Natumaini walioko Dar watueleze kama fukwe za bahari hasa Ocean Road kama zimeanza kutumika kupiga picha (za arusi). Creativity is mother of everything..natumaini madiwani wetu busara zitawaingia kichwani kuhusu yaliyonenwa na Mh. Rais.
Kikwete awapasha madiwani Dar
Veronica Mheta
Daily News; Thursday,January 29, 2009 @21:15
Rais Jakaya Kikwete amewataka madiwani wa Jiji la Dar es Salaam kubuni mbinu zitakazowawezesha kupata mapato badala ya kuzuia wananchi kutembelea au kupiga picha maeneo ya fukwe za bahari.
Aidha, amewataka madiwani kuacha tabia ya kuruhusu maeneo ya wazi yaliyotengwa kwa ajili ya michezo, wananchi kupumzika ambayo hivi sasa yamejengwa makazi ya watu au ghorofa za biashara.
Rais Kikwete aliyasema hayo juzi usiku Dar es Salaam katika hafla ya kumpongeza kwa utendaji wake wa kazi kwa kipindi cha miaka mitatu iliyoandaliwa na madiwani wa Jiji la Dar es Salaam. Alisema ni muhimu madiwani kubuni mbinu zitakazowasaidia kupata fedha badala ya kuwazuia wananchi kwenda maeneo ya fukwe kupiga picha za harusi au matukio mengine.
Alizitaka manispaa za Jiji kutoa tangazo kwa wananchi wanaotaka kutumia fukwe za bahari ili walipe fedha kidogo zitakazosaidia Jiji kupata fedha na si kuwazuia. Jamani ni aibu kuwazuia wananchi kupiga picha kwenye fukwe, toeni tangazo ili wanaotaka kutumia fukwe kwa matukio maalumu wapate vibali na si kuwazuia. Pia maeneo yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya michezo au mapumziko yawe wazi
zoeni takataka jiji liwe safi kwani nchi za nje wananunua takataka na kuzalisha vitu mbalimbali, alisema Rais Kikwete na kuongeza: Tatizo lenu madiwani si wabunifu wa kupata mapato, kusanyeni taka na mtangaze zabuni ili watu mbalimbali waje kuzinunua kwa kufanya hivyo mtakusanya vyanzo vya mapato.
Aliwasihi madiwani kutoruhusu ujenzi wa ghorofa kwenye baadhi ya mitaa, na badala yake anayetaka kujenga ghorofa apewe eneo linalostahili kujengwa ghorofa na si kwenye mitaa ambayo wananchi wamejenga nyumba za kawaida, akisema ujenzi huo wa ghorofa kwenye mitaa unachangia mazingira kuwa machafu kwa sababu hakuna mfumo wa kupitisha maji taka.
Pia aliwataka madiwani kuhakikisha malori ya mizigo yanaondoka eneo la Jangwani ili eneo hilo liwe wazi na vijana wapate sehemu za kucheza michezo mbalimbali, kwani enzi za zamani eneo hilo lilikuwa likitumika kwa michezo zaidi. Naye Naibu wa Jiji la Dar es Salaam, Ahmed Mwilima alisema wamezipokea changamoto hizo na kuahidi kuzifanyia kazi ili Jiji lipate mapato mengi.
Aliwataka madiwani wenzake kuacha tabia za kuogopa kujadili na kutoa uamuzi sahihi juu ya mambo mbalimbali. Aliwasisitiza kutokubali kupitisha ujenzi wa maeneo yaliyo wazi badala yake madiwani hao wasisitize maeneo yaliyo wazi kuachwa ili wananchi wapate sehemu za kupumzika au watoto kucheza; huku wakihakikisha Jiji linakuwa safi.
HabariLeo: Gwiji la habari Tanzania | Kikwete awapasha madiwani Dar