Hali si shwari ZANZIBAR
KUJIUZULU kwa Amina Salum Ali kutoka nafasi ya uwaziri wa nchi katika ofisi ya Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kumeelezwa kubeba ajenda nzito katika upangaji wa mustakabali wa baadaye wa baadhi ya wana-CCM Zanzibar.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili kwa muda sasa unaonyesha kwamba, kuwa ni maandalizi ya mwanasiasa huyo kujenga mazingira ya hatimaye kupata nafasi ya kuwania urais ifikapo mwaka 2010 visiwani kupitia kambi ya Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma.
Mpango huo pamoja na mambo mengine umemuweka katikati ya utekelezaji wake, kada huyo wa siku nyingi wa chama hicho ili asiweze pengine kuguswa na 'mawaa' ya ndani ya serikali ya Karume.
Mtazamo huo ni kinyume kabisa na mawazo ya kambi kadhaa ambazo zimeibuka ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar zinazojipanga na kujiandaa kwa kinyang'anyiro hicho cha kuwania urais wa visiwa hivyo kwamba kambi ya Dk. Salmin imeanza kumomonyoka baada ya kumpoteza Amina kutokana na kujiuzulu kutoka serikalini wiki moja iliyopita.
Amina ambaye alikuwa miongoni mwa wanachama wa CCM waliojitokeza kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais kupitia chama hicho katika hatua za awali mwaka 2000, aliomba kujiuzulu ili apate nafasi ya kutumikia nafasi ya kuiwakilisha Afrika katika Tume ya Umoja wa Mataifa (UN) inayoshughulia masuala ya bara hili, yenye ofisi yake New York nchini Marekani.
Wachambuzi wa masuala ya siasa za Zanzibar wameiambia Mwananchi Jumapili kuwa kuondoka kwa Amina katika serikali ya Rais Aman Karume kumekuja wakati muafaka na kwamba kwa kuwa ndiye mtu ambaye anatazamiwa kuwania kiti cha urais kwa mtazamo wa kambi hiyo, basi kazi hiyo huko nje mpya itampa uzoefu wa kimataifa.
"Kambi yake (kambi inayomuunga mkono Dk. Salmin) walitoa baraka kwa Amina kuondoka, kwanza ili aweze kujiweka mbali na serikali na la muhimu kwao wanadai kuwa ni Amina kujenga uzoefu wa kimataifa na kutafuta uungwaji mkono wa kimataifa," chanzo kimoja cha habari kimedokeza wiki hii.
Amina ambaye mbali ya kuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Kiongozi pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) ya CCM. Ndiye alikuwa kiongozi pekee ambaye ana ushawishi mkubwa katika kambi ya Dk Salmin licha ya kuwa katika SMZ, awamu ya sita chini ya Rais Amani Karume.
Mwananchi Jumapili imeelezwa kuwa kambi hiyo ya Dk. Salmin inaona kuwa Amina anayo nafasi kubwa ya kuweza kuiwakilisha katika kinyang'anyiro cha urais ifikapo mwaka 2010 kwa vile mtu mwingine aliyekuwa akitegemewa zaidi, Dk. Gharib Bilal, Waziri Kiongozi Mstaafu hadi kufikia wakati huo umri wake utakuwa umesogea zaidi kiasi cha kutokuwa na mvuto kwa wapiga kura ndani ya CCM.
Wakati Amina akipata nafasi ya kujitangaza kimataifa, kambi nyingine zinazolenga kuweka wawakilishi wake katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar mwaka 2010 nazo zinaendelea kujiimarisha jambo linazozua mivutano ya uongozi ndani ya SMZ na hata CCM kitaifa.
Kitendo cha Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi kuonekana kuwa ameanza kumpigia debe mtoto wake, Dk. Hussein Mwinyi ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano kuwania urais Zanzibar kinaelezwa kuwa kimemuweka njia panda Rais wa Muungano, Jakaya Kikwete.
Rais Kikwete ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa CCM inadaiwa kuwa anaonekana kuwa kama anamwandaa au kumtayarisha Naibu Waziri wa Usalama wa Rais, Mohammed Abood kuwania nafasi hiyo, kiasi cha kushindwa kumshawishi Mzee Mwinyi kuachana na harakati zake, hivyo kujikuta njia panda.
Mwanasiasa mwingine, Ali Juma Shamhuna, Naibu Waziri Kiongozi ambaye hivi karibuni amekuwa na sauti katika serikali ya Rais Karume ni mtu anayedaiwa kujiandaa kuwania urais 2010 huku akiwa kama vile ameasi kutoka kambi yake ya zamani, ile ya Dk. Salmin.
Habari kutoka ndani ya CCM Zanzibar zinaeleza kuwa Shamuhuna kwa sasa haungwi tena mkono na kundi lolote na kwamba kukubali kuwa msemaji katika masuala ambayo yanakinzana na CCM makao makuu, ni jambo ambalo linaondoa uwezekano wa yeye kuweza kupata nafasi ya kuwania kiti hicho.
Shamuhuna ambaye awali alipanda chati akiwa katika kambi ya Dk Salmin kwa kuwa mstari wa mbele kuikosoa serikali ya awamu ya sita ya Rais Karume alibadilika muda mfupi baada ya kuteuliwa kuwa waziri katika hiyo hiyo serikalini na kutumika kuwa msemaji katika masuala yenye utata.
Wafuatiliaji wa masuala ya Zanzibar wanatoa mfano wa hivi karibuni ambapo Shamuhuna alikuwa mtu wa kwanza kujitokeza wazi wazi kupinga mpango wowote wa kuangalia uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya mseto baina ya CCM na Chama cha Wananchi (CUF) visiwani humo.
Pamoja ukweli wa Shamuhuna kutumiwa na Rais Karume katika kuzungumzia hadharani masuala yenye utata, inadaiwa kuwa si miongoni mwa watua wanaopendekezwa na kambi ya kiongozi huyo kumrithi.
Watu walio karibu na Rais Karume wameiambia Mwananchi Jumapili kuwa chaguo lake ni Waziri Kiongozi wa serikali yake, Shamsi Vuai Nahodha, mtu ambaye anaaminika kuwa amekuwa mtiifu na inaelezwa kuwa tayari 'wazee' walio karibu na uongozi wa SMZ wameonyesha kumkubali.
Maelezo ya ndani kutoka serikali ya Zanzibar na ya Muungano pamoja na CCM ni kwamba suala la urais katika visiwa hivyo, ingawa bado lina zaidi ya miaka minne mbele kabla ya kufika kwa muda wake linaweza kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama tawala, ikiwa Rais Kikwete hataweza kutumia vizuri kete yake ya uenyekiti.