Waziri aitisha Chadema

Saint Ivuga

JF-Expert Member
Aug 21, 2008
54,363
58,386
Waziri aitisha Chadema Send to a friend Thursday, 03 March 2011 20:54 0diggsdigg

13wasiraleo.jpg
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Steven Wassira

Na Waandishi WetuWAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Steven Wassira amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kisije kikailaumu serikali itakapokosa uvumilivu na kutumia nguvu ya dola dhidi yake.
Wassira alisema chama hicho kinapandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya serikali na kuandaa mpango wa kuiondoa kwa nguvu serikali iliyoko madarakani.
Wakati Wassira akisema hayo, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango naye amekishukia chama hicho akisema maandamano yake hayana nia ya kushinikiza Dowans isilipwe, bali kuhamasisha vurugu nchini.

Kauli hizo za viongozi hao wa CCM, zimekuja siku tatu tu baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwaonya viongozi wa Chadema kwa kuandaa maandamano na kupandikiza mbegu mbaya za chuki dhidi ya serikali.

Rais Kikwete alisema hayo alipokuwa akilihutubia taifa katika hotuba ya mwisho wa mwezi Februari kupitia vyombo vya habari. Chadema kimekuwa kikifanya maandamano na mikutano ya hadhara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kupinga serikali kuilipa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans pamoja na kuzungumzia ugumu wa maisha.

Waziri Wassira, akizungumza katika kipindi maalumu kilichorushwa juzi usiku na Televisheni ya Taifa (TBC), alisema Chadema hakina haki ya kufikiria kuiondoa serikali madarakani.

"Hawawezi na hawana haki ya kufikiria kuiondoa serikali, hawana hiyo haki. Kikatiba hawawezi na kama itatokea itakuwa ni ukiukwaji wa katiba," alisema Wassira na kuongeza:

"Suala la kuiondoa serikali madarakani halipo na wakitaka mazungumzo, hilo halizungumziki... hatuna chuki na Chadema, lakini tunapingana nao wanapowashawishi watu wawaunge mkono katika yao. Hilo haliwezekani."

Akizungumzia kile Chadema inachosema inachokiita hali ngumu ya maisha, Wassira alisema: "Hali ngumu ya maisha inatokana na mtandao mrefu. Hivi sasa mafuta yako juu, pipa moja linafikia dola 150, sasa wanataka Rais Kikwete aende Uarabuni kusimamia kupanda bei za mafuta?"

"Mafuta ni kila kitu, sasa yakipanda si Tanzaia tu hata mataifa mengine ni hivyo. Hata ukienda China hivi sasa kuna mfumuko wa bei, ni wazi pia hata wanaotumia bidhaa za China, bei itakuwa juu kwa sababu dola imepanda."

Wassira alikishambulia Chadema akirejea kauli ya Rais Kikwete kuwa kinatumia vibaya nafasi na haki yao ya kuandamana kwa kueneza chuki kwa wananchi juu ya serikali yao.

"Dola ina mipaka yake ya kuvumilia. Uvumilivu ukizidi itatumika lakini kama wataendelea kupandikiza chuki, watawahadaa wananchi na kuwatia hofu, wananchi wanataka kuishi bila hofu...wakitaka tukae tuzungumze, bei zinapanda tufanye nini, huku tukidumisha amani."

"Hatuwezi kukaa kimya kuona eti kwa kuwa ni wapinzani wafanye wanavyotaka. Kuna mipaka yake, wakiendelea watakutana na mkono wa dola na wasije wakatulaumu."

Akinukuu vifungu vya Katiba, alisema: "Ibara ya 20 ya kifungu cha Katiba, inampa nafasi na haki kila mtu kukutana na yeyote na kutoa mawazo lakini, si kutumia nguvu kufikia malengo ya kisiasa. "Huku (kutumia nguvu) ni kuvunja katiba na hatutakuwa wavumilivu katika hili."

Wassira amekishauri Chadema kutulia akieleza kuwa watu hawakihitaji sasa kwa kuwa si muda mrefu wananchi wamepiga kura na kila mmoja ameona matokeo.

"Tuliingia wote katika mapambano ya ubunge na urais, zilipigwa kura na wananchi hao hao ndiyo walioamua. Sasa hawa wameshindwa kwa njia ya demokrasia, wanataka kutumia nguvu, hiyo haikubaliki...haikubaliki."

"Sawa, leo wanasema wanaizungumzia Dowans, kwanza iko mahakamani, halafu watakuwa na kipi kipya? Kama huyo Slaa (Dk Willibrod, Katibu Mkuu wa Chadema) siku zote, kampeni zote ameimba Dowans, ufisadi kasema sana lakini watu wakampa kura Kikwete..."

"Tunachotaka ni amani na umoja. Hii ya kusema nguvu ya umma inatoka wapi? Kama nguvu ya umma basi iko CCM kwa sababu wamepiga kura watu milioni tano, CCM wakapata milioni tatu wao (Chadema) milioni mbili, sasa nguvu ya umma ni nani hapa?"

Kwa mujibu wa Waziri Wassira, Serikali haitazuia haki ya mtu au kikundi kuandamana lakini, haitavumilia wanaotumia vibaya fursa hiyo... "Ni wazi Chadema wanatuonyesha wao ni washari, wanawatia hofu wananchi, tunawaambia waache kufanya hivyo.

"Katiba iko wazi, kuna vikao halali vya kuwasilisha yao na zaidi ni Bunge, tena uzuri bungeni unasema unavyotaka ilimradi usivunje sheria, sasa kuwakusanya wananchi na kuwaeleza unayotaka ni kuvunja sheria. "Kuna Sheria ya Usalama wa Taifa, kutangaza kutaka kuiondoa serikali madarakani ni kuvunja Sheria ya Usalama wa Taifa, hapo dola haitavumilia," alisema Wassira.

Alisema wananchi wanataka kuishi kwa amani kwani hawajui vita... "Vita wanayoijua ni ile ya Kagera mwaka 1978 na ilipiganwa katika mkoa mmoja wa Kagera, labda haya mabomu ambayo yamelipuka katika kambi za jeshi kwa bahati mbaya. "Upinzani si vitisho, ni hoja, kama wana hoja wasubiri kikao cha Bunge la Bajeti Juni, waje na mawazo yao, waje na hoja za upinzani lakini si vitisho."

Kauli ya Kilango
Akizungumza na gazeti hili jana, Kilango alitaka chama hicho kisiendelee kupandikiza chuki kwa jamii akieleza hasara yake kuwa ni kuleta maafa na kuua taifa. Alisema inasikitisha kuona viongozi wa Chadema wanatoa kauli za kuhamasisha vurugu badala ya kushinikiza Dowans isilipwe kama ilivyodai awali.

Alisema kama kweli Chadema kinataka Dowans isilipwe, kingeongeza nguvu za wanasheria ili kuhakikisha kesi iliyofungunguliwa mahakamani na wanaharakati inafanikiwa na si kuzunguka nchi nzima kumtaka Rais ajiuzulu.

“Najua ndugu zangu wa Chadema hawataki kusemeshwa lakini, mimi kama kiongozi nimeona ni vyema niwaambie ukweli. Kauli kama kumtaka Rais ajiuzulu hazifanani na lengo la kushinikiza serikali isiilipe Dawans,”alisema.

Aliongeza “Nilikataa, ninakataa na nitakataa serikali ya CCM kuilipa Dowans na si wabunge wa CCM tu, ambao wanakataa hilo, bali hata wanaharakati wa haki za binadamu, lakini kwa nini tutake Rais ajiuzulu badala ya kukazania dai la msingi?"

Alisema Chadema wasifikiri kuwa wao tu ndiyo ambao hawataki Dowans isilipwe, bali huo pia ni msimamo wa wabunge wa CCM katika azimio lao walilolipitisha wakati walipofanya kikao Februari mwaka huu na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete.

Kilango alisema kuwa ni muhimu Watanzania wakajiuliza kama kweli Chadema kuzunguka kwao ni kwa ajili ya kushinikiza serikali isiwalipe Dowans au la.

Kwa mujibu wa Kilango, kauli zinazotolewa na viongozi wa Chadema katika maandamano yao kama Kikwete ajiuzulu au iwe kama Misri na Tunisia, inaonyesha kuwa nia yao si Dowans isilipwe, bali malengo yao ni kutaka Rais ajiuzulu.

“Katika ulimwengu wa hekima na busara, binadamu yeyote yule angetazamia wote wanaopinga Dowans kulipwa wangeunganisha nguvu pamoja kuwasaidia wale ambao wamelichukua jambo hili kisheria na hasa tukijua wazi kwamba takriban Watanzania wote hawataki kodi zao zitumike kulipa Dowans,” alisema Kilango.

Kilango aliitahadharisha serikali kutopenda kufanya vitu kwa dharura na badala yake iwe inachukua tahadhari katika kutatua matatizo ya kitaifa likiwamo suala hilo la umeme.

Ameishauri kutengeneza mabwawa makubwa yatakayosaidia kuhifadhi maji na kuondoa adha ya kupungua kwa maji katika mabwawa yanayotumika kuzalisha umeme nchini.

“Lazima serikali nayo iangalie hili kwani mfumo wa kuhifadhi maji ya akiba kama uliopo nchini Marekani kule Tenessee, ungeweza kusaidia kipindi kama hiki cha ukame,” alisema.

Alisema gharama inayotumika kukodi mitambo ya dharura kila wakati tatizo linapotokea, zingeweza kutengeneza “Stigller’s gauge” kuzalishia umeme na gharama yake ni dola za Marekani 400 milioni tu.

“Wasiwasi wangu ni kwamba fedha nyingi zinazotumika kwa dharura ambazo zingeweza kutengeneza “Stigller’s gauge” ambayo iko sehemu za Chita katika Bonde la Kilombero,”alisema Kilango.

Mrema naye akerwa

Naye Mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema ameonya kuwa kuiondoa serikali iliyoko madarakani bila kufuata njia za kikatiba kunaweza kuzalisha matatizo makubwa na kuliangamiza taifa.

Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) alikuwa akizungumzia hali ya kisiasa nchini hususan maandamano na mikutano ya hadhara inayofanywa na Chadema.

Alisema licha ya kwamba hapingi maandamano hayo kwa kuwa yako kwa mujibu wa sheria, yakizidi yanaweza kuing’oa serikali iliyoko madarakani kama ilivyotokea Madagascar.

“Mimi siitetei CCM wala serikali ya Kikwete kwamba wasiondolewe madarakani kwa sababu wao hawana hatimiliki ya kutawala nchi hii, lakini njia za kikatiba zitumike kuwaondoa madarakani,” alisema Mrema na kuongeza:

“Maandamano ya Chadema ni halali lakini, tukiwazoesha watu maandamano kila kukicha tutafikia mahali kama wenzetu wa Misri, Somalia, Libya na Madagascar.”

Alisema ufisadi na matatizo mbalimbali yanayolikumba taifa sasa hayawezi kumalizwa kwa maandamano na kwamba njia za mkato zinaweza kuleta maafa makubwa nchini. Mrema alisema wapinzani wana kazi nyingi za kufanya ikiwamo matumizi ya fedha za umma katika halmashauri na Chadema wanatakiwa kubuni njia mbadala ya kufikisha ujumbe wao huo badala ya maandamano.

“Japokuwa mwaka 1995 niliandamana na kupigwa mabomu lakini, tunajifunza kwa sababu tunaona yanayotokea katika nchi nyingine,” alisema.

Alisema serikali ikiondolewa kwa njia ya nguvu za umma ambayo ni maandamano, vurugu na mambo mengine, itasababisha katiba ya nchi kufa na kuifanya nchi isiwe na katiba.

Huku akionyesha vitabu vya takwimu za hesabu za serikali, Mrema ambaye ni Mwenyekiti wa wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa alisema, wapinzani wamepewa kazi nyingi badala ya kukimbilia kwenye maandamano na mikutano tu.

“Wapinzani tumepewa na Bunge kazi ya kupambana na ufisadi hivyo, tutumie fursa hizo tuwakamate, ufisadi hauwezi kuondolewa kwa maandamano,” alisema.

Alisema kama serikali ikiondolewa madarakani kutakuwa na ombwe la uongozi na jeshi linaweza likachukua nchi wakiona inaingia kwenye migogoro.

Ataka Chadema wakamatwe
Katika hatua nyingine, Balozi wa amani wa taasisi ya Universal Peace Federation, Risasi Mwaulanga ametaka viongozi wa Chadema wakamatwe na kufunguliwa mashitaka ya uhaini kwa kile alichosema kuwa wanavuruga amani ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwaulanga alisema Chadema kinatumia fursa ya maandamano kumkashifu Rais Kikwete kitu ambacho ni uvunjifu wa amani.

“Hakika huu ni uhaini wa wazi ambao Chadema inaufanya, kwani umma unapokasirika na kupata hamasa mbaya, matokeo yake ni kuzigomea sera na kuwafanya wananchi kuacha kushiriki shughuli za maendeleo,” alisema Mwaulanga na kuongeza:

“Mwenyekiti wa Chadema na Katibu wake Mkuu wanapaswa kukamatwa, kufunguliwa mashtaka ya uhaini. Bunge linapaswa pia kutoa onyo kali kwa wabunge. Hali kadhalika, Msajili wa Vyama vya Siasa aangalie vifungu vya Katiba yake kuona uwezekano wa kukisimamisha au kukifuta chama hicho kwa usalama wa Taifa.”

“Vyama vya siasa vina haki ya kuandamana, ila ikitumiwa vibaya itavuruga amani. Kwa mfano, Chadema wanatumia maandamano kumpinga Rais Kikwete, huu ni uhaini kabisa.”

Mwaulanga pia alitumia nafasi hiyo kumpiga vijembe bila kumtaja jina Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa akidai kuwa amekuwa akitumia vyombo vya habari na majukwaa ya kidini kuikosoa CCM huku akitolea mfano kauli yake ya hivi karibuni kutaka mishahara ya watumishi wa umma ipande.

“Sasa mtu unataka wafanyakazi waongezwe mishahara, Rais atazitoa wapi fedha hizo?” alisema Mwaulanga.

Kwa mujibu wa Mwaulanga, kutumia majukwaa ya dini kupinga mipango au upungufu wa Chama na serikali kwa viongozi wa siasa si sahihi hata kidogo.

“Wanapokaribishwa na viongozi wa dini wanachopaswa kufanya ni kupinga mipango mibaya ya shetani kwa binadamu kumuasi Mwenyezi Mungu na siyo kuiponda serikali” alisema.

Habari hii imeandikwa na Ibrahim Bakari, Boniface Meena,Nora Damian na Elias Msuya
 
mama kilango, wabunge wa ccm wote walisema lini kuwa hawakubali kulipwa kwa DOWANS ?, unaposema ni msimamo wa wabunge wa ccm unamaanisha na ROSTAM naye anapinga na LOWASSA naye anapinga kulipwa kwa DOWANS? please acha kuupotosha umma wewe.
 
Hili ndilo tatizo la vyeo vya kupeana kwa misingi ya "Mwenzetu". Mtu anajipendekeza hadi anatia kinyaa. Kama kweli wana ubavu wakifute CHADEMA waone matokeo. Mimi sijaona lolote la Uhaini katika "Crusade" ya CHADEMA zaidi ya kuwaona CCM na vibaraka wao wakihunyahunya kutokana na madhambi yao kuumbuliwa hadharani na CHADEMA - chama pinzani ambacho kimsingi kazi yake ndiyo hiyo kwa kipindi cha miaka mitano tokea kwisha uchaguzi. Kama ni uhaini mbona hatukusikia kelele za wanaolaani sasa "Uhaini" Tume ilipokuwa inageuza matakwa ya wapiga kura waziwazi kwa malengo ya kuwanusuru na kushindwa watu waliokataliwa na wapiga kura ambayo ndiyo maana halisi ya Uhaini? Ajabu ni kwamba hilo lilitendeka kwa usaidizi wa vyombo vilivyotazamiwa kuuzuia Uhaini! Lakini kuandamana kulaani kupanda kwa gharama za maisha, hali ngumu ya kiuchumi, wizi ndani ya serikali unaohusisha viongozi wa juu, Rushwa ndani ya serikali am bapo fedha ya walipa kodi inafujwa na kufisadiwa si uhaini hata kidogo. Wanaosema hivyo au wanajipendekeza kwa JK na serikali yake, au wenyewe ni sehemu ya tatizo kama alivyo Wassira ambaye sasa amethibitisha mchovu na aliyeishiwa kabisaa sera.
Ingemfaa Wassira na watu wa umri wake wanaojihisi kuishiwa nguvu kama alivyo kuwaachia vijana kuepuka aibu ya kuropoka pumba kama tunazozishuhudia.
 
Back
Top Bottom