Rostam akanwa
2008-07-10 11:47:37
Na Lucy Lyatuu na Simon Mhina
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, limemkana Mbunge wa Igunga Bw. Rostam Aziz na kusisitiza kwamba, hana usafi kama alivyojitapa kwamba amesafishwa na kanisa hilo.
Aidha, Kanisa hilo limesikitishwa na kukanusha matamshi yake ya kulisifu kanisa kwa kutambua usafi wake kutokana na tuhuma za ufisadi zinazomkabili.
Taarifa ya KKKT iliyotolewa jana na kusainiwa na Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Balozi Richard Mariki, ilisema, kanisa halikuwa na taarifa ya ujio wa mwanasiasa huyo katika Usharika wa Kinondoni.
Taarifa hiyo ilisema kanisa limegundua kwamba, Bw. Rostam, alialikwa na kikundi kidogo ndani ya usharika huo ambacho hakikuwa na mamlaka ya kumwalika.
``Tunasikitika kusema kwamba, kanisa halikuwa na taarifa ya ujio wa Bw. Rostam na tunapenda kuwaarifu kuwa, taratibu za kuwaalika wageni kwenye shughuli za kikanisa, hazikufuatwa,`` ilisema taarifa hiyo.
Kanisa hilo limetoa taarifa hiyo kuafuatia kikao cha dharura cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi hiyo kilichofanyika juzi jijini Dar es Salaam, ambapo kilijadili kwa kina taarifa zilizoandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu Bw. Rostam, kutembelea Usharika wa Kinondoni.
Taarifa hizo zilihusu madai ya Bw. Rostam, akipongeza KKKT kutambua usafi wake kutokana na tuhuma za kashfa za ufisadi zilizotolewa dhidi yake kwa nyakati tofauti.
Alinukuliwa akisema hayo katika uzinduzi wa kanda za kwaya ya Amkeni iliyopo chini ya Usharika wa Kinondoni.
Aidha, taarifa hiyo ilisema kuwa madai yaliyotolewa na Bw. Rostam, hasa ya kudai kanisa limetambua usafi wake, si sahihi na nipotofu.
``Kutokana na ukikukwaji wa taratibu hizi hayo madai yaliyonukuliwa katika vyombo vya habari kwamba ujio wa Bw. Rostam katika usharika wa Kinondoni na tafsiri ya ujio huo kuwa Kanisa linatambua usafi wake si sahihi na nimadai potofu,`` ilisema sehemu moja wapo ya taarifa hiyo.
Ilisema kanisa hilo haliruhusu sharika zake zitumike kama jukwaa la kisiasa la kujisafisha au kuwasafisha mafisadi.
Badala yake ilisema KKKT imekuwa mstari wa mbele katika kupinga na kukemea mambo ya ufisadi na linaunga mkono juhudi zote za kuutokomeza uovu huo.
Kufuatia ujio huo batili wa Bw. Rostam katika kanisa hilo, KKKT imewaomba radhi waumini wake, wananchi na wale wote wenye mapenzi mema ambao kwa namna moja au nyingine wamekwazwa na tukio hilo.
``Jukumu la kanisa ni kuokoa roho za watu, na si kukumbatia mafisadi na wala rushwa,``ilisema.
Taarifa hiyo iliongeza kwamba, kuanzia sasa, kanisa litachukua tahadhari kubwa kuhakikisha kuwa jambo kama hilo halitokei tena.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Bw. Rostam alikiri kusikia habari za KKKT kumkana na kumkandia.Hata hivyo, alisema kwa vile habari hizo hajazipata rasmi, apewe muda ili aweze kutafakari kwanza.``Hilo ni jambo zito kidogo, ngoja nipate muda wa kutafakari,``alisema.
Jumapili iliyopita, Bw. Rostam alitembelea kanisa hilo na kushiriki katika uzinduzi wa kanda za kwaya ya Amkeni na kutoa msaada wa Shilingi milioni tano, seti ya vyombo vya muziki na jenereta lenye thamani ya Sh. milioni 2.6.