Mapema leo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Bw. Freeman Mbowe alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano ulioandiliwa na Kituo cha Demokrasia cha Tanzania uliofanyika kwenye hotel ya Pearl, Ubungo Plaza. Ifuatayo ni hotuba yake aliyoitoa kwa wadau waliokuwa wamekutana kujadilishi sheria ya uchaguzi ya 1992.
HOTUBA YA MGENI RASMI MH. FREEMAN MBOWE, MWENYEKITI WA CHADEMA, KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO WA WADAU WA KUPITIA SHERIA YA VYAMA VYA SIASA YA MWAKA 1992
MAHALI: BLUE PEARL HOTEL, UBUNGO PLAZA
DAR ES SALAAM.
TAREHE: 13 MACHI, 2008.
MH. Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD),
Waheshimiwa Wenyeviti wa Vyama vya Siasa,
Waheshimiwa wawakilishi na wajumbe wa vyama vya siasa,
Waheshimiwa wanataaluma, watoa mada,
Mabibi na Mabwana,
Naomba niwashukuru kwa kunipa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano huu. Pamoja na kazi nyingi nyingine zilizokuwa zimekwisha kupangwa kabla, ofisi yangu na mimi binafsi tumeona ni muhimu kukubali mwaliko wa TCD na kuja kushiriki nanyi katika tukio hili muhimu kidemokrasia na kisiasa kwa manufaa ya taifa letu.
Hii ni kutokana na umuhimu wa suala linalozungumziwa ambalo ni kupitia sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992. Naiomba TCD iendeleze mipango ya kutufanya tukutane mara kwa mara ili kupata mawazo mapya toka kwa wadau yatakayowezesha kuboresha sheria zetu kwa manufaa ya Watanzania wote.
Natambua kuwa, kuwepo kwa sheria inayotoa fursa na nafasi sawa kwa vyama vyote vya siasa ni msingi bora wa kukuza demokrasia nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kama mgeni rasmi, napata wakati mgumu kutoa fikra zangu kuhusiana na sheria ya vyama vya siasa kwani kama wanavyojua wote hapa mimi ni kiongozi wa chama mdau. Hata hivyo, kama Watanzania ni lazima tujipe ujasiri wa kutanguliza maslahi ya Taifa mbele ya maslahi ya vyama na hata maslahi binafsi.
Nina imani kuwa katika mkutano huu wa leo yatajadiliwa na kuazimiwa mambo mengi. Ni rai yangu kuwa ni vizuri kutafuta tena wasaa kuangalia utekelezaji wake, na pia kujikumbusha maazimio ya nyuma. Hii ni kutokana na ukweli kwamba katika kupima utekelezaji wake tunaweza kugundua pia sababu za kushindikana kwa baadhi yake kutekelezwa na hivyo kubuni njia mbadala itakayoharakisha utekelezaji wake.
Ninapenda kwa dhati kabisa kukipongeza kituo hiki cha Tanzania Centre for Democracy- (TCD) na washirika wake kwa kuwezesha fursa hii ambayo inatoa nafasi kwa wadau mbali mbali kufahamu sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992. Aidha, ni fursa ya kuweza kupendekeza maboresho pale yanapohitajika ikizingatiwa kuwa ni miaka 16 sasa tangu sheria hii ipitishwe na tumejifunza mambo mengi kutokana na uzoefu.
Nina hakika ni kiu ya kila Mtanzania anayeitakia mema nchi yetu kuona sheria ya vyama vya siasa inakuwa yenye kutoa haki na demokrasia pana katika uwanja wa siasa nchini mwetu. Kiu hii inachochewa zaidi na ukweli kuwa dira ya Taifa lolote sambamba na viongozi wake huchipukia kwenye vyama vya siasa. Sheria zenye hila hususan za upendeleo hupelekea Taifa kupata viongozi na dira angamizi.
Nchi yetu iliingia katika mfumo wa vyama vingi tena mwaka 1992, lakini pamoja na kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, sheria zetu hazikubadilika vya kutosha kulingana na hali halisi hivyo kutokidhi mahitaji ya chaguzi zilizofuata na zinazoendelea kufanyika ili kutoa fursa sawa au uwanja tambarare wa kisiasa kwa vyama vyote.
Vyama vya siasa tunaunga mkono jitihada za kuwafanya Watanzania kufahamu zaidi sheria mbali mbali na kuweza kutambua umuhimu wake katika utawala na uendeshaji wa nchi. Ni muhimu sana katika mkutano huu mapungufu yote kwa kadiri ya mtazamo wa wadau yakawekwa bayana na kufikishwa serikalini ili kuweza kuzingatiwa.
Mapungufu mengi yaliyopo kwenye sheria iliyopo leo, yamedumaza kwa kiwango fulani kupanuka kwa demokrasia katika nchi yetu. Kama Taifa, naamini hatujavuna kikamilifu faida na fursa ambazo zingeweza kupatikana kwa kuwa na uwanja tambarare wa kazi za siasa nchini mwetu. Ni vyema sasa fursa hii itumike kikamilifu na wanasiasa sasa tusihodhi mchakato wa kujitungia sheria na kuitekeleza.
Ni rai yangu kuwa wadau wengi iwezekanavyo nje ya wanasiasa washirikishwe kwani pamoja na mambo mengine, hatma na ustawi wa nchi yetu itategemea kwa kiasi kikubwa ubora wa sheria hii.
Aidha, ni matumaini yangu kuwa Serikali na hatimaye wabunge wote wataacha ushabiki wa vyama vya siasa na kufanya maamuzi ya busara kuhakikisha sheria hii sambamba na sheria nyingine zote zenye kupoka haki na uhuru wa wananchi kwa njia yeyote ile zinashughulikiwa haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Msingi wa sheria yeyote katika nchi yetu ni Katiba. Upungufu katika katiba hulazimisha au kuhalalisha upungufu katika sheria za nchi. Katiba ya nchi ndiyo msingi wa haki na wajibu wa wananchi na wananchi na taasisi mbalimbali kati taifa letu. Katiba ya nchi ndiyo msingi wa uhuru mbalimbali ambao umma wa watanzania unaweza kufurahia. Hivyo, lazima tujiulize, ni kwa kiasi gani katiba yetu imeweka misingi kamili ya kuweza siasa kufanyika katika nchi yetu na vyama vya siasa kuweza kutimiza wajibu wake kwa taifa. Na tujadili pia ni kwa vipi sheria ya vyama vya siasa izingatie misingi ya kikatiba.
Kama nchi, bila kujali itikadi; tunayo misingi taifa letu ikiwemo uhuru, umoja na usawa. Hivyo, ni lazima marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa tunayoyapendekeza lazima yahakikishe sheria mpya inalinda uhuru, usawa na umoja. Sheria ya vyama vya siasa ilinde uhuru wa vyama vya siasa na wanasiasa; lakini pia ilinde uhuru wa msajili wa vyama vya siasa. Sheria ya vyama vya siasa lazima iweke usawa katika uwanja wa kisiasa ikiwemo usawa katika rasilimali za kufanyia siasa. Sheria ya vyama vya siasa lazima iendelee kulinda misingi ya umoja katika taifa letu.
Chama cha siasa ni muungano wa watu wenye madhumuni ya kuchukua dola kupitia uchaguzi na kutekeleza malengo mbalimbali ya uchaguzi. Sheria ya vyama vya siasa inatoa mwongozo wa kutekeleza wajibu huu. Lakini hatma ya utekelezaji wa wajibu huu, ni uchaguzi; ambao unasimamiwa na sheria nyingine; sheria ya uchaguzi. Hivyo, hata tukitengeneza sheria nzuri namna gani ya vyama vya siasa; kama hatutarekebisha sheria zetu za uchaguzi, dhamira ya mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa haiwezi kutimia. Napenda kuchukua fursa hii kutoa rai kwa mamlaka zinazohusika kuanzisha mapema iwezekanavyo, mchakato wa kuzifanyia marekebisho sheria zetu za uchaguzi.
Ubora wa Katiba utatupa misingi bora ya taifa; ubora wa Sheria ya vyama vya siasa unawezesha vyama vya siasa kuweza kupata viongozi bora; ubora wa sheria ya uchaguzi; utatuwezesha kama taifa kupata viongozi bora katika ngazi zote. Uongozi bora utatuwesha kupambana na ufisadi na kusimamia rasilimali za taifa na hatimaye kuongeza kasi ya kuleta maendeleo Tanzania. Napenda kila mshiriki wa mkutano huu aone umuhimu wa kutoa mawazo yake bila kujali itikadi ya chama fulani kwa nia ya kuboresha sheria hii kwa manufaa ya Watanzania wote kwa ujumla.
Aksanteni wote na nawatakia mkutano mwema na wenye mafanikio.