Date::11/19/2008
Operesheni Sangara: yasaidia Chadema kuingia vijijini
Mwenyekiti wa CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe akihutubia wananchi.
Na Mussa Juma
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Oktoba 19 mwaka huu, kilizindua operesheni Sangara, katika mji wa Musoma mkoani Mara.
Operesheni hii ya Chadema, ilizinduliwa katika uwanja Mkendo na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa mji wa Musoma na vitongoji vyake.
Wazo la kuanzishwa operesheni hiyo, lilipatikana mjini Mwanza mapema mwaka huu baada ya viongozi wa juu ya Chadema kufanya ziara na mkutano wa hadhara katika mkoa huo.
Mara baada ya mkutano huo, hoja zilitolewa za kuwapo matawi ya chama kila mahali, uwepo wa viongozi kuanzia ngazi za mabalozi na hivyo ili iwe rahisi kuendesha siasa zenye tija na ushindi siku zijazo.
baada ya mawazo mengi kutokea ndipo tuliamua kuanzisha operesheni hii na mwanzo tulipanga izinduliwe mkoani Mwanza ila kutokana na historia ya kipekee ya mkoa wa Mara na ushindi ya kishindo tuliupata Tarime tuliona ni vyema kuanzia mkoa huu
huu, anasema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Chadema kimepanga kuitumia Operesheni hiyo katika mkoa wa Mwanza ili kuibua vuguvugu jipya la mageuzi hadi ngazi za vijiji likilenga kuhamasisha wananchi kuwa kitu kimoja na kutetea rasilimali na nchi na kupinga ufisadi.
Akizindua operesheni hiyo hivi karibuni, katika wilaya, kata na vijiji vya mkoa wa Mara, Mbowe anasema nchi inakwenda pabaya, hivyo Chadema wameona haiwezekanii kukaa kimya na kuacha mambo yaendee kuendeshwa kama ilivyo hivi sasa ndivyo sivyo.
Ndugu zangu nchi yetu inakwenda pabaya
serikali ya CCM imeshindwa kuwapa Watanzania maisha bora na mafisadi ndio wanatamba hivyo lazima tuunganishe nguvu bila kujali itikadi, tukombowe nchi yetu, anasema Mbowe.
Anasema lengo la operesheni sangara ni kupeleka madaraka kwa wananchi kuanzia ngazi za vijiji, hadi mikoani bila kusimama na kuwa kitu kimoja ili kuikomboa Tanzania kiuchumi.
Mbowe anasema, kushindwa kwa serikali ya CCM kuleta maisha bora licha ya kuwa nchi ina rasilimali za kutosha kunatokana na wasaidizi wa Rais Jakaya Kikwete kujali maslahi yao binafsi na kuacha taifa likiteketea.
Sisi Chadema tumeamua kuja kwenu wananchi kuwaeleza nchi yenu inakwenda pabaya na
tutakuwa pamoja majumbani kwenu, katika vijiji vyenu hadi kieleweke, anasema Mbowe.
Anasema nchi imejaa ufisadi hivyo matumaini ya watanzania kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye aliingia madarakani kwa kura nyingi yametoweka kabisa.
Ndugu zangu tusifanye tena makosa mwaka 2010 tushikamane tuiondowe CCM madarakani kwani chama hiki hakiwezi tena kuleta maendeleo kwa watanzania kwa sera zile zile,
watu wale wale eti kwa kauli mbiu ya ari mpya na nguvu mpya, anasema Mbowe.
Katibu mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa alikuwa akifafanua kitendo cha serikali kushindwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa ufisadi mapema kuwa ni kasoro kubwa kwa serikali ya CCM.
Anasema pamoja za serikali ya Rais Jakaya Kikwete kutoa maagizo mbali mbali kuhusu ufisadi, lakini hadi sasa bado hali ni mbaya na ufisadi unaendelea.
kuna ufisadi mkubwa katika nchi hii... hapa mkoani Mara kuna ufisadi wa Sh155 milioni katika mgodi wa Buhemba kupitia kampuni ya Meremeta inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), anaeleza Dk Slaa.
Dk Slaa anasema kuna tuhuma nyingi za ufisadi ambazo wamezitoa lakini wanashangaa serikali inashughulikia suala EPA pekee.
Dk Slaa anasema ni jukumu la wananchi kusimama kidete na kushinikiza mafisadi wote wachukuliwe hatua zinazostahili.
Operesheni hii inalenga kuwapa changamoto kila mmoja wetu ajuwe wajibu wake
sisi sote ni Watanzania tuna haki sawa hakuna ambaye ana haki kubwa zaidi ya mwingine hivyo ni lazima sote tudai haki hizo bila kujali itikadi zetu, anasema Dk Slaa.
Upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, alikuwa akihimiza umoja kwa vijana bila kujali itikadi zao kwani wao ndio watapata shida miaka ijayo.
CCM na viongozi wake wamechoka hata kwa mawazo hivyo ni jukumu letu sisi vijana kuungana
na kuwangoa madarakani, anasema Kabwe.
Tuna rasilimali nyingi lakini hazitunufaishi Watanzania
.tuna madini lukuki, wanyamapori, samaki na ardhi nzuri lakini vyote havitunufaishi kutokana na sera mbovu za CCM na serikali yake, anasema Kabwe.
Kikubwa kilichopatikana katika operesheni hiyo ya Chadema ni kufanikiwa kufika hadi vijiji wakati huu kabla ya uchaguzi na hivyo kupata wafuasi.
Hali hii ni dhahiri itazidisha upinzani kwa chama tawala katika chaguzi zijazo kwani kwa miaka mingi vyama vya upinzani vimekuwa vikingangania mijini pekee na vijijini kuiachia CCM kutamba.