Rostam: Nimeshtushwa
na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
July 11, 2008
SIKU moja tu baada ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) kutoa tamko dhidi yake, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM) ameeleza kushtushwa na kusikitishwa na tukio hilo.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana, Rostam ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema alikuwa akitarajia kuitisha mkutano na waandishi wa habari wakati wowote kuanzia sasa, ambao atautumia kueleza msimamo wake kuhusu tamko hilo la KKKT.
Nimeshtushwa na tamko hilo. Ingawa nazungumza nikicheka, lakini kwa kweli nina masikitiko makubwa. Ninachoweza kukueleza kwa sasa ni kwamba, nimefikia uamuzi wa kuitisha mkutano na waandishi wa habari katika siku chache zijazo, na kueleza kile nilichonacho kuhusu tukio hili zima, alisema Rostam.
Alipotakiwa kueleza iwapo bado alikuwa akiamini kwamba tamko hilo la KKKT lilitolewa kwa shinikizo lolote kama alivyogusia siku moja kabla ya tukio hilo, Rostam hakuwa tayari kueleza lolote, zaidi tu ya kusema kwamba atasema kila alichonacho katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Iwapo Rostam ataitisha mkutano na wanahabari, inaweza ikawa ni mara ya kwanza kwa mwanasiasa huyo kufanya hivyo tangu alipoingia katika siasa za wazi nje ya ubunge wake wa Igunga.
Ingawa Rostam hakuwa tayari kueleza nini alichokuwa akikusudia kusema, mmoja wa wanasiasa wa karibu naye, alilieleza Tanzania Daima kwamba, Rostam amepata kualikwa katika usharika wa Kinondoni siku zilizopita.
Ninachojua mimi ni kwamba haikuwa mara ya kwanza kwa Rostam kualikwa KKKT Kinondoni na kutoa mchango. Amepata kualikwa hapo mwaka 2005 au 2006 hivi kwa barua aliyopewa na mzee mmoja wa kanisa hilo, ambaye ni kiongozi wa juu kisiasa. Tafuteni hili mtalijua hilo, alisema mwanasiasa huyo.
Taarifa kutoka katika usharika huo zinaonyesha kwamba, viongozi wawili wanasiasa ambao ni wazee wa kanisa katika kanisa hilo la Kinondoni, ni Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta na Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa, wote wa CCM.
Uamuzi huo wa Rostam kuahidi kuitisha mkutano na wanahabari, unakuja kutokana na tamko la KKKT lililotolewa juzi ambalo lilikana kutambua mwaliko na kauli zilizotolewa na mbunge huyo mwishoni mwa wiki katika usharika huo wa Kinondoni.
Tamko hilo la KKKT lililotolewa juzi baada ya kikao cha dharura cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi hiyo, linaeleza kusikitishwa kwake na matamshi yaliyotolewa na Rostam wakati alipozungumza katika usharika huo Jumapili iliyopita.
Kwa mujibu wa tamko hilo lililosainiwa na Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Balozi Richard Mariki, KKKT imekana kutambua usafi wa Rostam dhidi ya tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwake.
Kanisa hilo pia lilikanusha kuwa na taarifa zozote kuhusu uamuzi wa kwaya ya Amkeni kumwalika Rostam katika hafla yao ya uzinduzi wa mkanda wao.
Tunasikitika ya kwamba kanisa halikuwa na taarifa ya ujio wa Rostam Aziz. Tunapenda kuwataarifu kwamba, taratibu za kuwaalika wageni kwenye shughuli kama hizi hazikufuatwa, linasomeka tamko hilo la KKKT katika sehemu moja.
Tamko hilo la KKKT lilitolewa siku chache tu baada ya Rostam kualikwa na kuwa mgeni rasmi katika Usharika wa Kinondoni wa kanisa hilo Jumapili iliyopita na kutoa matamshi mazito kuhusu masuala yanayohusu maadili na hali ya siasa.
Katika matamshi yake hayo, Rostam alilishukuru kanisa kwa kumwalika, na akatumia fursa hiyo kueleza kuwa taifa lilikuwa likipita katika kipindi kigumu kisiasa na kijamii, na akawataka waumini waliombee ili kulirejesha katika mstari ulio sahihi.
Mbunge huyo ambaye katika siku za hivi karibuni jina lake limetajwa katika tuhuma za ufisadi, hususan katika sakata la Richmond, aliwashukuru waumini wa Kikristo kwa kutenda haki, na kwa kutomtuhumu na kumshutumu mtu sambamba na kuwapinga watu wenye wivu na chuki.
Rostam alisema ana watoto watatu ambao aliahidi kanisani hapo kwamba, anataka awalee katika misingi safi ili wawe wananchi bora na waadilifu hapo baadaye.
Nawashukuru kwa kuamua kunialika kuwa mgeni rasmi leo. Hii ni ishara kwamba mmeamua kupuuza viji-maneno na upuuzi wa vijiweni. Nafurahi kuwa miongoni mwenu
hamtuhumu, hamshutumu, hampendi wenye wivu na wenye chuki, mnapenda haki. Ninao watoto watatu na nataka niwalee katika misingi hii, alisema Rostam huku akishangiliwa na umati wa watu walioshiriki hafla hiyo.
Alisema hivi sasa nchini, watu wameanzisha tabia ya kuchukiana, hata kufikia hatua ya kuzushiana uchawi na kuombeana vifo, kauli ambayo baadhi ya watu waliiona kuwa ilikuwa ikimlenga Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambaye ni mmoja wa wazee wa kanisa wa usharika huo huo alioalikwa Rostam.
Kutokana na matamshi na mwaliko huo wa Rostam, KKKT katika tamko lake la juzi, lilieleza kwamba, uchunguzi wao uliwawezesha kugundua kuwa, mbunge huyo alialikwa kanisani hapo na kikundi ambacho hakikuwa na mamlaka ya kufanya hivyo.
Kutokana na ukiukwaji taratibu hizi, hayo madai yaliyonukuliwa katika vyombo vya habari kwamba ujio wa Rostam katika Usharika wa Kinondoni na tafasiri ya ujio huo kuwa kanisa linatambua usafi wake, si sahihi, na ni madai potofu, alisema Mariki katika taarifa yake.
Kanisa hilo katika tamko lake hilo linasema msimamo wao hauruhusu sharika zake kutumika kama majukwaa ya kisiasa kujisafisha au kuwasafisha watuhumiwa wa ufisadi.
KKKT imekuwa mstari wa mbele katika kupinga na kukemea mambo ya ufisadi, na linaunga mkono juhudi zote za kutokomeza uovu...kanisa litachukua tahadhari kuhakikisha jambo kama hilo, halitatokea tena, linasema tamko hilo.
Katika hatua kubwa zaidi, kanisa hilo limefikia hatua ya kuwaomba radhi waumini wake wote wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ikiwa ni pamoja na kanisa zima la KKKT kutokana na tukio hilo.
Dayosisi ya Mashariki na Pwani inapenda kuwaomba radhi waumini wake wote, kanisa zima la KKKT na wale wote wenye mapenzi mema kwa nchi yetu ambao kwa namna moja au nyingine wamekwazwa na tukio hili, linasema tamko hilo.
Likiendelea, tamko hilo linaeleza kuwa, jukumu la kanisa ni kuokoa roho za watu na si kukumbatia mafisadi na walarushwa.
Pamoja na ukali wa maneno katika tamko hilo, KKKT haikueleza iwapo mchango wa shilingi milioni tano zilizotolewa na Rostam katika hafla hiyo zitarudishwa.