Fadhila Za Kusuluhisha Waliokhasimiana -1
Jamii


Fadhila Za Kusuluhisha Waliokhasimiana



Alhidaaya.com





Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)



لَّا خَيْرَ فِي كَثِيرٍ مِّن نَّجْوَاهُمْ إِلَّا مَنْ أَمَرَ بِصَدَقَةٍ أَوْ مَعْرُوفٍ أَوْ إِصْلَاحٍ بَيْنَ النَّاسِ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ ابْتِغَاءَ مَرْضَاتِ اللَّـهِ فَسَوْفَ نُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا ﴿١١٤﴾

Hakuna khayr katika minong’ono yao mingi isipokuwa anayeamrisha swadaqah, au mema, au kusuluhisha baina ya watu. Na atakayefanya hivyo kutaka radhi za Allaah, basi Tutampa ujira adhimu. [An-Nisaa: 114]



Na kasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam):

((ألا أخبركم بأفضل من درجة الصيام والصلاة والصدقة ؟ إصلاح ذات البين وفساد ذات البين هي الحالقة)) رواه أحمد وأبو داود والترمذي صحيح الجامع

"Je, nikujulisheni lililo na daraja bora kuliko Swawm na Swalah na Sadaqah? Ni kusuluhisha baina ya watu. Na ama kuharibu uhusiano (baina ya watu) ni uharibifu" [Ahmad na Abu Daawuud na At-Tirmidhy katika Swahiyhul-Jaami'i]



Katika mambo ya kheri Aliyoyataja Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) watu wanapozungumza kwa siri ni kuamrishana kutoa sadaka au kutenda mema. Kisha Ametaja kuhusu kupatanisha watu, jambo ambalo mara kwa mara hutokea katika jamii na khaswa jamii yetu. Na bila ya shaka ugomvi na ikhtilaaf ni katika silaha ya hatari kabisa anayopenda kuitumia Shaytwaan kufarikisha watu watengane na kuchukiana baada ya kuwa ni ndugu au marafiki au majirani au baina ya mume na mke. Lakini Uislamu haukuacha kutilia hima jambo la kusuluhisha ugomvi kwa kutukumbusha fadhila zake kubwa katika Qur-aan na Sunnah kama tunavyoona katika Aayah na Hadiyth hapo juu.



Lakini inasikitisha kuona kwamba jambo hili la kusuluhisha halikutiliwa mkazo sana katika jamii yetu, kwani wangapi tunasikia miongoni mwetu kuwa 'fulani kagombana na fulani na hawasemeshani', kisha zikapita siku na miezi na miaka hawa watu wako katika hali hii jambo ambalo Nabiy Swalla Allaahu amekataza kabisa zisipite zaidi ya siku tatu ndugu wa Kiislamu kuwa katika hali kama hiyo:

عن أبي أيوب الأنصاري رضي الله عنه قال : قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( لا يَحِلُّ لِمُسْلِمٍ أَنْ يَهْجُرَ أَخَاهُ فَوْقَ ثَلَاثِ لَيَالٍ ، يَلْتَقِيَانِ فَيُعْرِضُ هَذَا وَيُعْرِضُ هَذَا ، وَخَيْرُهُمَا الَّذِي يَبْدَأُ بِالسَّلامِ .(( رواه البخاري ومسلم و في رواية أبو داود بإسناد على شرط البخاري ومسلم

((فَمَنْ هَجَرَ فَوْقَ ثَلاَثٍ فَمَاتَ دَخَلَ النَارَ ))

Imetoka kwa Abu Ayyuub Al-Answariy (Radhwiya 'anhu) ambaye alisema: Kasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Haimpasi Muislamu amhame ndugu yake kwa zaidi ya siku tatu hata wanapokutana huyu anamgeuzia (uso) huyu na huyu anamgeuzia (uso) huyu. Na aliye mbora wao ni yule anayeanza kutoa salaam". [Al-Bukhariy na Muslim na katika Riwayaah ya Abu Daawuud]

((Atakayemhama (mwenzake) kwa zaidi ya siku tatu akafariki basi ataingia motoni))



Na huenda ikawa kila mmoja anataka kupatana na mwenziwe lakini Shaytwaan amewatia ari kuwa vipi aanze yeye? Na pia pengine huenda wakawa ni ndugu, au jamaa au jirani lakini hakuna mmoja wetu anayekimbilia kusuluhisha, sababu ni kwamba kila mmoja ameshughulika na kazi zake na maisha yake. Kwa hiyo tulichukulie hima jambo hili bila ya kuchelewesha kila inapotokea ugomvi baina ya ndugu wa Kiislamu na kufanya hivyo ni kumcha Allaah na kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na ndio sifa ya Waumini kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

فَاتَّقُواْ اللّهَ وَأَصْلِحُواْ ذَاتَ بِيْنِكُمْ وَأَطِيعُواْ اللّهَ وَرَسُولَهُ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ﴿١﴾

Basi mcheni Allaah na tengenezeni yaliyo baina yenu. Na mtiini Allaah na Rasuli Wake mkiwa ni Waumini.. [Al-Anfaal: 1]



Itaendelea sehemu ya pili In Shaa Allaah...





************
 
Allahu akbar yani kusuluhisha watu kuna daraja kubwa zaidi kuzidi swalah,swaumu na sadaq

Sasa tunafeli wapi ndugu zangu katika imani?

Na inasemwa kusuluhisha watu ni ucha mungu,haya wewe ambaye umegombana na ndugu yako Nabii swallallahu anasema lau ukifa katika hali hiyo waingia motoni,je unaridhia hali hiyo?

Ebu jifanye mjinga kwa kutaka suluhu kikubwa unafanya kwa kutaka radhi za Allah na salama yako kesho akhera

Wale ambao tunajua kuna ugomvi baina yetu basi tutae changamoto zetu,na.kama tunafahamu kuna ugomvi sehemu basi tukasuluhishe

Pata faida nyingine hakika uongo katika kusuhisha unafaa na hupati dhambi

Mfano unajua mimi na ndugu Adriz tumegombana,bazi waeza kwenda kwa Adriz na kumwambia " bwana Adriz ujue Etugrul anataka sana mpatane ila anashindwa akuanze vipi,na waeza enda kwa Etugrul na kumwambia hivyo hivyo " mwisho wa siku suluhu inapatikana

Ebu jiulize jamba ambalo uongo ndani yake unaruhusiwa ,je ni jambo dogo hilo mbele ya Allah?

Soma sehemu ya pili....
 
Fadhila Za Kusuluhisha Waliokhasimiana - 2



Alhidaaya.com





Tukiendelea na fadhila za kusuluhisha waliogombana wakakhasimiana, na iwapo baada ya kusoma mada hii tutazithamini fadhila hizi, basi kila mmoja wetu atakimbilia kufanya hima ya kupatanisha ndugu zetu wa Kiislamu waliokhasimiana. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amelichukia jambo hili kwani linavunja asili ya undugu wa Kiislamu kama Anavyosema :

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ ..﴿١٠﴾

Hakika Waumini ni ndugu, basi suluhisheni baina ya ndugu zenu. [Al-Hujuraat: 10]



Na kwa jinsi jambo hili lilivyochukiza hadi kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anakataa kupokea amali za watu waliokhasimiana mpaka wapatane, na hawasamehe watu hao:

عن أبي هريرة رضي الله عنه قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((تُعرض الأعمال في كل أثنين وخميس فيغفر الله لكل أمريء لايشرك بالله شيئاً، إلا إمرءاً بينه وبين أخيه شحناء فيقول: اتركوا هذين حتى يصطلحا)) رواه مسلم

Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba kasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Amali njema (vitendo vyema) hutandazwa kila Jumatatu na Alkhamiys, kisha Allaah Humghufuria kila mtu asiyemshiriki kitu Allaah, isipokuwa mtu aliyekuwa baina yake na baina ya ndugu yake uhasama, Husema: Waacheni hawa wawili mpaka wapatane)) [Muslim]



Kwa hiyo ni hatari kubwa kwa waliogombana kuwa wanapoteza umri wao bure kutenda mema na hali kumbe havipokelewi vitendo hivyo hadi wapatane.





Njia za kupatanisha Watu



1-Kwanza tia nia kuwa unafanya kupata Radhi na ujira mkubwa kutoka kwa Allaah na muombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akuwafikie jambo hili.



2-Msikilize kila mmoja malalamiko yake.



3-Ukishajua sababu ya ugomvi, watajie hatari ya kuhasimikiana kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)



4-Tafuta wakati na sehemu munaasib kwa wote wawili.



5-Ikibidi kusema uongo, inafaa katika jambo hili kwa kutaka kumridhisha mmojawao ili kuleta suluhisho kama alivyoruhusu Nabiy(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth:



((لَيْسَ الْكَذابُ الَّذِي يُصْلِحُ بَيْنَ النَّاسِ فَيَنْمِي خيرا أو يقول خيرا)) رواه البخاري ومسلم

"Si muongo yule anayesuluhusha watu kwa kusema uongo, kwani anaarifu mema au anasema mema [kwa lengo la kusuluhisha]" [Al-Bukhariy na Muslim]



6-Fanya uadilifu, usipendelee hata kama mmoja ni jamaa yako wa karibu au unampenda zaidi. Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

.فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ

Basi suluhisheni baina yao kwa uadilifu, na timizeni haki. Hakika Allaah Anapenda wanaotimiza haki. [Al-Hujuraat: 9]



Na Anasema tena Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa :

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاءَ لِلَّـهِ وَلَوْ عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَوِ الْوَالِدَيْنِ وَالْأَقْرَبِينَ ۚ إِن يَكُنْ غَنِيًّا أَوْ فَقِيرًا فَاللَّـهُ أَوْلَىٰ بِهِمَا ۖ فَلَا تَتَّبِعُوا الْهَوَىٰ أَن تَعْدِلُوا ۚ وَإِن تَلْوُوا أَوْ تُعْرِضُوا فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا ﴿١٣٥﴾

Enyi walioamini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu mtoapo ushahidi kwa ajili ya Allaah japokuwa ni dhidi ya nafsi zenu au wazazi wawili, au jamaa wa karibu. Akiwa tajiri au maskini Allaah Anawastahikia zaidi. Basi msifuate hawaa mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa au mkikanusha basi hakika Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [An-Nisaa: 135]





7-Wakishapatana In shaa Allaah omba du'aa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Awaendeleze masikilizano na mapenzi baina yao na muombe pia Akutakabalie juhudi yako.





Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atunufaishe kwa yale tunayojifunza na Atuajaalie miongoni mwa wale wanaosikiliza kauli (nyingi) wakafuata zile zilizo njema. Aamiyn.
 
Fiqh Ya Majina Ya Watoto



Alhidaaya.com





Ni Sunnah kutunza jina zuri, na katika majina mazuri ni:



'Abdullaah (Mja wa Allaah Subhanahu wa Ta'aala)

na

'Abdur-Rahmaan (Mja wa Mwingi wa Rahmah);



na majina ya ki kweli hasa ni:



Al- Haarith (Anayezaa)

na

Humaam (Hodari);



na majina mabaya zaidi ni:



Harb (Vita)

na

Murrah (Chungu)





Hadiyth ifuatayo imethibitisha:



((Majina yanayopendezewa kwa Allaah (Subhaana wa Ta'aalaa) ni 'Abdullaah na Abdur-Rahmaan.)) [imeripotiwa na Muslim.





Kwa Abu Daawuud kuna nyongeza ((Na majina ya ki kweli hasa ni Al-Haarith na Humaam, na mabaya zaidi ni Harb na Murrah)).





Na majina mabaya, na yale ambayo yanamaanisha vitu vibaya katika kutokuwepo kwao, ni makuruhu (Yasiyopendeza), kama vile:



Nujayh (fanikiwa),



Barakah (baraka),



Kulayb (kijimbwa),



Harb (vita),



Murrah (chungu),



Shihaab (kimondo),



Himaar (punda),



Aflah (fanikiwa sana),



Yasaar (wepesi),



Rabaah (faida), na



Naafi` (kunufaika)



na majina kama:



Sittun-nisaa (mwanamke wa wanawake wote) ni yanayogombezewa sana.



Na Mfalme wa Wafalme limekatazwa, kama ilivyokuwa:



'Shahenshaah',



na



Aqdhwaal-Qudhwaat (hakimu wa mahakimu).





Na inapendelewa kubadilisha majina mabaya na ambayo yanamaanisha vitu vibaya katika kutokuwepo kwao.





Na inapendelewa kwa mtoto wa kiume, mwanafunzi au mfanyakazi kutomwita kwa jina lake, na kwamba watu wazuri (wanaume na wanawake) wawe wana kun-yah, hata ikiwa hawana watoto wa kiume, na kun-yah huhusiana na mtoto wa kiume wa mwanzo.





Na imekatazwa kuwa na Kun-yah ya 'Abul-Qaasim kwa mtu ambaye jina lake ni Muhammad na vile vile kwa watu wengine, katika kipindi cha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na vile vile baadae ya hapo.





Tanbihi:



Kuna khitilafu baina ya madhehebu juu katika nukta hii- wengine wameshika kwamba katazo lake (kutumia kun-yah ya Abul-Qaasim) liliwekwa katika kipindi cha uhai wa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tu na si baada ya kufariki.





Na aliyeruka mipaka (faasiq) au mzushi asipewe kun-yah mpaka kukiwepo hofu ya fitnah, au ikiwa kwa sababu ya utambulishi, (kama vile Abu Lahab).





Na inapendelewa kwamba mtu asitumie kun-yah yake pekee (yaani bila ya kutimiza jina lake pia), isipokuwa akiwa anajulikana kwa kun-yah yake na sio kwa jina lolote isipokuwa hilo.





Na pia imekatazwa (Haraam) kumtania mtu kwa jina ambalo halipendi. Kama ikiwa anajulikana kwa jina jengine (ambalo halimchukizi) na hata kama jina hilo lina dhamiria kitu ambacho kinamhusu yeye ambacho ni cha kweli.





Kun-yah (Lakabu au Jina la kupachika)

Ushahidi uliombwa wa kuchukuliwa kun-yah kuwa ni Sunnah. Kuna vidokezo mbali mbali juu ya hili katika Hadiyth.





Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na kun-yah, na hakuna ushahidi wowote wa kuonyesha kwamba kuwa na kun-yah ilikuwa kwa yeye pekee, na hii ndio inayoamua ni Sunnah (kumfuata mtu katika kitu ambacho hakikua kwa ajili yake pekee (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).







Zaidi, kuna Hadiyth iliyoripotiwa na At-Tirmidhiy katika "Ash-Shamaail"





Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwita mvulana mdogo kwa kun-yah, kuonyesha kwamba si muhimu kuwa na mtoto kabla ya kutumia kun-yah.





Mazungumzo zaidi ya Hadiyth hizi yanapatikana katika Fat-h al-Baariy (maelezo ya Swahiyh Al-Bukhaariy).
 
Haki Za Wazazi Kuwatendea Ihsaan



'Khutbah ya Ijumaa



Alhidaaya.com





Allaah Aliyetukuka Anatuambia yafuatayo:



وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا ﴿٢٤﴾

Na Rabb wako Amehukumu kwamba: Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na (Ameamrisha) kuwafanyia ihsaan wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie, Uff! Na wala usiwakemee; na waambie maneno ya heshima.Na wainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma, na useme: Rabb wangu! Warehemu kama walivyonilea udogoni. [17: 23 – 24]



Allaah Aliyetukuka Amekariri katika surah saba tofauti kuhusu haki za wazazi kwa aina tofauti. Hata hivyo, kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa Qur-aan huwezi kupata maelezo yoyote kuhusu majukumu ya mzazi kwa watoto wake. Je, kuna hekima gani kwa Allaah Aliyetukuka kuwahimiza watoto kuwatendea wema wazazi na kutowahimiza wazazi juu ya majukumu yao kwa watoto wao? Ni jambo linalojulikana kuwa hata kwa wanyama, wanakuwa ni wenye kuwalinda na kutekeleza majukumu yao kwa watoto wao. Kwa ajili hiyo kuku anakuwa karibu na vijifaranga vyake ili kuvilinda wakati wa hatari.



Ni maumbile ya mwanadamu anapokuwa ni mzazi kutekeleza majukumu kwa watoto wake – majukumu ya msingi. Hata hivyo, watoto mara nyingi hujitazama wao wenyewe bila kujali kama mzazi anacho au hana. Mwanaadamu kimaumbile anapopata watoto hamu yake kubwa ni watoto wake na sio wazazi ambao ndio sababu ya kuja kwao. Kwa ajili hii Allaah Aliyetukuka Akatoa ufafanuzi mrefu kuhusu majukumu ya watoto kwa wazazi wao. Ukumbusho huu umekaririwa mara kadhaa ili kumpatia hisia mtoto atekeleza majukumu yake kwa mzazi wake.



Aayah ambayo imefafanua kwa kina suala hilo ni Aayah ya Suwrah 'Al-Israa' ambayo tumeitaja hapo juu. Amri ya kwanza iliyokuja katika Aayah hizo mbili zilizofuatana ni kumuabudu Allaah pekee bila ya kumshirikisha na yeyote wala chochote. Baada ya agizo hilo ni amri ya kuwatendea wema wazazi wawili. Kwa ile bahati ambayo anapata mtoto ni pindi wazazi wanapokuwa ni wakongwe na wako kwako wakiwa wanakutegemea wewe peke yako. Wakati huo utiifu wa kweli unajitokeza kwa kiasi kikubwa sana. Je, utawatazama kwa njia gani? Hakika huo ni mtihani mkubwa sana kwa mtoto au watoto wenye kulea wazazi wakongwe, ndio Allaah Aliyetukuka Akatoa maagizo Yake kuhusu wema na ihsani wanaofaa kufanyiwa. Katika walio kwako anaweza kuwa ni mzazi mmoja au wawili. Katika hali hiyo yao ya uzee wakiwa wanakutegemea wewe sio kinyume chake ndio utiifu wa kihakika unajulikana na ndio hapo pia hufai kuwaambia hata Ah au Uff au Uh na kadhalika.



Ibara iliyotumika hapa inamaanisha kuwa wewe pia si mtoto hivyo japokuwa mzazi wako bila shaka atakuwa ni mkubwa kuliko wewe. Ikiwa mzazi wako ni miaka themanini wewe huenda ukawa arobaini. Katika hali ya kuwa wapo kwako Allaah Aliyetukuka Anasema: "Usiwaambie Ah!" Wanazuoni wasema kuwa lau kuna neno dogo zaidi kuliko Uff basi Allaah Angelitumia lakini hakuna dogo zaidi. Katika Kiswahili chetu husema kuwapigia kitunu (kuguna). Hii ni alama ya kuonyesha kutoridhika kwako, hali hiyo isiwe ni yenye kutokea kabisa kwani sio sifa nzuri.



Pia usiwatolee ukali wala kuwakemea. Hii ni tabia ya utoto ambaye anakuwa hana hisia na jambo lolote linaweza kumkasirisha na hayo ndio maumbile ya mwanadamu anapozeeka. Wazazi wako walikuwa hawakukaripii ulipokuwa mdogo, nawe pia inatakiwa ufanye hivyo. Mbali na hayo unatakiwa useme nao maneno yaliyo mazuri, kauli za kuwafurahisha na sio kinyume chake. Bado Allaah Anaendelea kutupatia maagizo kuhusu kuwatendea wema wazazi wakati huo. Na baada kuwafanyia yote hayo basi pia kuwa mnyenyekevu kwao kwa kiwango cha juu. Bado hata baada ya kuwafanyia yote hayo utakuwa hujalipa ihsani na wema waliokufanyia. Ulipokuwa mdogo walisumbuka, walikopa, walikosa kula na mengineyo kwa ajili yako. Ihsani usiyoifahamu utailipa namna gani?



Hivyo ndio Allaah Aliyetukuka bado Anatuusia tuwe ni wenye kuwaombea du’aa kwa kusema: "Ee Rabb wangu! Warehemu wao kama walivyonilea nikiwa mdogo". Hii ina maana kuwa Ee Allaah! kwa kuwa mimi siwezi kuwalipa kwa waliyonifanyia basi warehemu wazazi wangu. Hii ni Aayah moja miongoni mwa Aayah nyingi inayotufundisha kuwaamili wazazi wanapokuwa wazee wakiwa kwetu.



Suala ni kuwa wengi wetu tuna wazazi, je muamala wetu kwao ni vipi? Utakuta kuwa wengi wetu huondosha kero (udhia na usumbufu) nyumbani huwa tunawapeleka wazazi wetu katika nyumba za wazee. Kufanya hivyo sio kwa sababu ya kuwa hakuna nafasi nyumbani wala hakuna cha kuwapa bali sababu kuu ni kuwa mke haridhiki kwa hilo. Huo sio ubinadamu kabisa. Allaah Anauliza: "Je, malipo ya wema yapo mengine ila wema?" Gari mara nyingi huwa tunalitazama likiwa ni jipya, lipo kazini na laleta pesa kwa mwenyewe lakini pindi linapozeeka anakwenda kulitupa mahali likimalizika kidogo kidogo. Hivyo ndivyo tunavyowafanya wazazi wetu wakati huu wetu wa leo.



Hakika ni kuwa haifai kuwepo majumba ya wazee katika jamii ya Kiislamu ikiwa tutakuwa tunafuata Uislamu inavyotakiwa. Lakini ni sikitiko kubwa sana kuona kuwa majumba hayo yanakithiri kila uchao. Huu si Uislamu. Kiislamu familia ni pana zikiwajumlisha wazazi wako, wazazi wa mke, mkeo, watoto wako na wajukuu na kadhalika. Lakini kwa kuwa fikra za kimagharibi zimetuvaa na kututawala tumejaalia kuwa familia ni wewe, mkeo na watoto wako basi. Leo katika nchi za kimagharibi wazee wamekuwa ni kero na kuna njia inayoitwa kuua kwa huruma inayotumika kuwamaliza na hivyo kuwapumzisha na mateso na udhia kwako.



Kiislamu sio hivyo bali kila wazazi wanapokuwa wazee ni nafuu kwetu kwa kiasi kikubwa. Imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema: “Mwana pua yake kusuguliwa na mchanga (amekhasirika)[1], kisha mwana pua yake kusuguliwa na mchanga, kisha mwana pua yake kusuguliwa na mchanga yule ambaye atawakuta wazazi wake wawili wakiwa wazee, mmoja au wote kisha asiingie Peponi?” [Muslim].



Hakika kwetu sisi wazazi kuwa wazee ni neema na ni mlango wa mtu kuingia (Jannah) Peponi. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema: "Pindi mtu anapokuwa na wazazi wake wakiwa kwake basi milango miwili ya Peponi yanafunguliwa kwake". Uamuzi wa kuingia au kutoingia ni wake. Na kinyume chake pia ni sahihi, hivyo ukiwafanyia ubaya milango miwili ya Motoni itafunguliwa kwa ajili yake.



Wazazi tulipokuwa wadogo walikuwa wakitutazama kwa hali na mali mbali na kutufurahikia lakini wanapokuwa wazee huwa tunawakodishia wafanyakazi wa kuwatazama. Wewe uliyetoka katika tumbo lake huona huwezi kushika uchafu wa mzee wako. Je, unadhania kuwa hisia zako na za mfanyakazi itakuwa sawa? Tunadhania kuwa kumuwekea mtumishi inatosha lakini hilo halitoshi kabisa na ipo haja ya sisi kuzingatia hilo na kujirekebisha kwa njia iliyo nzuri. Kwa ajili ya umuhimu wa suala hili kwa kukaririwa mara nyingi na Allaah Aliyetukuka ipo haja kwetu kukumbushana kila mara tunapopata nafasi na fursa.



Utiifu kwa wazazi unakuja baada ya utiifu kwa Allaah Aliyetukuka lakini utiifu kwa wazazi una mipaka. Ipo hali moja ambayo mtoto hafai kumtii mzazi wake nayo tumefahamishwa na Allaah katika Qur-aan. Allaah Anasema:



وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا ۖ

Lakini wakikushikilia kuwa Unishirikishe na ambayo huna elimu nayo, basi usiwatii. Na suhubiana nao kwa wema duniani. [Luqmaan: 15]



Hii ni hali ambayo hufai kuwatii kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: "Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba". Hata hivyo, katika hali yoyote ile ni lazima uwatii na hata wakikuamrisha mabaya wewe hufai kuwatii tu lakini unatakiwa usuhubiane nao kwa wema hapa duniani. Sababu ni kuwa haki yao ya uzazi haipomoki (haiondoki) kwa wao kufanya ubaya au kuamrisha mabaya.



Kila mmoja wetu ana wazazi wawili na huenda tukawa tunauliza ni nani katika wao mwenye haki zaidi kuliko mwengine. Jawabu la hilo tunapatiwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).



Imepokewa na Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu.) ambaye amesema: "Alikuja mtu kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: “Ewe Mjumbe wa Allah! Ni nani mwenye haki zaidi miongoni mwa watu kwa mimi kusuhubiana naye kwa wema?” Akasema: “Mamako”. Akasema: “Kisha nani?” Akasema: “Mamako”. Akasema: “Kisha nani?” Akasema: “Mamako”. Akasema: “Kisha nani?” Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): “Babako” [al-Bukhaariy na Muslim].

Na katika riwaya nyengine: “Ee Rasuli wa Allah! Nani ana haki zaidi kwa mimi kusuhubiana naye kwa wema?” Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): “Mamako, kisha mamako, kisha mamako, kisha babako, kisha wale waliokaribu, wale walio karibu nawe kijamaa”.



Hadiyth hii inatuonyesha kuwa mama ana sehemu tatu ziada za kufanyia wema na watoto kuliko baba. Na hii ni sababu ya shida na uzito anaopata wa kubeba mimba, kisha kuzaa na baadaye kunyonyesha.



Al-Qurtubiy amesema: “Mama anastahiki wema na ihsani zaidi kuliko baba, na amemtangulia baba katika mashindano hayo”.



Haya yalizungumzwa wakati ulimwengu hauna masuala ya gender (jinsia). Bila shaka, masuala hayo ni katika nadharia za kimagharibi lakini katika Uislamu kila mmoja anapatiwa haki yake anayostahiki na Allaah Aliyetukuka. Hapa mama hakupendelewa kabisa bali alipatiwa haki yake anayostahiki kulingana na wajibu wake aliopewa. Majukumu ya mama ni makubwa zaidi. Yeye ndiye aliyekubeba wewe kwa udhaifu juu ya udhaifu na mimba hiyo ikamletea matatizo na pia akaonja mauti akiwa hai. Na kuna msemo kwetu unaosema: "Kuzaa ni kuonja mauti". Mbali na maendeleo katika utabibu bado wapo wanawake wengi wanaoaga dunia wakati wa kuzaa. Na mama kwa kumpenda mtoto wake lau ataulizwa achukuliwe nani baina yake na mwanae basi atajibu achukuliwe naye, abaki mwanae katika uhai. Hii ni ruhuma (huruma) ya mwisho aliyonayo mama kwa mtoto wake. Baba akiwa na ruhuma nyingi atakuwa na wasiwasi wakati mkewe anajifungua lakini si zaidi ya hapo. Hata hivyo, ni masikitiko makubwa sana kuona leo vijana wanawachukulia akina mama kama kitambaa cha mkono, hatuwajali kabisa.



Tumenyonya maziwa ya mama kwa miaka miwili, hiyo ni kunyonya nguvu zake. Maziwa hayo hayakutoka katika mfereji. Allaah Aliyetukuka Anasema:



وَالْوَالِدَاتُ يُرْضِعْنَ أَوْلَادَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ ۖ لِمَنْ أَرَادَ أَن يُتِمَّ الرَّضَاعَةَ ۚ

Na wazazi wa kike wanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili, kwa mwenye kutaka kutimiza kunyonyesha. [Al-Baqarah: 233].



Baba hata akitaka vipi hawezi kukunyonyesha labda akusaidie kukushikia chupa ya maziwa.



Allaah Aliyetukuka Anasema:



وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ إِحْسَانًا ۖ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ كُرْهًا وَوَضَعَتْهُ كُرْهًا ۖ وَحَمْلُهُ وَفِصَالُهُ ثَلَاثُونَ شَهْرًا ۚ

Na Tumemuusia insani kuwafanyia wema wazazi wake wawili. Mama yake amebeba mimba yake kwa tabu na akamzaa kwa tabu, na kuibeba mimba na kuachishwa kwake kunyonya ni miezi thelathini. [Al-Ahqaaf: 15].



Hapa Allaah Anataja haki za wazazi wawili na kisha anabainisha uzito Aliopata mama hivyo kustahiki haki zaidi. Hakika shida na unyonge wa mama katika kubeba mimba yako ni mkubwa na kila miezi ilipokuwa inapita ndio udhaifu zaidi aliokuwa akipata. Si hayo tu bali mtoto si kama kifaranga ambapo anapoanguliwa tu anaanza kula bali mwanadamu ananyonya kwa miaka miwili kutoka kwa mamake.



Ama kuhusu fadhila nyengine za haki kwa wazazi ni Hadithi zifuatazo:



Imepokewa kwa Ibn Mas‘uud (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Nilimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): “Ni amali gani inampendeza Allah Aliyetukuka?” Akasema: “Ni Swalaah kwa wakati wake”. Nikasema: “Kisha ni ipi?” Akasema: “Kuwatendea wema wazazi wawili”. Nikasema: “Kisha ipi?” Akasema: “Jihadi katika Njia ya Allah” [al-Bukhaariy na Muslim].



Na imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: “Mtoto hawezi kumlipa babake (kwa yale aliyomfanyia) isipokuwa anapomkuta kuwa ni mtumwa, akamnunua kisha kumwacha huru” [Muslim, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy].



Pia kama ilivyo haki za wazazi na hasa ya mama, kuna kuwaasi wazazi. Kufanya hivyo ni katika madhambi makubwa kama alivyotuelezea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), yaani kumshirikisha Allaah Aliyetukuka na kuwaasi wazazi. Kumuasi mzazi si lazima umtusi au kumweka na njaa kama tulivyoona hata kuwaambia Uff.



Khasara ngapi mtu anapata kwa kukasirikiwa na mzazi wake. Hakika hii ni hasara kubwa ambayo Muislamu atapata ikiwa hataweza au atashindwa kuwajibika ipasavyo kwa kuwapatia wazazi wake. Allaah Aliyetukuka Atuepushe mbali na hilo.


[1] Hii ni kinaya ya mtu kudhalilishwa.
 
Historia Fupi Ya Palestina



Muhammad Al-Ma’awy



Alhidaaya.com





Ulimwengu wetu wa sasa umekuwa ni wa utandawazi (ulimwengushi) kwa kiasi ambacho yaliyo ndiyo yamekuwa siyo na ya makosa yamechukuliwa kuwa ni ya makosa. Ulimwengu umekuwa ukipigwa makombora na vyombo vya habari kwa njia moja au nyingine.



Mwenye kumiliki chombo cha habari cha kilimwengu anaweza kupeperusha au kuandika ya kwake na yakaweza kuchukuliwa kama ukweli mtupu. Ulimwengu umekuwa ni wenye kuchukua yote na wenye sauti kubwa kwa kuwa na vyombo hivyo wameweza kusikika mbali japokuwa hawana haki wa kupata wanayopata.



Kadhiya moja ambayo imeeleweka sivyo ni kadhiya ya historia ya Palestina. Waliojizatiti kuiweka katika hali hiyo iwe hivyo ni Wazeyuni bila kuwa na pingamizi kwa kuwa na sauti kubwa. Juhudi dhidi yao zimekuwa zikifanywa bila ufanisi wowote kwa sababu ya sauti kubwa waliyonayo wao. Taasisi kubwa na maarufu za vyombo vya habari zinamilikiwa nao kwa namna moja au nyingine. Mbali na hiyo hatufai kufa moyo kuhusu juhudi hizo kwani nusura hutokea baada tawfiki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliyetukuka, kisha juhudi zetu kwa kutumia njia tofauti.



Kwa sababu ya sifa zake Palestina, kama hali ya hewa, rutuba ya ardhi na upatikanaji wa maji safi ndio wavamizi wengi wamejaribu kuiteka ardhi hii na kuitawala kimabavu.



Makao ya awali yalianzishwa Palestina katika miaka ya 14000 hadi 8000 KI (Kabla ya kuzaliwa kwa ‘Nabiy ‘Iysa) kwa utawala wa Tatwafi. Na katika mwaka 8000 KI, mji wa Ariha (Jericho) ulianzishwa huko Palestina. Mji huo ulijengwa na wenyeji ukajengeka kwa njia ya mipango kama ilivyo miji ya kisasa.



Makabila ya mwanzo kuja kuweka makazi yao katika nchi ya Palestina ni yale makabila ya Wayebusi, Waamori, Wahiti, Wakanaani, Waamalika na Wafiniki. Makabila haya yalikaa katika maeneo tofauti ya nchi hiyo: Wakanaani waliweka makazi yao katika eneo la Gaza ilhali Wayebusi walibuni mji wa Yebus, ambao kwa sasa unajulikana kama mji wa al-Quds. Makabila haya yalihamia huko kutoka kusini mwa Bara Arabu takriban mwaka 3000 KI.



Katika mwaka wa 1900 KI, Nabii Ibraahim ('Alayhis-salaam) alihamia kutoka Iraq na kuja kuweka makazi yake katika mji wa Khalil. Hapo ndipo alipomzaa Nabiy Ismaa‘iyl na Ishaaq ('Alayhim-salaam) na baadaye kuzaliwa Nabii Ya‘quub ('Alayhis-salaam).



Katika kipindi 1800 – 1600 KI, Palestina ilitawaliwa na Waheksosi. Ni katika kipindi hiki katika mwaka wa 1750 KI ndio Nabii Ya‘quub ('Alayhis-salaam) alizaliwa.



Katika karne ya 16 KI (yaani mwaka wa 1580 KI), Bani Israili waliokuwa Misri walitiwa utumwani na Firauni wa wakati huo kuvamia na kuitawala Palestina kwa muda kabla ya sehemu hiyo kuingia katika utawala wa Kiislamu.



Mwaka 1250 KI, Nabiy Muwsaa ('Alayhis Salaam) aliagiziwa na Allaah Aliyetukuka atoke Misri ambako wana wa Israili walikuwa ni watumwa waende wakaishi katika ardhi tukufu. Kwa ajili ya ukaidi wao (Qur-aan 5: 21 – 26), walipigwa marufuku kuingia katika ardhi hiyo. Mbali na hilo walipigwa adhabu kali ya kutangatanga katika jangwa kwa muda wa miaka arobaini (40). Katika kipindi hicho, wale wote waliokuwa wamebaleghe walikufa katika jangwa kikabakia kizazi ambacho kililelekea katika maadili ya Kiislamu, Imani na uchaji Allaah kuingia katika ardhi hiyo tukufu. Kizazi hicho kilipata darsa ya ukakamavu, utii, kujitolea mhanga na malezi bora, hivyo kwa tawfiki ya Allaah Aliyetukuka kuweza kuingia ardhi hiyo mwaka 1190 KI wakiongozwa na Yusha bin Nuwh ('Alayhis-salaam). Wakati huo tayari Nabiy Muwsaa ('Alayhis-salaam) alikuwa ameaga dunia hivyo kutoweza kuingia katika ardhi hiyo.



Yusha bin Nuwh ('Alayhis-salaam) ndiye mwana Israili wa kwanza aliyeanzisha dola katika maeneo ya Palestina. Hata hivyo, wana wa Israili chini ya uongozi wa Yusha bin Nuhw ('Alayhis -salaam) hawakuweza kuliteka eneo lote la Palestina katika mipaka yake ya sasa na hata mji wa al-Quds haukuingia mikononi mwake. Ifahamike kuwa dola hiyo haikuwa katika misingi ya Kiyahudi kwani dini ya Kiyahudi ilikuwa haijabuniwa kamwe wakati huo bali ilikuwa ikipekeshwa katika misingi ya Kiislamu.



Dola hii haikukaa kwa muda kwani vurugu liliingia kati baada ya kuaga dunia Yusha bin Nuwh ('Alayhis-salaam), hivyo kushikiliwa na Ma-Qaadhi kabla ya kusambaratika kabisa kabisa. Kufikiwa na hayo, Bani Israili waliingia katika utawala wa Wapalestina ambayo asili yao ni Wakanaani. Kudhalilishwa kwao huko kuliwafanya watake msaada kutoka kwa Allaah Aliyetukuka ili warudi katika enzi zao (Qur-aan, 2: 246). Allaah Aliyetukuka Aliwateulia Twaaluut kuwa mfalme wao wa kuwaongoza wao kwenda kupambana na Wapalestina wakiongozwa na Jaaluut (Qur-aan, 2: 247). Bani Israili waligomba sana kuhusu uchaguzi huo, hata hivyo wapo waliokuwa na Imani ambao walisalimu amri na kujizatiti kwenda kupambana na Wapalestina. Wakati huo, Nabii Daawuud ('Alayhis-salaam) alikuwa kijana mdogo aliyejiunga na jeshi hilo ambalo kwa tawfiki ya Allaah Aliyetukuka liliweza kulishinda jeshi la Jaaluwt (Qur-aan, 2: 248-251). Ushindi huo ulipatikana mwaka wa 1025 KI. Twaaluut aliweza kuanzisha tena dola ya Kiislamu Palestina ikiwa inaongozwa na Bani Israili mpaka kufa kwake mnamo 1004 KI.



Baada ya kuaga dunia tu, hatamu za uongozi zilishikwa na Nabiy Daawuud (‘Alayhis-salaam) ambaye aliipanua dola hiyo kwa kasi kubwa sana. Ni wakati wake ndio mji wa al-Quds uliweza kutekwa. Nabiy Daawuud ('Alayhis-salaam) aliaga dunia mwaka wa 960 KI na kumuacha mtoto wake, Nabiy Sulaymaan ('Alayhis-salaam) katika utawala. Kwa upande wake naye, Nabiy Sulaymaan ('Alayhis-salaam) aliipanua dola hiyo lakini haikufika katika mipaka yake ya sasa. Nabiy Sulaymaan ('Alayhis-salaam) aliimarisha sana dola hiyo, akiwa yeye na babake wameitawala kwa misingi ya Kiislamu. Ilibaki hivyo hadi mwaka wa 922 KI pale naye alipoaga dunia.



Kufariki kwake kuliifanya dola hiyo igawanywe sehemu mbili: Dola ya Yuda (kusini) na Kizeyuni (kaskazini). Bani Israili waligawanyika katika koo zao kwa kiasi ambacho walianza kupigana wao kwa wao (baina dola mbili hizo) na ufisadi ukakithiri kwa kiasi kikubwa sana. Wakati huo ndio alitokea mtu kwa jina la Yuda aliyekiuka mipaka ya Dini na kuasi. Alipata wafuasi wengi na hapo kukazaliwa Dini ya Uyahudi.



Hali hiyo halisi ya mapambano baina ya Bani Israili iliwapelekea dola zao mbili hizo kudhoofika na mwisho katika mwaka wa 722 KI, dola ya Israili ilianguka na eneo hilo kutawaliwa na Wa-Asiria. Nayo dola ya Yuda ilivamiwa na mfalme Nubukadneza wa Babeli (Iraq) mwaka 586 KI, na dola hiyo kuingia katika utawala wa Kibabeli. Wana wa Israili wote walipelekwa uhamishoni huko Iraq kama watumwa. Hapo wengine wao walipata kukimbia na kuingia Ufursi (Iran) ambapo walijaribu kufanya mahusiano ya karibu na utawala wa huko hadi wakamtoa msichana wao kwa ajili ya kuolewa na mfalme wa Iran. Mafungamano hayo yalimfanya mfalme Cyrus wa Iran aunde jeshi kwa usaidizi wa Mayahudi ili kuivamia Palestina na kuwang’oa Wababeli. Cyrus alifanikiwa kuwashinda Wababeli kutoka Palestina na kuwapatia ruhusa Mayahudi kurudi katika nchi hiyo lakini hata hivyo waliorudi hawakuwa wengi, walikuwa wachache sana. Wengi miongoni mwao walibakia katika nchi ya uhamisho wao. Kushinda kwao kulitokea mwaka wa 538 KI. Hata hivyo, Mayahudi wakati wa utawala wa Kifursi hawakuwa na mamlaka wala madaraka yoyote lakini walipatiwa uhuru wa kufanya Ibadah zao bila kufuatiliwa, kuingiliwa wala kubughudhiwa na Wafursi.



Na katika mwaka 332 KI, Palestina ilivamiwa na kutekwa na Warumi wakiongozwa na Alexander kutoka Macedonia. Hata hivyo, Warumi hawakuweza kukaa huko kwa muda mrefu pale wafalme wa kutoka Syria walipovamia sehemu hiyo na kuitia katika utawala wao mwaka 198 KI.



Wayunani nao waliiteka ardhi hiyo mwaka wa 175 Ki na kuitawala. Mayahudi waliweza kujizatiti na kuiteka sehemu hiyo ya ardhi mwaka wa 166 KI na ikabaki mikononi mwao kwa kipindi cha miaka 4. Wasyria walirudi tena kwa kishindo na kuwashinda Mayahudi mwaka wa 162 KI. Hata hivyo, nao Mayahudi walijizatiti kwa mara nyingine tena wakaja wakawang’oa Wasyria kutoka sehemu hiyo mwaka 143 KI. Hapo waliweza kuibakisha ardhi hiyo katika utawala wao hadi mwaka 70 KI.



Kwa miaka saba baada ya huo mwaka wa 70 kukawepo vurugu kubwa hadi mwishowe Warumi wakaweza kuwashinda Mayahudi mnamo 63 KI. Kuanzia mwaka huo hadi mwaka wa 616 BI (Baada ya kuzaliwa kwa Nabii ‘Iysa) Palestina ilibaki katika utawala wa Warumi isipokuwa kile kipindi cha mapinduzi ya Mayahudi cha mwaka 66 BI na 132 – 135 BI. Hata hivyo, katika kipindi cha mapinduzi hayo ya Mayahudi serikali ya Roma ilituma wanajeshi wake wengi ili kuyasagasaga hayo mapinduzi. Ni wakati huo ndio serikali ya Kirumi ilipitisha sheria kuwa mji wa al-Quds haufai kukaliwa na Mayahudi.



Utawala wa Kirumi ulisitishwa kidogo na ule wa Wafursi mwaka wa 616 BI. Lakini utawala wa Wafursi haukukaa kwa muda mrefu kwani katika mwaka wa 624 BI walishindwa na Warumi katika vita ambavyo Allaah Amevizungumzia katika Suwrah Ruwm (30): Aayah 1 – 5. Warumi waliweza kusonga mbele hadi kuuteka mji wa al-Quds katika kipindi cha muda miaka 3 hadi 4.



Kipindi baada ya Sulhu ya Hudaybiyah ndicho kile ambacho Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alianza kupeleka barua kwa mataifa mbali na ndio barua hiyo ikamfikia mfalme wa Warumi, Hiraql (Heraclius) akiwa al-Quds mwaka wa 628 BI. Hapo ndio yalianza mapambano baina ya Waislamu wakiongozwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Warumi. Mji wa al-Quds uliingia mikononi mwa Waislamu wakati wa ukhalifa wa 'Umar bin al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye alifunga safari kwenda kuchukua funguo za mji kutoka kwa kasisi Sophronius mwaka wa 638 BI na hapo miji mingi ya Palestina ikaingia katika Dola ya Kiislamu. Nchi hiyo pamoja na nchi za Shaam zote zilibakia katika utawala wa Kiislamu hadi mwaka wa 1099 BI wakati ambapo Wakristo walikuja kuzivamia ardhi hizo katika vita vya Msalaba.



Watu wa Msalaba kutoka bara Ulaya waliweza kuwaua Waislamu 70,000 ndani ya eneo la Msikiti wa Aqswa. Wakristo waliweza kuitawala ardhi hiyo kwa muda wa miaka 88 ambapo harakati za kuikomboa zilipamba moto. Harakati hizo zilianzishwa na Nuurud-Diyn Zinkiy, mwanae Nuurud-Diyn Mahmuud na baadaye Swalaahud-Diyn Hasan al-Ayyuubiy ambaye aliweza kwa tawfiki ya Allaah kuirudisha Palestina kuwa katika Dola ya Kiislamu mwaka 1187 BI.



Kuanzia mwaka huo wa 1187 BI, Palestina ilibakia kuwa katika Dola ya Kiislamu hadi baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia (1917) ndio Palestina iliingia katika utawala wa Uingereza. Wenyeji wa al-Quds hawakusadiki masikio yao pale walipokusanyika kumsikiliza jemadari Allenby katika uwanja wa al-Quds. Allenby alisema kwa uwazi kabisa: "Leo ndio vita vya Msalaba vimekwisha". Kabla hata ya kuiteka na kuitawala ardhi hiyo, serikali ya Uingereza tayari ilikuwa imewaahidi Wazeyuni kuwa wakiondoka watawazawadia wao kipande hicho cha ardhi. Hayo yanapatikana katika ahadi au tangazo la Waziri wa Nje, Arthur James Balfour ya tarehe 2 Novemba 1917.



Na kweli kwa ahadi yao, Uingereza ilipoondoka Mei 1948 waliwaachia ardhi hiyo Wazeyuni wasiokuwa na mafungamano na ardhi hiyo. Hakika ni kuwa Mayahudi wakati huo na kabla ya hapo hawakuwa na kitambulisho cha aina yoyote ile. Hii ni kwa mujibu wa barua aliyoiandika Dkt Chaim Weizman ya 18 Aprili 1918 kwa mkewe: “Ni masikitiko makubwa kuona kuwa hapa hatuna chochote. Hapa hakuna hata taasisi moja ya Kiyahudi, lakini kumejaa minara (kumaanisha wingi wa Misikiti)”.



Ndugu zetu walianzisha harakati ya kutaka kujikomboa na minyororo ya ukoloni. Harakati ya kwanza ni ile iliyoongozwa na Sh. Abdul-Qaadir al-Qassaam, kutoka Syria mwaka 1925. Mwaka wa 1929 kulikuwa na Intifadha ya al-Buraaq, naye Sh. Al-Qassaam akauliwa mwaka wa 1935 alipokuwa anapambana na jeshi la Muingereza katika maeneo hayo matakatifu.



Kuanzia mwaka wa 1948, kumekuwa na vita baina ya Waarabu na Wazeyuni, lakini Waarabu wakashindwa sana kwa kutokuwa na kuwa wamoja na kauli moja, kutokuwa na mipango mizuri na wakati mwengine kushirikiana na dola haramu ya Kizeyuni. Hata hivyo, sababu kubwa ya kushindwa ni kule Waarabu kuichukulia kuwa hiyo ni kadhiya ya Waarabu tu na kutowajumuisha Waislamu wengineo.





Rejea:



Quds Qadhwiyah Kull Muslim.
Mustwafa Muhammad atw-Twahhaan, Filistwiyn wal Muaamaratul Qubraa.
Al-Islaam wal Qadhwiyatul Filistwiyniyah.
Dkt. Muhsin Muhammad Swaalih, atw-Twariyq ilal Quds.
Dkt. Muhammad Siddiq Qureishi, Zionism and Racism.
Dkt. Mohsen M. Saleh, The Palestinian Issue.
Mawlana Mawdudi, Tafhiymul Qur-aan.
Raymond Caroll, The Palestine Question.
Maryam Jamiylah, Islam versus Ahl al Kitab: Past and Present.
Dkt. Bhatt, Zionism and Internal Security.
Dkt. Muhsin Muhammad Swaalih, al-Haqaaiq al-Arba'una fil Qadhwiyatil Filistwiyniyah.
Tovuti: www.palestine-info.info
 
Afanye Wudhuu Kila Baada Ya Kunyonyesha?
Maswali: Twahara Wudhuu


SWALI:




Napenda kupata uhakika kuhusu wudhuu kamili mimi ninanyonyesha kwani ni lazima kila ninapotaka kutia wudhu kwa ajili ya swala nisafishe chuchu? Au naweza kunyonyesha nikiwa na wudhu kisha nikaendelea kuswali ama mpaka nikatawadhe tena?







JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu kwa swali lako hilo. Hakika ni kuwa kunyonyesha si katika mambo yenye kutengua au kuharibu wudhuu. Hivyo, unapomaliza kunyonyesha na ukawa una wudhuu wako utaweza kwenda kuswali bila kuchukua wudhuu mara ya pili.




Na Allaah Anajua zaidi
 
Akiwa Ameshaoga Kisha ukapita Muda Inabidi Atawadhe ili Kuswali?
Maswali: Twahara Wudhuu
SWALI:




Je waweza toka kuoga vizuri mtu kwako na wakati wa swala umewadia ukaswali bila kutawadha ikiwa una uhakika upo safi japo nyumbani? Natumai waislam wenzangu mmenielewa kidogo nategemea mafanikio kwenu ya kielimu kubwa msinisahau mie ni mwenzenu.










JIBU:




Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.




Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuoga na kupita kwa muda baada ya hapo.




Hakika ni kuwa kuoga na kutawadha ni vitu viwili tofauti. Kuoga ni kujiosha mwili mzima kwa utaratibu unaotaka wewe ilhali kutawadha ni kuosha viungo fulani kwa utaratibu ulioelezewa na Allaah Aliyetukuka katika Qur-aan na Mtume Wake mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Hata hivyo kila jambo ni kwa Niyah, ikiwa umeweka Niyah kuwa kuoga kwako huko kutajumuisha na twahara ya Hadathi ndogo kwa kuwakilisha Wudhuu, basi kuoga kwako kutakuwa kunatosheleza na utaweza kuswali baada ya kuoga kwako.




Kadhalika kuchukua Wudhuu ni jambo bora zaidi na mja hupata ujira kwa kutawadha au kuufanya upya Wudhuu wake.




Ama aliyeoga josho la kishari’ah na akataka kuswali, basi si lazima atawadhe hata kama alikuwa hajatawadha wakati akioga, kwani twaharisho la janaba linaondosha vile vile twaharisho la hadathi ndogo (kutokuwa na wudhuu). Hii ni kwa vile vizuizi vya janaba ni vingi zaidi kuliko vizuizi vya hadathi ndogo. Hivyo basi, kidogo humezwa na kingi.



Imepokelewa na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akisema:

“Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa hatawadhi baada ya kuoga janaba”. Hadiyth Sahihi kwa nyingine: Imetolewa na At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy na Ibn Maajah.



Na katika riwaya nyingine:

“Anaoga na anaswali rakaa mbili, na wala simwoni akifanya wudhuu baada ya kuoga.” Hadiyth Sahihi kwa nyingine: Imetolewa na Abuu Daawuud na Ahmad







Na Allaah Anajua zaidi
 
Anatokwa Na Upepo Wa Mbele Katika Swalaah Je Unabatilisha Wudhuu?
Maswali: Twahara Wudhuu


SWALI:



Assalaam Alaykum Wahmatullah Wabarakatuh ama baada ya maamkizi haya kwanza namshukuru Allah Azza wa Jalla kwa kuniwezesha kuwa hai leo hii na kuweza kuwasiliana nanyi.



Pili shukrani zangu ziende kwenu Alhidaaya kwa kutupa mafunzo yanayohusiana na dini yetu ya Kiislam na Inshaallah Mungu atawalipa malipo mema.



Swali langu ni kuwa ktk mambo yanayotengua udhu kutokwa na upepo sehemu za siri ni mojawapo, sasa hapo ningependa kutolewa utata je ni sehemu moja tu ya nyuma au zote mbili Maana mimi mwenzenu nina matatizo ya gesi niwapo ktk swala sana hutokwa na upepo sehemu ya mbele na hulazimika kukata swala kila baada ya rakaa moja na kwenda kutia udhu ni hivyo hivyo mpaka muda wa swala unakwisha ile swala husika sijaiswali je sheikh nifanyaje na wengine wanasema ukitoka upepo sehemu ya mbele haitengui udhu na wengine wanasema inatenguwa je nishike wapi naomba unitowe wasiwasi Alhidaaya ili angalau niwe na uhakika.







JIBU:



Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.





Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutokwa upepo sehemu ya mbele.



Kutokwa upepo wa mbele kwa wanawake ni jambo ambalo halitengui wudhuu wake. Hivyo ukitokwa na upepo sehemu za mbele basi hakuna tatizo na Swalah yako ni sahihi na huhitaji kwenda kuchukua wudhuu.



Na Allaah Anajua zaidi
 
Ikiwa Mtachezeana Tu Na Kutokwa Manii Inapasa Kukoga Josho?



Alhidaaya.com







SWALI



Assalamu aleikum,

Ninaelewa unaweza au mnaweza kugusana tupu baina ya mke na mume na ikawa hamtokuwa wenye kuhitajika kukoga Janaba.I sipokuwa kama ntatokwa na shahawa.

Swala langu lipo hapo najua vigumu kwa mwanamke kukumbana na umbile lauume au akawa mwenye kucheza nacho kiungo hicho bila kumtoka chochote. Kwa sisi inawezekana (wanaume) sasa tulijaalie suala hili kwa mwanamke ambae anajaribu kumridhisha mumewe, namzungumzia mwanamke hapa kwa sababu ana njia nyingi za kumridhisha mumewe kwa mfano: mkono, mguu kiuno au hata mdomo. Hivo wanaweza kuvitumia na khafla mume akajikuta tiari amekusha.Na mke akawa bado hajatokwa na chochote, Vipi hapa atahitajika kukonga na yeye. In Shaa Allaah liwe lenye kufahamika suala hili.





JIBU:



AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.





Tunavyoliona na kulisoma swali lako ni kwamba halipo wazi na kufuma pale panapotaka kuulizwa. Ni nasaha zetu kwa waulizaji wapendwa wawe ni wenye kuuliza swali moja kwa moja badala ya kuzunguka sana na hivyo hata kueleweka vibaya na wenye kujibu au kutoeleweka kabisa.



Ni muhimu ieleweke kuwa Wanazuoni wote wa Salaf (waliopita) na khalaf (wa sasa) wameafikiana kuwa ni wajibu kujitwaharisha kwa kuoga kwa yeyote yule (mwanamme na mwanamke) anayetokwa na manii akiwa usingizini au akiwa macho au kwa kujamiiana na pia pale mwanamke anapopata ada yake au damu anayotokwa baada ya uzazi. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Umm Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Ummu Sulaym (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) aliuliza: “Ee Rasuli wa Allah! Allaah Haoni haya juu ya ukweli. Mwanamke anaona katika usingizi kama anavyoona mwanamme, je ni juu yake kuoga?” Akasema: “Ndio, anapoona maji” [Al-Bukhaariy na Muslim]



Wametofautiana Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anuhum) kuhusu kuwajibika kuoga kwa kujimai. Miongoni mwao ni wale wenye rai kuwa zinapokutana ngozi mbili zilizotahiriwa basi inakuwa wajibu kwa wote wawili kukoga ikiwa wametokwa na manii au la. Hii ni rai ya Faqihi wakubwa na hii ndiyo kauli ya Jamhuwr (‘Ulamaa wengi).





Rai ya pili ni ile inayosema si wajibu kukoga ikiwa hawakushusha, na hii ni kauli ya baadhi ya watu wa Dhwaahiriy.



Dalili zilizotolewa kwa wenye kuunga kauli ya kwanza ni kama zifuatazo:





1. Amepokea Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema: “Anapokaa mmoja wenu baina ya viungo vinne vya mwili wake (yaani mkewe) na akafanya juhudi (jimai), basi inakuwa wajibu kuoga” [Ahmad na Muslim]





2. Amesema Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Anapokaa baina ya sehemu zake nne na zikakutana ngozi mbili zilizotahiriwa imekuwa wajibu kwao kuoga”.





3. Anahadithia Abu Muwsaa Al-Ash‘ariy (Radhwiya Allaahu ‘anhu): Kulizuka tofauti baina ya kikundi cha Muhajirina na kipote cha Answaariy, na tofauti yao ilikuwa Answaariy wakisema: “Josho la janaba linakuwa wajibu tu pale wanapotokwa na manii”. Lakini Muhajirina wakasema: “Pindi mtu anapostarehe na mwanamke kuoga inakuwa wajibu (ikiwa atashusha au la)”. Abu Muwsaa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema: “Sawa, mimi nitawatosheleza kwa hilo”. Abu Muwsaa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) “Nilisimama na nikaelekea kwa ‘Aishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) na kutaka ruhusa ambayo alinipatia”. Nikamwambia: “Ee Mama wa Waumini! Nataka kukuuliza kuhusu jambo fulani lakini naona haya kukuuliza”. Akasema: “Usione haya kuniuliza kuhusu jambo ambalo unaweza kumuuliza mamako aliyekuzaa, kwani mimi pia ni mama yako”. Kwa hili nikasema: “Ni kitu gani kinachofanya kuoga kunakuwa wajibu kwa mtu?” Akanijibu: “Umekuja kwa mtu mwenye ujuzi wa hilo. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ‘Yeyote mwenye kukaa kwenye sehemu nne (za mwanamke) na sehemu za siri zikagusana baina yao, josho la janaba itakuwa ni wajibu’” [Muslim, Ahmad na Maalik kwa maneno tofauti kidogo]





4. Dalili ya kauli ya pili ni Hadiyth hii: Aliulizwa ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akaambiwa: “Waonaje mtu anapostarehe na mkewe lakini hakushusha (hakutokwa na manii)?” Akajibu: “Atatawadha kama anavyotawadha mmoja wenu kwa ajili ya Swalaah, nimemsikia hayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) [Imenukuliwa na Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy katika kitabu chake Bidaayatul Mujtahid, Mjalada wa kwanza]





Wenye kauli ya kwanza wanafuata Hadiyth ya kwanza na nyenginezo ambao tumezitaja na kusema kuwa hukumu ya Hadiyth inayotumiwa na wenye kauli ya pili imefutwa. Na kutilia mkazo Hadiyth hiyo ya kwanza ni ile Hadiyth aliyopokea Ubayy bin Ka‘ab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: “Hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa ruhusa hiyo mwanzo wa Uislamu kisha akaamrisha kuoga (kwa wenye kujamiiana)” [Abu Dawuud].





Na pia maelezo ya ‘Aishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alipomjibu Abu Muwsaa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuhusu hilo.





Katika Hadiyth tulizozitaja hapo juu sehemu zilizotahiriwa ni utupu wa mwanamme na sehemu za siri za mwanamke. Hivyo, pindi utupu wa mwanaume unapoingia katika sehemu ya siri ya mwanamke, josho la janaba linakuwa wajibu kwa wote wawili. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:



وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا ۚ

Na mkiwa na janaba basi jitwaharisheni. [Al-Maaidah: 6]





Kusherehesha kuhusu mas-ala haya, Ash-Shaafi‘iy amesema: “Katika lugha ya Kiarabu, janaba inamaanisha tendo aina yoyote ya kukutana kimwili baina ya mume na mke, bila kujali kama manii yametoka au la. Ikiwa mtu atasema: “fulani na fulani” wana janaba kwa sababu ya kadhaa na kadhaa’, hii inamaanisha janaba kwa njia yoyote ya kujamiiana baina yao (mume na mke) hata ikiwa hakutakuwa na kushusha. Hakuna anaye kataa kuwa zinaa ambayo ina adhabu maalumu ni kukutana kimwili baina ya wawili hata ikiwa hakuna kutokwa kwa manii”.



Na hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Anatueleza kinaganaga pale Aliposema:



وَلَا جُنُبًا إِلَّا عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىٰ تَغْتَسِلُوا ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا

na wala mkiwa mna janaba isipokuwa mmo safarini mpaka muoge josho. Na mkiwa wagonjwa au safarini au mmoja wenu ametoka msalani au mmewagusa wanawake kisha hamkupata maji, basi mtayammam (ikusudieni) ardhi safi ya mchanga,[An-Nisaa: 43]





Na maana ya:



mmewagusa wanawake:



ni kukutana kimwili baina ya mume na mke kama anavyosema Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma)



Kwa hivyo hapana shaka kuwa ni lazima kuwe na kuingiliana kwa sehemu za siri ili mtu iwe ni wajibu kuoga, lakini ikiwa ni kugusana kama alivyosema muulizaji kwa kucheza cheza au kupigana busu au kushikana shikana au jambo jengine lolote mbali na kuingiliana hakutakuwa na uwajibu kwa mke kukoga ikiwa hatotokwa chochote vilevile na mume kadhalika. Lakini ikiwa mwanaume kama ulivyosema atatokwa na maji ya uzazi basi itabidi akoge. ‘Ulamaa wote wamekubaliana (wameafikiana) katika hili.



Na Allah Anajua zaidi
 
Katia Wudhuu Kisha Akaangalia Sinema Za Uchi Na Kusimkwa, Swalaah Yake?
Maswali: Twahara Wudhuu



SWALI:



Assalamu alayka, ama baada ya salamu mimi nikijana wa kiislamu ambae na penda kujifunza juu ya uislamu, Ustadh napenda kuuliza swali kama ifuatavyo, Kuna dhana kua mtu hutengukwa na udhu endapo atamgusa msichana/ mwanamke ambae anafaa kumuowa (na kwa mwanamume ni kama hivyo) kwa lengo la matamanio, sass swali liko hapa, mtu anapochukuwa udhu na baadae akaingia ktk vibanda vya sinema za ngono, akaangalia kiasi cha misuli yake kupata joto ila hakutokwa na chochote, muda wa swala ulivyo fika alitoka na kuelekea msikitini na akaanza kuswali kama wenzake.



Je? swala ya mtu huyu inakubalika na mtu huyu udhu wake upo?





JIBU:



Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.



Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kusimika wakati wa kutazama sinema ya ngono na kisha kuswali bila kuchukua wudhuu mara nyingine.



Ama kumgusa mwanamke ni makosa kwa mwanamme kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza hilo na kutuambia kuwa ni bora mtu kupigwa msumari wa chuma kuliko kushika mkono wa mwanamke asiye maharimu wake. Kufanya hivyo ni dhambi japokuwa hakuvunji wudhuu ikiwa amemshika bila matamanio.



Ama tukija katika swali lako la pili kuhusu kutazama sinema ya ngono na kusimika katika kutekeleza hilo. Hakika ni kuwa haifai kwa Muislamu – mwanamme na mwanamke kutazama sinema kama hizo na mwenye kutizama anapata dhambi ya kuzini kwani kila kiungo kinazini kama macho na viungo vinginevyo. Na huko pia ni kukaribia zinaa ambayo Allaah Aliyetukuka Ametukataza kufanya hivyo.



Anasema Aliyetukuka:



“Wala msikaribie uzinzi, kwani huo ni uchafu na njia mbaya kabisa” (al-Israa’ [17]: 32).

Ama kusimika (mishipa ya sehemu za siri kusimama) huko hakuvunji wudhuu, kwa hivyo anaweza kuswali bila kuchukua wudhuu kwa mara nyingine. Kwa hiyo, atapata madhambi kwa kutazama sinema ya ngono lakini Swalah yake itakuwa sahihi.



Na Allaah Anajua zaidi
 
Naam ndugu zangu endelea kufuatilia uzi huu utapata faida kubwa sana,nafarijika sana ninapoona views zinaongezeka,na hata zisingeongezeka bado ningefanya kazi hii hata kama wasomaji wangekuwa wachache,kwani ukifanya jambo kwa kutaka radhi za Allah,basi malipo yake yanatoka kwake

Kingine nitajitahidi kuleta kila aina ya elimu hapa ili mradi tupate ufahamu mkubwa wa Uislamu wetu

Tuendelee kuwa pamoja mkono kwa mkono hadi peponi inshaallah
 
TUNAENDELEA NA DARSA LA SWALA YA SWALLALLAHU ALAIH WASALLAM


035-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kusimama (Kuitadili) Kutoka Katika Rukuu Na Anachokisema Ndani Yake




KUSIMAMA (KUITADILI) KUTOKA KATIKA RUKUU NA ANACHOKISEMA NDANI YAKE



Kisha, alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akiunyanyua mgongo wake kutoka rukuu huku akisema:







Sami’a Allaahu liman Hamidah

Allaah Amemsikia mwenye kumsifu([1])





Alimuamrisha pia aliyeswali vibaya kufanya hivyo alipomwambia: ((Swalah ya mtu haitimii hadi… amesema Takbiyr … kisha akarukuu …. Kisha akasema 'Allaah Amemsikia mwenye kumsifu' hadi asimame kwa kunyooka sawa sawa))([2]).



Aliponyanyua kichwa chake, alikuwa akisimama wima na kunyooka sawa sawa hadi kila pingili ya uti imerudi sehemu yake.([3])





Kisha alikuwa akisema huku akiwa amesimama wima:







Rabbanaa Walakal-Hamdu

Ee Mola Wetu! Na Zako Sifa njema na shukrani za dhati.([4])





Aliwaamrisha wanaoswali wote sawasawa wakiweko nyuma ya Imaam au wasiweko nyuma ya Imaam kufanya hivyo, wanapoinuka kutoka rukuu kwa kusema: ((Swalini kama mlivyoniona nikiswali)).([5])



Alikuwa akisema pia: ((Imaam amewekwa kwa ajili ya kufuatwa …, anaposema ' Sami’a Allaahu liman Hamidah’ (Allaah Amemsikia mwenye kumsifu), basi semeni: '[Allaahumma] Rabbanaa Walakal-Hamd'. Allaah Atakusikilizeni, kwani hakika Allaah (تبارك وتعالى) Amesema katika ulimi wa Mtume Wake, (صلى الله عليه وآله وسلم), Allaah Anamsikiliza mwenye kumsifu)).([6])



Pia ametoa sababu ya kuamrisha hivi katika Hadiyth nyingine kwa kusema: ((... kwani mwenye kuwafikiana kauli yake na kauli ya Malaika, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)).([7])





Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akiinua mikono yake katika huku kusimama([8]) kwa namna zilizotangulia kuelezwa katika 'Takbiyra Ya Kufungulia', na husema hali ya kuwa amesimama - kama ilivyotajwa kabla- :



1.





Rabbanaa Walakal-Hamd'

Ewe Mola Wetu! Na Zako sifa njema na shukrani za dhati([9]). Na mara nyingine husema:



2.





Rabbanaa Lakal-Hamd'

Ewe Mola Wetu! Ni Zako sifa njema na shukrani za dhati([10]). Na mara nyingine huongezea matamshi mawili haya tamshi:



Allaahumma

Ee Allaah!([11])





3.







Allaahumma Rabbanaa Walakal-Hamd'

Ee Allaah! Mola Wetu! Na Zako sifa njema na shukrani za dhati.







4.













Allaahumma Rabbanaa Lakal-Hamd'

Ee Allaah! Mola Wetu! Ni Zako sifa njema na shukrani za dhati.





Alikuwa akiamrisha (wengine) kufanya hivi kwa kusema: ((Imaam anaposema 'Sami'a Allaahu Liman Hamidah' semeni: 'Allaahumma, Rabbanaa Lakal-Hamd', kwani mwenye kuwafikiana kauli yake na ya Malaika ataghufuriwa madhambi yake yaliyopita)).([12])



Mara nyingine alikuwa akiongeza:



5.







Mil-as Samaawaati, wamil- al Ardhi, wamil-a maa shi-ita min shayin ba’du

Zimejaa mbingu, na zimejaa ardhi, na zimejaa (sifa Zako) kwa Ulichokitaka baada yake.([13])





Au:



6.









Mil-as Samaawaati, [wamil-a]l Ardhi, wamaa baynahumaa, wamil-a maa shi-ita min shayin ba’du

Zimejaa mbingu na (zimejaa) ardhi na vilivyomo ndani yake sifa Zako, na zimejaa (sifa Zako) kwa Ulichokitaka baada yake.([14])



Mara nyingine aliongeza zaidi:



7.







Ahlath – thanaai wal Majdi, laa maani’a limaa a’twayta, wala mu’twiya lima mana’ta, walaa yanfa’u dhal jaddi minkal jaddu

Wewe ni Mstahiki wa sifa na Utukufu, hapana anayeweza kukizuia Ulichokitoa, wala mwenye kutoa Ulichokizuia, na wala haumnufaishi mwenye utajiri, kwani kwao Wewe ndio utajiri.([15])



Au mara nyingine ziada ilikuwa:



8.







Mil-as Samaawaati, wamil-al Ardhi, wamaa baynahumaa, wamil-a maa shi-ita min shayin ba’du, ahlath-thanaai wal Majdi, ahaqqu maa qaalal ‘abdu, wakullunaa laka ‘abdun, [Allaahumma] laa maani’a lima a’twayta, [wala mu’twiya lima mana’ta], walaa yanfa’u dhal jaddi minkal jaddu

Zimejaa mbingu na zimejaa ardhi na vilivyomo ndani yake sifa Zako, na zimejaa (sifa Zako) kwa Ulichokitaka baada yake, Wewe ni Mstahiki wa Sifa na Utukufu, ni kweli aliyoyasema mja Wako, na sote ni waja Wako, (Ee Allaah) hapana anayeweza kukizuia Ulichokitoa, (na wala kutoa Ulichokizuia), na wala haumnufaishi mwenye utajiri, kwani Kwako Wewe ndio utajiri.([16])



Mara nyingine alikuwa akisema katika Swalah ya usiku:



9.





LiRabbiyl Hamdi, li Rabbiyl Hamdu,

Kwa Mola wangu Sifa zote, Kwa Mola Wangu Sifa zote na shukrani za dhati.



Akikariri hadi kisimamo chake kilikuwa kirefu kama rukuu yake ambayo ilikuwa inakaribiana kwa urefu na kisimamo chake cha mwanzo, na alikuwa amesoma ndani yake Suratul-Baqarah.([17])





10.







Rabbanaa walakal Hamdu, Hamdan Kathiyran Twayyiban Mubaarakan fiyh [Mubaarakan ‘alayhi, kamaa Yuhibbu Rabbunaa Wayar-dhwaa]

Ee Mola wetu! Ni zako sifa njema sifa nyingi, nzuri, zenye Baraka (Baraka juu yake kama Anavyopenda Mola wetu na Kuridhika)([18])





Matamshi haya aliyasoma mtu aliyekuwa akiswali nyuma yake (صلى الله عليه وآله وسلم). Aliyasoma baada ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kunyanyua kichwa chake kutoka kwenye rukuu na alisema: 'Sami'a Allaahu Liman Hamidah'. Alipomaliza Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kuswali, alisema: ((Nani aliyesema hivi sasa?)) Yule mtu akasema: "Ilikuwa ni mimi ewe Mjumbe wa Allaah!" Hivyo Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)akasema: ((Nimewaona Malaika zaidi ya thelathini wanakimbilia kuwa wa kwanza kuyaandika)).([19])






[1] Al-Bukhaariy na Muslim.

[2] Abu Daawuud na Al-Haakim ambaye amesema ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubaliana naye.

[3] Al-Bukhaariy na Abu Daawuud. "Al-Faqaar" ni uti – "mifupa inayounda uti wa mgongo kutoka mwanzo wa shingo hadi kitokono" kama ilivyo katika Kamusi. Taz. pia Fat-h Al-Baariy (2/308).

[4] Al-Bukhaariy na Ahmad.

[5] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.

[6] Muslim, Abu 'Awaanah, Ahmad na Abu Daawuud.



TANBIHI: Hadiyth hii haithibitishi kwamba Maamuma hawashirikiani na Imaam katika kusema: 'Sami'a Allaahu Liman Hamidah'. Pia haithibitishi kuwa Imaam hashirikiani na Maamuuma wanaosema: 'Rabbanaa Walakal-Hamd', yote kwa kuwa Hadiyth hii haikuja kubainisha yale khaswa ambayo Imaam na Maamuma wanapaswa kuyasema katika nguzo hii, bali imekuja kueleza kwamba tahmiyd (Rabbana Walakal-Hamd) ya Maamuma inatakiwa isemwe baada ya tasmiy' (Sami'a Allaahu Liman Hamidah) ya Imaam. Hii imetiliwa nguvu kutokana na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisema tahmiyd hali ya kuwa yeye ni Imaam, na pia kwa ujumla wa kauli yake: ((Swalini kama mnavyoniona nnaswali)) ambayo inaonyesha kwamba Maamuuma waseme anayoyasema Imaam kama (Sami'a Allaahu Liman Hamidah) na mengineo. Wale ndugu waheshimiwa waliorejea kwetu kuhusu mas-ala haya watilie maanani haya, labda katika tuliyotaja kuna yenye kukinaisha. Na yeyote atakayetaka kujadii zaidi mas-ala haya arejee katika makala ya Al-Haafidh As-Suyuutwiy katika mas-ala hii kwenye kitabu chake Al-Haawy lil Fataawa (1/529).



[7] Al-Bukhaariy na Muslim. At-Tirmidhiy amesema ni Swahiyh.



[8] Al-Bukhaariy na Muslim. Huku kunyanyua mikono ni mutawaatir kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), na ni kauli ya Maulamaa wengi na baadhi ya Mahanafi. Taz. Tanbihi za nyuma katika (mlango wa) Rukuu.

[9] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.

[10] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.

[11] Al-Bukhaariy na Ahmad. Na kwa hakika Ibnul-Qayyim (رحمه الله) alikosea (katika nukta hii,) pale alipokanusha katika Zaad Al-Ma'aad usahihi wa riwaayah hii yenye kukusanya baina ya 'Allaahumma' na 'wa' pamoja na kuwepo kwake katika Swahiyh Al-Bukhaariy, Musnad Ahmad, An-Nasaaiy na Ahmad tena kupitia njia mbili (za usimulizi) kutoka kwa Abu Hurayrah, na katika Ad-Daaraimiy kutokana na Hadiyth ya Ibn 'Umar, na katika Al-Bayhaqiy kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriyy, na katika An-Nasaaiy tena kutokana na Hadiyth ya Abu Muusa Al-Ash'ariyy.

[12] Al-Bukhaariy na Muslim. At-Tirmidhiy amesema ni Swahiyh.

[13] Muslim na Abu 'Awaanah.

[14] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.

[15] Jadd: Bahati, Utajiri, Utukufu, nguvu, yaani Mwenye mali, watoto, cheo, uwezo na nguvu katika dunia hii. Hatoweza kunufaika navyo mbele Yako; Anavyomiliki havitomuokoa kutoka Kwako, lakini kitachomnufaisha na kumuokoa ni amali njema pekee.

[16] Muslim na Abu 'Awaanah.

[17] Muslim, Abu 'Awaanah na Abu Daawuud.

[18] Abu Daawuud na An-Nasaaiy kwa isnaad Swahiyh. Imetolewa katika Al-Irwaa (335).

[19] Maalik, Al-Bukhaariy na Abu
 
Wallah mimi binafsi nafaidika sana ninapo soma swala ya Nabii,mfano ilisemwa au ilifahamika kwamba anaposema imamu samia allahu liman hamidah kwamba maamuma sisi twasema tu rabbana lakal hamd tukiwa katika swala ya jamaa,lkn kumbe ile kauli ya swalini kama ninavyo swali inarejea kwamba nasi tuseme vile vile samia aallahu liman hamidah kisha tunasema rabban lakal hamd

Naichukua hii

Pili umeona kwanini Swalaa ni ibada muhumu sana mbele ya Allah,kwasababu nyiradi zote zinamsifia na kumtakasa Allah

Je,watakuwa sawa wenye kuswali mara tano na wasio swali kabisa?

Tafakari!
 
036-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kurefusha Kisimamo Hiki Na Wajibu Wa Kutulia Ndani Yake






KUREFUSHA KISIMAMO HIKI NA WAJIBU WA KUTULIA NDANI YAKE




Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akikifanya kisimamo chake hiki kuwa kirefu, (kama) unaokaribiana na urefu wa rukuu yake kama ilivyotajwa; bali, alikuwa akisimama mara nyingine mpaka msemaji husema: "Amesahau" [kutokana na kusimama kwake muda mrefu]".([1])




Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akiamrisha (wafanye) utulivu humo. Alimwambia aliyeswali vibaya ((…kisha nyanyua hadi unyooke sawa sawa hali ya kuwa umesimama (kila mfupa urudi mahali pake) [katika riwaaya nyingine] Unapoinuka nyoosha uti wako na nyanyua kichwa chako hadi mifupa irudi katika viungo vyake))([2]). Pia alimkumbusha kwamba: ((Swalah ya mtu haitimii kama hajafanya hivyo)).




Na alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Allaah عزوجل Hatazami Swalah ya mja asiyenyosha uti wake wa mgongo barabara baina ya rukuu zake na sijda zake)).([3])













[1] Al-Bukhaariy, Muslim na Ahmad. Imetolewa katika Al-Irwaa (namba 307).

[2] Al-Bukhaariy, Muslim, Ad-Daraamiy, Al-Haakim, Ash-Shaafi'iy na Ahmad.

TANBIHI: Maana ya Hadiyth hii iko dhahiri na wazi, nayo ni utulivu katika kusimama huku. Ama utumiaji wa Hadiyth hii unaofanywa na baadhi ya ndugu zetu katika watu wa Hijaaz na kwengineko kama ni dalili ya kuthibitisha kuweka mkono wa kulia juu ya kushoto katika kusimama, bila shaka iko mbali sana na riwaaya nyingi za Hadiyth. Bali ni hoja ni batili, kwani uwekaji uliotajwa, haukuja utajo wake katika kisimamo cha kwanza katika usimulizi wowote ule wa Hadiyth na katika matamshi yake (Hadiyth). Basi inakuaje kupelekea kutafsiri "mifupa irudi sehemu yake" iliyotajwa katika Hadiyth kuwa ni mkono wa kulia kuukumata mkono wa kushoto kabla ya rukuu?! Hii ingelitumika kama matamshi yote ya Hadiyth yangeasiriwa kumaanisha hivi. Basi vipi kuhusu wanavyohusisha maana iliyobainisha maana tofauti kabisa? Bali kuweka kwake hakuwezi kufahamika kutoka katika Hadiyth kabsia, kwa vile iliyokusudiwa 'mifupa' ni mifupa ya uti wa mgongo, kama ilivyothibitishwa katika Sunnah, "…alikuwa akisimama kwa kunyooka barabara hadi kila mfupa ulirudi sehemu yake."




Mimi binafsi, sina shaka kwamba kuweka mikono juu ya kifua katika kusimama ni uzushi unaopotoa, kwani haikutajwa katika Hadiyth zozote za Swalah juu ya kwamba ni nyingi mno. Ingelikuwa kutendeka huko kuna asili, ingelitufikia japo katika usimulizi mmoja. Juu ya hivyo, hakuna hata Salaf mmoja aliyefanya hivyo, wala hakutaja hata mmoja wa Maulamaa wa Hadiyth nijuavyo.




Hii hailingani na alivyonukuu Shaykh At-Tuwayjiriy katika Makala yake (Uk. 18-19) kutoka kwa Imaam Ahmad (رحمه الله), "Akipenda mtu, anaweza kuacha mikono yake pembeni, au akipenda anaweza kuweka kifuani mwake", kwani Imaam Ahmad hakuhusisha hii kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), bali alisema kutokana na ijtihaad na rai yake mwenyewe. Na rai inaweza kuwa imekosewa. Inapopatikana dalili sahihi dhidi ya uzushi inafuatwa na kuachwa hiyo ya uzushi, mfano kama hii, hivyo kauli ya Imaam yenye mapendekezo yake haikanushi uzushi wake kama alivyoandika Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyah (رحمه الله). Bali naona haya maneno yake ni ishara kwamba Imaam Ahmad hakuchukulia kuwekwa kulikotajwa juu kama ni kumethibitika katika Sunnah, kwani ameruhusu uchaguzi baina ya kutenda na kuacha kutenda. Je, anadhani Shaykh Mheshimiwa kwamba Imaam aliruhusu pia uchaguzi kuhusu uwekaji wa mikono kabla ya rukuu? Hivyo imethibitika kwamba kuweka mikono kifuani katika kusimama baada ya rukuu sio katika Sunnah. Haya ni majadiliano mafupi ya mas-ala haya ambayo yanaweza kujadiliwa katika maelezo zaidi kwa upana, lakini kutokana na uchache wa sehemu hapa, inatosha, na badala yake, ni ubainisho wangu dhidi ya Shaykh (At-Tuwayjiriy) katika Chapa ya tano (Uk. 30) chapa mpya.






[3] Ahmad na Atw-Twabaraaniy katika Mu'jam Al-Kabiyr ikiwa na isnaad Swahiyh.
 
037-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kusujudu, Kwenda Chini Kusujudu Kwa Kutanguliza Mikono






KUSUJUDU




Kisha alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم)akileta Takbiyr na kuporomoka chini kwa kusujudu([1]), na alimuamrisha aliyeswali vibaya afanye hivyo akimwambia: ((Swalah ya mtu ye yote haikamiliki hadi … aseme: 'Sami'a Allaahu Liman Hamidah' na mpaka anyooke sawa sawa, kisha aseme: 'Allaahu Akbar' kisha asujudu mpaka viungo vyake (vitulizane))).([2])




Pia alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) anapotaka kusujudu, huleta Takbiyr, (akitenganisha mikono yake mbali na ubavu wake) kisha ndio husujudu)([3])




Mara nyingine alikuwa akiinua mikono yake anaposujudu.([4])







KWENDA CHINI KUSUJUDU KWA (KUTANGULIZA) MIKONO




Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akitanguliza mikono yake ardhini kabla ya magoti yake.([5])




Alikuwa akiamrisha hivyo kwa kusema: ((Anaposujudu mmoja wenu, basi asiiname kama anavyoinama ngamia, bali atangulize mikono yake kabla ya magoti yake)).([6])




Na alikuwa pia akisema: ((Hakika mikono miwili inasujudu kama uso unavyosujudu, basi anapoweka mmoja wenu uso wake, aweke mikono yake na anapoinuka aiinue )).([7])







Na alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) viganja vyake (akivitanua)([8]) , akibana vidole vyake pamoja([9]) na kuvielekeza Qiblah.([10])




Na pia alikuwa akiviweka viganja vya mikono yake usawa na mabega yake([11]), na mara nyingine usawa na masikio yake([12]). Alikuwa akiimakinisha pua yake na kipaji chake na ardhi.([13])




Alimuambia aliyeswali vibaya: ((Unaposujudu, makinisha sijda yako))([14]). Na katika usimulizi mwingine: ((Unaposujudu, makinisha uso wako na mikono yako, hadi mifupa yako yote itulie mahali pake)).([15])




Na alikuwa pia akisema: ((Hakuna Swalah kwa ye ote yule isiyegusa pua yake ardhi kama kinavyogusa kipaji cha uso)).([16])




Alikuwa pia akimakinisha chini magoti yake na vidole vya miguu yake([17]), na akielekeza ncha za vidole vya mikono yake Qiblah([18]). Aliweka visigino vyake pamoja([19]). Aliweka miguu yake sawa sawa([20]) na aliamrisha hivyo.([21])




Hivi ni viungo saba ambavyo (صلى الله عليه وآله وسلم) alisujudia; viganja viwili vya mikono, magoti mawili, miguu miwili, kipaji cha uso na pua.




Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alivihesabu viungo viwili vya mwisho kama ni kiungo kimoja katika kusujudu kwani alisema: ((Nimeamrishwa kusujudu (katika riwaaya nyingine: Tumeamrishwa kusujudu juu ya viungo saba): Juu ya kipaji cha uso na akaashiria kwa mkono wake([22]), kwenye pua, na mikono, [katika riwaaya nyingine: viganja vya mikono], magoti na vidole vya miguu, na wala tusikunje([23]) nguo na nywele)).([24])




Alikuwa akisema: ((Mja anaposujudu, husujudu pamoja nae viungo saba: uso wake, viganja vya mikono yake, magoti yake, na miguu yake)).([25])




Na kuhusiana na mtu aliyeswali akiwa kafunga nywele zake([26]) kwa nyuma, Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mfano wake hakika ni kama mfano wa mtu anayeswali huku amefunga mikono yake [nyuma ya mgongo wake]))([27]). Akasema pia: ((Hiyo ni tandiko la Shaytwaan)), yaani anapokaa Shaytwaan, akikusudia mafundo ya nywele zake.([28])




Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) hailazi mikono yake([29]), bali alikuwa akiinyanyua mbali na ardhi na kuiweka mbali na mbavu zake kiasi kwamba weupe wa kwapa zake huonekana nyuma yake([30]), na pia kiasi kwamba lau mbuzi mchanga angelitaka kupita chini ya mikono yake angelipita.([31])




Alikuwa akifanya hivyo sana kiasi cha kwamba baadhi ya Swahaba zake walisema: "Tulikuwa tunahisi vibaya kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa sababu ya vile anavyoweka mikono yake mbali na mbavu zake anaposujudu.([32])




Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم)akiamrisha hivyo kwa kusema: ((Unaposujudu, weka viganja vyako (ardhini), na inua viwiko vyako ([33]). Na akisema: Kuweni sawa katika sujuud, na wala asitawanye mmoja wenu mikono yake mtawanyo wa [na katika riwaaya nyingine: kama anavyoitawanya] mbwa))([34]).

Na katika tamshi jingine na Hadiyth nyingine: ((Na wala asilaze mmoja wenu mikono yake kama mlazo wa mbwa))([35]).

Alikuwa pia akisema: ((Msitandaze mikono yenu [kama mtandazo wa mbuai (mnyama wa kuwinda). Lazeni mikono na tandazeni mikono mbali, kwani ufanyapo hivyo, huwa kila kiungo chako kinasujudu nawe)).([36])













[1] Al-Bukhaariy na Muslim.

[2] Abu Daawuud na Al-Haakim ambaye amekiri kuwa ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amewafikiana.

[3] Abu Ya'laa katika Musnad (284/2) ikiwa na isnaad nzuri na Ibn Khuzaymah (1/79/2) ikiwa na isnaad tofauti iliyo Swahiyh.

[4] An-Nasaaiy, Ad-Daaraqutwniy na Mukhlisw katika Al-Fawaaid (1/2/2) ikiwa na isnaad mbili Swahiyh. Kunyanyua mikono huku kumeripotiwa na Maswahaba kumi na Masalaf wengi wameona ni muono Swahiyh. Miongoni mwao ni Ibn 'Umar, Ibn 'Abbaas, Hasan Al-Baswriy, Twaawuus, mtoto wake 'Abdullaah, Naafi' mtumwa wa Ibn 'Umar aliyeachwa huru, Saalim mtoto wa Ibn 'Umar, Qaasim bin Muhammad, 'Abdullaah bin Diynaar na ‘Atwaa. Vile vile 'Abdur-Rahmaan bin Mahdi kasema: "Hii ni kutokana na Sunnah". Imefanywa na Maimamu wa Sunnah; Ahmad bin Hanbal, na imenukuliwa kutoka kwa Maalik na Ash-Shaafi'y.

[5] Ibn Khuzaymah (176/1), Ad-Daaraqutwniy na Al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubali. Hadiyth zote zinazopinga hii sio Swahiyh. Namna hii kumeidhinishwa na Maalik, na ripoti kama hiyo kutoka kwa Ahmad katika At-Tahqiyq ya Ibn Al-Jawzi (108/2). Al-Marwaz pia amenukuu kwa isnaad Swahiyh. Imaam Al-Awazaa'iy katika Masaail yake (1/47/1) akisema: "Nimewaona watu wakitanguliza mikono kabla ya magoti".

[6] Abu Daawuud, Tamaam katika Al-Fawaaid, na An-Nasaaiy katika Sunan As-Sughraa na Sunan Al-Kubraa (47/1) ikiwa na isnaad Swahiyh. 'Abdul-Haqq amekiri ni Swahiyh katika Al-Ahkaam (54/1) na akaendelea kusema katika Kitabu At-Tahajjud (56/1), "Ina isnaad madhubuti kuliko ya nyuma yake". Yaani Hadiyth ya Waail ambayo ni kinyume (magoti kabla ya mkono). Bali Hadiyth ya mwisho, pamoja nakuwa inapinga Hadiyth hii Swahiyh na iliyotangulia, sio Swahiyh katika isnaad wala katika maana, kama nilivyoelezea katika ‘Silsilatul-Ahaadiyth Adh-Dhwa'iyfah’ (Namba. 929) na katika Al-Irwaa (357).

Itambulikane kwamba njia ya kutofautisha na ngamia ni kutanguliza mikono kabla ya magoti kwa sababu ngamia anaanza kutanguliza magoti kwanza; magoti ya ngamia yako katika miguu yake ya mbele kama ilivyobainishwa katika Lisaan Al-'Arab na vitabu vingine vya Kiarabu, na kama ilivyotajwa na Atw-Twahaawiy katika Mushkil Al-Athaar na Sharh Ma'aani Al-Athaar. Pia Imaam Qaasim As-Saraqutwniy (رحمه الله) katika Ghariyb Al-Hadiyth (2/70/1-2), ikiwa na isnaad Swahiyh, kauli ya Abu Huraryah, "Asipige magoti mtu kama afanyavyo ngamia anayekimbia". Akasema Imaam, "Hii ni katika sajdah. Anasema kwamba mtu asijitupe chini kama anavyojitupa ngamia anayekimbia (asiyefugwa) kwa haraka na bila ya utulivu, bali aende polepole chini akitanguliza kuweka mikono yake kwanza, kisha yafuatie magoti. Na maelezo ya Hadiyth marfuu' imesimuliwa kuhusu jambo hili". Kisha akataja Hadiyth za juu.




Ama kauli ya ajabu ya Ibnul-Qayyim, "Maneno haya hayaeleweki na hayafahamiki na mabingwa wa lugha", inajibiwa na vyanzo tulivyovitaja pamoja na vingi vinginevyo ambavyo maelekezo yanaweza kutafutwa. Nimelezea pia kuhusu hii katika kubainisha uongo dhidi ya Shaykh At-Tuwayjiriy ambayo imechapichwa.




[7] Ibn Khuzaymah (1/79/2), Ahmad na Siraaj. Al-Haakim amekiri ni Swahiyh na Adh-Dhahabiy ameikubali. Imetolewa katika Al-Irwaa (313).

[8] Abu Daawuud na Al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubali.

[9] Ibn Khuzaymah, Al-Bayhaqiy na Al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh, na Adh-Dhahaby amekubali.

[10] Al-Bayhaqiy ikiwa na isnaad Swahiyh. Ibn Abi Shaybah (1/82/2) na Siraaj wamehusisha kuelekeza vidole vya mguu katika usimulizi mwingine.

[11] Abu Daawuud na At-Tirmidhiy ambaye amekiri ni Swahiyh, kama alivyokiri Ibn Al-Mulaqqin (27/2). Imetolewa katika Al-Irwaa (309).

[12] Abu Daawuud na An-Nasaaiy ikiwa na isnaad Swahiyh.

[13] Abu Dawuud na At-Tirmidhiy ambaye amekiri ni Swahiyh kama alivyokiri Ibn Al-Mulaqqin (27/2). Imetolewa katika Al-Irwaa (309).

[14] Abu Daawuud na Ahmad ikiwa na isnaad Swahiyh.

[15] Ibn Khuzaymah (1/10/1) ikiwa na isnaad nzuri.

[16] Ad-Daaraqutwniy, Atw-Twabaraaniy (3/140/1) na Abu Nu'aym katika Akhbaar Isbahaan.

[17] Al-Bayhaqiy ikiwa na isnaad Swahiyh, Ibn Abi Shaybah (1/82/2) na Siraaj. Wamehusisha nia kuelekeza vidole vya mguu katika usimulizi mwingine.

[18] Al-Bukhaariy na Abu Daawuud. Ibn Sa'd (4/157) amesimulia kutoka kwa Ibn 'Umar kwamba alipenda kuelekezea Qiblah kila sehemu ya mwili wake awezavyo wakati wa kuswali hata vidole gumba.

[19] Atw-Twahaawiy, Ibn Khuzaymah (Namba 654) na Al-Haakim ambaye amekiri kuwa ni Swahiyh, na Adh-Dhahaby amekubali.

[20] Al-Bayhaqiy ikiwa na isnaad Swahiyh.

[21] At-Tirmidhy na Siraaj. Al-Haakim amekiri ni Swahiyh na Adh-Dhahaby amekubali.

[22] Kuashiria huku kwa mkono kumefasiriwa kutokana na sarufi ya matini ya Kiarabu (Fat-h Al-Baariy).

[23] Yaani kuvikusanya na kuvizuia kutawanyika, kwa maana, kukusanya nguo au nywele kwa mikono katika rukuu na sujuud (An-Nihaayah). Makatazo haya sio katika Swalah, bali hata kabla ya Swalah imekatazwa kama walivyoongeza Maulamaa wengi katika makatazo. Hii imetiliwa nguvu zaidi kwa kuwakataza wanaume kuswali wakiwa wamefunga nywele zao, ambayo inafuatia baadaye.

[24] Al-Bukhaariy na Muslim. Imetolewa katika Al-Irwaa (310).

[25] Muslim, Abu 'Awaanah na Ibn Hibbaan.

[26] Yaani kubanwa juu au kusukwa.

[27] Muslim, Abu 'Awaanah na Ibn Hibbaan. Ibn Al-Athiyr amesema: "Maana ya Hadiyth hii ni kwamba kama nywele zake ingelikuwa zimelegea, zingelianguka ardhini katika sajdah; hivyo mtu atalipwa thawabu za kusujudu nywele. Lakini nywele zikifungwa, zitamaanisha kuwa hazikusujudu, kwani kamlinganisha na mtu ambaye mikono yake imefungwa pingu pamoja, kwa vile haitogusa ardhini kusujudu.

Inaelekea amri hii imewekewa mipaka kwa wanaume pekee na haiwahusu wanawake kama Ash-Shawkaaniy alivyonukuu katika Ibn Al-'Arabi.

[28] Abu Daawuud na At-Tirmidhiy ambaye amekiri ni nzuri. Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan amekiri ni Swahiyh. Taz. Swahiyh Abu Daawuud (653).

[29] Al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

[30] Al-Bukhaariy na Muslim. Imetolewa katika Al-Irwaa (359).

[31] Muslim, Abu 'Awaanah na Ibn Hibbaan.

[32] Abu Daawuud na Ibn Maajah ikiwa na isnaad Hasan.

[33] Muslim na Abu 'Awaanah.

[34] Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na Ahmad.

[35] Ahmad na At-Tirmidhiy ambaye amekiri ni Swahiyh.

[36] Ibn Khuzaymah (1/80/2), Al-Maqdisy katika Al-Mukhtaarah na Al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubali.
 
Allahu akbar kila ukisoma swala ya Nabii unajikuta una makosaa kadhaa

Binafsi nina tanguliza magoti kama ngamia,wallah tupo wengi,kuanzia adhuhur hii natanguliza mikono,je umeona raha ya kusoma ilivyo

Kuna wengi hawasujudu na pua wako wengi sana,baada ya kujua elimu hii,ukiwa msikitini mfahamishe mwingine kwa hekima na adabu

Binafsi huko nyuma nilikuwa naswali bila kuiweka pua ardhini,ndugu mmoja akanifahamisha alhamdulillah

Kwa kifupi ukisoma swala ya Mtume swallallahu alaih wasallam utagundua makosa yako na kujirekdbisha,ndio Mtume alisema ni bora kupata elimu ya mlango mmoja wa ibada na kujua namna ya kufanya ibada hiyo kuliko kuswali swala elfu moja za sunna

Na hii inatupa picha kwanini swala zetu hazituathiri na kutuepusha na maovu na machafu

Allah atufahamishe

Darsa litaendelea inshaallah
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…