Serikali kuingiza sheria za Kiislamu katika Sheria za Nchi ili zitumike katika mahakama zote kunaweza kuwa ni kinyume na Katiba yetu. Katiba inatamka kwamba kila raia ni sawa mbele ya sheria.
Kwa mfano, itakuwa ni kukinzana endapo kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu (ilyoingizwa ktk sheria za nchi) itakuwa ni halali kutokumrithisha mjane mali fulani iliyoachwa na marehemu mumewe. Mjane huyo huyo angeweza kurithishwa mali hiyo hiyo kwa mujibu wa sheria ya nchi. Kwa maneno mengine, sheria zetu zilizoidhinishwa na Bunge na kuingizwa ktk Statute Book, zisibague raia kutokana na dini zao.
Ni ukweli usiopingika kwamba mashauri mengi baina ya WaTz. sasa yanasuluhishwa na vikao vya ukoo kutegemea mila na desturi za jamii husika. Mashauri mengine hushughulikiwa na vikao vinavyoshirikisha viongozi wa dini, bora tu wahusika wakubaliane na maamuzi au ushauri wa msuluhishi.
Kutokana na ukweli huu, nashauri Serikali iruhusu kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi kwa madhumuni ya kushughulkia mashauri, yasiyo ya jinai, baina ya waumini wa Kiislamu wanaokubali kwa ridhaa yao wenyewe kutumia mahakama hiyo. Mahakama ya Kadhi isajiliwe kama taasisi huru chini ya Sheria ya Taasisi Zisizo za Kiserikali (Non-Govermental Organizations).
Kama NGOs zingine, Mahakama ya Kadhi isitegemee ruzuku toka Serikalini, bali iruhusiwe kukusanya michango ya hiari toka kwa waumini wa Kiislamu nchini na wafadhili wengine wa ndani na nje.
Kama NGOs zingine, Mahakama ya Kadhi iwajibike kutoa taarifa kwa Serikali juu ya mashughuli yake kila mwaka; na mapato na matumizi yake yawe ya wazi na yaweze kukaguliwa na Mkaguzi anayetambulika nchini kisheria.
Ijulikane na itambuliwe kwamba Muumini yeyote wa Kiislamu anayepeleka shauri lake mbele ya Mahakama ya Kadhi, asiporidhika na hukumu au uamuzi wa Mahakama, anaweza kukata rufaa katika mahakama ya kiraia. Mpangilio huu utahakikisha Waislamu wanaotaka watapeleka mashauri yao Mahakama ya Kadhi, na Statute Book yetu itabaki na Sheria zinazo-apply kwa raia wote bila kubagua.