Mrema alitisha Jukwaa la Wahariri
[Source Tanzania Daima]
na Mobini Sarya
MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, anakusudia kulishitaki Jukwaa la Wahariri na magazeti kadhaa ikiwa hataombwa radhi kwa kuchafuliwa jina lake, kwa kuhusishwa kutoa maneno ya uchochezi kwenye msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mrema alisema anataka magazeti na wahariri waliotumika kumchafua wamuombe radhi kwenye ukurasa wa mbele sambamba na kuambatanisha fidia ya sh bilioni mbili kila mmoja, vingenevyo atawafikisha mahakamani.
Nataka Jukwaa la Wahariri waniombe radhi ukurasa wa mbele pamoja na magazeti yaliyohusika kunikashfu bila kujali kuwa mimi Mrema nimewahi kuwa Naibu Waziri Mkuu wa nchi hii, Waziri wa Mambo ya Ndani na mbunge wa muda mrefu, kiongozi niliyefanya kazi hiyo kwa uaminifu mkubwa, alisema Mrema.
Alisema Oktoba 14 mwaka huu, bila kufuata haki, Jukwaa la Wahariri lilitoa taarifa ya upande mmoja iliyokuwa inalenga kumchafua na kukisambaratisha chama chake huku ikisafisha baadhi ya wanasiasa baada ya kudaiwa aligeuza kifo cha Wangwe mradi wa kisiasa.
Alisema taarifa hiyo ilitolewa baada ya kamati iliyoundwa kuchunguza kama kwenye kifo kile palitokea vitendo vilivyoashiria vurugu, katika ripoti hiyo watu 18 walihojiwa lakini yeye hakuwahi kupewa nafasi ya kusikilizwa licha ya kwamba wahusika wanajua ofisini kwake na namba yake ya simu.
Alinukuu ripoti hiyo pale inaposema kwa mfano Mwenyekiti wa TLP Augustine Mrema, kamati ilielezwa kwamba alitumia msiba huo kuchonganisha familia ya Wangwe na CHADEMA kiasi cha kuwashawishi waishushe bendera ya CHADEMA na kupeperusha ya TLP. Alisema CHADEMA wamemuua Wangwe.
Alidai licha ya taarifa hiyo kujionyesha kuwa ilikuwa na upungufu, ambayo hakidhi ripoti kamili, lakini viongozi wa jukwaa hilo waliisambaza kwenye vyombo vya habari kwa makusudi maalumu hata pale walipotahadharishwa kuwa inapendelea upande mmoja.
Aliongeza kuwa hata pale ilipofikishwa kwenye vyombo vya habari na ikaonekana kuwa taarifa hiyo inaegemea upande mmoja, wahariri wake walishindwa kujisumbua kuisoma zaidi ili wabaini upungufu wake kisha wamuulize, badala yake waliamua kuiandika hivyo hivyo.
Aidha, alisema katika kuonyesha kuwa ulikuwa mpango maalumu wa kuisambaratisha TLP, baada ya siku mbili alifanya mkutano na vyombo vya habari akaeleza athari za ripoti ile, lakini ni gazeti moja lililoandika habari yake na Jukwaa la Wahariri likishindwa kumuomba radhi hadharani na kumwalika kama walivyokuwa wamedai.
Kwa kuwa wameamua kutumika kusambaratisha chama changu nimeamua kuwapa siku hadi Novemba 13 mwaka huu wakishindwa kuniomba radhi na kunipatia vibilioni mbili nitakwenda, tutakutana mahakamani wanieleza aliyewatuma wanichafue, alisema.
Kwa mjibu wa malalamiko yake, tayari ameshampatia kazi wakili, Dk. Sengondo Mvungi kupitia Kampuni ya South Law Chamber kuhakikisha inawafungulia mashitaka wahariri hao.
Wahariri hao ni Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Sakina Datoo, Mhariri wa gazeti la Nipashe, Jesse Kwayu, Mhariri wa Mwananchi, Theofil Makunga na Mhariri Mtendaji wa Tanzania Daima, Absalom Kibanda na Muhingo Rweyemamu, ambaye alikuwa mjumbe wa kamati iliyotoa ripoti hiyo.
Wengine ni mwandishi wa Sauti ya Amerika (VOA) aliyemtaja kama mdhamini wa jukwaa hilo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Saed Kubenea, Katibu wa Jukwaa, Jamila Abdallah na mjumbe, Neville Meena.
MT TAKE: Mrema muda wake umepita hata mwenyewe analitambua hilo. Anaelezea mambo aliyofanya enzi hizo lakini hana la maana la kuonyesha alilofanya siku za karibuni. Katika kila chaguzi anazoshiriki mzee wetu ndivyo anavyozidi kupata uchache wa kura. Sasa anadiriki kutaka kwenda mahakamani kudai vibilioni kadha kutaka kuua magazeti ambayo yamekuwa mwiba kwa mafisadi. Ingefaa ajiuzulu siasa wakati watu bado wanakumbuka mema aliyofanya.