~ UCHAGUZI wa MOYO - 5 - "furaha ya mshindi"~

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,339
38,982
Na. M. M. Mwanakijiji

Kutangaza Nia

Kutangaza Nia

"Mwangaluka wa mayo!"
"Mwangaluka! Mhole mola?"
"Mola duhu"
"Mliho?"
"Tuli mhola"

Stanley alikuwa anaangalia kutoka dirisha la chumbani kwake kwenye uwanja wa nyumba yao pale kijijini. Ilikuwa ni nyumba ndogo ya vijana iliyokuwepo pembezoni mwa nyumba kubwa ya marehemu Mwalimu Maduku. Familia ya Maduku ikiwa imeshikamanishwa na mjane wa marehemu ilikuwa bado inaishi kwenye nyumba hiyo na kuendelea na maisha kama kawaida lakini bado pakijulikana zaidi kama kwa Mwalimu Maduku. Mama Eliza Maduku naye alikuwa ni mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi pale kijijini, alichukua nafasi iliyoachwa na marehemu mumewe. Stanley alijaribu kuangalia kwa shauku kubwa ni msichana gani aliyekuwa amepiga magoti kumsalimia mama yake Jumamosi ile asubuhi.

Hakuweza kumuona vizuri kwani yule binti alikuwa amempa ubavu huku sura yake ameingausha chini akizungumza kwa heshima na mama Maduku. Aliinuka chumbani mwake na kuinua shingo yake kwa nguvu zaidi kama mtua nayetaka kushuhudia tukio ambalo asingependa kumpita. Hakumfahamu binti yule mara moja lakini alihisi kwa asilimia mia moja kuwa alikuwa anamfahamu japo sura ilikuwa bado ni ngeni kutoka upande aliokuwa anamuangalia. Mara yule binti akainuka taratibu na kuendelea na safari yake akimalizia kumuaga mwalimu Eliza.

Stanley alishindwa kujizua alitoka chumbani kwake huku akiwa anamalizia kuvaa shati lake na kwenda moja kwa moja barazani ambako mama yake alikuwa anamalizia kumwagilia bustani yake ya maua mbele ya nyumba yake. Jua lilikuwa ndio limetoka lakini lilizibwa na mawingu ya asubuhi yaliyokuwa yanajaribu kupunguza makali yake. Mlio wa tetere na dudumizi ulisikika kutoka katika mti mkubwa uliokuwa karibu na nyumba hiyo. Asubuhi ilikuwa imeanza kama ilivyokuwa ikianza siku zilizopita, kwa sauti ya ndege wenye furaha wakiimba kwa kupokezana na kutegeana.

"Mbona mapema hivyo baba?"
"Mama yule ni nani?" Sijui kama alilisikia swali la mama yake au vipi lakini alionekana ana shauku ya kupewa jibu ya swali lake.
"Yule nani?" mama yake aliuliza huku akiwa amesimama mkono mmoja ameweka kiunoni na ule mwingine umeshikiliza guduria la maji. Alimuangalia mwanae kama kwa kumshangaa lakini akijifanya hajui anamuulizia nani.
"Mama yule binti amekusalimia hapo" alimjibu mama yake huku akiendelea kuangaza na kuona yule binti akimalizia kukata kona kuelekea madukani.
"Sasa wewe hata salamu jamani, eh" alicheka kwa kebehi lakini yenye kutuma ujumbe kwa mwanae.
"Mwangaluka mama"
"Mwangaluka Stanley" walicheka tena kwa pamoja. Kulikuwa na mapenzi makubwa kati ya mama na mtoto. Akiwa ni mtoto wa mwisho wa kiume wa Mwalimu Maduku Stanley alipendwa na kaka zake na aliabudiwa na dada zake. Hata kaka zake waliomtangulia walipoenda kuanza maisha yao yeye alibakia pale kuwa msaada mkubwa kwa wazazi wake. Wadogo zake wa kike ambao walikuwa secondari walimchukulia kweli kama kaka yao kwani kiumri walikuwa karibu naye zaidi kuliko kakazao wawili wakubwa ambao wote walikuwa wameshaanza maisha yao.
"Kaka Stanley, we humjui yule?" Suzy alizungumza akitokea ndani ya nyumba akiwa ameshika ufagao mkubwa.
"Simjui Suzy niambieni basi" alisema kwa shauku, wote wakacheka na wakati huo huo Belinda naye alitokea kujiunga na kikao hicho cha jumamosi asubuhi. Stanley alijua leo kabanwa na kina mama watatu, ilikuwa ni kawaida yao kumlinda kaka yao lakini wakati huo huo kumfanya vituko. Mwenyewe alijiona kama ni mfalme wa kasri la mzee Maduku. Na kwa kweli dada zake na mama yao walimuona hivyo.

Stanley alikuwa anamiaka ishirini na mawili tu. Alikuwa amemaliza kidato cha sita kwenye shule ya sekondari ya misheni lakini hakupata nafasi ya kuchaguliwa kuendelea na masomo ya juu. Hata hivyo alikuwa ameanza kibarua pale pale kijijini akifanya kazi na shirika la misaada la Waswedi la SIDA. Alikuwa ndiyo dereva na mkalimani wao. Alikuwa ni kijana nadhifu na mcheshi sana na waswedi walimpenda sana. Alikuwa hazoei watu haraka lakini akishazoea basi alikuwa na urafiki wa moyoni kabisa. Wajihi wake alikuwa ni mrefu kwa wastani lakini mwembamba. Alikuwa na mikono mirefu sana kama baba yake. Ilikuwa ni mojawapo ya vitu ambavyo vilimtofautisha sana na wenzake kwani kwa namna moja au nyingine ilikuwa rahisi sana kuona urefu wa mikono yake. Sasa ubishi mkubwa mara nyingi ulikuwa ni kama ni vidole ndiyo vilikuwa virefu au mikono yenyewe ilikuwa ni mirefu.

"Sasa mtaniambia ni nani yule au ndio hadi nipige magoti" sauti yake ilikuwa kali kidogo lakini macho yake yalimuangukia Suzy, dada yake kipenzi na kitinda mimba wao.
"Kaka, yule ni mjukuu wa Mzee Mswahili"
"Mjukuu wa Mzee Mswahili? Katokea wapi, mbona nawafahamu wajukuu zake"
"Chausiku huyo alikuwa anasoma Dar amekuja likizo, wenyewe wanasema mara mwisho alipokuja hapa ilikuwa akiwa darasa la saba sasa hivi naye amemaliza kidato cha sita" huyo alikuwa ni mama Eliza.

Stanley akaanza kurudi nyuma kwa haraka na kukumbuka. Alimkumbuka. Lakini hakumkumbuka kama binti aliyekomaa mwenye mvuto na haiba ya nguvu ya kuweza kumfanya mtu yeyote kugeuza shingo mara tatu tatu. Chausiku.

"Yule ni Chausiku?" aliuliza kwa hamaki
"Eehehehehe" dada na mama yake wakuanganisha vicheko vyao. Alijisikia kutatizika. Hakuelewa kama ni kweli au ilikuwa ni uzushi tu. Alijiambia kuwa yule haiwezekani kuwa alikuwa ni Chausiku. Aliapa haiwezekani kuwa ni Chausiku akitoa sababu elfu moja na moja za kwanini isingewezekana kuwa ni Chausiku. Aliondoka na kurudi chumbani kwake akiwa na maswali mengi juu ya yule binti, alijiandaa kwenda kwa Bw. Stevennson meneja wa mradi wa umeme wa jua pale kijijini. Chausiku lilikuwa ni jina ambalo hakuwa amelifikiria kwa zaidi ya miaka saba. Lakini siyo tu jina sura na umbile aliloliona asubuhi ile lilikataa kabisa kuingia kichwani mwake kuwa ni Chausiku mchokozi, mtukutu na mwenye maneno sana. Haiwezekani, alijiambia.

* * *

"Mmemuona Chausiku nyinyi?" Alfred aliwauliza marafiki zake jioni ya jumamosi ile huku wakiangalia mechi ya mpira wa miguu uwanja wa shule ya msingi.
"Aisee nimemuona, huwezi kuamini kapendeza kweli" Rajabu alijibu
"Yaani huwezi kuamini ni yeye" alidakia Simoni.

Stanley alikuwa anakodolea macho mpira huku mawazo yake yakiwa mbali kabisa na uwanja huo. Marafiki zake wakamshtua.
"Stanley wewe vipi?" Alfred akamuuliza
"Kuhusu nini?"
"Kuhusu Chausiku"
"Aaah, amefanya nini" wenzake wakacheka lakini wakamshangaa alikuwa wapi wakati wao wanamwaga sifa za Chausiku kama waliokuwa wameajiriwa kufanya kazi hiyo.
"Wewe umemuona?" Simoni akamrushia swali tena.
Stanley akatulia kwa sekunde kadhaa na kuwasimulia jinsi siku yake ilivyoanza. Aliwaambia jinsi kutwa nzima ile alikuwa anamuwaza Chausiku. Marafiki zake hao walianza kucheka kwanza na kumshangaa, lakini walicheka zaidi kwa sababu Stanley alikuwa anazungumza utadhani alikuwa ni mwenye mali. Lakini waalimshangaa na kuona kama mwenzao kapata bahati ya pekee iliyokuwa inamngojea tu. Kwa pamoja wakaanza kubishana ni jinsi gani kila mmoja angeweza kumpata na angefanya naye nini ili kupata nafasi hiyo. Yalikuwa ni mazungumzo ya vijana waliokomaa karibuni ambao maisha yao yalikuwa yanatishiwa kuwa ni ya kushtuliwa mioyo miaka mingi sana ijayo kila binti mzuri akipita mbele yao. Stanley hata hivyo alijisikia wivu kooni wenzake walipoelezea mambo waliyokuwa wanayaotea kufanya na Chausiku. Wao walikuwa wanatania, yeye alikuwa amepania.

"Acheni bwana!" Stanley alisema kwa hasira
"We vipi, una hasira kama ndio demu wako bwana" kwa lafudhi kali ya kisukuma Simoni alimshangaa Stanley.
"Hata kama siyo demu wangu lakini.." alishindwa kumalizia kusema maana hakujua angewaambia nini rafiki zake.
"Hahaha, usituambie umemdondokea bwana" Bakali alicheka huku akimsukumiza kwa mzaha.
"Mimi sijui bwana" na wengine nao wakacheka. Lakini macho ya Stanley yalikuwa hayana utani.
"Hutanii? Kweli umempenda"? Alfred alimuuliza huku wenzake wakikaa kimya kumuangalia Stanley. Stanley alikiri alichokuwa anakisikia moyoni. Alisema wazi kuwa vyovyote itakavyokuwa ni lazima azungumze na Chausiku na ikiwezekana amueleze ukweli, amueleze masaibu aliyojikuta nayo moyoni. Wenzake walimsikiliza, walimuonea huruma, walimuelewa. Waliahidi kumsaidia kwa namna yoyote ile.

Stanley alijua kuwa tayari moyo wake umetekwa na Chausiku na alijijua amewekwa kifungoni na kuwa mtu pekee mwenye ufunguo wa gereza hilo la maisha ni Chausiku. Alijua vile vile kuwa ili aweze kumpata na kuwa naye itahitaji kutengeneza mambo mengi ya huko nyuma, kwani hao wawili walikuwa na historia, walishapigana miaka saba nyuma na Stanley anakumbuuka jinsi alivyocharazwa viboko na marehemu baba yake kwa sababu ya Chausiku. Lakini Chausiku aliyemuona asubuhi ile hakuwa yule wa shule ya Msingi. Stanley alijiambia liwalo na liwe, lakini ataufuata moyo wake. Aliomba msaada wa rafiki zake wamsaidie kuweza kufikia lengo lake ambalo lilikuwa ni kupiga kura na hatimaye kupata ushindi wa kuuteka moyo wa Chausiku.

Stanley alitangaza nia, ya uchaguzi wa moyo. Marafiki zake walimsikiliza, walimuonea huruma na kila mmoja akajikuta anaachilia wazo lake na wote kumuunga mkono Stanley kuwa ndiye mgombea wao katika uchaguzi huo wa moyo. Walimtia shime aende jimboni kwa wapiga kura kuwasikiliza. Lakini vile vile aweze kutangaza nia. Stanley alikubali. Walikuwa wametoka eneo walilokuwepo na kwenda pembezoni kabisa ya uwanja ambako walikuwa wanapanga mikakati yao. Walishtushwa na mlio wa kipenga cha mwisho. Timu ya kijiji chao ilishinda mabao mawili bila. Ilikuwa ni dalili ya mpambano uliokuwa mbele ya Stanley.

Jimboni

Kijasho chembamba kilianza kumtoka Stanley alipofika kwenye mimbari kusoma somo la kwanza. Alipoanza tu kusema "somo la kwanza kutoka kitabu cha Kutoka" aliyainua macho yake na kuangalia waumini. Macho yake yaligongana moja kwa moja na macho ya msichana aliyekuwa amekaa benchi la nne hivi mbele upande wa kushoto kwake Stanley. Msichana huyo alikuwa amekaa nyuma ya kundi la masista waliokuwa wamependeza katika mavazi yao meupe yaliyopambwa na misalaba mikubwa iliyong'ara vifuani mwao. Alikuwa ni Chausiku.

Chausiku alikuwa amevaa tofauti na wasichana wengine mle kanisani. Wengi walikuwa wamevaa sketi na blazu na wengine magauni lakini kila mmoja wao alikuwa pia amejifunga kanga kwa namna fulani. Wengi walikuwa pia wamevaa vilemba vya kila namna. Chausiku alikuwa amevaa gauni jekundu iliyokolea ambayo kola yake na vifungo vya mbele vilikuwa vya rangi nyeusi. Nywele zake zilizopakwa mafuta zilikuwa zimefungwa nyuma kwa butu moja huku kiasi kidogo kikiangukia kwenye jicho lake la kushoto. Alikuwa amevaa miwani ya rangi nyeusi na kuwa kama mwalimu fulani hivi. Alikuwa amejipaka rangi nyekundu ya mdogo na nyusi zake zilikuwa zimetengenezwa vizuri kabisa kuupamba uso wake. Kwa kila kipimo alikuwa ameshinda shindano la warembo ndani ya kanisa hilo kama shindano kama hilo lingeruhusiwa. Hereni zake ndogo nyekundu zilining'inia masikioni mwake.

Stanley alirudisha macho yake kwenye kitabu cha masomo ya siku ile lakini akili yake iligoma. Alijaribu kujiuliza kama Chausiku alimkonyeza au alitabasamu walipoganisha macho yao. Alitamani kurudi kumuangalia tena. Alijizuia. Msukumo ulikuwa ni kama wa paka ambaye amemuona panya lakini anaambiwa asimsogelee. Alianza kusoma somo hilo la kwanza kutoka katika Agano la Kale. Sauti yake ilikuwa inakwama kwama huku kijasho kikijitokeza kwenye paji lake la uso. Stanley aliweza kuyasoma maandishi bila hata kujua yanahisi nini. Macho yalisoma maandiko hayo kwa mazoea ya kufuata herufi tu lakini akili yake yote ilikuwa inafikiria na kuwaza Chausiku anafikiria nini, alitamani ajiangalia kama yuko nadhifu.

Alipofika mwisho na kutangaza kuwa "hilo ndilo neno la Mungu" waumini walipojibu "tumshukuru Mungu" yeye mwenyewe alijikuta anaitikia moyoni "amina". Aliteremka kutoka kwenye mimbari hiyo na kuelekea upande wa kwaya ya kanisa hilo la kijiji ambako yeye alikuwa ni mwimbaji. Kabla hajakaa chini aliangalia tena upande aliokuwa ameketi Chausiku. Macho yao yakagongana tena, safari hiyo alikuwa na uhakika kuwa Chausiku hakutabasamu wala kukonyeza. Ila macho yake yalisema kitu ambacho Stanley hakuweza kukitafsiri mara moja hakujua kama ilikuwa ni huzuni, uchungu au kitu kingine ambacho hakuweza kukipatia jina mara moja.

Ibada ilipofika mwisho Stanley hakutaka kushangaa shangaa pale nje na kusalimia watu kama ilivyokuwa kawaida ya waumini weng siku ya jumapili. Aliamua kuelekea nyumbani mara moja kubadilisha nguo zake kwani alikuwa amepanga kwenda kwa Mzee Mswahili jioni hiyo kuwasalimia na kujaribu kuona kama angeweza kuonana na Chausiku. Tangu jana yake mawazo yake yote yalikuwa juu ya msichana huyo.

Simon na wenzake walimshangaa kwanini alikuwa anawahi kurudi nyumbani kuliko ilivyokawaida na yeye aliwaambia tu kuwa kuna shughuli nyumbani alikuwa anawahi. Aliwahi kufika nyumbani na hakukuwa na mtu mwingine yeyote kwani mama yake na dada zake alikuwa amewaacha kanisani wakija taratibu na kundi la kina mama wengine. Alivua shati lake na kubakia na vesti yake tu. Alikuwa ni kijana mwembamba lakini ambaye alikuwa amejaza misuli kutokana na shughuli mbalimbali za Useremala alizokuwa akizifanya wakati wa jioni na mwisho wa juma na kujiongezea kipato. Ulikuwa ni ufundi ambao aliurithi kutoka kwa baba yake. Alichukua pasi na kuijaza mkaa akaimwagia mafuta ya taa na kuiwasha, akaiweka nje ipigwe na upepo. Aliingia chumbani kwake na kuchagua nguo za kuvaa. Alisubiri pasi ipate moto wa kutosha aanze kunyosha nguo. Mawazo yake yote yalikuwa kwa Chausiku.

"Ka' Stanley" sauti ya Suzy ilimshitua wakati anamalizia kuvaa viatu vyake tu
"Naam"
"Chai tayari"
"Haya nakuja Suzy"

"He! Mwenzetu mbona umetoka hivyo" mama yake alikuwa wa kwanza kumshangaa. Alimsogelea Stanley na kumtengeneza kola yake iliyokuwa haijakaa vizuri. Staley alikuwa ananukia manukato ya "Yu" ambayo yalikuwa maarufu kwa vijana pale kijijini.
"Natoka kidogo"
"Kutoka gani huku?" dadake mwingine alidakia
"Mnatafuta umbeya tu" alipojibu hivyo wote walicheka. Kama ilivyokuwa kawaida yao siku ya Jumapili familia ilibariki chakula na wakakaa mezani kula kifungua kinywa. Walizungumza mambo mbalimbali na kabla hawajamaliza kabisa chakula Stanley aliwaaga kuwa anatoka. Wakamtakia kila la kheri alikokuwa anaenda. Alichukua baskeli yake, akaidandia na kuelekea upande wa mashariki wa kijiji.

Haikumchukua muda sana alifika barazani kwa mzee Mswahili. Na kama alivyotarajia hakupokelewa na mtu mwingine isipokuwa mzee Mswahili mwenyewe. Alimsalimia kwa Kisukuma, mzee Mswahili aliitikia kwa Kiswahili. Hilo halikuwa jambo geni kwani hakuna mtu ambaye aliwahi kumsikia mzee Mswahili akizungumza Kisukuma. Alikuwa anakisikia Kisukuma vizuri kabisa lakini alikuwa anapenda sana kuzungumza Kiswahili fasaha wakati wote na ndiyo sababu alijulikana kijijini na hata miji ya jirani kama Mzee Mswahili.

"Hujambo bwana"
"Sijambo mzee, hatukukuona kanisani leo, wazima hapa"
"Ah..huko kanisani kwenu myeyusho tu." Nusura Stanley aangushe kicheko.
"Siku moja moja babu siyo mbaya"
"Haya karibu, kwema huko kwenu"
"Kwema kabisa".
"Vuta hivyo kiti hapo"

Stanley alivuta kitu na kuketi pembeni ya mzee Mswahili ambaye alikuwa anavuta sigara yake huku mikono yake ikiwa imeshikiliza gazeti la MwanaHalisi mikononi mwake la wiki iliyopita. Mzee Mswahili alianza kulalamika mambo ya ufisadi vitu ambavyo Stanley alikuwa havifuatilii kabisa. Mzee Mswahili alikuwa ni kama shihata ya kijiji kwani alijua yote yanayoendelea Tanzania kutokana na kusoma sana magazeti na kusikiliza radio za ndani na vituo vya utangazaji wa vya nje. Alianza kumuonesha Stanley habari mbalimbali na jinsi gani Tanzania inahitaji mabadiliko. Alikuwa ni kama mwanasiasa fulani. Mzee Mswahili hakuhitaji kujua nini kimemleta kijana huyo hapo nyumbani siku hiyo ya Jumapili kwani mara kwa mara vijana na wazee huja na kupiga soga naye na kumsikiliza habari alizonazo hivyo alishazoea kukaa na kuzungumza. Tena kwa siku kama hiyo ya Jumapili ikifika majira ya jioni kundi la vijana huwa wanakuja hapo kuzungumza naye na kupata hekima aliyonayo na kuzungumza naye mambo yote yanayohusu siasa na maisha na wakati mwingine kusikiliza visa vyake vya wakati wa ujana wake alipokuwa akifanya kazi jijini Dar-es-Salaa hadi alipostaafu katikati ya miaka ya tisini.

Wakati wanazungumza hapo nje, dalili zote zilionesha kuwa jikoni mambo yalikuwa yanaiva. Harufu ya mchuzi wa nyama ilifunika angala la nyumba ya mzee Mswahili katika hali iliyosababisha midomo ya Stanley kujaa mate kwa hamu. Stanley alikuwa amekaa akijaribu kuangaza angaza kiujanda kuona kama angeweza kumuona Chausiku. Aliweza kusikia sauti ya kina mama wakizungumza jikoni na mjukuu wa mwisho wa mzee Mswahili alikuwa amekaa kwenye meza ndani akimalizia kufanya kazi yake ya shule. Pale nje ilikuwa ni kama mahali pa mikutano mifupi mifupi kwani wazee na vijana waliokuwa wakipita pale walitumia dakika chache kuwasalimia.

Wakiwa wanaendelea na mazungumzo walisikia hatua za miguu zikija nyuma yao kutoka mlango wa mbele wa nyuma. Chausiku alikuja akiwa amejifunga kanga kiunoni lakini bado akiwa na gauni lake lile jekundu alilokuwa nalo kanisani. Alipiga magoti mbele ya mzee Mswahili. Macho yake yaligongana tena na Stanley ambaye alijivuta kukaa vyema kwenye kiti chake kwani kutokea kwa Chausiku kwa ghafla hivyo nusura kumsababishe roho itoke mwilini mwake.

"Babu chakula tayari" Alisema kwa heshima huku macho yake ameyaangusha chini.
"Asante mama"

Chausiku akainuka kurudi jikoni. Hakufika mbali.

"Chiku" ndivyo mzee huyo alivyolichakachua jina la mjukuu wake. "Mbona humsalimii mwenzio hapa?, heshima gani hii; usituletee mambo yenu ya Dar" alifoka kidogo.
"Mambo?" alisema huku akiyazungulusha macho yake angani. Kabla Stanley hajajibu Chausiku alikuwa ameshaingia ndani. Hata hivyo shingo ya Stanley ilimfuatilia hadi anaingia ndani akiufuatilia mwendo wa chiku. Alijisikia kutaka kumuita. Hakujua kilichomkuta. Mzee Mswahili hakuchelewa alikilazimisha kichwa cha Stanley kurudi kwenye usawa wa kati kwa kibago kilichopigwa kisogoni kwa haraka kama mtu aliyejaribu kuua nzi.

"Wewe vipi, mbona unamuangalia mjukuu wangu hivyo?" aling'aka
"Aah samahani mzee.. uuuh.. mmh" alianza kumung'unya maneno
"ndicho kilichokuleta nini?"
"Hapana mzee"
"Usitake kuniharibia mjukuu wangu"
"Hapana mzee nilikuwa nawaza tu"
"ndiyo hayo mawazo yabakie humo humo kichwani"
"ndiyo mzee"
"Haya twende kula"

Stanley alijisikia kutetemeka hadi figo na maini. Kile kibao kilimkumbusha kuwa yupo hapo kwa mzee Mswahili. Aliinuka taratibu na kumfuata mzee Mswahili, alikwepesha kabisa macho yake kumuangalia Chausiku ambaye aliwapokea hapo ndani akiwa ameshikilia bakuli na birika la maji ili kuwaosha mikono. Pale mezani walikuwepo yeye mzee Mswahili, Stanley na mjukuu yule wa kiume ambaye wakati huo alikuwa amehamisha vitabu vyake na kuviweka pembeni. Kabla hawajaanza kula mjukuu wa kiume akawakumbusha kubariki chakula. Kwa uvuvi mzee Mswahili alisubiri mjukuu wake huyo kipenzi amalizie sala. Walivamia ugali huo wa kisukuma uliosindikizwa na nyama ya kuku ya mchuzi, na mchicha wa kukaangwa ukiteremshiwa na maji ya baridi yaliyotoka kwenye mtungi mkubwa uliokuwa kwenye kona ya sebule hiyo.

Walipomaliza kula walipiga soga kidogo na mzee Mswahili kama ilivyokuwa kawaida yake alitoka tena nje na kuketi upenuni pale,hata hivyo wakati huo alimuagiza Stanley kuhamisha viti vyao hadi mbali kidogo tu ya nyumba chini ya mti wa Krismasi uliokuwa umependeza kwa rangi yake ya kijani na maua ukiashiria mwelekeo wa mwisho wa mwaka. Waliendelea kupiga soga za hapa na pale huku mzee Mswahili wakati huo akiwa anasoma makala za gazeti la Uhuru ambalo mzee huyo alihakikisha hakosi nakala yake hata likichelewa vipi. Ilipofika mida ya saa kumi hivi Stanley aliamua kuaga kurudi nyumbani. Alikuwa na uhakika kabisa kuwa kweli Chausiku ni mjukuu wa mzee Mswahili na alishakata tamaa kuwa haiwezekani hata kuzungumza naye kwani yule mzee alikuwa ni mnoko.

"Mzee miye narudi nyumbani nimefurahi sana leo"
"Hamna neno, msalimie sana mama yako na wadogo zako"
"Bila ya shaka mzee, ukihitaji msaada mzee hapa wewe nitumie ujumbe"
"Vizuri sana Stan, tena naweza kukutumia kesho au jumanne"
"Hamna neno mzee mshinde vyema". Aliinuka taratibu na kumpa mkono mzee Mswahili ambaye aliupokea huku mkono wake wa kushoto ukipeleka mbali sigara yake nyingine na kupuliza moshi pembeni ya mdomo wake. Jua lilikuwa taratibu limeanza kupunga mkono wa baibai jioni hiyo. Kulikuwa na hali fulani ya utulivu ambao huwezi kuupata mahali pengine popote isipokuwa katika kijiji cha Kiafrika.

"Chiku!" Mzee Mswahili aliita kwa nguvu kidogo
"Bee Babu" sauti iliitikia. Chausiku alikuja mbele ya babu yake na kupiga goti.
"Mwenzio anaondoka humuagi?"
"Kwa heri!" alimuangalia na kusema na kurudisha macho yake chini.
"We vipi, ndio kuaga gani huko?" Mzee Mswahili alikuja juu. "Kwani mmegombana?" aliuliza.
"Hapana babu"
"Haya msindikize mwenzio kidogo umtoe hapa nyumbani nyie vijana wa siku hizi sijui mkoje" alishangaa huku akitoa maagizo. Stanley hakuamini masikio yake na hakujua kama ni mtego anategewa au nini.
"Ndiyo babu" Chausiku aliinuka na kwenda ndani. Aliporudi alirudi na mfuko uliokuwa umejaa nyanya na vitunguu. Bibi yake alikuwa ana bustani ya nyanya na vitunguu na mara nyingi wageni walipokuja hapo nyumbani waliondoka na nyanya kidogo. Muda wote huo bibi yake alikuwa bado hajarudi kutoka katika shughuli zake kanisani.

Stanley alimpokea mzigo huo kwa heshima na kumuambia kwa Kisukuma "Wabeja ukinkulu"
"Wabeja kulumba!" alijibu. Vidole vyake viligusana na vile vya Stanley chini ya mfuko huo na umeme kama wa radi ulipasua mwili wake. Alimuachia kwa haraka mfuko huo. Stanley aliaga na akisindikizwa na Chausiku alianza kuondoka akiwa ameuweka mzigo kwenye kiti cha baskeli huku akiikokota baskeli taratibu.

"Chausiku unanikumbuka mimi?"
"Kwanini nisikukumbuke?"
"Sasa mbona unajibu kwa ukali?"
"Hivi wewe unaujua ukali?"
"mmh!" Stanley aliishiwa maneno, walikuwa wanatembea taratibu bila maneno kwa sekunde chache.
"Kwani nimekukosea nini?"
"mmh.. watu wengine bwana"
"Una maana gani watu wengine?"
"Hamna kitu". Walikuw wametembea kama mita thelathini tu kutoka nyumbani na Stanley alikuwa tayari kuikwea baskeli yake.
"Naweza kupata muda wa kuzungumza na wewe?" alimuuliza Chausiku.
"Mbona tunazungumza?"
"Hapana, nataka turudishie urafiki wetu"
"Urafiki?"
"Jamani Chausiku tulikuwa marafiki tulipokuwa wadogo"
"Msisitizo upo kwenye neno 'tulikuwa'". Kimya kikapita tena wakati kundi la kina mama wakiwapita.
"Yaani hatuwezi kuwa marafiki tena?" aliuliza Stanley. Moyo ulikuwa unamdunda, kijacho kilikuwa kinamtiririka kwenye kwapa zake. Alishindwa kuyaangalia macho ya Chausiku. Akili zake zilikuwa zinanguka kama pia asijue aseme maneno gani ili kumfanya Chausiku aweze japo kumsikiliza.
"Sidhani kama inawezekana labda hadi uniombe msamaha"
"Msamaha?"
"kwani nimezungumza Kiingereza? Ndiyo msamaha"
"Kwa lipi tena?"
"Yaani unajifanya umesahau kabisa?" Stanley hakusahau lakini hakudhania lilikuwa ni jambo kubwa. Alimuomba msamaha kutoka moyoni huku midomo yake ikitetemeka. Alikiri kuwa alifanya vibaya kumchongea nyumbani kwa babu yake kitu ambacho kilimsababisha Chausiku alambe mboko na baadaye kukasirika na kutaka kurudi kwa wazazi wake Dar japo alipenda sana kuwa na bibi yake. Machozi yalimlenga kidogo Chausiku alipomsikia Stanley anaomba msamaha.
"Umenisamehe?" aliuliza Stanley
"Miye sijui." aligeuza macho yake yasigongane na ya Stanley. Ilikuwa ni mara ya tatu kwa siku hiyo mmoja wao akipata tabu ya kuangaliana na mwenzie machoni.
"Kesho unafanya nini?"
"Sijui"
"Unafikiri Mzee Mswahili atakuacha unisindikize mjini?"
"Sasa unaulizia huku kwanini hukumuuliza mwenyewe kule?"
"Sasa si nilitaka nikuulize wewe kwanza?"
"Sijui itabidi urudi kumuuliza". Alishindwa la kusema. Hakutaka kurudi kule tena kwani jua lilikuwa limezidi kwenda. Alimshukuru kwa mzigo huo na kumuaga. Alidandia baskeli yake na kumuangalia tena. Chausiku alikuwa bado amesimama hapo hapo anamuangalia.
"Usiku mwema"
"Asante na wewe".

Stanley alianza kuendesha baskeli yake. Alikuwa hatua kama tano tu kutoka kwa Chausiku alilazimika kusimama ghafla.

"Stan!" Sauti ya Chausiku ilimuita. Aligeuka
"Nitakuwa posta saa nne asubuhi!" Chausiku alisema na kugeuka kuanza kutembea kurudi kwao. Stan nusura apige kelele ya asante. Alimuangalia Chausiku akitembea kwa madaha huku akitingisha kidogo viungo vile alivyojaliwa na muumba wake katika staili ile ya kale ya "Singida-Dodoma, Singida-Dodoma". Alianza tena kukanyaga mwendo. Alimpigia kengele mama mmoja aliyekuwa na kiroba kichwani ambaye alichepukia pembeni.

Aliamua kuwa kesho ni lazima aanze kumwaga sera. Alijiuliza ataweza vipi kuchepuka toka kazini asubuhi hiyo kwenda pale Posta. Alishaamua kuwa liwalo na liwe saa nne asubuhi atakuwa Posta ya mji wa Bariadi. La kwanza alijua ni lazima atengeneze ilani yake ya uchaguzi wa moyo.

MPINZANI

Saa tatu na nusu ilipofika Stanley alikuwa tayari amefika Posta. Aliomba ruhusa kazini kuwa kuna mgeni wa familia alikuwa anakuja kutoka Arusha na yeye aliagizwa kwenda kumpokea. Kwa vile haikuwa kawaida ya Stanley kuomba omba ruhusa kazini wazungu wake hawakumfanyia hiana walimpa baraka zote. Posta ya Bariadi haiko mbali sana na stendi ya mabasi hivyo Stanley alipofika kitu cha kwanza ni kuingia posta kuhakikisha kuwa Chausiku hakumuwahi na alipotoka hapo alienda kwenye mgahawa wa mama mama Stella ambao ulikuwa ni miongoni mwa migahawa iliyopo pale kituoni. Uzuri wa mgahawa huo uliangalia moja kwa moja mlango wa kuingilia posta. Stanley alikaa kwenye benchi moja huku macho yake yakitalii huku na kule kuhakikisha kuwa kila anayeingia posta pale aliweza kumuona.

Aliagiza chai ya rangi na chapati. Aliulizwa vijiko vingapi vya sukari akasema vitatu. Alipoanza kufungua kinywa hapo mawazo yake yote yalikuwa katika taswira aliyobaki nayo tangu jana alipoachana na Chausiku pale njiani. Bado katika mawazo yake alimuona Chausiku alivyokuwa mgumu na baadaye alivyomuita jina lake na kumpa miadi kiana. Lakini zaidi aliendelea kumuona mawazoni mwake Chausiku akitembea kama twiga wa Serengeti kurudi kwao. Kila fundo alilokunywa la chai alihisi utamu wa sukari ambao ulikuwa ni kama methali ya utamu aliokuwa akijisikia akimuwazia Chausiku. Harufu ya hiliki ilikuwa imetanda pale huku mabasi ya kutoka Magu na yale yanayotoka Shinyanga yakiingiana kutoka kituoni hapo. Wakati anakunywa chai kelele zaidi ziliongezeka wakati basi la Zuberi lilipoingia hapo kwa mbwembwe kibao.

Ilikuwa katika kelele hizo ndipo macho yake yalipomuona kwa mbali Chausiku akiingia posta akiwa amefuatana na rafiki yake. Moyo ulianza kumuenda mbio huku akijikuta anafikicha viganja vyake. Kama aliyekuwa kwenye mashindano ya kula alianza kushindilia chapati na kuteremshia na chai kiasi cha kumfanya mama Stella amuonye asije akaungua bure, anywe taratibu. Alijitahidi kujizuia ili ampe muda kidogo Chausiku afanye kilichompeleka pale posta na akitoka tu basi aende. Alikuwa na uhakika Chausiku hakumuona. Alijilamba midomo yake kama mtu aliyekuwa anatamaa ya vitu vingine zaidi ya chapati!

Kama dakika kumi hivi Chausiku alitoka akiwa ameongozana na rafiki yake. Alipotoka aliangaza macho kwa haraka haraka na wala hakumuona Stanley ambaye wakati huo alikuwa anamalizia kumlipa mama Stanley. Wakati Stanley anageuka na kuanza kuelekea alipo Chausiku kama mkosi au njama gari dogo la Corolla lilisimama kati ya alikokuwa Stanley na ilikokuwa posta kwani ilikuwa njia fupi inayotenganisha posta na stendi.

"Chausiku mambo!!" sauti ya kiume iliita kutoka kwenye gari. Chausiku aliangalia kwa hamasa akidhania kuwa ni Stanley. Aliyemuona alikuwa ni Daniel Makundi.
"Hey Danny!!" Chausiku alipaza sauti yake. Macho yake yaliwaka kwa hamasa na akamsahau kabisa Stanley.
Danny aliyekuwa abiria kwenye gari lile aliamua kufungua mlango wa abiria na kutoka kuelekea alikokuwa Chausiku. Wakati huu wote Stanley alikuwa ameganda kama sanamu akiangalia bila kuamini kilichokuwa kinatokea mita chache tu kutoka alipokuwepo.
"Mambo vipi Chausiku, duh, uko bomba" alisifia Danny
"Asante, umekuwa bonge la mtu" naye alirudisha sifa
"Kidogo tu mtu wangu; umekuja lini"
"Nna siku chache tu hapa"
"Duh, yaani umebadilika sana isipokuwa sura yako ile ile" Alisema Danny huku akimuangalia kwa karibu.
"Danny, kutana na rafiki yangu Celina"
"Mambo vipi" Danny alinyosha mkono wake wa kulia kumsalimia Celina ambaye wakati huo alikuwa amepigwa na haya kidogo maana alijua walitarajia kumuona Stanley na uchangamfu wa Chausiku kwa Danny ulimkwaza kidogo, alijisikia moyo ukimnyong'onyea. Alikuwa anajiuliza Stan yuko wapi maana alikuwa anazidiwa kete asubuhi na mapema.

"Mnaenda wapi asubuhi hii" Danny aliuliza. Wakati huo wote dereva aliyekuwa na Dannya alikuwa ameegesha gari pembeni zaidi ili kupisha magari mengine yaliyokuwa yanatoka na kuingia kituoni hapo.
"Tulikuja posta tu sasa tunarudi nyumbani" Chausiku alijibu.
"Mmeshakunywa chai?" aliuliza. Walibabaika kidogo na kabla hawajajibu, Danny alidakia "twendeni basi tupate breakfast kidogo tuzungumze kidogo sijakuona siku nyingi umekuwa mwali kabisa" alisema huku akiyadondosha macho yake kuanzia usoni, kifuani, kiunoni hadi miguuni mwa Chausiku. Chausiku alijisikia kutetemeka.

"Twende pale kwa Mama Stella" alionesha mkono wake ulipokuwepo mgahawa ule maarufu. Hapo ndipo macho ya Stanley na Chausiku yalipogongana na yeye kuzinduliwa katika dimbwi la mawazo lililokuwa limemkaba kama jinamizi la usiku wa manane. Stan alimuangalia tena Chausiku lakini ilikuwa ni zamu ya Chausiku kukwepesha macho yake kana kwamba hakumuona. Stanley alitambua mara moja kuwa kundi lile la watu watatu lilikuwa linaelekea upande aliokuwepo na hakuwa na mahali pa kukimbilia. Danny alimuaga rafiki yake na kumuambia awafuate pale kama baada ya nusu saa hivi. Walipovuka barabara walielekea moja kwa moja huku wakicheka. Sekunde chache tu walikuwa mbele ya mgahawa wa mama Stella.

"Hey Stanley" alikuwa ni Celina aliyemchangamkia kwa furaha kuliko Chausiku ambaye alionekana kama mtu ambaye amekutwa akifanya kitu cha aibu.
"Mambo Celina"Alimjibu.
"Hi Stan" Chausiku alijitahidi na kutoa salamu. Alikuwa anaangalia pembeni hakutaka kabisa kugonganisha macho yake na Stan.
"Mambo vipi Stanley" Danny alimsalimia huku akijaribu kumpita kuelekea kwenye benchi moja; mkono wake ulijaribu kumvuta Chausiku ambaye alifuata kama mbuzi apelekwaye malishoni. Stan alishindwa kujua cha kufanya. Aliwapisha wapite na yeye akatoka nje kabisa. Alijisikia hasira, donge la uchungu likimkaba na kutaka apige kelele. Alitamani amvute mkono Chausiku na kuanza kumhoji, hata hivyo alijua hana haki hiyo kwani hata sera zenyewe hajamwaga bado. Alipigwa na upepo kidogo hapo nje huku akili yake ikienda mwendo kasi wa treni ya umeme kujiuliza afanye nini. Aondoke tu, atake maelezo au atafute nafasi nyingine. Alitembea tembea akizunguka zunguka hapo hapo huku mikono ikiwa mfukoni. Aliamua la kufanya.

"Danny, samahani naweza kuzungumza na Chausiku mara moja" alisema baada ya kurudi ndani hapo na kwenda moja kwa moja kwa aliyejua ni mpinzani wake.
"Unaniuliza mimi kwani nimemfunga pingu?" lilikuwa jibu la kejeli lakini lenye ukweli.
"Naweza kuzungumza nawe kidogo?" alimgeukia Chausiku ambaye wakati huo alikuwa hata kumwangalia hakutaka kumwangalia.
"Danny unaniruhusu?" Chausiku aliuliza. Danny alielekeza tu kwa mkono waende zao kuzungumza.
"Chai ikifika utakuwa umerudi siyo?" alisema kama kwa kuagiza au kutoa amri ya chini chini. Stanley alijiambia mawazoni kuwa Chausiku anahitaji mtu atakayemheshimu kiukweli siyo kumburuza. Chausiku alikuja nje ya mgahawa huo.

"Chausiku nilidhani ulitaka kukutana na mimi leo" alianza kulalamika Stan
"Mimi nilisema nitakuwa posta sikusema uje"
"Kweli hukutaka kukutana na mimi?"
"mmh..ndiyo lakini sikukuona pale"
"Nilikuwa nakusubiria hapa ili umalize shughuli zako"
"Sasa kama hukuwepo nalako halipo"
"Chausiku nisamehe lakini unajua jinsi ninavyojisikia juu yako"
"Umejuaje kama najua? Unajisikia nini" alianza majibu yake ya shari na ya mkato.
"Tangu tuko wadogo ulijua ninakupenda na sasa tumefika mahali pa kufanya maamuzi yetu nilitaka nipate nafasi nikutamkie hivyo" alisema kwa sauti ya juu kidogo iliyowafanya baadhi ya watu wageuze shingo zao kuwaelekea.
"Unanipenda? Hivi umesahamu ulivyosababisha nichapwe na babu hadi mimi kuamua kuondoka hapa?" alianza kuja juu, macho yake yalilengwa na machozi kidogo "tulikuwa marafiki lakini ulikuwa unanionea kila wakati halafu leo ati unasema ulikuwa unanipenda". Pumzi yake iliongezeka na sauti yake ilikuwa ya juu.
"Chiku, ulikuwa utoto, tulikuwa hatujui mambo haya; na laiti ningekuwa na uwezo wa kurudisha muda nyuma ningerudisha kila kitu kibaya nilichosema au kukufanyia; siwezi" alizungumza kwa sauti ya juu. Watu waliokuwa karibu yao waliacha shughuli zao na kuanza kuwaangalia vijana hao wawili.
"Samahani Stanley siwezi kuwa na wewe" alisema na kugeuka kurudi ndani ili kukwepa kuwapa watu faida zaidi. Stanley bila kujijua alijikuta amenyosha mkono wake kumvuta binti yule asiende wamalize kuzungumza. Lilikuwa kosa.

Hakujua ni kitu gani kilimpiga lakini alijua amepigwa na mtu pale alipoona nyota za rangi rangi zikipeperuka angani na ladha ya damu ikigusa ulimi wake. Watu walipiga kelele kwa kushtuswa na hakukuwa aliyepiga kelel sana kama Chausiku. Wakati fahamu inamrudia baada ya kupotea kwa sekunde chache, Stanley alikuwa amelamba udongo.

"Amekuambia hataki kuwa na wewe unataka kumlazimisha?" ilikuwa sauti kali ya Danny akiwa amesimama kati ya Stanley na Chausiku. Mikono na midomo ikimtetemeka. Stanley alijaribu kuinuka ili akae sawa. Hakupewa muda. Danny alimpiga teke la ubavuni lilimrusha pembeni. Ndipo watu walipoamua kuingilia kati na kumzuia Danny.
"Danny usimpige bwana, twende zetu" alilia Chausiku huku akimvuta Danny watoke hapo. Celina alikuwa analia akiomba msaada watu wamsaidie. Wakati huo huo rafiki yake Danny ambaye waliacha muda kidogo alikuwa anaingia tu hapo na kukuta vurumai hiyo. Danny alimshika mkono Chausiku na kumwelekeza liliko gari.
"Selina twende!!" Chausiku alipiga kelele kwa rafiki yake ambaye alikuwa bado anajaribu kumuinua Stan. Aliona anachelewa akakimbia haraka na kumshika mkono Selina kumvuta kuelekea lilikokuwako gari. Wakati huo watu walikuwa wanajaribu kumsaidia Stanley kuinuka kwani bado alikuwa ameshikilia ubavu wake akisikiliza maumivu. Alijihisi kutaka kukojoa na kutapika kwa wakati mmoja. Kundi hilo la watu watatu pamoja na dereva waliingia kwenye gari na kutoweka.

Stanley aliamka taratibu huku akipewa pole na watu waliokuwa karibu pale, alijisikia unyonge na hasira; lakini zaidi alijisikia aibu na kuonewa. Aliinuka na kujipukuta. Mama Stella alikuja na kumpa maji kusukutua mdomo wake na kumuuliza kama anahitaji kukaa chini kidogo. Hakutaka kufanya hivyo na badala yake aliaga kuondoka hapo stendi na kwa mwendo wa kujikongoja aliondoka pole pole. Akili yake ilipomrudia taratibu alijua kuwa amepata mpinzani. Hakuwa tayari kusalimu amri kwani aliamini kabisa kuwa bado ana nafasi ya kuuteka moyo wa Chausiku. Wimbo wa "mwenye mapenzi haoni, ingawa macho anayo" ulianza kucheza kichwani mwake. Alitabasamu kidogo huku akijizuia kutonesha maumivu ya mdogo kufuatia kile kibao cha kukumbukwa na kusimuliwa.

Kilichotokea alikiona ni gharama ya mapenzi tu na sehemu ya kampeni chafu ya mpinzani wake. Moyo wake ulikuwa umedhamiria kushinda uchaguzi huo na kushinda lilikuwa ni kusudio lake. Aliwapigia simu rafiki zake wakutane jioni kupanga mkakati wa ushindi, mkakati utakaohakikisha kuwa yeye anabakia kuwa ni mgombea pekee. Lakini alijua kuwa kwenye upinzani wa mtu kama Danny kupita bila kupingwa ni ndoto kwani kulihitaji nguvu za ziada. Aliapa kuwa atalipiza kisasi na vyovyote itakavyokuwa ni lazima ashinde. Alipiga simu simu kazini kuwataarifu kuwa asingeweza kwenda kazini kabisa siku hiyo kama alivyotarajia kwani alikuwa ameomba ruhusa kwa muda ule wa asubuhi tu. Alirudi nyumbani na kujipumzika akisubiri jioni ifike akutane na washikaji wake. Danny ni lazima alipe, alijiambia.

USIKU WA SOGOTA

Chausiku aliingia nyumba kwao karibu saa sita za usiku akitokea kwa Danny. Ilikuwa ni siku ya Jumanne. Alikuwa ameaga mapema kuwa anaenda kuonana na rafiki zake akiwemo Selina lakini kiukweli alikuwa ameenda nyumbani kwa Danny. Baada ya tukio la jana yake pale Stendi Chausiku aliondoka akiwa ameumia moyoni na akiwa amejaa hasira. Hata walipomuacha Stan pale akichechemea kwenye gari alikuwa mkali kama mbogo.

"Kwanini ulimpiga Danny" alimhoji kijana huyo
"Samahani kwa kweli hasira zilinizidia"
"Zilikuzidia vipi wakati tayari nilikuwa niko na wewe?"
"Mimi sijui nilidhani labda alikuwa anakukorofisha tu" Wakati huo wote Selina alikuwa amekaa kimya akiangalia nje ya gari na kujifanya kama mtu asiyesikia malumbano yaliyokuwa yanaendelea humo.
"Sasa jamani Stan atanifikiriaje"
"Wewe unajali nini?"
"Una maana gani ninajali nini; yeye ni rafiki wa familia yetu na kitu kile kumtokea hakujanipa furaha kabisa"
"Chausiku samahani kwa kweli naona shetani alinipitia tu; nilijisikia wivu alipokuvuta mkono" Danny alilalamika huku sautti yake ikikatika kidogo kufichua hisia iliyokuwa imemshika moyoni. Katika ujana wake huo na nafasi yake alikuwa amewapata wasichana wengi na kuwa nao na mahusiano ya kimapenzi. Lakini hakuna aliyekuwa na hamu ya kuwa naye tena hata kwa milele yote kama Chausiku. Historia yao ilianzia shuleni kama ilivyokuwa kwa Stan na Chausiku. Tofauti kubwa ni kuwa Dannya likuwa amewatangulia wao miaka kama miwili hivi; kwa hiyo ilikuwa ngumu sana kuwa na mahusiano na binti wa shule ya msingi wakati yeye anaenda kidato cha kwanza. Lakini alikuwa anamhusudi mjukuu huyo wa mzee Mswahili na hata alipoondoka kijijini pale na kupokea kwa muda alikuwa ameacha pengo moyoni mwake. Kumuona ile jana yake pale stendi ilirejesha hisia zote na matumaini ambayo alidhani yamepotea.

Koo lilimkauka wakati wanawapeleka Chausiku na mwenzake nyumbani kwao. Baada ya majibizano yaliyokuwa na hisia za pande mbili gari liliingiwa na ukimya wa kukata na shoka. Walipoachana nao mara baada ya kuwafikisha nyumbani, Danny alimuomba msamaha tena Chausiku huku machozi yakimlengalenga. Chausiku alimsikiliza na moyoni alijikuta anapata joto la kumsamehe. Alijua kwa kila kipimo alikuwa ni kijana mzuri na anakumbuka wakati wa shuleni alivyoingilia kati ugomvi kati ya Stan na yeye; ugomvi uliosababisha Chausiku aondoke kijijini pale. Alikuwa na uhakika wa asilimia mia moja kuwa Danny alikuwa naye anampenda vile vile. Lakini moyo wake ulijikuta kwenye njia panda ya mapenzi. Vijana wawili toka utotoni mwake wote wakiwa wamekomaa walikuja kama radi na mvua katika maisha yake. Alijikuta anashindwa kufanya uchaguzi wa moyo. Walipoagana pale Danny alimuomba kama ataweza kumsamehe aende kesho yake ili wazungumze zaidi. Alikuwa na uhakika kuwa Stan hawezi kumsamehe baada ya tukio la jana yake na hivyo aliamua kuwa angeenda kwa Danny.

Hivyo hiyo Jumanne aliporudi usiku huo nyumbani ajikuta na furaha na huzuni kwa wakati mmoja. Furaha ya kile kilichotokea kati yake na Danny lakini huzuni kwa sababu laiti kingekuwa kimetokea kati yake na Stanley. Alikumbuka alipofika nyumbani kwa Danny majira ya saa kumi na moja na kumkuta Danny akimsubiri kwa hamu. Nyumbani pale palikuwa kimya huku televisheni ikirusha kituo cha Star Tv ikiwa hewani. Siku hiyo Chausiku alikuwa amevaa sketi ya jeans na tsheti ya rangi nyeusi iliyokuwa imeandikwa "Baby" mbele ya kifua chake kilichokuwa kinaonesha kujaliwa kwake kimaumbile. Alijifunga mkanda mwekundu kiunoni uliogawanya umbili lake katika umbo la nane ambalo halikuwa na mjadala. Nywele zake alizifunga tena kama alivyokuwa amezifunga Jumapili pale kanisani.

"Karibu sana Chiku, nimefurahi umekuja" Danny alionesha wazi hamasa yake kwa kumkaribisha ndani binti huyo.
"Asante, lakini sitakaa sana" alisema bila kujijua kama alikuwa anajichongea au anajitetea.
"Hamna neno, wala sitakukawiza sana" alisema Danny ambaye baada ya mgeni wake kuketi alimuuliza kama angependa kunywa kitu chochote, soda, bia, maji au maziwa! Chausiku alichagua maji. Danny alielekea jikoni kuchukua maji.
Sebule ya Danny ilikuwa ni kubwa kiasi ikiwa imepambwa vizuri huku kila kitu kikiwa kimepangwa kama vile ilikuwa ni kwenye jumba la maonesho ya samani. Kwa kila kipimo nyumba hiyo ilionekana kama iliyonyanyuliwa kutoka Dar au Arusha mjini na kupandikizwa Bariadi. Mapazia yake na kila kitu ndani kilikuwa ni cha kisasa. Chausiku alikumbuka kuona dishi kubwa la setelaiti likipamba nyumba hiyo. Kitu kimoja ambacho pia kilikuwa dhahiri ni taa za umeme; mle ndani ilikuwa kana kwamba Danny alikuwa anaogopa giza kwani karibu taa zote zilikuwa zimewashwa na giza lilikuwa bado halijaingia kule nje.

Danny alirudi na glasi ya maji ikiwa na vipande vya barafu. Alimuwekea kwenye stuli iliyokuwa mbele yake iliyochongwa kwa mfano wa mgongo wa tembo na kuwekwa kioo.
"asante" Chausiku alishukuru
"Wabeja kulumba" Danny alisema kwa Kisukuma safi kabisa.
Chausiku alitabasamu kidogo. Waliangalia kidogo tv wakati Danny akitafuta maneno ya kuingia nayo.
"Samahani sana yale yaja, natumaini utakuwa umenisamehe" Nusura Chausiku amjibu kwa kejeli kama angekuwa hajamsamehe asingeenda pale; lakini aliitikia tu na kumhakikishia kuwa amemsamehe.
"Sijui kitu gani kilinipitia, nilivyokuona jana nilichanganyikiwa na nilijiambia moyoni mbinguni wamepoteza malaika" alisema kwa maneno ya kiutongozaji
"hahaha acha vituko, na huyo malaika ndiyo nani?"
"Nani mwingine si wewe jamani" alisema huku akiteremsha sautiy ake chini kwa kibezi cha ukorofi. Joto lilimpanda Chausiku ghafla. Mchirizi wa ubaridi uteremka kuanzia kisogoni, kwenye uti wa mgongo hadi chini kidogo tu ya kiuno. Alimeza fundo la maji.
"Hapa unanizuga tu, wasichana wote ambao unao wote hao si malaika, malaika nije kuwa mimi?" alisema kama kwa kunung'unika lakini akiwa anauliza swali zito.
"Chausiku siwezi kukuficha; ndio nimewahi kuwa na wasichana na hiyo wala si siri. Lakini sasa nimefika mahali nataka kutulia"
"Mmh Danny mimi hapa ni wa kupita tu"
"Una maana gani"
"Nimekuja kwa muda halafu baadaye nageuza kurudi Dar, sasa nikishaondoka itabidi uwarudie wasichana wako siyo?" aliuliza.
"Kama nina uwezo nisingependa uondoke tena; umeondoka mara moja kwenye maisha yangu sitaki uondoke tena". Danny alisema kwa msisitizo huku akihakama kutoka kwenye kocha alilokuwa amekalia na kwenda kukaa kwenye sofa ambayo kama malkia Chausiku alikuwa anatawala. Chausiku hakutarajia kuwa hisia za Danny zilikuwa zimezama hivyo. Akili yake ikamzungusha kupima faida na hasara na akajikuta faida ya kuwa na Danny ilizidi sana hasara ya kutokuwa naye au kuwa na mtu mwingine. Moyo ulimdunda.

"Danny, hata hatujafahamiana tena sasa kuzungumza hayo yote ni ngumu kwangu"
"Mimi sina haraka tunaweza kuchukua muda kufahamiana Chausiku"
"Na hakuna kupiga watu tena!"
"Nakuahidi isipokuwa kama inalazimika" walicheka.
"Ni lazima uwaambie wasichana zako uko na mimi"
"Bila ya shaka"
Kimya kidogo kilitanda hapo. Danny aliuchukua mkono wa Chausiku viganjani mwake na kuuminya kidogo. Chausiku hakumzuia.
"Twende tukazungumzia chumbani basi"
"Tunaweza kuzungumzia hapa hapa bwana" alijaribu kukataa kwa aibu
"Bwana tuzungumze huku tumejilaza chini eh, sitakutafuna acha woga" Chausiku alikaa kimya. Dannya alifanya kitu ambacho Chausiku alikuwa hajajiandaa nacho. Alimvuta karibu na kumteremshia busu la moto na kuligandisha kwa sekunde chache. Kabla Chausikua hajajua la kufanya ulimi wa Danny ulipiga hodi kwa ugomvi. Hakuwa na jinsi isipokuwa kutoa ushirikiano. Pole pole walianza kubusiana huku wakinung'unika; na kwa dakika kama kumi walianza kufanyiana mambo ya mahaba na kama watu hulewa ashki basi Chausiku alikuwa amelewa bwii; alijisikia kizunguzungu chenye raha. Danny alipoinuka na kumnyanyua kwa mkono wake Chausiku alifuata kama ndama anayerudishwa zizini. Au kama mbuzi akipelekwa kwa mchinjaji. Waliiingia chumbani.

Alikuwa amelala bado chumbani akikumbuka yote hayo na yaliyofuatia. Lakini alijisikia kujuta kwani moyo wake ulitamani yote yaliyotokea na maneno yote aliyoambiwa na Danny yangekuwa yametoka kwa Stanley. Alijiambia kuwa maji yameshamwagika na hayawezi kuzoleka. Lakini hakuna mtu mwingine aliyejua; alijipa ujasiri kuwa si lazima ajifunge na Danny namna hiyo kama angeweza kupata namna ya kupata na mahaba ya Stan labda angeweza kweli kufikia uamuzi mzuri wa moyo wake. Alijua ilimpasa kufanya kitu ili asije kujuta baadaye. Alivua nguo zake na kuvaa gagulo lake la usiku na kujilaza kitandani. Alianza kufikiria ni kwa namna gani angeweza kuhakikisha Danny na Stan hawakutani au hawajui jambo hilo. Alipata wazo ambalo alijua anayo masaa tu kuweza kulifanikisha. Kwa mara nyingine hakukuwa na mtu mwingine wa kumsaidia isipokuwa rafiki yake Selina. Alianza kupanga mkakati huku macho yake yakianza kuishia taratibu usingizini.
* * *
SIKU ya Jumatano ilipofika majira ya saa kumi za jioni Stan alibeba kitabu chake cha nyimbo na kudandia baskeli yake kuelekea kanisani kwa ajili ya mazoezi ya kwaya ambapo yeye alikuwa ni mwimbani wa sauti ya tatu. Jua lilikuwa linaaga taratibu kuelekea Magharibi likisindikizwa na upepo wenye joto uliobeba harufu mwanana ya mwisho wa siku. Moyo wake bado ulikuwa mzito na mwili wake bado ulikuwa umebeba maumivu kwenye upande wa kulia wa mbavu zake. Haikumchukua muda alifika pale Kanisani ambapo mara moja macho ya wanakwaya wenzake yalimkaribisha kwa ujumbe wa pole.

"Pole Stan" ndiyo ilikuwa salamu kubwa aliyoipata huku wengine wakilalamika kuwa yule Danny ndiyo ulikuwa mtindo wake huo; mtindo wa kugombana na watu. Wakiwa wanamsubiri mwalimu wao wa kwaya walianza kusimuliana jinsi Danny alivyowahi kupigana au kukoroshina na watu mbalimbali pale kijijini kisa kikiwa ni wanawake au ulevi wake tu. Lakini wote walikubaliana kuwa ilikuwa vigumu kupambana naye kwa sababu anatoka familia ya kitajiri na jina la familia yake lilikuwa linaheshimika sana maeneo ya Bariadi hadi Meatu na Shinyanga Mjini ambapo walikuwa na Hoteli ya kisasa.

Miongoni mwa wanakwaya wengine waliokuwepo pale alikuwepo Selina. Selina alifika dakika chache akiwa ameambatana na kaka yake ambaye alikuwa ndiye mwalimu wa kwaya hiyo. Wakati wanafika wanakwaya bado walikuwa wanacheka na kupiga gumzo huku kila mmoja akiwa aidha ameshikilia daftari lake la nyimbo au ameweka chini daftari hilo huku wakicheka na kutaniana. Kwa Stan ilikuwa ni wakati wa faraja kwani alikuwa yuko katikati ya kundi la rafiki zake ambao wameunganishwa kiroho zaidi. Hata wakati Selina na kaka yake wanafika pale alikuwa tayari ameanza kuchangamka.

Alipomuona Selina moyo wake ulinyong'onyea tena. Selina hakuweza kumuangalia Stan machoni bali aliwasalimia wenzake pale kwa salamu yao ya kikatoliki "Tumsifu Yesu Kristu" na wote kwa mkupuo waliitikia "Milele Amina". Mwalimu Sebastian naye aliwasalimia na kuelekea moja kwa moja ndani huku kundi zima la wanakwaya likimfuatia kama bata anavyofatwa na vifaranga vyake. Kila mmoja alichukua nafasi yake kama ilivyokuwa mazoea na mara moja mazoezi ya nyimbo mpya yalianza; kwani hiyo ilikuwa ndiyo kawaida ya kujifunza nyimbo mpya.

Kwenye majira ya saa kumi na mbili hivi jua lilikuwa linarusha miale yake ya mwisho na kuanza kuzama taratibu. Wakati huo huo kwaya ilikuwa inamalizia wimbo wa nne mpya huku ukisindikizwa na ala za muziki na kufanya anga la eneo la kanisa hilo kupambwa kama vile na sauti za malaika. Waliopita maeneo hayo ya kanisa walijipatia burudani ya bure.

Walipomaliza mazoezi Stan aliagana na wenzake huku akiwa amekumbatia baskeli yake ambapo kwenye kiti cha nyuma aliweka kitabu chake cha nyimbo. Alikuwa yuko karibu kuondoka aliposikia sauti ikimuita.

"Stan!" Ilikuwa ni sauti ya Selina.
"Naam" alijibu na kumgeukia. Kwa sekunde chache hakujua kama alitakiwa kusema kitu au kusikiliza.
"Una muda kidogo"
"Of course, Selinda nini tena?"
"Nina ujumbe wako"
"Kutoka kwa nani tena maana sasa hivi bwana" hakumalizia kauli yake.
"Chiku kanituma, anaomba muonane"
Picha iliyomjia sekunde hiyo ilikuwa ni ya ile ngumi au kibao kilichomfanya aonje ladha ya damu mbele ya kadamnasi ya abiria, vibaka na wapita njia siku mbili kabla. Wazo la yeye kuangushwa tena chini na kuanza kupigwa mateke na kushindwa kujitetea lilimfanyia vinyweleo hadi vya mgongoni kusimama.
"Sijui kama ni wazo zuri hilo Selina, wewe unajua kilichonikuta juzi sitaki kukutwa na makubwa zaidi ya yale" alisema kwa unyonge. Alipanda baskeli tayari kuondoka. Hakuwa na ujasiri wa kumsikiliza Selina akibembeleza.
"Stan, unaniamini?"
"Unajua nakuamini labda kuliko mtu mwingine yeyote ukiondoa familia yangu"
"Basi nisikilize." Stan alijikuta amejifunga mwenyewe kwa kauli yake. Aliinamisha kichwa chini na kujiuma mdomo wake wa chini kwa sekunde moja ya haraka. Alishusha pumzi. Huku shingo yake ikiegemea bega lake la kulia kwa uvivu alimuangalia Selina akiwa tayari kumsikiliza.
"Nakusikiliza"
"Stan, Chausiku anajisikia vibaya kweli na angependa kukuona"Alianza Selina kumpigia kampeni rafiki yake, "Alitaka kuja hapa yeye mwenyewe leo lakini kutokana na mazingira yenyewe hakutaka kukuweka katika hali nyingine ya matatizo". Aliendelea kumuambia jinsi Chausiku alivyoumizwa na kitendo cha yeye kupigwa kwa ajili yake. Sauti ya Selina ilibeba uchungu wa aina fulani; kwa mbali machozi yalimulikamulika.
"Kweli angepena umpe nafasi nyingine" alimaliza.
"Nitaweza vipi Selina lakini?"
"Stan, kesho kuna Sogota kule Ikungulyabashashi na Chiku anataka uende kule" alisema Selina akimaanisha ngoma maarufu ya Kisukuma iliyokuwa ikiongozwa na Maganigani. Maganini alikuwa ni mmoja wa wachezaji mahiri wa ngoma za kisukuma ambaye alijitofautisha na wachezaji wengine wakongwe kwa kubuni mitindo mipya ya kucheza ngoma na uvaaji na kujipatia umaarufu. Kila mwaka kundi lake lililopewa jina lake likicheza mtindo huo wa Sogota lilipita kijiji na kijiji katika mashindano ya ngoma. Kwa hiyo alipokumbushwa kuwa Sogota itakuwa si mbali na pale kijijini japo ni mwendo kidogo alifurahia. Lakini wazo la kwenda mahali kumfuata huyo binti kwa kweli halikumvutia kabisa kwani alishafanya hivyo mara moja na yakamkuta yaliyomkuta.
"Kwa kweli wazo ni zuri lakini nimeshaumwa na nyoka bwana"

"Wewe nenda, yeye haendi kwa ajili yako anataka kwenda ngomani si unajua mtoto wa mjini anataka mambo ya nyumbani kidogo" alisema na kuachia kicheko cha kivivu. Stan hakuwa tayari kushawishika. Alimkatalia Selina kuwa asingeweza kwenda kule kwa ajili ya Chausiku. Aliombwa kusikiliza, alisikiliza na kukataa. Aliamua kuondoka huku akimuacha Selina akiondoka akifuatana na kaka yake. Giza lilikuwa limeanza kuingia na Stan alielekea nyumbani ili kupata chakula cha jioni na baadaye kukutana na rafiki zake ili kupeana michapo ya siku ile. Alitaka kupata ushauri wao.

* * *

Midundo ya ngoma za Maganigani ilikuwa inapasua anga la Ikungulyabashashi. Kati ya ngoma zilizopendwa karibu eneo zima la usukuma ilikuwa ni hiyo ya Sogota. Kundi kubwa lilikuwa limewazunguka wachezaji wa ngoma hiyo huu upande mmoja wapiga ngoma zile kubwa za kisukuma wakiwa wanafuatana kwa namna ya kusisimua macho na mifupa. Wachezaji wa kike walikuwa wamejifunga kiunoni na kifuani kwa kanga zilizofanana. Wachezaji wa kiume walikuwa wamevaa soksi ndefu za rangi nyekundu na nyeupe zilizowabana hadi magotini, na juu wakiwa wameva rangi kama hizo hizo lakini wakiwa wamezingushia tepe mbalimbali. Walikuwa wamependeza kweli. Maganigani mwenyewe ndiyo alikuwa kinara huku akishangiliwa jinsi alivyoweza kujirusha rusha kwa manjonjo ya kila aina. Vigelegele na makofi vilisikika na kufanya usiku huo kuvuta watu wengi kutoka vijiji vya jirani na hata vijiji vya mbali.

Ilipofika majira ya karibu saa nne za usiku ngoma zilinoga. Na ilikuwa ni kawaida ya Maganigani kuruhusu mashabiki wake kuingia kati na kujimwaga. Selina, Chausiku na wasichana kutoka bariadi hawakuchelewa kwani hicho ndicho kilichowapaleka pale usiku huo. Mdundo wa ngoma ukaanza na mabinti walikuwa kama waliopagawa. Waliungwa mkono na kundi la wasichana wengine kutoka Gamboshi, Kasoli, Mhango, Mwamapalala na hata sehemu za mbali kama Malita. Wote waliingia na kucheza kwa zamu wakipokezana. Kijasho kiliwatoka. Miili yao ilisisimka.

Vijana wa kiume nao hawakuchelewa, na wenyewe wakaanza kuingia kwenye ngoma hiyo ya Sogota. Kila mmoja alitamani kujirusha alipoona kundi la wasichana wageni wameingia kucheza. Simon, na wenzake nao walikuwa wanaangalia kwa pembeni tu. Mara ya tatu Selina na Chausiku na wenzao wakaingia tena kujimwaga. Mlio wa filimbi na vigelegele ulitosha kabisa kuwashawishi kina Simon nai kuingia tena. Watu waliripuka kwa furaha maana kundi hilo la vijana lilikuwa na mbwembwe; walimfanya Maganigani mwenyewe kucheza nao.

Stan alishindwa kujizuia. Mwili wake wote ulipiga kelele "cheza cheza". Alikuwa amesimama pembeni akiwaangalia kina Selina na macho yake yalikuwa kwa Chausiku ambaye alionesha umahiri mkubwa wa kuvingirisha vingirisha kiuno chake kwa mbwembe na midadi. Alishangiliwa kila wakati kibwagizo kilipopiga na yeye kuanza kucheza kwa kukatika huku akigandisha kufuatisha mapigo ya ngoma. Stan akaamua kujiingiza kwenye ngoma hiyo na kushangiliwa.

Stan alisifika kijijini hapo kwa kucheza Sogota. Usiku huo wote walikuwa wanamuuliza kwanini hachezi kwani walizoea kumuona kwenye mashindano hayo na amewahi kushinda katika tarafa yao. Alipoingia mlio wa ngoma ulizidi, vigelegele na filimbi zilipulizwa kwa nguvu zaidi. Kulikuwa na manyunyu ya mvua yameanza kuanguka na kuchanganyika kwake na udongo kulileta harufu ya vumbi katika anga la ngomani pale. Mwanzoni walikuwepo wachezaji kumi na mbili lakini alipoingia Stan walibakia wachezaji sita tu; wakilingana wakiume na wa kike. Stan alicheza nyuma ya Chausiku.

Walinguka wakifuata ngoma na kwa madaha na macho ya watazamani yaliwaangalia Stan na Chausiku walivyokuwa wakicheza wakipeana midadi. Kilipopigwa kibwagizo cha "geuka ucheze naye" watu walipagawa kwani wawili wawili hao waligeukiana na kucheza wakitazamani huku wakizungusha viuno vyao. Macho ya Stan yaliwaka tamaa; lakini ya Chausiku yalizidi.

"Lele lele lelele, aie asusa" manju alirudia kwa sauti na kuitikiwa. Ulikuwa ni wimbo walioiba toka mojawapo ya vikundi vya utamaduni vya Tanga na wakauingiza kwenye nyimbo zao. Kwa kadiri kibwagizo kilivyonoga ndivyo wachezaji walivyozidi kusogeleana kila ilipofika "geuka ucheze naye". Stan na Chausiku wao walienda mbali zaidi kwani walipogeukiana mara yatu kulikuwa na "zeto distance" kati yao. Miili yao iligusana, harufu ya jasho na manukato ilichanganyikana; macho yao yalipokodoleana ni wazi kulikuwa na sumaku kati yao, sumaku ya mapenzi iliyopita mapenzi tu ya muda. Ilikuwa ni kiu na njaa ya mahaba kati yao.

Walipogeuka kuendelea kuzunguka tena Stan alijikuta anageuka na kuangaliana na Danny aliyekuwa mstari wa mbele kama mita moja na nusu tu kutoka alipokuwepo yeye. Nusura azimie. Macho yake yaligongana na ya Stan na neno ghadhabu halikutosha kuelezea kilichokuwemo kwenye macho yale. Stan alijisikia kutetemeka na pamoja na jasho lote la usiku ule alijisikia ubaridi hadi kwenye unyayo. Alijaribu kuyaepesha macho yake na kuangalia chini. Danny alikuwa ameshika kitu kinachong'ara mikononi mwake. Stan alitaka kukimbia, alitaka kupiga kelele kutahadharisha watu. Alichelewa.

Danny alipiga hatua mbili tu na hakufanya wajia alinyanyua kisu chini kwa chini bila kukiinua juu na kumsogelea Stan ambaye alikuwa amepigwa na bumbuwazi. Ni wakati huo huo Chausiku aliona kitendo hicho; alipiga kelele "ana kiisu!!" Wote walichelewa. Stan hakujua kilianza kuingilia upande gani. Ngoma ilizimika na kelele huku watu wakikimbia kutawanyika kwani hawakujua nini kinaendelea hapo. Stan alifanikiwa kupiga ukelele mmoja tu "nakufaaaaa". Selina naye alikimbia hapo wakati mmoja na Chausiku.BUSU LA MSHINDI

Kundi la wanakwaya kutoka Katoliki la Bariadi mjini la Mt. Yohana au maarufu kama kwa Fr. Gappa walikuwa wamekusanyika nje ya hospitali ya Wilaya ya Bariadi. Pamoja nao walikuwepo marafiki na jamaa wa karibu wa Stan. Walikuwa wanapata watu karibu ishirini hivi wote wakiwa wamemzunguka mwenyekiti wa vijana wa parokia hiyo aliyeitwa Aquilina Manumbu. Aquilina alikuwa ameshikilia rozali mkononi akiwaongoza wenzie katika kusali mafungu ya mateso. Vijana wengine wengi walianza kukusanyika hospitalini hapo majira ya saa nane za usiku mara tu walipopata taarifa ya kuchomwa kisu kwa Stan kwenye ngoma ya Sogota kule Inkulyabashashi. Simon na wenzake nao walikuwa na mgongwa tangu wakati wa tukio na walienda naye pamoja akiwa anavuja damu. Walimkimbiza kwa kutumia gari la mfanyabiashara mmoja ambaye aliamua tu kupumzika pale akiwa Safarini kwenda Mwanza na alikuwa amesikia sifa za Sogota na kutaka kushuhudia.

Alipofikishwa hospitali Stan alikuwa hajitambui na moja kwa moja alikimbizwa chumba cha upasuaji ambapo juhudi kubwa za kuyaokoa maisha yake zilifanyika. Jambo la kwanza ambalo madaktari na wauguzi walifanya ni kuhakikisha kwanza haendelei kupoteza damu na wakati huo kuchukua vipimo vya X-rays ili kuweza kuona ni madhara gani yalikuwa yamemfikia kutokana na kujeruhiwa huko. Walifanikiwa kumuweka katika hali ya kutengemaa karibu sa kumi za alfajiri wakiongozwa na Dk. Pius Katogoro, mganga mkuu wa wilaya hiyo. Ilipofika saa kumi na moja za alfajiri upasuaji wa kwanza ulikamilika ambao ulifunga jeraha kubwa upande wa kushoto chini kidogo tu ya moyo wa Stan. Ilipofika saa nne za asubuhi upasuaji wa pili mkubwa ulikamilika ambao ulifunga jereha kubwa upande huo huo wa kushoto ambapo kisu kilipopenya kilipasua mbavu moja na kuchana pafu la kushoto na kusababisha maumivu makali sana. Stan alipofikishwa hospitali alikuwa tayari amepoteza fahamu na sauti pekee aliyoitoa ilikuwa ni ya mguno.

Wanakwaya na kundi la vijana pale nje walikuwa wanaendelea na sala zao huku kila mmoja akiwa hajui nini cha kufanya au nini kilikuwa kinaendelea kule ndani. Hata hivyo kule ndani, Stan alikuwa amepepelekwa kwenye chumba cha uangalizi wa karibu (ICU) akiwa amewekewa mashine ya kumsaidia kupumua, amefungwa dripu ya damu na dripu ya maji. Vile vile alikuwa amewekwa mirija mbalimbali kutoka kifuani ambayo ilikuwa ikifuatilia hali ya moyo wake.

Pembeni yake alikuwepo mama yake na dada zake Belinda na Suzy ambao waliruhusiwa kuwa humo majira ya saa tatu nne na nusu mara baada ya Stan kuletwa kwenye chumba hicho cha wagonjwa mahututi. Waliambiwa wasimsumbue mgonjwa na wamuangalie tu kwani hali yake haikuwa nzuri bado. Alikuwa anapigania uhai wake. Machozi yalikuwa yanatiririka kwenye mashavu ya Susan bila kukoma. Belinda naye alikuwa anavuta makamasi tu huku macho yake yakiwa yamevimba kwa kulia karibu masaa yote tangu taarifa hizo za kujeruhiwa kaka yake zilipowafikia. Mama yao alikuwa hajalia bado; uso wake ulikuwa umejaa mshangao wa simanzi. Hakusema lolote wala kuonesha kitu chochote zaidi ya kumkazia macho mtoto wake aliyelala hospitalini hapo. Aliomba malaika, watakatifu na mizimu ya mababu zake kumuonea huruma mtoto wake huyo.

"Samahani mama" nesi mmoja aliingia na kuwaomba radhi
"Bila ya samahani sista" mama alimjibu
"Padre Gappa amekuja, aingie?"
"Bila ya shaka"
Pd. Gappa aliingia mle chumbani na kuwasalimia kwa kisukuma na kusemezana nao kwa kisukuma akiwapa pole. Lafudhi yake ya Kisukuma ilikuwa imechanganyika na lafuthi yake ya Kimarekani nchi ambayo alikuwa anatoka. Fr. Gappa alijulikana kila sehemu pale Shinyanga na katika kuta za Kanisa Katoliki nchini jina lake halikuwa geni kabisa. Alikuwa anasifiwa kwa kuokoa Bariadi iwe jangwa kwa kampeni yake ya kupanda miti. Haikumchukua muda Pd. Gappa alifungua mkoba wake na kuanza kutoa huduma ya sakrementi ya Mpako wa Wagonjwa. Miongo michache tu Sacrementi hiyo ilijulikana kama Sakramenti ya Mpako wa Mwisho na watu walisubiri hadi dakika za mwisho kabisa kuomba padre aitoe wakiamini kuwa mgonjwa yuko karibu kuaga dunia. Ni miaka iliyofuatia Mtaguso wa Vatican II ndiyo sakramenti hiyo imekuwa ikitolewa katika hali ya ugonjwa na haikuhitaji mtu awe mahututi ili apatiwe. Hata hivyo siku hiyo ilionekana kweli ilikuwa ni huduma ya mwisho toka kwa padre yule yule aliyembatiza Stan akiwa mtoto mchanga. Ilikuwa ni huduma ya faraja.

Stan hakujua nini kinaendelea; alikuwa bado amefumba macho yake. Mara baada ya kumaliza huduma hiyo Pd. Gappa aliwaaga kwa maneno ya faraja na kuwabariki na kuwaambia wampatie taarifa wakati wowote hali ya mgonjwa ikibadilika. Mama na binti zake walibakia tena peke yao. Walitamani mzee Maduku angekuwepo. Waliomba awaangalie na kuwaombea huko aliko.

Kwenye majira ya saa sita hivi za mchana nesi aliwaomba wanafamilia hao wampishe ili aweze kumpatia huduma mbalimbali mgonjwa na kuangalia majeraha ya upasuaji yanaendeleaje. Walipotoka tu kwenye chumba cha uangalizi maalum kulikuwa njia fupi iliyowafikisha kwenye sehemu ya wageni kungojea wagonjwa wao ambayo nayo ilikuwa na watu wengi kidogo. Belinda na Suzy walikuwa wameshikana mikono wakitembea sambamba na mama yao wote watatu walikuwa wamejifunga kanga kiunoni na kuzungushia upande mwingine mabegani. Mama yao alikuwa amevaa na kilemba vile vile.
Waliona viti vitatu vilivyokuwa wazi pamoja. Walipoketi tu mara kwenye mlango wa kuingilia ukumbi huo kutoka jengo la wagonjwa wa nje ukafunguliwa. Chausiku na Selina waliingia hapo taratibu na kutoka mahali ambapo mama Maduku na bintize walipokuwa wameketi waliweza kuonana nao uso kwa uso. Kidogo Chausiku akasita na nusura amfanye Selinda kujikwaa nyuma yake. Kwa mwendo kama wa kutokuwa na uhakika alielekea walipoketi kina Suzy.

Suzy uvumilivu ukamshinda.
"Unafuata nini hapa!" alisema kwa sauti ya juu akiinuka kutoka kwenye kiti chake. Ukumbi mzima uliingiwa na ukimya wa ghafla huko maneno hayo yakiacha mwangwi uliotikisa mapazia meupe ya ukumbi huo. Ilikuwa sauti kali iliyojaa hasira, uchungu, mshangao na aina ya chuki ambayo maneno yasingeweza kuifafanua. Selina na Chausiku walijikuta wanafunga breki ghafla kwa pamoja kabla hawajaendelea mbele, macho yao yalimuangalia mama Stan. Walitetemeka mikono, miguu hadi nywele zao. Waliweza kuyasikia macho ya watu wote yakiwaangalia kwa mshangao.
"Suzy embu waache wenzio" mama akajaribu kumtuliza binti yake kwa sauti ya upole. Belinda naye akadakia.
"Mama, hawa wanafuata nini hapa? Hawa ndio sababu kaka yuko hapa" Belinda naye alisimama . Kimaumbile na kiumri Suzy na Belinda walikuwa ni wadogo kulinganisha na Selina na Chausiku, lakini walivyosimama mbele yao wazo la Daudi kumpiga Goliathi lilionekana linawezekana sana.
"Samahani Belinda" Chausiku alijaribu kusema kitu
"Samahani yako itatusaidia vipi?" Suzy akang'aka na dada yake naye akadakia.
"Unafikiri samahani yako itamsaidia kaketu sasa hivi?"
Selina alikuwa amejiinamisha kichwa chake machozi yakimtoka. Hakujua aseme nini. Mama Stan aliamka na kuwageukia watoto wake kwa ukali ambao hawakuwa wamewahi kuuona.
"Nyinyi mna wazimu!? Embu kaeni chini" alifoka akitumia sauti yake ambayo alikuwa anaitumia darasani wakati watoto walipojaribu kuwa watukutu. Belinda na Suzy walijikuta wanakaa chini ghafla huku bado wakitetemeka kwa hasira.
"Wenzenu wamekuja kuwapa pole, kwanini msipokee?" aliwauliza na wote wakadondosha macho yao chini. Akawageukia kina Chausiku na kuwakaribisha kwa kuwanyoshea mkono wake kuwasalimia. Mabinti hao walishukuru mbingu kwa kitendo hicho. Wakamuamkia na kumpigia goti kila mmoja kusindikiza maamkizi yao. Lile goti la Kisukuma. Walimtaarifu mama Stan kuwa kule nje kuna kundi la wanakwaya na marafiki wa Stan wanamuombea apone. Mama Stan hakuamini; alihisi kutaka kulia. Lakini alijiambia ni wakati wa kugangamala na si wakati wa kulia. Aliwaagiza mabinti zake wasibiri pale ili aende nje kuonana na kuwapa taarifa kidogo za maendeleo ya mgonjwa. Chausiku na Selina waligeuza na kuelekea walikoingilia; mama Stan alikuwa nyuma yao huku akiizungusha tena vizuri kanga yake mabegani mwake.

Walipotoka nje hakuamini macho yake. Kulikuwa na vijana karibu mia moja wakiwa wamekaa katika kundi moja wakiimba mapambio na kusali. Kila baada ya kumaliza rozari moja waliimba mapambio. Walipomuona tu wote walikaa kimya, huku macho yake yakifuatia hatua zake alivyokuwa akiwaelekea.
"Mama pole na mgonjwa" alisema Aquilina huku wenzie nao wakirudia pole hizo.
"Asante sana"
"Mgonjwa anaendeleaje"
"Hivyo hivyo tu, asanteni kwa sala zenu" aliwapa taarifa kwa ufupu juu ya hali ya mgonjwa na upasuaji uliofanyika na hali aliyokuwa nayo. Walikuwa wameshapata taarifa kidogo toka kwa Pd. Gappa lakini walipomsikia mama huyo wengine walibaki wanamshukuru Mungu. Aliwahakikishia kuwa Stan alikuwa anahitaji sana sala zao kama ataweza kuvuka hapo. Aliwaambia kwa sasa hakuna la kufanya na wangeweza kwenda nyumbani na labda kuanzia kesho kama hali itakuwa imepata unafuu wa kutosha watamhamishia chumba cha wagonjwa wa kawaida ambako angeweza kupokea wageni.

"Mama tumechanga kidogo kutoa pole yetu" Regina alisema akimkabidhi mama Stan bahasha ya kaki iliyokuwa na fedha taslimu ndani yake. Juu yake ilikuwa imeandikwa Pole Stan - 245,300Tsh. Kiasi hicho kutoka kwa vijana hao kilikuwa kikubwa kuliko alivyotarajia. Mama Stan hakutegemea kabisa alishukuru na machozi yalianza kumlenga lenga kwa mbali; alijikaza tena kwa kujiambia kuwa huo haukuwa wakati wa kulia.

Baada ya dakika chache aliwashukuru na kuwaaga kurudi ndani kuungana na binti zake. Vijana waliamua kusali rozali ya Utukufu na mmoja mmoja wakaanza kutawanyika kutoka hospitali hapo. Hadi wote kuondoka pale ilikuwa imefika saa tisa kamili. Saa kumi walikuwa wamekubaliana kuwa na misa ya kumuombea Stan kabla hawajaanza mazoezi ya kwanya siku hiyo.

Mida hiyo hiyo kaka yake mkubwa na Stan naye alikuwa amewasili hapo hospitali moja kwa moja akitokea Mwanza. Aliwashukuru vijana waliokuwa bado wanarandaranda hapo na kuelekea ndani ambako alikumbatiana na dada zake na mama yake na kuwapa pole kwa kuuguza. Aliwaruhusu waende nyumbani kuandaa chakula cha jioni na yeye atabaki na mgonjwa. Ukawa ni mwanzo wa kupokezana kumuuguza mgonjwa kati ya wana familia hiyo. Kaka mwingine wa baba yao mdogo kutoka Shinyanga naye alikuwa yuko njiani.

* * *​

Stan alikaa hospitali kwa takribani mwezi mzima na nusu. Tangu ajeruhiwe zilipita siku tano ndipo alipoanza kurejewa na fahamu yake. Ilimchukua muda kuweza kuelewa mambo mbalimbali yaliyoendelea tangu siku ile ya Sogota. Aliendelea kupata matibabu hapo hospitali chini ya uangalizi maalum kwa wiki nyingine tatu kwani wakati kidonda cha ubavuni kilipokuwa kinapona wakakuta kuwa amepata maambukizi mengine pale hospitali ambayo yaliongezea haja ya uangalizi maalum.
Wiki ya nne akiwa hospitali Stan aliweza kuketi vizuri na kuzungumza. Kwa karibu wiki nne tangu ajeruhiwa Selina na Chausiku walikuwa wanaenda kumuangalia pale hospitali. Hakukuwa tena na ugomvi kati ya Suzy na Belinda dhidi ya mabinti hao. Hawakuwa wanazungumza vizuri lakini walikuwa wanavumiliana tu kwa ajili ya mgonjwa.
Ilipoanza wiki ya tano, Selina alikuja peke yake kumuona kitu kilichomshangaza Stan ambaye alikuwa anasubiri kwa hamu kila siku kumuona Chausiku.
"Chausiku yuko wapi?" Stan alimuuliza Selina ambaye siku ya mwisho pale hospitali alikuja peke yake.
"Ameshindwa kuja leo"
"Kuna tatizo?"
"Hapana alikuwa anjiandaa kuondoka kurudi Dar"
"Sasa ndio ameshindwa kuja kuaga?"
"Amesema atajaribu kuja jioni" Selina alijibu. Hakuja siku hiyo.

Stan aliruhusiwa kutoka hapo wiki mbili baadaye akiwa amekosa jibu la uhakika la kwanini Chausiku aliacha kuja kumuanglaia hospitali. Alikuwa bado anachechemea kidogo lakini kwa namna bora zaidi alikuwa amepata nguvu mwilini na utengemavu. Macho yake maangavu yalikuwa bado yanawaka kwa furaha ya maisha. Alipofika nyumbani alikuta nyumba imepambwa kwa maua na wanakwaya wenzake walikuwa wanamsubiri na kumpigia vigelegele. Waliamua kumuandalia tafrija fupi ambayo iliambatana na kuchinjwa mbuzi. Vijana wote na familia nzima ilikuwepo kufurahia uwepo wake hapo. Tafrija yenyewe ilitanguliwa na Misa ya Shukrani iliyoongozwa na Pd. Gappa. Tafrija iliendelea usiku huo wa Ijumaa hadi karibu saa sita za usiku. Stan alikuwa ameketi tu kwenye kiti chake akifurahia muziki na stori za marafiki zake. Wakati wanaelekea ukingoni Selina alikuja na kumnong'oneza kitu Stan.
"Yuko wapi"
"Sebuleni" Stan aliamka taratibu na kuelekea sebuleni. Sebuleni alimkuta Mzee Mswahili na Chausiku. Mama Stan naye alikuwa yupo hapo. Baada ya kumuamkia mzee huyo Stan aliketi kwenye kochi akiangaliana moja kwa moja na mzee Mswahili.
"Stan, mjukuu wangu tumekuja usiku huu" alianza mzee Mswahili, "kutaka kukuomba radhi kabisa ya familia yetu kwa yote yaliyokukuta" alisema mzee Mswahili. Stan alishangaa kama hilo lilikuwa jambo muhimu hivyo lingeweza kusubiri hata kesho yake. Hakuona um,uhimu wa wao kuja usiku huo, hakusema kitu.
"Na hasa ndugu yako huyu aje akuombe radhi yeye mwenyewe" alisema mzee Mswahili huku akielekeza mkono wake kumwelekea Chausiku ambaye wakati wote huo alikuwa ameinamisha kichwa chake. Alipoinuka macho yake yalikuwa yamelowa machozi. Kulikuwa na ukimya.
"Mwombe msamaha ndugu yako"
"Stan samahani" alisema maneno hayo mawili kwa unyonge, hatia na uchungu mkubwa. Alijipangusha macho yake huku akivuta makamasi yasimdondoke. Mama Stan alijikuta anaanza kuchuruzika machozi kwenye mashavu yake; machozi ambayo yalitapanyika kufuata makunyazi mepesi ya uso wake wa kiutuzima. Stan alikuwa hana la kusema. Lakini aliamua kukiri mbele ya mzee Mswahili kuwa alimpenda sana Chausiku na wala hana kinyongo naye kabisa na kuwa kama ingekuwa ndani ya uwezo wake angeweza hata kwenda kuchumbia huko. Kwa kawaida mambo hayo huzungumzwa na washenga katika mazingira maalum siyo kama yaliyokuwa wakati huo. Mzee Mswahili mwenyewe alikiri kujua hilo kwani alikumbuka jinsi Stan alivyomuangalia Chausiku siku ile alipoenda pale nyumbani kwake. Ukimya ulitanda tena.
"Tumekuja usiku huu kwa sababu kesho asubuhi Chausiku anaondoka kurudi Dar"
"Mbona haraka nilidhani alipanga kuwepo hapa hadi x'mass?" alishangaa mama Stan
"Ndiyo lakini naona wazazi wake wametaka arudi kule mara moja" Hakukuwa na ubishi. Chausiku bado alikuwa analia. Baada ya mazungumzo hayo mafupi Mzee Mswahili na Chausiku waliaga na kutoka nje. Ngurumo ya gari iliwapokea na Stan alitaka kuangalia ni gari lakini hakuwana haraka ya kuweza kuliona alipoinuka hadi kufika mlangoni gari lilikuwa linamuaga kwa mbali kwa taa zake za rangi ya chungwa zikitokomea gizani.

Ulipita mwezi mwingine mzima wa majonzi na uchungu. Stan alikuwa amerejea katika afya yake kwa kiasi kikubwa sana kiasi cha kuweza kwenda na marafiki zake kuangalia mpira na kuanza tena kuimba kwaya. Maandalizi ya siku kuu ya Krismasi yalikuwa yamepamba moto. Tukio la kujeruhiwa kwake lilibakia kuwa ni la masimulizi kijijini pale. Danny alirudi kijijini pale na hakuna lolote lililotokea kwake. Aliendelea kuwa mtu huru mtaani pale.

Siku mbili kabla ya Krismasi Selina alimtafuta Stan baada ya mazoezi pale Kanisani. Ilikuwa ni majira ya saa kumi na mbili na nusu hivi; Mwalimu Sebastian alikuwa anamalizia kufanya masahihisho kwa wanakwaya na kujaribu kupanga nao orodha ya nyimbo za Krismasi. Selina alimfuata Stan aliyekuwa nje akipiga soga na vijana wenzake wa sauti ya tatu na sauti ya nne.
"Nina ujumbe wako kaka Stan" Selina alisema baada ya kuwasalimia vijana hao.
"Mmh, kutoka wapi tena jamani" ubaridi mwingine ulimjia ghafla; alijihisi kunyong'onyea.
"Usiogope nimepata barua toka kwa Chausiku" alimuambia na kumnyoshea mkono uliokuwa na barua iliyokunjwa vizuri lakini ikiwa nje ya bahasha yake.
"Imekuja lini"
"Nimepata leo hii ilikuwa na barua yangu vile vile" Selina alimjibu. Mara baada ya kumkabidhi alimuaga na kurudi ndani kumsubiri kaka yake. Stan aliichukua hiyo barua na kuiweka mfukoni. Hakutaka kuisoma hapo akiwa amepania kuisoma mara akifika nyumbani. Alipiga soga tena na wenzake kwa muda kidogo na kuwaaga kuelekea nyumbani kwao. Mara baada ya chakula cha jioni aliwaaga ndugu zake na kwenda chumbani kwake ambako aliwasha taa na kuichukua barua iliyokuwa mfukoni mwake; aliketi kwenye kiti kilichokuwa karibu na kitanda chake huku akiiweka barua hiyo juu ya meza. Pole pole alianza kuisoma neno kwa neno, mstari kwa mstari:

Mpendwa Stan,

Salamu nyingi zikufikie hapo nyumbani wewe, mama pamoja na Belinda na Suzy. Ni matumaini yangu kuwa wote hamjambo kabisa na mnaendelea vyema na shughuli zenu za kila siku. Upendapo kujua hali yangu, miye mzima lakini mwenye huzuni tele.
Stan, kosa kubwa nililolifanya kwako ni kutokuwa tayari kupokea ukweli wa upendo wako siku ile ya kwanza ulipokuja nyumbani. Nilikuwa natamani sana niwe na wewe lakini kiburi changu kilinilazimisha kutaka nikuone ukiteseka kunipata. Sikutegemea mateso hayo yangekuwa yale ya kujeruhiwa na kuumizwa; nilidhani ningekusumbua tu kidogo halafu tuweze kuwa marafiki wapendanao. Katika kufanya hivyo nilitaka kukupa wivu siku ile pale stendi ya basi; kwa kweli siku ile ni kweli nilikuwa nimefurahi kumuona Danny lakini furaha yangu kubwa ni kujua ulikuja kuonana nami. Nilipokuona niliamua tu nitakuwa na wewe lakini nilitaka upate wivu kidogo. Sikutarajia kabisa kwamba Danny angekushambulia namna ile. Naomba unisamehe sana.

Nilifanya kosa jingine kwani niliingiwa na majaribu nilipoenda kwa Danny na ushawishi wake ulinifanya nijisikie kama ningeweza kuwa na pande zote mbili. Nilifanya kosa zaidi nilipokubali kulala naye nikiamini ningeweza kumfanya awe kama buzi langu hivi wakati nikiwa hapo kijijini. Nasikitika kuwa sasa hivi nina ujauzito wa miezi miwili. Hiki ndicho kilichonifanya niondoke kijijini hapo mapema kuliko nilivyotarajia.

Sina mengi ya kusema ila naomba msamaha sana kwani nina uhakika nilikuwa chaguo la moyo wako lakini mimi japo ulikuwa ni pendekezo langu niliusaliti moyo wangu kwa kutokuchagua wewe kuliko kitu kingine chochote. Nakutakia maisha mema huko mbeleni na mafanikio na nitafurahi kusikia kuwa umenisamehe.

Pse. Ukinisamehe nitakuja tena nikuombe "msamaha" kiukweli.

Mwenye jeraha la moyo,

Chausiku
Stan alishindwa kujizuia; ilikuwa ni zamu yake kulia. Alijua katika shindano hilo ni yeye aliyeshindwa. Hakutaka kusema lolote isipokuwa alijisikia uchungu sana. Alijilaumu kumpenda mtu asiyejua kupenda na ambaye kwake mapenzi ilikuwa ni mchezo wa aina fulani. Alitamani ardhi ipasuke ili adidimie na kusahauliwa. Hakutaka kuirudia barua ile tena lakini bado ilikuwa mikononi mwake akijiuliza afanye nayo nini. Aliamua kurukia kitandani katika majonzi; alijua Krismasi ya mwake ule ilikuwa ni mbaya na angekuwa na uwezo asingeshiriki kabisa. Aliwaza taratibu jinsi gani moyo na mwili wake ulivyojeruhiwa kwa kupenda mtu asiyependeka. Usingizi ulimchukua taratibu akiwa amechoka kufikiria na kuhuzunika. Aliingojea siku ambayo angeweza kweli kupata nafasi ya kuwa na Chausiku.

* * *​
Usiku wa harusi ulikuwa ni wa kukumbuka. Aliyewafungisha ndoa hakuwa mwingine isipokuwa Pd. Gappa. Harusi ilifungwa pale Parokiani kwenye Kanisa la Mt. Yohana la mjini Bariadi. Ilikuwa mojawapo ya harusi za kukumbukwa katika mji wa bariadi. Harusi yenyewe ilinogeshwa na ushiriki wa Maganigani mwenyewe na kundi zima la wachezaji wa ngoma wa Sogota. Pale walipotangazwa kuwa sasa ni mume na mke, kanisa zima lilirindima kwa ngoma za kisukuma zilizopambwa kwa midundo ya mahadhi ya kumfanye hata kiziwe afuatishie mapigo yake.

Sherehe za harusi zilifanyika katika ukumbi mkubwa wa parokia hiyo hiyo. Bibi harusi alikuwa ameshabadilisha kutoka gauni lake la harusi na kuvaa gauni linalobana la rangi nyeupe inayong'ara na kuvaa shela fupi kidogo. Alikuwa amevaa glovu nyeupe za kumetameta. Alikuwa amependeza sana na akiwa amekete pembeni alipendeza kama malkia pembeni ya mfalme wake. Watu walitoka sehemu mbalimbali kwa ajili ya harusi hiyo; kuanzia Dar-es-Salaam, Shinyanga, Tabora na Mwanza. Wengi waliohudhuria sherehe hiyo ya harusi walifanya hivyo kwa ajili ya kumhusudu Stan na hasa kwa kile simulizi la yaliyomkuta lilikuwa limetangaa karibu eneo zima la Shinyanga, habari za harusi hiyo zilifika hadi Sayu Sayu na Ngoleleji hadi mpakani kabisa mwa Tabora.

Saa tano na nusu bwana na bibi harusi waliaga ukumbini ili waende kupumzika hotelini ambako walikuwa wamekodisha kwa wiki hiyo. Walisindikizwa na kaka zake Stan na kuachwa hapo wapumzike. Chumba chao cha harusi kilikuwa kimepambwa vizuri na kitanda kilikuwa kimefunikwa mashuka mekundu ya hariri yaliyokuwa na michirizi ya rangi nyeupe.
Bibi harusi aliingia bafuni kubadilisha. Stan alivua suti yake pale pale chumbani na kuirusha kwenye kochi lililokuwa pembeni na kubakia na nguo za ndani tu. Alipanda kitandani. Bibi harusi alikuja akiwa amebakia na nguo ya ndani na sidiria tu. Mwanga hafifu wa taa nyekundu ulimfanya apendeze na kuonekana kama mtu wa kwenye njozi. Mkufu wake wa dhahabu aliopewa zawadi na mumewe ulining'inia kifuani, ulikuwa umetundikiwa kidani chenye umbo la mioyo miwili iliyoungana. Pete ya dhahabu ya ndoa iliyokuwa imechirizwa majina yao ilitulia kwenye chanda chake.
"Mpenzi wewe ni mzuri" Stan alishindwa kujizuia
"Wewe zaidi Mr. wangu" walicheka. Bibi harusi alipanda kitandani na kukaa juu ya Stan aliyekuwa amelala chali anamuangalia. Alijiinamisha na kumpatia busu la taratibu. Stan alizungusha mikono yake mgongoni kwa mke wake na kufungua kifungo cha chuma kilichounganisha sidiria yake. Ilipofunguka tu matiti yake yakaajiachia. Alimsaidia kuivua. Alipomaliza tu bibi harusi alirudi kumbusu tena mumewe. Lakini haikuchukua sekunde kwani Stan alimzungusha mke wake huyo na kumgeuza awe chini ili yeye awe juu. Ulikuwa ni usiku wao wa ndoa. Ilikuwa ni ahadi ya bibi harusi kutokutana naye hadi usiku huo wa ndoa. Alikuwa na hamu na shauku. Hakutaka kuwa na papara. Taratibu alimchojoa mke wake nguo iliyosalia mwilini
Alipopiga hodi kwenye malangu ya utukufu wake wa kike, yaliyopambwa kwa visima vya maji ya kheri Stan alishindwa kujizuia. Alimuita jina lake kama vile kwa mara ya kwanza.
"Stan!" alimuita nayeye kwa sauti ambayo aliapa ingekuwa kila mtu anajaliwa sauti moja tu ya mwisho kabla ya mauti basi hiyo ndiyo ilikuwa chaguo la moyo wake.

Waliibariki ndoa yao katika utakatifu wake wote. Ilikuwa ni ndoto ikitimia. Uchaguzi wa moyo wake ulitimia. Alikumbuka jinsi alivyokata tamaa kumpata Stan, na alikumbuka usiku ule wa Krismasi mwaka mmoja kabla; usiku uliofuatia matukio ya machungu na huzuni ya Stan kushambuliwa na Danny katika sakata lililoshuhudiwa na rafiki yake kipenzi. Alipata faraja kwani siku ile rafiki yake naye alikuwepo kama alivyokuwa katika maisha yao yote na alikuwa ni msaada mkubwa wa kuwaandaa marafiki wa kike wa bibi harusi.
Bibi harusi alitoa ushirikiano wote wa mapenzi kwa mume wake kwa mara yao ya kwanza. Alijichekea moyoni, jinsi gani aliweza kumpata mwanamme pekee aliyemuwazia na kumtamania tangu utoto. Lakini ni usiku ule wa Krismasi mwaka mmoja kabla ndio aliamini kweli bahati ilibarikiwa na neema ilituzwa. Usiku wa kuzaliwa kwa penzi kati yao. Walimaliza kuibariki ndoa yao na walibaki wamekumbatiana, Stan akiwa na uso angavu wa shujaa aliyekamilisha kazi kubwa aliyopewa na moyo wake. Alikuwa amejaa matumaini.
"Mpenzi, nakupenda"
"Nakupenda mfalme wangu"
"Siwezi kusahau Krismasi, ulivyonikatalia nilidhani unanitania"
"Nilikuahidi zawadi yako ya uvumilivu"
"Asante sana furaha yangu"
"Wabeja kulumba wa ngosha" Walicheka. Walibusiana tena na kucheka. Alimpapasa mumewa wake kifua chake, na yeye alichezea nywele zake zilizokuwa na harufu nzuri. Walikumbushiana usiku ule wa Krismasi ambao siku hiyo ilikuwa ni tunda lake kuu. Walibusiana tena. Walicheka. Walikumbuka.

* * *​
Mama Stan aliwakaribisha ndugu, jamaa na marafiki wengi kwa siku kuu ya Krismasi pale nyumbani. Miongoni mwao ilikuwa ni familia ya mwalimu Sebastian ambaye alikuja na mke wake na mtoto wake wa kiume na pamoja naye alikuwepo Selina vile vile. Kulikuwa na vyakula vingi pale nyumbani ambapo kundi la kina mama wa UWATA walishiriki kupika na tafrika kwa kweli siku hiyo ilikuwa nyumbani kwa kina Stan. Baada ya kula pilau la nguvu pamoja na kuteremshia kwa vinywaji mbalimbali vya moto na vya baridi jenereta liliwashwa na na kijana mpiga muziki kutoka Magu alikuwepo na vyombo vyake. Kulikuwa karibu watu mia hamsini pale nyumbani wakila na kunywa na kucheza muziki chini ya usiku mwangavu wa mbalamwezi.
Stan alikuwa mwenye furaha sana na siku hiyo alikuwa amechangamka kupita kawaida. Kwenye majira ya saa tatu za usiku muziki ulikuwa umenoga; kama wenyewe wlaiyokuwa wanasema ilikuwa ni miziki ya kikongo, bongo flava na nyimbo za Beyonce. Vijana na wazee wote walijimwaga uwanjani hapo kwa zamu. Stan alijikuta ana hamu ya kuzungumza na Selina kwani tangu alipopokea barua ile alikuwa amewaza mengi sana na kwa namna fulani alijihisi kama mjinga fulani. Alianza kumtafuta Selina katika kadamnasi ya watu; kile alikomtafuta hakumuona. Aliwauliza mabinti wengine na kila mmoja alidokeza tu kuwa "alikuwepo" lakini hakuna aliyejua Selina yuko wapi. Aliingia ndani ambapo kina mama wengine walikuwepo.
"Jamani mmemuona Selina?" aliwauliza na kwa mpigo wote walitingishwa vichwa vyao wakiashiria hapana au walimjibu kwa maneno. Stan alianza kuingia na wasiwasi lakini hakutaka kuuonesha. Mwezi ulikuwa unaangaza eneo hilo vizuri kabisa kiasi cha kuweza kuona kutoka mbali. Stan alimuuliza Mwalimu Sebastian kama dada yake amemuaga kurudi nyumbani, Sebastian alikanusha. Stan alianza kujiuliza binti angekuwa wapi majira yale. Kabla ya kusababisha tafrija ivurugike kwa kuanza kumtafuta binti aliamua kwenda mahali fulani ambapo aliona ni jaribio la mwisho.
Aliondoka taratibu akipita nyuma ya nyumba yake na kuchukua njia fupi iliyokuwa inaelekea zahanati ya kijiji. Aliachana na sauti za muziki kwa mbali na kuanza kupokelewa na sauti za wadudu wa usiku na za vyura waliokuwa wakishangilia Noeli hiyo. Umbali kama wa mita mia moja toka zahanati njia ilichepuka kidogo na kuelekea ofisi za Kata. Kulikuwa na nyumba chache eneo hilo lakini karibu watu wote walikuwa wamekusanyika nyumbani kwao yeye. Hakuna mtu yeyote njiani. Nyuma ya ofisi za Kata kuna mawe makubwa yaliyopangiliana vizuri kuangalia mji wa Bariadi kwa mbali.

Kwenya mawe hayo Stan na vijana walipenda kwenda tangu utoto kucheza na kutafuta ukimya. Kama kulikuwa na mahali popote ambapo binti yule angeweza kuwepo wakati basi ilikuwa ni pale. Stan alielekea na kutoka mbali aliweza kuona kivuli cha mtu amekaa juu ya jiwe kubwa zaidi pale. Alikuwa amempa mgongo. Stan alipanda taratibu.
"Selina" aliita, hakujibiwa. Aliendelea kupanda na alipofika karibu alikuwa na uhakika kuwa ilikuwa ni Selina. Alisikia sauti ya kwikwi tu ikimtoka.
"Selina nini dada?" alimuita. Selina alimgeukia na kumuangalia machoni kwa macho ya uchungu, upole na majuto yaliyochanganyika na shauku ya kumuona. Alichukua kanga yake na kujipangusha uso; aligeuza uso wake kuangalia Bariadi. Stan hakuwa na la kusema na yeye aliketi pembeni yake wakiwa wako karibu upande kwa upande bila kugusana. Aliivuta miguu yake kuja kifuani yake na kuishikilia mbele yake kwa kuunganisha mikono yake. Hakuwa na la kusema. Selina bado alikuwa analia taratibu.
"Niambie unalia nini?" alimuuliza
"Hamna kitu"
"Hamna kitu wakati unalia, lazima kuna kitu; kuna mtu kakuudhi?"
"Hapana, ni makosa yangu mwenyewe tu"
"Haya umefanya nini".
Kimya.
"Selina umefanya nini jamani?"
"Sina ujasiri"
"Ujasiri wa nini; kati ya watu majasiri wewe ni namba moja" alisema Stan. Na kuanza kumkumbushia nyakati mbalimbali ambapo Selina alionesha ujasiri ambao wasichana wengine wasingethubutu. Selina alikuwa haogopi mtu yeyote. Alivyozidi kumsimulia kama kumchangamsha Selina alijikuta anatabasamu na kucheka kidogo huku akiguna. Alimkumbusha jinsi Selina alivyowahi kwenda kwa Pd. Gappa kumlalamikia pale parokia ilipoamua kufuta timu ya netiboli ya parokia pasipo sababu ya msingi. Aliweza kumshawishi padre yule hadi timu ile ikarudishwa na sare mpya juu. Mwaka mmoja baadaye timu hiyo ilinyakua kombe la Netiboli la mkoa wa Shinyanga.
"Samahani Selina" Stan alisema baada ya ukimya wa muda kidogo.
"Samahani ya nini sasa?"
"Sijui kwanini nilikuwa kipofu"
Kimya.
"Selina, tumekuwa pamoja na tumeshirikiana katika vitu vingi lakini hakuna siku niliyokuangalia zaidi ya Selina tu wa kawaida"
"Si ulikuwa unamuangalia Chausiku tu?" alijibu na maneno hayo yakakata kama upanga wa moto moyoni mwa Stan.
"Ni kweli, ni katika kumfikiria yeye aliyekuwa mbali nimepoteza nafasi ya kuangalia huyu aliye karibu". Waligeukiana macho. Waliangaliana na Selina aliyaangusha macho yake chini tena. Stan aliuchukua mkono wa kulia wa Selina kwa mkono wake wa kushoto na kuvifunga vidole vyao pamoja. Aliutomasa kidogo. Selina hakuamini. Sayari na nyota zilionekana kujipanga upya katika angali hilo zikizunguka mwezi mwangavu.
"Naomba unisamehe na unipe nafasi katika moyo wako" alimuomba Selina kwa kumuangalia machoni. Selina hakutegemea maneno hayo, hakutegemea siku hiyo ingeweza kuja; alishakata tamaa na Stan.
"Unamaanisha au kwa sababu Chausiku hayupo?"
"Selina, ukweli nadhani sikutaka kukiri kilichokuwa mbele yangu; lakini nimefikiria jinsi tulivyo karibu nadhani hata familia labda zimetushangaa kwanini hatujawa pamoja kiukweli" alisema na wote wakacheka.
"Si unajua walikuwa wanatuita wachumba" walicheka wote kwa pamoja.
"Naomba uwe mpenzi wangu wa moyo wangu kuanzia sasa hata milele"
"Hata milele, unanichumbia kabisa" walicheka tena
"Sipotezi tena nafasi na siko tayari kupata mpinzani!" Walikuwa kimya tena kwa dakika kadhaa.
"Stan, unaniomba kitu kikubwa kweli!"
"Nafahamu"
"Lakini umechelewa sana bwaana" alisema kwa sauti nyororo ya madaha.
"Nimechelewa tena?"
"Ndiyo, mimi nilishafanya uchaguzi wa moyo wangu juu yako siku nyingi kweli"
"Acha utani"
"Nilikuchagua tukiwa shule ya msingi na nimekuwa nikikuota na kukufikiria hadi nakonda" alisema kwa maneno matamu yaliyokuwa kama ulimbo masikioni mwa Stan.
"Sasa mbona ulikubali kutumiwa na Chausiku?"
"Sasa ningefanya nini wakati wewe ulikuwa umefanya uchaguzi mwingine?" Stan alimuomba msamaha sana. Alikumbuka matukio mbalimbali katika maisha yao jinsi hao wawili walivyokuwa karibu. Walikuwa wamesogeleana karibu wakipigwa na upepo taratibu uliozirusha nywele za Selina nyuma kama maua yanavyopigwa na upepo. Sauti ya muziki ilisikika kwa mbali kweli na mbalamwezi ilikuwa ikiwaangaza. Selina alikuwa amevalia sketi fupi pamoja na blauzi ya mauamaua, iliyokuwa na kamba mbili zilizovunga kifua chake. Kwa mara ya kwanza Stan aligundua kwa namna ya pekee kuwa jinsi huyo alikuwa ni mzuri wa kila namna. Macho yake ya mviringo ya rangi ya kahawia yalilindwa na nyusi kubwa nyeusi na kope ambazo zilikuwa bado hazijachakachuliwa. Midomo yake myembamba ilikuwa imepakwa rangi nyekundu iliyofifia. Katika kiza hicho uzuri wa binti huyo ulimulikwa na kuangazwa.
"Unaangalia nini?" Selina alimshtusha Stan ambaye alikuwa amekodoa macho utadhani mwanasayansi akiangalia darubini
"Nakuangalia wewe"
"Hahahah, yaani miaka yote umeniona leo ndio umeamua kuniangalia" alicheka. Stan alipitisha mkono wake juu ya uso wa binti huyo na kuzirudisha nywele zake nyuma. Selina aliangusha macho yake chini kwa haya tena.
"Nafurahi umeniruhusu nikuangalie." alisema na wote wawili nyuso zao zilikuwa zimekaribiana. Stan aliangalia midomo ya Selina ambayo ilikuwa inang'ara na kama iliyomuita kwa jina lake. Stan aliamua kufanya kweli. Alimsogelea taratibu huku mikono yake ikizunguka kiuno cha Selina juu ya mwamba huo mkubwa. Selina alijileta mwenyewe karibu ya Stan na midomo yao ikakutana. Hakukuwa na sauti ya vyura wala wadudu; hakukuwa na sauti ya muziki; ilikuwa ni sauti moja ya busu la ushindi. Midomo yao ilikutana kama ufunguo na kufuli lake; ikashikana huku ndimi zao zikipigana mieleka ya mapenzi.
"Aah Stan!" alilalamika Selina na kujitoa mikononi mwa kijana huyo. Wakapokelewa kwa mbali na sauti ya wimbo wa Awilo Longomba, Carolina. Walikuwa wanahema kwa nguvu.
"Stan unanitaka kwa usiku huu tu au unanitaka kabisa ndani ya moyo wako?" Selina alimuuliza huku akinyanyuka. Alipukuta mikono yake vumbi la miamba hiyo. Stan naye alisimama. Katika usiku huo juu ya miamba hiyo wakimulikwa na mbalamwezi na kuachilia vivuli vyao vikiangukia majabari hayo na kuwafanya waonekane kama sanamu za kuchongwa.
"Selina, niamini kutoka moyo wangu kabisa; sikutaki kwa siku moja au kwa usiku mmoja; nnakutaka kwa maisha yangu yote; Nataka uwe mke wangu na mama wa watoto wangu" alisema huku akiwa amemvuta Selina mikono yake na kuishikilia huku wakiangaliana.
"Stan, usiuchezee moyo wangu!" alisema Selina huku machozi yakimtoka.
"Naapa chini ya mbingu hii, sitathubutu!" chozi la huba lilidondoka kwenye jicho la kushoto la Stan. Selina alijipeleka tena mwenyewe mikononi mwa Stan na kumuangushia busu la taratibu na upole. Likatua kama tone la mvua kwenye udongo mkavu; likazama hadi mifupani mwa Stan. Wakakumbatiana katika usiku huo wa Krismasi.
"Basi tusizame sana tutashindwa kujizuia" alisema tena Selina ana kujitoa tena mikononi mwake.
"Labda wewe, mimi naweza"
"Aah wapi hakuna mwanamme anayeweza"
"Umejuaje?"
"Najua tu" wote wakacheka. Waliteremka toka kwenye majabari huku wameshikana mikono na kuanza kurudi nyumbani ambako watu walikuwa wanamalizia sherehe hiyo ya Krismasi. Ulikuwa ndio mwanzo wa pendo lao; pendo ambalo lilipandwa katika machozi. Walipofika nyumbani wameshikana mikono watu hawakusoma mengi; mpaka siku ilipopelekwa posa kwa kina Selina.

MWISHO

Simulizi hili ni la kutunga, mfanano wowote wa majina watu, mahali au matukio fulani fulani ni wa kinasibu. Majina ya baadhi ya wahusika yametumiwa kwa usanii tu. Haki zote za kunakili au kutoa katika namna nyingine yoyote iwe kwa kuchapa, video, au kunakili zimehifadhiwa na JamiiForums.com
 
Yegomasika

JF-Expert Member
Mar 21, 2009
13,170
61,235
MMKJ ungeanza na Stanley alikuwa amekaa nje ya nyumba yao akiota moto wa samadi ya ng'ombe. He he he!!!.:teeth:
 
Preta

JF-Expert Member
Nov 28, 2009
24,325
18,665
mwanakijiji si vizuri ujue....mbona sasa leo umetupa kidogo namna hiyo....
 
WiseLady

JF-Expert Member
Jan 22, 2010
3,272
529
Mistari michache lkn imenoga,natabiri stanley kutangaza nia kwa binti vry soon.
Mwanakijiji nasubiri uhondo
 
Jay One

JF-Expert Member
Nov 12, 2010
15,084
12,426
screw politics... nadhani we need a relief.. si unajua baada ya Super Bowl wanaulizwa wanataka kwenda wapi...???

Ur right mkuu hata USA leo wameanza Thanksgiving unajua sometimes politics it impresses people sometimes it distresses, i am so distressed, but still CHANGE IS coming, natuliza stress hapa kidogo meanwhile mapambano yanaendelea
 
birungi

JF-Expert Member
Oct 6, 2010
390
13
wabeja sana
hadithi ni nzuri,naahidi kuifatilia ila tu isiwe ndefu sana ikawa kikwazo kupata matoleo tofauti.
 
Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,339
38,982
wabeja sana
hadithi ni nzuri,naahidi kuifatilia ila tu isiwe ndefu sana ikawa kikwazo kupata matoleo tofauti.

Hapana itakuwa moja ya hadithi fupi sana.. natumaini itafikia mwisho wiki hii hii.. so stay tuned kwenye post ya kwanza hiyo hiyo...
 
FirstLady1

JF-Expert Member
Jul 29, 2009
16,793
5,333
Asante sana mzee mwanakijiji hadithi tamu kweli kweli endelea kutupa uhondo wa dada Chausiku
 
Ferds

JF-Expert Member
Oct 27, 2010
1,264
190
Na. M. M. Mwanakijiji

Kutangaza Nia

Kutangaza Nia

"Mwangaluka wa mayo!"
"Mwangaluka! Mhole mola?"
"Mola duhu"
"Mliho?"
"Tuli mhola"

Stanley alikuwa anaangalia kutoka dirisha la chumbani kwake kwenye uwanja wa nyumba yao pale kijijini. Ilikuwa ni nyumba ndogo ya vijana iliyokuwepo pembezoni mwa nyumba kubwa ya marehemu Mwalimu Maduku. Familia ya Maduku ikiwa imeshikamanishwa na mjane wa marehemu ilikuwa bado inaishi kwenye nyumba hiyo na kuendelea na maisha kama kawaida lakini bado pakijulikana zaidi kama kwa Mwalimu Maduku. Mama Eliza Maduku naye alikuwa ni mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi pale kijijini, alichukua nafasi iliyoachwa na marehemu mumewe. Stanley alijaribu kuangalia kwa shauku kubwa ni msichana gani aliyekuwa amepiga magoti kumsalimia mama yake Jumamosi ile asubuhi.

Hakuweza kumuona vizuri kwani yule binti alikuwa amempa ubavu huku sura yake ameingausha chini akizungumza kwa heshima na mama Maduku. Aliinuka chumbani mwake na kuinua shingo yake kwa nguvu zaidi kama mtua nayetaka kushuhudia tukio ambalo asingependa kumpita. Hakumfahamu binti yule mara moja lakini alihisi kwa asilimia mia moja kuwa alikuwa anamfahamu japo sura ilikuwa bado ni ngeni kutoka upande aliokuwa anamuangalia. Mara yule binti akainuka taratibu na kuendelea na safari yake akimalizia kumuaga mwalimu Eliza.

Stanley alishindwa kujizua alitoka chumbani kwake huku akiwa anamalizia kuvaa shati lake na kwenda moja kwa moja barazani ambako mama yake alikuwa anamalizia kumwagilia bustani yake ya maua mbele ya nyumba yake. Jua lilikuwa ndio limetoka lakini lilizibwa na mawingu ya asubuhi yaliyokuwa yanajaribu kupunguza makali yake. Mlio wa tetere na dudumizi ulisikika kutoka katika mti mkubwa uliokuwa karibu na nyumba hiyo. Asubuhi ilikuwa imeanza kama ilivyokuwa ikianza siku zilizopita, kwa sauti ya ndege wenye furaha wakiimba kwa kupokezana na kutegeana.

"Mbona mapema hivyo baba?"
"Mama yule ni nani?" Sijui kama alilisikia swali la mama yake au vipi lakini alionekana ana shauku ya kupewa jibu ya swali lake.
"Yule nani?" mama yake aliuliza huku akiwa amesimama mkono mmoja ameweka kiunoni na ule mwingine umeshikiliza guduria la maji. Alimuangalia mwanae kama kwa kumshangaa lakini akijifanya hajui anamuulizia nani.
"Mama yule binti amekusalimia hapo" alimjibu mama yake huku akiendelea kuangaza na kuona yule binti akimalizia kukata kona kuelekea madukani.
"Sasa wewe hata salamu jamani, eh" alicheka kwa kebehi lakini yenye kutuma ujumbe kwa mwanae.
"Mwangaluka mama"
"Mwangaluka Stanley" walicheka tena kwa pamoja. Kulikuwa na mapenzi makubwa kati ya mama na mtoto. Akiwa ni mtoto wa mwisho wa kiume wa Mwalimu Maduku Stanley alipendwa na kaka zake na aliabudiwa na dada zake. Hata kaka zake waliomtangulia walipoenda kuanza maisha yao yeye alibakia pale kuwa msaada mkubwa kwa wazazi wake. Wadogo zake wa kike ambao walikuwa secondari walimchukulia kweli kama kaka yao kwani kiumri walikuwa karibu naye zaidi kuliko kakazao wawili wakubwa ambao wote walikuwa wameshaanza maisha yao.
"Kaka Stanley, we humjui yule?" Suzy alizungumza akitokea ndani ya nyumba akiwa ameshika ufagao mkubwa.
"Simjui Suzy niambieni basi" alisema kwa shauku, wote wakacheka na wakati huo huo Belinda naye alitokea kujiunga na kikao hicho cha jumamosi asubuhi. Stanley alijua leo kabanwa na kina mama watatu, ilikuwa ni kawaida yao kumlinda kaka yao lakini wakati huo huo kumfanya vituko. Mwenyewe alijiona kama ni mfalme wa kasri la mzee Maduku. Na kwa kweli dada zake na mama yao walimuona hivyo.

Stanley alikuwa anamiaka ishirini na mawili tu. Alikuwa amemaliza kidato cha sita kwenye shule ya sekondari ya misheni lakini hakupata nafasi ya kuchaguliwa kuendelea na masomo ya juu. Hata hivyo alikuwa ameanza kibarua pale pale kijijini akifanya kazi na shirika la misaada la Waswedi la SIDA. Alikuwa ndiyo dereva na mkalimani wao. Alikuwa ni kijana nadhifu na mcheshi sana na waswedi walimpenda sana. Alikuwa hazoei watu haraka lakini akishazoea basi alikuwa na urafiki wa moyoni kabisa. Wajihi wake alikuwa ni mrefu kwa wastani lakini mwembamba. Alikuwa na mikono mirefu sana kama baba yake. Ilikuwa ni mojawapo ya vitu ambavyo vilimtofautisha sana na wenzake kwani kwa namna moja au nyingine ilikuwa rahisi sana kuona urefu wa mikono yake. Sasa ubishi mkubwa mara nyingi ulikuwa ni kama ni vidole ndiyo vilikuwa virefu au mikono yenyewe ilikuwa ni mirefu.

"Sasa mtaniambia ni nani yule au ndio hadi nipige magoti" sauti yake ilikuwa kali kidogo lakini macho yake yalimuangukia Suzy, dada yake kipenzi na kitinda mimba wao.
"Kaka, yule ni mjukuu wa Mzee Mswahili"
"Mjukuu wa Mzee Mswahili? Katokea wapi, mbona nawafahamu wajukuu zake"
"Chausiku huyo alikuwa anasoma Dar amekuja likizo, wenyewe wanasema mara mwisho alipokuja hapa ilikuwa akiwa darasa la saba sasa hivi naye amemaliza kidato cha sita" huyo alikuwa ni mama Eliza.

Stanley akaanza kurudi nyuma kwa haraka na kukumbuka. Alimkumbuka. Lakini hakumkumbuka kama binti aliyekomaa mwenye mvuto na haiba ya nguvu ya kuweza kumfanya mtu yeyote kugeuza shingo mara tatu tatu. Chausiku.

"Yule ni Chausiku?" aliuliza kwa hamaki
"Eehehehehe" dada na mama yake wakuanganisha vicheko vyao. Alijisikia kutatizika. Hakuelewa kama ni kweli au ilikuwa ni uzushi tu. Alijiambia kuwa yule haiwezekani kuwa alikuwa ni Chausiku. Aliapa haiwezekani kuwa ni Chausiku akitoa sababu elfu moja na moja za kwanini isingewezekana kuwa ni Chausiku. Aliondoka na kurudi chumbani kwake akiwa na maswali mengi juu ya yule binti, alijiandaa kwenda kwa Bw. Stevennson meneja wa mradi wa umeme wa jua pale kijijini. Chausiku lilikuwa ni jina ambalo hakuwa amelifikiria kwa zaidi ya miaka saba. Lakini siyo tu jina sura na umbile aliloliona asubuhi ile lilikataa kabisa kuingia kichwani mwake kuwa ni Chausiku mchokozi, mtukutu na mwenye maneno sana. Haiwezekani, alijiambia.

* * *

"Mmemuona Chausiku nyinyi?" Alfred aliwauliza marafiki zake jioni ya jumamosi ile huku wakiangalia mechi ya mpira wa miguu uwanja wa shule ya msingi.
"Aisee nimemuona, huwezi kuamini kapendeza kweli" Rajabu alijibu
"Yaani huwezi kuamini ni yeye" alidakia Simoni.

Stanley alikuwa anakodolea macho mpira huku mawazo yake yakiwa mbali kabisa na uwanja huo. Marafiki zake wakamshtua.
"Stanley wewe vipi?" Alfred akamuuliza
"Kuhusu nini?"
"Kuhusu Chausiku"
"Aaah, amefanya nini" wenzake wakacheka lakini wakamshangaa alikuwa wapi wakati wao wanamwaga sifa za Chausiku kama waliokuwa wameajiriwa kufanya kazi hiyo.
"Wewe umemuona?" Simoni akamrushia swali tena.
Stanley akatulia kwa sekunde kadhaa na kuwasimulia jinsi siku yake ilivyoanza. Aliwaambia jinsi kutwa nzima ile alikuwa anamuwaza Chausiku. Marafiki zake hao walianza kucheka kwanza na kumshangaa, lakini walicheka zaidi kwa sababu Stanley alikuwa anazungumza utadhani alikuwa ni mwenye mali. Lakini waalimshangaa na kuona kama mwenzao kapata bahati ya pekee iliyokuwa inamngojea tu. Kwa pamoja wakaanza kubishana ni jinsi gani kila mmoja angeweza kumpata na angefanya naye nini ili kupata nafasi hiyo. Yalikuwa ni mazungumzo ya vijana waliokomaa karibuni ambao maisha yao yalikuwa yanatishiwa kuwa ni ya kushtuliwa mioyo miaka mingi sana ijayo kila binti mzuri akipita mbele yao. Stanley hata hivyo alijisikia wivu kooni wenzake walipoelezea mambo waliyokuwa wanayaotea kufanya na Chausiku. Wao walikuwa wanatania, yeye alikuwa amepania.

"Acheni bwana!" Stanley alisema kwa hasira
"We vipi, una hasira kama ndio demu wako bwana" kwa lafudhi kali ya kisukuma Simoni alimshangaa Stanley.
"Hata kama siyo demu wangu lakini.." alishindwa kumalizia kusema maana hakujua angewaambia nini rafiki zake.
"Hahaha, usituambie umemdondokea bwana" Bakali alicheka huku akimsukumiza kwa mzaha.
"Mimi sijui bwana" na wengine nao wakacheka. Lakini macho ya Stanley yalikuwa hayana utani.
"Hutanii? Kweli umempenda"? Alfred alimuuliza huku wenzake wakikaa kimya kumuangalia Stanley. Stanley alikiri alichokuwa anakisikia moyoni. Alisema wazi kuwa vyovyote itakavyokuwa ni lazima azungumze na Chausiku na ikiwezekana amueleze ukweli, amueleze masaibu aliyojikuta nayo moyoni. Wenzake walimsikiliza, walimuonea huruma, walimuelewa. Waliahidi kumsaidia kwa namna yoyote ile.

Stanley alijua kuwa tayari moyo wake umetekwa na Chausiku na alijijua amewekwa kifungoni na kuwa mtu pekee mwenye ufunguo wa gereza hilo la maisha ni Chausiku. Alijua vile vile kuwa ili aweze kumpata na kuwa naye itahitaji kutengeneza mambo mengi ya huko nyuma, kwani hao wawili walikuwa na historia, walishapigana miaka saba nyuma na Stanley anakumbuuka jinsi alivyocharazwa viboko na marehemu baba yake kwa sababu ya Chausiku. Lakini Chausiku aliyemuona asubuhi ile hakuwa yule wa shule ya Msingi. Stanley alijiambia liwalo na liwe, lakini ataufuata moyo wake. Aliomba msaada wa rafiki zake wamsaidie kuweza kufikia lengo lake ambalo lilikuwa ni kupiga kura na hatimaye kupata ushindi wa kuuteka moyo wa Chausiku.

Stanley alitangaza nia, ya uchaguzi wa moyo. Marafiki zake walimsikiliza, walimuonea huruma na kila mmoja akajikuta anaachilia wazo lake na wote kumuunga mkono Stanley kuwa ndiye mgombea wao katika uchaguzi huo wa moyo. Walimtia shime aende jimboni kwa wapiga kura kuwasikiliza. Lakini vile vile aweze kutangaza nia. Stanley alikubali. Walikuwa wametoka eneo walilokuwepo na kwenda pembezoni kabisa ya uwanja ambako walikuwa wanapanga mikakati yao. Walishtushwa na mlio wa kipenga cha mwisho. Timu ya kijiji chao ilishinda mabao mawili bila. Ilikuwa ni dalili ya mpambano uliokuwa mbele ya Stanley.

Jimboni

Kijasho chembamba kilianza kumtoka Stanley alipofika kwenye mimbari kusoma somo la kwanza. Alipoanza tu kusema "somo la kwanza kutoka kitabu cha Kutoka" aliyainua macho yake na kuangalia waumini. Macho yake yaligongana moja kwa moja na macho ya msichana aliyekuwa amekaa benchi la nne hivi mbele upande wa kushoto kwake Stanley. Msichana huyo alikuwa amekaa nyuma ya kundi la masista waliokuwa wamependeza katika mavazi yao meupe yaliyopambwa na misalaba mikubwa iliyong'ara vifuani mwao. Alikuwa ni Chausiku.

Chausiku alikuwa amevaa tofauti na wasichana wengine mle kanisani. Wengi walikuwa wamevaa sketi na blazu na wengine magauni lakini kila mmoja wao alikuwa pia amejifunga kanga kwa namna fulani. Wengi walikuwa pia wamevaa vilemba vya kila namna. Chausiku alikuwa amevaa gauni jekundu iliyokolea ambayo kola yake na vifungo vya mbele vilikuwa vya rangi nyeusi. Nywele zake zilizopakwa mafuta zilikuwa zimefungwa nyuma kwa butu moja huku kiasi kidogo kikiangukia kwenye jicho lake la kushoto. Alikuwa amevaa miwani ya rangi nyeusi na kuwa kama mwalimu fulani hivi. Alikuwa amejipaka rangi nyekundu ya mdogo na nyusi zake zilikuwa zimetengenezwa vizuri kabisa kuupamba uso wake. Kwa kila kipimo alikuwa ameshinda shindano la warembo ndani ya kanisa hilo kama shindano kama hilo lingeruhusiwa. Hereni zake ndogo nyekundu zilining'inia masikioni mwake.

Stanley alirudisha macho yake kwenye kitabu cha masomo ya siku ile lakini akili yake iligoma. Alijaribu kujiuliza kama Chausiku alimkonyeza au alitabasamu walipoganisha macho yao. Alitamani kurudi kumuangalia tena. Alijizuia. Msukumo ulikuwa ni kama wa paka ambaye amemuona panya lakini anaambiwa asimsogelee. Alianza kusoma somo hilo la kwanza kutoka katika Agano la Kale. Sauti yake ilikuwa inakwama kwama huku kijasho kikijitokeza kwenye paji lake la uso. Stanley aliweza kuyasoma maandishi bila hata kujua yanahisi nini. Macho yalisoma maandiko hayo kwa mazoea ya kufuata herufi tu lakini akili yake yote ilikuwa inafikiria na kuwaza Chausiku anafikiria nini, alitamani ajiangalia kama yuko nadhifu.

Alipofika mwisho na kutangaza kuwa "hilo ndilo neno la Mungu" waumini walipojibu "tumshukuru Mungu" yeye mwenyewe alijikuta anaitikia moyoni "amina". Aliteremka kutoka kwenye mimbari hiyo na kuelekea upande wa kwaya ya kanisa hilo la kijiji ambako yeye alikuwa ni mwimbaji. Kabla hajakaa chini aliangalia tena upande aliokuwa ameketi Chausiku. Macho yao yakagongana tena, safari hiyo alikuwa na uhakika kuwa Chausiku hakutabasamu wala kukonyeza. Ila macho yake yalisema kitu ambacho Stanley hakuweza kukitafsiri mara moja hakujua kama ilikuwa ni huzuni, uchungu au kitu kingine ambacho hakuweza kukipatia jina mara moja.

Ibada ilipofika mwisho Stanley hakutaka kushangaa shangaa pale nje na kusalimia watu kama ilivyokuwa kawaida ya waumini weng siku ya jumapili. Aliamua kuelekea nyumbani mara moja kubadilisha nguo zake kwani alikuwa amepanga kwenda kwa Mzee Mswahili jioni hiyo kuwasalimia na kujaribu kuona kama angeweza kuonana na Chausiku. Tangu jana yake mawazo yake yote yalikuwa juu ya msichana huyo.

Simon na wenzake walimshangaa kwanini alikuwa anawahi kurudi nyumbani kuliko ilivyokawaida na yeye aliwaambia tu kuwa kuna shughuli nyumbani alikuwa anawahi. Aliwahi kufika nyumbani na hakukuwa na mtu mwingine yeyote kwani mama yake na dada zake alikuwa amewaacha kanisani wakija taratibu na kundi la kina mama wengine. Alivua shati lake na kubakia na vesti yake tu. Alikuwa ni kijana mwembamba lakini ambaye alikuwa amejaza misuli kutokana na shughuli mbalimbali za Useremala alizokuwa akizifanya wakati wa jioni na mwisho wa juma na kujiongezea kipato. Ulikuwa ni ufundi ambao aliurithi kutoka kwa baba yake. Alichukua pasi na kuijaza mkaa akaimwagia mafuta ya taa na kuiwasha, akaiweka nje ipigwe na upepo. Aliingia chumbani kwake na kuchagua nguo za kuvaa. Alisubiri pasi ipate moto wa kutosha aanze kunyosha nguo. Mawazo yake yote yalikuwa kwa Chausiku.

"Ka' Stanley" sauti ya Suzy ilimshitua wakati anamalizia kuvaa viatu vyake tu
"Naam"
"Chai tayari"
"Haya nakuja Suzy"

"He! Mwenzetu mbona umetoka hivyo" mama yake alikuwa wa kwanza kumshangaa. Alimsogelea Stanley na kumtengeneza kola yake iliyokuwa haijakaa vizuri. Staley alikuwa ananukia manukato ya "Yu" ambayo yalikuwa maarufu kwa vijana pale kijijini.
"Natoka kidogo"
"Kutoka gani huku?" dadake mwingine alidakia
"Mnatafuta umbeya tu" alipojibu hivyo wote walicheka. Kama ilivyokuwa kawaida yao siku ya Jumapili familia ilibariki chakula na wakakaa mezani kula kifungua kinywa. Walizungumza mambo mbalimbali na kabla hawajamaliza kabisa chakula Stanley aliwaaga kuwa anatoka. Wakamtakia kila la kheri alikokuwa anaenda. Alichukua baskeli yake, akaidandia na kuelekea upande wa mashariki wa kijiji.

Haikumchukua muda sana alifika barazani kwa mzee Mswahili. Na kama alivyotarajia hakupokelewa na mtu mwingine isipokuwa mzee Mswahili mwenyewe. Alimsalimia kwa Kisukuma, mzee Mswahili aliitikia kwa Kiswahili. Hilo halikuwa jambo geni kwani hakuna mtu ambaye aliwahi kumsikia mzee Mswahili akizungumza Kisukuma. Alikuwa anakisikia Kisukuma vizuri kabisa lakini alikuwa anapenda sana kuzungumza Kiswahili fasaha wakati wote na ndiyo sababu alijulikana kijijini na hata miji ya jirani kama Mzee Mswahili.

"Hujambo bwana"
"Sijambo mzee, hatukukuona kanisani leo, wazima hapa"
"Ah..huko kanisani kwenu myeyusho tu." Nusura Stanley aangushe kicheko.
"Siku moja moja babu siyo mbaya"
"Haya karibu, kwema huko kwenu"
"Kwema kabisa".
"Vuta hivyo kiti hapo"

Stanley alivuta kitu na kuketi pembeni ya mzee Mswahili ambaye alikuwa anavuta sigara yake huku mikono yake ikiwa imeshikiliza gazeti la MwanaHalisi mikononi mwake la wiki iliyopita. Mzee Mswahili alianza kulalamika mambo ya ufisadi vitu ambavyo Stanley alikuwa havifuatilii kabisa. Mzee Mswahili alikuwa ni kama shihata ya kijiji kwani alijua yote yanayoendelea Tanzania kutokana na kusoma sana magazeti na kusikiliza radio za ndani na vituo vya utangazaji wa vya nje. Alianza kumuonesha Stanley habari mbalimbali na jinsi gani Tanzania inahitaji mabadiliko. Alikuwa ni kama mwanasiasa fulani. Mzee Mswahili hakuhitaji kujua nini kimemleta kijana huyo hapo nyumbani siku hiyo ya Jumapili kwani mara kwa mara vijana na wazee huja na kupiga soga naye na kumsikiliza habari alizonazo hivyo alishazoea kukaa na kuzungumza. Tena kwa siku kama hiyo ya Jumapili ikifika majira ya jioni kundi la vijana huwa wanakuja hapo kuzungumza naye na kupata hekima aliyonayo na kuzungumza naye mambo yote yanayohusu siasa na maisha na wakati mwingine kusikiliza visa vyake vya wakati wa ujana wake alipokuwa akifanya kazi jijini Dar-es-Salaa hadi alipostaafu katikati ya miaka ya tisini.

Wakati wanazungumza hapo nje, dalili zote zilionesha kuwa jikoni mambo yalikuwa yanaiva. Harufu ya mchuzi wa nyama ilifunika angala la nyumba ya mzee Mswahili katika hali iliyosababisha midomo ya Stanley kujaa mate kwa hamu. Stanley alikuwa amekaa akijaribu kuangaza angaza kiujanda kuona kama angeweza kumuona Chausiku. Aliweza kusikia sauti ya kina mama wakizungumza jikoni na mjukuu wa mwisho wa mzee Mswahili alikuwa amekaa kwenye meza ndani akimalizia kufanya kazi yake ya shule. Pale nje ilikuwa ni kama mahali pa mikutano mifupi mifupi kwani wazee na vijana waliokuwa wakipita pale walitumia dakika chache kuwasalimia.

Wakiwa wanaendelea na mazungumzo walisikia hatua za miguu zikija nyuma yao kutoka mlango wa mbele wa nyuma. Chausiku alikuja akiwa amejifunga kanga kiunoni lakini bado akiwa na gauni lake lile jekundu alilokuwa nalo kanisani. Alipiga magoti mbele ya mzee Mswahili. Macho yake yaligongana tena na Stanley ambaye alijivuta kukaa vyema kwenye kiti chake kwani kutokea kwa Chausiku kwa ghafla hivyo nusura kumsababishe roho itoke mwilini mwake.

"Babu chakula tayari" Alisema kwa heshima huku macho yake ameyaangusha chini.
"Asante mama"

Chausiku akainuka kurudi jikoni. Hakufika mbali.

"Chiku" ndivyo mzee huyo alivyolichakachua jina la mjukuu wake. "Mbona humsalimii mwenzio hapa?, heshima gani hii; usituletee mambo yenu ya Dar" alifoka kidogo.
"Mambo?" alisema huku akiyazungulusha macho yake angani. Kabla Stanley hajajibu Chausiku alikuwa ameshaingia ndani. Hata hivyo shingo ya Stanley ilimfuatilia hadi anaingia ndani akiufuatilia mwendo wa chiku. Alijisikia kutaka kumuita. Hakujua kilichomkuta. Mzee Mswahili hakuchelewa alikilazimisha kichwa cha Stanley kurudi kwenye usawa wa kati kwa kibago kilichopigwa kisogoni kwa haraka kama mtu aliyejaribu kuua nzi.

"Wewe vipi, mbona unamuangalia mjukuu wangu hivyo?" aling'aka
"Aah samahani mzee.. uuuh.. mmh" alianza kumung'unya maneno
"ndicho kilichokuleta nini?"
"Hapana mzee"
"Usitake kuniharibia mjukuu wangu"
"Hapana mzee nilikuwa nawaza tu"
"ndiyo hayo mawazo yabakie humo humo kichwani"
"ndiyo mzee"
"Haya twende kula"

Stanley alijisikia kutetemeka hadi figo na maini. Kile kibao kilimkumbusha kuwa yupo hapo kwa mzee Mswahili. Aliinuka taratibu na kumfuata mzee Mswahili, alikwepesha kabisa macho yake kumuangalia Chausiku ambaye aliwapokea hapo ndani akiwa ameshikilia bakuli na birika la maji ili kuwaosha mikono. Pale mezani walikuwepo yeye mzee Mswahili, Stanley na mjukuu yule wa kiume ambaye wakati huo alikuwa amehamisha vitabu vyake na kuviweka pembeni. Kabla hawajaanza kula mjukuu wa kiume akawakumbusha kubariki chakula. Kwa uvuvi mzee Mswahili alisubiri mjukuu wake huyo kipenzi amalizie sala. Walivamia ugali huo wa kisukuma uliosindikizwa na nyama ya kuku ya mchuzi, na mchicha wa kukaangwa ukiteremshiwa na maji ya baridi yaliyotoka kwenye mtungi mkubwa uliokuwa kwenye kona ya sebule hiyo.

Walipomaliza kula walipiga soga kidogo na mzee Mswahili kama ilivyokuwa kawaida yake alitoka tena nje na kuketi upenuni pale,hata hivyo wakati huo alimuagiza Stanley kuhamisha viti vyao hadi mbali kidogo tu ya nyumba chini ya mti wa Krismasi uliokuwa umependeza kwa rangi yake ya kijani na maua ukiashiria mwelekeo wa mwisho wa mwaka. Waliendelea kupiga soga za hapa na pale huku mzee Mswahili wakati huo akiwa anasoma makala za gazeti la Uhuru ambalo mzee huyo alihakikisha hakosi nakala yake hata likichelewa vipi. Ilipofika mida ya saa kumi hivi Stanley aliamua kuaga kurudi nyumbani. Alikuwa na uhakika kabisa kuwa kweli Chausiku ni mjukuu wa mzee Mswahili na alishakata tamaa kuwa haiwezekani hata kuzungumza naye kwani yule mzee alikuwa ni mnoko.

"Mzee miye narudi nyumbani nimefurahi sana leo"
"Hamna neno, msalimie sana mama yako na wadogo zako"
"Bila ya shaka mzee, ukihitaji msaada mzee hapa wewe nitumie ujumbe"
"Vizuri sana Stan, tena naweza kukutumia kesho au jumanne"
"Hamna neno mzee mshinde vyema". Aliinuka taratibu na kumpa mkono mzee Mswahili ambaye aliupokea huku mkono wake wa kushoto ukipeleka mbali sigara yake nyingine na kupuliza moshi pembeni ya mdomo wake. Jua lilikuwa taratibu limeanza kupunga mkono wa baibai jioni hiyo. Kulikuwa na hali fulani ya utulivu ambao huwezi kuupata mahali pengine popote isipokuwa katika kijiji cha Kiafrika.

"Chiku!" Mzee Mswahili aliita kwa nguvu kidogo
"Bee Babu" sauti iliitikia. Chausiku alikuja mbele ya babu yake na kupiga goti.
"Mwenzio anaondoka humuagi?"
"Kwa heri!" alimuangalia na kusema na kurudisha macho yake chini.
"We vipi, ndio kuaga gani huko?" Mzee Mswahili alikuja juu. "Kwani mmegombana?" aliuliza.
"Hapana babu"
"Haya msindikize mwenzio kidogo umtoe hapa nyumbani nyie vijana wa siku hizi sijui mkoje" alishangaa huku akitoa maagizo. Stanley hakuamini masikio yake na hakujua kama ni mtego anategewa au nini.
"Ndiyo babu" Chausiku aliinuka na kwenda ndani. Aliporudi alirudi na mfuko uliokuwa umejaa nyanya na vitunguu. Bibi yake alikuwa ana bustani ya nyanya na vitunguu na mara nyingi wageni walipokuja hapo nyumbani waliondoka na nyanya kidogo. Muda wote huo bibi yake alikuwa bado hajarudi kutoka katika shughuli zake kanisani.

Stanley alimpokea mzigo huo kwa heshima na kumuambia kwa Kisukuma "Wabeja ukinkulu"
"Wabeja kulumba!" alijibu. Vidole vyake viligusana na vile vya Stanley chini ya mfuko huo na umeme kama wa radi ulipasua mwili wake. Alimuachia kwa haraka mfuko huo. Stanley aliaga na akisindikizwa na Chausiku alianza kuondoka akiwa ameuweka mzigo kwenye kiti cha baskeli huku akiikokota baskeli taratibu.

"Chausiku unanikumbuka mimi?"
"Kwanini nisikukumbuke?"
"Sasa mbona unajibu kwa ukali?"
"Hivi wewe unaujua ukali?"
"mmh!" Stanley aliishiwa maneno, walikuwa wanatembea taratibu bila maneno kwa sekunde chache.
"Kwani nimekukosea nini?"
"mmh.. watu wengine bwana"
"Una maana gani watu wengine?"
"Hamna kitu". Walikuw wametembea kama mita thelathini tu kutoka nyumbani na Stanley alikuwa tayari kuikwea baskeli yake.
"Naweza kupata muda wa kuzungumza na wewe?" alimuuliza Chausiku.
"Mbona tunazungumza?"
"Hapana, nataka turudishie urafiki wetu"
"Urafiki?"
"Jamani Chausiku tulikuwa marafiki tulipokuwa wadogo"
"Msisitizo upo kwenye neno 'tulikuwa'". Kimya kikapita tena wakati kundi la kina mama wakiwapita.
"Yaani hatuwezi kuwa marafiki tena?" aliuliza Stanley. Moyo ulikuwa unamdunda, kijacho kilikuwa kinamtiririka kwenye kwapa zake. Alishindwa kuyaangalia macho ya Chausiku. Akili zake zilikuwa zinanguka kama pia asijue aseme maneno gani ili kumfanya Chausiku aweze japo kumsikiliza.
"Sidhani kama inawezekana labda hadi uniombe msamaha"
"Msamaha?"
"kwani nimezungumza Kiingereza? Ndiyo msamaha"
"Kwa lipi tena?"
"Yaani unajifanya umesahau kabisa?" Stanley hakusahau lakini hakudhania lilikuwa ni jambo kubwa. Alimuomba msamaha kutoka moyoni huku midomo yake ikitetemeka. Alikiri kuwa alifanya vibaya kumchongea nyumbani kwa babu yake kitu ambacho kilimsababisha Chausiku alambe mboko na baadaye kukasirika na kutaka kurudi kwa wazazi wake Dar japo alipenda sana kuwa na bibi yake. Machozi yalimlenga kidogo Chausiku alipomsikia Stanley anaomba msamaha.
"Umenisamehe?" aliuliza Stanley
"Miye sijui." aligeuza macho yake yasigongane na ya Stanley. Ilikuwa ni mara ya tatu kwa siku hiyo mmoja wao akipata tabu ya kuangaliana na mwenzie machoni.
"Kesho unafanya nini?"
"Sijui"
"Unafikiri Mzee Mswahili atakuacha unisindikize mjini?"
"Sasa unaulizia huku kwanini hukumuuliza mwenyewe kule?"
"Sasa si nilitaka nikuulize wewe kwanza?"
"Sijui itabidi urudi kumuuliza". Alishindwa la kusema. Hakutaka kurudi kule tena kwani jua lilikuwa limezidi kwenda. Alimshukuru kwa mzigo huo na kumuaga. Alidandia baskeli yake na kumuangalia tena. Chausiku alikuwa bado amesimama hapo hapo anamuangalia.
"Usiku mwema"
"Asante na wewe".

Stanley alianza kuendesha baskeli yake. Alikuwa hatua kama tano tu kutoka kwa Chausiku alilazimika kusimama ghafla.

"Stan!" Sauti ya Chausiku ilimuita. Aligeuka
"Nitakuwa posta saa nne asubuhi!" Chausiku alisema na kugeuka kuanza kutembea kurudi kwao. Stan nusura apige kelele ya asante. Alimuangalia Chausiku akitembea kwa madaha huku akitingisha kidogo viungo vile alivyojaliwa na muumba wake katika staili ile ya kale ya "Singida-Dodoma, Singida-Dodoma". Alianza tena kukanyaga mwendo. Alimpigia kengele mama mmoja aliyekuwa na kiroba kichwani ambaye alichepukia pembeni.

Aliamua kuwa kesho ni lazima aanze kumwaga sera. Alijiuliza ataweza vipi kuchepuka toka kazini asubuhi hiyo kwenda pale Posta. Alishaamua kuwa liwalo na liwe saa nne asubuhi atakuwa Posta ya mji wa Bariadi. La kwanza alijua ni lazima atengeneze ilani yake ya uchaguzi wa moyo.

Ngalo nang'ho lekaga e limela shi, lolaga lolo wakenangola ubononu....................... lebachage sh ele second page namhala
 
Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

0 Reactions
Reply
Top Bottom