Si magari yake tu, tunamtaka pia Zitto
Fidelis Butahe na Elizabeth Ernest
MWENYEKITI wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia amesema chama hicho hakihitaji msaada wa magari pekee kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe bali pia kinamhitaji yeye kujiunga nacho.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mbatia alisema licha ya msaada wake wa magari, Zitto akitaka kujiunga na NCCR-Mageuzi wanampokea kwa mikono miwili.
“Wapinzani tuna lengo moja kubwa; kuing’oa CCM sasa kama Zitto katoa magari kwa Kafulila (David) ubaya uko wapi? Sio magari tu hata yeye akija NCCR- Mageuzi, hii ndio demokrasia tunayoizungumzia,†alisema Mbatia na kuongeza;
“Zitto ameona kuwa Kafulila ana uwezo wa kuwawakilisha wananchi wa Kigoma Kusini bungeni, umefika wakati wapinzani tukapeana nafasi na kusaidiana kama hivi hii ndio demokrasia, huyu Zitto anaweka maslahi ya Watanzania mbele kuliko ya chama na hivyo ndivyo inavyotakiwaâ€
Alisema kuwa chama chake hakina kinyongo na kiongozi huyo wa Chadema na kwamba kinamkaribisha muda wowote akitaka kujiunga nacho.
Naye Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema kuwa Zitto kumsaidia Kafulila ni jambo la kawaida na kusisitiza kuwa mbona Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kumpigia kampeni mgombea wa NCCR-Mageuzi Jimbo la Musoma Vijijini mbona hilo haliongelewi.
''Mwalimu Nyerere aliwahi kumpigia kampeni mgombea wa NCCR-Mageuzi , Balozi Paul Ndobho na kuwaambia wapiga kura kuwa wasimchague mgombea wa CCM kwa kuwa alikuwa hafai hivyo wamchague wa upinzani hilo Chadema vipi hawalioni,'' alisema Mrema na kuongeza;
''Unajua wapinzani lengo letu ni moja kwa hiyo tunapokuwa na urafiki wakati tuko vyama tofauti na kusaidiana kwa vitu vidogo kama magari na fedha kwa ajili ya kampeni hilo ni jambo la kheri, ndio umoja wa wapinzani huo,''
Alisema siasa za Zitto ni zaidi ya chama alichokuwa na kusisitiza kuwa mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini ni kiongozi ambaye chama chochote kinaweza kumshawishi ajiunge nacho kutokana na tabia yake ya kujali na kuipenda demokrasia.
“Sisi TLP tulikuwa tukimtaka sana Zitto ajiunge katika chama chetu, siasa zake ni zaidi ya Chadema, hata mimi nilipokuwa nikipata matatizo yeye peke yake kutoka Chadema ndio alikuwa akinitafuta na kunijulia hali na yeye mpaka kesho anapigania niwe Mbunge wa Vunjo,†alisema Mrema ambaye ametangaza kuwania ubunge Jimbo la Vunjo.
Jana kulikuwa na taarifa za uhakika za Zitto kutangaza kuwa atamuunga mkono swahiba wake, David Kafulila kugombea ubunge Jimbo la Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi na tayari ametoa magari matatu kwa ajili ya kumsaidia kujiimarisha jimboni huko.
Vyanzo vya habari vilidokeza kuwa kiongozi huyo wa Chadema ameamua kumuunga mkono Kafulila ili kuhakikisha jimbo hilo linaondoka mikononi mwa CCM na kubaki upinzani.
Katika Uchaguzi Mkuu w 2005, NCCR-Mageuzi ilishika nafasi ya pili huku Chadema ikishika nafasi ya tatu kwenye matokeo ya ubunge. Katika uchaguzi wa mwaka 2000, jimbo hilo lilichukuliwa na NCCR-Mageuzi kabla ya 2003 kuchukuliwa na CCM katika uchaguzi mdogo.
Katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa hivi karibuni, Chadema ilijizolea viti 12, NCCR-Mageuzi 11 na CCM ilipata viti 20. Kulingana na takwimu hizo, upinzani uliongoza.
Mwaka 2005 kama Chadema ambacho kilishika nafasi ya tatu kingeiunga mkono NCCR-Mageuzi, Jimbo hilo sasa lingekuwa katika mikono ya upinzani kwa kuwa kura za kambi hiyo zilikuwa nyingi kuliko za CCM.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Zitto anaamini kwamba, Kafulila ndiye aliyejenga Chadema kama chama ikiwa ni pamoja na kuimarisha mahusiano na NCCR-Mageuzi katika maeneo ambayo chama hicho kina nguvu.
“Zitto amekwisha weka bayana kuwa katika Uchaguzi Mkuu ujao upande wa jimbo hilo anamuunga mkono Kafulila kwa kuwa anaamini atashinda na kuimarisha upinzani,†kilisema chanzo cha kuaminika.
Maelezo hayo ya Kabwe yamekuja huku Kafulila akijiandaa kwenda jimboni humo kuhutubia mikutano ya hadhara akitumia magari ya Zitto katika ziara yake mkoani Kigoma itakayoanza Desemba 8, mwaka huu akiwa na viongozi wa kitaifa wa NCCR-Mageuzi.
Kafulila aliliambia gazeti hili jana kuwa atatumia magari ya Zitto kwa kuwa ni rafiki yake wa karibu.
''Mimi na Zitto ni marafiki wa siku nyingi, tayari nimezungumza naye na amekubali kunisaidia kama rafiki yake wala sijakodisha," alisema Kafulila juzi na kuongeza:
"Amenipa magari yake kwa ajili ya usafiri kwa sababu nitaondoka na watu wangu huku Dar kwenda Kigoma''.
Alifafanua kuwa jambo kubwa analokwenda kufanya Kigoma ni kuwaeleza wanachama wa Chadema sababu zilizomwondoa kwenye chama hicho na hatima yake kisiasa.
source; http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=16383