Nadhani tangu aingie madarakani, raisi atakuwa ameshajaza pasipoti kama mbili ama tatu hivi kwa uchache, kwa sababu pasipoti zetu zina leaf kama 48 na yeye kasafiri mara kadhaa sana (just kidding).
GT,
Unajua Membe anashangaza na kusikitisha sana kwa utetezi wake wa safari za raisi wetu ambazo tunazipigia kelele. Hivi yeye anafikiri anaongea na 'laymen' sio? Unapoamua kuwaita wawekezaji ujue kuna kitu kinakosekana mahali fulani nyumbani kwako ambacho hakiwavutii. Wawekezaji makini sio watu wa kusubiri kuitwa na kubembelezwa kuwekeza mahali, wao wana mikakati na taratibu zao za kusaka masoko na sehemu za kuwekeza mitaji yao, kiasi kwamba kama mahali fulani pana biashara ambayo mtu anaweza kuwekeza mtaji wake basi wao hufika hata kabla ya kufuatwa na kubembelezwa. Mfano, Afrika Kusini wao wana madini ya aina mbali mbali, hawana haja ya kwenda Ulaya na kuwambia wazungu kwamba wana dhahabu! Ila wazungu ndio wanaifuata dhahabu ya Afrika kusini. Uwekezaji wote wanaopigia kelele akina Membe na wenzake ni katika madini tu, mbona hatuoni viwanda vikubwa vinavyoajiri maelfu ya watu vikianzishwa Tanzania? Mbona hatuoni wawekezaji wa kuaminika katika kilimo? Mazingira ya uwekezaji Tanzania hayavutii na sio tambarare kama viongozi wanavyotaka kutuaminisha kwa sababu:-
1. Miundombinu Mibovu
Barabara nyingi za Tanzania hazipitiki wakati wa masika. Na hii ni tabia sugu ya barabara zetu ambazo zimesahauliwa na sirikali. Unapomuita mwekezaji ili awekeze katika mbuga zetu, ambazo barabara zake si za kuaminika, sidhani kama ataitikia kwa moyo wote. Hakuna haja ya mtu wa Bukoba kupitia Kenya na Uganda anapotaka kwenda mkoani kwake, kama anasafiri kwa basi! Mbona wanaokwenda Ruvuma na Mbeya hawapitii Msumbiji ama Zambia wanapokwenda mikoani kwao? Hali kadhalika, viwanja vidogo vya ndege (airstrips)vingi vimesahaulika, hii nayo inakatisha sana tamaa wawekezaji. Hatuna reli za kuaminika. Bandari zetu ndio sina hata la kusema, zinafanya kazi pole pole sana na kazi zinazofanyika ni chini ya kiwango. Wateja wazikimbia, wanapitishia mizigo nchi jirani. Mwekezaji gani makini atakayepoteza muda bandarini na kupigwa faini na wateja wake kwa kuwacheleweshea biashara zao? Hatuko makini na kile tunachotaka kukifanya.
2. Urasimu
Kuna urasimu sana katika serikali na taasisi zake. Huduma nyingi zinapatikana kwa kuwalamba watu miguu ama kutoa rushwa, sasa kwa wawekezaji makini ambao wanataka kuwekeza mitaji yao mikubwa na yenye maana hawawezi kukubali urasimu huu na mizunguko isiyoisha, ya njoo kesho, kwa sababu muda ni mali.
3. Nishati
Tanzania tuna matatizo makubwa sana ya nishati, hapa namaanisha mafuta na umeme, ambavyo ni nyenzo muhimu sana kwa maendeleo yoyote yale. Umeme wetu ni wa kuazima, kwa maana ya kwamba si wa uhakika/kuaminika. Umeme unakatika bila taarifa, ukija unakuwa pungufu na kadhalika. Mtu anakuwa hana uhakika kama masaa machache baadaye atakuwa na umeme ama la! Sasa kwa mtu ambaye anafukuzana na oda za wateja lazima apate umeme wa uhakika ili azalishe kile wateja wake wanachokihitaji kwa muda huo. Umeme wetu hutegemea maji kwa asilimia 90 ili uzalishwe! Mvua zikigoma na umeme hakuna! Nani mwehu wa kuwekeza katika mazingira ya namna hii? Tunacheza! Bei za mafuta haziaminiki! Leo hivi, kesho vile. Miaka ya nyuma enzi za TIPER (RIP), angalau bei zilikuwa hazibadiliki kila mara kama sasa.
4. Hatuna Utashi wa Kisiasa
Viongozi wetu wengi hawana utashi wa kisiasa wa kuwavutia wawekezaji, sijajua shida iko wapi. Kila nikiangalia televisheni za nchi za nje, nawaonea sana wivu wenzetu wanavyotangaza biashara zao, hasa utalii. Nchi kama Malaysia, Trinidad na Tobago na India zimejaza matangazo ya utalii wa nchi zao katika runinga hizi, sisi kinatushinda nini? Hatuna pesa za kulipia matangazo haya? Hatutaki kujitangaza? Hatuwezi kujitangaza? Shida ni nini? Nani atutangaze? Nani awajibike kwa hili?
Nahitimisha kwa kusema kwamba, kama tunataka wawekezaji wa maana, ni lazima tufagie nyumbani kwetu pawe pasafi ili hao wanaoingia kuwekeza wakute hakuna uchafu. Hapo watakuja hata bila kuitwa, kwa sababu "CHEMA CHAJIUZA".
Ni Mtazamo tu!