Dowans yamchanganya Mkurugenzi wa Tanesco
2009-03-06 11:25:31
Na Mashaka Mgeta
Kuna mkanganyiko mkubwa ndani ya Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) kutokana na mwenendo wa mambo ulioshuhudiwa jana na kundi la waandishi wa habari.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Idris Rashid, aliitisha mkutano na waandishi hao, lakini baada ya kuwaweka kwa zaidi ya saa tatu na nusu, akauahirisha kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ``anafanya mazungumzo muhimu` na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima.``
Tukio hilo, limekuja siku moja baada ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kuiasa serikali kuhusu nia yake ya kununua mitambo ya Dowans.
Kwa mujibu wa Sitta, ununuzi huo, pamoja na mambo mengine, unaweza kuibua masuala yaliyotokea katika kashfa ya mkataba tata wa Richmond, uliosababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu.
Pia waliokuwa mawaziri, Nazir Karamagi (Nishati na Madini) na Dk. Ibrahim Msabaha (Afrika Mashariki) walijiuzulu kwa kashfa hiyo.
Dk. Rashid aliitisha mkutano huo uliokuwa uanze saa 9:00 alasiri, lakini ilipofika saa 12:30, alitoa taarifa ya kuahirishwa kwake.
Kwa hali hiyo, waandishi wa habari walitumia zaidi saa tatu na nusu kumsubiri bila mafanikio.
Taarifa ya kuahirishwa kwa mkutano huo, ilitolewa na Ofisa Habari wa Tanesco, Ray Naluyaga, kwa niaba ya Dk. Rashid.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka kwa maofisa habari wa Tanesco, Malima, alifika Tanesco kiasi cha robo saa kabla ya kuanza kwa mkutano wa Dk. Rashid na waandishi na kukutana moja kwa moja na Mkurugenzi huyo.
Hata hivyo, mmoja wa maofisa waliokuwa wakiwasilisha taarifa kwa waandishi wa habari, Fatuma Mruma, alifika kwenye chumba cha mkutano saa 10:16 na kusema, baada ya kuwasili Malima, hotuba iliyaondaliwa na Dk. Rashid ilikuwa inafanyiwa marekebisho.
``Wanarekebisha hotuba ya Mkurugenzi, hivyo tunaomba muendelee kusubiri,`` Mruma, aliwaambia waandishi wa habari, kisha kuahidi kwamba kazi hiyo ingekamilika katika muda wa dakika tano.
Hata hivyo, Mruma hakuwa tayari kuelezea sababu za hotuba hiyo kufanyiwa marekebisho.
Ilipofika saa 11:10 waandishi walitoka nje ya ukumbi kama ishara ya kutaka kuondoka, lakini Naluyaga aliwarejesha kwa ahadi kuwa, Dk. Rashid alikuwa na `ujumbe mzito` wa kuelezea.
Tangu wakati huo, waandishi na wapiga picha waliendelea kusimama nje ya Makao Makuu ya Tanesco, hadi ilipofika saa 12:05, Naluyaga alipowataka kuingia ukumbini kwa madai kuwa Dk. Rashid alikuwa anatoka ofisini kwake (kuelekea ukumbini).
Hata hivyo waandishi waligoma kurejea ukumbini hadi Mkurugenzi huyo atakapoingia.
``Hii ni janja tu, pengine wanataka tuingie ndani ili watoke na sisi tukose picha za kuwapiga,`` alisikika mwandishi mmoja akisema.
Ilipofika saa 12:35 Naluyage aliwajulisha waandishi kuwa Dk. Rashid ameahirisha mkutano huo.
Hata hivyo, taarifa za ndani kutoka Tanesco zilidaiwa kuwepo mvutano kati ya Dk Rashid na Malima, kuhusu hoja iliyokusudiwa kutolewa na Mkurugenzi huyo.
Ingawa hakuweza kuthibitisha ama kukanusha taarifa hiyo, Naluyaga alisema, ``kwa hali ilivyo inaonekana kuna jambo kubwa huko juu, ingawa haimaanishi kuwa ni mvutano maana sote tupo huku chini.``
Ingawa hoja iliyokusudiwa kuwasilishwa jana na Dk. Rashid haikujulikana, kuna taarifa kuwa huenda ililenga kuzungumzia sakata la ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme inayomilikiwa na kampuni ya Dowans.
Hii ni mara ya pili Dk. Rashid anakuwa katika hali ya mvutano katika uongozi wake. Mwaka juzi aliandika barua ya kujiuzulu baada ya kuto fautiana na bodi ya shirika hilo kutokana na kukatiwa umeme kwa kiwanda cha sementi Tanga.
Alibadili uamuzi huo.
SOURCE: Nipashe