Na Ramadhan Semtawa
SIKU chache baada ya naibu katibu mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kulalamika kuingiliwa kwenye anuani yake ya barua pepe, Jeshi la Polisi limesema kuingilia mawasiliano ya faragha ya mtu ni jinai na kumtaka mwanasiasa huyo atoe taarifa polisi ili waanze kulishughulikia.
Zitto, ambaye yuko Ujerumani ambako anasoma, alikaririwa na vyombo vya habari wiki iliyopita akidai kuwa anaingiliwa mawasiliano katika anuani yake ya barua pepe (e-mail), kitu alichosema ni aghalabu kufanywa hata na Idara ya Usalama wa Taifa.
Zitto, ambaye juzi alituma barua pepe kwenye gazeti hili kulalamikia kitendo hicho huku akitangaza kutembea na barua ya kujiuzulu uongopzi Chadema, alieleza kusikitishwa na kitendo hicho ambacho alidai kinafanywa na chama chake.
Hata hivyo, DCI Manumba alipoulizwa jijini Dar es Salaama jana kuhusu malalamiko ya Zitto, alijibu: "Sisi hutujapata rasmi malalamiko hayo, lakini akileta tutachunguza kwa kuwa si sahihi kuingilia mawasiliano ya mtu."
Kwa mujibu wa DCI Manumba, mawasiliano ya barua pepe na mengine ni faragha hivyo ni makosa kwa mtu yeyote kuingilia mawasiliano ambayo hayamhusu.
"Kwa kawaida ni makosa kuingilia mawasiliano ya mtu siku zote tukipata taarifa kama hizo tunachoweza kufanya ni kuchunguza kuthibitisha kwanza kwani ni suala kitaalamu zaidi," alifafanua DCI Manumba.
DCI aliongeza kwamba, siku zote wamekuwa wakichunguza malalamiko yote yanayofikishwa kwao kama yanahusiana na uingiliaji wa faragha ya mtu ikiwemo mawasiliano yake.
Alifafanua kuwa iwapo mlalamikaji akifikisha malalamiko yake, wao huwa hawasiti kuchunguza bila kuangalia jambo lenyewe lina mlengo gani.
"Ni sawa na mtu akimpiga mkewe sisi tukiletewa taarifa, kwanza tunachunguza halafu tunachukua hatua za kisheria kwa mhusika baada ya kujiridhisha. Kwa hiyo hata yeye (Zitto) akileta tutachunguza," aliongeza.
"Siku zote tunafanyia kazi taarifa zinazotufikia, kama kuna mtu anazo taarifa akileta kwamba mawasiliano yake yameingiliwa tutafanyia kazi tukio hilo ili kujiridhisha."
Malalamiko ya Zitto yalitokana na taarifa iliyotolewa na chama hicho kilichodai kuwa ofisa habari aliyetimuliwa, David Kafulila anatumia anuani ya barua pepe ya Zitto visivyo halali. Kafulila na Zitto ni marafiki wakubwa.
"Sitaki kugombana na mtu mimi. Wala msiniweke kwenye kifungo cha siasa. Ni bora niishi huru kuliko katika mateso ya siasa za kipumbavu kabisa. Nitafanya maamuzi ambayo hayajawahi kufikiriwa," alisema Zitto katika taarifa yake kwa Mwananchi.
Alisisitiza kwamba kamwe hatasukumwa na Chadema na kwamba "wanapaswa waniache nipumzike na kufanya mambo yangu".
"Hakuna mtu ananayeweza kuzungumza kwa niaba yangu hata kama ni rafiki yangu, siasa siyo chaguo langu la pekee katika maisha," alisema.
Katika kuonyesha kuchukizwa na baadhi ya taarifa alizoziita za kizushi zilizoandikwa na gazeti moja la kila siku (si Mwananchi), Zitto, alisema: "Faragha yangu ni faragha yangu, Zitto ni Zitto kama yeye na siyo mali ya Chadema.
Akizungumzia uhusiano wake na Kafulila aliyehamia NCCR-Mageuzi kutoka Chadema, Zitto alisema: "Siku zote msimamo wangu umekuwa kwa wale wanaokandamizwa... na katika hili David (Kafulila) ndiye anayekandamizwa."
Alisisitiza kwamba kamwe hatasukumwa na Chadema katika kufanya mambo yake.
"Hakuna mtu ananayeweza kuzungumza kwa niaba yangu hata kama ni rafiki yangu, siasa siyo chaguo langu la pekee katika maisha yangu."
"Msimwandame Kafulila. Mumwache mtoto wa watu. Mmeshamwita sisimizi inatosha. Msijaribu kunigombanisha na Kafulila. Sitaki... sitaki... sitaki," aling'aka Zitto.