dunia na Akhera.
 
Hutuba ya Ijumaa: Umuhimu wa Swala (Sala)

Khutba ya Kwanza:

Sifa zote njema ni za Allah, Mola wa walimwengu wote. Tunamsifu, tunamshukuru, na tunamuomba msaada Wake. Tunashuhudia kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allah, na kwamba Muhammad ni Mtume Wake na Mjumbe Wake wa mwisho.

Enyi waumini! Naogopeni Allah kwa kumcha, na shikamaneni na uislamu wa kweli, kwa sababu hiyo ndiyo njia ya wokovu duniani na Akhera.

Swala ni nguzo ya dini. Mtume (Swalla aallahu alaih wasallamu ) amesema:
"Kilicho kati ya mtu na ukafiri ni kuacha swala." (Muslim)

Swala ni mwasiliano ya moja kwa moja kati ya mja na Mola wake. Ni faradhi tano kwa siku ambazo Allah hakuteremsha kwa njia ya kawaida – bali alimwinua Mtume (Swalla aallahu alaih wassallam) mpaka mbinguni (Isra wal Mi’raj) ili apewe swala. Hili pekee linaonesha ukubwa wake.

Allah anasema:
“Hakika swala humzuia mtu na mambo machafu na maovu...” (Al-Ankabut: 45)

Khutba ya Pili:

Enyi waumini! Wazazi wawaswalimishe watoto wao, viongozi wawaongoze watu wao, na kila muislamu ajihisabu. Swala ni alama ya utii, utiifu na unyenyekevu. Mtu asiye swala, hata akitoa sadaka au kufanya mema, bado hayatoshi bila kusimamisha swala.

Tuanze na Fajr – tuamke kwa Mola wetu.
Tusikose Dhuhr, Asr, Maghrib na Isha – kwani swala ndiyo uhai wa roho.

Tumuombe Allah atufanye miongoni mwa wenye kusimamisha swala kwa khushuu na daima, na awajaalie watoto wetu kuwa watu wa swala pia.

Wabarakallahu fikum.
 
UJUMBE WA LEO:

Hakika yule ambaye anakata udugu na ndugu zake waislamu au ndugu yake miongoni mwa ndugu zake hakika atamkuta Allah hana haja nae

Amesema Mtume swalla aallahu alaih wasallam Muislamu hapaswi kuacha kuongea na ndugu yake muislamu zaidi ya siku tatu

Na wale ambao wamekata undugu hakika aamali/matendo yao mema hayapokelewi mpaka wapatane
 
Maswali: Bid'ah - Uzushi


Kusoma Aayah Fulani Au Surah Mara Kadhaa



Alhidaaya.com



SWALI:



A.w.w.katika Ibada Zetu Tunaambiwa Soma Aayah Hiyi Mara Kadha Allah Atakuzawadiya Hiki. Je Hiyo Ni Shirki?





JIBU:



AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho





Tunatakiwa tufahamu kuwa ikiwa kusoma huko mara hizo kumetokana na Hadiyth zilizo Swahiyh utakuwa ni mwenye kupata thawabu na kupata hicho ulichoambiwa. Ikiwa kusoma huko ni katika Itikadi zetu, au maneno ya kutungwa kwa kuzuliwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) utakosa thawabu na kukuingiza katika madhambi. Hivyo, ni muhimu kutazama usahihi wa visomo hivyo kabla ya kuvishika na kuvifuata.





Lazima kutahadhari na mas-ala ya uzushi kwani yamezidi mno kutokana na wepesi wa mawasiliano. Hivyo ni wajibu wa Muislamu kuhakikisha kwanza habari inayomfikia kuhusu ibada zake kabla ya kuzifanyia kazi au kuzisambaza. Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:





Hatari Ya Kueneza Hadiyth Dhaifu Na Visa Vya Uongo

Suratul-An'aam Isomwe Siku 40 Kuondosha Mitihani Ya Dunia?

Kusoma Majina Ya Allaah Kwa Idadi Maalum





Na Allaah Anajua zaidi
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…