Maoni ya Kamati Kuhusu Azimio la Bunge Kuridhia Makubaliano Kati ya Tanzania na Dubai Kuhusu Ushirikiano wa Uendelezaji na Uboreshaji Bandari Tanzania

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
3,464
13,079

MAONI YA KAMATI YA PAMOJA KUHUSU AZIMIO LA BUNGE KURIDHIA MAKUBALIANO KATI YA SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA SERIKALI YA DUBAI KUHUSU USHIRIKIANO WA KIUCHUMI NA KIJAMII KWA AJILI YA UENDELEZAJI NA UBORESHAJI WA UTENDAJI KAZI WA BANDARI TANZANIA LA MWAKA 2023​

SEHEMU YA KWANZA​

UTANGULIZI​

Maelezo ya Awali
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 60 (6) (b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari, 2023, naomba kuwasilisha Maoni ya Kamati ya Pamoja Kuhusu Azimio la Bunge Kuridhia Makubaliano Kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai Kuhusu Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii kwa Ajili ya Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji Kazi wa Bandari Tanzania la Mwaka 2023. Maoni haya yanawasilishwa Bungeni kufuatia uamuzi wako wa busara wa kuunda Kamati ya Pamoja, itokanayo na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kwa mujibu wa Kanuni 143 (1).

Mheshimiwa Spika, Kamati inatambua kwamba uamuzi wa kuunda Kamati ya Pamoja ni muendelezo wa jitihada zako za dhati za kuhakikisha kwamba, masuala muhimu ya kitaifa ambayo yanayogusa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu, yanapewa uzito unaostahili na

kufanyiwa uchambuzi wa kina ili Bunge liweze kutoa uamuzi sahihi na wenye manufaa kwa Taifa. Uamuzi wako huo ni muendelezo wa jitihada zako za kuhakikisha kwamba Bunge, kwa niaba ya Wananchi, linatekeleza wajibu wake ipasavyo wa kuisimamia na kuishauri Serikali kwa mujibu wa Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya Mwaka1977.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Wajumbe wa Kamati ya Pamoja, naomba nitumie fursa hii kukupongeza kwa dhati kabisa kwa namna ambavyo umelisimamia jambo hili katika mchakato wake wote hadi kufikia hatua hii ambapo Taarifa ya Kamati ya Pamoja inawasilishwa ili Bunge lako Tukufu lifanye uamuzi kwa hoja iliyowasilishwa na Serikali.

Namna Kamati Ilivyofanya Kazi
Mheshimiwa Spika, baada ya kupokea maelekezo ya kulishughulikia jambo hili kwa mujibu wa Kanuni ya 108 (1) na (2), Kamati ya Pamoja ilianza kazi yake mara moja na kufanya yafuatayo: -
Kufanya uchambuzi wa awali na baadae kupokea Maelezo ya Serikali kuhusu Mapendekezo ya Azimio la Kuridhia Makubaliano husika siku ya Jumatatu tarehe 5 Juni, 2023;

Kupokea na kuchambua Maoni ya Wadau yaliyowasilishwa mbele ya Kamati siku ya Jumanne tarehe 6 Juni, 2023. Aidha, Kamati ilipokea maoni yaliyowasilishwa kwa njia ya mtandao ambapo mpaka wakati Kamati inakamilisha kazi yake ilipokea maoni kutoka kwa wadau sabini na mbili (72).

Kufanya uchambuzi wa kina wa Makubaliano husika kwa kuzingatia Uchambuzi wa Awali, Maelezo ya Serikali pamoja na Maoni ya Wadau yaliyowasilishwa kwa njia tofauti, kazi hii ya uchambuzi ilifanyika kuanzia tarehe 7 - 9 Juni, 2023.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, Kamati hii ilifanya tathimini kwa kuzingatia Kanuni ya 107 (2) (f) na (g) ili kupima iwapo kuna kuna manufaa au athari ambazo Tanzania itapata kutokana na mapendekezo ya Serikali kwa Bunge kuridhia Makubaliano husika.

Mheshimiwa Spika, tathimini iliyofanyika, ilikuwa na lengo la kujihakikishia kwamba, Makubaliano ambayo Serikali imeingia na inapendekeza Bunge kuridhia, unakuwa na manufaa kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu na si vinginevyo.

Chimbuko la Makubaliano
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 28 Februari, 2022, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (Tanzania

Ports Authority [TPA]) iliingia Makubaliano ya Awali (Memorandum of Understanding) na Kampuni ya DP World inayomilikiwa na Serikali ya Dubai (Government of Dubai). Kamati ilitaarifiwa kwamba, Makubaliano hayo yalikuwa na lengo la kubainisha maeneo mahsusi ya ushirikiano ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu, maeneo maalum ya kiuchumi (special economic zones), maeneo ya maegesho na utunzaji mizigo (logistics parks) na maeneo ya kanda za kibiashara (trade corridors) nchini.

Mheshimiwa Spika, baada ya hatua hiyo, tarehe 25 Oktoba, 2022 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai zilisaini rasmi Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii kwa Ajili ya Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji Kazi wa Bandari za Bahari na Maziwa Tanzania, yaani The Intergovernmental Agreement Between The United Republic of Tanzania and The Emirate Of Dubai Concerning Economic and Social Partnership for The Development and Improving Performance of Sea and Lake Ports in Tanzania.

SEHEMU YA PILI​

UCHAMBUZI WA KAMATI​

Msingi wa Uchambuzi
Mheshimiwa Spika, hoja iliyowasilishwa na Serikali inapendekeza kwamba Bunge lako Tukufu liliridhie Makubaliano Kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai Kuhusu Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii kwa Ajili ya Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji Kazi wa Bandari Tanzania kwa lengo la kutimiza masharti ya Ibara ya 63 (3) (e) ya Katiba.

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa Bunge kujadili hoja ya kuridhia Mikataba ya Kimataifa umeainishwa katika Kanuni ya 107 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge ambapo, pamoja na masuala mengine, utaratibu huo umeweka bayana kwamba, Serikali ina wajibu wa kuwasilisha hoja yake Bungeni pamoja na Makubaliano yanayokusudiwa kuridhiwa.

Mawanda ya Uchambuzi
Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kwamba, Kamati ilifanya uchambuzi kwa kupitia Ibara zote za Makubaliano pamoja na viambatisho vyake ili kupata uelewa wa kutosha kuhusu masharti yaliyomo pamoja na maudhui ya masharti hayo.

Mheshimiwa Spika, Katika kufanya uchambuzi wa Makubaliano hayo, Kamati ilizingatia pia masuala ya msingi kulingana na masharti ya Kanuni ya 107 (2) yakiwemo yafuatayo: -
Wajibu wa nchi baada ya kusaini Makubaliano;

Kiwango ambacho Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezingatiwa katika Makubaliano;
Manufaa ambayo Tanzania itapata kutokana na Makubaliano hayo; Iwapo kutakuwa na athari zozote kutokana na Makubaliano; naJambo jingine lolote lenye tija kwa Taifa kutokana na Makubaliano husika.

Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, maoni na ushauri wa Wajumbe wa Kamati, Maelezo ya Serikali, pamoja na maoni yaliyowasilishwa na Wadau mbalimbali, yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza mawanda ya uchambuzi wa Kamati ili kulishauri Bunge kufanya uamuzi kwa mujibu Kanuni ya 111 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

Masuala ya Msingi Yaliyozingatiwa na Kamati Katika Uchambuzi
Aina ya Makubaliano
Mheshimiwa Spika, moja kati ya jambo la msingi ambalo Kamati ilizingatia katika uchambuzi wake, ni kutaka kufahamu na kujiridhisha kwamba Nchi yetu imeingia Makubaliano ya aina gani na Serikali ya Dubai. Baada ya kuihoji Serikali kuhusu suala hili ili kujirdhisha kikamilifu, Kamati imebaini kwamba, Makubaliano yaliyopo ni baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai juu ya kuweka msingi wa kisheria (legal framework) wa uendelezaji wa bandari. Aidha, aina ya ubia, kiasi/kiwango cha ubia, na maeneo ya ubia yataainishwa kwenye Mikataba ya Utekelezaji (Host Government Agreements na Individual Project Agreements) itakayokuja kuingiwa iwapo Bunge litaridhia Azimio hili.

Lengo la Makubaliano
Mheshimiwa Spika, katika uchambuzi wake, Kamati imebaini kwamba lengo la Makubaliano yanayopendekezwa kuridhiwa (Objective of the Agreement), kwa mujibu wa Ibara ya 2 ya Makubaliano hayo, ni kuweka msingi wa kisheria katika maeneo ya ushirikiano ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya

kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu, maeneo maalum ya kiuchumi (special economic zones), maeneo ya maegesho na utunzaji mizigo (logistics parks) na maeneo ya kanda za kibiashara (trade corridors). Aidha, maeneo mengine ya ushirikiano ni katika kujenga uwezo (capacity building), kuhaulisha maarifa, ujuzi, na teknolojia (transfer of knowledge, skills and technology), kuimarisha taasisi za elimu na kusaidia upatikanaji wa masoko

Mheshimiwa Spika, kama tulivyoeleza hapo juu, makubaliano haya yanaweka msingi wa kisheria baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania na Serikali ya Dubai, na si Mkataba wa mradi wowote wa bandari. Miradi yote itakayotekeklezwa itatatekelzwa kwa Mikataba ya Utekelezaji itakayotaja mawanda, faida, na kufafanua kwa kina masuala ya kiuwekezaji.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika uendeshaji wa bandari, ni sehemu ya jitihada ambazo nchi yetu inapaswa kuziunga mkono ili kuongeza ufanisi wa utendaji wa bandari zetu. Hata hivyo, ni vyema Serikali ikahakikisha kwamba, katika kutafuta wawekezaji wa sekta hii muhimu kwa uchumi wa nchi na uendelevu wa biashara baina yetu na mataifa

mengine, kunakuwepo na umakini, weledi na uwazi bila kuathiri maslahi mapana ya nchi katika kuongeza pato la Taifa kwa maendeleo ya nchi.

Mawanda ya Utekelezaji wa Makubaliano Mheshimiwa Spika, Wajumbe walihoji ili kupata ufafanuzi kwa Serikali iwapo utekelezaji wa Makubaliano husika utahusisha taasisi zipi na iwapo utazigusa bandari zote nchini, au ni kwa bandari ya Dar es Salaam peke yake. Msingi wa hoja hii ni kutaka kujua kiwango cha utekelezaji wa ubia katika uendeshaji wa bandari nchini.

Mheshimiwa Spika, Kamati imebaini kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ndio yenye jukumu la kutekeleza maeneo ya ushirikiano kuhusu Makubaliano haya kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa upande wa Serikali ya Dubai, Kampuni ya DP World na washirika wake ndio zitakuwa taasisi za utekelezaji. Utekelezaji huo utafanyika kupitia Mikataba ya Utekelezaji (Host Government Agreements na Individual Project Agreements).

Mheshimiwa Spika, aidha, Kamati ilitaarifiwa kuwa, pamoja na ushirikiano huo, nchi yetu itakuwa na haki ya kuitaarifu Serikali ya Dubai kuhusu fursa nyingine za uwekezaji katika maeneo ya bandari,

maeneo huru ili kuwezesha taasisi za Dubai kuwasilisha mapendekezo ya uwekezaji katika maeneo hayo. Kuhusu uwekezaji husika, DP World na washirika wake ndio watakuwa na jukumu la kutafuta fedha za uwekezaji kwa ajili ya uendelezaji wa shughuli za uwekezaji.

Manufaa ya Makubaliano kwa Nchi
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa mapendekezo ya kuridhia Makubaliano haya yaliyowasilishwa na Serikali, kuridhiwa kwa Makubaliano haya kutakuwa na manufaa yafuatayo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania:
Kuongeza fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutokana na uwekezaji mkubwa na ongezeko la shehena ya mizigo itakayopitia bandari ya Dar es Salaam. Aidha, maeneo mengine ya ushirikiano ni katika kujenga uwezo (capacity building), kuhaulisha maarifa, ujuzi, na teknolojia (transfer of knowledge, skills and technology), kuimarisha taasisi za elimu na kusaidia upatikanaji wa masoko.

Kuongezeka kwa ufanisi katika uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi na kuleta tija stahiki katika mnyororo wa thamani wa huduma za bandari nchini.Kuongezeka kwa Pato la Taifa kutokana na uboreshaji wa shughuli za kibandari. Kuongezeka tija na kuwezesha mwendelezo wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo imekuwa ikijengwa na Serikali kama vile: - Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge Railway - SGR)

Ujenzi wa meli za mizigo katika maziwa makuu; na
Mradi wa Lango la Bahari la Bandari ya Dar es Salaam (Dar es Salaam Maritime Gateway Project - DMGP).
Kuchagiza na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi zikiwemo kilimo, utalii, viwanda, mifugo, uvuvi, biashara na usafirishaji na hivyo kuboresha ustawi wa Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, kama Taifa, suala la uwekezaji wowote wa kimkakati unaofanywa na Serikali kwa lengo la kuchangia kukua kwa sekta mtambuka kama ilivyo kwa ujenzi wa reli, mradi wa kuzalisha umeme, maendeleo ya kilimo, na kukuza utalii, Bunge hili lina wajibu wa msingi wa kuunga mkono

jitihada hizo, sambamba na kutimiza wajibu wake wa kuishauri na kuisimamia Serikali ipasavyo. Kwa muktadha huo, uwekezaji wowote ambao una lengo la kuongeza ufanisi wa bandari zetu, manufaa yake ni bayana.

Suala la Kutoyumbishwa Kwa Makubaliano Mheshimiwa Spika, Ibara ya 30 ya Makubaliano haya inaweka masharti ya kuwa na uthabiti, uimara na uhakika wa kutoyumbisha Makubaliano (stabilization). Serikali za nchi husika zinakubaliana kuwa, mazingira ya kisheria na kimakubaliano kuhusu uwekezaji huu yatakuwa ya uthabiti na ya kuridhisha kwa Serikali zote mbili. Taarifa zote kuhusu uthabiti wa Makubaliano zitakubaliwa kati ya Kampuni ya DP World au Kampuni husika ya mradi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Aidha, masharti ya uthabiti wa Makubaliano yatawekwa katika Mikataba ya Utekelezaji (Host Government Agreements and Individual Projects Agreements) itakayoingiwa kati ya Tanzania na Kampuni ya mradi. Katika tarehe ya kusainiwa Makubaliano haya, itatumika kama rejea ya tarehe ya uthabiti katika kufanya mabadiliko yoyote ya Kisheria au mabadiliko ya kikodi yanayoweza kuathiri miradi husika.

Mheshimiwa Spika, maudhui ya masharti haya ni utaratibu wa kimkakati baina ya pande za Makubaliano kuhakikisha kwamba maslahi ya pande zote mbili yanalindwa kikamilifu kulingana na mazingira ya kiushindani na ni utaratibu wa kawaida katika Mikataba ya Kimataifa.

Suala la Ukomo wa Muda/Uhai wa Makubaliano Mheshimiwa Spika, Ibara ya 23 (1) hadi (4) ya Makubaliano haya inazungumzia kuhusu taratibu za kusitisha Makubaliano. Kamati imefanya uchambuzi wa Ibara ya 23 na kubaini kwamba iwapo Serikali itakuwa makini na usimamizi wa Makubaliano haya, bado kuna nafasi kubwa ya kusitisha Makubaliano wakati wowote ule iwapo kutatokea mgogoro baina ya pande zote mbili za Makubaliano haya na Mikataba ya Utekelezaji.

SEHEMU YA TATU​

MAONI NA USHAURI WA KAMATI​

Mheshimiwa Spika, Kamati imefanya na kukamilisha uchambuzi wake, na hivyo kuwasilisha Bungeni ili Bunge liweze kufanya kazi yake kwa mujibu wa Ibara ya 63 (3) (e) na kuiwezesha Serikali kuendelea na taratibu nyingine. Hata hivyo Kamati imeona ni muhimu Serikali ikayazingatia kwa lengo la kuweka mazingira mazuri kwenye uandaaji wa Mikataba ya Utekelezaji (Host Government Agreements na Individual Project Agreements) ili kuwa na tija na kukidhi kiu/matakwa ya wananchi kama ifuatavyo: -

Mikataba Yenye Maslahi kwa Taifa
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kamati imebaini kwamba Makubaliano yanayopendekezwa kuridhiwa na Bunge yataweka msingi (framework) ili sasa Serikali iende hatua nyingine ya kusaini Mikataba ya Utekelezaji, Kamati inashauri kwamba, Mikataba yote itakayofuata katika kutekeleza masharti ya Makubaliano haya iwe na tija, na yenye kulinda maslahi mapana ya nchi ya Tanzania na watu wake. Aidha, Kamati inaitaka Serikali kuhakikisha kwamba mikataba hiyo inajumuisha maoni ya wadau muhimu katika sekta mtambuka ili kuhakikisha kwamba, masuala ya msingi yanazingatiwa katika kuboresha mawanda ya utekelezaji wake.

Ukomo wa Mikataba na Masharti ya Tathimini Mheshimiwa Spika, Kamati inasisitiza kwamba uhai wa Mikataba ya Utekelezaji itakayosainiwa itaje muda maalum wa utekelezaji wa miradi ambao utazingatia maslahi mapana ya nchi. Vilevile, mikataba hiyo iwe na kipengele kinachoelekeza wabia kufanya tathimini ya utekelezaji wa miradi ya uwekezaji, na kuvunja Makubaliano iwapo utekelezaji huo hautafanyika kama ilivyokusudiwa.

Uhakika wa Ajira na Fursa kwa Watanzania
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Makubaliano yanayopendekezwa kuridhiwa na yana sura ya ubia, hivyo basi, Kamati inaishauri Serikali: -
Kuhakikisha kwamba ajira za Watanzania zinalindwa na kuweka mfumo thabiti wa mgawanyo wa ajira baina ya nchi wabia; Kunakuwepo na utaratibu wa kuwajengea uwezo wafanyakazi wa bandari kwa lengo la kuhaulisha ujuzi, maarifa na teknolojia; na Kushirikisha makampuni ya Kitanzania katika utekelezaji wa miradi ya uwekezaji.

Menejimenti ya Uwekezaji
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa utekelezaji wa Makubaliano unakusudia kuweka ushirikiano kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na DP World, na kwa kuwa bado TPA atakuwa msimamizi wa karibu wa miradi ya uwekezaji wa bandari kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, hivyo basi Kamati inashauri yafuatayo: -
Mikataba ya ubia kati ya TPA, DP World na makampuni mengine izingatie maslahi ya nchi; Serikali iendelee kusimamia usalama kwa kuzingatia kwamba bandari ni sehemu nyeti; Serikali iendelee kukaribisha wawekezaji wengine katika maeneo ambayo hayajapata wawekezaji.

SEHEMU YA NNE​

HITIMISHO​

Shukrani
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kukushukuru kwa dhati kabisa wewe binafsi, ukisaidiwa na Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuliongoza vema Bunge hili na kwa namna ambavyo umeipa Kamati hii ushirikiano. Maelekezo, ushauri na busara zako vimekuwa ni nyenzo muhimu katika ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Kamati hii bila kuingilia uhuru wa majadiliano, mwenendo na maamuzi yaliyofikiwa na Kamati hii. Kwa hakika, umeonesha dira, na ukomavu wa kisiasa na kiuongozi ili kukuza demokrasia ndani ya Kamati, Bunge na nchi kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru kwa dhati kabisa, Wajumbe wa Kamati ya Pamoja, ambao pamoja na kutofautiana kimawazo, kimtazamo na kiitikadi, lakini bado wamekuwa wavumilifu, kuheshimu mawazo ya wengine, na hatimaye kufikia makubaliano ya pamoja (consensus) ili kulishauri Bunge hatua ya kuchukua. Kwa kutambua mchango wao katika kujadili Hoja hii, naomba majina yao yaingie katika Taarifa Rasmi za Bunge kama ifuatavyo: -

1.​
Mhe. Moshi Selemani Kakoso, Mb. - MWENYEKITI
2.​
Mhe. Jerry William Silaa, Mb.
3.​
Mhe. Anne Kilango Malecela, Mb.
4.Mhe. Augustine Vumma Hole, Mb.
5.Mhe. Abbas Gulam Tarimba, Mb.
6.Mhe. Abdallah Jafari Chaurembo, Mb.
7.Mhe. Abubakar Damian Asenga, Mb.
8.Mhe. Aeshi Alfan Hillary, Mb.
9.Mhe. Ahmed Mabkhut Shabiby, Mb.
10.Mhe. Aida Joseph Kenani, Mb.
11.Mhe. Ally Anyigulile Mlaghila Jumbe, Mb.
12.Mhe. Amina Ali Mzee, Mb.
13.Mhe. Amina Daud Hassan, Mb.
14.Mhe. Angelina Malembeka, Mb.
15.Mhe. Assa Nelson Makanika, Mb.
16.Mhe. Bonah Ladislaus Kamoli, Mb.
17.Mhe. Capt. Abbas Ali Hassan Mwinyi, Mb.
18.Mhe. Catherine Valentine Magige, Mb.
19.Mhe. Charles Muguta Kajege, Mb.
20.Mhe. Deonatus Philip Mwanyika, Mb.
21.Mhe. Dkt. John Danielson Pallangyo, Mb.
22.Mhe. Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mb.
23.Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, Mb.
24.Mhe. Eng. Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mb.
25.Mhe. Francis Kumba Ndulane, Mb.
26.Mhe. Fratey Gregory Massay Mb.
27.Mhe. Fredrick Edward Lowassa, Mb.
28.Mhe. George Natany Malima, Mb.
29.Mhe. Ghati Zephania Chomete, Mb.
30.Mhe. Haji Amour Haji, Mb.

31.​
Mhe. Innocent Edward Kalogeris, Mb.
32.​
Mhe. Livingstone Lusinde, Mb.
33.​
Mhe. Maryam Azan Mwinyi, Mb
34.​
Mhe. Matha Nehemia Gwau, Mb
35.​
Mhe. Mbarouk Juma Khatib, Mb.
36.​
Mhe. Miraji Jumanne Mtaturu, Mb.
37.​
Mhe. Mohamed Maulid Ali, Mb.
38.​
Mhe. Mwatum Dau Haji, Mb.
39.​
Mhe. Nora Waziri Mzeru, Mb
40.​
Mhe. Rose Vicent Busiga, Mb.
41.​
Mhe. Santiel Eric Kirumba, Mb.
42.​
Mhe. Stella Simon Fiyao, Mb.
43.​
Mhe. Sylvia Francis Sigula, Mb.
44.​
Mhe. Zuena Athumani Bushiri, Mb.

Mheshimiwa Spika, Kamati inamshukuru Mtoa Hoja, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb) pamoja na Naibu Waziri (Sekta ya Uchukuzi) Mhe. Atupele Alfredy Mwakibete (Mb) kwa ushirikiano ambao wameipatia Kamati wakati wa uchambuzi wa Azimio la Kuridhia Makubaliano huu. Aidha, nawashukuru watendaji wote wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa ushirikiano walioipatia Kamati ya Pamoja, na kutoa ufafanuzi pale walipohitajika kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa, nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa umma wa Watanzania na watu wote

wenye nia njema na nchi hii, ambao walitenga muda wao kuitikia wito wa Kamati na kufika kutoa maoni yao mbele ya Kamati na pia kwa kuwasilisha maoni yao kwa maandishi kwa njia za kielektroniki.

Mheshimiwa Spika, mwisho lakini sio kwa umuhimu, nawashukuru Watumishi wa Ofisi ya Bunge chini ya Uongozi wa Katibu wa Bunge, Bi. Nenelwa J. Mwihambi, ndc, kwa uratibu wa Shughuli za Kamati na kutoa ushauri wa kitaalam wakati wa uchambuzi wa mapendekezo ya kuridhia Makubaliano hadi kukamilika kwa taarifa hii.

Uamuzi wa Hoja

Mheshimiwa Spika, kwa mamlaka ambayo Bunge limepewa kwa mujibu wa Ibara ya 63 (3) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya Mwaka 1977, naomba sasa lijadili na kuridhia Makubaliano Kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai Kuhusu Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii kwa ajili ya Uendelezaji na Uboreshaji wa Utendaji Kazi wa Bandari Tanzania, kama yalivyowasilishwa na Mtoa Hoja.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha, na ninaunga mkono Hoja.

Habari zaidi, soma:
  1. Sakata la DP WORLD: Rais Samia asema Serikali itatafuta mbia wa kuiendesha bandari ya Dar, sasa kuchangia robo tatu ya bajeti ya nchi
 

Attachments

  • MAONI YA KAMATI YA PAMOJA MEZANI.pdf
    347.9 KB · Views: 7
Sasa kama ishu ni kuwa na mitambo na tekenojia ya kisasa tunashindwa nini sisi kama taifa kuwekeza?

Cranes za kisasa zinapatina . Utalaamu wa kisasa unapatikana.

Au ndio kusema waarabu ndio wanauwezo pekee wa kufunga cranes na mitambo ya kisasa?

Au ndio hivyo tena.? Damu nzito kuliko maji?
 
Hii tender, zabuni inabidi itangazwe upya kuwe na ushindani. Masharti na vipengele tuweke sisi.

Kuzipitia tuwakilishwe na vichwa mawakili wenye akili na uzalendo.
 
Ni mtu mmoja mwenye upeo, mkarimu na mimali yake yote lakini yupo wazi kuongea fikra zake na maoni yake. Tafadhali jionee mwenyewe:

 
Ni mtu mmoja mwenye upeo, mkarimu na mimali yake yote lakini yupo wazi kuongea fikra zake na maoni yake. Tafadhali jionee mwenyewe:

Fox, suala syo ana mali kiasi gani au anaongeaje.
Suala ni vipengele vibovu ktk mkataba.
 
Mbona tuna udongo,tuna mawe tumeshindwa kutokomeza nyumba za nyasi, mwendokasi mabus Wana Kila kitu kuanzia abiria, magari, barabara lakini wameshindwa
 
African is a cursed race! Myself I'm not an African. I am a Hebrew - GALATIANS 3:29.

Ni mtu aliyelaaniwa pekee ndiye anashindwa kumlisha na kumkamua ng'ombe wake! Hadi aombe msaada kwa jurani, loooh, aibu!


YESU NI BWANA NA MWOKOZI.
 
Sasa kama ishu ni kuwa na mitambo na tekenojia ya kisasa tunashindwa nini sisi kama taifa kuwekeza?

Cranes za kisasa zinapatina . Utalaamu wa kisasa unapatikana.

Au ndio kusema waarabu ndio wanauwezo pekee wa kufunga cranes na mitambo ya kisasa?

Au ndio hivyo tena.? Damu nzito kuliko maji?

Mbona mlishindwa mpaka mkawapa TICTS kwa miaka 25? Wakawalamba. Huna wewe uwezo wa fedha za kuiboresha bandari kwa sasa.

Wacheni mfundishwe namna ya kuendesha bandari kisasa, wewe utashinda na watu ambao mpaka Uingereza wamewawachia bandari kubwa mbili wawaendeshee.

Kosa kubwa la Waafrika ni ujinga wa kujifanya tunajuwa lakini ukweli ni kuwa hatujuwi lolote. Siyo maneno yangu hayo, maneno ya Dhahabu Nyeusi, bofya chini hapo ukamuone anavyowapa ukweli:

 
Mbona tuna udongo,tuna mawe tumeshindwa kutokomeza nyumba za nyasi, mwendokasi mabus Wana Kila kitu kuanzia abiria, magari, barabara lakini wameshindwa
Wameshindwa CCM. Tuanze na katiba mpya, vyama vipya, wagombea huru, tume huru, tuone.

CCM wamekaa vya kutosha madarakani.
 
African is a cursed race! Myself I'm not an African. I am a Hebrew - GALATIANS 3:29.

Ni mtu aliyelaaniwa pekee ndiye anashindwa kumlisha na kumkamua ng'ombe wake! Hadi aombe msaada kwa jurani, loooh, aibu!


YESU NI BWANA NA MWOKOZI.

Africa inaangushwa kwa kuthamini nguvu zao na kutojitambua, kukosa umoja.

Wanatenganishwa kirahisi kwa dini, ukanda, vyama, asali, maneno matamu, madaraka.

Uzalendo, uaadilifu na uaminifu ni zero. Inawezekana kujitambua na kufanikiwa kama Waafrika.
 
African is a cursed race! Myself I'm not an African. I am a Hebrew - GALATIANS 3:29.

Ni mtu aliyelaaniwa pekee ndiye anashindwa kumlisha na kumkamua ng'ombe wake! Hadi aombe msaada kwa jurani, loooh, aibu!


YESU NI BWANA NA MWOKOZI.

Kashindwa kujikomboa mwenyewe wakamtundika juu ya mti, atakukomboa wewe?

Tumia kichwa chako kufikiri japo kidogo.

Afrika hatuna laana , biblia inasema atundikwae juu ya mti ndiyo mwnye laana.
 
Sasa kama ishu ni kuwa na mitambo na tekenojia ya kisasa tunashindwa nini sisi kama taifa kuwekeza?

Cranes za kisasa zinapatina . Utalaamu wa kisasa unapatikana.

Au ndio kusema waarabu ndio wanauwezo pekee wa kufunga cranes na mitambo ya kisasa?

Au ndio hivyo tena.? Damu nzito kuliko maji?
Hamuwezi lolote kufanya zaidi ya uwizi
Nyie sahv endeleeni kuimba na kukata mauno tu
Vyoo vya umma tu mnashindwa kuvisimamia
Mwendokasi mradi tu unaenda tia maji tia maji

Ova
 
Fox, suala syo ana mali kiasi gani au anaongeaje.
Suala ni vipengele vibovu ktk mkataba.
Soma mapedekezo ya kamati.

Kipengele gani kibovu? Nimeusoma mkataba zaidi ya mara kumi, kila swali lenu linajijibu kwenye mkataba. Sema kipengele kipi tukupe jibu kutoka ndani ya mkataba.

Wewe utashindana na hiyo kamati hapo juu?
 
Mbona mlishindwa mpaka mkawapa TICTS kwa miaka 25? Wakawalamba. Huna wewe uwezo wa fedha za kuiboresha bandari kwa sasa.

Wacheni mfundishwe namna ya kuendesha bandari kisasa, wewe utashinda na watu ambao mpaka Uingereza wamewawachia bandari kubwa mbili wawaendeshee.

Kosa kubwa la Waafrika ni ujinga wa kujifanya tunajuwa lakini ukweli ni kuwa hatujuwi lolote. Siyo maneno yangu hayo, maneno ya Dhahabu Nyeusi, bofya chini hapo ukamuone anavyowapa ukweli:

Acha upuuzi. Ticts ilikuwa ni ufisadi kama huu mnaofanya sasa
 
Back
Top Bottom