Mengi awataka Watanzania kuacha woga
2007-01-13 09:36:42
Na Joseph Mwendapole
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Bw. Reginald Mengi, amesema woga ni adui mkubwa wa maendeleo na amewataka Watanzania na watu wengine duniani kujiamini wanapotafuta maendeleo.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na ujumbe wa wanafunzi 40 kutoka Chuo Kikuu cha Yale cha nchini Marekani.
Alisema mtu anapotaka kuanzisha biashara ama mradi, anapaswa kujiamini na kuacha woga ili aweze kufanikiwa.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI), Bi. Christine Kilindu na aliyekuwa Mwakilishi wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi David Mwakawago.
Bw. Mengi alisema yeye binafsi alizaliwa kwenye umaskini wa kupindukia, lakini ameweza kufika hapo alipo kutokana na kuamini kuwa anaweza kufanya mambo makubwa.
Alisema mbali na kujiamini, watu wanapaswa kumweka mbele Mwenyezi Mungu katika mambo wanayoyafanya na kwamba wakifanya hivyo Mungu hawezi kuwaangusha.
Alisema mtu anayefanya biashara anapaswa kuwa na wazo na biashara kabla ya kupata mtaji na alionya kuwa kutafuta mtaji kabla ya kupata wazo la biashara kunaweza kusiwe na manufaa.
"Mimi nilipata wazo kwanza kabla ya kutafuta mtaji, niligundua kuwa peni zimeadimika nikaanza kujifunza kutengeneza peni na sehemu ya nyumba yangu nikaigeuza kuwa kiwanda," alisema.
Alisema baada ya kupata wazo la biashara ya kufanya ndipo alipoanza kutafuta mtaji kwa kukopa katika benki mbalimbali.
Alisema kilichomsaidia mpaka kufika hapo alipo ni imani aliyoiweka kwa Mwenyezi Mungu na kujiamini yeye binafsi kuwa anaweza kufanya mambo makubwa.
"Siku zote nilikuwa nikisema kuwa 'I can, I will and I must', na maneno hayo ukiyaangalia ni marahisi lakini yana maana kubwa sana, kujiamini ni kitu kikubwa ili uweze kufanikiwa, " alisema.
Aidha, alisema Watanzania na watu wengine wanapaswa kuona umaskini wanaokabiliwa nao kama changamoto badala ya kuuona kama tatizo endapo wanataka kukabiliana nao.
Alisema katika Bara la Afrika, watu wameshindwa kuondokana na umaskini kutokana na kuuona umaskini kama tatizo, badala ya kuuona kama changamoto.
"Mimi binafsi niliuona umaskini kama changamoto kwa hiyo nikajitahidi kukabiliana nao, kila nilichokabiliana nacho niliona kama changamoto na nikapambana nacho kwa nguvu zote," alisema.
Aliongeza kuwa, watu wengi wanashindwa kupata maendeleo kwa sababu ya umaskini unaowakabili, hali inayowafanya waishi kwenye hali ngumu kwa maisha yao yote.
"Ukiamini kuwa huwezi, mawazo yako yatakuelekeza kuthibitisha kuwa kweli huwezi na ukiamini kuwa unaweza mawazo yako yatakuelekeza kuthibitisha kuwa unaweza," alisema.
Alisema kwa kutojiamini, nchi nyingi barani Afrika zimejikuta zikiita wataalamu kutoka nje ya nchi kufanya kazi ambazo wangeweza kufanya wananchi wa kawaida.
Alisema kuku alishindwa kuruka kama ndege kwa kuwa aliamini kuwa hawezi kuruka angani, hivyo alishauri watu kuiga mfano wa ndege aliyeamini kuwa ana uwezo wa kuruka na akafanikiwa.
Alisema wako watu wanaoshindwa katika masuala mbalimbali kabla ya hata kuanza kutokana na kuweka mbele woga na imani kuwa hawawezi.
Aliwataka wanafunzi hao kuwa wananuia makubwa katika maendeleo na kwamba mtu anayenuia makubwa hupata makubwa, wakati anayenuia madogo hupata madogo.
Bw. Mengi alisema mtu anayetaka kufanya biashara anapaswa pia kuhakikisha anakuwa na washiriki wazuri wa kufanya nao biashara ili aweze kukuza mtaji wake na kupata masoko mengi.
Kuhusu uwekezaji nchini, Bw. Mengi alisema watu wengi wanaokuja kuwekeza hawaijui vyema Tanzania na aliwashauri kushirikiana na wazalendo watakapokuja kuwekeza.
Alisema kuna nafasi nyingi za uwekezaji ambazo wakizitambua zinaweza kuwa za manufaa kwao na alitoa mfano wa sekta ya Teknolojia ya Mawasiliano (IT).
SOURCE: Nipashe
http://www.ippmedia.com/ipp/nipashe/2007/01/13/82220.html