*Ni wale wa makosa ya jinai waliompekua Dar
*Asema wana mkono mrefu katika kuchunguza
Na Ramadhan Semtawa
SIKU moja baada ya wakili wake J Lewis Madorsky, kuibuka na kutema cheche, Andrew Chenge amesema makachero wa kuchunguza Makosa Makubwa ya Jinai kutoka Uingereza yaani Serious Fraud Office (SFO), ni mahiri na wenye mkono mrefu, hivyo hakuna kitu kitakachofichwa.
Wakili Madorsky ambaye alizungumza na Mwananchi juzi kutokea Marekani ikiwa ni chombo cha kwanza cha habari nchini Tanzania kuongea nacho, alisema atamtetea Chenge popote duniani na atalipua mabomu kuhusu baadhi ya wanasiasa wanaomchafua mteja wake.
Kauli hiyo mpya ya Chenge inatoa taswira kwamba, sakata hilo kwa sasa linapaswa kusubiri matokeo ya SFO ambayo itatoa hatima ya ukweli au uongo wa tuhuma zinazomkabili.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Chenge alisema mkono mrefu wa SFO utaweka bayana kila kitu kuhusu tuhuma zake; ndiyo maana sasa ameamua kukaa kimya.
Chenge alifafanua kwamba, anachotaka Watanzania wapate ni usahihi na ukweli wa tuhuma zake na si maneno ya kufikirika.
"Sioni haja ya kuendeleza mbinu zisizo na msingi, SFO wana mkono mrefu, hivyo kama ni ukweli utafahamika baada ya uchunguzi wao," alisisitiza Chenge.
Waziri huyo wa zamani wa Miundombinu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa zaidi ya miaka kumi, alisema hadi sasa bado taarifa kuhusu tuhuma zake zimekuwa zikipotoshwa na baadhi ya watu.
Alisema ni vema mkanganyiko huo wa taarifa ukaondolewa kwa Watanzania kusubiri taarifa sahihi za SFO.
"Maana hadi sasa kuna baadhi ya Watanzania hawataki kuelewa ukweli, ni vema sasa wakasubiri kupata taarifa sahihi ili kuondoa mkanganyiko huo wa taarifa," alisisitiza.
Chenge aliongeza kwamba, asichotaka yeye ni kuona Watanzania wanadanganywa kuhusu tuhuma zinazomkabili ndiyo maana anasisitiza wavute subira ili wapate matokeo ya uchunguzi wa SFO.
"Sitaki Watanzania wapewe taarifa ambazo zinapotosha ukweli wa jambo lenyewe lilivyo," aliongeza Chenge.
Kuhusu taarifa kwamba makachero wa SFO walikuta nyumbani kwake kila aina ya fedha kama Duka la Kubadilishia Fedha, alisema mengi yatasemwa, lakini ukweli utabainika baada ya uchunguzi.
"Kwa kipindi hiki kila kitu kitasemwa, nafikiri jambo la msingi ni kusubiri matokeo ya uchunguzi wa SFO."
Chenge ni mmoja wa viongozi waandamizi wa serikali ambao SFO inawachunguza kuhusiana na tuhuma za kuhusika katika sakata hilo.
Kuchunguzwa kwa Chenge haimaanishi kwamba, ameiba au amekula rushwa, isipokuwa SFO inataka kuona Sh1.2 bilioni ambazo amezihifadhi katika akaunti yake moja katika kisiwa cha Jersey kama zina uhusiano na sakata la ununuzi wa rada kutoka BAE System ya Uingereza.
Ndani ya serikali ya Tanzania, inaelezwa sakata hilo linagusa vigogo kumi (Top Ten) wa serikali iliyopita kuanzia Rais mstaafu Benjamin Mkapa na baadhi ya mawaziri, naibu waziri mmoja na makatibu wakuu katika serikali ya sasa.
Chenge anaelezwa kukutwa na kiasi hicho katika akaunti yake moja katika kisiwa hicho cha Jersey, hivyo kufanya makachero hao wa SFO kuchunguza mabilioni hayo kama yana uhusiano na rada iliyonunuliwa mwaka 2002.
Ununuzi wa rada hiyo ambayo pia ilimtikisa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair, inaelezwa kuwa ghali kwa nchi maskini kama Tanzania ambayo ingeweza kununua rada ya Sh 5 bilioni kuliko hiyo ya Sh 70 bilioni.
SFO inaangalia fedha Sh12 bilioni, ambazo dalali wa biashara hiyo alipewa kama aliweza kuwahonga vigogo hao wa serikali kuanzia Rais mstaafu Mkapa na vigogo hao wengine tisa akiwemo Chenge.
Matokeo ya uchunguzi huo yanasubiriwa kwa hamu nchini, ili kuondoa utata na kuweka ukweli kuhusu tuhuma hizo dhidi ya Chenge huku pia Watanzania wakitaka kuona vigogo wengine zaidi wanawajibika baada ya Chenge kufanya hivyo kwa kujiuzulu uwaziri.
Source: Gazeti Mwananchi