Lipumba amshika pabaya Ben Mkapa
na Charles Mullinda
VIONGOZI wa vyama vitano vya upinzani, wamesema wana wasiwasi na utetezi uliokuwa ukitolewa na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, katika ununuzi wa rada iliyoibua kashfa nzito nchini Uingereza.
Wamesema Mkapa anapaswa kueleza anachokijua kuhusiana na ununuzi wa rada hiyo ili ajisafishe machoni mwa Watanzania na jumuiya ya kimataifa kama hakuhusika katika amana hiyo.
Wamemtaka atangaze mali alizochuma kwa muda wa miaka kumi, kipindi alichokuwa madarakani kama alivyofanya wakati akiingia madarakani ili Watanzania wajue utajiri alionao sasa, ili ulinganishwe na mali alizoingia nazo madarakani.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliotanguliwa na maandamano ya kulaani ununuzi wa rada hiyo jana, katika viwanja vya jangwani, Dar es Salaam, viongozi hao, walisema Mkapa alitetea kwa nguvu ununuzi wa rada hiyo na kueleza kwamba tenda yake haikuwa na chembe ya rushwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema ya kuwa wakati wa mchakato wa ununuzi wa rada hiyo, wananchi, vyama vya upinzani na nchi wahisani walipinga kununuliwa kwa rada hiyo, lakini hawakufanikiwa kwa sababu Mkapa aliziba pamba masikioni.
Wahisani, wananchi na vyama vya upinzani vilipinga kununuliwa kwa rada hii, lakini Rais Mkapa akiwa Australia alitetea inunuliwe na kueleza kuwa mpango mzima haukuwa na chembe ya rushwa.
Sasa imebainika kuwa rushwa iligubika mpango mzima, tunataka kujua kama Mkapa hakuhusika na rushwa hii, ni vizuri ajitokeze awaeleze Watanzania kwa nini alitetea sana inunuliwe!
Pia tunataka atangaze mali zake kama alivyofanya wakati akiingia madarakani, alipoutangazia umma kuwa ana nyumba moja hapa Dar, moja Masasi, miche 100 ya korosho na shamba ambalo halijaendelezwa nje ya jiji la Dar es Salaam, tunataka kujua baada ya miaka 10 ya urais amechuma mali kiasi gani ili tulinganishe na ile aliyoingia nayo madarakani.
Tunasema hivi kwa sababu kashfa hii ilitokea wakati wa Awamu ya Tatu aliyokuwa akiiongoza, na pesa iliyoibiwa ni nyingi mno, kwa vile baada ya kuachia madaraka aliwaomba radhi Watanzania kuwa wamsamehe kwa aliyowakosea, itakuwa vizuri kama atatusaidia kuzirejesha nchini hizo sh bilioni 15, alisema Lipumba.
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour, Augustine Mrema, alisema mwaka 1991 ndipo alianza kujua jinsi Tanzania inajengwa na wenye moyo na inavyoliwa na wenye meno.
Alisema katika kipindi cha utawala wa Awamu ya Tatu aliandamwa na kesi nyingi ambazo maelekezo ya kuziendesha yalikuwa yakitoka Ikulu, lakini alifanikiwa kujinasua kwa sababu alikuwa na kinga iliyotolewa na Bunge ya kutoshitakiwa.
Baadhi ya wanakamati wa kamati ya Bunge iliyokuwa ikisikiliza kesi yake ya kuwahutumu baadhi ya vigogo wa serikali kuhongwa sh milioni 900 walizadiwa vyeo mbalimbali, ukiwamo uwaziri na Rais mstaafu Mkapa.
Alisema vyeo hivyo walipewa baada ya kumkingia kifua Mkapa ili asihojiwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na alikuwa amemtaja katika sakata hilo.
Viongozi wengine wa vyama vya upinzani waliounga mkono maneno ya Lipumba na Mrema, ni Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Shaibu Akwilombe.
Kadhalika, viongozi hao walimshangaa Rais Jakaya Kikwete kutokasirishwa na taarifa za kuwapo kwa rushwa katika ununuzi wa rada na kueleza kuwa hatua yake hiyo inatia shaka.
Mwenyekiti wa UDP, Cheyo, alisema alitegemea kusikia Rais Kikwete akitoa kauli ya kukasirishwa na taarifa za kuwapo kwa rushwa katika ununuzi wa rada, lakini anamshangaa kusema kuwa aibu hiyo ni ya Waingereza.
Nilitegemea kumsikia Rais Kikwete akisema amekasirishwa na tuhuma za kuwapo kwa rushwa ya sh bilioni 15 katika ununuzi wa rada hiyo, fedha ambazo zilifaa kwenda kwenye ujenzi wa shule, ajabu anasema hiyo ni aibu ya Waingereza.
Ninawaomba Watanzania wamuonyeshe Rais Kikwete kuwa wamekasirishwa na rushwa hii, tofauti na yeye. Kama Wazungu wameweza kumkarisha chini Brair ambaye nchi yake imechukua pesa za Watanzania maskini, kwa nini sisi tusikasirike? alihoji Cheyo.
Alionya kuwa kitendo cha Rais Kikwete kutokerwa na ufisadi unaofanywa na baadhi ya watu, kitaipeleka nchi pabaya na itabaki kuwa tegemezi milele.
Mrema yeye alimponda Rais Kikwete kuwa kazi kubwa anayoweza kuifanya kwa ufasaha ni kutembelea wagonjwa hospitali na wafungwa gerezani.
Hatutaki rais mzuri, uzuri wake unatusaidia nini? Anacheka cheka tu, anakwenda hospitali kutembelea wagonjwa, anawaombea wapone, hivi tulimchagua kuombea wagonjwa? Rais huyu ni sheikh? Kama kweli ni mwanamume arejeshe hizo sh bilioni 15 ziliporwa, alisema Mrema aliyezungumza kwa hisia kali jana.
Alisema kwa mujibu wa uchunguzi alioufanya amegundua rada hiyo ilinunuliwa kwa shinikizo la Serikali ya Marekani ambayo Tanzania sasa ni mshirika wake wa karibu.
Mrema alisema kuwa Marekani iliishinikiza Tanzania kununua rada hiyo ili kuweza kuona sehemu zote za Afrika Mashariki pamoja na Pembe ya Afrika, lengo kuu likiwa kupambana na ugaidi.
Alishangaa kuwa Tanzania imekubali kutekeleza masilahi ya Marekani kwa kutumia pesa za Watanzania ambao ni masikini wa kutupwa tofauti na wananchi wa Marekani.
Naye Prof. Lipumba alisema kashfa ya rada iko wazi na Rais Kikwete anapaswa achukue hatua za haraka kuwashughulikia wote waliohusika na kashfa hiyo ili wananchi wasimnyoshee kidole kuwa na yeye alihusika katika mpango huo.
Akizungumzia historia ya mpango wa kununuliwa kwa rada hiyo, Profesa Lipumba alisema mpango mzima ulianza kupangwa mwaka 1995 lakini viongozi waliokuwa wakihusika waliogopa kuutekeleza kwa kumuhofia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14, mwaka 1999.
Waliogopa kwa sababu walijua kuwa angeupinga kwa nguvu, alisema Profesa Lipumba.
Alisema baada ya kufa kwa Mwalimu mwaka 1999, mpango huo ulianza kutekelezwa na alidai kwamba dola milioni nane za Marekani ziliwekezwa kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mpango huo.
Profesa Lipumba alisema kwamba ingawa viongozi waliohusika walijua kuwa rada hiyo ina teknolojia ya kizamani na ilikuwa imeshindwa kununuliwa popote duniani kutokana na ubovu iliokuwa nao, waliendelea na mpango huo bila kujali madhara hayo.
Mimi baada ya kujua mpango huo nililiandikia barua Bunge nikiliomba lizuie ununuzi wa rada hiyo, lakini Waziri wa Fedha wa wakati huo alinijubu kuwa pilipili iliyoko shamba inakuwashia nini?
Bi Claire Short wa Uingereza naye kwa kutambua ubovu wa rada hiyo na kuwaonea huruma Watanzania alipinga kwa nguvu kununuliwa kwake na akasafiri hadi hapa nchini, akakutana na Mkapa ili am-support kupinga kununuliwa rada hiyo.
Ajabu Mkapa alisema Watanzania wanataka rada hiyo hiyo, akaishiwa nguvu, rada ikanunuliwa, kamisheni iliyotengwa kwanza ilikuwa asilimia moja lakini dili lilipofanikiwa ikawa asilimia 30, alisema Profesa Lipumba.
Alionya kuwa mipango yote inayofanywa na serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya BAE System na wakala wake aliyeko Jijini Dar inapaswa kuchunguzwa ili kujua pesa ya Watanzania iliyopotea.
Aliitaja baadhi ya mipango hiyo kuwa ni pamoja na ununuaji wa ndege ya rais na mpango unaoendelea sasa wa kununua helikopta.