Sherehe hizi za Chenge za nini?
John Bwire Mei 7, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
WA kwanza alikuwa Edward Lowassa. Lakini baadhi yetu tulimwelewa. Ilikuwa ni taharuki tu ya joto la wakati huo.
Yeye alikuwa Mtanzania wa pili kujiuzulu uwaziri mkuu, baada ya Julius Nyerere mwaka 1962, japo sababu zao zinapishana sana. Kwa historia hiyo, baadhi wanaweza kufumbia macho mapokezi yake makubwa Monduli.
Lakini haya anayofanya Andrew Chenge, Waziri wa miundombinu aliyejiuzulu, hakika yanadhihirisha namna maadili yetu kama Watanzania yanavyozidi kuzama topeni.
Taarifa kutoka jimboni kwake, Bariadi Magharibi, zinasema kuwa wana CCM wa huko wameandaa sherehe na mapokezi ya kufa mtu.
Kwa mujibu wa Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Bariadi, Nasunga Lyabuyenze, wananchi wa Bariadi Magharibi wameandaa mapokezi makubwa na ya kihistoria kwa mwanasiasa huyo (Chenge) licha ya tuhuma za ufisadi zinazomkabili.
Tusingejali sana kama sherehe kubwa kama hii inayoandaliwa ingekuwa inahusiana na vitu kama vile Chenge kumtoa binti yake, au kumwoza kijana wake. Hakuna angejali kama sherehe hizo zingekuwa za siku yake ya kuzaliwa, ama za kuadhimisha kumbukumbu yoyote ya masuala yake, ama ya familia yake.
Lakini kumwandalia mapokezi kamambe kama hayo kiongozi anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi na ambaye baada ya yeye mwenyewe kuzipima ameamua kujiuzulu, hakika si kitu cha kufurahisha hata kidogo kwa wananchi wowote makini.
Tumebaki na mshangao huku tukijiuliza maswali mengi. Ni nini ambacho wenzetu hawa wa Bariadi Magharibi wanakifurahia kutoka kwa Chenge ambacho walibakinacho moyoni hadi alipoandamwa na tuhuma za ufisadi na kujiuzulu? Je, mapokezi haya yana baraka za makao makuu ya CCM?
Vyovyote vile; huu ni utamaduni ambao wenzetu wa Bariadi wanataka kuuanzisha lakini ambao kwa ujumla wake hautasaidia kujenga nchi hii masikini ambayo imekuwa ikikwamishwa na vitendo visivyo na tija vya baadhi yetu, vinavyorudisha nyuma maendeleo. Toka lini tuhuma za ufisadi likawa ni jambo zuri la kufurahisha na kusherehekea?
Ni kweli kwamba Chenge anaheshimika sana jimboni kwake. Ni kweli pia kwamba kabla ya tuhuma dhidi yake kuanikwa, wengi walikuwa na imani naye kubwa. Ni kweli pia kwamba baada ya haya yote yaliyomfika anahitaji watu wa kumliwaza. Ni hulka ya binadamu. Nasi tunaielewa. Lakini ni kweli pia huku kunakoandaliwa na wanajimbo lake ni kumliwaza kwa aina yake kwenye tafsiri ya kuuenzi ufisadi.
Na wala Chenge si waziri wa kwanza kujiuzulu nchini. Majuzi tu hapa mawaziri wawili katika Baraza alilokuwamo walijiuzulu. Lakini hatujasikia Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, ambao kwa macho ya umma wa kawaida, wana tuhuma kama za Chenge, wakitutangazia jinsi wapiga kura wao wanavyofurahia tuhuma zilizowafika hadi kuwandaalia mapokezi ya kishindo.
Na si hao tu. Tutashangaa kama Watanzania watakuwa wamesahau kwamba katika muda si mrefu uliopita, kina Dk. Juma Ngasongwa, Iddi Simba, Profesa Simon Mbilinyi, Dk. Hassy Kitine na Kilontsi Mporogomyi walijiuzulu kwa tuhuma mbalimbali, lakini hatukupata kusikia wakiandaliwa mapokezi ya kuwapongeza majimboni kwao.
Kwamba leo Chenge anataka kuonyeshwa kwamba amefanya jambo la kishujaa sana na hivyo kustahili mapokezi makubwa, ni utamaduni ambao haupaswi kuachwa ukue, na kwa hakika ni jambo linalodhihirisha ni jinsi gani CCM imekosa uongozi wenye busara katika jimbo hili.
Lakini pia, kwa kiasi fulani, inaonyesha ni namna gani CCM inashindwa kuongoza vyema wanachama wake na jumuiya zake.
Maana, haiwezekani jumuiya ya vijana ya chama hicho mkoa wa Tanga (UVCCM-Tanga) itoe tamko la kuwataka viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi wajiondoe madarakani halafu katika wiki hiyo hiyo, CCM wilaya ya Bariadi imwandalie mapokezi kamambe mmoja wa hao wanaotuhumiwa kwa ufisadi!
Ni dhahiri kuna mushkeli, na itashangaza kama uongozi wa juu wa CCM utashindwa kusoma maandishi ukutani na kuanza kuchukua hatua kudhibiti utamaduni huu wa kuuenzi ufisadi ambao unatutia aibu sote.