Kubwajinga
JF-Expert Member
- Jan 23, 2008
- 2,193
- 299
Hatukubali Mkapa adhalilishwe -Pinda
*Asema wataalamu wetu ni butu kujadili mikataba
*Azungumzia mapokezi ya vigogo waliowajibishwa
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imesema haipo tayari kuona Rais mstaafu Bw. Benjamini Mkapa anadhalilishwa kwa kuzomewa hadharani na haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atayebainika kufanya hivyo kwani kufanya hivyo ni ukiukaji wa utawala wa sheria.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda alipokutana na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari katika mkutano wa kufahamiana na kubadilishana mawazo ambapo pia walipata fursa ya kumuuliza maswali.
Akijibu swali kuhusu taarifa za madai ya kukamatwa kwa baadhi ya watu wanaotuhumiwa kumwita Rais huyo fisadi hivi karibuni, Bw. Pinda hakuthibitisha wala kukanusha jambo hilo lakini alisema kamwe hafurahii kuona Rais Mkapa anazomewa anapopita mitaani.
Bw. Pinda alisema yapo mambo yanaweza kufanywa lakini si sahihi hata kidogo kumzomea kiongozi huyo na kwamba vitendo vya kumdhalilisha kamwe havitaruhusiwa katika nchi inayofuata misingi ya utawala wa sheria.
" Hatuwezi kuwa watu wasiojiheshimu, kwa lengo hilo hapana ! waliomwita mhujumu uchumi huenda tabia yao haikuwa ya Kitanzania. Siwezi kufurahia kuona Mkapa anapita anazomewa hata kidogo ! Yapo mambo yanaweza kufanywa, kumshtaki mtu si tatizo lakini sio sahihi kumhukumu mtu bila taratibu kufikiwa," alisema na kusisitiza;
Vitendo vya kumdhalilisha kama Taifa tuseme hapana ! katika nchi inayoongozwa chini ya utawala wa sheria tusichukue sheria mikononi. Siafiki Rais Mkapa kuzomewa, ana heshima yake ni binadamu anastahili heshima, zipo taratibu zinazotakiwa," alionya
Akijibu swali lililohoji usafi wa mawaziri waliobaki madarakani baada ya Rais Jakaya Kikwete kupangua baraza hilo, Bw. Pinda alisema hawezi kuwathibitisha kwa hilo kwani waliomo serikalini ni binadamu kama watu wengine na kufafanua kuwa jukumu lake kama Waziri Mkuu ni kuhakikisha timu hiyo inafanya kazi kwa maadili yanayokubalika na umma.
Alisema Rais Kikwete anajitahidi kutambua na kuteua viongozi wazuri bali matatizo yanayojitokeza ni wahusika wenyewe wanapoingia kwenye dhamana hizo na kusisitiza kwamba suala la uadilifu vita dhidi ya rushwa ni vita endelevu.
"Rais amejitahidi kutambua watu wazuri lakini wanapoingia wanaanza kuhangaika kuangalia huku na huko. Yapo yaliyotokea siku za nyuma lakini hawa tuliona tutazidi kusisitiza suala la uadilifu. Hii ni vita endelevu. Hakuna rushwa inayotoka mbinguni zote zinatoka humu humu," alisema.
Richomond
Kuhusu swali la nani anaendelea kupokea pesa zinazodaiwa kulipwa kampuni hiyo kila siku na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),Bw. Pinda, alisema kampuni hiyo sasa haipo na majukumu yake yalichukuliwa na Dowans ndiyo inapaswa kuhusishwa kwa hilo.
Hata hivyo, alisema uchunguzi kuhusu mapendekezo yaliyotolewa na Tume teule ya Bunge iliyochunguza mchakato wa zabuni ya Richmond bungeni yanaendelea kufanyiwa kazi na tayari kwenye maeneo mengine utekelezaji unaendelea.
Sambamba na hilo alizungumzia mkataba Kampuni ya Kupakua na Kupakia Mizigo Bandarini ya (TICTS) na kueleza kuwa pamoja na uhalali wake umeonekana kuwa na dosari nyingi.
Bw. Pinda alisema kinacholiumiza Taifa sasa na uwezo hafifu wa wataalam kupitia na kukubaliana juu ya mikataba mbalimbali. Alisema kutokana tatizo hilo serikali itaangalia uwezekano wa kushirikisha kamati huru za wataalam wa masuala ya sheria kupitia na kutoa mapendekezo ya mikataba mbalimbali kabla haijasainiwa, ili kupunguza dosari hizo.
Aliko Balali
"Ukiniuliza yuko wapi sijui" alisema Bw. Pinda alipoombwa kutoa taarifa za uhakika kuhusu aliko gavana huyo wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania
( BoT) . Alisema Bw. Balali anahitajika kutokana na masuala ya BoT na kurudia kauli ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bw. Salva Rweyemamu kwamba gavana huyo akihitajika si jambo kubwa, atapatikana.
Mapokezi vigogo
Akijibu swali lililohoji kuwa anajisikia viongozi waliowajibishwa kwa tuhuma za ufisadi kupokelewa kwa makeke majimboni mwao, alisema huo ni mtazamo wa wananchi wao majimboni na kwamba tuhuma hizo haziwaondolei upendo wao. Alisema serikali haina uwezo kuwahukumu kabla ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Bw. Pinda aliwataka watendaji wote wakiwemo mawaziri kuwa wazi kwa vyombo vya habari na kushirikiana kutoa taarifa, binafsi alisema amejipangia utaratibu wa kukutana na wahariri kila baada ya miezi mitatu kujadili na kujibu hoja mbalimbali kwa manufaa ya jamii.
Alivipongeza vyombo hivyo na kueleza kuwa sasa vimeifikisha serikali pagumu kutoka na umakini wa kufuatilia masuala mbalimbali jambo ambalo alisema kuna mambo mengi yanayofanyika sasa ambayo kama vyombo hivyo vingelala yasingefanyika.
" Vyombo vya habari vimetufikisha pagumu tuliomo serikalini, tunafanya kazi mmesukuma mambo, kama 'press' ingelala yasingefanyika " alisema na kuahidi kuwa serikali itajitahidi kuhakikisha uhuru zaidi kwa vyombo vya habari unakuwepo.
Mkuu Mushi,
Nakubaliana na wewe kabisaa, muda wao umeshapita. Kama hata mwanasheria Pinda naye haelewi uhuru wa kukosoa, uhuru wa hotuba (hata kama ni kwa kuzomea) na uwajibishwaji wa viongozi na wananchi. Kiongozi (kwa kuzomewa au otherwise) ni wajibu wao. Kuwakamata wanaotumia uhuru wao na sauti zao ni uonevu na kuwanyima raia rukhsa ya kukosoa hadharani hata kama ni kwa kuzomea ni lazima usitishwe mara moja. Shame on you Pinda.