Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



050-Majosho Yaliyo Mustahabbu



Alhidaaya.com



1- Kwa ajili ya ‘Iyd mbili



Imepokelewa toka kwa Al-Faakih bin Sa'ad kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alikuwa akikoga wakati wa ‘Iyd el fitr na ‘Iyd el adh-ha. Lakini Hadiyth hii ni Dhwa’iyf sana. [ Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (1316)].



Lakini inaweza kutolewa dalili juu ya kustahabiwa hilo kwa yaliyothibiti toka kwa 'Aliy bin Abi Twaalib na Ibn 'Umar kuwa imepokelewa toka kwa Zaadhaan kuwa mtu mmoja alimuuliza ‘Aliy Allaah Amridhie kuhusu kuoga. Akamjibu akimwambia:

"Oga kila siku ukipenda". Akasema: "Hapana. Kuoga kunakotakikana hasa". Akamwambia: "Siku ya Ijumaa, Siku ya Arafah, Siku ya Kuchinja na Siku ya Fitwr". [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ash-Shaafi'iy katika Musnadi yake (114) na kwa njia yake Al-Bayhaqiy 3/278)].



Na imepokelewa toka kwa Naafi'i kwamba ‘Abdullaah bin 'Umar alikuwa akikoga siku ya ‘Iyd el Fitwr kabla ya kwenda sehemu ya kuswalia. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Maalik (426), na kutoka kwake imepokelewa na Ash-Shaafi'iy katika Al-Ummu (1/231)].



2- Kuzindukana baada ya kupoteza fahamu



Kwani Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alioga baada ya kupoteza fahamu. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (687) na Muslim (418) katika Hadiyth ndefu iliyopokelewa toka kwa 'Aaishah]. Na hii ilikuwa katika maradhi yake aliyofia.

Na Ijma’a imenukuliwa juu ya kusuniwa hilo, na Maulamaa wanasema kwamba akili kukaa sawa baada ya wendawazimu ni sawa na kupoteza fahamu.



3- Kuhirimia Hijjah na ‘Umrah



Ni kwa Hadiyth ya Zayd bin Thaabit kwamba yeye alimwona Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) amebadili nguo kwa ajili ya kuhirimia na kisha akakoga.[Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (831). Na tizama Al-Irwaa (149)].



Na mwanamke hata kama atakuwa na hedhi au nifasi ataoga, kwani Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alimwamrisha Asmaa bint 'Umays akoge wakati alipojifungua katika Hijjah. [Hadiyth Swahiyh: Itakuja katika mlango wa Hijjah]. Haya yataelezwa zaidi katika mlango ha Hijjah.



4- Kuingia Makkah



Ni kwa Hadiyth ya Ibn 'Umar kwamba yeye alikuwa haingii Makkah ila hulala Dhiy Tuwaa mpaka asubuhi, halafu hukoga, kisha huingia Makkah mchana. Inaelezewa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alilifanya hilo.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1573) na Muslim (1259)].



5- Baada ya kila jimai kama atarudiarudia



Ni kwa Hadiyth ya Abi Raafi'i kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) aliwazungukia wakeze usiku mmoja huku akikoga kwa huyu na kwa yule. Nikasema: "Ee Rasuli wa Allaah! Kwa nini usikoge mara moja tu"?

Akasema:

((هذا أزكى وأطيب وأطهر ))

((Hili ni utakaso zaidi, jema zaidi na twahara zaidi)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (216) na Ibn Maajah (560)].



6- Baada ya kumwosha maiti (kama Hadiyth ni Swahiyh)



Imepokelewa Hadiyth Marfu’u toka kwa Abu Hurayrah:

(( من غسل ميتا فليغتسل ))

((Mwenye kumwosha maiti, basi akoge)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (3162), At-Tirmidhiy (993) na Ibn Maajah (1461). At-Tirmidhiy, Ibn Hajar na Al-Al Baaniy wamesema ni Hasan. Tizama Al-Irwaa (1/174). Lakini inavyoelekea inahitaji ukaguzi hivi, kwani Hadiyth imekosolewa].



7- Kwa mwenye damu ya istihaadhwah kwa kila Swalaah



Amri ya kukoga kwa mwanamke mwenye damu ya istihaadhwah wakati wa kila Swalaah imekuja katika mjumuiko wa Hadiyth Dhwa’iyf. [Irejee katika Jaami'u Ahkaam An-Nisaa (1/230-237)].



Lakini imethibiti toka kwa Aaishah akisema: “Ummu Habiybah alisumbuliwa na damu ya istihaadhwah kwa muda wa miaka saba. Akaja kumuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu Alayhi wa Aaalihi wa Sallam) kuhusiana na tatizo hilo. Rasuli akamwamuru aoge, na akamwambia kwamba huo ni mshipa. Naye akawa anaoga kwa kila Swalaah.”[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (327) na Muslim (334)].



Ash Shaafi’iy Allaah Amrehemu anasema: “Alilomwamuru Rasuli ni kuoga na kuswali tu, kwani katika maneno yake hakuna amri yoyote ya kuoga kwa kila Swalaah. [Amri hii ya kuoga ni mutwlaq, haionyeshi kukariri. Huenda Ummu Habiybah alifahamu kwamba ametakiwa kufanya hivyo kwa dalili fulani, hivyo akawa anaoga kila anapotaka kuswali. (Fat-h Al-Baary (1/509)].



Na sina shaka yoyote kwamba kuoga kwake kulikuwa ni kwa kupenda kwake mwenyewe kinyume na alivyoamrishwa, na mlango wa hilo uko wazi kwake”. [Sunan Al-Bayhaqy (1/349)].



Ninasema: “Hii ni kauli ya Jamhuri ya Maulamaa toka Salafu na waliokuja baada yao kwamba mwanamke mwenye damu ya istihaadhwah si lazima aoge kila Swalaah”.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



051-Niya Ni Sharti Ya Kusihi Kukoga



Alhidaaya.com





Hii ni kwa vile kukoga ni ‘ibaadah isiyojulikana ila kupitia sharia, na kwa ajili hiyo, niya imekuwa ni sharti humo. Niya yenyewe, ni moyo kuazimia tendo la kukoga ikiwa ni kufuata na kuitii Amri ya Allaahu (Subhaanahuu Wata'alaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam). Allaahu (Subhaanahuu Wata'alaa) Anasema:

((وما أمروا إلا ليعبدوا الله مخلصين له الدين))

((Na hawakuamrishwa ila kwa ajili ya kumwabudu Allaah wakimtakasia Yeye Dini)). [Al-Bayyinah (98:5)]



Ikhlaasw ni kusudio la kujikurubisha kwa Allaahu (Subhaanahuu Wata'alaa) na kumwelekea Yeye tu katika kutekeleza yale Aliyoyafaradhisha kwa Waja Wake Waumini.

Na Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) anasema:

((إنما الأعمال بالنيات))

((Hakika amali ni kwa niya)).[Hadiyth Swahiyh: Imekwishatajwa].

Na hili la kukoga ni amali. [Angalia Mlango wa ((Niya Ni Sharti Ya Kuswihi Wudhuu uk.40))].
 
Naam ndugu zangu katika imani wale tunao fuatilia darsa wallah tunaongeza sana maarifa na Allah azidi kutufahamisha zaidi

Ningependa kugusia kipengele cha nia kama post ya mwisho ilivyoeleza,hakika nia mahala pale ni moyoni

Na inasemwa haijawi kushuhudiwa Mtume swallallahu alaih wassallamu akitamka nia makhususi mdomoni kwake,kwakuwa nia ni kukusudia au kuazimia kufanya jambo fulani nalo huwa ndani ya moyo wako,na hiyo ndio nia

Nikupe mfano,hivi ikiwa kesho ni jumapili unataka kwenda kariakoo,je huwa unakusudia ndani ya moyo kuwa kesho utaenda kariakoo au huwa unasema kwa sauti "kesho natia nia ya kwenda kariakoo"

Jibu ni kwamba huwa inapita tu moyoni kwako si ndio? Naam hata nia nayo ni hivyo hivyo

Mfano wa pili hivi ukisikia adhana ya adhuhur,si unajua kwamba unaenda kuswali swala ya adhuhur? Kama unajua kwamba unaenda kuswali swala ya adhur basi hiyo ndio nia yako

Kwahiyo inasemwa ukishafika pale msikitini pakishakimiwa wewe wala hauna haja ya kuleta mambo mengi,sema allahu akbar ingia ndani ya swala

Hata mtume hakuwahi kusikika akitamka nia kwa tamko lolote lile,kilichobaki kwetu ni mazoea ambayo yanatupa shida


Mfano mwingine unapoenda kutia udhu si ina maana ulishakusudia kutia udhu ndio maana umeenda pale kwenye bomba,au umechota maji yako,na hiyo ni nia ishapita tayar,sana sana utasema bismillah kama sunna

Uislamu ni mwepesi sana ila tunautia uzito,yani huko mashambani hata hapa mjini watu wamezoeshwa kutiliwa nia wakati wa mfungo wallah huu ni msiba

Na huko mashambani watu hawafungi mpaka waende kwa sheikh eti wakanuizwe,tunayafanya mambo yawe magumu bila sababu

Unapoenda kuoga janaba ina maana ishapita moyoni mwako kwamba unajanaba na unaenda kuoga kujitakasa,na hiyo ndio nia yako

Na kwa nifasi nayo iko hivyo hivyo

Umeona ni simpo tu

Darsa litaendelea......
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



052-Nguzo Ya Kuoga



Alhidaaya.com





Ni kukieneza kiwiliwili chote kwa maji. Uhalisia hasa wa kuoga ni kububujisha maji kwenye kiwiliwili chote na kufika maji hayo katika kila unywele na ugozi. Na hili limethibiti katika Hadiyth zote zinazoelezea kuhusu picha ya namna alivyokuwa akikoga Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam). (Hadiyth hizi nitazielezea hivi karibuni). Na kati ya Hadiyth hizo ni Hadiyth ya ‘Aaishah (Allaah Amridhie):

((..kisha anamimina maji juu ya kiwiliwili chake chote)). [Hadiyth Swahiyh: Matni na takhriyj yake zitakuja karibu].



Al-Haafidh amesema katika Al-Fat-h (1/361):

“Usisitizo huu (wa kusema “kiwiliwili chake chote”) unaonyesha kwamba yeye alieneza kiwiliwili chake chote kwa josho”.



Na katika Hadiyth ya Jubayr bin Mutw-‘am kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) amesema:

((أما أنا، فآخذ ملء كفي ثلاثا فأصب على رأسي، ثم أفيض بعد ذلك على سائر جسدي))

((Ama mimi, huchukua ujazo wa kiganja changu mara tatu, kisha namimina juu ya kichwa changu, kisha nabubujisha baada ya hapo juu ya kiwiliwili changu chote)). [Hadiyth Swahiyh: Ahmad ameikhariji kwa tamko hili (4/81), na katika Al-Bukhaariy (254) na Muslim (327) kwa ufupisho].



Lingine linaloonyesha kuwa nguzo pekee ya kukoga ni kukieneza kiwiliwili chote kwa maji, ni Hadiyth ya Ummu Salamah aliyesema:

“Nilisema: Ee Rasuli wa Allaah! Mimi ni mwanamke ninayesuka sana nywele, je, nizifumue wakati wa kukoga janaba?” Akasema:

(( لا، إنما يكفيك أن تحثي على رأسك ثلاث حثيات، ثم تفيضين عليك الماء فتطهرين))

(( Hapana, bali yakutosha kumwagia kichwa chako mateko matatu, kisha utajimiminia maji utwaharike)).



Ama kusugua viungo, kusukutua na kupaliza maji wakati wa kukoga, kauli yenye nguvu inasema kuwa hayo yote ni Sunnah kama tutakavyoeleza mbeleni. Na haya ndiyo madhehebu ya Jamhuri.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



053-Yaliyosuniwa Wakati Wa Kukoga (Picha Ya Josho Kamili)



Alhidaaya.com





Mhimili katika mlango huu ni Hadiyth mbili:



1- Hadiyth ya ‘Aaishah (Allaah Amridhie) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alipokuwa akikoga janaba:

“Alianza, akaiosha mikono yake miwili, kisha akatawadha kama anavyotawadha kwa ajili ya Swalaah, kisha huingiza vidole vyake katika maji, kisha hufikicha kwavyo mizizi ya nywele zake, halafu humimina [Na katika riwaya nyingine: mpaka anapopata uhakika kwamba ameshatotesha ngozi yake, humimina] juu ya kichwa chake mateko matatu kwa mikono yake, kisha humimina maji juu ya ngozi yake yote”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (330), Abuu Daawuud (251), An-Nasaaiy (1/131), At-Tirmidhiy (105) na Ibn Maajah (603)].



2- Hadiyth ya Maymuuna (Allaah Amridhie). Alisema:

“Nilimtengea Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) maji ya kukoga, akaosha mikono yake mara mbili au tatu, kisha akajimiminia maji kwenye mkono wake wa kushoto kwa kutumia mkono wake wa kulia akaosha utupu wake [Na katika riwaya nyingine: utupu wake pamoja na uchafu ulioipata], kisha alisugua mkono wake kwenye udongo au ukutani [kisha akauosha], kisha alisukutua na kupaliza, akauosha uso wake, mikono yake miwili na kichwa chake, kisha alijimiminia maji juu ya kiwiliwili chake, kisha alisimama kando, akaosha makanyagio yake mawili, nikampa kitambaa, kisha akaambatisha mkono wake hivi na wala hakukitaka”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (266) na Muslim (317)].



Ninasema:

“Kutokana na Hadiyth hizi mbili na nyinginezo, tunahitimisha tukisema kuwa, linalopendeza ni kuwa kuoga janaba kunatakikana kuwe katika picha ifuatayo:



1- Kuosha mikono miwili mara tatu kabla ya kuiingiza katika chombo au kuanza kukoga kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah:

((Alianza, akaiosha mikono yake miwili….)).



Na katika tamko la Muslim (317) kwa Hadiyth ya Maymuuna:

((Akaosha viganja vyake viwili mara mbili au mara tatu, kisha akaingiza mkono wake katika chombo…)).



Al-Haafidh amesema katika Al-Fat-h (1/429):

“Inawezekana kuwa aliviosha kwa ajili ya kuvisafisha uchafu. Pia yawezekana kuwa huo ni mwosho wa kisharia wakati wa kuamka usingizini”.



2- Kuosha uchafu wa utupu kwa mkono wa kushoto kutokana na maelezo ya Hadiyth ya Maymuunah. Ama kuukamata utupu kwa mkono wa kulia, hilo ni makruhu kutokana na Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam):

((إذا بال أحدكم فلا يأخذن ذكره بيمينه، ولا يستنجى بيمينه، ولا يتنفس في الإناء))

((Anapokojoa mmoja wenu, basi asiikamate kabisa dhakari yake kwa mkono wake wa kulia, wala asistanji kwa mkono wake wa kulia, na wala asipumulie ndani ya chombo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (154) na Muslim (267)].



3- Kuosha mkono (baada ya kuosha utupu) na kuusafisha kwa sabuni au mfano wake kama mchanga. Maymuuna katika Hadiyth yake anasema:

((Kisha akaambatisha mkono wake ardhini akaupangusa kwa udongo, kisha akuosha….)).



Na katika tamko jingine:

((Kisha akapiga ardhi kwa mkono wake wa kushoto, akausugua msuguo wa nguvu)). [Hii ni kauli ya Muslim (317)].



An-Nawawiy katika Sharh Muslim (3/231) anasema:

“Ni kwamba inapendeza kwa anayestanji kwa maji anapomaliza, aoshe mkono wake kwa udongo (mchanga) au “ashnaan” (mada mfano wa sabuni) au ausugulie na mchanga au ukuta ili usafike vizuri kutokana na uchafu”.



4- Kutawadha wudhuu kamili kama anavyotawadha kwa ajili ya Swalaah. Na hili limethibiti katika Hadiyth za ‘Aaishah na Maymuuna.



Al-Haafidh katika Al-Fat-h (1/429) anasema:

“Inawezekana kuwa kuanza kutawadha kabla ya kukoga, ni Sunnah ya kando, kwa kuwa ni lazima kuviosha viungo vya wudhuu pamoja na kiwiliwili chote wakati wa kukoga. Na inawezekana kuwa badala ya kuviosha tena wakati wa kukoga, itatosheleza kuoshwa kwake wakati wa kutawadha. Na yeye ametanguliza kuosha viungo vya wudhuu kwa ajili ya kuvipa hadhi yake, na ili mwenye kukoga apate picha ya twahara zote mbili; kubwa na ndogo”.



Ninasema:

“Kutawadha kabla ya kukoga ni Sunnah kwa Jamhuri ya Maulamaa kinyume na Abuu Thawr, Daawuud na Adh-Dhwaahiriy”. [Fat-h Al-Baariy (1/426), Al-Majmu’u (1/186) na Al-Istidhkaar (3/59)].



Faida Mbili



Faida Ya Kwanza



Hukmu Ya Kusukutua Na Kupaliza Maji Puani Wakati Wa Kukoga

Katika mlango wa wudhuu, tulieleza kwamba Maulamaa wamehitilafiana katika kauli nne kuhusu kusukutua na kupaliza maji puani wakati wa kutawadha. Nasi tulitilia nguvu kwamba ni lazima kusukutua na kupaliza maji puani.



Ama kukoga, Ath-Thawriy, Abuu Haniyfah na wenzake pamoja na Ahmad, Atwaa na Ibn Al-Mubaarak ambao madhehebu yao ni mashuhuri, msimamo wao ni kuwa kusukutua na kupaliza maji puani ni lazima wakati wa kukoga janaba. [Angalia marejeo ya mas-ala katika Nguzo za Wudhuu].



Na kati ya dalili zao ni:



1- Hadiyth iliyopokelewa Marfu’u:

((المضمضة والإستنشاق ثلاثا للجنب فريضة))

((Kusukutua na kupaliza maji puani ni mara tatu, kwa mwenye janaba ni fardhi)). [Hadiyth Mawdhu’u (ya kutungwa): Imefanyiwa "ikhraaj" na Ad-Daara Qutwniy (1/115). Pia imepokelewa Mursal. Tazama kitabu cha Naswb Ar-Raayat (1/87)].



2- Hadiyth iliyopokelewa Marfu’u:

((من ترك موضع شعرة من جسده لم يغسلها فعل به كذا وكذا من النار))

((Mwenye kuacha sehemu ya unywele katika kiwiliwili chake asiuoshe, ataadhibiwa vibaya motoni)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (249), Ibn Maajah (599) na Ahmad (1/94). Angalia Adh Dha’iyfah (930)].



3- Hadiyth iliyopokelewa Marfu’u:

((أداء الأمانة غسل الجنابة، وتحت كل شعرة جنابة))

((Kutekeleza amana ni kukoga janaba, na chini ya kila unywele kuna janaba)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa "ikhraaj" na Ibn Maajah (598) kwa Sanad Dhwa’iyf. Tazama At-Talkhiysw (1/142)].



Hadiyth zote hizi ni Dhwa’iyf na hazifai kutolewa dalili.



4- Ni kitendo chake Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) kilichoelezewa katika Hadiyth ya Maymuuna (kwa kiashirio wazi), na katika Hadiyth ya ‘Aaishah (iliyojumuisha wudhuu), hayo yanabainisha Kauli Yake Allaahu (Subhaanahuu Wata'alaa):

(( وإن كنتم جنبا فاطهروا ))

(( Na mkiwa na janaba, basi jitwaharisheni)). [Al-Maaidah (5:6)].



5- Ni kwamba kuosha kiwiliwili chote ni wajibu, na uso ni sehemu ya kiwiliwili. Na kwa hivyo, imekuwa ni lazima kusukutua na kupaliza maji puani, kwani mawili haya ni sehemu ya uso kama tulivyosema katika mlango wa wudhuu.



Ama waliosema kuwa hilo ni Sunnah, nao ni Maalik, Al-Layth na Al-Awzaa’iy ambao ni Jamhuri, dalili zao ni:



1- Kutawadha wakati wa kukoga si wajibu [kama ilivyotangulia], na kusukutua na kupaliza maji puani ni katika mambo yanayoambatana na wudhuu. Na kama wudhuu haupo, basi yanayoambatana nao pia hupomoka. [Fat-h Al-Baariy (1/443)].



2- Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) kuyafanya mawili hayo, hakuonyeshi kuwa ni wajibu kwa kuwa tu amefanya, bali ni kwa kuonyesha kuwa hayo ni mazuri na yanapendeza kuyafanya. Nayo hayaonyeshi wajibu ila ikiwa ni ubainisho wa mjumuiko uliofungamana na wajibu. Na hapa mambo si hivyo. [Fat-h Al-Baariy (1/432)].



3- Ni kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) kwa Abuu Dharri wakati alipomuuliza kuhusu janaba iliyompata akakosa maji:

(( الصعيد الطيب وضوء المسلم، وإن لم يجد الماء عشر حجج، فإذا وجد الماء فليمسه بشرته))

((Mchanga twahara ni kitwaharisho kwa Muislamu hata kama hakupata maji kwa miaka kumi. Na akiyapata maji, basi ayagusishe ngozi yake)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (124), Abuu Daawuud (233), An-Nasaaiy (1/171) na wengineo kwa njia tofauti. Yenye nguvu zaidi ni ya Abuu Qulaabah toka kwa ‘Amri bin Bijdaan toka kwa Abuu Dharri ikiwa Marfu’u kama ilivyo katika Al-‘Ilal ya Ad Daaraqutwniy (1113), Ibn Abiy Haatim (1/11) na ‘Amri ambaye hajulikani. Hadiyth hii ina ushahidi toka kwa Abuu Hurayrah, na pana mvutano wa yeye kuifanya Hasan. Lakini katika Al-Irwaa, Al-Al Baaniy amesema kuwa ni Swahiyh].



Wamesema: “Al-Basharah” ni ngozi ya nje, na kwa hivyo haihusiani na kusukutua na kupaliza maji.



4- Hadiyth ya Jubayr bin Mutw-am. Amesema: “Tulielezana kuoga janaba mbele ya Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) naye akasema:

(( أما أنا، فآخذ ملء كفي ثلاثا فأصب على رأسي، ثم أفيض بعد ذلك على سائر جسدي))

((Ama mimi, huchukua ujazo wa kiganja changu mara tatu, kisha namimina juu ya kichwa changu, kisha nabubujisha baada ya hapo juu ya kiwiliwili changu chote)). [Hadiyth Swahiyh: Imeelezewa karibuni].



Na katika tamko:

((أما أنا فأحثي على رأسي ثلاث حثيات من ماء فإذا أنا قد طهرت))

((Ama mimi, basi humwagia mateko matatu ya maji juu ya kichwa, na hapo nakuwa nimetwaharika)). [Ash-Shawkaaniy amenukuu toka kwa Al-Haafidh kauli yake: “Neno lake (Basi hapo ninakuwa nishatwaharika), halina asili yoyote sawasawa katika Hadiyth Swahiyh au Hadiyth Dhwa’iyf].



Na tamko hili halifai.



5- Ni neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) kwa Ummu Salamah:

(( إنما يكفيك أن تحثي على رأسك ثلاث حثيات من ماء، ثم تفيضين عليك الماء، فإذا أنت قد طهرت))

(( Hakika yakutosha kumwagia kichwa chako mateko matatu ya maji, kisha utajimiminia maji, na hapo unakuwa umetwaharika)).



Ninasema:

“Lau si Hadiyth ya mwisho ya Ummu Salamah, basi wajibu wa kusukutua na kupaliza maji puani ungelikuwa na sauti ya nguvu. Lakini Hadiyth ya Ummu Salamah, inaonyesha kwa kielelezo cha nguvu kwamba kiasi kitoshelezacho katika kukoga ni kile kilichotajwa, na hakukutajwa humo kusukutua wala kupaliza maji. Na wala haisemwi: “Mawili hayo yanaingia katika neno lake (kisha unajimiminia maji), kwani maana ya kumimina, haiyagusi mawili haya kama inavyoonekana wazi.



Hivyo basi, madhehebu ya Jamhuri inayosema kuwa kusukutua na kupaliza ni jambo mustahabb na wala si wajibu wakati wa kukoga, ndiyo yenye nguvu kwangu. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.



Faida Ya Pili



Ni Wakati Gani Miguu Miwili Huoshwa?



Lililo wazi kutokana na Hadiyth ya Maymuuna ni kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alikawisha kuosha makanyagio yake mawili mpaka pale alipomaliza kukoga.



Al-Bukhaariy katika tamko lake anasema:

“Alipomaliza kukoga, aliosha miguu yake”.



Ama Hadiyth ya ‘Aaishah, hakuna kingine humo zaidi ya kuwa tu Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alikuwa akitawadha kabla ya kukoga. [Katika riwaya ya Muslim (316) kutoka kwa ‘Aaishah, mwishoni mwa Hadiyth hii anasema: “..kisha akamimina juu ya kiwiliwili chake chote, kisha akaosha miguu yake miwili”. Ni ziada ambayo haikuhifadhiwa. Tizama ‘Ilal Muslim ya Hirawiy (69), Attamhiyd (22/93) na Fat-h Al-Baariy ya Ibn Rajab (1/234)]. Na kwa ajili hiyo, Maulamaa wamekuwa na mielekeo minne kutokana na Hadiyth hizi mbili: [Fat-h Al-Baariy ya Ibn Hajar (1/362), Al-Mughniy (1/288), Sharh Al-‘Umdah (1/371) na Al-Khilaafiyaat cha Al-Bayhaqiy (2/425)].



1- Ni mustahabbu kukawisha kuosha miguu miwili wakati wa kukoga kutokana na Hadiyth ya Maymuuna. Haya ni madhehebu ya Jamhuri.



2- Ni kutawadha wudhuu kamili kabla ya kukoga kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah. Sababu ni kuwa Hadiyth hii inaelezea alivyokuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) akifanya aghalabu kinyume na Hadiyth ya Maymuuna ambaye ameelezea josho moja tu. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na riwaya ya Maalik na Ahmad.



3- Mtu anakhiyarishwa, ima kuanza kuosha miguu miwili pamoja na wudhuu au kuiosha mwishoni. Hii ni riwaya ya Ahmad.



4- Kama mtu anaoga sehemu isiyo safi, basi ataiosha miguu yake mwishoni. Na kama si hivyo, basi ataiosha mwanzoni wakati akitawadha. Haya ni madhehebu ya Maalik.



Ninasema:

“Mwelekeo huu wa mwisho ndio wenye nguvu zaidi. Lakini pamoja na yote hayo, jambo hili lina wasaa na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.



5- Ni kumimina maji juu ya kichwa mara tatu mpaka yafike katika mashina ya nywele.



6- Ni kuanzia upande wa kulia wa kichwa kisha upande wa kushoto.



7- Kufikicha (kusugua) nywele. Hadiyth ya ‘Aaishah inasema:

((Kisha hufikicha nywele zake kwa mkono wake mpaka anapohakikisha kuwa ameilowesha ngozi yake, hapo humiminia juu yake maji mara tatu..)).



Imepokelewa vile vile toka kwa ‘Aaishah akisema:

(( Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alipokuwa akikoga janaba, hutaka aletewe kitu kama “alhilaab”, huikamata kwa kiganja chake, kisha huanza kwa upande wake wa kulia wa kichwa, kisha upande wake wa kushoto….)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (258) na Muslim (318)].

“Alhilaab” ni chombo kinachojaa mkamuo mmoja wa maziwa ya ngamia (Ma’alim As-Sunan) cha Al-Khattwaabiy (1/69).



Na imepokelewa toka kwa ‘Aaishah vile vile akisema: (( Mmoja wetu alipokuwa akipatwa na janaba, huchukua kwa mkono wake mateko matatu juu ya kichwa chake, kisha huchukua maji kwa mkono wake juu ya upande wake wa kulia na kwa mkono wake mwingine juu ya upande wake wa kushoto. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (277)].



Faida



Je, Ndevu Huasuliwa Wakati Wa Kukoga Janaba?



Jamhuri ya Maulamaa ambao ni Maalik, Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy na Ibn Hazm wamesema: “Haimlazimu kuziasulia, bali ni jambo mustahabbu”. [Al-Muhalla (2/33), Al-Awsatw (2/127) na At-Tamhiyd (22/95)].



Ninasema:

“Hili mahala pake ni pale yanapokuwa maji yanafika hadi kwenye ngozi, na kama si hivyo, basi ni lazima kuziasulia ili kuyafikisha maji ndani yake. Na la akiba zaidi kwa vyovyote, ni kuziasulia ndevu zake kutokana na ujumuishi wa neno la ‘Aaishah: ((basi huasulia kwayo mashina ya nywele zake”.



8,9- Kumimina na kuyaeneza maji katika kiwiliwili chote kwa kuanzia upande wa kulia kisha wa kushoto.



Kumimina na kueneza maji katika kiwiliwili kizima ni jambo lililothibiti katika Hadiyth zote zinazotoa picha ya josho lake Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam).

Ama kuanzia kulia, ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema:

((Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) kulikuwa kunampendeza kuanza kwa kulia akivaa viatu, akitembea, akijitwaharisha na katika mambo yake yote)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (168) na Muslim (268)].



Faida Mbili



Faida Ya Kwanza



Kujimiminia Maji Kiwiliwili Chote Kunakuwa Ni Mara Moja Tu.



Na hili liko wazi katika muktadha wa Hadiyth mbili za ‘Aaishah na Maymuuna. Ndani ya Hadiyth hizi, pametajwa kuoshwa mara tatu mikono miwili na kichwa. Ama kiwiliwili kizima, ‘Aaishah anasema:

((Kisha anamiminia juu ya kiwiliwili chake chote)).



Na Maymuuna anasema:

((Kisha alimiminia juu ya kiwiliwili chake)).



Na Ibn Batwaal amesema: [Fat-h Al-Baariy (1/439)].

“ Na kwa vile suala halikuainishwa kwa idadi, basi lichukuliwe chini ya ilivyotajwa, nayo ni mara moja, kwani asli ni kutozidisha juu yake”.



Ninasema:

“Na hili ni mashuhuri katika madhehebu ya Ahmad na masahibu wa Maalik. Shaykh wa Uislamu amelikhitari hili. Na Jamhuri wamestahabbu kufanya mara tatu”.



Faida Ya Pili



Hukmu Ya Kusugua Viungo Vya Kukoga [Al-Muhalla (2/30), Al-Istidhkaar (3/63), Al-Mughniy (1/290), Bidaayat Al-Mujtahid (1/55) na As-Sayl Al-Jarraar (1/113)]

Maulamaa wamekhitalifiana:



Je, ni sharti kupitisha mkono katika kiwiliwili kizima wakati wa kukoga? Au yatosha kumimina maji tu katika kiwiliwili chote hata kama mtu hakupitisha mkono wake katika kiwiliwili chake?

Au kwa maana nyingine tunasema: Je, kukoga kunatimu kwa kujimiminia maji tu au ni lazima pia kusugua juu ya kitu?



Jamhuri ya Maulamaa (kinyume na Maalik na Al-Mazniy) wanaona kuwa hakuna ulazima kusugua, bali ni mustahabbu. Na lau kama mtu atajimwagia maji mwenyewe katika kiwiliwili chake, basi atakuwa ametekeleza aliyowajibishwa na Allaahu (Subhaanahuu Wata'alaa). Hali kadhalika, akipiga mbizi majini na maji yakaupata mwili wake wote.



Dalili za makundi mawili katika suala hili ni zile zile zilizokwishatangulia kuelezewa katika hukmu ya kusukutua na kupaliza maji puani.



Na lililo wazi ni kuwa kusugua ni jambo mustahabbu na wala si wajibu.



Na Hadiyth ya ‘Imraan ibn Haswiyn – pamoja na Hadiyth ya Ummu Salamah inayatilia nguvu madhehebu haya katika kisa cha “Al-Muzaadatayn”. Humo panaelezwa: ((… na mwisho wa hilo ulikuwa ni kumpa chombo chenye maji yule ambaye imempata janaba, akasema: Nenda, halafu ujimiminie”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (344)].



Na kwa haya, lau mtu akisimama chini ya bafu la manyunyu (bomba la kuogea), na maji yakafika katika kiwiliwili chake chote, basi kukoga kwake ni sahihi kukiambatana na niya.
 
Naam kwa kutilia mkazo hapa jambo la msingi ni kuhakikisha mwili wako wote umegusa maji

Ila ukichukulia tu kujimwagia kama kujimwagia inamaana kuna sehemu kama za makwapa lazima upitishe mkono ili maji yapate kuenea na sehemu nyingine zote ambazo haziko wazi inabidi ufanye jitihada maji yapate kuenea

Na imesemwa kujimwagia maji mara moja,lkn kikubwa ni mwili kuenea maji,kwahiyo waeza jimwagia zaidi ili mradi ni wajibu mwili upate maji

Katika vitabu vidogo vya fiqh vinasema makopo tisa,kwa maana kulia matatu,kushoto matatu na jumla au kati matatu

La muhimu mwili wako uloe maji wote

Darsa linaendelea....
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



054-Kuoga Mwanamke Janaba



Alhidaaya.com





Anavyooga mwanamke janaba ni sawa na anavyooga mwanamume. Na mwanamke kama amesuka nywele zake, basi haimlazimu kuzifumua bali atalazimika tu kuhakikisha kuwa maji yanafika hadi kwenye mizizi ya nywele. Hii ni kutokana na Hadiyth ya Maymuuna aliyesema:

“Ee Rasuli wa Allaah! Mimi ni mwanamke ninayependa sana kusuka nywele zangu. Je, nizifumue kwa ajili ya kuoga janaba?”

Rasuli akamwambia:

(( Hakika yakutosha kumwagia kichwa chako mateko matatu ya maji, kisha utajimiminia maji, na hapo unakuwa umetwaharika)). [Hadiyth Swahiyh: Imeshatajwa sana nyuma.]



Na imepokelewa na ‘Aaishah aliyesema:

“Tulikuwa tukioga tukiwa na “adh-dhimaad” nailhali tuko na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) sawasawa tukiwa tumehirimia au hatujahirimia”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (254) na Al-Bayhaqiy (2/182)].



Adh-dhimaad ni dawa ya kupaka kwenye nywele. Inazifanya zishikamane na zinyooke kama zilizonatishwa na gundi na kuwa kama rasta.



Na ‘Aaishah alimshambulia ‘Abdulaah bin ‘Amri kwa kuwaamuru wanawake kufumua nywele zao wakati wa kuoga. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (331), An-Nasaaiy (1/203) na Ibn Maajah (604)].
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



055-Kuoga Mwanamke Hedhi Na Nifasi



Alhidaaya.com





[Ni kutoka kitabu changu cha Fiqh As-Sunnah Lin An-Nisaai (uk. 49) na Jaami’u Ahkaamin Nisaai cha Shaykh wetu (1/116 na ya baada yake) pamoja na nyongeza kidogo].



Namna ya kuoga hedhi na nifasi ni sawa na kuoga janaba. Lakini pamoja na hivyo, wakati wa kuoga hedhi na nifasi huongezewa yafuatayo:



1- Kutumia sabuni na mfano wake kama mada za kusafishia pamoja na maji.



Hii ni kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah aliyeeleza kwamba Asmaa alimwuuliza Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) kuhusu kuoga hedhi. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) akamwambia:

((Atachukua mmoja wenu maji na mkunazi ajitwaharishe. Ajitwaharishe vizuri, kisha ajimiminie maji kichwani na ajisugue msuguo wa nguvu mpaka maji yafike katika mashina ya kichwa chake. Kisha atajimwagia maji na atachukua kitambaa ajisafishe nacho)).

Asmaa akasema: “Ni vipi atajisafisha nacho”?!

‘Aaishah akasema: “Subhaana Allaah! Unajisafisha nacho hivi”.

‘Aaishah akasema kana kwamba hataki lisikike: “Utafuatisha kwacho athari ya damu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (314) na Muslim (332) na tamko ni lake].



2- Kufumua nywele ili maji yafike hadi katika mashina ya nywele.



Ni kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) katika Hadiyth iliyotangulia:

“Kisha ajimwagie kichwani, na akisugue msuguo wa nguvu mpaka yafike kwenye ngozi ya kichwa”.



Na Hadiyth hii ni dalili ya kuwa haitoshi tu kujimwagia maji kama ilivyo katika josho la janaba, na hasahasa pakizingatiwa kuwa katika Hadiyth hiyo hiyo, bibi huyo alimuuliza kuhusu kuoga janaba naye akasema:

“Kisha ajimwagie kichwani, na akisugue mpaka yafike kwenye ngozi ya kichwa”.



Na hapa Rasuli hakutaja kusugua kwa nguvu ili kutofautisha kati ya josho la janaba na josho la hedhi.



Maulamaa wametofautiana kuhusiana na hukmu ya kufumua nywele wakati wa kuoga hedhi. Ash Shaafi’y, Maalik, na Abuu Haniyfah wanaona kwamba hilo ni jambo mustahabu na wala si lazima. [Al-Mughniy (1/227), Al-Muhallaa (2/38), Nayl Al-Awtwaar (1/311) na Tahdhiyb As-Sunan (1/293) pamoja na Al-‘Awn]. Dalili zao ni:



1- Hadiyth haielezei wazi juu ya ulazima wa kufumua nywele.



2- Hadiyth ya ‘Aaishah aliyoielezea kuhusiana na Hijjah ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) anaposema: “Ikanifikia Siku ya Arafah nami niko hedhini. Nikamlalamikia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam), naye akaniambia: “Acha ‘Umrah yako, fumua nywele zako na hirimia Hajji..” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (317) na Muslim (1211)].... ni kuwa, josho hili linahusiana na ihraam, na wala si josho la hedhi. Kwa hivyo, Hadiyth hii haifai kuwa ni dalili.



3- Hadiyth ya ‘Aaishah isemayo kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia wakati yuko hedhini: “Fumua nywele zako na uoge”.[Isnadi yake ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (641). Angalia pia Al-Irwaa (1/167).]…ni kuwa jibu la Hadiyth hii ni kama jibu la Hadiyth iliyopita, zote ni Hadiyth moja. Na tamshi la “uoge” wamelichukulia kwa maana ya josho la ihraam.



4- ‘Abdullah bin ‘Amri alipowaamuru wanawake kufumua nywele zao wakati wa kuoga, Bi ‘Aaishah alikipinga kitendo hicho.



Ama Maimamu wanaosema ni wajibu kufumua nywele wakati wa kuoga hedhi, hao ni pamoja na Al Imaam Ahmad, Al Hasan, na Twaawuus. Dalili zao ni Hadiyth hizo hizo zilizopita. Hayo yamehakikiwa na Al-’Allaamah Ibn Al-Qayyim (Rahimahul Laah) [Tahdhiyb As-Sunan (1/293 na kurasa zinazofuatia) pamoja na ‘Awn Al-Ma’abuwd]….. ambaye amezijibu pingamizi za Jamhuri kwa haya yafuatayo:



1- Wanaposema kuhusiana na Hadiyth ya ‘Aaishah wakati akihiji kwamba ilikuwa ni katika ihram, basi ni sahihi. Lakini josho la hedhi ndilo josho lililokaziwa zaidi kuliko majosho mengineyo yote, kwani Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam), ameamuru katika josho hilo mambo ambayo hakuyaamuru katika josho jinginelo kama vile kujitwaharisha kwa ukina na umakinifu zaidi. Na kwa ajili hiyo, alimwamuru azifumue nywele ikiwa ni kumzindusha juu ya ulazima wa kufanya hivyo, kwani kufanya hivyo, kunaondosha hadathi kwa njia fanisi zaidi.



2- Ama Hadiyth yake alipokuwa na hedhi isemayo: “Fumua nywele zako na uoge”… ni kuwa Hadiyth hii kusemwa katika wakati usio wa Hijjah kunawezekana sana na hususan tunapojua kwamba wapokezi wake wa Sanad ni katika waliohifadhi Hadiyth nyingi.



3- Ama ‘Aaishah kukipinga kitendo cha ‘Abdullah bin ‘Amri, bila shaka ilikuwa ni pale bwana huyo alipowaamuru akina mama kufumua nywele zao wakati wa kuoga janaba. Bibi ‘Aaishah alisema: “Anastaajabisha sana Ibn ‘Amri huyu!! Ati anawaamrisha wanawake wafumue nywele zao wakati wa kuoga!! Kwa nini basi asiwaambie wakanyoa nywele zao kabisa!! Mimi nilikuwa naoga pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) katika chombo kimoja..”[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (331), An Nasaaiy (1/203), na Ibn Maajah (604)].



Bila shaka ni kuwa Bi ‘Aaishah alikuwa akioga pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) janaba ambapo walikuwa wakiogea chombo kimoja, lakini si katika josho la hedhi!! Na juu ya msingi huu, ni wajibu kwa mwanamke afumue nywele zake hasahasa wakati wa kuoga hedhi na nifasi, na hili ndilo la akiba zaidi. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.



3- Kufuatilisha athari ya damu kwa kitambaa kilichotiwa miski au mafuta uzuri mengine yoyote.



Itakuwa ni vizuri atumie kitambaa au pamba iliyochovewa kidogo miski, kisha aiingize kwenye utupu wake baada ya kuoga. Pia atazisafisha vizuri sehemu zote zilizoingiwa na damu katika mwili wake, na hii yote ni kwa ajili ya kujitakasa na harufu mbaya. Haya yote yamethibiti katika Hadiyth ya ‘Aaishah iliyotangulia.



Mwanamke anaruhusiwa kufanya hivi hata kama yuko katika kipindi cha eda ya kufiwa na mumewe, au mtu wake mwingine kutokana na Hadiyth ya Umuu ‘Atwiyyah inayohusiana na mambo anayokatazwa mwenye eda isemayo: “Wala hatujitii manukato, wala hatuvai nguo za rangi rangi isipokuwa nguo za kawaida zisizovutia. Alitupa ruhusa wakati wa kujitwaharisha pale mmoja wetu anapooga hedhi tujitie kidogo mafuta uzuri”.



Haya yatakuja katika mlango wake katika kitabu hiki InshaAllaah Ta’alaa.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



056-Kukausha Viungo Baada Ya Kuoga



Alhidaaya.com





Katika kuelezea huko nyuma namna Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alivyokuwa akioga, Hadiyth ya Maymuunah inasema: “Nikampa nguo, (na katika riwaya nyingine: taulo), naye hakuichukua huku akiikung’uta mikono yake miwili”. Hadiyth hii imetolewa hoja kwamba ni karaha kujifuta mwili baada ya kuoga. Madai haya hayana mashiko kwa haya yafuatayo:



1-Lililofanyika ni tukio la hali inayoweza kubeba tafsiri tofauti. Inawezekana kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) hakuichukua taulo kwa sababu ya jambo jingine lisilohusiana na ukaraha wa kujifuta, bali kwa jambo linalohusiana na taulo yenyewe, au inawezekana alikuwa na haraka na kadhalika.



2-Hadiyth hii ni dalili kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) ilikuwa ni kawaida yake kujifuta. Na kama haikuwa kawaida yake, basi asingeletewa taulo.



3-Kukung’uta maji kwa mkono wake ni dalili kwamba hakuna ukaraha wa kujifuta maji, kwani yote mawili ni tendo la kuondosha maji mwilini.



Kikhulasa tunasema: “Hakuna ubaya kujifuta maji baada ya kuoga. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



057-Masuala Yanayohusiana Na Kuoga



Alhidaaya.com





- Si lazima kutawadha baada ya kuoga



Aliyeoga josho la kisharia na akataka kuswali, basi si lazima atawadhe hata kama alikuwa hajatawadha wakati akioga, kwani twaharisho la janaba linaondosha vile vile twaharisho la hadathi ndogo. Hii ni kwa vile vizuizi vya janaba ni vingi zaidi kuliko vizuizi vya hadathi ndogo. Hivyo basi, kidogo humezwa na kingi.



Imepokelewa na ‘Aaishah akisema: ((Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa hatawadhi baada ya kuoga janaba)). [Hadiyth Swahiyh kwa nyingine: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (107), An-Nasaaiy (1/137) na Ibn Maajah (579)].



Na katika riwaya nyingine: ((Anaoga na anaswali rakaa mbili, na wala simwoni akifanya wudhuu baada ya kuoga)). [Hadiyth Swahiyh kwa nyingine: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (250) na Ahmad (6/119)].



Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhumaa) amesema: “Kama hukugusa utupu wako baada ya kumaliza kuoga, basi ni wudhuu gani ulio kamili zaidi ya kuoga?” [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdurraaziq katika Al-Muswannaf (1039)].



Ninasema:



“Juu ya haya, panazalikana nukta kwamba si lazima kwa mwenye kuoga janaba kunuwia kuondosha hadathi ndogo. Na haya ndiyo madhehebu ya Jamhuri na Ibn Taymiyah. [Al-Mabsuwtw (1/44), Ash-Sharh As-Swaghiyr (1/65), Al- Ummu (1/36), Majmu’u Al-Fataawaa (21/397) na Al-Muhalla (2/44)].



Ama Mahanbali, wao wanaona kwamba akinuwia twahara mbili, basi zote mbili zitamtosheleza. Lakini akinuwia kuoga janaba tu, basi hana ila hilo alilolinuwia tu. [Al-‘Uddat Sharh Al-‘Umdah (uk.48)].



- Yakikusanyika mawili yenye kuwajibisha kuoga kama hedhi na janaba, au janaba na ijumaa



Hapa josho moja tu litamtosheleza yote mawili kama atayanuwia yote mawili. Hii ni kauli ya Mafuqahaa wengi. [Al-Mughniy (1/292) bali imenukuliwa Ijma’a juu yake katika ((Rahmat Al- Umma Fiy Ikhtilaafi Al-Aimmah)) (uk 51). Na Ijma’a hii imetenguliwa kinyume na Ibn Hazm katika Al-Muhalla (uk.42-47). Mwanachuoni Arifu na Mweledi Al-Albaaniy amekubaliana naye katika Tamaam Al-Minnah (uk 126)].



- Mwanamke akiwa na janaba kisha akaingia hedhini kabla hajaoga



Kauli sahihi zaidi ya Maulamaa ni kuwa haimlazimu kuoga janaba, bali itamlazimu aoge janaba na hedhi kwa pamoja na ayanuwie yote mawili wakati damu ya hedhi inapokatika. Haya ni madhehebu ya Ahmad. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (299) na Muslim (321)].



Maulamaa wengine wanaona kwamba itamlazimu kuoga janaba, kisha hedhi inapokatika, ataoga josho la hedhi. Haya ni madhehebu ya ‘Atwaa, An-Nakh’iy na Al-Hasan.



Nao wengine wamesema kuwa itamlazimu aoshe utupu wake, kisha damu inapokatika aoge.

Kauli zote hizi mbili hazina dalili yoyote, na lililo sahihi na sawa zaidi ni kauli ya kwanza.



Lakini hili halimkatazi kuwa akitaka kuoga janaba au kuuosha utupu wake, kisha aoge damu inapokatika, basi atafanya hivyo na hakuna kosa lolote kwake, lakini si lazima.



- Inajuzu kwa mwanamume kuogea mabaki ya maji ya mkewe



Hili limekwishaelezewa kiuchambuzi katika mlango wa (Hukmu za Maji).



- Inajuzu mume kuoga pamoja na mkewe



Inajuzu wote wawili kuangaliana tupu zao bila ya ukaraha wowote. Imepokelewa na ‘Aaishah akisema:

((Nilikuwa naoga mimi na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) katika chombo kimoja [yeye ananiwahi, nami namwambia: niachie mimi niachie] wote tukiwa na janaba)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (299) na Muslim (321)].



- Haijuzu kuoga uchi hadharani



Kama akijisitiri watu wasimwone, basi hakuna ubaya. Tumekwishaitaja Hadiyth ya Maymuunah akisema: ((Nilimwekea Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) maji ya kuoga [na pazia yake] akaosha mikono yake miwili…..)).



Na imethibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) kwamba Muusa Alayhi Ssalaam alioga uchi, hali kadhalika Ayyuub Alayhi Ssalaam. Lakini hili ni faraghani.



- Anayepatwa na hadathi wakati wa kuoga



Mwenye janaba akipatwa na hadathi kabla ya kumaliza kuoga, basi atakamilisha wala hatoanza upya, kwani hadathi haitengui josho, hivyo basi kuwepo kwake hakuathiri josho, bali ni juu yake kutawadha.



Na hii ni kauli ya Maulamaa wengi akiwemo ‘Atwaa na Ath-Thawry. Ibn Qudaamah na Ibn Al-Mundhir wamelikubali hilo.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



058-Masuala Yanayohusiana Na Mwenye Janaba



Alhidaaya.com





- Inajuzu kwa mwenye janaba kuchelewesha kuoga



Si lazima kuoga mara tu baada ya kupata janaba ingawa kufanya haraka inakuwa ni bora zaidi na utakasifu zaidi.



Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah akisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikutana naye katika njia moja ya Madiynah akiwa na janaba, naye akamhepa asimwone. Kisha alikwenda akaoga. Baadaye alikuja na Rasuli akamwuuliza:

((Ulikuwa wapi ee Abuu Hurayrah?))

Akajibu: “Nilikuwa na janaba, nikaona uzito kukaa nawe nikiwa sina twahara”. Akasema:

((سبحان الله، إن المسلم لا ينجس))

((Subhaana Llaah. Hakika Muislamu hanajsi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (283) na Muslim (371)].



Na imepokelewa na Anas kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akiwazungukia wakeze usiku mmoja nailhali wakati huo anao tisa. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (284) na Muslim (309)].



Kisha kuharakisha kuoga janaba, bila shaka kwa ngazi ya kwanza kabisa kunakuwa ni kwa ajili ya Swalaah. Na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa mara nyingine akilala kabla ya kuoga kama tutakavyoona baadaye.



- Inajuzu kwa mwenye janaba kulala kabla ya kuoga, kama atatawadha



Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema:

(( Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anapotaka kulala hali ya kuwa ana janaba, huosha utupu wake na hutawadha wudhuu wa Swalaah)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (288) na Muslim (305)].



Na ‘Abdullah bin Qays alimwuuliza akimwambia: “Ni vipi alikuwa akifanya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) akiwa na janaba? Je, alikuwa akioga kabla ya kulala, au akilala kabla ya kuoga?” ‘Aaishah akamjibu:

((Yote hayo alikuwa akiyafanya. Huenda akaoga kisha hulala, na wakati mwingine hutawadha kisha hulala)).

Akasema ‘Abdullaah bin Qays: “Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyefanya wasaa katika jambo”.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (307)].



Na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia ‘Umar bin Al-Khatwaab alipomuuliza kuhusu janaba inayompata usiku:

((توضأ، واغسل ذكرك، ثم نم))

((Tawadha, osha dhakari yako, kisha lala)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (290) na Muslim (306)].



- Hakuna ubaya kwa mwenye janaba kusoma Qur-aan na kugusa Msahafu



Haya yamekwishaelezewa kwa ufafanuzi katika mlango wa wudhuu. Basi rejea huko.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



059-Je, Inajuzu Kwa Mwenye Hedhi Na Mwenye Janaba Kuingia Msikitini Na Kukaa Humo?



Alhidaaya.com





Jamhuri ya Maulamaa wakiwemo Maimamu wanne na wengineo (kinyume na Adh-Dhwaahiriyyah) wanasema kuwa ni haramu kwa mwenye hedhi, mwenye nifasi na mwenye janaba kukaa Msikitini. Hayo yamepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas na Ibn Mas-’oud . [Al-Majmu’u (2/184) na baada yake, Al-Mughniy (1/145) na Al-Lubaab Sharh Al-Kitaab (1/43). Ash-Shaafi’iy na Ahmad wamejuzisha kupita Msikitini bila kukaa, na Al-Muhalla (2/184) na baada yake].



Wenye kupinga hili wametoa dalili zifuatazo:



1- Ni Neno Lake Allaah (Subhaanahuu wa Ta’alaa):

((يا أيها الذين آمنوا لا تقربوا الصلاة وأنتم سكارى حتى تعلموا ما تقولون ولا جنبا إلا عابري سبيل حتى تغتسلوا))

((Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah hali mmelewa, mpaka myajue mnayoyasema, wala hali mna janaba – isipokuwa mmo safarini – mpaka mkoge)). [An-Nisaai (4:43)]



Wanasema kuwa makusudio ya Swalaah hapa ni sehemu za kuswalia, nazo ni Misikiti. Na katika Aayah, mwenye janaba anazuiliwa kuingia humo isipokuwa tu kama ni msafiri. Kisha wakawaweka mwenye hedhi na mwenye nifasi katika kipimo kimoja na mwenye janaba!!



Wenye kujuzisha hili wamewajibu wakisema:



Hii ni moja kati ya taawili mbili za masalaf katika Aayah hii. Na taawili nyingine ni kuwa makusudio ni Swalaah yenyewe, na si Msikiti. Kwa hivyo basi, maana inakuwa: Na wala msikaribie Swalaah mkiwa na janaba ila baada ya kuoga, isipokuwa kama mko safarini, basi hapo, swalini kwa kutayamamu. Na kwa ajili hiyo, Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) Anasema baada ya hapo:

((وإن كنتم مرضى أو على سفر....فلم تجدوا ماء فتيمموا))

((Na mkiwa wagonjwa, au mmo safarini………na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi)).



Kisha kuna mlahadha katika kipimo cha mwenye hedhi kwa mwenye janaba, kwani mwenye hedhi ana udhuru na hawezi kuoga kabla ya kutwaharika damu, na wala hawezi kuiondosha hedhi yake kinyume na mwenye janaba ambaye anaweza kuoga.



2- Ni Hadiyth ya Jisrah binti Dujaajah toka kwa ‘Aaishah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((إنى لا أحل المسجد لحائض ولا جنب))

((Hakika mimi sihalalishi Msikiti kwa mwenye hedhi wala kwa mwenye janaba)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (232), Al-Bayhaqiy (2/442) na Ibn Khuzaymah (2/284). Tazama Al-Irwaa (193)].



Wenye kujuzisha wamejibu wakisema:

Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, haifai kutolea hoja, kwani Hadiyth imezungukia kwa Jisrah, naye hawezi kuwa amepokea Hadiyth peke yake.



3- Hadiyth ya Ummu ‘Atwiyya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) aliamuru kuwatoa vijizee vikongwe, waliotawishwa na wenye hedhi kwenda Swalaah ya ‘Iyd ili washuhudie kheri na du’aa ya Waislamu, na wenye hedhi hukaa kando na sehemu ya kuswalia. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (324) na Muslim (890)].

Wamesema: Na ikiwa hali ni hii kwa upande wa sehemu za kuswalia, basi Misikiti ni awla zaidi kuzuiwa.



Wenye kujuzisha wamejibu wakisema:

Makusudio ya “Al-Muswalla” katika Hadiyth ni Swalaah, kwani Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) na Maswahaba wake walikuwa wakiswali ‘Iyd uwanjani na si Msikitini, na ardhi yote ni twahara, na haijuzu kuzuiliwa huko kuihusu baadhi ya Misikiti tu bila ya mingine. Kisha imepokelewa Hadiyth hiyo hiyo kwa tamko:

((فأما الحيض فيعتزلن الصلاة))

((Ama wenye hedhi, hao hukaa mbali na Swalaah)).

Na Hadiyth hii iko katika Swahiyh Muslim na kwingineko.



4- Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akielemeza kichwa chake kwangu nailhali yuko jirani na Msikiti, nami namweka sawa nikiwa hedhini.”



Wamesema: Akajizuilia kumweka sawa Msikitini kwa vile yeye ana hedhi.



Wenye kujuzisha wamejibu wakisema:

Hili walilolitolea dalili haliko wazi. Inawezekana kuwa hakuingia kutokana na sababu nyingine isiyokuwa hedhi kama kuwepo wanaume Msikitini na mfano wa hilo.



Kisha wenye kujuzisha mwenye hedhi na janaba kuingia Msikitini wametoa dalili hizi zifuatazo:



1- Ni utakasifu wa kiasili. Kwa vile hakuna makatazo yoyote sahihi, asili itakuwa ni uhalali. Muislamu ameruhusiwa kuswali mahala popote Swalaah inapomkuta.



2- Imethibiti kwamba washirikina waliingia Msikitini kwa kufungiwa humo na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam). Na Allaah Amesema:

(( إنما المشركون نجس فلا يقربوا المسجد الحرام بعد عامهم هذا))

((Hakika washirikina ni najsi, basi wasiukaribie Al Masjidul Haraam baada ya mwaka wao huu)).[At-Tawbah (9:28)]



Ama Muislamu, yeye ni twahara kwa hali zote kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam):

((إن المسلم لا ينجس))

((Hakika Muislamu hanajsiki)). [Hadiyth Swahiyh: Imetangulia karibuni].



Hivyo basi, vipi azuiwe Muislamu kuingia, na kafiri aruhusiwe?!



Wenye kupinga wamejibu wakisema:

Sharia imefarakisha kati ya Muislamu na kafiri, na kwa kufarakisha huku, dalili imepatikana juu ya uharamu wa kukaa mwenye janaba na hedhi Msikitini, na imethibiti makafiri kuwekwa mahabusu humo!!. Na sharia inapofarakisha, haijuzu kusawazisha. Na hii ni qiyaas pamoja na matni, nayo imeharibika!!



Ninasema:

“Hii ikiwa imethibiti matni, nalo li wazi!”



3- Hadiyth ya ‘Aaishah isemayo: “Kijakazi mweusi alikuwa katika kitongoji cha Waarabu, wakamwacha huru. Kisha alikwenda kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) akasilimu. Akawa na kijihema ndani ya Msikiti.”[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (439)].



Wamesema: Mwanamke huyu anakaa ndani ya Msikiti wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam), na wanawake kawaida yao ni kupata hedhi, lakini Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) hakumzuia kutokana na hilo, wala hakumwamuru atoke nje ya Msikiti anapopatwa na hedhi.



Wenye kupinga wamejibu wakisema:

Ni dhahiri kwamba mwanamke huyu hakuwa na jamaa zake wala hifadhi isipokuwa Msikiti, akalazimika kuishi humo. Hivyo, hawezi kupimiwa na mwanamke mwingine. Na hili ni tukio la hali maalumu ambalo dalili ya wazi ya kuzuia haipingwi na tukio hili!!



4- Hadiyth ya Abuu Hurayrah kuhusiana na mwanamke aliyekuwa anasafisha Msikiti akafariki, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) akamuulizia. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (458) na Muslim (956). Kwa wawili hawa kuna shaka kama alikuwa ni mwanamke au mwanamume. Lakini kwa tamko la Hadiyth iliyopo kwa Abuu Khuzaymah na Al-Bayhaqiy (4/48) kwa Sanad Swahiyh, inatilika nguvu kwamba ni mwanamke].



Mwanamke huyu hakulazimika kusafisha Msikiti nyakati zote, na wala Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) hakumkataza akae mbali na Msikiti wakati wa hedhi.



5- Hadiyth ya Abuu Hurayrah kuhusiana na Ahlus Swafah kulala ndani ya Msikiti wakati wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6452) na At-Tirmidhiy (479).



Wenye kupinga wamejibu wakisema:

Ahlus Swafah hawakuwa na ndugu wala jamaa wala chochote kama inavyoonekana wazi katika matni ya Hadiyth.



6- Imethibiti katika Swahiyh kwamba Ibn ‘Umar alikuwa akilala Msikitini wakati ni kijana kapera. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (3530) na Muslim (2479)].

Na kijana mara nyingi anapolala huota, lakini hakukatazwa kukaa Msikitini wakati anapokuwa na janaba.



Wenye kupinga wamejibu wakisema: Haikuelezwa kwamba Rasuli alilijua hilo akamkubalia!!

Wenye kujuzisha wamejibu wakisema: Lau kama hilo lingefichika kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam), basi kwa Allaah Mtukufu halifichiki, na kwa hivyo, ilitakikana ajulishwe hilo kwa njia ya wahyi ili amkataze.



Imejibiwa: Si lazima wahyi uteremke ili kumjulisha kila kosa linalofanywa na Maswahaba. Ni mara ngapi Maswahaba wamefanya makosa kwa kutojua kwa dalili ya kuuliza kwao maswali wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam).



7- ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha) alipopata hedhi wakati wa Hajji, Rasuli alimruhusu kufanya amali zote za Hajji isipokuwa kuzunguka Al-Ka’abah. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1650). Itakuja kwenye mlango wa Hijjah].



Hii inaonyesha kwamba inajuzu kwake kuingia Msikitini, kwa kuwa mwenye kuhiji lazima aingie humo.



Wenye kupinga wamejibu wakisema:

Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alitaka kumfundisha kwamba inajuzu kwa mwenye hedhi kufanya amali zote za Hijjah isipokuwa twawaaf. Ama hukmu ya kuingia Msikitini, yeye anajua kwamba hilo ni marufuku kwani yeye ndiye msimulizi wa Hadiyth. Kisha Rasuli hakumkataza kuswali akiwa hedhini – na mahujaji wanaswali -. Je, inawezekana tukasema aswali na yeye yuko hedhini?!!



Ninasema: "Jibu hili lina mwelekeo ikiwa patathibiti Hadiyth inayokataza, nayo ni Dhwa’iyf".



8- Hadiyth ya 'Aaishah aliyesema: "Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) aliniambia: "Nipe kijijamvi toka Msikitini". Nikamwambia: "Nina hedhi". Akasema: Hedhi yako haiko mkononi mwako". [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (298), Abuu Daawuud (261), At-Tirmidhiy (134) na An-Nasaaiy (1/192)].



Hili linatuhisisha kwamba kijijamvi kilikuweko Msikitini, naye Rasuli akashikilia Bi 'Aaishah aingie Msikitini ili ampatie.



Wenye kupinga wamejibu wakisema:

Hadiyth imekuja kwa tamko jingine lisemalo: " Wakati Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) akiwa Msikitini alisema: ((Ee 'Aaishah! Nipatie nguo)) Akasema: Nina hedhi. Akasema: Hedhi yako haiko mkononi mwako."[Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (299) na An-Nasaaiy (1/192)].



Hadiyth hii iko wazi kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa Msikitini wakati 'Aaishah na kijijamvi alikuwa nje. Akamwamuru aingize mkono wake tu na si mwenyewe.



Ninasema: "Hadiyth hii inabeba hili na lile. Hivyo yatakikana kuipomosha isiwepo kwenye dalili za makundi mawili".



9- Athar ya 'Atwaa bin Yasaar aliyesema: "Niliwaona watu katika Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) wakikaa Msikitini na wao wana janaba, wanapotawadha wudhuu wa Swalaah."[Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa ”ikhraaj” na Sa’iyd bin Mansour katika Sunanih (4/1275)].



Ninasema: "Baada ya mapitio haya ya hoja za wenye kupinga na wenye kujuzisha kuhusiana na kukaa Msikitini kwa wenye janaba, hedhi na nifasi, linaloonekana ni kuwa dalili za wapingaji hazipandi kufikia uharamu wa kukata ingawa mimi ninapiga breki katika suala hili. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi".
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



060-Kutayammamu



Alhidaaya.com





(Katika mlango huu, nilifaidika sana kutokana na utafiti uliotayarishwa na kaka yangu Twaariq Saalim (Allaah Amlipe jaza Yake ) kwa ajili ya kujipatia “Master” katika sharia).



Kutayammamu Kilugha Na Kisharia [Al-Majmu’u (2/238), Al-Mughniy (1/148) na Al-Mabsuwtw (1/106)]

Kilugha ni kukusudia. Ikisemwa: ،(تيممت فلانا، يممته، تأممته وأممته)inamaanisha: Nimemkusudia fulani.



Allaah Mtukufu Anasema:

((ولا تيمموا الخبيث منه تنفقون))

((Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya..)). [Al-Baqarah (2:267)].



Ama kisharia, ni kuukusudia mchanga wa juu ya ardhi kwa ajili ya kuhalalika yanayohalalishwa na wudhuu na kuoga.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



061-Usharia Wa Kutayammamu



Alhidaaya.com





Kutayamamu kumethibiti katika Qur-aan, Hadiyth na Ijma’a.



1- Katika Qur-aan, ni Neno Lake Allaah Mtukufu:

((فلم تجدوا ماء فتيمموا صعيدا طيبا))

((na hamkupata maji, basi tayamamuni kwa vumbi lililo safi)). [Al-Maaidah (5:6)]



2- Katika Hadiyth, ni neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam):

((جعلت الأرض كلها لي ولأمتي مسجدا وطهورا، فأينما أدركت رجلا من أمتي الصلاة، فعنده مسجده وعنده طهوره))

(( Ardhi yote imefanywa kwangu na kwa umati wangu kuwa ni sehemu ya kuswalia na kujitwaharishia. Na popote itakapomkuta Swalaah yeyote katika umma wangu, basi hapo ndipo pake pa kuswalia na pake pa kujitwaharisha)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (2/222) kupitia ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa babaye toka kwa babuye].



Na Hadiyth ya ‘Imraan bin Haswiyn, amesema:

“ Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) aliswali, kisha akamwona mtu mmoja kajitenga kando hakuswali na wengine. Akamwambia:

((يا فلان، ما منعك ألا تصلي مع القوم؟))

(( Ee fulani! Una nini usiswali na watu?)) Akajibu: “Ee Rasuli wa Allaah! Nimepata janaba na maji hakuna”. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) akamwambia:

((عليك بالصعيد فإنه يكفيك))

((Tumia vumbi, kwani linakutosheleza)).

Maji yalipopatikana, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alimpa mtu huyo chombo cha maji akamwambia:

((اغتسل به))

(( Ogea)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (348) na Muslim (1535)].



3- Ama Ijma’a, Ibn Qudaamah katika Al-Mughniy (1/148) amesema:

“Umma wote kwa jumla umejuzisha kutayamamu”.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



062-Ni Kipi Kinatosheleza Tayammumi?



Alhidaaya.com





Kutayamamu kunakuwa ni badala ya wudhuu na josho la janaba wakati maji yanapokosekana au kuwa vigumu kuyatumia. An-Nawawiy amesema:



“Haya ndiyo madhehebu yetu. Na hivi ndivyo walivyosema Maulamaa wote katika Maswahaba, Taabi’iyna na waliokuja baada yao isipokuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab, ‘Abdullaah bin Mas-’oud na Ibrahiym An-Nakhi’y ambaye ni Taabi’iy. [Imekuja katika Swahiyh Al-Bukhaariy (345) na Muslim (796) kuwa Ibn Mas-’oud amekataza kutayamamu kwa ajili ya janaba na kuwa Abu Muusa alimpinga kwa Aayah.



Ninasema: “Huenda Ibn Mas-’oud kulipinga hilo, kumetolewa juu ya yale yaliyo sahihi kwake toka kwa At-Twabariy (9606) wakati alipolifasiri Neno Lake Allaah Mtukufu: ((أو لامستم النساء)) akisema kuwa الملامسة ni chini ya kujamii].



Hawa wamelizuia, yaani wamezuia kutayamamu kwa ajili ya hadathi kubwa”.



Ibn As-Swibaagh na wengine wamesema kuwa inasemekana kuwa ‘Umar na ‘Abdullaah waliachana na msimamo wao.



Jamaa zetu hawa na Jamhuri wametoa dalili ya Kauli Yake Allaah Mtukufu:

((إذا قمتم إلى الصلاة فاغسلوا وجوهكم))

((Mnaposimama kuswali, basi osheni nyuso zenu)).

Hadi Neno Lake:

((وأن كنتم جنبا فالطهروا))

((Na mkiwa na janaba, basi jitwaharisheni)).



Kisha Allaah Mtukufu Akasema:

((فلم تجدوا ماء فتيمموا))

((na hamkupata maji, basi tayamamuni)).

Na hili linarejea kwa wote wawili; asiye na wudhuu na mwenye janaba. [Al-Majmu’u (2/240)].



Ninasema:

“Kuna dalili nyingine juu ya usharia wa kutayamamu kwa ajili ya hadathi kubwa. Ni Neno Lake Allaah Mtukufu:

((أو جاء أحد منكم من الغائط أو لامستم النساء فلم تجدوا ماء فتيمموا صعيدا طيبا))

((Au mmoja wenu ametoka chooni, au mmewagusa wanawake na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi)). [An-Nisaa (4: 43)].



Makusudio ya kugusana hapa ni tendo la kujamii kwa mujibu wa kauli ya mjumuiko wa Maulamaa akiwemo Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu Anhu). [Tafsiyr At-Twabariy (9583) kwa Sanad Swahiyh kutoka kwake].



Kisha kuna Hadiyth Swahiyh zilizopokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) zinazofahamisha kuwa kutayamamu hutosheleza janaba. Kati ya Hadiyth hizo ni:



1- Hadiyth tuliokwisha ielezea ya ‘Imraan bin Haswiyn wakati Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alipomwambia mwenye janaba:

((عليك بالصعيد فإنه يكفيك))

((Tumia mchanga, kwani unakutosha)). [Imekubaliwa na Al Bukhaariy na Muslim. Imeelezewa karibuni].



2- Hadiyth ya ‘Ammaar bin Yaasir, amesema: “Nilipata janaba, kisha nilijigaragaza mchangani, nikamjulisha Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) juu ya hilo, akaniambia:

:إنما كان يكفيك هكذا))

((وضرب يديه على الأرض، ومسح وجهه وكفيه

((Hakika ilikuwa inakutosha hivi:

Akapiga mikono yake miwili juu ya ardhi, akaosha uso wake na viganja vyake viwili)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukaariy (338) na Muslim (798)].



Je, Maiti Hutayamamishwa Maji Yakikosekana?



Maiti hutayamamishwa kama aliyehai maji yakikosekana, kwani kuoshwa maiti ni lazima. Tumekwishaeleza nyuma kuwa mchanga hutwaharishiwa maji yakikosekana. [Angalia Al-Muhalla (2/158)]
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



063-Hali Ambazo Kutayammamu Kunaruhusiwa





Kutayamamu kunaruhusika katika hali mbili:



1- Maji yanapokosekana, ni sawa safarini au mjini.



2- Inapokuwa vigumu kuyatumia. Na hili lina picha mbalimbali zitakazoelezewa baadaye InshaAllaah.



Allaah Mtukufu Anasema:

((وإن كنتم جنبا فالطهروا وإن كنتم مرضى أو على سفر أو جاء أحد منكم من الغائط أو لامستم النساء فلم تجدوا ماء فتيمموا))

((Na mkiwa na janaba, basi jitwaharisheni, na mkiwa wagonjwa au mkiwa safarini, au ametoka mmoja wenu chooni, au mmewagusa wanawake na hamkuyapata maji, basi tayamamuni)). [Al-Maaidah (5:6)].



Si Lazima Safari Iwe Ndefu Ili Msafiri Apate Ruksa Ya Kutayammamu



Endapo maji yatakosekana, itampasa msafiri atayamamu sawasawa ikiwa safari ni ndefu au fupi katika kauli mbili Swahiyh zaidi za Maulamaa, kwa vile safari katika Aayah Tukufu haikuainishwa kama ni fupi au ndefu. [Al-Muhalla (2/116) na Al-Mughniy (1/148)].

Ushahidi wa hilo ni:



1- Hadiyth ya ‘Aaishah (Allaah Amridhie), amesema:

“Tulitoka na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam) katika baadhi ya safari zake. Tulipokuwa Baydaa au Bidhaat Al-Jaysh, kidani changu kilikatika. Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam) alipiga kambi ili kukitafuta, na watu nao wakapiga kambi pamoja naye, hawako sehemu yenye maji na maji hawana. Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam) akalala mpaka akapambaukiwa bila kuwepo maji. Na hapo Allaah Mtukufu Akateremsha Aayah ya kutayamamu:

((فتيمموا صعيدا))

((Basi ukusudieni mchanga)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (334) na Muslim (764)].



2- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar kwamba yeye alitokea Al-Juruf na alipofika Al-Mirbad alitayamamu. Alipangusa uso wake na mikono yake miwili na akasali alasiri. Kisha aliingia Madiynah nailhali jua limepanda. Hakurejesha Swalaah. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Maalik (Twahara uk.73) na Al-Bayhaqiy (1/224)].



Ash-Shaafi’iy amesema: Al-Juruf ni sehemu karibu na Madiynah.



Si Lazima Safari Iwe Halali



Ni sahihi kuwa msafiri hutayamamu katika safari yake (maji yanapokosekana) sawasawa ikiwa alisafiri safari ya halali au safari ya haramu. Kwa kuwa kutayamamu ni faradhi, haijuzu kuacha kinyume na ruksa nyinginezo. Na kwa vile kutayamamu ni hukmu isiyohusiana na safari tu, imeruhusiwa katika safari za haramu kama kupukusa juu ya khufu siku na usiku wake. [Al-Muhalla (2/137), Al-Mughniy (1/150) na Al-Awsatw (2/32)].



Ninasema:



“Na kwa vile faradhi haipomoki kwa msafiri, imekuwa ni lazima kwake afanikishe sharti ya kusihi kutayamamu, lakini madhambi atayapata kutokana na safari yake ya haramu. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



064-Mwenye Maji Kidogo Ambayo Hayatoshi Ila Kwa Baadhi Ya Viungo Vyake





Katika suala hili, Maulamaa wamehitilafiana katika mielekeo miwili:



Wa kwanza:



Ataosha viungo awezavyo kuviosha na vilivyobaki atatayamamu. Haya ni madhehebu ya Ahmad, Ibn Hazm na moja kati ya kauli mbili za Ash-Shaafi’iy. [Al-Muhalla (2/137), Al-Mughniy (1/150) na Al-Awsatw (2/32)].



Hoja yao ni Neno Lake Allaah Mtukufu:

((فاتقوا الله ماستطعتم))

((Mwogopeni Allaah kiasi muwezavyo)). [At-Taghaabun ( 64:16)].



Na kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam):

((إذا أمرتكم بأمر فائتوا منه ماستطعتم))

((Nikiwaamuruni jambo, basi lifanyeni kiasi muwezavyo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (7288) na Muslim (3199)].



Ibn Hazm amesema:



“Na huyu anaweza kuviosha baadhi ya viungo vyake vya wudhuu au kuoga sehemu ya kiwiliwili chake, lakini hawezi sehemu zilizosalia, hapo ikafaradhishwa kwake aoshe kwanza viungo anavyoweza kuviosha katika wudhuu au josho hadi kiungo atakachokifikia, na maji yanapoisha, itamlazimu kutayamamu kwa viungo vilivyosalia kwa kulazimika. Na hilo ni lazima, kwani hana maji mengine ya kujitwaharishia. Basi ni wajibu kwake kufidia kwa mchanga kama Alivyoamuru Allaah Mtukufu”.



Wa pili:



Atatayamamu tu moja kwa moja. Mwelekeo huu ni madhehebu ya Abuu Haniyfah, Maalik na moja ya kauli mbili za Ash Shaafi’iy. Pia mjumuiko wa Masalaf wamesema hili hili. [Al-Majmu’u (2/312) na Majmu’u Al-Fataawaa (21/453)].



Wamesema:

“Haikusanywi pamoja twahara ya maji na twahara ya tayamumi; ni ima hii au ile”.

Ibn Al-Mundhir ametoa dalili kuunga mkono mwelekeo huu akisema: [Al-Awsatw ya Ibn Al-Mundhir (2/34)].



“Allaah Mtukufu Anasema:

((وإن كنتم جنبا فاطهروا))

((Mkiwa na janaba, basi jitwaharisheni))



Amewajibisha kwa mwenye janaba kuoga kwa maji, na kama hakuyapata, basi atayamamu. Na Amewajibisha kwa mwenye kumfanyia mkewe dhwihaar, amwache huru mtumwa, na kama hakumpata, basi afunge miezi miwili. Na alipokuwa mwenye kumiliki sehemu ya mtumwa lakini kiilivyo ni kama hammiliki na Allaah Akamfaradhishia kufunga, basi mwenye maji ya kuoshea baadhi ya viungo vyake tu, amekuwa ni kama asiyenayo Akamfaradhishia kutayamamu. Na jibu kuhusu mwenye kufanya tamattui na ana fedha pungufu za kununulia mnyama wa kuchinja, au aliyevunja kiapo chake na uwezo wake uko chini ya kuwalisha masikini kumi, basi hukmu yao ni kama ya hao tuliowataja.



Ama kufaradhiwa faradhi mbili kwa hao tuliowataja, hilo halijuzu.”



Ninasema:



“Na huenda lililo dhahiri zaidi ni kuwa atatayamamu tu moja kwa moja ili kutokusanya kati ya asili na badali. Pia ni kwa vile, lau kama hana maji ya kutosha kwa viungo vyake vyote vya wudhuu au vya josho na akatumia badali (kutayamamu), basi anakuwa amefanya lile aliloliweza katika Amri ya Allaah na Rasuli Wake pia. Na linalonidhihirikia mimi ni kuwa huyu ambaye anatayamamu baada ya kuosha baadhi ya viungo vyake, bila shaka anakuwa ameipata twahara kwa kutayamamu tu, na wala si kwa kuosha na kutayamamu kwa pamoja, kwani kuosha baadhi ya viungo vyake kunakuwa hakuna maana yoyote baada ya kuwa na uhakika kwamba maji aliyonayo hayamtoshi. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.



Mwenye Maji Akihofia Kukabiliwa Na Kiu Yeye Mwenyewe, Au Mwenzake, Au Mnyama Wake Kama Atayatumia



Ibn Al-Mundhir amesema: [Al-Awsatw (2/28)]



“Maulamaa tunaowajua vyema, wote wamekubaliana kuwa msafiri akijihofia nafsi yake kiu naye ana kiasi kidogo tu cha maji ya kujitwaharishia, basi atayabakisha maji yake kwa ajili ya kunywa, na atatayamamu”.



Na Ibn Qudaamah amesema: [Al-Mughniy (1/165). Tazama Al-Majmu’u (2/281)]



“Mwenye kuhofia wanyama wake, huhofia kupotea mali yake. Mfano wake ni kama mtu kuyapata maji, na kati yake na maji hayo kukawa na mwizi anayeweza kupora chochote katika mali yake, au mnyama mkali anayeweza kumdhuru mnyama wake. Na kama akimkuta mwenye kiu anayemhofia kufa, itamlazimu amnyweshe na yeye atatayamamu”.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



065-Ikiwa Kuna Maiti, Mwenye Janaba, Mwenye Hedhi na Mwenye Najsi Mwilini, Na Maji Yaliyopo Hayatoshi Ila Kwa Mmoja Wao Tu, Nani Atapewa Kipaumbele?





1- Ikiwa maji ni milki ya mmoja wao, basi atakuwa yeye ndiye mwenye haki nayo zaidi. Hili ndilo lililopitishwa na Jamhuri. [Al-Majmu’u (2/316) na Al-Mughniy (1/170)].



2- Ikiwa hayamilikiwi na yeyote kati yao, basi hukmu ni kama ifuatavyo:



(a) Maiti ana haki zaidi kuliko hao wenye hadathi kama walivyosema Ash-Shaafi’iy na Ahmad. [Al-Majmu’u (2/318) na Al-Mughniy (1/170)].Hii ni kwa sababu mbili:



Sababu ya kwanza ni kuwa huu ndio mwisho wa maiti. Kwa ajili hiyo, amehusishwa na twahara timilifu zaidi kati ya mbili. Walio hai kwa hali yoyote, watayapata maji baadaye.



Sababu ya pili ni kuwa makusudio ya kumwosha maiti ni kumsafisha, na hili haliwezekaniki kwa mchanga, wakati ambapo makusudio ya kujitwaharisha kwa walio hai ni kupata idhini ya kuswali, na hili linapatikana kwa kutayamamu.



(b) Mwenye najsi ndiye mwenye haki zaidi ya maji kuliko wenye hadathi. Wameyasema haya Mashaafi’iy na Mahanbali. [Al-Mughniy (1/171) na Al-Majmu’u (2/319)]

An-Nawawiy amesema: “Kwa sababu hakuna badali ya twahara yake”.



(c) Mwenye hedhi ana haki zaidi kuliko mwenye janaba. Hii ni kutokana na uzito wa hadathi yake, na kwa kuwa yeye anaitekeleza haki ya Allaah Mtukufu na haki ya mumewe ya kuruhusika kumwingilia.



Katika suala hili kuna mvutano. Kwa Mahanbali na Mashaafi’iy kuna njia mbili. Na kwa Mashaafi’iy kuna njia ya tatu, nayo ni kuwa wako sawasawa na watapiga kura. [Al-Mughniy (1/171) na Al-Majmu’u (2/319)]



(d) Akikusanyika mwenye janaba na mwenye hadathi, maji yaliyopo yatatizamwa. Ikiwa yatatosha kuogea janaba, basi mwenye janaba atakuwa na haki zaidi. Na kama hayatoshi, basi mwenye hadathi. [Yaliyotangulia].



(e) Akikusanyika maiti na mwenye najsi mwilini, hapa kuna mvutano. [Al-Mughniy (1/170) na Al-Majmu’u (2/318)]



Atakayekubaliana na sababu tuliyoitaja ya kumtanguliza maiti kabla ya mwenye hadathi, basi maji ni haki ya maiti.



Na atakayekinaika kuwa mwenye najsi mwilini hana badali nyingine ya kutwaharika, basi atakuwa ndiye mwenye haki zaidi.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



066-Kutayammamu Mgonjwa Ambaye Anajihofia Madhara Kama Atatumia Maji





Jamhuri ya Maulamaa (Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Ibn Hazm na wengineo), wanaona kuwa ikiwa mgonjwa atajihofia nafsi yake kuhiliki ikiwa atatumia maji, basi inajuzu kwake kutayamamu kwa Neno Lake Allaah Mtukufu:

((وإن كنتم مرضى أو على سفر.....فلم تجدوا ماء فتيمموا))

((Na mkiwa wagonjwa au safarini……na hamkupata maji, basi tayamamuni)). [Al-Maaidah (5:6)].



Amesema Mujaahid: “Hii ni kwa mgonjwa aliyepatwa na janaba. Akijihofia nafsi yake, basi ana ruhusa ya kutayamamu kama msafiri anapokosa maji”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Raazik kwa Sanad Swahiyh]. Na kwa Neno Lake Allaah Mtukufu:

((ولا تقتلوا أنفسكم))

((Na wala msiziue nafsi zenu)).[An-Nisaai (4:29)].



Hii ni katika wakati ambapo ‘Atwaa na Al-Hasan wamekataza mgonjwa kutayamamu isipokuwa katika hali ya kukosekana maji tu kutokana na Aayah inavyosema. [‘Abdul Raazik amelipokea hili katika Al-Muswannaf (861) kwa Sanad Swahiyh].



Na jibu la hili ni kuwa Aayah ni hoja ya kutupa sisi nguvu, na taqdiyr yake ni:

((Mkiwa wagonjwa; mkashindwa au mkahofia kutumia maji, au mkawa safarini na hamkupata maji, basi tayamamuni)). [Al-Majmu’u (2/330)].



Mgonjwa Akihofia Kuzidi Ugonjwa Wake Au Kukawia Kupona Kwa Kutumia Maji, Je Atatayammamu?



Jamhuri ya Maulamaa (Abu Haniyfah, Maalik, Ash-Shaafi’iy katika moja ya kauli zake mbili na Ibn Hazm), wanaona kwamba si lazima mgonjwa ahofie kuhiliki ndipo atayamamu, bali hata yule ambaye wudhuu unamwongezea ugonjwa au unachelewesha kupona, basi atayamamu kutokana na ujumuishi wa Aayah ya Suwrat Al-Maaidah. [Al-Mabsuwtw (1/121), Al-Majmu’u (2/331), Al-Muhalla (2/116), Al-Awsatw (2/26) na Majmu’u Al-Fataawaa (21/399)].



Na pia kutokana na Kauli Yake Allaah Mtukufu:

((يريد الله بكم اليسر ولا يريد منكم العسر))

((Allaah Anawatakieni wepesi na wala Hawatakieni uzito)). [Al-Baqarah (2:185)]



Ibn Hazm amesema: “Dhiki na uzito vimeondoka (na Sifa zote njema ni za Allaah) sawasawa ikiwa ugonjwa utazidi au haukuzidi. Kadhalika, ikiwa atahofia kuzidi ugonjwa, basi hilo ni uzito na dhiki vilevile”.



Na imepokelewa toka kwa Ahmad na Ash-Shaafiiy katika moja ya kauli zake mbili kwamba ili kuruhusika kutayamamu, ni lazima iwepo hofu ya kudhurika. Na madhehebu ya Jamhuri ndio sahihi zaidi. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



067-Nini Atafanya Mwenye Jeraha?



Alhidaaya.com





Suala hili lina matawi juu ya asli. Ni kuwa, je, inawezekana kukusanya kati ya asili na badali, yaani baina ya wudhuu au ghusli na tayammumi?



Suala hili lishazungumziwa kwa uchambuzi. [Angalia ukurasa wa 192 wa Kitabu hiki].



Waliopinga kukusanya kati ya viwili (asili na badali) kama Abuu Haniyfah na Maalik, nalo ndilo tulilolitilia nguvu katika mlango uliopita, wao wanaangalia kilicho kichache zaidi kwa kilicho kingi zaidi. Ina maana kuwa endapo sehemu kubwa ya mwili ina majeraha, basi mtu atatayamamu bila kuviosha viungo vizima vilivyobakia. Na ikiwa sehemu kubwa ya mwili ni nzima, atauosha mwili na ataacha sehemu yenye majeraha. [Al-Mabsuutw (1/112) na Al-Majmu’u (2/333)].



Ama wale waliojuzisha kukusanya kati ya ghusli na tayammumi, wanasema kuwa ataosha sehemu nzima ya mwili na yenye majeraha ataifanyia tayammumi. Ash-Shaafi’y na Ahmad wamelisema hili, na Shaykh wa Uislamu anaonekana kama amelikhitari. [Al-Mughniy (1/162), Al-Majmu’u (1/162) na Majmu’u Al-Fataawaa (21/466)].



Ninasema: “Inavyoonekana ni kuwa rai ya kwanza ndio sahihi zaidi kama ilivyotangulia, na hakuna katika mlango huu Hadiyth yoyote Swahiyh iliyopokelewa toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam). Lakini pamoja na haya, kuna Hadiyth ya Jaabir iliyopokelewa. Anasema: “Tulitoka kwenda safari. Mtu mmoja kati yetu alijeruhiwa na jiwe kichwani. Alipolala aliota usingizini (akamwaga), na alipoamka aliwauliza wenzake: “Je, mwaweza kunipatia idhni ya kutayamamu? Wakasema: “Hatuwezi kukuruhusu kutayamamu nawe una uwezo wa kuyatumia maji.” Mtu yule alioga akafa. Tulipokuja kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam) alijulishwa hilo naye akasema:

((Wamemwua, Awaue Allaah! Kwa nini wasiulize kama hawajui? Teguzi la asiyejua ni kuuliza. Hakika ilikuwa inamtosheleza tayammumi; akifunge kidonda chake kwa kitambaa, kisha apukuse juu yake, na sehemu iliyobaki ya mwili aioshe)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (336), Ad-Daara Qutwniy (1/190) na Al-Bayhaqiy (1/237). Sanad yake ni Dhwa’iyf. Al-AlBaaniy ameifanya Hadiyth Hasan kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas iliyopo kwa Abuu Daawuud (337) na Ibn Maajah (572). Hadiyth hii ni “Munqatwi-’i” na haifai kutolewa ushahidi].



Hadiyth hii ni Dhwa’iyf. Walioidhoofisha ni Al-Bayhaqiy, Ibn Hazm na wengineo ingawa Al-Albaaniy ameifanya kuwa Hasan.



Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar, akisema: “Endapo jeraha halikufungwa, basi ataosha sehemu za pembeni yake tu, na hatoliosha jeraha lenyewe.” [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy].



Na imepokelewa kwa njia sahihi toka kwa ‘Ubayd bin ‘Umayr kuhusiana na mtu aliyepatwa na janaba akiwa na jeraha. Amesema: “Aoshe sehemu ya pembeni tu, na maji yasikurubie jeraha lake”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Raaziq (865)].



Na hili liko sanjari na madhehebu ya Abuu Haniyfah na Maalik, nalo ndilo lenye nguvu. Na Allaah Ndiye Mjuzi
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…