Mohamed mkokota: Mpigania uhuru wa Tanganyika aliyeomba kibali cha kwenda kutawala Uingereza

Manyanza

JF-Expert Member
Nov 4, 2010
9,529
14,430
Na Kizito Mpangala ..

"Mohamed Mkokota, hautaweza kupata eneo la kutawala Uingereza kwa sababu wewe ni mweusi na pia wewe siyo Mwingereza." Lilikuwa jibu la Gavana wa Kiingereza nchi ya Tanganyika aliyemwakilisha Malkia wa Uingereza akimjibu bwana Mohamed Mkokota wa Lindi mwaka 1939.

Lindi hapa pichani. Umewahi kufika? Naam, ni Lindi kwa Wamwera, Wangindo, Wamatumbi, Wayao na wengine. Lindi inaelezwa kwamba jina hilo lilitolewa na wageni kutoka Oman, wakapaita Lindi (yaani "Deep Channel"). Ukisafiri kwa basi barabara inapita kando ya bahari, unaona mandhari yake yalivyo ni "deep channel" kweli kweli. Historia yetu ina mengi na vile hayajatunzwa zaidi katika maandishi kwa manufaa ya wengi, basi kwa kidogo hiki nisemacho nawe ubahatike kupata maarifa haya kujua tulikotoka na tuende vipi kwingineko.

Kwanza sijapata picha ya Mohamed Mkokota, ikiwa mtu anayo basi anaweza kutusaidia. Safari ya kupigania uhuru wa Tanganyika kwa wengi huipata kuanzia zama za Mwalimu Julius Nyerere lakini kwa wengi pia huipata kuanzia nyuma ya Zama za Mwalimu Julius Nyerere. Kisini mwa Tanganyika palikuwa na watu wenye nia ya kuona nchi yao inaendeshwa na wazawa. Mmoja kati yao ni ndugu Mohamed Mkokota wa Ruponda.

Mohamed Mkokota alikuwa na ujuzi wa kutengeneza nguo kwa mashine yake ambayo baadae alinyang'anywa na Serikali na kumpiga marufuku kufanya kazi hiyo. Akawa hana pa kujiingizia kipao! Nguo alikuwa akitengeneza ziliitwa Likwia. Mashine yake aliyonyang'anywa ilipelekwa Nachingwea kwani walijua asingeliweza kuifuata huko mbali.

Ndugu Mohamed Mkokota alikuwa mereketwa wa utawala wa Maliwali ambapo matendo yo na dhulma yaliwaudhi wananchi lakini hawakusikilizwa hata walipotoa taarifa kwa D.C na kwa P.C wa Lindi. Mohamed aliona kuwa ipp haja ya wananchi wa Lindi kuwa na viongozi wazawa badala ya waliopo ambao wengi walikuwa ni wenye asili ya Kiarabu na wenye viburi kwa kuwa Serikali ya Kiingiereza iliwalinda. Wananchi walifanya mashauri polepole na kutaka Maliwali wenye asili ya Kiarabu waondolewe na badala yao wawekwe Maliwali wazawa.

Mohamed Mkokota alikuwa mipngoni mwa waliojitokeza katika madai hayo lakini ajabu ni kuwa yeye hakuwania kupata nafasi ya kuwa Liwali lakini alifanya vile kwa manufaa ya wengi na jakuwa na mpango wa kuwa Liwali ila tu pawepo na Maliwali wazawa. Katika hao waliojitokeza kwenye madai hayo, Mohamed ndiye alionekana kuwa mstari wa mbele kupigania uhuru wa watu wake wajitawale. Aliandika maombi kadhaa kwa D.C na P.C wa Lindi lakini viongozi hao hakuona sababu yoyote ya kufanya hivyo.

Mkokota alipoona kuwa anapuuzwa na maombi yake hayafanyiwi kazi, alimua kuondoka Lindi kwenda Dar es Salaam kuonana na Gavana. Ilikuwa ni mwaka 1939. Haikuwa safari nyepesi hasa upande wa malazi haikuwa na ndugu Dar es Salaam isipokuwa rafiki yake mwalimu Herman Abdallah Mkalipwelela aliyekuwa akifundisha katika shule ya Mchikichini. Alifika Dar es Salaam kwa rafiki yake huyo na kumweleza nia yake ya kuonana na Gavana.

Mkokota alijadili na rafiki yake nakna ya kumfikia Gavana kwani haikuwa rahisi kumfikia kiongozi mkubwa vile. Siku iliyofuata baada ya kupeana mbinu, Mohamed Mkokota alikuwa tayari kwenda Ikulu Magogoni kuonana na Gavana. Alipofika Ikulu alipokelewa na alionana na Gavana. Wakiwa ofisini Mohamed alicheza na akili ya Gavana kwa kumtega kwa mtego mdogo tu ambapo Gavana alinasa mwenyewe vizuri kabisa kwenye mawindo ya Mohamed Mkokota.

Mkokota humo ofisini alimwambia Gavana "nimefika hapa ili nipate kibali na hati ya kusafiria nataka kwenda Uingereza ili nipate eneo la kutawala huko Uingereza." Gavana alimjibu "Mohamed Mkokota, hutaweza kutawala Uingereza kwa sababu wewe ni mweusi na pia siyo Mwingereza." Jibu hilo lilikuwa ndiyo mlango uliofumguliwa na Gavana ili Mohamed aingie na kueleza kilichomleta. Kwa hakika hakuwa na nia ya kwenda kutawala Uingereza ila alitumia mtego hup ili kumnasa Gavana kisha yeye aeleze kilichomleta. Basi akajibu "Ikiwa haiwezekani kwa Mmwera wa Lindi kutawala Uingereza, inawezekaje basi watu wa mataifa mengine kutawala taifa jingine?" Hapa aliwalenga Maliwali wa wenye asili ya Kiarabu na wakoloni kwa ujumla. Hapo Gavana ilibidi amsikilize Mkokota madai yake. Kisha alamruhusu arudi nyumbani.

Baadae Gavana baada ya kufanya mazungumzo na Mohamed Mkokota, alipeleka taarifa kwa D.C na P.C wa Lindi kuwa Maliwali wote wenye asili ya Kiarabu waondolewe na badala yao watafutwe Maliwali wapya wazawa. Taarifa hiyo ilipuuzwa na haikifanyiwa kazi na badala yake ukazuka uhasama baina ya Mohamed Mkokota na D.C na P.C wa Lindi. Gavana kwenye taarifa yake alisema madai ya Mohamed Mkokota ni sahihi hivyo kufanyike mabadiliko. Mkokota aliporudi kutoka Dar es Salaam aliitwa na D.C wa Lindi na kuhojiwa. Mkokota aliwajibu kwamba alitaka wananchi wenyewe kutawala nchi yao. Hapa unaona wazi kwamba Mkokota alipigania uhuru wa Tanganyika kwa eneo lake la Lindi. Fikra zake za wananchi wenyewe kutawala nchi yao ilikuwa ni ya wengi Tanganyika wakati huo.

Amri ya Gavana haikufanyiwa kazi. Badala yake kukawa na uadui mkubwa uliotokea baina ya Liwali Kasim Saidi na Mohamed Mkokota, wote wa Ruponda. Uadui wao ni wa kihistoria. Uadui huo kati yao ulidumu kwa miaka 8. Yaani tangu mwaka huo 1939 hadi mwaka 1947.

Tangu Mkokota alipofanya uamuzi wa kwenda Dar es Salaam kuonana na Gavana, aliporudi aliishi kwa kusumbuliwa hapa na pale. Alishitakiwa kwa D.C wa Lindi zaidi ya mara tatu akidaiwa kuwa mtu hatari anayeipinga na kukwamisha shughuli za Serikali. Hayo pia yamo hata sasa kwamba unaweza kupuuzwa katika ofisi za umma au kwenye mabenki kama alivyowahi kudokeza kaka Emmanuel Kihaule kwenye mabenki kulivyo. Basi ukidadisi utaonekana mtu ynayetazamika kwa jicho la namna nyingine hasi badala ya chanya. Ndivyo alivyotazamwa Mohamed Mkokota.

Hata hivyo, Mkokota hakuacha kupigania uhuru na haki ya Tanganyika kujitawala hasa akipiganua kwa upande wa Lindi. Mkokota alionekana kuwa aduni namba moja wa Serikali huko kusini. Alipigania eneo hilo kuwa na Maliwali wazawa/wazalendo badala ya wale wenye asili ya Kiarabu na Kiingereza, ambapo aliamini kuwa haiwezekani kwa mataifa mengine kutawala taifa jingine na kuwaweka kando wazawa wasipate nafasi za uongozi ili wawe wanaaikiliza madai mbalimbali ya wananchi wenzao na kuyawasilisha Serikalini kwa weledi badala ya viongozi wageni wasiojua vema jamii za wazawa.

Mkokota alilamatwa na kupelekwa Mahabusu huko Ruponda. Mkokota alisaidiwa na rafiki yake kutoka Mahabusu. Na hiyo ilitokana na uhasama aliouanzisha Liwali Kasim Saidi wa Ruponda. Baada ya uhasama wa miaka minane, habari zilimfikia rafiki yake mpendwa Dar es Salaam. Ni Mwalimu Herman Abdallah wa shule ya Mchikichini. Sasa hivi Mchukichini ni mahali maarufu kwa masomo ya ziada yaani Tuition.

Habari zilipomfikia Mwalimu Herman Abdallah Mkalipwelela mjini Dar es Salaam, alijitosa na kuwa upande wa rafiki yake, hivyo Liwali Kasim Saidi akajiingiza, bila kujua, kwenye vita n watu wawili; Mohamed Mkokota na rafiki yake aliyemsaidia kuonana na Gavana, Mwalimu Herman Abdallah Mkalipwelela. Kwenye jamii kuna wakati unaweza kujiona unapambana na mtu mmoja lakini kumbe unapambana na kundi kubwa. Kuna watu wana watu wao, yaani ukimchokoza mmoja basi watajitokeza wenzake bila wewe kujua kuwa upo kwenye pambano na kundi badala ya mtu mmoja. Kuwa makini.

Kisa hiki pia kinatyonyesha changamoto ya mawasiliano wakati huo. Fikiria muda ambao Mohamed Mkokota alianza kuandamwa na pia muda ambao rafiki yake alipata taarifa hizo. Maana yake ni kwamba ikiwa Mwalimu Herman Abdallaha angetwaliwa na Allah basi Mkokota angeendelea peke yake kupambana.

Hatimaye mwaka 1947 Serikali iliamua kumpa haki Mohamed Mkokota na kuepusha madhara ya uadui uliokuwa ukiendelea baada ya Mwalimu Herman Abdallah kuonfeza nguvu kwa rafiki yake dhidi ya Liwali Kasim Saidi aliyekuwa upande wa Serikali. Serikali iliona Mohamed Mkokota hakomi licha ya vitisho alivyopata na pia kuwekwa Mahabusu, lakini aliendelea kupigania haki na uhuru wa Tanganyika kupitia eneo lake la Ruponda, Lindi, ili kuwe na Maliwali wazawa/wazalendo.

Basi Serikali alifikia uamuzi wa kumuondoa Liwali Kasim Saidi na kumuweka Liwali mpya bwana Mohamed Chingwelu. Mafanikio haya ya Mohamed Mkokota ambaye hakuwa na uchu wa kupata eneo la kutawala, yalileta mabadiliko makubwa ya Maliwali huko Lindi japokuwa hayakutatua matatizo yote ya uonevu na dhulma kwa wananchi. Lakini hatua ya kwanza ya mfanikio yake, Mkokota, ilionekana.

Harakati za Mohamed Mkokota baadae zilichochea/kuhamasisha wengine kuwa karibu na masuala ya Kiserikali na kupigania uhuru wa maeneo yao ili yatawaliwe na wazawa. Vilevile tunapata somo juu ya urafiki bora. Ni mfako wa kuigaa kwa urafiki wa Mohamed Mkokota na Mwalimu Herman Abdallah kwamba urafiki si wakati wa raha tu, bali hata katika matatizo.

Haijulikani wazi kama kuna namna yoyote ya kumuenzi ndugu Mohamed Mkokota. Ujasiri wake wa kwenda kuonana na Gavana ulikuwa wa kipekee hasa umbali uliopo kati ya Dar es Salaam na Lindi. Mohamed Mkokota ni mfano wa kuigwa katika maisha wakati wa mapambano ya jambo lolote lenye manufaa baadae. Huu ndiyo ujasiri wa mpigania uhuru Mohamed Mkokota kutoka Lindi.
 
Back
Top Bottom