Habari Wanaforum leo niemkuja na hii habari ambapo Rais Kikwete amtetea Mkapa, Kabla hatujapata habari kamili, picha hiyo ni updates ya ziara ya Kikwete kutoka kwa mtandao wa vijana 'wetu' wa KikweteShein.com au JakayaKikwete.com :-
The President of the European Commission,Mr Jose Manuel Barroso welcomes President Jakaya Mrisho Kikwete to the EU Headquarters in Brussels Belgium this morning.The two leaders later held a press conference in which the EU President pledge continued cooperation with tha Tanzanian government Praising President Kikwete's insights on various challenges facing Tanzania.On his part President Kikwete pledged continued cooperation with the commission on implementing various joint development programmes. (Picha na Maro, Freddy)
(Source JakayaKikwete.com)
Back to the topic:- Habari kutoka kwa mwandishi wa Rais kutoka huko Ubelgiji
SAKATA LA RADA... JK: Hakuna sababu Mkapa kujitetea
Kutoka gazeti 'letu' la Uhuru
Na Maura Mwingira, Brussels,Ubelgiji inasema
RAIS Jakaya Kikwete amesema haoni sababu ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, kusimama hadharani na kuzungumzia suala la ununuzi wa rada.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete ilitokana na swali aliloulizwa na mmoja wa Watanzania wanaoishi mjini hapa, Abubakar Hiza, ambaye alitaka ufafanuzi kuhusu uchunguzi unaoendelea wa ununuzi wa rada na alitaka Rais mstaafu Mkapa, atoe tamko na aseme kwa uwazi na ukweli mambo yalikuwaje.
"Hivi mnataka mzee Mkapa atoe sauti, sauti kuhusu jambo gani? Mnataka aseme, aseme nini, naona tumwache mzee wa watu," alisema Rais Kikwete.
Aliyasema hayo alipokuwa akisalimiana na Watanzania wanaoishi Brussels, Ubelgiji, baada ya kuwasili kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambayo madhumuni yake ni kuonana na kuzungumza na Rais wa Jumuia ya Ulaya, Kamishna wa Maendeleo na Misaada ya Kibinadamu na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Fedha katika Serikali ya Ubelgiji.
Alifafanua kuwa suala la uchunguzi wa ununuzi wa rada linafanywa na Serikali ya Uingereza, kupitia kitengo chake maalum, kwa kile kinachoamini kulikuwa na tuhuma za rushwa kati ya vongozi wa kampuni ya 'BEA System' na wakala aliyehusika na ununuzi wa rada.
Alisema Serikali ya Tanzania ilichofanya ni kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo, pale ilipoomba kuja nchini na kumhoji wakala huyo.
"Uingereza haituchunguzi sisi, wanaichunguza kampuni yao na viongozi wa kampuni hiyo, tena kampuni ya serikali, wanachunguzana wao kwa wao, kuona kama kuna tuhuma zozote za rushwa, na sisi tulitoa ushirikiano wote," alisema Kikwete.
Aliongeza kuwa suala hilo linaihusu Tanzania na serikali imelifikisha mikononi mwa Taasisi ya Kuchunguza Rushwa (PCB) ili nao wachunguze na kujua ukweli na kisha kutoa taarifa.
"Ikionekana wametudhulumu tutaona namna ya kufurukuta ndiyo maana tunashirikiana nao, matumaini yetu ni kwamba watatupatia taarifa ya nini kimetokea, lakini kwa kuwa tuna maslahi nalo na sisi tumewataka PCB walitazame suala hilo," alifafanua.
Aliongeza kuwa siyo uuzwaji wa rada kwa Tanzania pekee yake unachunguzwa, bali hata Afrika ya Kusini, Saudi Arabia nako kampuni hiyo inatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Akijibu swali kuhusu kupanda kwa bei ya umeme na athari zake kwa mwananchi, hifadhi ya mazingira na suala la Net Group kushindwa kazi ya menejimenti, Rais Kikwete alisema upandaji wa bei ya umeme ulikuwa ni wa lazima kutokana na gharama za uzalishaji.
Alifafanua kuwa TANESCO ilitaka umeme huo upande kwa asilimia 25 lakini serikali ilikataa na kuruhusu asilimia hiyo sita ambayo alisema siyo kiwango kibaya sana, kulinganisha na asilimia 25 kwa kuwa hakuna njia mbadala.
Koraniga Mkora, alitaka serikali kuangalia upya ada ya sh. 770,000 wanayolipa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa ni kubwa mno nakupendekeza ipunguzwe ili wanafunzi wengi wapate elimu hiyo na taifa kujipatia wataalamu wa kutosha.
Akijibu hoja hiyo na ile ya kutaka wakuu wa mikoa wapigiwe kura na wananchi badala ya kuteuliwa na cheo cha mkuu wa wilaya kifutwe, Rais alisema uendeshaji wa serikali kokote duniani upo katika mifumo miwili.
Aliitaja mifumo hiyo kuwa ni viongozi wa kuteuliwa na wale wa kupigiwa kura, mifumo ambayo ndiyo inayotumiwa na serikali ya Tanzania.
Alisema tofauti na madiwani au wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya ni wawakilishi wa serikali katika maeneo yao, hivyo watateuliwa na serikali badala ya kupigiwa kura na wananchi na kuwa cheo cha mkuu wa wilaya hakiwezi kufutwa.
Kuhusu ada ya sh. 770,000, alisema hiyo siyo ada kamili waliyotakiwa watoe kwa kuwa serikali imefidia sehemu iliyobaki.
Alisema serikali haiwezi kupunguza ada hiyo kwa sababu imeshafanya mengi ya kutosha katika kusaidia wanafunzi.
Katika hatua nyingine, Shila Malegesi, aliitaka serikali kutoharakisha katika uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki, kwa kile alichosema kuwapo tofauti kubwa na za msingi kati ya Tanzania na wana jumuiya wengine.
Alisema asingependa kuwapo kwa shirikisho hilo na kuwa: "Uundwaji wa shirikisho ni suala nyeti, Watanzania ni wastaarabu sana kuliko hao tunaotaka kuungana nao. Serikali yetu lazima ilipe umuhimu wa pekee kabla ya kufikia uamuzi."
"Hivi sasa tu serikali haitoi upendeleo kwa Wazalendo, tunashuhudia wageni wakipata ajira, kwa nini tusifanye kama wenzetu wa Ulaya ambao mtu wa nje hapati kazi kirahisi," alisema Malegesi.
Malegesi pia alilalamika kwamba tovuti ambayo wananchi wameshauriwa kupeleka maoni yao kuhusu shirikisho lao, haipatikani kwa urahisi na hivyo kufanya maoni yao kutowafikia walenga na kuchapishwa kwenye vyombo vya habari.
Akijibu hoja hiyo, Rais Kikwete alisema serikali itayashughulikia kwa ukamilifu maoni yote yatakayotolewa na wananchi na kutafakari mwelekeo muafaka wa uundaji wa shirikisho na aliwataka wananchi kutoogopa kuwasilisha maoni au hisia zao.
Watanzania hao, walimpongeza Rais Kikwete kwa hatua mbalimbali anazochukua katika kuwatumikia wananchi, kupambana na vitendo vya rushwa, ujambazi, elimu na uboreshaji wa mishahara ya watumishi wa umma na kuwa sasa wafanyakazi serikalini wanajivunia kufanya kazi serikalini.
Rais Kikwete aliwahimiza Watanzania hao kutosahau nyumbani kwa kuchangia maendeleo ya nchi yao na familia zao, kuheshimu sheria za nchi wanazoishi na kutojihusisha na vitendo vya uhalifu