Nani aliwaambia Ikulu kwamba ni rahisi kumchunguza mshika mkoba wa mafisadi? 😕
Posted Date::5/27/2008
Ikulu: Ni kazi kubwa kumchunguza Chenge
* Simba asema taarifa kamili baada ya siku mbili
* Chenge arejea kimya kimya kutoka Uingereza
Na Muhibu Said
Mwananchi
SERIKALI imesema uchunguzi wa tuhuma za kumiliki dola za Marekani 1 milioni (zaidi ya Sh1.2 bilioni) kwenye akaunti ya aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, iliyoko katika Kisiwa cha Jersey, bado unaendelea kwa vile ni kazi kubwa kuufanya.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba, alisema jana kuwa kutokana na hali hiyo, ni vema vyombo vya uchunguzi vikaachwa ili vikamilishe kazi yake.
"Kifupi, uchunguzi unaendelea. Tusubiri kazi iendelee. Ni kazi kubwa, tuviache vyombo" alisema Waziri Simba alipoulizwa na mwandishi wa Mwananchi jana.
Hata hivyo, Waziri Simba alisema atakuwa na taarifa kamili kuhusu suala hilo baada ya siku mbili, kuanzia jana.
Chenge ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), anachunguzwa na Taasisi ya Kuchunguza Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza, ijulikanayo kwa jina la Serious Fraud Office (SFO).
Hivi karibuni Chenge aliondoka nchini kuelekea Uingereza na tayari amesharejea nchini.
SFO inamchunguza Chenge, ili kubaini kama fedha anazodaiwa kuzimiliki katika kisiwa hicho, zina uhusiano wowote na zile zinazoaminika kutolewa kwa njia ya rushwa wakati Tanzania iliponunua rada ya kijeshi kutoka Uingereza kwa Paundi za Uingereza milioni 28 (Sh70 bilioni), mwaka 2002.
Biashara ya ununuzi wa rada hiyo, ilifanywa kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza.
Waziri Simba alisema uchunguzi kuhusu biashara ya ununuzi wa rada hiyo, nao unaendelea.
Tuhuma dhidi ya Chenge za kujilimbikizia fedha hizo, ziliibuliwa na Gazeti la The Guardian la Uingereza katika toleo lake la Aprili 12, mwaka huu ambalo lilieleza kuanza kwa uchunguzi dhidi yake, kutokana na akaunti yake kukutwa na kiasi hicho cha fedha.
Wiki chache, baadaye serikali ilisema Chenge anachunguzwa na vyombo mbalimbali vya kitaifa na kimataifa, ili kubaini kama ana kesi ya kujibu mahakamani, kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.
Katika taarifa hiyo, Waziri Simba alisema kama serikali itajiridhisha kuwa Chenge ana kesi ya kujibu, atafikishwa mahakamani ambako mambo yote yatajulikana.
Awali, Waziri Simba alipoulizwa na mwandishi wa Mwananchi anachukuliaje taarifa za waziri kumiliki fedha nyingi kiasi hicho, alijibu: "Hata mimi nashangaa kama wewe, kama alizipata kihalali au la."
"Lakini kuna mtu nimemwambia, labda kauza ng'ombe wao wote ndio alipata hizo pesa, au ana biashara nyingine," alisema Waziri Simba.
The Guardian katika habari yake hiyo iliyowekwa katika mtandao wa intaneti, liliripoti kuwa taarifa hizo zinakuja ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), kwa kushirikiana na SFO na taasisi za uchunguzi za Uswisi na Jersey zilipoanza kuchunguza kuhusu kashfa nzima ya ununuzi wa rada.
Gazeti hilo lilimkariri Chenge, akikiri kwamba fedha hizo ni mali yake na akatumia fursa hiyo kukanusha kuwapo kwa uhusiano wowote, kati ya fedha hizo na kashfa ya ununuzi wa rada, uliofanywa wakati yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), katika serikali ya awamu ya tatu.
Septemba 15, mwaka jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, walimtaja Chenge katika orodha ya vigogo 11, wakiwamo viongozi kadhaa wa serikali nchini kuhusika na ufisadi wa mabilioni ya shilingi za walipakodi.
Baadaye, Septemba 19, Waziri Chenge aliliambia gazeti hili kuwa walioibua hoja ya ufisadi dhidi ya viongozi wa serikali kama wakipata au kama wana ushahidi, yeye binafsi anatoa ruksa waupeleke katika vyombo vya dola ili ufanyiwe kazi.
Chenge alisema hapendi malumbano, isipokuwa yote yaliyozungumzwa atahitaji kuyaona kwa maandishi na uonyeshwe ushahidi wa yeye kuhusika moja kwa moja na ufisadi uliotajwa.
Aprili 17, mwaka huu, alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JNIA), Chenge aliwaambia waandishi wa habari kuwa tuhuma za Sh 1 bilioni anazodaiwa kumiliki katika akaunti Uingereza, ni za "vijisenti".
Alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya kuziita vijisenti Sh1.2 bilioni, alisema: "Kila mtu ana viwango vyake na ana haki ya kusema anavyotaka. Na mtu akikutuhumu, unajua nafsini mwako".
Hata hivyo, siku mbili baadaye, Chenge alikaririwa na vyombo vya habari akiwaomba radhi Watanzania kutokana na kauli yake hiyo, akisema kuwa ilitokana na kuathiriwa na kabila lake la Kisukuma.
Siku chache baadaye, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu, alikaririwa na vyombo vya habari akitangaza kuhusu uamuzi wa Chenge wa kujiuzulu Uwaziri wa Miundombinu, uliopongezwa na Rais Jakaya Kikwete kwamba, ni jambo pekee alilokuwa akilitegemea kutoka kwa Chenge.