By Charles Mullinda anasema wanawasiwasi wanamwogopa Mkapa.
RAIS Jakaya Kikwete na serikali yake, Laurence Masha na Kampuni ya IMMMA, Ridhwan Kikwete na Fatma Karume, wana wasiwasi, lakini Benjamin William Mkapa hana wasiwasi. Nadhani nimepatia.
Nadhani wapo wengine wengi wenye wasiwasi, sababu ni ile ile ya kumuogopa Mkapa. Lakini hawa niliowataja sina shaka kabisa kwamba wana wasiwasi zaidi.
Nadhani watu hawa wana wasiwasi kwa sababu wanaogopa kuchafuliwa majina yao, na mtu pekee anayeweza kuyachafua na wakashindwa kujisafisha ni Mkapa, siku ambayo ataamua kuvunja ukimya na kuzungumzia tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwake.
Zisome sababu zinazonifanya nidhani hivyo. Fikiria kama Mkapa atakapokuwa akizungumza madai ya yeye kufumbia macho rafu za waziwazi zilizofanywa na baadhi ya wana CCM waliokuwa wakiwania kuteuliwa kuwa wagombea urais kupitia chama hicho mwaka 2005 na kubainisha kuwa ni kweli aliyeteuliwa kugombea ambaye sasa ndiye rais wetu, yaani Rais Kikwete, alipatikana kwa mizengwe, wananchi watamtazama kwa jicho lipi?
Kwa mfano, Mkapa katika maelezo yake, anatamka kwamba alilamizika kubadili taratibu za upigaji kura wa kumpata mgombea wa CCM kwa makusudi ili kumuwezesha Kikwete ashinde. Anaendelea kueleza kuwa alitaarifiwa kuhusu baadhi ya waliokuwa wakiwania kuteuliwa kuwashawishi wajumbe kwa fedha (rushwa) lakini akakaa kimya kama anavyofanya sasa kwa makusudi tu, halafu anagusia kidogo pia kuhusu kambi moja kutumia silaha ya kuwachafua wagombea wengine ili mgombea wao ashinde, Watanzania watamwelewaje mgombea aliyeshinda?
Hapa ni dhahiri kwamba Mkapa atakuwa amekiri makosa aliyoyafanya, lakini naamini Watanzania wataguswa zaidi na maelezo kwamba uteuzi wa mgombea wa CCM uligubikwa na mizengwe. Kikwete atakuwa amechafuliwa, na nadhani wengi watamuona kama rais aliyeingia madarakani kwa njia zisizo kubalika. Haya, Mkapa huyo huyo siku hiyo kama itatokea kweli, anaeleza kwamba yeye kama rais alikuwa na wasaidizi na washauri waliokuwa wakimsaidia kutekeleza majukumu yake ya urais. Anaeleza kuwa aliwaamini wasaidizi wake hao lakini kwa makusudi waliamua kumwangusha kwa kumshauri vibaya au kufumbia macho baadhi ya vitendo vya ufisadi, halafu anamtaja Rais Kikwete kama mmoja wa waliokuwa wasaidizi wake katika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Itakuwaje hapo?
Nadhani Mkapa anaweza kusema hivyo kwa sababu hata aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, niliwahi kumsikia akijitetea hivyo hivyo baada ya kuandamwa na kashfa ya Richmond. Hapa hata mimi napata wasiwasi, naogopa kwa sababu sijui itakuwaje siku hiyo!
Tuendelee; mimi naamini Mkapa hataishia hapo, atakuwa na maelezo mengi ya kujisafisha yeye binafsi na serikali aliyokuwa akiiongoza kwa sababu inatajwa kuwa ndiyo iliyoulea na kuukumbatia ufisadi. Kama kiongozi mstaafu na mzee mwenye busara za kutosha, anamchagua waziri mmoja ambaye hakuwemo katika baraza lake lakini sasa anatajwa tajwa kuwa kabla hajaingia serikali, kampuni aliyokuwa akiiongoza ilijihusisha na ufisadi. Hamtaji moja kwa moja waziri huyo, anaanzia mbali kidogo kwa kunukuu maelezo ya mmoja wa wakurugenzi wanaoiendesha kampuni hiyo kwa sasa, baada ya vinara wake kadhaa kuteuliwa kuingia serikalini kuitumikia serikali iliyoshinda kwa kishindo uchaguzi mkuu ambao tayari Mkapa atakuwa ameisha uchafua.
Anaeleza miongoni mwa kampuni zilizosaidia kusajili kampuni zinazodaiwa kujihusisha na ufisadi zilikuwa na uhusiano wa karibu na wasaidi wake, hivyo kwa sababu si rahisi yeye kujua kila kitu, inawezekana zilitumia mwanya huo kufanya mambo mabaya yalinayomtia matatani sasa.
Mkapa, kwa kujiamini kabisa kama ilivyo kawaida yake na kwa sauti yake nzito ambayo hupenda kuitumia anapokuwa akizungumzia masuala mazito, anaitaka Kampuni ya IMMMA ambayo mmoja wa wakurugenzi amekwishakiri kuwa iliteuliwa na kampuni mashuhuri ya wanasheria duniani ya Denton Wilde Sapte ya London, kumsaidia mteja wao kusajili Kampuni ya Deep Green Finance Ltd, ikiwaomba wafanyakazi wake wawili, kushikilia hisa moja kila mmoja kwa ajili ya usajili huo.
Anaelezea kushangazwa na kampuni hiyo kuwa ndiyo iliyokamilisha kazi ya usajili wa Deep green Finance Ltd, Septemba 2004 na 2005, ambapo hisa hizo zilizokuwa zikishikiliwa na wafanyakazi wawili wa Kampuni ya IMMMA, zilihamishiwa kwa waliokusudiwa kuwa wanahisa.
Katika hali anayoweza kuieleza kuwa ya kushitushwa na taarifa hizo ambazo labda anasema kuwa alizisoma tu kwenye magazeti, anasema anakubali uchunguzi ufanywe ili kubaini ukweli kuhusu kampuni hii kuhusika kutoa msaada kisheria wa kusajili kampuni iliyokomba mabilioni ya Watanzania.
Nadhani IMMMA wanaomba jambo hili lisitokee, kwa sababu litaibua mapya na yaliyojificha. Najaribu kuota kama itatokea hivyo, naona kuwa Watanzania wataanza kuhoji uhusiano wa watoto wawili wa marais wa taifa hili, Fatma Karume na Ridhiwan Kikwete, na IMMMA.
Watajiuliza, iweje kampuni hii inayodaiwa na imekwishakili kuisaidia moja ya kampuni zinazodaiwa kuiba fedha za Watanzania iwaajiri watoto wa watawala wetu? Amini usiamini, hawatakuwa na habari, na ufafanuzi ulikwisha kutolewa kuhusu ajira au ubia wao katika kampuni hiyo. Watakuwa na wakati mgumu.
Lakini atakayekuwa katika wakati mgumu zaidi ni Masha, mwanasiasa kijana mwenye bahati ya kupata vyeo vikubwa tangu akingali kijana mdogo, ambaye sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani. Na ndiyo maana nikaeleza kuwa nadhani ana wasiwasi, kama yeye pia anawaza kama mimi.
Huenda akawa anakumbuka maswali ya msingi niliyowahi kumuuliza katika moja ya makala zangu kuwa anapaswa kuwaeleza Watanzania kwamba kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge na baadaye kuteuliwa kuwa naibu waziri na sasa waziri kamili, hakuwahi kuhusika hata kwa tone moja na shughuli zozote za kifisadi zinazodaiwa kufanywa na Kampuni ya Deep Green?
Kwamba wakati Deep Green Finance inasajiliwa alikuwa wapi? Serikalini au katika kampuni yake? Wakati inafungua akaunti alikuwa wapi na shughuli zake zilikuwa zipi wakati inachota mabilioni ya fedha zetu kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alikuwa tayari waziri, mbunge au mkurugenzi wa kampuni hiyo?
Ni maswali mapesi kabisa, kwa sababu majibu yake naamini Masha anayo, lakini katika hali tuliyo nayo, yanataka mtu kuwa na moyo wa chuma kuyajibu, kwa sababu ya mabadiliko ya mioyo ya Watanzania kwa sasa. Ni vigumu kuwaaminisha hata kwa jambo la kweli iwapo unatuhumiwa kwa ufisadi!
Tukubaliane, katika hali kama hii, katika ndoto kama hizi ninazoota nikiwa macho, wasiwasi ni jambo la lazima. Na kama kuna mtu anabisha, basi tumuombe Mungu amuongoze Mkapa kuzungumza kama ninavyofikiri na kuota.
Sijui hiri rijamaa rmemuhoji Mkapa naona kama ni onyo kwa Muungwana dah kaazi kweri kweeri.