Joseph Lugendo
Daily News; Friday,March 06, 2009 @20:00
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) , Dk. Idris Rashidi, ametangaza uamuzi wa kujitoa kwa shirika hilo katika nia ya kununua mitambo ya kufua umeme ya Dowans.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya kutolewa taarifa alizodai kuwa ni za uongo na zilizojaa utashi wa kisiasa zaidi, dhidi ya utaalamu wa Tanesco na kwamba zimechangia kuvunja nguvu ya mamia ya wafanyakazi wa shirika hilo wanaofanya kazi usiku na mchana kuhakikisha nchi inapata umeme wa uhakika.
Akisoma uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari katika makao makuu ya Tanesco, Dar es Salaam leo, Rashidi alisema kuwa taarifa hizo zilinukuliwa na vyombo vya habari katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, kutoka kwa wanasiasa, wananchi waandamizi aliowaita kwa Kiingereza kuwa ni 'Senior Citizens' na watu wazito wenye majukumu na dhama kubwa.
Aidha, Rashidi ambaye alikataa kuulizwa maswali na kuwataka waandishi kuvuta subira mpaka muda wa maswali na majibu utakapofika bila kutaja siku wala saa, alionya kuwa sasa wananchi ndiyo watakaofanya uamuzi wa mwisho.
"Ni imani yetu kwamba tumeshajieleza na kujenga hoja za kutosha, na umma wa Watanzania utafanya uamuzi wao wakati nchi itakapokuwa imegubikwa na giza, hospitali hazitoi huduma, viwanda havizalishi na wanafunzi vyuoni wakishindwa kusoma," alisema Rashid.
Kwa mujibu wa Rashidi, Desemba 2008 Tanesco iliwasilisha tathmini ya hali halisi ya uzalishaji wa umeme nchini, iliyoainisha mahitaji na matarajio ya uzalishaji kwa muda wa kati na mrefu. Taarifa hiyo iIionyesha kuwa, kwa wakati huo upungufu wa nishati ya umeme ulikuwa megawati 150, na kwamba ukuaji wa mahitaji ya nishati hiyo ni megawati 75 kila mwaka.
Ilijenga hoja alizoziita kuwa ni za kitaalamu na si za kuangalia upepo wa kisiasa, kwamba kutokana na hali ya upungufu uliokuwapo, na ongezeko la mahitaji kwa kila mwaka, ifikapo Desemba 2009, Tanzania itakuwa ikikabiliwa na upungufu wa megawati 225. Alisema tathmini ya hali ya mvua ambayo ndiyo chanzo cha umeme mkubwa kuliko wote na nafuu zaidi, iliyotokana na utabiri wa hali ya hewa, ilionyesha kuwa mvua za mwaka huu hazitalingana na viwango vya kawaida.
Kwa mujibu wa Rashidi, tayari mvua katika mikoa ya Mbeya na Iringa, ambayo ndiyo vyanzo vikuu vya maji ya Bwawa la Mtera, ni za kiwango cha chini na katika maeneo mengine zimesimama. Hoja hiyo ilifafanua kuwa Tanesco ilikuwa na mpango wa mwaka 2009 wa kukamilisha miradi miwili ya kuzalisha umeme ukiwamo wa Kiwira uliokuwa uzalishe megawati 200 na wa Tegeta megawati 45.
Hata hivyo kwa mujibu wa Dk. Rashidi, mradi wa Kiwira uliathirika kwa alichoita kuwa ni malumbano ambayo yamesababisha wawekezaji wakubwa waliotarajiwa kushiriki, kujitoa. Pia mradi wa Tegeta ambao katika mipango ya Tanesco, ulikuwa uanze kuzalisha umeme mwaka huu, umechelewa na sasa utaanza uzalishaji Oktoba 2009.
Kutokana na hoja hizo, Tanesco ilifanya tathmini ya zabuni ya Dowans ya kuuza mitambo yake iliyotangazwa kwenye vyombo vya habari mwaka jana, na kupeleka mapendekezo wizarani ya kununua mitambo hiyo, kwa kuzingatia kuwa haitoshi kupeleka taarifa ya tatizo la uzalishaji wa nishati na mahitaji, bila mapendekezo ya ufumbuzi wa suala hilo.
Mapendekezo hayo yalizingatia pia unafuu na ubora wa mitambo ya Dowans, na yalitolewa kwa tahadhari kwa nia ya kuepusha Tanesco kuingia kwenye mtego usiokwepeka, wa kukodi mitambo hiyo wakati nchi ikiwa kwenye giza katika siku za usoni. Aidha, huku ikijua kuwa ununuzi wa mitambo hiyo si ufumbuzi kamili wa tatizo hilo, Tanesco iliishauri serikali kukaa na wataalamu wa shirika hilo kujadili mpango wa haraka kuhakikisha kunakuwa na uzalishaji wa megawati zisizopungua 200, katika kipindi cha miezi 24 tangu Desemba 2008.
Mjadala huo ulikuwa ulenge katika kuharakisha baadhi ya miradi iliyochelewa kuanza ya Kiwira, Tegeta na Ruhuji ambao ni wa maji megawati 350 na mwingine wa Mnazi Bay wa gesi megawati 300. Mtendaji huyo wa TANESCO alisema miongoni wa 'Senior Citizens' wanaodaiwa kupotosha umma, walipata nafasi ya kukaa na Tanesco kubadilishana mawazo kuhusu hali ya umeme, na mara zote shirika hilo limekuwa likieleza kuwa litakuwa tayari kupokea maelekezo kutoka Kamati za Bunge na Serikali kwa kuwa ndizo taasisi za usimamizi na za uwakilishi wa wananchi.
Alisema, "Hivi karibuni kiongozi mmoja amenukuliwa akisema jitihada hizi ni za kusafisha mafisadi, ni kukiuka taratibu za nchi". Rashid alifafanua kuwa kiongozi huyo hakuwa sahihi kwa kuwa hakuna wakati wowote ambao Tanesco ilisema kwamba ununuzi wa mitambo hiyo hautazingatia taratibu husika za kisheria.
Alisema mitambo hiyo haiuzwi dukani kama mavazi au trekta na kutoa mfano wa mtambo wa Warstsila ambao ulinunuliwa kwa dharura ambapo taratibu zote kuanzia zabuni mpaka kupatikana kwa nishati, ilichukua miezi 18, wakati kwa sasa Tanzania inatakiwa kupata mitambo ya dharura ili Septemba nchi isikumbwe na giza. Uamuzi wa Tanesco kujitoa katika ununuzi wa mitambo hiyo, unatokana na mjadala ulioibuka baina ya wanasiasa juu ya hatua hiyo. Mjadala huo ulitokana na kitendo cha Kamati mbili za Kudumu za Bunge kukinzana katika ushauri juu ya ununuzi huo.
Kamati ya Nishati na Madini ikiongozwa na William Shelukindo (CCM) ilishauri serikali isiruhusu Tanesco kununua mitambo hiyo wakati Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma chini ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe (CHADEMA) iliunga mkono ununuzi. Hali hiyo ilisababisha Spika wa Bunge, Samuel Sitta kuingilia kati na kutoa mwongozo ambao kwa upande wake, alikuwa akiitahadharisha serikali juu ya uamuzi huo wa kununua mitambo inayodaiwa kuwa imeshatumika.
Wakati huo huo, Theopista Nsanzugwanko anaripoti kuwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeisisitiza serikali ifuate na kuheshimu Sheria ya Manunuzi ya Umma kwa kutafuta mitambo mipya kutatua tatizo la umeme nchini. Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Francis Kiwanga alisema nia ya TANESCO na Serikali ya kununua mitambo hiyo ya kampuni binafsi ya Dowans ambayo ni ya mitumba, ni kinyume na sheria na misingi ya utawala bora.
Alisema jitihada hizo zinakiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004 na kutengeneza msingi wa uvunjaji wa sheria. ÒKuhusu malumbano ya Bunge na Serikali kuwa ibara ya 63(2) ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inalipa Bunge madaraka kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri serikali katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa KatibaÓ alisema Kiwanga.