Nyerere na mgawanyiko wa dodoki lake
Jenerali Ulimwengu Machi 5, 2008
NIMEKUWA nikielezea dalili zinazoonyesha kudhoofu kwa chama kilicho madarakani, CCM, mara kwa mara nikijaribu kuonyesha ni wapi kulikotokea kudhoofu huko.
Safari ya kisiasa ya vyama vya siasa, kama ilivyo katika safari nyingine zote katika maisha, huweza kuchukua mikondo ambayo haikutazamiwa, hata na wale wanaoviongoza. Sheria ile ile ya matokeo yasiyotarajiwa inaweza kuwashangaza hata wajuzi wa mambo.
Kifupi, hebu tudurusu mambo makuu yaliyotokea katika historia ya TANU na CCM. Kwanza kilikuwa ni chama cha ukombozi wa Mtanzania na Mwafrika, kilichojengeka katika falsafa ya utu wa binadamu, upendo na mshikamano. Kisha kikawa ni chama cha uongozi wa serikali, kikakamata madaraka ya dola kikiwa na nia ya kutekeleza falsafa hiyo na kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kikabuni sera madhubuti kwa lengo la kutekeleza falsafa hiyo. Kikajenga mahusiano ya karibu na wananchi kwa kusikiliza matakwa yao na kuyaandalia mikakati ya kuyatekeleza. Kikaielekeza na kuisimamia serikali ili itende yale yatakayowanufaisha wananchi.
Lakini, taratibu, katika kukua kwake, chama kikaanza kuchukua taswira ya dola, kikajichanganya na serikali, kikawa ni chama-dola. Kikaanza kujenga tabia za ki-imla. Mawazo yaliyotofautiana na mkuu wa chama (na kundi dogo lililojifanya kukubaliana naye kabisa) yakawa ni marufuku. Kikawaengua wale walioonekana kama wenye fikra zisizoendana na mkondo mkuu wa fikra zilizokubalika.
Bila kujua, na bila kupenda, chama kikajikuta kimejitenga na wananchi wa kawaida, kikajiunga na dola. Kikaacha kuongoza; kikawa ni mhimili mwingine wa dola. Hata zile sera zilizobuniwa na chama ili kumkomboa mwananchi wa chini zikatekelezwa kiimla, na matokeo yake yakawa ni kumuumiza mwananchi aliyelengwa kukombolewa. Tumekwisha kujadili matatizo ya utekelezaji wa sera za Ujamaa na ujenzi wa vile vilivyoitwa Vijiji vya Ujamaa.
Kimsingi, chama cha siasa ni makutano ya watu wenye fikra zinazofanana, pamoja na tofauti zao ndogo ndogo. Lengo kuu linakuwa ni moja, hata kama zitaelezwa kwa namna tofauti, kila mmoja akiongeza mbwembwe zake na kutumia lugha yake. Dira inakuwa ni moja, hata kama inabidi mara kwa mara kubadilisha mwelekeo wa chombo kufuatana na ukali wa upepo na uzito wa mawimbi baharini.
Chombo kilichoko baharini kina nahodha, na nahodha ndiye kiongozi mkuu, na kila mtu aliyemo ndani ya chombo hicho anamtarajia kuwa atafanya maamuzi yatakayokipeleka chombo hadi pwani. Lakini nahodha lazima awe na masarahangi, wasaidizi wake, wanaomsaidia kuwaongoza mabaharia walio chini yake, na sarahangi hana budi kumshauri nahodha kwa uwazi bila kumchelea.
Masarahangi nao hawana budi kuwasikiliza mabaharia, hata kama ujuzi wa mabaharia wa kawaida unaweza kuwa mdogo sana ukilinganishwa na ujuzi alio nao nahodha au masarahangi wake. Kila mmoja ndani ya chombo, kwa nafasi yake na kwa kiwango kinachokubalika katika mpangilio wa safari, anayo nafasi ya kutoa fikra zake kuhuzu mwenendo wa safari.
Mchakato wa kupeana ushauri kuhusu mwenendo wa safari haufuti madaraka ya mwisho ya nahodha, bali unamjenga, kwa sababu maamuzi yake ya mwisho (na ambayo kila baharia hana budi kuyatekeleza bila ubishi) yanakuwa yametokana na mchango wa fikra za kila mwanamaji aliyemo ndani ya chombo.
Kwa kiasi kikubwa, kama nilivyoeleza awali, TANU, na baada yake, CCM, vilipoteza mwelekeo huu, na kutokana na hilo uongozi wake ukawa unamtegemea kiongozi mkuu ambaye alikuwa habishiwi.
Hakuna shaka moyoni mwangu hata kidogo kwamba Mwalimu Julius Nyerere alikuwa nahodha mahiri na shupavu, mtu mwenye misimamo thabiti na asiyeyumbishwa na jambo lo lote, si tamaa ya mali wala nguvu za mabeberu. Lakini Mwalimu aliiruhusu hali ya kuzungukwa na akina Bwana Ndiyo kiasi kwamba, hatimaye, akajikuta anasikiliza ushauri wake yeye mwenyewe. Ushauri wa aina hii, kama tunaweza kuuita ushauri, ni ushauri tasa, hauzai.
Watu waliomzunguka Nyerere, na ambao walilazimika kukubaliana na kila alichosema na kufanya, si kwamba wote walikuwa watu waovu, au wasiokuwa na akili nzuri. Mazingira walimokuwa yaliwafanya wakubali kukaa kimya hata pale walipoamini kwamba makosa yanafanyika. Wachache waliodiriki kubisha walikiona cha mtema kuni, na waliobaki wakajenga busara ya kukaa kimya.
Tukumbuke, Mwalimu Nyerere, pamoja na uwezo wake mkubwa na ushawishi usio wa kawaida kwa wananchi, hakuwa katili. Hata pale alipowafanya waliompinga kuona cha mtema kuni, hakuna aliyepoteza maisha yake kutokana na msimamo wa kisiasa. Ni kweli, wapo walioumia, waliowekwa kizuizini, waliopelekwa uhamishoni, na wengi waliopoteza ajira. Lakini hakuna aliyekufa kutokana na shughuli hii, na hili si jambo dogo katika Afrika ya wakati huo (na hata ya leo).
Hata hivyo, hali halisi ilijenga kabila zima la wanafiki, watu waliojipendekeza kwa Mwalimu kwa kukubali kila jambo lake bila kubishi na kujitambulisha kama waumini wa dhati wa sera zake. Unafiki huo unadhihirika leo kwa wale ambao bado wamo ndani ya michakato ya kisiasa lakini hawana lo lote la kuwatambulisha na Mwalimu wala sera zake.
Viongozi waliokuja baada ya Mwalimu walirithi hali hii bila kuwa na uwezo wa kifikra wa Nyeyere. Mwalimu aliweza kuyasimamia masuala kadhaa yaliyokuwa na umuhimu mkubwa kwake na kuyafuatilia siku hadi siku, huku akitembelea vijiji na kufanya kazi za sulubu, bega kwa bega na wananchi. Nani atasahau operesheni za Kigoma na Dodoma, kwa mfano?
Wakati wa ujana wake, bado akiwa mwenye nguvu za mwili na uangavu wa akili, Nyerere alitumia muda wake mwingi kuwafundisha na kuwanasihi watu wake, huku akijibidisha kujifunza yeye mwenyewe. Nani amesahau misemo yake, kama Jifunze kusoma, wakati ni huu? Au Mvua za kwanza ni za kupandia? Nani miongoni mwetu tuliokuwapo wakati huo, amesahau maneno yake kuhusu matumizi ya marejea? Sasa tuulizane, nani anayasema maneno haya hivi leo? Ni dhahiri kwamba Mwalimu alikuwa mwalimu.
Lakini kadri alivyoongeza umri na kuanza kuchoka kimwili ( na akili yake kuelemewa na mzigo wa kufikiri kwa niaba ya wote) ndivyo tulivyoona uzee na uchovu wa chama na serikali yake. Maumbile hayaruhusu mtu mmoja kuendelea milele kufanya kazi ya kufikiri kwa niaba ya watu wote. Atachoka tu, na hatimaye atakufa. Haya tumeyaona.
Kwa sababu wakati wa umri wake wa tija alishindwa kujenga chama imara chenye misingi endelevu, kuondoka kwake, kwanza kutoka madarakani na pili duniani, kulikiacha chama kilichochoka kama alivyokuwa kachoka yeye, na tangu hapo hakijaweza tena kurejea taswira yake ya awali. Mwalimu mwenyewe, kama nilivyosema katika sura zilizotangulia, alipata wasaa wa kukichunguza chama chake na kukishangaa jinsi kilivyokuwa kimepoteza silika yake asilia.
Hivi sasa tunakiona chama ambacho hakina mwelekeo wo wote wa kifalsafa, si falsafa ya uhafidhina wala uanamapinduzi. Kwa maneno yake mwenyewe Mwalimu, kimekuwa ni kama dodoki au kokolo, kinameza kila kinachokutana nacho ziwani. Kwa maneno mengine, si chama tena bali ni utaratibu au mpangilio unaoruhusu kundi fulani la wajasiriamali wa aina mahsusi kujikusanya kila baada ya muda fulani kugawana madaraka na kufanya wapendavyo.
Kabla hajatutoka, Mwalimu alisema kwamba ili kuimarisha misingi ya demokrasia nchini, chama alichokianzisha mwenyewe, CCM, kilikuwa hakina budi kugawanyika ili kujenga upinzani wa kweli. Najua wakuu wengi ndani ya chama hicho walimwona kama msaliti, lakini ninaelewa kwamba alingamua kwamba chama hicho kilikwisha kupoteza nguvu ya kifalsafa ya kukifanya kiendelee kuwa kitu kimoja.
Inawezekana vile vile kwamba Mwalimu alijaribu kusababisha mgawanyiko huo lakini akashindwa, jambo ambalo nitalijadili mbele ya safari.
Je, huo mgawanyiko alioutaka Mwalimu utatokea?