Suley2019
JF-Expert Member
- Oct 7, 2019
- 1,815
- 4,565
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, amekosoa hatua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutaka kufanya maandamano kupinga miswada ya sheria za uchaguzi na ugumu wa maisha akisema ni dalili ya kupungua kwa uvumilivu nchini.
Wasira amesema hayo leo Januari 17,2024 alipofanya mahojihano na Mwananchi Digital huku akisisitiza kuwa viongozi wa chama hicho akiwamo Mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu Mkuu John Manyika na Makamu Mwenyekiti, Tundu Lissu walikuwa wabunge na wanajua utaratibu huo.
Wasira aliyewahi kuwa waziri katika wizara tofauti katika awamu zilizopita, amesema Chadema inapaswa kusubiri mchakato wa kibunge kuyajadili na kuyatolea uamuzi maoni yaliyokusanywa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria na si kuandamana.
Wasira amesema hayo siku ambayo pia vyama 13 vya upinzani visivyo na wabunge vimetoa tamko la kupinga maandamano hayo.
Hata hivyo, John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema alipoulizwa kuhusu wanaoyapinga amesema "tunaweka pamba maskinioni, ratiba ya maandamano bado iko vilevile na Katibu Mkuu wetu ameshatoa ratiba ya namna shughuli zitakavyofanyika".