Gavana Daudi Balali ajiuzulu
*Amwandikia Kikwete barua akiwa Marekani
Na Mwandishi Wetu
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Daudi Balali, amejiuzulu.
Habari za Gavana Balali kujiuzulu, zilipatikana Dar es Salaam jana kutokana na barua aliyomwandikia Rais Jakaya Kikwete akiwa Boston, Marekani, ambako amelazwa akitibiwa.
Nakala ya barua hiyo ambayo Majira iliipata jana, inaonesha kuandikwa juzi na kusainiwa na Bw. Balali mwenyewe, ikieleza kuwa kutokana na afya yake, hawezi kuendelea kutimiza wajibu wake kikamilifu.
"Mheshimiwa, kama unavyoelewa, nimelazwa hospitalini kwa zaidi ya miezi mitatu sasa hapa Boston, Marekani, kutokana na upasuaji mkubwa niliofanyiwa.
"Kwa matatizo yaliyojitokeza ya hali yangu ya kiafya, sioni kama kuna dalili za kuonesha ni lini nitakuwa nimepona kabisa na hata kuendelea na wajibu wangu kikazi.
"Kwa mazingira hayo, naona inafaa niachie nafasi hii na hivyo naandika barua ya kujiuzulu kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania," barua hiyo ya ukurasa mmoja ilisema.
Ili kufahamu kama barua hiyo imefika Ikulu na ni nini majibu yake, Majira iliwasiliana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Bw. Salvatory Rweyemamu, ambaye alisema hakuna mawasiliano yoyote rasmi yaliyokwishafanywa kati ya Gavana na Rais.
"Mpaka sasa ninapozungumza nawe, hakuna mawasiliano yoyote rasmi kati ya pande mbili hizi husika, lakini kama yatakuwapo yatashughulikiwa kwa taratibu na kanuni za kawaida zilizopo na vyombo husika," alisema Bw. Rweyemamu.
Hatua hii ya Bw. Balali imekuja huku uchunguzi wa ubadhirifu ndani ya BoT ukiwa tayari umekamilika na ripoti amekabidhiwa Rais kwa hatua zaidi.
Uchunguzi huo uliagizwa na Serikali kufanyika ili kubaini kama kulikuwa na ubadhirifu ndani ya BoT hasa ukishusisha ujenzi wa majengo mawili 'twin towers' ya Benki hiyo.
Serikali ilifanya uchunguzi huo kupitia Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambapo Kampuni binafsi ya Uingereza ya Ernst & Young ilifanya ukaguzi huo na kuwasilisha ripoti yake kwa Rais.
Uchunguzi huo ulitokana na shinikizo kutoka kambi ya Upinzani ambayo kupitia Katibu Mkuu wa CHADEMA ambaye pia ni Mbunge wa Karatu, Dkt. Wilbroad Slaa, ilitangaza ilichokiita orodha ya mafisadi, huku Gavana Balali akiwa mmoja wa waliotajwa kuhusiana na ubadhirifu ndani ya BoT.
Kutokana na shinikizo zaidi kutoka Upinzani kutaka Rais Kikwete atoe kilichomo katia ripoti hiyo, juzi CCM kupitia kwa Katibu wake Mwenezi, Bw. John Chiligati, aliwataka wanasiasa kuvuta subira ili baada ya mapitio ya ripoti hiyo, Rais atautangazia umma.
Juzi akizungumza na waandishi wa habari, Rais Kikwete aliulizwa kuhusu aliko Bw. Balali kutokana na hisia kuwa pengine amekimbia kashfa ya BoT, alisema yuko Marekani anaumwa na yuko kwenye matibabu.
Source: Majira