Mlipueni na fisadi Mkapa na mafisadi wengine wote wanaohusika na wizi wa shilingi bilioni 288 toka BOT, badala ya kumlipua fisadi mmoja mmoja
Posted Date::5/30/2008
Wabunge wa CCM kumjadili aliyekuwa waziri Chenge
*Ni kuhusu tuhuma za kumiliki mabilioni,wajipanga kumlipua bungeni
Na Ramadhan Semtawa
Mwananchi
TUHUMA zinazomkabili Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge kuhusiana na mabilioni ya shilingi aliyoyaficha kwenyea akaunti yake moja katika Kisiwa cha Jersey, zinatarajiwa kutikisa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho bungeni.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti hii limezitapata, Kamati ya Uongozi ya CCM bungeni inayoundwa na wajumbe wote wa Kamati Kuu (CC), akiwemo Waziri Mkuu intakutana mara baada ya Mkutano wa Bunge la bajeti kuanza mjini Dodoma Juni 11, mwaka huu kujadili masuala kadhaa likiwemo la tuhuma za Chenge kuficha fedha nje ya nchi.
Taarifa hizo zinadai kuwa baadhi ya wajumbe hao pamoja na kusubiri matokeo ya uchunguzi Taasisi ya Kuchunguza, Kukamata na Kufungua Mashitaka ya Makosa Makubwa ya Jinai (Serious Fraud Office) ya Uingereza, watataka kujua Chenge aliztoa wapi Sh1.2 bilioni.
Inadaiwa kuwa wabunge pia wamekerwa na kauli alizota Chenge kabla ya kujiuzulu kwani alionekana kufanya hivyo baada ya shinikizo kubwa ikiwemo la vyombo vya habari.
Taarifa hizo ziliongeza kwamba, baadhi ya wabunge hao wanahoji kwamba, inawezekana vipi mtu ambaye alikuwa mtumishi wa umma ajilimbikizie kiasi hicho kikubwa cha fedha katika akaunti moja, tena ya kificho.
Chanzo hicho habari kilifahamisha kwamba, baadhi ya wabunge watasubiri hotuba ya Waziri Mkuu, kuona kama atagusia suala hilo ama la.
''Wabunge wanataka kujua vipi mtu aliyekumbwa na tuhuma nzito za ufisadi ajiuzulu kwa shinikizo,'' kilisema chanzo hicho na kuongeza:,
''Hadi aandikwe sana na magazeti ndiyo afikirie kujiuzulu. Mimi ni mmoja wa wabunge watakaotumia jukwaa hilo kumlipua,'' alisema Mbunge mmoja kwa sharti la kutotaja jina.
Mbunge huyo ambaye siku za karibuni amejijengea umaarufu mkubwa kwa kukemea ufisadi kwa nguvu akiwa bungeni, alisema haiwezekani suala la Chenge likaasha kimya kimya.
Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wabunge ambao wanaonekana kuwa wakali bungeni katika mambo ya ufisadi, walipoulizwa katika ofisi ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam jana, walithibitisha kuwa jukwaa lao ni bungeni.
"Mimi siwezi kuzungumzia suala hili juu juu, nina 'forum' (jukwaa) ambayo ni Bunge, hivyo tusubiri, lakini nitamlipua," alisema Mbunge mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake litajwe gazeni.
Hilo likitarajiwa kutikisa kamati hiyo na hata baadhi ya wabunge kupanga kumlipua Chenge bungeni, Gavana wa Benki Kuu (BoT) Profesa Benno Ndulu, aliliambia gazeti hili, jana kwamba benki hiyo inasimamia sheria kuhusu uwekaji fedha nje si mtu.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa wa CCM, ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, Kapteni John Chiligati, alimtaka mwandishi awasiliane na Katibu wa Kamati hiyo, Ali Ameir Mohamed ambaye ni Mbunge wa Donge (CCM).
"Mimi ni mjumbe tu sijajua ajenda za kamati katika mkutano huu kamati hiyo, ni vema ukamuuliza Katibu wake ambaye ni Ali Ameir," alisema Chiligati.
Alipoulizwa kwamba, kuwa anachukuliaje suala hilo na uwezekano wa kulifikisha katika kamati hiyo, alijibu tena, " nafikiri Katibu ndiye anayejua hilo."
Naye Ameir, alipoulizwa alisema hadi sasa hakuna ajenda kikao hicho iliyoandaliwa kwani kwa utaratibu wa sasa, kikao pia kinategemea mapendekezo kutoka kwa wajumbe.
"Hadi sasa sijaanda ajenda hata moja, ajenda zetu sasa hivi pia zinatokana na mapendekezo ya wajumbe wa kamati na tunatarajia kukutana baada ya kuanza mkutano wa Bunge mjini Dodoma," alisema na kuongeza
"Ajenda ya mjumbe ikifika hapa huangaliwa na ikikubalika hujadiliwa ndani ya kamati".
Alifahamisha kwamba, baada ya kamati ya uongozi kupitisha, ajenda hupelekwa kwa wabunge wote wa CCM.
Wakati Ameir na Chiligati wakisema hivyo, duru kutoka ndani ya kamati hiyo, zilisema sakata la Chenge ambaye pia ni mjumbe wa CC limegusa baadhi ya wajumbe wa kamati na wabunge wengine wa CCM ambao wanataka lijadiliwe kwa kina.
Hayo yakiwa ndani ya CCM, Gavana wa Benki Kuu (BoT) Profesa Ndulu alifafanua kwamba Bbenki inasimamia sheria na si kumjadili Chenge.
Alisema hadi sasa suala la Chenge linachunguzwa na kuongeza kwamba, BoT haiwezi kumjadili mtu badala ya kusimamia sheria.
"Sisi tunasimamia sheria, hatuangalii mtu mtu akibainika hatumjadili yeye bali sheria, sasa hili suala jana (juzi) tumelizungumza kisheria lakini watu wanataka kujadili mtu, kuna uchunguzi unafanyika,"alisema Ndulu.
Chenge ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa miaka kumi na kujiuzulu akiwa Waziri wa Miundombinu, anachunguzwa na SFO kuona kama Sh1.2 bilioni anazomiliki kisiwani Jersey, zina uhusiano na ununuzi tata wa rada.
SFO inamchunguza Chenge kuona kama mabilioni hayo ambayo mwenyewe huita 'vijisenti', yana uhusiano na biashara ya kifisadi ya rada kati ya Kampuni ya BAE System na serikali ya Tanzania katika kipindi cha mwaka 2002.
Hata hivyo, mwenyewe alisema ni vema watu wakasubiri uchunguzi wa SFO ambao sasa uko katika hatua za mwisho.