Dorothy Semu: Mwaka 2024 tutapigania maisha ya heshima kwa Watanzania wanyonge

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
Utangulizi.

Tumetimiza siku 10 tangu tuumalize 2023 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2024. Kwa kawaida tumezoeleka kuzungumza na umma kupitia vyombo vya habari kuhusu mambo mbalimbali yaliyojiri kwa mwaka mzima mwishoni mwa mwaka.

Tangu kuundwa kwa chombo hiki mwezi Februari 2022 kimekuwa chombo mbadala wa Serikali kwa kumulika, kufuatilia, kukosoa na kuzalisha mapendekezo ya kimtazamo, fikra na kisera juu ya maamuzi na utendaji wa Serikali na vyombo vyake tanzu.

Leo katika Mkutano huu nitaeleza kwa kifupi sana mambo makubwa tuliyoyapigania mwaka 2023 na kutoa mwelekeo wa jumla wa Baraza Kivuli la ACT Wazalendo kwa Mwaka 2024
  • Hoja na mambo tuliyopigania mwaka 2023.
  • Kupanda kwa gharama za maisha kwa watanzania
Kwa mwaka mzima tumeshuhudia kwa nyakati mbalimbali wananchi wakilalamikia hali ngumu ya maisha inayosababishwa na kupanda kwa bei mbalimbali za bidhaa na huduma (bidhaa za chakula; bidhaa za mafuta ya petroli, Diseli na mafuta ya taa; bidhaa za mbolea na kupanda kwa nauli za mabasi na daladala kwa upande mmoja. Kuporomoka kwa bei za mazao ya wakulima kama vile korosho, pamba na tumbaku kwa upande mwingine).

ACT Wazalendo imekuwa ikitoa mapendekezo ya kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha kwa; Kutoa wito wa kuiwezesha kibajeti Wakala wa taifa wa chakula (NFRA) ili iweze kununua na kuhifadhi chakula cha kutosha na kuwawesha wakulima kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao. Pia, kupunguza matumizi ya bidhaa na huduma kutoka nje hususani bidhaa za mafuta kwa kutumia nishati mbadala ya Gesi asilia kwenye vyombo vya usafiri ili kuokoa matumizi makubwa ya fedha za kigeni na kuingiza mfumuko wa bei (imported inflation)
Serikali ilichukua mapendekezo ya kuiwezesha NFRA ingawa kwa bajeti kiduchu. Aidha, bado Serikali inajivuta katika kuchukua hatua za kupunguza matumizi ya uagizaji wa bidhaa na huduma ambazo tunaweza kuzizalisha ndani au kupata mbdala.

Migogoro ya Ardhi nchini.
Nchi yetu imeendelea kughubikwa na migogoro ya ardhi katika maeneo na ngazi mbalimbali. Changamoto ya migogoro ya ardhi nchi inazidi kuwa kubwa kila uchao, ipo migogoro kati ya wafugaji na wakulima, wananchi dhidi ya Serikali, wananchi dhidi ya wawekezaji lakini kwa nyakati zote waathirika ni wananchi, wao ndio wanaopoteza haki zao za kutumia ardhi. Mara kadhaa tunashuhudia mauaji, mapigano, ufukuzwaji na uondolewaji wa wananchi kwenye ardhi zao.

Mara kadhaa tumekuwa tukieleza migogoro kati ya wakulima na wafugaji hii tumeikuta bado ni changamoto kubwa maeneo mengi pia yapo yale yanayochomoza kama vile Mikoa ya kusini (Lindi, Mtwara na Ruvuma) hii inatokana na ufinyu wa maeneo bora au kutofuatwa kwa matumizi bora ya ardhi yaliyopangwa na vijiji.

Sura ya pili ya migogoro inatokana na kuibuka kwa utitiri wa Makampuni ya ununuzi na uuzaji wa ardhi, viwanja (Real Estates) kitendo kinachochochea ardhi kugombaniwa; Wajanja wachache wanatazama ardhi kama mtaji wa kukuza biashara na kuvuna faida- wanawapora (disposses) wananchi kwa bei za chini. Hali hiii ipo zaidi maeneo yanayoathiriwa na kupanuka kwa miji mikubwa hivyo kumeza maeneo ya pembezoni kama vile Mkuranga, Kisarawe, Kibaha, Bagamoyo (Maeneo yanazungukwa na DSM)- kwa mwenendo miaka 5 ijayo hali itakuwa mbaya zaidi.

Sura ya tatu, wimbi kubwa la wawekezaji; mwelekeo na mtazamo wa serikali kupitia hotuba na kauli za viongozi kuhusu ardhi, umejengeka kuona kwamba ardhi ni mtaji au bidhaa. Kwa mtazamo huu, ardhi inapaswa itumike kutengeneza faida zaidi kuliko kukidhi mahitaji ya kijamii. Serikali imekuwa ikitoa upendeleo kwa wawekezaji kwa gharama ya maisha ya wananchi kwa kuporwa au kunyang'anywa ardhi kisheria kwa jina la uwekezaji.

Dhana iliyojengwa na watawala kwa muda mrefu kwamba wazalishaji wadogo ni kikwazo cha maendeleo, hivyo serikali inapaswa kuwapa fursa au kuwawezesha wakulima wakubwa hasa wawekezaji kuweza kupata ardhi kwa urahisi kwa misingi ya kwamba ndio wenye uwezo na ujuzi wa kuyaendeleza maeneo yao kwa faida.

Kutokana na dhana hii tumeishia kuona uporaji na unyang’anyi wa ardhi za vijiji na wanavijiji kwa wananchi kulazimishwa au kulazimika kuhama katika ardhi zao ili kupisha uwekezaji wa Serikali au watu, taasisi na makampuni binafsi wamekuwa wakipunjwa fidia. Kupitia dhana hii ya uwekezaji uchwara unaojali wazalishaji wakubwa na kuwakandamiza wazalishaji wadogo ndio inachochea migogoro nchini.

Sura ya Nne; Taasisi za Serikali kupora ardhi ya wananchi; matukio ya namna hiyo tumeyakuta kuanzia Pwani; Mamlaka ya Bandari imepora ardhi ya wananchi zaidi 120 Kisiju ili Kujenga Bandari bila kutoa fidia tangu mwaka 2017. Wakala wa misitu (TFS) kuchukua ardhi ya wananchi maeneo ya muhoro wilaya ya Rufiji, Mkoani Pwani kwa kuzuia mazao yao, kuwakamata vijana na kuwaweka vizuizini na wengine kujeruhiwa.Katika jitihada za kuwasemea wanachi kupitia kupokea malalamiko, ziara, utafiti pamoja na ripoti mbalimbali za kitaalamu tumekuta Migogoro ya ardhi ni moja ya matataizo makubwa sana nchini, na kama itaendelea hivi basi ipo hatari ya kupungua kwa uzalishaji na hata jamii nyingi kukumbwa na baa la njaa, kufa kwa mifugo.

ACT Wazalendo tumekuwa tukilisemea jambo hili mara kwa mara kwa kumshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda tume maalum (Presidential commission of inquiry) kama ile ya prof. Shivji iliyozaa sheria ya ardhi namba 4 na 5 ya mwaka 1999 kupitia na kuchora upya ramani na kupanga matumizi bora ya ardhi yanayoendana na wakati na mahitaji ya sasa ili kuondoa kabisa migogoro iliyopo sasa
Hoja za kibajeti
Katika kazi kubwa tulizozifanya mwaka uliopita ni kuchambua Bajeti za Kisekta za Serikali, Bajeti kuu ya Serikali na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali hoja kubwa tulizozisukuma kwa kifupi ni zifuatazo;
  • Kupanda kwa bei za chakula; Serikali iiwezeshe Wakala wa hifadhi ya Chakula NFRA pamoja na Bodi ya mazao mchanganyiko CPB kuweza kununua na kuhifadhi na kusambaza mazao mchanganyiko ya chakula ili wakati bei zikipanda wayaingize sokoni ili kupoza bei ya mazao kwa wananchi.
  • Kukua kwa deni la Taifa; Serikali ipunguze uwiano wa mikopo ya kibiashara kwenye deni la Serikali hadi kufikia asilimia 20 ifikapo mwaka 2025.
  • Kuongezeka kwa tozo na kodi; Serikali ijielekeze kubuni vyanzo vingine vya mapato (non-tax revenue) vitakavyosaidia kugharamia Bajeti ya Serikali kuliko kuongeza tozo na ushuru kwa wananchi wanyonge. (Iondoe kabisa tozo yote ya miamla ya Simu na Benki, kupunguza tozo kwenye bidhaa muhimu kama vile mafuta ya kula, petroli, diseli, saruji, ngano na sukari pamoja na Mbolea ili kukabiliana na mfumuko wa bei).
  • Kudhibiti mianya ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma na kuwachukulia hatua wote wahusika kwenye ubadhirifu. Kama vile fedha za mikopo kwa vijana, Wanawake na watu wenye ulemavu kuunganishwa na mfumo wa hifadhi ya jamii.
  • Serikali isimamie mgao wa fedha za Muungano kwa usawa na kwa mujibu wa kanuni. Serikali iufuate katiba ya nchi kwa kuanzisha Akaunti ya Pamoja ya Fedha kwa mujibu wa sheria
  • Serikali kuzingatia sheria na taratibu za manunuzi ili kuzuia ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma.
Hoja hizi kubwa za kibajeti bado hazijafanyiwa kazi na Serikali ni chache sana zimechukulia lakini utekelezaji wake sio wenye ufanisi mkubwa.
Mambo ya nje
OWAKI pia imefanya kazi za mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Waziri kivuli wa mambo ya nje tumekua miongoni mwa mambo hayo ni;
  • Sakata la watanzania wanaoshikiliwa katika magereza mbalimbali nchini Msumbiji, ambao hadi sasa hawajapatiwa ufumbuzi wowote, na tayari mwezi disemba tumemwandikia barua waziri wa mambo ya nje kufuatilia suala hilo.
  • Kuwatia nguvu na kushirikiana na nchi zingine zilizopatwa na majanga au maafa mbalimbali kwa kutoa salamu za pole na kutembea balozi zao hapa nchini; Mathalani Uturuki, Morocco na Libya kufuatia mafuriko na matetemeko ya ardhi yaliyoyakumba maeneo hayo.
  • Kupigania uraia pacha kwa watanzaia waliochukua uraia wa nchi zingine kwa kuanzia kundi maalum kwa watanzania wenye vipaji vya michezo.
  • Kuwashika mkono wananchi wengine nje ya Tanzania kupigania demokrasia ya uchaguzi na uhuru wa vyama vingi.
  • Ushiriki wa Baraza katika Mabadiliko ya sheria, Sera, Mijadala ya kitaifa na sera.
Ofisi ya wasemaji wa kisekta (OWAKI) au baraza kivuli kama ilivyozoeleka imekua ikishiriki mambo mengi ya kisera, kisheria na Mijadala ya kitaifa miongoni mwa mambo tuliyoshiriki ni
Maboresho ya Sera ya Elimu na Mitaala
Maoni yetu kwenye mjadala wa sera ya elimu na mitaala ulikuwa kwenye sehemu tatu;
  • Lugha ya kufundishia iwekwe wazi.
  • Falsafa ya Elimu ya kujitegemea imewekwa kuegeshwa tu kwenye sera hii
  • Suala la ugharamiaji wa Elimu bado halijawekwa wazi.
  • Mswada (sasa sheria) wa Bima ya Afya kwa wote
Tunaendelea kusisitiza kufungamanisha bima ya afya na hifadhi ya jamii ili kujenga uwezo wa wananchi kupata huduma kwa usawa.
Uwekezaji katika Bandari ya Dar es salaam
Wito wetu ni kuhakikisha bandari inaendesha kwa ubia wa 50/50 kati ya Tanzania na Kampuni ya DP World.
Miswada ya Sheria za uchaguzi na vyama siasa

Tulianza kuhakikisha kwamba Serikali inapeleka bungeni maoni ya wadau wa mageuzi ya kisiasa ili kuweka mazingira mazuri ya uendeshaji wa siasa zetu nchini. Ingawa serikali imechukua hatua hiyo bado miswada hii haijagusa maeneo muhimu ili kuimarisha demokrasia. Mwaka huu 2024 tunaenda kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Tanzania Bara. Tunarudia wito wetu kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa usisimamiwe na TAMISEMI na badala yake usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi.

B: Mwelekeo wa Baraza Kivuli kwa mwaka 2024
Kama nilivyoeleza hapo awali kwamba mwaka uliopita ulikuwa wa mgumu sana kwa wananchi wa kawaida. Hali hiyo haijabadilika sana licha ya kuonyesha kwamba kuna hatua tumezifanya kama baraza ili kuleta nafuu kwa watu. Kwa mwaka huu tutaongeza jitiahada zaidi na kwa robo ya kwanza tutapigania zaidi mambo yafuatayo;
  • Kuendelea kupigania unafuu wa gharama za maisha kwa kutoa mapendekezo zaidi ya kudhibiti kupanda kwa bei za bidhaa
  • Kuishinikiza Serikali kutazama upya bei za nauli za mabasi na daladala nchini
  • Kutopatikana kwa uhakika kwa huduma ya umeme (mgawo)
  • Kupigania haki na usalama wa ardhi kwa wananchi mijini na vijijini ili kumaliza migogoro ya ardhi nchini
  • Marekebisho ya kanuni ya kukotoa mafao ya wastaafu (Kikotoo cha mafao)
Hitimisho.
Katika miaka miwili tumeendelea kuwa sauti ya watanzania, kupaza sauti katika masuala mbalimbali, hata hivyo Serikali imekua ikilazimisha kupitisha sheria mbovu zinazowakandamiza wananchi mfano sheria ya huduma za Habari na sheria ya Bima ya Afya kwa wote, tunauanza mwaka 2024 tukiwa na ari kubwa huku tukitegemea ninyi wanahabari na Vyombo vya Habari mtatupa ushirikiano wa kutosha katika kupaza sauti za watanzania.

Ahsanteni sana!
Ndg. Dorothy Jonas Semu,
Waziri Mkuu Kivuli,
ACT Wazalendo,
10 Januari, 2024.
Dar es Salaam.
 
Utangulizi.

Tumetimiza siku 10 tangu tuumalize 2023 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2024. Kwa kawaida tumezoeleka kuzungumza na umma kupitia vyombo vya habari kuhusu mambo mbalimbali yaliyojiri kwa mwaka mzima mwishoni mwa mwaka.
Tangu kuundwa kwa chombo hiki mwezi Februari 2022 kimekuwa chombo mbadala wa Serikali kwa kumulika, kufuatilia,
Dar es Salaam.
Mtafukuzwa zanzibar na chama kimekufa! Take care
 
Utangulizi.

Tumetimiza siku 10 tangu tuumalize 2023 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2024. Kwa kawaida tumezoeleka kuzungumza na umma kupitia vyombo vya habari kuhusu mambo mbalimbali yaliyojiri kwa mwaka mzima mwishoni mwa mwaka.
Kwa huku bara wala hamna joto lolote la watu kujua mnachoongea. Ni kweli mmeandika kisomi, lakini serekali hii haijali maandiko ya kisomi, Bali inajali shinikizo toka kwa watu wa kawaida.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom