🕌 Khutuba ya Ijumaa :

Mada – Kuacha Maasi na Kurudi kwa Allah


Khutuba ya Kwanza:

Alhamdulillahi rabbil-‘aalamin. Tunamshukuru Allah kwa neema ya uhai, uislamu, na kutuwezesha kufika siku hii tukufu ya Ijumaa. Tunamsifu na kumuomba msamaha wake. Tunamuomba Allah awateremshie rehma na amani Mtume wetu Muhammad ﷺ, familia yake, maswahaba wake, na wote wanaofuata njia yake kwa uaminifu hadi siku ya mwisho.

Ndugu zangu Waislamu,
Leo tunazungumzia jambo nyeti na la msingi sana katika maisha yetu ya kila siku – kuacha maasi na kurudi kwa Allah.

Maasi ni sababu kubwa ya matatizo katika maisha ya mtu binafsi, familia na hata jamii nzima. Allah anasema katika Qur'an:

“Madhara yameonekana katika nchi na bahari kwa sababu ya yale yaliyofanywa na mikono ya watu, ili Allah awaonyeshe baadhi ya (matokeo ya) waliyo yatenda, huenda wakarejea (wakafanya toba).”
(Surat Ar-Rum: 41)

Maasi hupunguza baraka, huzua matatizo yasiyoisha, na kuifanya nafsi ya mtu kuwa nzito kwa ibada. Wakati mwingine tunashangaa kwa nini dua zetu hazijibiwi — ni kwa sababu ya madhambi ambayo tunayafanya wazi au kwa siri.

Mtume Muhammad ﷺ amesema:
*“Mja anapofanya dhambi, doa jeusi huandikwa moyoni mwake. Akiendelea kufanya dhambi, doa huongezeka mpaka moyo wake hufunikwa...”
(Hadith - Tirmidhi)

Ndugu zangu, tusidharau dhambi. Dhambi huanza kidogo, lakini huathiri sana maisha ya mtu. Kila mja anapaswa kujichunguza. Je, tuko karibu na Allah au mbali naye? Turejee kwa toba kabla ya kutubainikia mauti.

Khutuba ya Pili:

Alhamdulillah. Ndugu zangu waislamu, toba ni njia ya huruma ya Allah. Hakuna dhambi kubwa mbele ya Allah iwapo mja atatubu kwa ikhlasi. Allah anasema:

“Sema: Enyi waja wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msiikate tamaa na rehema ya Allah. Hakika Allah husamehe madhambi yote. Hakika Yeye ni Msamehevu na Mwenye kurehemu.”
(Surat Az-Zumar: 53)

Tusione haya kurejea kwa Allah. Toba ya kweli ni ile inayoambatana na majuto, kuacha kabisa maasi, na kujitahidi kutorudia tena.

Ili tuwe salama na maisha yetu yawe na baraka, yafuatayo ni muhimu:
  • Kuswali kwa wakati.
  • Kujiepusha na dhambi, hata zile "ndogo".
  • Kusoma Qur’an na kuitafakari.
  • Kuwa karibu na watu wema.
  • Kuomba dua ya msimamo katika dini.

Mtume ﷺ alituombea dua:
“Ewe Mgeuzaji wa nyoyo, uthibitishe moyo wangu juu ya dini yako.”

Tumalizie kwa kumuomba Allah:
Ewe Allah! Tujalie tuache maasi, utupe nguvu ya kutii, turehemu na utusamehe. Tufishe hali ya uislamu, na tuingie peponi bila adhabu. Ameen.

Wassalamu Alaikum Warahmatullah Wabarakatuh.
 
Nukuu ya matumaini kutoka kwa Mtume Muhammad ﷺ:

"Ajabu ya hali ya Muumini! Hakika hali yake yote ni kheri. Na hilo si kwa yeyote isipokuwa kwa Muumini: Akipewa neema anashukuru, na hiyo ni kheri kwake. Akipatwa na shida anasubiri, na hiyo ni kheri kwake."
(Hadith - Muslim)

Hii inatufundisha kuwa hata katika matatizo, kuna baraka endapo tutavumilia kwa subira.
 
Kuzini Kabla Ya Ndoa Ni Dhambi? Baada Ya Kuolewa Amegundua Mume Hana Nguvu Za Kiume, Aachike Asiingie Katika Maasi?
Maswali: Zinaa-Liwati



Asaalaaam Aleykum

Nina swali linanitatiza kuzini kabla ya ndoa ni dhambi na ikitokea ukampenda mtu na kufunga ndoa bila kukutana kimwili halafu baada ya ndoa unagundua mwenzio ana mapungufu ya nguvu za kiume na tayari mna watoto, na kuzini nje ya ndoa ni dhambi kumuacha mume kwa ajili ya tatizo hilo sidhani kama ni haki, na kujisaidia mwenyewe kujipunguzia tamaa ya mwili ni dhambi je unashaurije hapa. Mume nampenda na sitaki kuwanyima watoto mapenzi ya baba na mama.









JIBU:



Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.



Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuzini kabla ya ndoa na matatizo ya ukosefu wa nguvu za kiume.



Hakika ni kuwa ni dhambi kubwa kwa mwanamme na mwanamke kuzini kabla au baada ya ndoa. Japokuwa madhambi ya kuzini ndani ya ndoa ni makubwa zaidi hata adhabu yake hapa duniani ni kubwa zaidi kuliko zinaa kwa wale wasioa au kuolewa.



Allaah Aliyetukuka Ametuonya juu ya zinaa pale Alipotuambia:

“Wala msikaribie zinaa kwani huo ni uchafu na ni njia mbaya kabisa” (al-Israa’ [17]: 32).



Ama adhabu hapa duniani kwa mwenye kuzini kabla ya kuoa au kuolewa ni kupigwa mijeledi mia moja bila huruma (an-Nuur [24]: 2).



Mapenzi ni kawaida baina wanaadamu kwa jinsi moja au nyingine. Na huenda mwanamke akavutiwa na mwanamme na akatamani kuwa mwanamme huyo awe mumewe kama vile alivyompenda Khadiyjah binti Khuwaylid (Radhiya Allaahu ‘anha) Mtume wa Allaah, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hata hivyo, mapenzi hasa ya jinsia mbili tofauti ni baada ya kufungamana kwa uhusiano unaokwenda sambamba na shari’ah ya Kiislamu.




Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:




Kufanya Mapenzi Bila Ya Kitendo Cha Ndoa Kwa Ambaye Hajaolewa?




Kulala Pamoja Bila Ya Kufunga Ndoa









Ni hakika kuwa baada ya kuoana ndio hujitokeza mambo mengi sana baina ya wanandoa. Na huja wakagundua mambo ambayo walikuwa hawayajui hivyo kuwa ni changamoto kubwa sana baina ya wanandoa ambayo inaweza kutishia uhusiano wao wa kuishi pamoja. Matatizo hayo hutokea kwa mume au mke kwa namna moja au nyingine. Ukosefu wa nguvu kwa mume katika ndoa ni sababu moja ambayo shari’ah imempatia haki mwanamke aende kwa Qaadhi ili aombe talaka. Shari’ah imeliangalia hilo katika madhara ambayo anaweza kuyapata. Kwa hiyo, inabidi mke achague dhara dogo katika madhara mawili. Na katika kesi yako, kuna madhara mawili, moja kubwa la kubaki na mume na huku unazini ambayo kishari’ah mzinifu aliyeoa au kuolewa anahukumiwa kupigwa mawe mpaka kufa au dhara dogo la kuomba talaka ili upate nafasi ya kuolewa na mwanamme mwingine. Hivyo, utaona kuchagua dhara dogo hapo ni nafuu zaidi kwako na kwa dini yako ikiwa unahisi hutoweza kuvumilia kabisa kubaki katika ndoa bila tendo la ndoa.



Hata hivyo, ushauri wetu kwako ni kuwa jaribu kuzungumza na mumeo aende kwa wataalamu wa magonjwa ya uume ili aweze kutibiwa kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufahamisha kuwa hakuna ugonjwa usiokuwa na dawa yake. Kwa kutafuta matibabu huenda ndoto yako ya kubakia na mume unayempenda ikatimia. Wala usikate tamaa kwani Muislamu hafai kukata tamaa na rehema ya Allaah Aliyetukuka. Hata ikiwa hamkufanikiwa na matibabu ya hospitali basi nenda kwa wataalamu wa tiba ya kitwabibu kutumia miti shamba na madawa mengine ya Ki-Sunnah. Pia musisahau nyote wawili kumuomba Allaah Aliyetukuka ili amuondolee mume wako tatizo hilo na Allaah Aliyetukuka ni Mwenye kujibu du’aa zetu. Kwa hivyo, ikiwa umeshindwa kukaa na mumeo na ugonjwa huo kubakia hata baada ya kutafuta matibabu basi unaweza kuomba talaka kutoka kwake au kwa Qaadhi na hiyo ni haki yako.



Ama kujipunguzia matamanio ya kimwili kwa njia moja au nyingine kama kutumia vidude vya kiume vya kutengeneza, kujisaga na njia nyingine zozote ni haramu katika shari’ah ya Kiislamu. Ikiwa unataka kupungunza matamanio basi chukua agizo la Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kufunga. Na pia unaweza kujishughulisha kwa kufanya mazoezi na kuutumia muda wako kwa harakati tofauti ili uweze kuzitumia nguvu za ziada katika mambo hayo ya faida kwako kwa mwili.



Ikiwa unampenda kweli mumeo basi utamsaidia katika kupata dawa na matibabu ili muendelee kubakia pamoja. Na pia unaweza kumsaidia kwa kutofanya haraka wakati wa tendo la ndoa. Kwa sababu ya udhaifu anatakiwa yeye aende taratibu na wewe pia umuendeshe mumeo taratibu wakati mnastarehe. Mnaweza kuanza na maneno matamu yanayohusiana na tendo hilo la ndoa, busu, kushikana shikana na mwisho kabisa tendo lenyewe. Kufanya hivyo kunaweza kumweka yeye katika hali nzuri na yale mapungufu yakafunikika.



Twawaombea kila la kheri katika uanandoa wenu pamoja na kutatulika kwa udhaifu huo wa mumeo inshaAllaah.



Na Allaah Anajua zaidi
 
Kuzini Na Kushika Mimba Nini Hukmu Yake
Maswali: Zinaa-Liwati
SWALI:



Assalam aleykum warahmatuLLAH wabarakaatuh. shukran ndugu zetu kwa kutuelimisha mengi na inshALLAH Mungu atakulipeni kheri kwa jitihada zenu.



Amma baad. Mimi napenda kuuliza, je kama mwanamke hajaolewa na akabainika amepata ujauzito bila ya mume je ujauzito huu unaweza ukasimama kama ni ushahidi wa kuwa yeye ni mzinifu? Na kama jibu ni ndio, je kama nchi anayoishi ni nchi inayohukumu kiislam atapaswa kupata adhabu ya kiislam ya mzinifu? Pia kama ni kesi ya mke wa mtu ambae mume wake anaishi mbali na yeye, lakini mke wa mtu huyu akapata ujauzito bila kuwepo mumewe jee ujauzito huu utamfanya mwanamke ahukumiwe kifo cha mawe katika nchi zinazohukumu kiislam? Wassalam aleykum.



WABILLAHI TAWFIQ




JIBU:



Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.



Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu hukumu ya kuzini na kushika mimba.

Ni jambo linaloeleweka kuwa Shari‘ah ya Kiislamu ni samehevu kwa kiasi kikubwa na ikiwa upo uwezekano wa kuondosha adhabu basi hakimu anatakiwa afanye hivyo. Yapo mambo kadhaa ambayo yanatakiwa yafahamike ile tuweze kupata uamuzi muafaka kwa suala hili bila ya kubakisha utata wa aina yoyote ule. Mambo yenyewe ni kama yafuatayo:



1. Inatakiwa mwanzo tuelewe maana ya uzinzi. Nayo ni kujamiiana kati ya mwanamme na mwanamke bila ya kuwa na uhusiano wa kishari’ah wa mume na mke kati yao kwa hiari yao bila ya kutenzwa nguvu. Wawili hao waweza kuwa wameoa au kuolewa au hawajahi kuoa au kuolewa.



2. Kiislamu zinaa ni uovu na uhalifu wenye kustahiki adhabu kinyume na nadharia nyingine zote.



3. Uislamu hautegemei sharia ya kuadhibu ili kuokoa ubinadamu kutokana na hatari ya zinaa bali umeweka mikakati na hatua za marekebisho na kuzuia kwa kiwango kikubwa. Ki Shari‘ah, unatoa adhabu kama hatua ya mwisho baada ya kuwafundisha na kuwahimiza watu warekebishe tabia zao na unawachukulia hatua madhubuti za kuwazuia watu wasizini. Lengo halisi la Uislamu, ni kwamba watu wasizini kabisa, na kamwe lisitokee tukio la kulazimisha kuitumia hiyo adhabu kali sana. Kwa ajili ya lengo hilo, Uislamu kwanza kabisa unamtakasa mtu: humjaza mtu hofu ya Allaah Aliyetukuka, Mwenye uwezo wa kila kitu na kumpatia matarajio ya kuwa mahali pema lau atafuata maagizo na kuacha makatazo.



4. Zinaa yenye kuhukumiwa adhabu ni ile ambayo kichwa cha mwanamme cha dhakari yake itaingia kwa mwanamke hata kama ni kidogo. Kukutwa mwanamme na mwanamke kitandani kuwa wamekumbatiana, wako uchi, wanapigana busu, haya yote hayatoshi kuamua kuwa wao wamezini.



5. Ukweli tu kuwa mtu amezini hautoshelezi kumchukulia kuwa ni mhalifu. Kwani yapo masharti ambayo lazima yatekelezwe na yatimizwe. Ama akiwa hajaoa au kuolewa, mkosa awe ni baleghe, na awe na akili timamu, kwani mtoto au mwendawazimu akizini hakuna adhabu. Ama kuhusu zinaa ya waliooa au kuolewa, yapo masharti ya ziada, nayo ni awe huru (mjakazi anapata adhabu nusu), awe ameoa au kuolewa kihalali, awe pia amejamiiana na mkewe baada ya ndoa na mkosa awe Muislamu (japokuwa Maimaam wengine wamelipinga hilo).



6. Ili kuweza kumhukumu mtu kwa kosa la zinaa ni budi kuthibitisha kuwa amekifanya kitendo hicho kwa radhi yake. Kama mtu atalazimishwa kuzini, yeye si mhalifu wala hastahiki adhabu.



7. Shari‘ah ya Kiislamu haimpi yeyote madaraka isipokuwa serikali kumhukumu mzinzi, na si kingine ila mahakama ya Kiislamu ndiyo yenye mamlaka ya kuwaadhibu wahalifu hao. Ni kongamano la wanachuoni wote kuwa amri iliyomo katika Aayah ya 2 ya Suratun Nuur (24): “Wapigeni mijeledi”, haikuelekezwa kwa watu wa kawaida kuwa ndio wana mamlaka ya kupiga wengine mijeledi.



8. Chini ya Shari‘ah ya Kiislamu, adhabu ya zinaa ni sehemu ya Shari‘ah ya nchi. Hivyo, basi itawathubutikia watu wote katika nchi ya Kiislamu. Ni Imaam Maalik pekee ndiye mwenye rai tofauti na hiyo.



9. Shari‘ah ya Kiislamu haimlazimishi mtu kukiri (kuungama) kosa la zinaa, wala haiwalazimishi wale wenye habari ya tukio hilo kwenda kuiarifu serikali. Lakini kosa likibainika kwa serikali, hapo hamna tena nafasi ya kusamehe. Hiyo ni kutokana na Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Kama yeyote miongoni mwenu ni mhalifu wa maadili, bora abaki katika sitara ya Allaah, lakini akitubainishia kosa lake, bila shaka tutamhukumu kwa Shari’ah ya Allaah” (Abu Daawuud).



10. Chini ya Shari‘ah ya Kiislamu, zinaa si kosa la kulipiwa fidia ya pesa au mali.



11. Serikali ya Kiislamu haitomchukulia hatua yoyote mtu yeyote kwa kosa la zinaa hadi pale utakapothbitishwa uhalifu wake. Bila uthibitisho serikali haitoweza kutoa adhabu. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya al-Bukhaariy na Ibn Maajah juu ya mwanamke aliyekuwa akiendesha umalaya Madiynah, kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Kama ningekuwa wa kumpiga mawe mtu yeyote hadi kufa bila uthibitisho, kwa hakika ningehakikisha kuwa mwanamke huyu amepigwa mawe hadi kufa”.



12. Uthibitisho wa kwanza unaowezekana wa zinaa, ni kwamba ushahidi madhubuti uhakikkishwe dhidi ya mhalifu. Vipengele muhimu vya Shari‘ah ni:

i. Qur-aan inaamuru wazi wazi kuwe na angalau mashahidi wanne walioshuhudia kwa macho yao ili kuthibitisha kosa hilo.

ii. Mashahidi wawe wa kuaminika kufuatana na Shari‘ah ya Kiislamu ya ushuhuda, yaani wasiwe ni waongo.

iii. Mashahidi wote watoe ushuhuda kuthibitisha kuwa wamewaona mwanamme na mwanamke katika kitendo chenyewe cha kujamiiana, kama kidole ndani ya pete.

iv. Uafikiane ushahidi wa mashahidi kuhusu wakati, mahali na watu waliofanya kitendo hicho.



13. Kuna hitilafu ya maoni kuhusu mimba ya mwanamke huru asiye na mume anayejulikana, kuwa mimba hiyo ni ushahidi tosha wa uhalifu wa uzinifu au la. Kwa rai ya ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) huu ni ushahidi tosha na Imaam Maalik ameifuata rai hiyo. Hata hivyo, wengi wa wanachuoni wana rai kuwa mimba tu si thibitisho la kumpelekea mwanamke kurujumiwa au kupigwa mijeledi mia moja. Ni lazima adhabu kali kama hiyo zijitegemeze aidha juu ya ushahidi au kukiri kosa kwa mtuhumiwa mwenyewe. Moja kati ya kanuni za msingi za Shari‘ah ya Kiislamu ni kwamba faida ya shaka imwendee mshitakiwa. Na hili linaungwa mkono na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Epukeni adhabu kila mnapokuta mpenyo wa kuiepuka” (Ibn Maajah). Amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Jaribuni kuepuka kuwaadhibu Waislamu kila inapowezekana, na kama kuna njia ya mshitakiwa kuiepuka adhabu, mwachilieni. Kosa katika hukumu ya kumwachilia mshitakiwa ni bora kuliko kosa katika kumwadhibu bila haki” (at-Tirmidhiy). Kufuatana na kanuni hii, kuwepo kwa mimba si ushahidi thabiti wa zinaa, japokuwa una nguvu sana upande wa shaka, kwani upo uwezekano wa mbegu ya kiume kuingia hata bila ya kujamiiana, na hivyo kumfanya mwanamke kupata uja uzito. Hata uwezekano huo mdogo wa shaka unatosha kumwepusha mshitakiwa na adhabu ya kutisha na kali ya zinaa.



14. Badala ya ushuhuda, kitu kingine kinachoweza kuthibitisha hatia ya zinaa ni kukiri kwa mhalifu mwenyewe. Kukiri huku ni lazima kuwe kwa maneno wazi na rahisi, na mhalifu ni lazima akubali kuwa amezini na mwanamke au mwanamme aliye haramu kwake. Pia ni lazima akiri kuwa kitendo cha zinaa kilikamilika kwa hali zote. Mahakama nayo iridhike kwamba mhalifu anakiri kosa kwa hiari na kuwa akili yake ni timamu wala si mlevi. Jambo la kujitolea ushahidi mwenyewe lilifanyika katika uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe naye akaamuru wahalifu watiwe adhabu ya kishari’ah. Mfano ni mwanamme Ma‘iz bin Maalik al-Aslamiy na la yule mwanamke wa Ghaamidiyah.



15. Kulingana na kesi hizo mbili zilizotajwa kwa muhtasari hapo juu ni wazi kuwa aliyekiri kuzini hatasailiwa kuhusu mtu aliyezini naye.



Hizi ni baadhi ya nukta na vipengele muhimu ambavyo vitatusaidia kuhusu masuala ya kuadhibiwa kwa mzinifu mwanamme au mwanamke. Kwa muhtasari ni kuwa ujauzito si ushahidi tosha kwa uhalifu wa zinaa kwani mwanamke akileta tashwishi ndogo sana basi adhabu ni lazima iondolewe kwake.

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

Nini Hukmu Ya Kuzini Ndani Ndoa?

Nini Hukumu Ya Mwenye Kuzini Kwa Siri?

Nini Hukmu Ya Watoto Wa Nje Ya Ndoa?

Na Allaah Anajua zaidi
 
Kuzini Ndani Ndoa Nini Hukmu Yake?
Maswali: Zinaa-Liwati


SWALI:

Assalaam alaykum.

Kwanza natoa shukran zote kwa kuwepo website hii na pia nawapa shukran nyote munaoa tusaidia tuliyokua hatuyajui nawatakia kila la kheir shukran

Swali langu ni.

Naomba kuuliza kua mke akiwa amezini na akamtamkia mume wake kua amefanya hicho kitendo itakua ameachika kwa kufanya hicho kitendo au mpaka mume ampe talaka ndioa kaachika. Na pia itakua mke keshaharamika kwa mume wake? Au, naomba majibu inshaalla mapema ikiwezekana ameen







JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran kwa ndugu yetu kwa swali lako hili. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuepushe na magonjwa haya ya zinaa na maasiya mengineyo. Ieleweke kuwa mke ana madhambi kwa kitendo hicho chake cha kuzini. Kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Allaah, wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Allaah isipokuwa kwa haki, wala hawazini - na atakayefanya hayo atapata madhara, Atazidishiwa adhabu Siku ya Qiyaamah, na atadumu humo kwa kufedheheka” (25: 68 – 69).

Lau kama kungelikuweko Dola ya Kiislamu ambayo ingelitimiza adhabu ya kumpa mwenye kuzini, basi bila shaka maasi haya yangeliogopewa na kila Muislamu. Hivyo bila shaka hakuna yeyote ambaye angelithubutu kufanya maasi haya.

Hivyo ingelibidi kwa kukiri kwake kuwa kazini, hukumu yake ingekuwa ni kuuliwa kama ndio Hadd (Adhabu) yake hapa duniani, na kesho Akhera atakuwa amesamehewa. Hadd yake ni kupigwa mawe mpaka kufa.

Mke kama huyu bado hajaachika mpaka mume wake ampatie talaka.

Mke huyo bado ni mke wa mtu na ikiwa mume atamsamehe kwa kule kutaka msamaha kwake basi ndoa yao itabakia vile vile. Na lau mume ataona kuwa hataweza kubaki naye basi atampatia talaka naye atakuwa ni mwenye kukaa eda lakini kwa sababu ya kosa lake hatakaa kwa mumewe. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

“Ewe Nabii! Mtakapo wapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao. Na fanyeni hisabu ya eda. Na mcheni Allaah, Mola wenu Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Allaah, msiikiuke. Na mwenye kuikiuka mipaka ya Allaah, basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui; labda Allaah ataleta jambo jengine baada ya haya” (65: 1).

Maelezo ya maana ya Aayah hii kama alivyoelezea Shaykh 'Abdallah Swaalih Al-Farsy katika 'Qur-aan Takatifu'.

Surah hii inataja habari nyingi zilizokhusiana na talaka. Talaka kama alivyosema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) dhahiri shahiri katika Hadithi zake.

Talaka imewekwa itokee itakapotokea dharura iwe kama dawa si chakula. Na wenye kuoana wa kikwetu wameifanya talaka ndicho chakula cha ndoa, lazima kutokea kwa kila mwenye kuoa.

Basi hapa zinatajwa kidogo sharti za kuacha:

i) Fatwalliquu-hunna li'ddatihinna

Na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifasiri tamko hili kwa kuwa hapana ruhusa kumuacha mwanamke anapokuwa yumo:

a) Miezini au

b) Katika tahara lakini wampeta kuonana katika tahara hiyo.

Mwanamume akipandwa na hamaki akataka kumuacha mkewe hana ruhusu kumuambia: "Nimekuacha". Lazima amuulize kwanza yumo miezini (katika hedhi) au safi. Akiwa yumo miezini hana ruhusa kumuacha. Akimuacha atapata dhambi. Wala mtu asiyaonee ajabu haya. Haya yanatajwa katika vitabu vyote vya Fiqhi, vikubwa na vidogo hata katika kijitabu kidogo hiki cha Safina.

Kama yuko miezini, basi itampasa angojee mpaka aingie katika tahara ndipo amuache. Na Wakati huo hawataachana tena kwani shetani atakuwa kisha kuruka zamani.

Na ikiwa yumo katika tahara waliyoingiliana, basi lazima angojee mpaka tahara hiyo ishe, aingie miezini, ishe ada yake ya mwezi aingie katika tahara. Kabla ya kuingiliana amuache. Wala hawataachana vile vile kwani shetani atakuwa ameruka zamani.

ii) Laa tukhrijuuhunna min buyuutihinna



Msiwatoe katika majumba yao. Yaani ukimuacha huna ruhusa kumtoa nyumbani. Asalie katika nyumba hiyo hiyo kwa kula na kupewa nguo mpaka eda yake ishe, kama ilivyo vile katika Aayah ya 6 na ya 7 za Surah hii hii.



Mume ndiye ajitenge chumba mbali na choo mbali. Ikiwa hapana nafasi, basi atoke yeye mume akatafute nyumba nyingine ya kukaa mpaka ishe eda ndiyo bibi atokea na achukue vyake. Na wala hatawahi kutoka kwani pengine watakuwa wamekwisha kurejeana. Inataka awe shetani mkubwa huyo hata muda wa miezi mitatu kuwa bado tu hajawatoka! Basi hii ndio Laalla-Llaaha Yuhdithu Ba'ada Dhaalika Amra.

iii) Wa-ahswul-'iddah

Wadhibiti siku za eda ili warejeane kabla ya kumalizika.

Na Allah Anajua zaidi
 
Mke Baada Ya Kuachika Kaingia Katika Maasi Ya Zinaa, Na Nini Hukmu Ya Mawasiliano Kwa Walioachana?
Maswali: Zinaa-Liwati
SWALI



A. aleykum nafurahi sana na majibu yenu ila nilikua nataka kuuliza
ikiwa mke na mume wameachana na wamezaa watoto lakini yule mwanamke baada ya kuachana na mume akajiingiza kwenye ukahaba nini hukum yake? Na ni halali kuwasliana na mume alieachana nae kwa njia ya simu?





JIBU:



Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.





Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu mke kuingia katika maasiya baada ya kuachwa, na mawasiliano baina ya walioachana.

Hakika mwanamke kuingia kwenye zinaa baada ya kuachwa ni dhambi kubwa. Kama kungekuwa na shar’iah ya Kiislamu yenye kutawala leo hii basi hukmu yake ni kuuliwa.



Hata hivyo, la kufanywa wakati huu ni kutafutwa njia muafaka za kumshauri na kumnasihi aache maasiya hayo kwani ni dhambi kubwa kwake. Na kufanyika hilo kunaweza kutumiwa njia mbali mbali kama vile kutumiwa wazazi wake, jamaa zake, wanavyuoni wa Kiislamu na njia nyenginezo.



Ama mume na mke walioachana wanaweza kuwasiliana kwa simu kwa dharura ima kuhusiana na maslahi ya watoto wao na mfano wa hayo yanayokubalika kishari’ah. Ama mawasiliano ya wao kusalimiana na kukumbushana ya nyuma, hayo ni mambo yasiyofaa kwani yanapelekea kuleta fitna na kukurubia zinaa.



Na Allaah Anajua zaidi
 
Mke Kazini Kisha Kakanusha Kwa Mumewe Kwa Kuapa Nini Hukmu Yake?
Maswali: Zinaa-Liwati


SWALI:

Mme yuko ulaya kaowa afrika kwa kuwakilishwa na ndugu, sasa katika hali yakusubiri safari yakuletwa Ulaya mke katokea kuzini; alipokuja kufika ulaya mme akawa na kapewa habari zote na ushahidi wote wa zina ya mkewe lakini pamoja na ushahidi mke kakataa hadi akalazimishwa kuichukuwa Qu'ran na akapa kwa ajili yakuokoa ndowa na aibu. Kuna kosa hapa? Kwa pande zote mbili. Asalam alaykum warrahmatullahi wabarra



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuzini kwa mke wa mtu. Zinaa ni kitendo kibaya kwa Muislamu mwanamme au mwanamke kufanya na inabidi kila Muislamu kufanya juhudi ya kutoingia katika dimbwi hilo la maasiya. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Amuepushe kila Muislamu na madhambi hayo na mengine.

Zinaa si jambo rahisi mtu tu kusema kuwa mtu Fulani amezini bali kunatakiwa ushahidi kama Alivyosema Allaah Aliyetukuka:

“Na wanaowasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi wane, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio wapotovu” (24: 4).

Hapo juu umetuelezea kuwa upo ushahidi wa kuzini kwa huyo mke bila kutuambia ushahidi wenyewe ni upi na kama ni wa kuonekana kitendo hicho kufanyika, je, ni wa watu wangapi walioshuhudia?. Je, walipatikana mashahidi wanne kama inavyotakiwa? Je, mashahidi hao walikuwa wakimvizia na kumdadisi dadisi? Je, mashahidi walimuona mke huyo akiwa na mwanamme kitandani na uchi wa mume ukaingia katika uchi wa mke kama piston inavyoingia katika engine ya gari? Au ni vipi?

Maelezo hayo yote hayapo katika swali lako. Na kama mlituma watu wakumchunguza mjue ya kwamba mmefanya makosa kisheria. Ikiwa mashahidi hawakufika wanne pia ushahidi wenyewe haukubaliwi kisheria hadi wapatikane wanne. Na ikiwa mnamsingizia tu basi mtakuwa na dhambi kubwa zaidi linahitajia mpigwe bakora themanini kwa ajili ya hilo.

Hakika ni kuwa huwa tunafanya makosa kwa kuoa kisha kumuacha mke mbali ilhali mume yuko Ulaya kwa muda mrefu kabla ya kumchukua. Hiyo inampatia matamanio msichana ambaye yuko peke yake, na shetani wa kijini na wanaadamu ndio huwa wamepata fursa ya kumghilibu mpaka aingie katika madhambi.

Ama kuhusu ibara yako kuwa aliapa kwa kulazimishwa ili kuondoa aibu haifai kamwe kusemwa na Muislamu. Je, ulimfunua kifua chake na ukaona ni hivyo? Sisi tunatakiwa kuhukumu yalio dhahiri na ya siri tumuachie Allaah Aliyetukuka. Ikiwa mke ameapa kuwa hakufanya kitendo hicho basi chukueni dhahiri hiyo. Ama masuala ya kutumia msahafu kuapia, ni mas-ala yasiyo na dalili, msahafu haukuletwa kuapia, bali kinachoapiwa ni jina la Allaah, tena kiapo kiwe cha dharura na si utani utani. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuwa mwenye kubidi kuapa basi aape kwa jina la Allaah. Hakusema aape kwa jina lake (Mtume) au kwa msahafu au kwa chochote kingine.

Ingia katika kiungo kifuatacho upate Swali na Jibu kuhusu kukatazwa kuapia msahafu:

Kuapa Kwa Qur-aan Inafaa?

Na ikiwa mume alikuwa na wasiwasi akaona hataweza kuishi na mke huyo alikuwa afanye hivyo kabla ya kujamiiana naye na kumuachia nusu ya mahari.

Mas-ala ya zinaa tusiyachukulie kwa wepesi kama tunavyofanya kwani ni jambo zito sana.

Twawatakia kila la kheri bwana na bibi ikiwa wameamua kuishi pamoja na kusahau yaliyosemwa kabla.

Na Allaah Anajua zaidi
 
Mke Kazini Kisiri Kisha Mume Kamsamehe, Ni Makosa?
Maswali: Zinaa-Liwati
SWALI:

Halafu ninaswali: tumeambiwa binadamu asokuwa na wivu ni kama nguruwe na ataingiya motoni. Mkee alikuwa akiishi Afrika na mume ulaya wameishi mbalimbali kwa miaka mitatu ikatokea mke amezini halafu kaja kwa mume wake akamuambiya kwamba kipindi kile hawakuwa pamoja ilimtokea kuzini mume akaamuwa amemsamehe (tume ambiwa binadamu asokuwa na wivu nikama nguruwe na ataingiya motoni sasa vipi hapo)? Mtu mke wake kaziniwa kisiri halafu kaomba msamaha kwa mumewe kuapa kuto kurudia akasamehewa sasa vipi kuna makosa? Je, inajuzu?



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kusamehe makosa ya mwenzio. Mwanzo tunataka kurekebisha msemo ulioutaja kuwa asiokuwa na wivu ni kama nguruwe na ataingia motoni si Hadiyth bali huenda ukawa ni msemo wa Kiswahili unaotumiwa na Waswahili. Hata hivyo, tufahamu kuwa hayaa ni katika Imani na hayaa inaelezwa katika machimbuko ya kisheria.

Hakika alilolifanya huyo mwanamke ni jambo chafu na ovu na khiyana ya hali ya juu kabisa. Na si rahisi kwa mtu mwenye ghera kuweza kuendelea kuishi na mtu wa namna hiyo. Lakini pia tufahamu kuwa Uislamu umeweka milango ya toba wazi na kila dhambi linaweza kutubiwa maadam haijafika ile hali ambayo toba haikubaliki tena.

Wanazuoni wanatuambia kuwa toba inatakiwa kwa kila dhambi ambalo mwanaadamu atafanya. Na ili kutubia kwa Allaah Aliyetukuka ni lazima utimize masharti yaliyowekwa, na kwa kuwa swali lako linaingia haki ya binaadamu ndani yake kukubaliwa toba yako ina masharti manne:

i) Kujivua na maasiya (kujiondoa katika madhambi).

ii) Kujuta kwa kufanya dhambi.

iii) Kuazimia kutorudia tena dhambi hilo.

iv) Kutaka msamaha kutoka kwa aliyemdhulumu (Imaam Abi Zakariya

Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy, Riyaadh asw-Swaalihiyn, uk. 41 – 42).

Kulingana na swali lako ni kuwa mke huyo ametekeleza yote hata lile sharti gumu la kuonana na mumewe ana kwa ana na kumueleza alilofanya na kuwa hatafanya tena. Kwa kuwa mume mwenyewe amemridhia na kumuamini huwa makosa yake (mke) yamesamehewa. Hiyo ni kuwa aliyefanyiwa ameridhia na kinyongo kishamtoka.

Kukosa ni ubinaadamu na mbora wa anayekosa ni yule mwenye kutubia na kujirekebisha. Tazama jinsi gani Ma’iz na yule mwanamke wa al-Ghaamidiyah walivyojileta kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kutakaswa kwa kosa lao la kuzini kwa sababu ya kuoa na kuolewa walipigwa mawe hadi kufa. Kwa hukumu hiyo kutekelezwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuwa wametubu kiasi ambacho lau toba yao itagawiwa watu wa Madiynah ingewafunika wote

Tunawaombea kheri baada ya mume kumsamehe mkewe kwa kosa kubwa alilolifanya. Na ni juu ya mke akachukulia ihsani hiyo kwa kutorudia tena daima kosa hilo. Zinaa hasa ikiwa mwanamke ameolewa au mume ameoa ni dhambi kubwa lenye kustahiki adhabu iliyowekwa na sheria. Pia ni juu ya mume isiwe ndio adhaa kutoka kwake kwa sababu ya kumsamehe huko. Awe kweli amesamehe na asiwe ni mwenye kumkumbusha ihsani hiyo mkewe wakati wamegombana.

Na Allaah Anajua zaidi
 
Mke Kuoa Mwanamke (Usagaji) Na Mume Kuoa Mwanamume Mwenziwe (Uliwati) Baada ya Kukubaliana
Maswali: Zinaa-Liwati
SWALI:




Je ikiwa mwanamke akikubali kuoa mke wa mwanaume anaempenda na mwanaume akikubali kuoa mume we na wakaelewana mahali hio inaweza kua ni ndoa tosha. Naomba jibu kwenye hayo masuali maana yake nimekosa jibu ndio mana nimependelea kuwauliza nyie mumetuzidi ilmu.



Ahsante sana SHUKRA










JIBU:




Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.







Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuoana kwa jinsi. Swali hili ndugu yetu halikukaa sawa, lau itakuwa sivyo tulivyoelewa basi utaliandika vizuri ili tupate kuelewana na kukujibu kwa njia safi kabisa.




Tulivyoelewa ni kuwa je, kisheria inafaa kwa mwanamme kumuoa mwanamme mwenziwe na mwanamke vivyo hivyo ikiwa wamekubaliana? Jambo hili katika sheria ni miongoni mwa dhambi kubwa hata kushinda kosa la zinaa. Kujamiiana baina ya mwanamme na mwenziwe na mwanamke na mwenziwe ni kinyume na maumbile na dhambi kubwa lenye kustahiki adhabu kali sana kisheria.




Kwa muhtasari, ndoa hizo hazikubaliki kisheria, ya Kiislamu.




Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:




Zinaa-Liwati




Na Allaah Anajua zaidi.
 
Mke Kupashwa Habari Kuhsu Uzinzi wa Mumewe Na Kaapishwa Kuwa Asitaje Aliyempasha
Maswali: Zinaa-Liwati
SWALI:




Asalaaam aleikum warahmatulrahi wabarakatah. NINA SWALI NATAKA JIBU LAKE; Mke wa mtu kaambiwa na mtu ambaye hataki kumtaja kwa sababu huyo aliesema maneno hayo kamuapisha kuwa asimwabie mtu yoyote na maneno aliyomwambia ni kuwa mume wake ana mwanamke mwingine wa nje (HAWARA) na anatembea nae na kuwa mumewe anafanya mambo mabaya ya qaumu lut na huyo mwanamke. Mke kuambiwa khabari hizo kamkasirikiya sana mume wake wa miaka 30 kafikia hatua ya kudai talaka, Mume kamuapuia kua khabari hizo ni za urongo na fitina tu na kamtaka mkewe amtaje huyo muongo lakini mke hataki kumtaja eti kaapishwa asimtaje. SWALA je akimtaja atadhurika? (kwa kiapo alichokula) na nini hukumu ya huyo mke kusikiza fitina hizo na kutoamini maneno ya mumewe?












JIBU:




Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.




Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mke kupashwa habari na mtu kuhusu uzinzi na ubaya wa mumewe. Hakika tumejirudisha nyuma sana kwa kuwa na mambo kama haya yanayoendlea katika jamii yetu ambayo ni jamii ya kutakia mema na undugu baina yao. Muislamu mwema ni yule ambaye anaziba makosa ya watu na huku anajaribu kuwanasihi ili waache maasiya hayo. Muislamu anatakiwa zaidi awe ni mwenye kunasihi na sio kufedhehi mwingine kwa njia yoyote ile.




Na jameni ndugu Waislamu, fitna hizi zimekithiri na sasa zimeelekea kuvunja majumba ya watu walioishi kwa muda mrefu, miaka thelathini kwa tuhma ambazo hazina msingi wa aina yoyote. Nasaha kwa ndugu zetu ni kuwa ikiwa mtu amekuja kukupasha habari ya mtu yeyote yule inatakiwa umwambie kuwa ngojea nimuite mwenyewe. Kufanya hivyo ni kuweza kupima ukweli wake. Ikiwa ni kweli atakuwa yuko tayari kwa hilo lakini akiwa si mkweli atakuwa ni mwenye kupapatika na kukwambia achana ya suala hilo, basi yaishe na mengineyo mengi. Mtu akikuambia hivyo basi tahadhari naye sana na jaribu kumweuka kwani si mwema kwako.




Kwa sasa cha kufanya ni mambo mawili:




Mwambie yule aliyekuambia kwamba nataka kutatua tatizo hili ambalo umeniletea kwa tunakuta mimi, wewe na mume wangu.






Mwamini mumeo na usahau fitna za watu wenye kutaka kuharibu nyumba za watu.



Na jambo ambalo ni jema kwa mama huyo kufanya ni kutengeneza uhusiano wake na mumewe na aepukane na huyo aliyekuja kutia fitna na kusahau yaliyopita wala usiwe ni mwenye kulitaja tena.







Bonyeza viungo vifuatavyo upate makala muhimu kuhusu fitna kama hii:




Madhara Ya An-Namiymah (Kufitinisha Baina Ya Watu Wachukiane) 1 Maana, Hukumu Na Adhabu Zake




Madhara Ya An-Namiymah (Kufitinisha Baina Ya Watu Wachukiane) 2 - Sababu za Kufitinisha, Sifa Za Mfitinishaji










Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Awaondolee mahasidi na vitimbi vya wafitinifu.




Na Allaah Anajua zaidi.
 
Mtoto Aliyezaliwa Nje Ya Ndoa Nani Walii Wake Na Mwenye Jukumu Naye? Allaah Atamsamehe?
Maswali: Zinaa-Liwati
SWALI:




Asalamalkum,




Nina maswali matatu kuhusu mtoto wa nje ya ndoa (mtoto haramu).




1. akitaka kuolewa au kuoa nani anaetoa idhini?




2. je kama alishaolewa na akaachika kuolewa tena mara ya pili anaweza kuolewa bila kutaarifu kwao?




3. kama mtu aliolewa akiwa ana uja uzito mchanga wa week 4 kwa kuficha aibu yake lakini bila kujua kama hairuhusiwi kuolewa ukiwa na uja uzito na wakazaa watoto 2 na kisha akatengana na mumewe ndipo alipotambua kwamba hawakutakiwa kuowana wakati akiwa na uja uzito je? watoto hawa 2 wote ni wa haramu? Na nani mwenye haki ya kuishi na hawa watoto? Je kuna msamaha juu ya jambo ili mbele ya Allah subuhana wa taala.



naomba sana ufahamisho katika maswaala haya







JIBU:




Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.




Shukrani zetu za dhati kwa maswali yako kuhusu ndoa.

Muislamu kwanza anapaswa kufahamu kuwa hakuna mtoto haramu kwa kuwa kishari’ah mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa si mwana haramu bali kitendo ndicho kilicho haramu.




Mtoto hana makosa kabisa mbele ya shari’ah na anapokuwa mkubwa na akawa mwema basi wema wake utamuingiza yeye Peponi. Huyu mtoto anaitwa mtoto wa kitanda.




Mtoto huyo aliyezaliwa kwa watu wawili waliofanya zinaa akiwa ni mvulana akitaka kuoa hahitaji idhini ya yeyote. Anaweza kupelaka posa mwenyewe au akapelekewa na jamaa zake upande wa mama. Ama msichana anapotaka kuolewa basi kwa kuwa hana wazazi wa kuumeni, Qaadhi akiwepo hapo alipo atakuwa ndiye walii wake au Imaam au Shaykh.




Ikiwa mwanamke huyo ameolewa kisha akaachwa akiwa anata kuolewa mara ya pili itabidi asirudie kosa la mara ya kwanza afuate njia zilizowekwa na shari’ah. Miongoni mwazo ni yeye kukubali kuolewa na huyo mume, kuwepo kwa walii na mashahidi wawili waadilifu.




Kuolewa akiwa mwanamke ana uja uzito haifai lakini ikiwa kumefanyika kwa kutokujua Allaah Aliyetukuka Anasemehe hilo.




Hata hivyo, baada ya kujua ni lazima mke huyo amwambie mumewe kuwa walifanya makosa kuoana akiwa na mimba, kumaanisha huyo mtoto aliyezaliwa si wa baba huyo kabisa. Ama hiyo Nikaah iliyofungwa katika hali hiyo ya uja uzito itakuwa sio sahihi na hivyo mnapaswa mjivue kwenye ndoa hiyo, mtubie na kisha baada ya toba ya kweli mtaweza tena kufunga ndoa upya.




Baada ya kujulikana hilo, ingawa mume hatokuwa na madhambi kwa kufichwa jambo hilo, ila mke atapata madhambi kwa kumficha mumewe.




Ama watoto waliozaliwa baada ya hapo watakuwa ni watoto wa wanandoa hao wawili. Ikiwa mtoto mmoja kati ya hao wawili ni yule aliyekuwa tumboni wakati wa ndoa huyo ndiye atakayekuwa si mtoto wa huyo baba lakini ni mtoto wa mama. Hivyo huyo wa pili ndiye atakayekuwa wa huyo baba.




Mama ana haki ya kuishi na yule aliyekuwa tayari matumboni wakati wa ndoa na huyo wa pili pia akiwa ni mdogo. Mwanamke huyo akiolewa huyu baba atakuwa na haki ya kukaa na huyu mtoto wapili.







Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:




Watoto Baada Ya Ndoa Ya Uzinifu




Nini Hukmu Ya Watoto Wa Nje Ya Ndoa?




Nimeolewa Huku Nina Mimba Nini Hukumu Ya Mtoto Wa Kitendo Cha Zinaa?







Mtoto Aliyezaliwa Nje Ya Ndoa Vipi Anaweza Kutambulishwa Kama Ni Mtoto Wa Nani Kwenye Ndoa Yake, Na Ataandikishwaje Kwenye Cheti










Ama kuhusu kutubia maasi haya ni kwamba Allaah Hupokea toba ya mja Wake kwa maasi yoyote kwani yeye ni Mwingi wa Kughufuria. Linalopasa ni kufanya toba ya kweli ambayo mashari yake kama yafutayo:

1. Kuomba maghfira

2. Kuacha hayo maasi

3. Kujuta na kuweka nia (azma) kuwa hatorudia tena

4. Kuzidisha vitendo vyema

5. Kama kaidhulumu haki ya mtu basi ni kuirudisha hiyo haki.




Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:




Tawbah




Tawbah Ya Kweli Na Masharti Yake




Ndoa Baada Ya Kutubu Zinaa




Kumuoa Aliyezini Baada Ya Kutubia




Wazinifu Waliotubu Wanaweza Kufunga Ndoa Na Waliotakasika







Na Allaah Anajua zaidi
 
Umuhimu wa funga za Sunna katika Uislamu ni mkubwa, na zina faida nyingi za kiroho, kiafya na kijamii. Hapa chini ni baadhi ya faida hizo:

1. Kuleta ukaribu na Allah
Mtume Muhammad (s.a.w) alisema:
"Mja wangu huendelea kujikurubisha Kwangu kwa Sunna mpaka nampenda…" (Hadith Qudsi – Bukhari).
Funga za Sunna huonyesha unyenyekevu na upendo wa mja kwa Mola wake.

2. Kufidia mapungufu ya funga za faradhi
Siku ya Kiyama, funga za Sunna zitakamilisha mapungufu ya funga za Ramadhani kama kuna kasoro.

3. Kusamehewa madhambi
Funga kama ya Ashura au Arafa zinaleta msamaha wa madhambi ya mwaka mmoja uliopita au ujao.

4. Kuendeleza roho ya ibada
Huimarisha nidhamu ya kiroho hata nje ya Ramadhani, na humzoesha Muislamu kuwa mnyenyekevu daima.

5. Faida za kiafya
Kufunga mara kwa mara husaidia mwili kupumzika, kusafisha sumu, na kuimarisha kinga ya mwili.

---

Funga Maarufu za Sunna:
  • Funga ya Jumatatu na Alhamisi – Mtume alikuwa akiifunga mara kwa mara.
  • Funga ya siku sita za Shawwal – Baada ya Ramadhani.
  • Funga ya siku ya Arafa – Kwa wasio Hajj, huondoa madhambi ya miaka miwili.
  • Funga ya Ashura (10 Muharram) – Inafidia madhambi ya mwaka mmoja uliopita.
 
hapa chini ni faida za kila aina ya funga ya Sunna maarufu katika Uislamu:

---

1. Funga ya Jumatatu na Alhamisi
Faida:
- Ni siku ambazo matendo hupandishwa kwa Allah. Mtume (s.a.w) alisema:
"Matendo huonyeshwa kwa Allah siku ya Jumatatu na Alhamisi, nami hupenda matendo yangu yaonyeshwe nikiwa nimefunga." (Tirmidhi)
  • Hukuza utaratibu wa kiroho wa kila wiki.
  • Husaidia kudhibiti matamanio na nafsi.

---

2. Funga ya Siku Sita za Shawwal
Faida:
  • Yeyote atakayefunga Ramadhani kisha akafunga siku sita za Shawwal, huandikiwa thawabu kama aliyefunga mwaka mzima. (Muslim)
  • Huonyesha kuwa mja anaendeleza ibada hata baada ya Ramadhani.
  • Ni njia ya kumshukuru Allah kwa kukamilisha Ramadhani.

---

3. Funga ya Arafa (9 Dhul Hijjah)
Faida:
  • Kwa wasio Hajj, hufuta madhambi ya mwaka uliopita na ujao. (Muslim)
  • Ni siku yenye fadhila kubwa sana, Allah hujivuna kwa viumbe wake mbele ya Malaika.
  • Huinua daraja za mja mbele ya Allah.

---

4. Funga ya Ashura (10 Muharram)
Faida:
  • Hufuta madhambi ya mwaka uliopita. (Muslim)
  • Ni siku ambayo Allah alimnusuru Musa (a.s) dhidi ya Firauni.
  • Mtume alihamasisha kufunga siku hiyo pamoja na ya 9 au 11 Muharram ili kujitofautisha na Mayahudi.

---
 
Hapa kuna ratiba rahisi na inayotekelezeka ya kufunga funga za Sunna kwa mwezi mzima:

---

Ratiba ya Wiki kwa Wiki (Kila Mwezi):

Wiki ya Kwanza:
  • Jumatatu – Funga (Sunna)
  • Alhamisi – Funga (Sunna)

Wiki ya Pili:
  • Jumatatu – Funga
  • Alhamisi – Funga
  • Ijumaa (ikiambatana na Alhamisi au Jumamosi) – Inaruhusiwa

Wiki ya Tatu:
- Tarehe 13, 14, 15 ya kila mwezi wa Hijria – Funga ya Ayyamul Bidh
(hizi ni funga za siku za mwezi wa kiarabu kuwa mpevu, na zina thawabu kubwa – Abu Dawud)

Wiki ya Nne:
  • Jumatatu – Funga
  • Alhamisi – Funga
  • Ikiwezekana ongeza Ijumaa au Jumamosi ukiziambatanisha.

---

Ratiba ya Kipekee ya Miezi Maalum:
  • Mwezi wa Muharram: Funga Ashura (10) na siku ya 9 au 11.
  • Mwezi wa Dhul Hijjah: Funga siku 9 za mwanzo, hasa ya Arafa (9).
  • Mwezi wa Shawwal: Funga siku zozote 6 baada ya Eid.

---

Ushauri wa Utekelezaji:
  • Anza polepole: Funga angalau Jumatatu moja na Alhamisi moja kwa mwezi.
  • Tumia kalenda ya Kiislamu kufuatilia Ayyamul Bidh.
  • Mweke mwenzi wa kufunga nawe, ili mpate hamasa.
  • Siku za Eid (Eid al-Fitr & Eid al-Adha) na siku 3 za Tashriq (11–13 Dhul Hijjah) hazifungwi.

---
 
Ndugu zangu katika imani Allah anasema mwanaadamu yoyote anayoyafanya ni kwa ajili yake mwenyewe,kama akifanya maovu ni hasara kwa nafsi yake na akifanya mema ni kwa faida ya nafsi yake mwenyewe,na hakuna hata mmoja ambaye atadhulimiwa

Kwahiyo mwenye akili ni yule ambaye atakayefanya mambo mema zaidi ili ajikurubishe kwa Allah,mwisho wa siku awe na mwisho mwema
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…