Nilikuwa naomba utupe darasa namna ya kutawaza na kuanza kuswali na hatua zake zote kama itapendeza utuandikie kwa kiarabu na utafsili kk wa kiswahili kwa asiyejua imraisishie kutamka natanguliza shukran kwa tunapo iendea Ramadhan
Bismillahi Rrahmani Rrahiim
Sifa njema na shukrani za dhati zinamstahiki Mola ambaye amewapa ubora wanaadamu kwa elimu na matendo juu ya viumbe vyote.
Na rehma na amani ziwe juu ya Mtume Muhammad Bwana/Kiongozi wa waarabu na wasiyo waarabu, na rehma na amani ziwe juu ya watu wa nyumbani kwake (familia yake) na sahaba zake ambao ni chemchemi za elimu na hekima.
Ijapokuwa ombi lilielekezwa kwa mtu mwengine ila si vibaya kusaidiana katika kheri. Kuhusu udhu tutakwenda hatua kwa hatua kama mtiririko wa vitabu vya fiqhi vilivyoanza kwa kuweka wepesi na mtu apate uelewa wa haraka kuhusiana na suala zima la udhu na kuendea ibada.
Kwenye udhu kuna vipengele vifuatavyo:
1)Furuudhul udhui (faradhi za udhu)
2)Sunanil udhui (sunna za udhu)
3)Nawaaqidhul udhui(vitenguzi vya udhu). Aidha, kuna;
4)Sharti za udhu.
I: FARDHI ZA UDHU
Fardhi za udhu zipo 6. Ya kwanza ni;
1)Nia
2)Kuosha uso
3)Kuosha mikono mpaka kwenye mirfaqi
4)Kupaka maji kichwani
5)Kuosha miguu mpaka kwenye vifundo vya miguu (kurefusha kiasi si mbaya)
6)Kufuata utaratibu.
I:1 UFAFANUZI NIA
Fardhi ina maanisha vitu vya lazima. Nia ni wakati unaosha uso kwa wakati mmoja. Ukipenda unaitamka ukipenda inakaa moyoni.
I:2 KUOSHA USO
Uso ki fiqhi wanaufafanuaje: Uso ni kuanzia maoteo ya nywele kutoka juu mpaka chini ya taya kwa urefu (na taya inaishia karibia na shingo). Sikio mpaka sikio kwa upana. Sehemu yote ya uso lazima ipate maji. Ikiwa una ndevu chache lazima zishike maji. Ikiwa una ndevu nyingi ni zishike maji kwa nje si lazima uzitifue zishike maji mpaka ndani.
I:3 KUOSHA MIKONO
Kuosha mikono ni mpaka kwenye mirfaqi (kifundo cha juu kuelekea sehemu yenye kigimbi). Ikiwa kama mtu alipata ajali kikabakia kiwiko basi aoshe sehemu iliyobaki. Ikiwa kama imekatika mpaka kwenye mirfaqi basi aoshe sehemu ya juu iliyobaki hata kama kwa udogo.
I:4 KUPAKA MAJI KICHWANI
Hapa faradhi ni kupaka maji sehemu ya kichwa tena mara moja, si kichwa kazima (sunna ndiyo kichwa kizima ila faradhi ni sehemu ya kichwa).
I:5 KUOSHA MIGUU
Kuosha miguu mpaka kwenye vifundo viwili vya miguu na kuhakikisha vidole navyo vinapata maji.
I:6 KUFUATA UTARATIBU
Nao ni kama ulivyoelezewa kwa mtiririko wa juu. Ikiwa uliosha uso na upo kwenye hatua ya kuosha miguu na ukagundua kuna sehemu ya uso haijapata maji, basi unatakiwa kuanzia hapo hapo kwenye uso na uhakikisha wote unapata maji na kisha unamalizia kwa utaratibu kama nilivyoelezea juu. Ikiwa ni mikono nayo ukagundua haikushika maji yqani hukuosha vizuri basi utaanzia hapo hapo kwenye mikono na kisha kuendelea na utaratibu.
II: SUNANIL UDHUI (SUNNA ZA UDHU)
Sunna za udhu ni zifuatazo: Kupiga mswaki, kusema bismillah, kuosha viganja viwili kabla ya kuingiza mikono kwenye chombo (ikiwa unatumia chombo), kusukutua, kupandisha maji puani, majosho kuyafanya mara tatu, na sunna ya kichwa kupaka maji kichwa kizima yaani chote. Kuesua vidole vya miguu kwa kutumia kidole kidogo cha mkono wa kushoto kwa kuanzia kidole kidogo cha mwisho wa mguu wa kulia mpaka kurudi nyuma kidole gumba cha mguu wa kulia na kisha kuanzia kidole gumba cha mguu wa kushoto mpaka kumalizia kabisa n.k Pia unasomo dua ya kumaliza kushika udhu.
NB: NAMNA YA KUTIA UDHU
Utaanza kwa kusema Bismillahi , kisha;
1)Utaosha viganja vyako mara 3, kisha
2)Utasukutua maji mdomoni mara 3
3)Kisha, utapandisha maji puani na kupenga × 3, kisha
4)Utaosha uso × 3 (kwa utaratibu wa juu kama ulivyofafanuliwa, na kwa wakati huo unaitamka Nia yako kwa maana moyo wako uwe dhahiri kuwa unatia udhu). Kisha,
5)Utaosha mikono ×3 (kurefusha mpaka juu yake si mbaya)Kisha
6)Utapaka maji kichwani kwa viganja vyako kushika maji kisha utapaka kwa kuanza mbele sehemu ya kichwa na mikono yako utairudisha nyuma ya kichwa na kisha unaipeleka mbele, na hali ya kuwa unamaliza tukio la mikono kumalizikia kwa mbele, vidole vyako vya shahada vyote viwili unasafisha masikio kwa ndani na vidole gumba vinasafisha kwa nje. Hili tukio unafanya mara moja.
7)Kisha, unamalizia kwa kuosha miguu (kurefusha mpaka juu yake si mbaya) kama utaratibu wa juu ulivyoelezewa
8)Baada ya hapo unamalizia dua ya kutia udhu.
Nayo ni hii: Ash hadu anlaa ilaha illallah wah daw laa shariika lah wa ash hadu anna muhammadan abduhu warasuuluh, Allahummaja-alnii minal mutatwahhirin waja-alnii min ibaadikas swaalihiin subhanakallahuma wabihamdika, ash hadu anlaa ilaha illa anta astaghfiruka wa-atuubu ilayka.
Utiaji udhu wa namna hii ni kwa mujibu wa mwenendo wa Imam Shafii.