Rev. Kishoka
JF-Expert Member
- Mar 7, 2006
- 4,526
- 1,552
Utangulizi:
KWANZA, natoa shukrani za wazi kwa Sheikh Ido Mohammed Iddi wa Msikiti wa Mnyamani kwa kuwa mstari wa mbele kuzungumzia haki ya Waislamu kuwa na Mahakama yao ya Kadhi kama ilivyo Zanzibar, Kenya na sehemu nyingine Afrika. Yeye na viongozi wengine wa Kiislamu tunaomba wasikate tamaa maana ushindi ni wa Allah -Subuhana wa taalaa na sio viumbe hapa duniani.
FAIDA ZA MAHAKAMA YA KADHI
Baada ya kusema hayo, leo napenda kuanza kwa kuzungumzia faida za kuwa na Mahakama ya Kadhi na hasara zitakazotokana na kutokuwepo kwa Mahakama ya Kadhi-kama ilivyo kuwa huko nyuma, ilivyo sasa na baya zaidi hali itakavyokuwa huko mbele.
Faida za mahakama ya Kadhi pamoja na mengineyo zaweza kugawanya katika makundi matatu makubwa: Faida katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo wa kudumu na usiobeba dhambi mbele ya Mungu hususan, kuhusu kifamilia na maisha ya kila siku ya Muislamu; faida zitakazotkana na kutatua matatizo ya maingiliano ya kiuchumi na kijamii kwa Waislamu; na faida zitakazopatikana kutokana na kutatua matatizo ya Uongozi, Usimamizi na Uadilifu miongoni mwa viongozi wa misikiti na taasisi mbalimbali za Kiislamu.
Matatizo ndani ya familia na jamii za Kiislamu:
Kundi hili la kwanza la hoja ni kuhusiana na maisha ya kila siku. Hapa tunaonesha madhambi Waislamu wanayolazimishwa kuyabeba kwa sababu ya kukosekana mahakama ya Kadhi:Matatizo ya mahusiano ya kiuchumi na kijamii
- . Hukumu za ndoa kufanyika kwa mujibu wa sheria za Kiislamu na Kitabu cha Mwenyezi Mungu-Al-Furqhan.
- . Talaka hazitatolewa tena nje ya kile kilichoamrishwa na Mwenyezi Mungu na mahakimu ambao wakati mwingine si Waislamu.
- . Ujanja unaofanywa na watu kurithi pale wasipostahili kurithi utafichuliwa na watakaomrithi mtu kwa kiasi kikubwa watakuwa ni wale tu wanaostahili haki hiyo.
- . Familia zinazotekelezwa zitatunzwa na mifuko maalum itakayopatikana kutokana na zaka na sadaka za Waislamu ambayo baadhi yake itapewa ofisi hiyo ya Kadhi.
- . Mayatima watalindwa hasa pale wanapokuwa wadogo lakini wazazi wao wameacha mali mbalimbali ambazo zitakuja wafaa ukubwani.
- . Wazee wengi wa Kiislamu, hasa katika mikoa ya Pwani na kwingineko, ambao kwa sasa wanaishi kwa dhiki na ukata mkubwa wataangaliwa kwa namna moja au nyingine na mahakama hiyo na hivyo kuondoa uwezekano wa watu wa dini nyingine kuwaritadisha watu hao uzeeni kutokana na ufukara wao na kukosa taasisi ya kitaifa inayowajali na kuwatunza wazee
- . Masuala ya elimu na taasisi za elimu za Kiislamu yatapata ofisi moja au mbili za kuyasimamia na hivyo kupunguza udhaifu na uendeshaji mbaya uliopo hivi sasa.
- . Aidha taasisi za tiba za Kiislamu zitakuwa chini ya macho makali ya idara za ofisi ya Kadhi ili kuona haki inatendeka kwa kutolewa huduma muhimu kwa gharama zinazokubalika ndani ya wakati tuliomo.
- . Masuala ya kibenki na taasisi za fedha yataangaliwa ili yaendane na kutowaingiza Waislamu katika dhambi wasiyoiona au kuijua.
- . Kadhalika shughuli za huduma mbalimbali na biashara zitasimamiwa ili zikidhi haja ya wateja Waislamu na wasio Waislamu na vilevile kuhakikisha kuwa biashara zote zinakuwa za halali kwa upande wa Waislamu na zinazofanyika kwa njia ya halali bila kuwapunja, kudhulumu au kuwanyonya wateja.
- . Masuala ya uwekezaji na mitaji ambayo sasa yanafuata utaratibu unaoendana zaidi na dini nyingine yatapata usimamizi wa kuhakikisha kuwa sasa yanaendana na maagizo ya Mwenyezi Mungu.
- . Juu ya yote maingiliano na wasio waislamu yataratibiwa ipasavyo na kuhakikisha Waislamu wanawatendea haki watu wengine na wao pia wanatendewa haki na watu wengine ikiwemo watawala na viongozi wa dini nyingine.
- . Mahakama ya Kadhi itatoa mchango mkubwa katika kutenganisha masuala ya dini na kisiasa na hasa misikitini jambo ambalo sasa limekosa mtu wa kudhibiti.
- . Mahakama ya Kadhi itachambua Taassisi za Kiislamu zilizopo ili kuzifuma upya ziondokane na viongozi wabovu na waovu ili Waislamu warejeshe imani kwa viongozi wao pamoja na umoja na mshikamano ndani ya taasisi hizo zinazoyumba kwa sasa kutokana na kuvamiwa na siasa na wanasiasa.
- . Kuchochea imani, uzuzi na ubunifu miongoni mwa Waislamu ili waweze kuwaamini viongozi wao kwani kila kitu sasa kitakuwa wazi chini ya Ofisi ya Kadhi na hivyo kuwezesha Waislamu kutunisha mifuko yao mbalimbali na kuacha kabisa kwa taasisi za Kiislamu kutegemea serikali au wanasiasa na ruzuku katika kuendesha mambo yao.
Matatizo ya taasisi, uongozi, na viongozi wa KiislamuHasara za Waislamu kunyimwa haki yao ya msingi ya kuwa na Kadhi:
- . Ofisi yaKadhi pia itakuwa mstari wa mbele katika kulinda mali za Waislamu. Tofauti na ilivyo sasa ambapo baadhi ya Waislamu na wasio waislamu wanaweza wakauza au kununua mali za Wakfu za Waislamu na kulindwa na sheria isiyo ya Kiislamu kutokana na udhaifu wa kutokuwa na Mahakama ya Kadhi ambayo ingelikuwa ina hakiki mali zote za Waislamu na kuwekea mikataba lakiri isiyoweza kubadilishwa ila kwa amri ya Mahakama hiyo tu.
- . Baadhi ya taasisi, wilaya, mikoa hadi ngazi ya Taifa zina viongozi wabovu ambao wanalindwa na wanasiasa na mahakama zilizopo. Endapo mahakama ya Kadhi itakuwapo basi itawashughulikia viongozi wabovu na waovu kwa namna inayochunga mambo ya Waislamu yasikwame.
- . Inasemekana kwamba mali bila daftari hupotea bila habari. Misikiti na taasisi nyingi za Kiislamu karibu katika ngazi zote zina matumizi mabaya sana ya fedha na hakuna wa kuwawajibisha kutokana na kutokuwepo na Mahakama ya Kdhi ambayo ingelikomisheni wataalamu wa mambo ya fedha wa Kiislamu kubuni na kuanzisha mfumo wa uhasibu kwa ajili ya misikiti na taasisi hizo utakaopaswa kufuatwa na wote na vilevile kuwa na wakakguzi wa shughuli za dini na za kibiashara kwa Waislamu ili kuona hakuna wajanja wanofanya vitu vyao ndani ya taasisi hizo wakati wote. Kiujumla Ofisi ya Kadhi itawezesha Waislamu kuweka taratibu za uhasibuna utunzaji madaftari na utunzaji kumbukumbu za fedha au mali, mapato na matumizi miongoni mwa misikiti na taasisi nyingine za Kiislamu.
- . Ofisi hiyo ya Kadhi itakuwa pia na majukumu ya kuwasimamia wakaguzi maalum wa Kiislamu kukagua mali za waislamu kwa mujibu wa sheria za Kiislamu na kuwachukulia hatua wanaokiuka taratibu na miiko iliyowekwa tofauti na ilivyo hivi sasa.
- . Ofisi ya Kadhi itakuwa na mchango mkubwa pia katika kusaidia kusimamia makadirio na utozaji wa zaka tofauti na ilivyo sasa ambapo kutokana na kutokuwa na Ofisi ya Kadhi Waislamu ndio walio wengi katika lindi la umasikini kwa sababu umekosekana mfumo unaokubalika wa kukusanya zaka na kuwaondoa Waislamu waliomo katika umasikini kutoka kwenye lindi la ufukara unaowatia katika ukafiri kirahisi mno,
Aidha, haya pia yataendelea kuwasibu Waislamu tofauti na wenzao wa dini nyingine ambao dini zao zina mifumo ndani kwa ndani inayoshughulikia masuala kama haya lakini wao Waislamu hawana:
- . Kesi za ndoa kuhukumiwa ndivyo isivyo (yaani nje ya Kitabu cha Allah).
- . Masuala ya talaka kuamuliwa kinyume cha sheria za Kiislamu.
- . Wenye kustahili mirathi kunyimwa au kupunja na wasiostahili mirathi kupewa urithi usio halali.
- . Familia, yaani, mke na watoto wanaotekelezwa kucheleweshewa haki yao kutokana na mlolongo wa mashtaka kama haya mahakama za kawaida. Ugumu mkubwa katika kutambua kama waliotekelezwa kweli ni nasaba kwa mme au ni watu wa kupachikiwa.
- . Mayatima wa Kiislamu kulelewa na wasio Waislamu na hivyo kuwa katika hatari ya kupoteza au kupotoshewa imani yao.
- . Wazee wengi wa Kiislamu kuendelea kuteseka uzeeni kutokana na kukosekana kwa huduma nzuri na ya uhakika kwa watu kama wao katika jamii.
- . Elimu na taasisi nyingine za Kiislamu kuendelewa kuendeshwa ovyo ovyo kwa sababu hakuna mlezi wa taasisi hizo ambaye hawezi kuwa mwingine ila Muislamu muadilifu na mcha-Mungu ambaye ni kadhi na bingwa wa sheria na hukumu za Kiislamu kuhusu masuala husika.
- . Huduma za tiba kwa Waislamu zimekuwa zikibadilika lakini nazo zinakabiliwa na matatizo ya menejimenti, kiutawala, kiuendeshaji, kifedha na kimaendeleo kwa kukosa msimamizi mkuu kama Kadhi na Ofisi yake.
- . Katika miaka hii ambapo Waislamu wamefunguka macho kuhusu dhambi ya RIBA ni muhimu Waislamu kuwa na Kadhi ambaye kwa mashirikiano na Maulama wa ndani na nje wanaweza kupitishwa fatwa mbalimbali kuhusu masuala ya kibenki na kifedha. Kukosekana kwa mahakama ya Kadhi kunachangia kwa kiasi kikubwa Waislamu wengi kula kuchwao kuingia kwenye dhambi ya KULA AU KULISHA wengine RIBA.
- . Kutokana na kutoijua DINI yao vyema maelfu ya Waislamu sasa hivi wamejiingiza katika uwekezaji na mitaji haramu. Haya yote yamesababishwa na kukosekana kwa Mahakama ya Kadhi ambayo ingelibainisha kinaugaubaga ni uwekezaji na mitaji ipi ni halali na ipi ni haramu kwa Waislamu.
- . Kwa ujumla Mahakama ya Kadhi ambayo inapingwa na Wakatoliki ni chombo cha kuhakikisha kuwa mahusiano kati ya waumini wa dini hizi mbili yanafanywa bora zaidi na hapaachiwi mianya ya vikundi vidogo vidogo ndani ya dini zetu inayoweza kutumika kuvunja umoja na amani wa nchi hii.
Tofauti na baadhi ya watu wanavyoamini Mahakama ya Kadhi haitaingilia :
Hitimisho:
- . kesi zinazowahusu wasio Waislamu.
- . haitahukumu nje ya Sheria za Kiislamu ambazo zinakubalika katika jamii ya kisekula ya leo.
- . Haitokata watu mikono wala kupiga watu mawe.
- . Haitashughulika na masuala ya watu wa dini zingine haya yataachiwa mahakama za kisekula.
- . Badala ya kuorojesha amani na mshikamano kati ya Watanzania itasaidia sana kuhakikisha kuwepo kwa umoja na amani ya kudumu inayojengwa juu ya misingi ya haki na usawa.
- . Haitotumia fedha za seikali isipokuwa kwa kiwango kile kile ya mizigo ya kesi itakayopunguziwa mahakama za kisekula.
Ni hitimishe kwa kusema kwamba, Kuwepo kwa mahakama ya Kadhi hautokuwa ushindi wa upande mmoja, kwamba hawa wameshindwa na wale wameshinda. La, hasha! Ushindi huu ni ushindi kwa wote, Kwa Waislamu, kwa Watu wa dini nyingine, kwa wasiojua wanachokipinga na kwa Watanzania wote kwa ujumla. Kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi ni kuwepo kwa figa la tatu kwa Jamhuri ya Muungano ambayo hadi wa leo imekuwa ikisimamia juu ya mafiga mawili- figa na Kanisa Katoliki na ubalozi wa Vatican nchini na lile la Serikali ya Kisekula peke yake na kulisahau figa la tatu-Mahakama ya Kiislamu.
Yeyote atakayeikataa Mahakama ya Kadhi haitakii mema Tanzania na hawatakii mema Watanzania. Mungu Mkubwa na hana mpinzani! Mungu Ibariki Tanzania, na pia Wabariki watu wote wanaokuabudu wewe tu!
Sheikh,
Kwanza karibu jamvini, jisikie uko nyumbani.
La pili ambalo naomba niliongelee baada yakuona ufafanuzi wako ni kuwa kuna mkoroganyo wa kuelewa ni kwa nini kunahitajika kuwa na mahakama ya Kadhi.
Kutokana na maelezo yako ya kina, mahakama hii haitaishia kusimamia masuala ya ndoa na mirathi pekee, bali ni Serikali kamili ambayo itakuwa inashughulikia maslahi ya Waislamu pekee.
Sasa ninachojiuliza kutokana na maelezo yako hasa unaposema dini nyingine zinavyofanya mambo, je ni kwa nini mambo ya kijamii na kiroho yawe chini ya mahakama ya kisheria na si Baraza au Taasisi kuu ya Kiislamu?
Nafahamu kuna mgawanyiko mkubwa sana kuhusu Bakwata na kutofautiana kwa ideology ama kutokana na mapokeo tofauti ya Quran au Ubinadamu na upeo wa kupambanua mambo. Sasa kwa nini basi kusifanyike kwanza upatanishi na kuundwa kwa Taasisi kuu ya Waislamu wa madhehebu yote na kuweka sheria na kanuni za kujiongoza kabla ya kukimbilia kusema tunataka mahakama?
Ikiwa kwenye hii mahakama ya Kadhi ambao watakuwa mahakimu na wenye kuamua mashauri watakuwa ni watu ambao wako kwenye upande mwingine wa Shilingi na kushindwa kutoa haki ya kweli kutokana na mapokeo yao ya imani na ubinadamu, huoni kuwa tatizo la kusema kuwa Bakwata ni batili au si kamilifu litahamia kwenye mahakama ya Kadhi?
Umezungumzia maslahi ya Waislamu kwa mambo ya elimu, yatima na wazee kwa kuyaoanisha kana kwamba ni mabovu kwa waislamu pekee. Je shule na elimu ya Kiislamu unayozungumzia ni ya kufundishia Dini na Imani ya Uislamu au elimu dunia (msingi, Sekondari hata chuo)? Je Yatima na wazee ambao unadai wanatelekezwa na Serikali (au dini kama ulivyoonyesha) ni tatizo la Waislamu pekee au ni la Taifa zima?
Ninachopinga ni kule kutaka shughuli za jamii ambazo zinaweza kufanywa kwa kutumia Jumuia na Taasisi binafsi au za Kidini kugeuzwa na kushurtishwa kuundiwa vyombo maalumu vya kidini ndani ya Serikali.
Nitakupa mfano, Catholic Charities na Lutheran Welfare Services, zimejisajili kama taasisi binafsi kutokana na madhehebu yao. Zimeunda shule za kidini (mafundishi ya dini pekee) na shule za kawaida, zina zahanati na huduma za jamii kusaidia yatima, walemavu, wazee, ombaomba na wengine wengi bila kuhoji dini ya yule anayekuja omba msaada.
Sasa kwa nini Jumuiya ya Waislamu isiwe na vyombo kama hivi ambavyo si vya Kiserikali au kutegemea uendeshaji wake kupitia Serikali?
Hata kwenye suala la ndoa na mirathi, ikiwa mtu hatakubaliana na maamuzi ya mahakama ya Kadhi, kutokana na mapokeo na tafsiri yake ya Quran, je mtu huyu atakuwa na haki kwenda kwenye mahakama ya Serikali kutaka shauri lake litatuliwe?
Sababu ya kuyasema haya ni kutokana na kuingiliana kwa tamaduni zetu asilia na dini zetu tulizozipokea, Ukristo na Uislamu. Na hata katika dini hizi, tunapokea mafundisho kwa tafsiri mbali mbali kiasi kwamba hakuna absolute definition au understanding kutokana na mapokeo yetu kama binadamu ambayo yanajengwa na tabia na mazingira.
Leo hii mfano, Wakristo hatuwezi kusema tunataka mahakama ya Kikristo huku mapekeo yetu na uendeshaji wa jamii zetu za Kikristo zina tofauti, Maprotestanti na Wakatoliki wakiwa na mapokeo tofauti na mifumo tofauti ya ibada na uendeshaji kwa kutumia dini hiyo hiyo moja.
Mfano, kwa Wakatoliki, viongozi wake wa kidini wanakatazwa kuoa. Lakini hakuna mahali popote katika Biblia iliposema kuwa viongozi wa Kanisa ni mwiko kuoa. Sasa kama Padiri akitaka kuoa, shurti aachane na Upadiri, hawezi kuenda mahakama kuu na kusema aendelee kuwa Padiri na hapo hapo awe ameoa.
Same mechanism nahisi itakuwa ndani ya sehemu za Sharia, ambako waumini na hata viongozi wasiokubaliana na maamuzi ya kanuni, je watakimbilia mahakama ya Serikali na dola kupata haki? au itawabidi wakubali kanuni za Taasisi?
Kwa maelezo yako ya kinagaubaga, yaelekea suala la Mahakama ya Kadhi ni zaidi ya suala la kuamaua matatizo ya ndoa na mirathi pekee. Mimi binafsi nimepokea maoni yako sawa na mtu anayetaka kuwa na himaya au serikali yake ndani ya serikali, badala ya kuwa ni suala la mambo ya kiroho.
Sasa nadhani sia ajabu kuna wengi waliopokea suala hili la kutaka kurudishwa kwa mahakama ya Kadhi sawa na nilivyokupokea mimi ambavyo ni tofautu na nilivyolipokea mapema suala la kuwepo mahakama ya kadhi.
Nitakachoshauri ni kwanaza kupatikana kwa upatanishi na kufungamana kwa Jumuiya zote za Kiislamu na kuunda Taasisi moja yenye nguvu na mamlaka ambayo ndani yake basi ndiko Mahakama iundwe. Kinyume cha hayo, mvurugano ndani ya jamii hautapata ufumbuzi hata kama Mahakama ya Kadhi itaanza kazi.
Sisi ni binaadamu na tuna udhaifu wa kimwili na kiroho, kwa mtaji huo, inabidi tuwe na makubaliano ya kweli kwanza kushirikiana na kufanya mambo ambayo ni ya faida na yale yasiyofaa tuyaache. Ikiwa kutakuwa na umoja na kuondokana na tofauti ambazo zimeonekana hivi karibuni hata za kuzidiana akili na kujiuzia mali za misikiti na jumuiya, basi hata mahakama itakapokuja, haitakuwa na sura au mapokeo ambayo ni hasi.