Naama ndugu zangu naona wale tunao fuatilia darsa tunapata faida kubwa kuhusiana na mafunzo ya najisi na namna ya kuindoa

Kuhusu viatu zamani walikuwa wanaswali navyo kutokana na mazingira ya misikiti enzi hizo haina mabusati kama ya leo hii

Lkn jua kwamba kuswali na viatu hakuja haramishwa kwa maneno ya wanazuoni au wasomi wa dini,ila kwa akili ya kawaida tu,ikiwa kwako tu ukiweka zulia unavua viatu je vp kuhusu msikitini? Akili haikubaliani kabisa au sio

Lakini pili na kuogopa kuswali na najisi ambayo ipo katika viatu kama hujawa makini kuiondosha

Ila siku katika tembea zako duniani ukaona watu wanaswali na viatu usishangae


Endelea kufuatilia darsa kheri kubwa itapatikana
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



010-Je, Ni Lazima (Kutumia) Maji Katika Kuondoshea Najsi? Au Inajuzu Kuondoshea Kwa Vimiminika Vinginevyo Au Mada Nyinginezo?



Alhidaaya.com







Maulamaa wamehitalifiana katika suala kwa kauli mbili mashuhuri:



Kauli ya kwanza:



Ni sharti kutumia maji kuondoshea najsi. Haiswihi kwa kinginecho ila kwa dalili.

Na hili ndilo mashuhuri katika madhehebu ya Maalik na Ahmad. Na pia ni madhehebu ya Ash-Shaafi'iy katika "Al-Jadyd" (rai mpya). Ash-Shawkaany na waliomfuata, ameliunga mkono hili. [Bidaayat Al-Mujtahid (1/99), Al-Ummu (1/49) na As Sayl Al-Jarraar (1/49)].

Na hoja yao ni:



1- Neno Lake Ta'aala

((وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّن السَّمَاء مَاء لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ))

((Na Anawateremshieni maji toka mbinguni ili Awatwaharisheni kwayo)).[Al Anfaal (8:11)]

Pamoja na dalili nyinginezo zinazotaarifu kwamba maji ni twahara.



2- Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru maji yamwagwe juu ya mkojo wa bedui. [Imepasishwa na Al-Bukhaariy na Muslim].

Wamesema kwamba amri ni ya wajibu, na kwa hivyo haitoshelezi kuondosha najsi ila kwa maji!!



3- Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama ilivyo katika Hadiyth ya Abuu Tha'alabah, aliamuru kukiosha chombo cha Ahlul-Kitaab kwa maji. [Imepasishwa na Al-Bukhaariy na Muslim. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5170) na Muslim (1930)].



4-Amesema Ash-Shawkaany: "Maji ndio asili katika kutwaharisha najsi kwa kusifiwa na Allaah Mpangaji sharia kuwa ni twahara yenyewe na yenye uwezo wa kutwaharisha kingine. Hivyo, haiwezekani yakaachwa kikatumika kingine ila kama litathibiti hilo toka kwa Allaah Mpangaji sharia. Na kama si hivyo, basi haiwezekani, kwani itakuwa ni kuufumbia macho ujulikano huo wa kuwa ni twahara yenye uwezo wa kutwaharisha kingine na kutumia kitu kingine kisichojulikana kuwa ni twahara chenye uwezo wa kutwaharisha kingine. Na hiyo ni kutoka nje ya vile mikondo ya kisharia inavyokwenda".



Kauli ya pili:



Inatosheleza kujitwaharisha kwa kila chenye kuweza kuondosha najsi, na si lazima maji.

Na haya ndio madhehebu ya Abuu Haniyfah, na riwaya nyingine toka kwa Maalik na Ahmad, na kauli ya zamani ya Ash-Shaafi'iy, na Ibnu Hazm. Nalo ndilo chaguo la Shaykh wa Uislamu Ibnu Taymiyah, na pia Mwanachuoni Mkubwa Ibnu 'Uthaymiyn. [Al-Badaai-’i (1/83), Fat-hul Qadiyr (1/200), Majmuu Al-Fataawaa (21/475), Al-Muhallaa (1/92-94) na Ash Sharh Al- Mumti’i (1/361-363)].



Ni kauli yenye nguvu kwa yafuatayo:



1- Kwamba maji kuwa ni twahara yenyewe na yenye uwezo wa kutwaharisha kingine, hakuzuii kingine kuwa ni chenye kutwaharisha vilevile. Kwani kaida inasema: "Kukosekana sababu maalumu, hakuhukumii kuondoka kisababisho maalumu, sawasawa ikawa dalili au isiwe dalili". Kwa vile chenye kuathiri kinaweza kuwa ni kitu kingine. Na hii ndio hali halisi kwa upande wa najsi. [Ash Sharhu Al-Mumti’i (1/362)].



Ninasema (Abuu Maalik): "Bali baadhi ya vimiminika kama vile siki na madawa ya kusafishia ya viwandani, huondosha najsi kama maji au zaidi kuliko maji".



2- Kwamba Allaah Mpangaji sharia Ameamuru kuondosha najsi kwa maji katika mambo maalumu, lakini Hakuamuru amri jumuishi kwamba kila najsi iondoshwe kwa maji.



3- Kwamba sharia imeruhusu kuondosha baadhi ya najsi bila kutumia maji kama kustanji kwa jiwe, au kuvisugua viatu kwa mchanga, au kutwaharika nguo inayoburuzika kwa ardhi, na mengineyo yaliyotangulia.



4- Kwamba kuondosha najsi hakuingii kwenye amri, bali kunaingia katika mlango wa kujiepusha na kilichokatazwa. Na ikitokea (ikaondoshwa) kwa sababu yoyote ile, basi hukmu itathibiti. Na kwa ajili hiyo, niya haishurutishwi katika kuondosha najsi. Lakini kama itaondoka kwa kitendo cha mtu aliyenuia, basi atalipwa thawabu kwa hilo. Na kama si hivyo, ikiondoshwa bila kitendo chake wala niya yake, basi athari itaondoka, na hatokuwa na thawabu wala madhambi.



Na hili linatiliwa nguvu na kwamba tembo inapobadilika na kuwa siki, basi inakuwa imetwaharika – kwa wale wanaosema kuwa pombe ni najsi – kwa makubaliano ya Waislamu.



Ninasema (Abuu Maalik): "Lenye nguvu ni kuwa najsi inapoondoka kwa kitu chochote, hukmu yake inaondoka na inakuwa ni twahara".



Hapa Kuna Faida Kadhaa



1- Mtu mwenye najsi katika nguo yake au mwili wake, kisha akatumia mada yoyote twahara ya kusafishia – yasiyo maji – ili kuondosha najsi hiyo, basi hilo humtosheleza na wala si lazima aoshe kwa maji.



2- Haijuzu kutumia vyakula au vinywaji katika kuondoshea najsi bila dharura, kwani huo ni uharibifu wa mali. [Majmuu Al-Fataawaa (21/475)].



3-Utwaharishaji bila maji kwa (kutumia) vimiminika vingine au mada nyinginezo, utafanyika tu katika (kiini cha) najsi yenyewe katika nguo au mwili au mahala. Ama utwaharishaji wa kihukmu (twahara ya hadathi) kama vile wudhuu, kuoga na mfano wake, haukamiliki ila kwa maji.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



011-Kustanji (Kuchamba)



Alhidaaya.com







Maana Ya Kustanji Na Hukmu Yake



Kustanji ni (neno la Kiarabu katika wazn wa) "Istif'-aal" kutokana na neno: (نجوت الشجرة) yaani: "Nimeukata mti". Ni kana kwamba amejiondoshea adha.

Na katika istilahi, ni kusafisha athari ya kilichotoka kwenye njia mbili (ya mbele na nyuma) kwa jiwe au karatasi na mfano wake.

Pia huitwa "Al-Istijmaar" kwa vile mtu hutumia vijiwe vidogo katika kustanji, na na huitwa pia Al-Istitwaabah", kwa vile mtu huutakasa mwili wake kwa kuuondoshea uchafu. [Al-Mughniy (1/205)].





Hukmu Yake:



Kustanji ni lazima kwa kila kilichozoeleka kutoka katika njia mbili kama mkojo, madhii na kinyesi (kwa mujibu wa Jamhuri ya Maulamaa kinyume na Abuu Haniyfah). [Mahanafi wamesema: Kustanji ni Sunnah iliyokokotezwa madhali najsi haijavuka sehemu yake ya kutokea. Wanatolea dalili Hadiyth isemayo: ((Mwenye kustanji kwa vijiwe, basi afanye kwa idadi ya witri. Mwenye kufanya, basi kafanya vizuri, na ambaye hakufanya, basi hapana ubaya kwake)). Na hii ni Hadiyth Dhwa’iyf. Angalia Kitabu cha Dhwa’iyf Al Jaami’i (5468)].



Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):



((إذا ذهب احدكم إلى الغائط فليستطب بثلاثة احجار فإنها تجزيء عنه))

((Anapokwenda mmoja wenu haja kubwa, basi astanji kwa vijiwe vitatu, kwani vinamtosheleza)). [Hadiyth Hasan. Kuna Hadiyth kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (40), An-Nasaaiy (1/18), Ahmad (6/108 – 133) kwa Sanad Dhwa’iyf. Kuna Hadiyth nyingine kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine yenye kuitilia nguvu. Angalia Al-Irwaa (44)].



Na hii ni amri, nayo ni amri ya wajibu. Kisha neno lake:



((فإنها تجزيء))



((kwani humtosheleza))…





…na neno kutosheleza hutumika katika wajibu. Na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:



((لا يستنجى أحدكم بدون ثلاثة أحجار))



((Asistanji mmoja wenu kwa chini ya vijiwe vitatu)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (262), An-Nasaaiy (1/16), At-Tirmidhiy (16) na Abuu Daawuud].



Na katazo la kupunguza chini ya vijiwe vitatu, kunahukumia uharamu. Na itakapokuwa ni haramu kuacha baadhi ya najsi, basi kuiacha yote ni vibaya
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



012-Kitu Gani Hutumika Kustanjia?



Alhidaaya.com









Inatosheleza kustanji kwa moja ya vitu viwili:





1- Mawe na mfano wake kati ya kila kitu kigumu chenye kuondosha najsi na kisicho na thamani kubwa.



Ni kama karatasi, vitambaa, mbao na vyote vyenye kutakasa najsi.

Imepokelewa toka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:



((إذا ذهب احدكم إلى الغائط فليستطب بثلاثة احجار فإنها تجزيء عنه))

((Anapokwenda mmoja wenu haja, basi astanji kwa vijiwe vitatu, kwani hivyo humtosheleza)). [Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (40), An Nasaaiy (1/18), Ahmad (6/108 – 133) kwa Sanad Dhwa’iyf. Kuna Hadyth nyingine kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine yenye kuitilia nguvu. Angalia Al- Irwaa (44)].

Haijuzu kustanji kwa chini ya vijiwe vitatu, kwa kauli hizi zenye nguvu:



(a) Ni kwa Hadiyth ya Salmaan, amesema:



"Hakika alitukataza sisi (yaani Rasuli (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuelekea Qibla wakati wa kukidhi haja kubwa au ndogo, au kustanji kwa mkono wa kulia, au kustanji kwa chini ya vijiwe vitatu, au kustanji kwa kinyesi au mfupa".[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (262), An-Nasaaiy (1/16), At-Tirmidhiy (16) na Abuu Daawuud].



(b) Imepokelewa toka kwa Jaabir, amesema:



Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((إذا استجمر أحدكم فليستجمر ثلاثا))



((Anapostanji mmoja wenu kwa vijiwe, basi astanji mara tatu)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad, Ibn Abu Shaybah, na Ibn Khuzaymah. Al Huwayniy Allaah Amhifadhi anasema kwamba Sanad yake ni Swahiyh katika kitabu cha Badhl Al Ihsaan].



(c) Imepokelewa toka kwa Khilaal bin As-Saaib toka kwa baba yake ikiwa ni Marfu’u:



((إذا دخل أحدكم الخلاء فليتمسح بثلاثة أحجار))



((Anapoingia mmoja wenu msalani, basi ajipanguse kwa vijiwe vitatu)). [Hadiyth Hasan kutokana na yaliyotangulia. Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr (7/6623). Angalia Al-Badhl (1/352)].





Ninasema (Abuu Maalik): "Ikiwa patasafika kwa vijiwe vitatu, basi ni vyema. Na kama si hivyo, itabidi kuongeza zaidi ya vitatu mpaka pasafike".



Haifai kustanji kwa mifupa au kinyesi cha mnyama kutokana na Hadiyth ya Ibnu Mas'uud kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:



(( لا تَسْتَنْجُوا بِالرَّوْثِ وَلا بِالْعِظَامِ فَإِنَّهُ زَادُ إِخْوَانِكُمْ مِنَ الْجِنِّ ))



((Msistanji kwa kinyesi cha mnyama wala mifupa, kwani hivyo ni masurufu ya ndugu zenu katika majini)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (682), At-Tirmidhiy (18) na Ahmad (1/436)]



Na imepokelewa toka kwa Ibnu Masu'ud, amesema:

"Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda haja, akaniamuru nimletee vijiwe vitatu. Nilipata viwili na nikatafuta cha tatu lakini sikukipata. Nikachukua kinyesi cha mnyama nikamletea. Alivichukua vijiwe viwili na akakitupa kinyesi. Akasema:

((هذا ركس))



((Hii ni najsi)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (156) na wengineo. Imeshatajwa nyuma].





2- Maji



Imepokelewa toka kwa Anas, amesema:



"Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiingia msalani, na mimi na kijana pembeni mwangu tunabeba ndoo ya maji na kiegemeo, na yeye (Rasuli) akistanji kwa maji".[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (151), Muslim (270, 271) na wengineo].



Na kustanji kwa maji ni bora zaidi kuliko kustanji kwa mawe, kwani Allaah Mtukufu Amewasifu watu wa Qubaa kwa kustanji kwa kutumia maji.



Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Allaah Amridhie) ikiwa marfu'u:

"Aayah hii iliteremka kwa watu wa Qubaa:

(( فِيهِ رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُواْ))



(( Humo wamo watu wanaopenda kujitakasa)).[At Tawbah ( 9:108)].



Akasema: "Walikuwa wakistanji kwa maji, na Aayah hii ikateremka kuwazungumzia wao". [Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (44), At-Tirmidhiy (3100) na Ibn Maajah kwa Sanad Dhwa’iyf. Kuna Hadyth nyingine kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine yenye kuitilia nguvu. Angalia Al-Irwaa (45)].



At-Tirmidhiy anasema (1/31): “Hili ndilo ambalo Wanachuoni wanalolifanya. Wamekhitari kustanji kwa maji ingawa kustanji kwa mawe kunawatosheleza. Wamependelea kustanji kwa maji na wamelionelea hilo ni bora zaidi. Na hayo hayo ameyasema Sufyaan Ath-Thawriy, Ibn Al-Mubaarak, Ash-Shaafi'iy, Ahmad na Is-haaq na wengineo”.





Mtu Hastanji Kwa Kutokwa na Upepo, Na Si Lazima Kustanji Kabla ya Kutawadha



Si lazima kustanji kwa mtu aliyetokwa na upepo au aliyeamka toka usingizini. Ibnu Qudaamah anasema:

" Hatujui katika hili mahitilafiano yoyote".

Abuu ‘Abdullah anasema:

"Hakuna katika Kitabu cha Allaah wala katika Hadiyth za Rasuli Wake kwamba mtu astanji kwa kutokwa na upepo, bali linalompasa ni kutawadha".



Na imepokelewa toka kwa Zayd bin Aslam katika Neno Lake Allaah Mtukufu:



((إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلاةِ فاغْسِلُواْ وُجُوهَكُمْ))

((Mnaposimama kwa ajili ya Swalaah, basi osheni nyuso zenu)). [Al Maaidah (5:6)].



..akisema: "Mnapotoka usingizini, na Hakuamuru jingine zaidi. Hivyo basi, inaonyesha si lazima, kwa kuwa la wajibu hubainishwa na shariyah. Na hapa Aayah haikutaja kustanji, wala kustanji huko hakuko katika maana iliyoelezewa, kwani kustanji kumewekwa kwa ajili ya kuondosha najsi, na hapa hakuna najsi.." [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (1/206)].



Kustanji si lazima kuungamane na wudhuu, hilo halikusuniwa na wala halikupendezeshwa kama wanavyodhani watu wengi, bali hiyo ni ‘ibaadah peke yake kando. Makusudio yake ni kupatakasa mahali kutokana na najsi. Na wala hakuna yeyote aliyenukuu kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akistanji kila anapotawadha au aliamuru hilo.
 
OLE WAO WANAO PUNJA VIPIMO NA MIZANI

Ndugu zangu katika imani hakika ucha mungu hauishii kwenye hizi ibada za swala na funga,ila ucha mungu unahusiana na namna gani unaendesha maisha yako kwa ujumla wake

Kila hatua na harakati za maisha yako inabidi uwe mcha mungu,ufuate maamrisho ya Allah na kuchunga mipaka yake na makatazo yake

Kwa wale wote ambao katika miamala yenu ya biashara ambao mnatumia vipimo kuwapimia watu au mizani katika kutoa huduma zenu,hakika mtumie vipimo sahihi na mizani sahihi la sivyo mtakuja kukutana na ghadhabu za Allah

Ikiwa tu serikali ina taasisi maalumu ya WAKALA WA VIPIMO kuhakikisha haki inapatikana katika vipimo na mizani,je vipi kuhusu Allah mtukufu ambaye anajua na kuona kila kitu?

Iwe ni mfanya biashara wa mafuta sheli,je pump zako ziko sawa hazipunji lita za mafuta?

Kwa hakika tutaulizwa kwa kila kitu na Allah mtukufu,niliwahi kuandika huko nyuma siku ya kiama tutakuwa na kisimamo cha miaka 50,000 hapo kila mwanadamu atakuwa na usaili na Allah mwenyewe,hapo mwanadamu kuna mambo atabisha hakufanya ndio Allah ataruhusu vitu vitoe ushahidi juu yako,ardhi itasema,mikono itasema na kila kitu ambacho kita hitajika kutoa ushahidi kitafanya hivyo


Kuna aya nyingi sana zinazungumzia kuhusiana na swala la vipimo na mizani,mathalani tuangalie haya hizi katika Suratil Mutwafifin



Hapo Allah amekemea vikali sana kuhusiana na maswala ya kupunja vipimo na mizani,kwahiyo tuwe makini sana ndugu zangu hakika Allah ni mwenye kujua na kuona



Na nabii Yusufu baada ya kuwa mkuu wa hazina za nchi kule Misri alisema hakika yeye anatimiza vipimo pale anapo wapimia watu

Kwahiyo ndugu zangu wale wote ambao kwa namna moja au nyingine shughuli zenu zinahusiana na vipimo na mizani basi mcheni Allah hakika yeye ni mjuzi na hakimu muaminifu kila mtu atalipwa kwa kile alicho kichuma

Tumche Allah
 
Naam darsa la fiqh linaendelea kuna ibara au vipengele hamsini na kitu,ni wewe tu kazi kwazo kujifunza

Hakika kusoma na kupata elimu kwa muislamu ni wajibu ndio maana aya za kwanza kushuka katika qur'an zilimtaka Mtume swalla llahu alaih wassallamu asome



Kwahiyo muislamu hatakiwi kuwa mjinga katika elimu ya dini au secular

Azimia kusoma na kupata maarifa yatakayo kusaidia


Tunaendelea na sehemu ya 013
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



013-Baadhi Ya Adabu Za Kustanji



Alhidaaya.com







Kati ya adabu ambazo inatakikana mtu ajipambe nazo wakati wa kustanji ni:



1- Asistanji kwa mkono wa kulia



Ni kutokana na Hadiyth ya Abuu Qataadah, amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( لا يمسكن احدكم ذكره بيمينه وهو يبول، ولا يتمسح من الخلاء بيمينه، ولا يتنفس في الاناء))

((Asikamate kabisa mmoja wenu dhakari yake kwa mkono wake wa kulia wakati anakojoa, wala asijisafishe haja kwa mkono wake wa kuume, wala asipumulie ndani ya chombo)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy ( 153) Muslim (267) na wengineo].



Na imepokelewa toka kwa Salmaan, amesema: “Mtu mmoja aliniambia: “Hakika mwenzenu huyu anawafundisheni hata kwenda haja kubwa”. Akasema (Salmaan): “Ndiyo. Ametukataza kuelekea Qiblah wakati wa kukidhi haja kubwa au ndogo, ametukataza kustanji kwa mikono yetu ya kulia, au kustanji kwa chini ya vijiwe vitatu”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (262), Abuu Daawuud (7), At-Tirmidhiy (16) na An-Nasaaiy (1/16).





2- Asiuguse utupu kwa mkono wake wa kulia



Ni kwa Hadiyth ya Abuu Qataadah iliyotangulia.



3- Ausugue mkono wake kwenye udongo, au auoshe kwa sabuni na mfano wake baada ya kustanji



Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah, amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akiingia msalani, nilikuwa nikimpelekea maji katika kijidoo kidogo, halafu hustanji na kisha huupangusa mkono wake juu ya ardhi”. [Hadiyth Hasan Lighayrihi. Imefanyiwa “ikhraaj” na …(45), Ibn Maajah (678) na An-Nasaaiy (1/45). Angalia Kitabu cha Al-Mishkaat (360)].



Hili linatiliwa nguvu na Hadiyth ya Maymuunah isemayo: “Kisha Rasuli alijimwagia maji juu ya utupu wake, akauosha kwa mkono wake wa kushoto, kisha akaupiga mkono wake juu ya ardhi, halafu akauosha”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (266) na Muslim (317)].



4- Aunyunyizie utupu wake maji pamoja na nguo yake baada ya kukojoa ili kuondosha shaka na wasiwasi



Imepokelewa na Ibn ‘Abbaas kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha mara moja, halafu akaunyunyizia maji utupu wake. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ad-daaramiy (711) na Al-Bayhaqiy (1/161). Al-Albaaniy amesema katika kitabu cha Tamaam Al-Minnah (uk. 66) kwamba Sanad yake ni Swahiyh juu ya sharti ya Masheikh wawili].
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



014-Ni Vipi Mgonjwa Wa Kichocho Au Mfano Wake Anastanji?



Alhidaaya.com





Mwenye kichocho, atastanji na kutawadha kwa kila Swalaah. Na vinavyomtoka vinakuwa havina madhara yoyote kwake madhali wakati wa Swalaah nyingine haujaingia. Na hii ndiyo kauli sahihi zaidi kati ya kauli mbili za Maulamaa. Kauli hii imesemwa na Abuu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-haaq, Abuu Thawr na wengineo.



Mwenye ugonjwa huu, atakuwa na hukmu ya damu ya istihaadhwah. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelizungumzia hilo aliposema:



((انما ذلك عرق، وليست بالحيضة، فاذا أقبلت الحيضة فدعي الصلاة، فاذا ذهب قدرها، فاغسلي عنك الدم وصلي))

((Hakika hiyo ni damu ya mshipa na si ya hedhi. Na hedhi ikija, basi acha Swalaah. Muda wake ukimalizika, oga ujitwaharishe damu, kisha swali)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (228), Muslim (333) na wengineo. An-Nasaaiy (1/185) ameisimulia kwa tamko la: “Basi oga ujitwaharishe na damu, utawadhe na uswali” kwa nyongeza ya “utawadhe”, nayo ni “Shaadha”. An-Nasaaiy na Al-Bayhaqiy ( 1/327) wameikosoa. Naye Muslim ameashiria kwamba ina walakini, na Al-Bukhaariy hakuifanyia “ikhraaj”. Angalia “Jaami’u Ahkaamin Nisaa” kilichotungwa na Sheikh wetu Mustwafa Al- ‘Adawy – Allaah Amnyanyulie hadhi yake – (1/223-226)].



Na kwa upande wa Al-Bukhaariy, amesema: Na akasema Ubayy: “Kisha tawadha kwa kila Swalaah mpaka uje wakati huo”. [Tamko hili linawezekanika kuwa ni Marfu’u toka kwa kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au kutoka kwa kauli ya ‘Urwa bin Az Zubayr msimulizi wa Hadiyth toka kwa ‘Aaishah. Aliwajibu kwa kauli hiyo akina mama waliomuuliza kuhusiana na hilo kama ilivyo kwa Ad-Daaramy (1/199). Al Haafidh katika “Al-Fat-h” (1/332), amepondokea kwenye uwezekaniko wa kwanza, na Al-Bayhaqiy kwenye “As-Sunan” (1/344), amepondokea kwenye uwezekaniko wa pili. Naye Sheikh letu – Allaah Amhifadhi – ameitilia nguvu katika “Jaami’u Ahkaamin Nisaa” (1/227)].



Ninasema (Abuu Maalik): "Hukmu hii bila shaka ni kwa mwenye udhuru kwa ajili ya kumwondoshea uzito. Na hakuna shaka kuwa sharia imekuja kwa ajili ya kuuondoshea umma uzito. Allaah Mtukufu Anasema:

(( يُرِيدُ اللَّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ ))

(( Allaah Anawatakieni wepesi na wala Hawatakieni uzito)).[Al-Baqarah: (2:185)]



Maalik na wengineo wanaona kwamba haimpasi mgonjwa huyo kustanji wala kutawadha ila tu kama atapata hadathi nyingine".



Ninasema (Abuu Maalik): "Ama kutokupasa kutawadha kwa kila Swalaah endapo kama hajapata hadathi, huenda hilo lina mwono kwa wale waliotia udhwa’iyf katika kuongezwa neno “na utawadhe kwa kila Swalaah” katika Hadiyth iliyotangulia. Na lenye nguvu hapa ni kutawadha kwa kila Swalaah kama itakavyokuja katika mlango wa hedhi. Ama kutopasa kustanji, basi hilo halina cha kuzungumziwa, kwani anaweza kutokwa na kinacholazimisha kustanji na akawa na wasaa wa kufanya hivyo kabla ya Swalaah bila ya uzito wowote. Anachosamehewa ni kile tu kinachomtoka wakati wa Swalaah kwa ajili ya kuepuka uzito. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi".
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



015-Adabu Za Kukidhi Haja



Alhidaaya.com





Mwenye kutaka kukidhi haja ndogo au kubwa, inatakikana ajihimu kwa adabu zifuatazo:



1. Ajisitiri na ajiweke mbali na watu na hasa hasa uwandani.



Imepokelewa na Jaabir (Radhi za Allaah ziwe juu yake), amesema: “Tulitoka na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika safari. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hafiki uwandani, isipokuwa hupotea asionekane”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (2) na Ibn Maajah (335), na tamshi ni lake].





2- Asiwe na kitu chenye utajo wa Allaah Mtukufu [Angalia Al-Majmuu (2/87), Al-Mughniy (1/227) na Al-Awswat (1/342)].



Ni kama pete iliyotiwa nakshi ya Jina la Allaah na vinginevyo. Hii ni kwa vile kulitukuza Jina la Allaah Mtukufu ni jambo ambalo kidini linajulikana na wote. Allaah Mtukufu Anasema:



ذَلِكَ وَمَنْ يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّهِ فَإِنَّهَا مِنْ تَقْوَى الْقُلُوبِ

(( Ndivyo hivyo! Na anayetukuza alama za ‘Ibaadah za Allaah, basi hayo ni katika taqwa ya nyoyo)). [Al-Hajji (22:32)).



Hii ni kwa yaliyopokelewa toka kwa Anas kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiivua pete yake anapoingia msalani. [Hadiyth Dwa’iyf. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy na Ibn Maajah. Al-Albaaniy kasema ni Dhwa’iyf.



Na Hadiyth hii ni Munkar, wahafidhi wameitia dosari.



Na linalojulikana ni kwamba pete ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa imetiwa nakshi iliyoandikwa “Muhammad Rasuwlul Laah”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5872), Muslim (2092) na wengineo.]



Ninasema (Abuu Maalik): “Ikiwa pete hii au mfano wake imesitiriwa kwa kitu kama kuwekwa mfukoni au sehemu nyingine kama hiyo, basi itajuzu kuingia nayo. Ahmad bin Hanbal anasema: “Akitaka ataifumbata katika kiganja chake”.



Ikiwa atahofia kupotea kama ataiacha nje, basi itajuzu kuingia nayo kwa vile imelazimu. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.



3- Apige BismiLlaah na ajilinde kwa Allaah wakati wa kuingia msalani



Atafanya hivi kama ataingia sehemu iliyojengwa (choo). Lakini kama itakuwa ni uwandani, basi atafanya hivyo wakati anapoinyanyua nguo yake. Hii ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):



((ستر مابين الجن وعورات بني آدم اذا دخل أحدهم الخلاء أن يقول: بسم الله))

((Kinga iliyoko kati ya jini na tupu za wanaadamu anapoingia mmoja wao msalani, ni kusema “BismiLlaah”)).[Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy na Ibn Maajah. Angalia “Swahiyh Al- Jaami’i” (3611)].



Na imepokelewa na Anas (Radhi za Allaah ziwe juu yake) akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anasema wakati anapoingia msalani:



اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِك من الْخُبُثِ وَالْخَبَائِثِ



((Ee Allaah! Hakika mimi ninajilinda Kwako na majini wa kiume na majini wa kike)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (142) na Muslim (372)].



4- Atangulize mguu wa kushoto wakati wa kuingia, na mguu wa kulia wakati wa kutoka



Abuu Maalik: “Sikupata katika hili kauli thibitishi toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lakini Ash-Shawkaaniy amesema katika “As-Saylu Al-Jarraar” (1/64): Ama kutanguliza mguu wa kushoto wakati wa kuingia na mguu wa kulia wakati wa kutoka, basi hili lina hikmah yake. Ni kuwa vitu vitukufu huanziwa kwa kulia na visivyo vitukufu huanziwa kwa kushoto. Na bila shaka yenye kuonyesha hilo yamekuja katika ujumuishi.”



5- Asielekee Qiblah au kukipa mgongo wakati anapokaa kukidhi haja



Ni kwa Hadiyth ya Abu Ayyuub Al-Answaariy (Radhi za Allaah ziwe juu yake) aliyepokea toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), amesema:



(( إذا أتيتم الغائط فلا تستقبلوا القبلة ولا تستدبروها، ولكن شرقوا أو غربوا))

((Mnapokwenda haja kubwa, msikielekee Qiblah wala msikipe mgongo, bali elekeeni mashariki au magharibi)).

Abuu Ayyuub anasema: “Tukafika Shaam, tukakuta vyoo vimejengwa kuelekea Ka’abah, tukawa tunakiepa na kumwomba Allaah Mtukufu maghfirah”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (394), Muslim (264) na wengineo.



Lakini hata hivyo, imepokelewa kwa njia sahihi toka kwa Ibn ‘Umar kwamba amesema: “Siku moja nilipanda juu ya paa la nyumba yetu, nikamwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya matofali mawili akikidhi haja na ilhali ameelekea Baytul Maqdis”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (145), Muslim (266) na wengineo.]



Na ikiwa ameelekea Baytul Maqdis na yeye yuko Madiynah, basi atakuwa ameipa mgongo Ka’abah!!



Ninasema (Abuu Maalik): “Na ili kuzifahamu Hadiyth hizi mbili, kuna kauli nne mashuhuri za Maulamaa: [Amezitaja An Nawawiy kwenye Al-Majmuu’i (2/82), na Al-Haafidh kwenye Al-Fat-h (1/296), na ameongeza kauli tatu nyingine].



1- Ni kuwa katazo la kuelekea Qiblah na kukipa mgongo ni kwa hali zote sawasawa ikiwa ndani ya jengo au uwandani.



Haya ni madhehebu ya Abuu Haniyfah, Ahmad na Ibnu Hazm. Shaykh wa Uislamu pia ana msimamo huu. Ibnu Hazm amelinukulu hili toka kwa Abuu Hurayrah, Abuu Ayyuub, Ibn Mas’uud na Suraaqah bin Maalik. Pia amepokea toka kwa Atwa’a An-Nakh’i, Ath-Thawriy, Al-Awzaa’iy na Abuu Thawr. [Al-Muhallaa (1/194), Al-Fat-h (1/296), Al-Awswat (1/334), As Sayl Al-Jarraar (1/69) na Al-Ikhtiyaaraat Al- Fiqhiyyah (8)]. Wametoa hoja yao kwa kuitumia Hadiyth ya Abuu Ayyuub iliyotangulia.



Wameijibu Hadiyth ya Ibn Umar kwa mambo haya:



(a) Lililokatazwa linatangulizwa kabla ya lililoruhusiwa.



(b) Hakuna ndani ya Hadiyth hiyo kwamba hilo lilikuwa baada ya kukatazwa kuelekea Ka’abah au kuipa mgongo.



(c) Kitendo chake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakipingani na kauli inayouhusu umma isipokuwa kwa lile lenye dalili yenye kuashiria kwamba alitaka kumuiga katika hilo. Na kama si hivyo, basi kitendo chake kilikuwa kinamuhusu yeye mwenyewe.



Ninasema: “Huenda kauli yao hii ya mwisho inapata nguvu ya kuwa Ibn ‘Umar kumwona Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumeafikiana naye bila ya kukusudia. Kana kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutaka kwa hilo kubainisha hukmu mpya ya kisharia”.



2- Ni kuwa katazo hilo linahusiana na sehemu wazi tu lakini si ndani ya jengo.



Hili limesemwa na Maalik na Ash-Shaafi’iy. Kwa kauli yao hii, wao wamepitia mkondo wa kukusanya baina ya dalili mbili. Wamesema: “Kaida isemayo “Kauli hutangulizwa kabla ya kitendo”, bila shaka hutumiwa katika hali ya kuthibiti umahususi, na umahususi huo hauna dalili yoyote”.



3- Ni kuwa inajuzu kukipa mgongo Qiblah lakini haifai kukielekea.



Hili limehadithiwa toka kwa Abuu Haniyfah na Ahmad, wakiuchukulia udhahiri wa Hadiyth ya Ibn ‘Umar na Hadiyth ya Abuu Ayyuub.



4- Ni kuwa inajuzu kuelekea Qiblah na kukipa mgongo katika hali zote.

Hii ni kauli ya ‘Aaishah, ‘Urwah, Raby’a na Daawuud. Hoja yao wanasema kuwa Hadiyth zimegongana, na kwa hivyo suala linarejea katika asili yake ya uhalali.



Ninasema (Abuu Maalik): ”Huenda kauli ya kwanza ya kuharamisha kabisa hali zote mbili, ndiyo dalili yenye nguvu zaidi na yenye kinga zaidi kuitumia. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.



5- Ajiepushe kabisa na maneno ila kwa dharura.



Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar (Radhi za Allaah ziwe juu yake) akisema kwamba mtu mmoja alimpitia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa anakidhi haja ndogo, akamsalimia na Rasuli hakujibu. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (370), Abuu Daawuud (16), At Tirmidhiy, An Nasaaiy (1/15) na Ibn Maajah (353).



Kujibu maamkizi ni wajibu. Na Rasuli alipoacha kujibu, inaonyesha kuwa ni haramu kuzungumza na hasahasa kama ni kumtaja Allaah Mtukufu. Lakini ikiwa atazungumza kwa ajili ya haja isiyoepukika kama kumwongoza mtu, au kuomba maji au mfano wa hayo, basi itaruhusika kutokana na dharura. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.



6- Ajiepushe kukidhi haja njiani wanamopita watu, sehemu wanapopumzikia kupata kivuli na mfano wa sehemu hizo.



Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:



((اتقوا اللاعنين، قالوا: وما اللاعنان يا رسول الله؟ قال: الذي يتخلى في طريق الناس أو في ظلهم))

((Waogopeni wawili waliolaaniwa)). Wakasema: Ni nani hao wawili waliolaaniwa ee Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Ni yule anayejisaidia njiani wanamopita watu au katika kivuli chao)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (68) na Abuu Daawuud(25)].



7- Ajiepushe kukojoa mahala pa kuogea.



Na hasahasa kama maji yanajikusanya mahala hapo kama kwenye hodhi (bath tub) na kadhalika. Kwani Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu kukojoa mahala anapoogea. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na An Nasaaiy (1/130) na Abuu Daawuud (28)].



8- Ajiepushe kukojoa katika maji yaliyotuama tuli.



Ni kwa Hadiyth ya Jaabir aliyesema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza watu kukojoa katika maji yaliyotuama. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (281) na An Nasaaiy (1/34).



09- Atafute sehemu laini wakati wa kukojoa na ajiepushe sehemu ngumu ili kujikinga najsi isimrudie.



10- Ashikamane na adabu za kustanji tulizotangulia kuzitaja.



11- Aseme wakati anapotoka: “Ghufraanak”.



Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anatoka msalani, alikuwa akisema: “Ghufraanak”.[Hadiyth Hasan Lighayrihi. Imefanyiwa “ikhraaj” na At Tirmidhiy (7), Abuu Daawuud (30) na Ahmad
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



016- Je, Inafaa Mtu Kukojoa Kwa Kusimama?



Alhidaaya.com





Katika mlango huu, kuna Hadiyth tano toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Tatu kati ya hizo ni Hadiyth Swahiyh. Katika Hadiyth ya kwanza, ‘Aaishah anakanusha Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kukojoa kwa kusimama. Na katika Hadiyth ya pili, inaelezwa kuwa alikojoa kwa kusimama, na ya tatu inaelezwa kuwa alikojoa kwa kukaa (kuchuchumaa).

Ama Hadiyth mbili Dhwa’iyf, moja inakataza kukojoa kwa kusimama na nyingine inakuelezea kukojoa kwa kusimama kama ni utovu wa hishma. Hadiyth zenyewe ndizo hizi:





1- Hadiyth ya ‘Aaishah, amesema: “Atakayewaambieni kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikojoa kwa kusimama, basi msimsadiki. Hakuwa akikojoa ila kwa kuchuchumaa”.[Hadiyth Swahiyh Lighayrih. Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (12), An-Nasaaiy (1/26), Ibn Maajah (307) na Ahmad (6/36)].





2- Hadiyth ya Hudhayfah, anasema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda mwishoni mwa jalala la watu, akakojoa kwa kusimama. Mimi nilijivuta kando, lakini aliniambia nikurubie. Nilikurubia mpaka nikasimama nyuma yake, akatawadha na kupukusa juu ya khofu zake mbili”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (226), Muslim (273), na wengineo].





3- Ni Hadiyth ya ‘Abdur-Rahmaan bin Hasanah, amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitutokea akiwa ameshika mkononi mwake kitu kama ngao. Alikiweka kitu hicho, kisha akakaa nyuma yake na kukojoa akikielekea”.[Hadiyth Swahiyh Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (22), An-Nasaaiy (1/27), Ibn Maajah (346) na Ahmad (4/196)].



4- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar, amesema: “Alisema ’Umar: Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniona nikikojoa kwa kusimama akaniambia:

((يا عمر، لا تبل قائما))

((Ee ‘Umar! Usikojoe kwa kusimama)).

Akasema: “Sikukojoa tena kwa kusimama”. [Hadiyth Dhwaiyf. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (308), Al-Bayhaqiy (1/202) na Al-Haakim (1/185). At- Tirmidhiy amesema ni “Hadiyth Mu’allaq” na Dhwaiyf (1/67 – Ahwadhiy)].





5- Imepokelewa toka kwa Buraydah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:



(( ثلاث من الجفاء: أن يبول الرجل قائما، أو يمسح جبهته قبل أن يفرغ من صلاته، أو ينفخ في سجوده))



((Mambo matatu ni utovu wa adabu: Mtu kukojoa kwa kusimama, au kuupangusa uso wake kabla hajamaliza kuswali, au kupuliza wakati yuko katika sijdah)). [Hadiyth Munkari. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy katika kitabu cha “At-Taariykh” (496) na “Al-Bazzaaz” (1/547). Al-Bukhaariy na At-Tirmidhiy, wamesema ni Hadiyth Munkar, lakini imethibiti kutokana na kauli ya Ibn Mas-’oud].





Ninasema (Abuu Maalik): “Kutokana na Hadiyth hizi, Maulamaa wametofautiana juu ya hukmu ya kukojoa kwa kusimama katika kauli tatu”: [Al-Majmuu (2/98) na Al-Awswat (1/333)].





1- Ni karaha bila ya udhuru



Haya yamesemwa na ‘Aaishah, Ibn Masu’d na ‘Umar katika moja ya riwaya mbili. Pia Abuu Muusa, Ash-Sha’abiy, Ibn ‘Uyaynah, Hanafiy na Shaafi’iy.



2- Kunajuzu kwa hali yoyote



Haya yamesemwa na ‘Umar (katika riwaya ya mwisho), ‘Aliy, Zayd bin Thaabit, Ibn ‘Umar, Sahl bin Sa’ad, Anas, Abuu Hurayrah na Hudhayfah. Hii ndiyo kauli ya wafuasi wa madhehebu ya Hanbali.



3- Kama mtu yuko sehemu laini ambapo mkojo hauwezi kumrukia itajuzu, lakini kama si hivyo, basi ajizuie.



Haya ni madhehebu ya Maalik. Kauli hii imeungwa mkono na Ibn Al Mundhir.

Ninasema (Abuu Maalik): “Lenye nguvu ni kwamba hakuna ukaraha wowote wa kukojoa kwa kusimama madhali mtu ana uhakika kwamba mkojo hauwezi kumrukia. Hii ni kwa sababu zifuatazo:



1- Ni kwamba hakuna Hadiyth yoyote Swahiyh iliyopokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyokataza hilo.



2- Ni kuwa yaliyopokelewa kuhusu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kukojoa kwa kukaa (kuchuchumaa), hayapingani na kujuzu kukojoa kwa kusimama, bali hilo linaashiria kujuzu kwa yote mawili.



3- Ni kwa kuthibitika kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikojoa kwa kusimama.



4- Ni kuwa ‘Aaishah kukanusha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kukojoa kwa kusimama, kumejengewa juu ya kile anachokijua yeye kwa mujibu wa yale ambayo Rasuli anayafanya akiwa nyumbani. Kwa hiyo kukojoa kwake nje ya nyumba yake kwa kusimama, hakukanushiki. Na hakuna shaka kwamba kutojua jambo, hakumaanishi kwamba jambo hilo halipo. Na aliyejua kama vile Hudhayfah na wengineo, ni hoja kwa yule ambaye hakujua, na kwamba jambo yakinishi hutangulizwa kabla ya kanushi. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



017- Sunnah Za Hulka Asilia



Alhidaaya.com





Nini Maana Ya Sunnah Za Hulka Asili? Ni Zipi Sunnah Hizo?



Sunnah za hulka asili ni mambo ambayo mtu akiyafanya, huipata hulka asili ambayo Allaah Amewaumbia kwayo waja, Atawakusanya wakiwa nayo (Siku ya Qiyaamah), na Amewapendelea waifanye ili wawe juu ya ukamilifu wa sifa na utukufu wa sura.



Mambo haya ni mwenendo wa kale ambao Manabii waliuchagua na sharia zote zikakubaliana juu yake. Inakuwa ni kama jambo la kimaumbile waliloumbiwa kwalo watu. [Nayl Al-Awtwaar (1/109) na Umdat Al-Qaariy cha Al’ Ayniy (22/45)].



Maslaha ya kidini na kidunia hufungamana na mambo ya hulka asili ambayo hudirikiwa kwa ufuatiliaji. Kati ya mambo hayo ni kuliweka umbo katika picha nzuri na kuutakasa mwili ndani na nje, na kwa mapana na marefu. [Faydh Al-Qadiyr cha Al-Minnaawiy (1/38)].



Baadhi ya mambo haya yamepokelewa katika haya yafuatayo:



1- Hadiyth ya Abuu Hurayrah, amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:



((الفطرة خمس: الختان، والاستحداد، وقص الشارب، وتقليم الأظافر، ونتف الآباط))

((Hulka asili ni matano: Kutahiri, kunyoa kinena, kukata sharubu, kukata kucha na kunyofoa vikwapa)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5891) na Muslim (257)].





2- Hadiyth ya ‘Aaishah, amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:



((عشر من الفطرة: قص الشارب، واعفاء اللحية، والسواك، واشتنشاق الماء، وقص الأظفار، وغسل البراجم، ونتف الابط، وحلق العانة، وانتقاص الماء))

((Mambo kumi ni katika hulka asili: Kunyoa sharubu, kuziachilia ndevu, kupiga mswaki, kupaliza maji puani, kukata kucha, kuosha vifupachanda, kunyofoa nywele za kwapa, kunyoa kinena na kustanji)).



Mus’ab mmoja wa wapokezi wa Hadiyth anasema: “Nimelisahau la kumi kama halitakuwa ni kusukutua”.[Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (261), Abuu Daawuud (52), At-Tirmidhiy (2906), An-Nasaaiy (8/126) na Ibn Maajah (293).



Kutokana na Hadiyth hizi mbili, tunafahamu kuwa mambo ya hulka asili hayaishilii kwenye haya kumi tu, bali yako mengineyo. Kwa ufupi mambo haya ni:





Kutahiri.
Kustanji.
Kupiga mswaki.
Kukata kucha.
Kukata sharubu.
Kuachilia ndevu.
Kunyoa kinena (mavuzi).
Kunyofoa nywele za kikwapa.
Kuosha vifupachanda na sehemu ambazo uchafu hujikusanya kama kwenye mibano ya vidole, makunjano ya masikio na kadhalika.
Kusukutua na kupaliza maji puani.
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



018-Kutahiri



Alhidaaya.com





Maana Na Hukmu Yake



Kutahiri (katika Lugha ya Kiarabu) ni kisoukomo (Maswdar) cha kitenzi ,(ختن)yaani amekata. Na kutahiriwa ni ima kukata ngozi inayofunika kichwa cha uume, au kukata ngozi iliyopo upande wa juu wa utupu wa mwanamke (ukeketaji). [Angalia Tuhfat Al-Mawduwd cha Ibn Al-Qayyim (uk 106, 132) na Al-Majmuu (1/301)].



Ama kwa upande wa hukmu yake, Maulamaa wana rai tatu:



1- Ni wajibu kwa mwanamume na mwanamke.

2- Ni jambo mustahabu kwao.

3- Ni wajibu kwa mwanamume, lakini kwa mwanamke ni mustahabu.



Ibn Qudaamah katika kitabu cha Al Mughny (1/85) anasema: “Ama kutahiriwa, hilo ni wajibu kwa wanaume na ni ukirimio kwa upande wa haki ya wanawake na wala si lazima kwao. Hii ndio kauli ya Maulamaa wengi….”



Naye An-Nawawy katika kitabu cha Al Majmu’i (1/301) anasema: “Na madhehebu sahihi kwa matni ya Ash-Shaafi’iy na yaliyokubaliwa kwa sauti moja na Jamhuri ya Maulamaa ni kuwa kutahiriwa ni wajibu kwa wanaume na wanawake…”



Ninasema (Abuu Maalik): “Ama kutahiriwa mwanamume, inavyoonekana ni kuwa jambo hilo ni la lazima kutokana na dalili zifuatazo:



1- Hilo ni mila ya Ibraahiym (‘Alayhis Salaam). Kwani imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:



((أختتن إبراهيم خليل الرحمن بعد ما أتت عليه ثمانون سنة))

((Kipenzi cha Ar-Rahmaan Ibraahiym alitahiriwa baada ya kufikisha miaka 80)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6298) na Muslim (370)].



Na Allaah Mtukufu Anamwambia Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):



((ثُمَّ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ أَنِ اتَّبِعْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفاً وَمَا كَانَ مِنَ المُشْرِكِينَ))

((Kisha Tukakufunulia ya kwamba ufuate mila ya Ibraahiym mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina)).[ An-Nahl (16:123].



2- Ni kwa yale yaliyopokelewa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia mtu mmoja aliyesilimu:



((ألق عنك شعر الكفر واختتن ))

((Jitakase na taka za ukafiri na utahiriwe)). [Al-Albaaniy ameifanya Hadiyth Hasan kwa



Hadiyth nyingine kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (356) na Al-Bayhaqiy (1/172). Katika Sanad yake kuna wapokezi wawili wasiojulikana pamoja na mkatiko. Lakini Al-Albaaniy amesema kuwa ni Hadiyth Hasan kwa Hadiyth nyingine kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine aliyoinasibishia katika Swahiyh ya Abuu Daawuud (383). Na katika “Al-Irwa’i” (79), “mimi sikuviona”. An-Nawawiy na Ash-Shawkaaniy wamesema kuwa ni Dhwa’iyf].



3- Kwamba kutahiriwa ni katika ‘ibaadah ya Waislamu, na ni sifa yao maalumu inayowatofautisha na Mayahudi na Wakristo. Na kwa ajili hiyo, imekuwa ni wajibu kama zilivyo ‘ibaadah nyinginezo.



4- Ni kwamba kutahiri ni kukata sehemu ya mwili, na hili ni haramu, na la haramu halihalalishwi ila kwa la wajibu.



Haya ndio madhehebu ya Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad. Lakini Maalik amelichukulia msimamo mkali na kusema: “Mtu ambaye hakutahiriwa, basi hafai kuwa Imaam na ushahidi wake haukubaliwi”. Na Maulamaa wengi wamenukulu toka kwa Maalik akisema kuwa hilo ni Sunnah. Lakini kuacha Sunnah kwa mujibu wa Maalik, ni dhambi. [Tuhfat Al-Mawduwd (uk 113)].



Ama kwa mwanamke, bila shaka sharia ya kutahiriwa amewekewa. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:



(( إذا التقى الختانان وجب الغسل))

((Zinapokutana tupu mbili zilizotahiriwa, ni lazima kukoga)).[Hadiyth Swahiyh. Ibn Maajah ameitoa kwa tamko hili (611). Na katika Swahiyh Mbili, imekuja kwa tamko la: ((Na utupu kuugusa utupu, hakika imepasa kuoga))].



Na "Al-Khitaanaani" ni mahala pa kukatwa katika dhakari ya kijana na utupu wa msichana. Na hii yaonyesha kuwa wasichana walikuwa wakikeketwa.



Kuna Hadiyth zilizopokelewa juu ya wajibu wa kumkeketa mwanamke. Hadiyth zote hizo zimekosolewa. Kati ya Hadiyth hizo ni ile ya Ummu ‘Atwiyyah aliyesema kwamba kuna mwanamke fulani aliyekuwa akikeketa mjini Madiynah. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:



((لا تنهكي، فإن ذلك أحظى للمرأة وأحب إلى البعل))

((Usikate sana, kwani hilo linampa hadhi zaidi mwanamke na linapendwa zaidi na mume)).[Hadiyth Dwa’iyf. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (5271), na amesema ni dhwa’iyf].

Na katika riwaya:



(( إذا خفضت فأشمي ولا تنهكي، فإنه أنضر للوجه، وأحظى عند الزوج))

((Unapokata, basi bakisha kidogo wala usikate chote, kwani hilo linapendeza zaidi usoni na linashabikiwa zaidi na mume)). [Hadiyth Munkar: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Khatiyb katika kitabu cha At-Taariykh (5/327). Tazama pia Jaami’ul Ahkaam An-Nisaa’i (1/19)].



Hadiyth hizi Sanad zake ni Dhwa’iyf ingawa Mwanachuoni Al-‘Allaamah Al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika As-Silsilat As-Swahiyhah (722).



Na kama mambo ni hivi, basi mwenye kusema anaweza kusema: “Kutahiri ni wajibu kwa wanawake kama ilivyo kwa wanaume ingawa Hadiyth hizi ni Dhwa’iyf. Kwani asili ni kuwa wote wawili wako sawa katika hukmu isipokuwa kama kuna dalili ya kuwapambanua, na dalili hiyo haipo”.



Na mwingine anaweza kusema: “Bali hilo ni jambo mustahabu, na ni takrima kwa mwanamke, lakini si wajibu. Na picha ya kupambanua hapa kati ya mwanamume na mwanamke ni kuwa kutahiriwa kwa upande wa mwanamume, kuna maslaha kwake yanayofungamana na utwahara ambao ni moja kati ya sharti za Swalaah. Kwani endapo kama govi hilo litabakia, basi mkojo hubaki na hujikusanya ndani”. [Muono huu ameuelezea Mwanachuoni Al-‘Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu) kama ilivyo katika Al-Mumti’i (1/134)].



Ama kwa upande wa mwanamke, faida kubwa kwake ni kuwa kukeketa humpunguzia matamanio yake. Na hii ni kutafuta ukamilifu na wala si katika mlango wa kuondosha adha.



Ninasema (Abuu Maalik): “Kukeketa wanawake kunazungukia kati ya mustahabu na wajibu. Na imepokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:



(( الختان سنة للرجال مكرمة للنساء))

((Kutahiriwa ni Sunnah kwa wanaume na ukirimio kwa wanawake)).[Hadiyth Dhwa’iyf].



Lakini Hadiyth hii ni dhwa’iyf. Na lau kama ingelikuwa ni Swahiyh, basi ingemaliza mzozo. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi."
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



019-Kupiga Mswaki



Alhidaaya.com







Maana Yake Na Usharia Wake



Ni neno linalotokana na kitenzi (ساك) anaposugua. Ama maana ya kiistilahi ni kutumia kijiti au mfano wake kwenye meno ili kuondosha unjano na mabaki mengineyo. [Nayl Al-Awtwaar (1/102)].



Inapendeza zaidi kutumia mswaki nyakati zote kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( السواك مطهرة للفم، مرضات للرب))

((Mswaki ni utwaharisho kwa mdomo, na maridhio ya Mola)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (1/50), Ahmad (6/47, 62) na wengineo.]



Kupiga mswaki kunakuwa ni mustahabu zaidi katika nyakati zifuatazo:





1- Wakati wa kutawadha



Ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((لَوْلَا أَنْ أَشُقَّ عَلَى أُمَّتِي لَأَمَرْتُهُمْ بِالسِّوَاكِ مع الوُضُوءٍ))

((Lau kama si kuuonea uzito umma wangu, basi ningeliwaamuru kupiga mswaki sambamba na wudhuu)).[Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad, nayo iko katika Swahiyh Al-Jaami’i (5316)].





2- Wakati wa kuswali



Ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((لَوْلَا أَنْ أَشُقَّ عَلَى أُمَّتِي لَأَمَرْتُهُمْ بِالسِّوَاكِ عند كل صلاة))

((Lau kama si kuuonea uzito umma wangu, basi ningeliwaamuru kupiga mswaki kila wakati wa Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6813), na Muslim (252)].





3- Wakati wa kusoma Qur-aan



Ni kutokana na Hadiyth ya ‘Aliyy anayesema: “Tumeamrishwa kupiga mswaki. Amesema (yaani Rasuli): ((Mja anaposimama katika Swalaah, humjia Malaika akasimama nyuma yake huku akiisikiliza Qur-aan na kumsogelea. Huendelea kusikiliza na kumjongelea hadi anakiweka kinywa chake kwenye kinywa chake. Na hapo mja hasomi Aayah yoyote, isipokuwa huingia ndani ya kinywa cha Malaika huyo)). [Al-Al Baaniy kasema ni Swahiyh. Al-Bayhaqy ameifanyia “ikhraaj” (1/246). Angalia kitabu cha Asw Swahiyhah (1213).





4- Wakati mtu anapoingia nyumbani kwake

Ni kutokana na Hadiyth ya Al Miqdaam bin Shurayh toka kwa baba yake. Anasema:

“Nilimuuliza Aa’ishah: Ni jambo gani la kwanza alilokuwa akilifanya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapoingia nyumbani? Akasema: Ni kupiga mswaki”.



5- Wakati wa kuamka kwa ajili ya Swalaah ya Usiku



Ni kutokana na Hadiyth ya Hudhayf anayesema:

((Rasuli Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam alikuwa akiyasafisha meno yake kwa mswaki wakati anaposimama kuswali tahajjudi)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (246) na Muslim (255)].



Ni vizuri zaidi kutumia mswaki wa miti (Al Araak) wakati wa kupiga mswaki. Na kama haukupatikana, basi utatosheleza mswaki wa aina nyingine wenye uwezo wa kusafisha kinywa na kung’arisha meno. Ni kama miswaki ya brashi pamoja na dawa maalum za meno. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi
 
Swahiyh Fiqh As-Sunnah



Mlango Wa Twahara



020-Je, Kuna Wakati Maalum Wa Kukata Kucha, Kukata Sharubu,

Kunyofoa Nywele Za Kikwapa Na Kunyofoa Kinena?





Alhidaaya.com





Mambo haya hayana wakati maalumu wa kuyafanya, bali kinachoyadhibiti ni haja. Wakati wowote mtu anapohisi kwamba anahitajia kulifanya moja wapo, basi huo ndio wakati wake. La muhimu ni kuwa mtu asijiachie zikapita zaidi ya siku arobaini bila ya kufanya chochote. Na hii ni kutokana na Hadiyth ya Anas aliyesema:



((Tumewekewa muda wa kuwa tusiachie zikapita siku zaidi ya arobaini bila kukata sharubu, kukata kucha, kunyofoa nywele za kikwapa na kunyoa kinena)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (275) na wengineo].
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…