HOFU kubwa imetanda jijini hapa baada ya kundi la wafanyabiashara ndogo maarufu kama Wamachinga, kuvamia mitaa na kufanya fujo, huku wakitaka wafanyabiashara wenye maduka kufunga biashara zao.
Fujo hizo zilizofanyika juzi zilikwenda sambamba na kurusha mawe na kuzuia magari kupita maeneo walimopita wao wakiwa njiani kwenda ofisi za Mkurugenzi wa Jiji. Hali hiyo ilitokana na hasira waliyokuwa nayo, baada ya kuondolewa kwenye maeneo waliyopangiwa juzi kuuzia bidhaa zao.
Tafrani hiyo ilianza saa tatu asubuhi baada ya askari wa mgambo wa Jiji wakishirikiana na polisi, kuwaamuru Wamachinga hao kufunga biashara zao, jambo ambalo awali walitii.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye, upepo uligeuka kwani Wamachinga hao walipita madukani na kuwaamuru wenye maduka kuyafunga au wajiandae kwa vurugu.
Wamachinga hao walidai, kwamba walitaka haki sawa itendeke kwa kufunga biashara zote, badala ya kuzuia watu wa kada fulani huku wengine wakiachwa wafanye shughuli zao, hasa wenye biashara ya maduka.
"Tunasema lazima waturudishe maeneo yetu tuliyopangiwa juzi na Mkuu wa Mkoa Abbas Kandoro, ni kwa nini Jiji watuondoe? Mpaka kieleweke," walisikika Wamachinga hao wakisema huku kundi kubwa likipita Barabara ya Nyerere kuelekea Barabara ya Nkrumah.
Madai ya Wamachinga hao ya kutaka warudishwe Makoroboi, Miti Mirefu na Mirongo yalipingwa na Mkurugenzi wa Jiji, Wilson Kabwe, akisema lazima wahame maeneo hayo kwa kuwa yako katikati ya Jiji.
Jana wakitembea mguu kwa mguu na Kandoro, Meya wa Jiji la Mwanza, Josephat Manyerere na wakuu wengine wa idara walibaini maeneo yanayofaa na kuwapangia Makoroboi, Vitunguu Soko Kuu, karibu na Nyumba ya kulala wageni ya Zimbabwe na Mirongo Community Centre.
Hata hivyo, Kabwe alishikilia msimamo kuwa, mwenye mamlaka ya kupanga wafanyabiashara hao ni ofisi yake na si ya Mkuu wa Mkoa au Wilaya.
Alisema ni marufuku wafanyabiashara hao kufanyia biashara zao katikati ya Jiji akiwataka kuhamisha mara moja vizimba vya biashara zao na kwenda maeneo waliyopangiwa kisheria.
Hadi gazeti linaondoka ofisi za Mkurugenzi wa Jiji Wamachinga hao wapatao 500 walikuwa wakitaka kuuona uongozi wa halmashauri, ili washinikize kurudishwa kwenye maeneo walikoondolewa.