NA MAGRETH KINABO
SPIKA wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta, amesema suala ya la kuwapatanisha Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya IPP, Reginald Mengi na mbunge wa Mkuranga, Adamu Malima, litazungumzwa baadaye bungeni. Akizungumza na Uhuru jana, Spika Sitta, alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa kama limefikia hatua gani.
"Kama umekuja kuhusiana na suala hili, siwezi kulizungumzia, kwa sasa linaonekana kuwa ni gumu, mimi nimeshachafuliwa jina, nimeshitakiwa hadi kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM). "Mimi naona mtuachie tulizungumzie sisi wenyewe ndani kwa ndani kwa wakati huu, ila kwa sasa siwezi kusema lolote... tutalizungumzia bungeni," alisema Spika Sitta.
Katika kikao cha bunge kilichopita, Spika Sitta alisema angewapatanisha Mengi na Malima kwa kuwaita pembeni wakati wowote. Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Malima kudai kuwa ITV inayomilikiwa na Mengi imekuwa ikitumia muda mrefu kurusha hewani habari zake kuliko za kitaifa au viongozi mfano habari za Rais Jakaya Kikwete.
Wakati huohuo, Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) imesema haiwezi kusema lolote kuhusu uchunguzi unaondelea wa tuhuma za rushwa dhidi ya baadhi ya wabunge. Awali, Mbunge wa Moshi Mjini Philemon Ndesamburo, alidai kuna baadhi ya wabunge wamehongwa ili kupindisha ukweli kuhusu mzozo baina ya Mengi na Malima. Kwa mujibu wa barua ya TAKURU iliyoandikwa na kutolewa jana na Idara ya Elimu kwa Umma, Makao Makuu ilieleza kwamba kwa sasa taasisi hiyo haiwezi kuelezea kazi inayoendelea kwa sababau za kiuchunguzi.
"Uchunguzi utakapokamilika umma utafahamishwa," ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Taasisi hiyo ilisema taaluma ya uchunguzi ina miiko yake, ikiwa ni pamoja na kutozungumzia masuala yanayoingilia uhuru wa raia.