Kuna habari kuhusu safari za nje za aliyekuwa rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, ambazo ziliandikwa kwenye gazeti la RAI la
Novemba 27 - Disemba 3, 2003 (wakati bado linamilikiwa na Jenerali Ulimwengu na waandishi wenzake, na kabla hawajauza hisa
kwa Rostam Aziz na wafanyabiashara wenzake - au sijui ni kwa Rostam Aziz peke yake?).
"Rais huyo hulipwa dola za Marekani 30,000 (sawa na sh.32,000,000) kwa siku wakati wa ziara hizo..."
"Mpaka wakati ripoti iliyozaa makala hii inaandikwa mwaja jana [mwaka 2002]...Rais Obasanjo alikuwa amefanya ziara 93 za nje za jumla ya siku 279, na wakati huo akiwa bado katika kipindi chake cha kwanza cha miaka minne ya urais wake."
Kwa mujibu wa habari hizo, Rais Obasanjo katika miaka mitatu ya mwanzo ya urais wake alikuwa amelipwa dola za Kimarekani milioni 8.37 kwa uhalali kabisa kwa mujibu wa viwango anavyostahili kama rais wa Nigeria.
Hapo bado mshahara wake.
Na memsap wake (Mola aweke roho yake mahala pema peponi) alikuwa anapata dola 12,000 kwa mwezi, ikiwa ni posho ya mavazi, kwa mujibu wa habari hizo za RAI.
Kwa mujibu wa hoja niliyoisikia hivi karibuni JK ni mtu makini na anaona njia halali ambayo anayo kwa ajili ya kula 'matunda ya uhuru wa Tanganyika na mapinduzi ya Zanzibar' ni kwa kupanga safari za nje ambako taratibu halali zitamuwezesha naye kupata posho nzuri tu ya safari.
Ukichukulia kuwa amekaa muda mrefu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na pengine alionja hizo posho katika safari zake za uwaziri, inaweza kuleta mantiki kuwa hiyo ndiyo anaona kwake kuwa njia halali ya kujipatia riziki.
Inawezekana wakati wakereketwa wanachakarika kumpigia debe awe rais wa Tanzania, Mheshimiwa alikuwa anawaza: "siku nikiukwaa urais, safari za nje zitanikoma!"
Hoja yangu ndogo ni kuwa JK amesahau kuwa yeye siyo tena Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Somo la leo: Usiige kwenda haja kwa tembo...
Foti Mwarobaini