Andiko hili limenitafakarisha sana. Tuache kwanza habari ya Joanah. Tujiulize sisi wenyewe, sisi ambao hatujui siku, saa, wala muda wetu umefika lini, tumejiandaaje?
Huenda unaandika hapa kumpa pole, kumwonea huruma au kumfariji mtoa mada kwa sababu ameambiwa ana prognosis ya miezi miwili au chini ya hapo.
Lakini hebu geuza swali hilo kwako mwenyewe. Kama ingekuwa wewe umeambiwa, “Una miezi miwili tu au chini ya hapo,” ungefanya nini?
Wengi wetu tungeanza kusema, Nitajikaribisha zaidi kwa Mungu. Nitatubu. Nitasali zaidi. Nitawaomba msamaha nilio wakosea. Nitawasamehe walionikosea. Nitakaa karibu na familia yangu na watu ninaowapenda. Nitatengeneza mambo yangu na Mungu.
Vizuri kabisa! Lakini swali ni hili, Kwa nini tusifanye hivyo sasa?
Kwa nini tusimtafute Mungu kwa moyo wote wakati bado hatujaambiwa tuna miezi miwili?
Kwa nini tusitubu leo, badala ya kusubiri siku tutakayoogopa kifo?
Kwa nini tusisamehe leo, badala ya kusubiri dakika za mwisho?
Kwa nini tusimpende Mungu leo kwa nguvu zetu zote, badala ya kusubiri mwili utakapokuwa hauna nguvu tena?
Tunajua kabisa kwamba kifo hakitupi appointment. Hakipigi simu kusema, “Nakuja kesho saa 10.” Hakituandikii ujumbe kusema, “Jiandae, zimebaki siku 30.”
Wengine wanapewa taarifa ya muda wao. Sisi wengine tunaishi bila taarifa hiyo.
Na labda hapo ndipo kuna tofauti kubwa.
Yeye amepewa kile ambacho sisi hatujapewa. Nafasi ya kuhesabu siku zake.
Lakini sisi tunaishi kana kwamba tumepewa miaka mingi.
Tunapanga kesho, mwezi ujao, mwaka ujao… lakini hatujui kama tutafika huko.
Huenda mtu anayejua amebakiza miezi miwili ndiye aliyeanza kuishi kwa umakini kuliko yule anayefikiri ana miaka ishirini mbele yake.
Kwa hiyo, tusimwangalie tu kwa huruma.
Tujitazame sisi wenyewe.
Kama leo ungeambiwa huu ndio mwezi wako wa mwisho, ungeendelea na maisha haya haya?
Ungeendelea kubeba chuki hiyo?
Ungeendelea kuahirisha toba?
Ungeendelea kusema, “Nitabadilika baadaye”?
Ungeendelea kuishi mbali na Mungu?
Kama jibu ni hapana, basi kwa nini unasubiri mpaka uambiwe una muda mfupi wa kuishi?
Neema si kuambiwa siku yako ya mwisho. Neema ni kupewa leo.
Leo bado unaweza kutubu.
Leo bado unaweza kusamehe.
Leo bado unaweza kurekebisha.
Leo bado unaweza kumtafuta Mungu.
Leo bado unaweza kusema, “Bwana, niko hapa.”
Kwa hiyo, huenda hatuna neema ya kujua tumebakiwa na muda gani kama alivyoambiwa yeye. Lakini tunayo neema kubwa zaidi ambayo mara nyingi tunaipuuza.
Tunaishi leo.
Na leo ndiyo siku ya kujiandaa.
Usisubiri prognosis ikufundishe thamani ya maisha. Usisubiri kifo kikufundishe kumtafuta Mungu. Usisubiri dakika za mwisho ndipo uanze kuishi kwa ajili ya Mungu.
Kwa sababu ukweli mchungu ni huu:
Sote tuna prognosis tofauti ni kwamba hakuna aliyetuambia tarehe yake.
Tafakari.
Chukua hatua.
Mungu atusaidie tusije tukatamani tungepewa zile siku tunazopoteza leo. 🙏