Zizini TV: Kwenye zizi la ng'ombe, Chui ndiye Mhubiri mkubwa wa "Amani na Utulivu"?

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Joined
Mar 10, 2006
Posts
34,092
Reaction score
43,265

Na. M. M. Mwanakijiji

Sijui ni 'genius' gani huyo ambaye ameanzisha hili la kuwa "tunataka amani kwanza". Kwa wiki hasa baada ya Oktoba 29 kumekuwa na jitihada kubwa ya kujaribu kugeuza mambo kinyumenyume. Sasa tunaambiwa "amani kwanza" ndio mambo ya "haki" yaje baadaye. Hili sijui limeanzaje na limeanzishwaje hadi kufikia watu wenye akili timamu wakaanza kulikumbatia.

Ninachoogopa ni kuwa tunatakiwa tuamini kabisa kuwa "utulivu, na kutokuwepo na vurugu" ndiyo "amani" yenyewe. Kwamba, wenzetu hawa wanatafsiri amani ni "hali ya utulivu, bila ugomvi, mabishano, mapigano, au kujibishana na watawala". Kwa wenzetu hawa "amani" kwao ni ile hali ya kuwa na utulivu. Yaani, Ukiwakuta watu wawili wanagombana ukiwaamulia basi umeleta "amani". Yaani, kama hawapigani basi "kuna utulivu". Kwa muda mrefu Watanzania tumeaminishwa kuwa nchi yetu ni "nchi ya amani" kwa maana ya kwamba hakuna "ugomvi, mapigano, vurugu n.k". Na kwa sababu hiyo tumeaminishwa kuwa lengo letu kama taifa ni kuwa katika hali ya utulivu.

Kwenye zizi la ng'ombe chui anaweza kuwa mhubiri mkubwa wa 'amani na utulivu'? Yaani, ukimuuliza chui atakuambia kwa kirefu ni kwanini ni muhimu kwa ng'ombe, mbuzi, na kondoo zizini kuwa katika hali ya utulivu ili kudumisha "umoja, na mshikamano" wa wanyama wote zizini. Kwenye mahojiano na Televisheni ya "Zizini TV" Bw. Chui alipoulizwa kwanini walitumia nguvu kubwa kuua wanyama zizini hasa walipoleta vurugu zizini Bw. Chui alisema kuwa hakuelewa kwanini wanyama wanadai haki zizini wakati wanapewa vyakula kila siku na maji ya kunywa na kuwa vurugu zizini ni kukosa shukrani!

Chui ana kila sababu ya msingi ya kutaka utulivu zizini. Bahati mbaya katika wanyama walioko zizini kuna wengine wanapenda kuwe na utulivu kwa sababu wanaamini wakifanya hivyo chui hatawageuza msosi wa jioni! Wale wenye kufurahia utawala wa chui wanaamini kabisa na watajaribu kuwashawishi wengine waamini kuwa ni bora kuwa na "amani" kuliko kuwa na 'haki'.

Sasa haki kwa maneno ya kawaida ni "kile ambacho mtu anastahili bila kudhulumiwa". Yaani, haki ni kila mtu anachodai kuwa ni mali yake iwe ni hadhi, maisha, ujira, utu n.k Vitu ambavyo mtu ni vya kwake na asidhulumiwe hivyo ndiyo haki yake. Msemo wa "mnyonge mnyongeni haki yake mpeni" una maana kubwa sana. Kwamba, hata kama mtu ni mnyonge lakini anachake anachostahili basi mpeni hata kama mmeshaamua kumnyonga!

Hakuna humu duniani watu wanaoitwa "wapigania amani" Dunia imetetewa na "wapigania uhuru" na 'wapigania haki". Hata hivyo wapo watu wanaosimamia "amani' lakini wanafanya hivyo kwa kupigania 'uhuru na haki' na si vinginevyo. Msemo wa wahenga kuwa "amani haiji ila kwa ncha ya upanga" una maana ya kuwa wakati mwingine ili kuwe na amani ni lazima dhulma iondolewe hata kama ni kwa vita. Ndiyo maana Vita ya Pili ya Dunia ilipiganwa ili kuleta amani Ulaya kwa kuondoa dhulma ya Manazi!

Kupinga dhulma na kutaka haki ni miongoni mwa matakwa makubwa ya dini zetu hizi. Ni kwa sababu hiyo tunaposikia watu wenye imani wanapuuzia "haki" na wanaishusha haki chini ati kwa kisingizio cha "amani" ni lazima tuwakatalie. Amani ni zao la haki na si vinginevyo. Unaweza ukawa na "amani" lakini kukawa na dhulma katika jamii lakini watu wanaimba "amani amani". Matukio ya hivi karibuni yanatudokeza kuwa hata sasa watu wanalalamikia 'dhulma" japo kunaonekana kuna "amani na utulivu".

Tusikubali kudanganyika kwa kulazimishwa kutulia ili tutawaliwe kwa kwa amani. Tukumbuke kuwa wakoloni walitaka kuwe na "amani na utulivu" katika makoloni yao ili watawale wapendavyo. Walipotokea watu kama kina Mandela, Nyerere, na wengine walionekana ni 'wavuruga amani' na walishtakiwa kwa kufanya "uchochezi'. Tanzania ya sasa chini ya CCM hii hii tumeanza kuona geresha hii kubwa ikirudiwa; tuwaache watawale wapendavyo ili tuwe na "amani'. Tusiwapinge, tusiwakatalie, na tusiwaonyeshee mikono. Na jambo kubwa ambalo hawataki tulifanye ni kuwafanya wengine wawachukie na wawakatae.

Lakini kama nilivyosema mbuzi, kondoo na ng'ombe ambao kila siku wanaona wenzao wanaenda kutolewa msosi, wanakamatwa, wanaenda kuchinjwa wana haki ya kugoma, kuhoji, na kupinga? Au kwa vile zizini kunaakiwa kuwe na amani wakubali tu wakae kimya ili kuwe na amani? Au ndiyo yale yaliyoandikwa kwenye kitabu cha "Animal Farm"?

Haki ndiyo msingi wa amani na si kinyume chake. Hakuna AMANI BILA HAKI. Hakuna Amani mahali penye "dhulma".

Kama Quran inavyosema katika Sura 4:135 Enyi mlio amini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu (haki), mtowao ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ijapo kuwa ni juu ya nafsi zenu, au wazazi wawili na jamaa zenu. Akiwa tajiri au masikini Mwenyezi Mungu anawastahikia zaidi. Basi msifuate matamanio, mkaacha kufanya uadilifu(haki). Na mkiupotoa au mkajitenga nao basi Mwenyezi Mungu anajua vyema mnayo yatenda

Ni wito huo tunaona kwenye Isaya 1:17 jifunzeni kutenda mema! Tafuteni haki, watieni moyo walioonewa.
Teteeni shauri la yatima, wateteeni wajane.

Amani haiwezi kusimama penye dhulma; na dhulma ni kukosekana kwa haki. Lakini tukimuuliza chui atatuambia "ni lazima kuwe na amani kwanza kabla sijawapa haki yenu". Na wapo watakaokubali na kukumbatia hili. Wengine bado watakataa.
 
Laiti yule mama angemsikiliza polepole japo kidogo tu na akafanya angalau kwa sehemu aliyoshauriwa Leo angekuwa anakunywa juisi/wine kwenye kisiwa chochote Cha starehe hapa duniani yeye na wajukuu zake. Ila sasa yaliyotokea sijui kama amekaa moyo ukiwa na amani kabisa kama ilivyo kuwa kabla ya there 29 October
 
Watu laghai huwa wanafikiri wao pekee ndio waujuao ukweli; wakati hayo wanayotaka watu wayakubali kuwa ni ukweli ndio ulaghai wenyewe.

Kutokana na ufinyo wa upeo na kukosa elimu na akili za uelewa, ni vigumu sana kujuwa kama kweli Samia anajuwa uzito wa mambo mengi ambayo hutaka watu wayachukulie kuwa ni ukweli unaotoka kwa kiongozi wa ngazi ya juu kabisa.

Nimetafakari sana na kutazama historia ya huyu mwanamke tokea ashike madaraka, sioni jambo hata moja ambalo alilizungumzia kwa wananchi na kutoa ahadi juu yake; na ahadi hiyo ikatimizwa kama ilivyo ahidiwa.

Huyu ni mtu ambaye naona maisha yake yote kaishi kwa uongo uongo tu!
 
Wahuni wote wanaona amani ni mhm bila kujali unapata haki.

Ndiyo maana wanafanya ufisadi na kutaka wasihojiwe ili muwe na amani.

Wanaiba kura na kuunda safu zao za uongozi usiokubalika na wananchi, wanataka mtulie kwa amani bila kujali mmepoteza haki yenu.

Ni wapumbavu kweli kweli. Mimi siwezi kuwa sehemu ya wapumbavu.
 
Amani haiwezi kusimama penye dhulma; na dhulma ni kukosekana kwa haki.
 
Amani haiwezi kusimama penye dhulma; na dhulma ni kukosekana kwa haki. Lakini tukimuuliza chui atatuambia "ni lazima kuwe na amani kwanza kabla sijawapa haki yenu". Na wapo watakaokubali na kukumbatia hili. Wengine bado watakataa.
Inatulazimu waTanzania tutafute njia ya kueleza na kutetea (justify anayoyafanya Samia Suluhu Hassan na wengine wote wanaoungana naye katika kuhimiza AMANI bila ya kuwepo HAKI.

Hawa wote wanaamini AMANI ni kutokuwepo na kuhoji hata wakati HAKI inapokonywa. Na hata kama kuhoji kutakuwepo, kuwe katika njia inayowapendeza hao wanaolinda AMANI bila ya kuwepo HAKI.

Unayedai HAKI ni lazima utumie lugha wanayoitaka wao; na kama wakiichukulia kuwa ni lugha isiyo ya STAHA wewe unayedai haki unatafuta kuvuruga AMANI wanayoilinda wao kwa njia zao za ukandamizi; ikiwa ni pamoja na kuondoa uhai wa huyo anayedai HAKI.

Na unapodai HAKI, hutakiwi kuzua TAHARUKI kwa namna unavyoomba hiyo haki Hapa ni lazima uwe muungwana kwa kudai HAKI kimya kimya, wengine wote wasijue kuwa unadai HAKI toka kwa watawala. Hata kama unatumia lugha ya STAHA, lakini habari yako ukaiwasilsha kwa uwazi; hilo ni kuzua TAHARUKI katika jamii

Sasa, kama unadai HAKI kimya kimya ili usianzishe taharuki, maana yake ni kuwa hao wanaolinda AMANI ndio watakaoamua kutoa HAKI au kutotoa HAKI. Uamuzi wa wao; wewe mtafuta HAKI huna nafasi ya kujitetea upate HAKI; ndiyo maana ya siri.


Mara nyingi, msisitizo umekuwa ni MAZUNGUMZO, kama unatafuta HAHI. Mazungumzo hayo wao walinda AMANI ndio wataamua mazunguzo yawe ya mwelekeo gani na kwa wakati gani. Kwa hiyo wao ndio watakaoamua hatma ya mazungumzo (Rejea Mazungumzo ya Maridhiano CHADEMA Mbowe, na CCM, Samia). Hiyo ndiyo maana kuu ya kutaka na kuhimiza kila mara MAZUNGUMZO; huku wakitunza AMANI kwa mitutu ya Bunduki.

Kuna mambo mengi ya kumweleza Samia na kundi linalosisitizia AMANI,; hususan BAKWATA, bila ya uwepo wa HAKI.

Sasa nadharia yangu ni kuwa, baada ya kuyapima yoote haya ni kuwa bila sjhaka kuna chimbuko la huu uamini wa kuwa na AMANI bila ya uwepo wa HAHI.
Nadharia yangu ni katika taratibu za kitamaduni/kistaarabu ambao pengine unaendana pia hadi katika mafundisho ya kidini. binafsi sina ufahamu wowote wa dini ya kiislam inafundisha nini katika maswala kama haya; lakini pia haiwezi ikawa ni kwa bahati tu, Samia Suluhu Hassan, akawa anahimiza uwepo wa AMANI isiyo ambatana na HAKI; na lugha hiyo hiyo ikawa ndiyo sahihi kwa sehemu kubwa ya BAKWATA na waumini wengine wa dini hiyo.
Ni lazima patakuwepo na muunganiko katika tamaduni au mafundisho ya dini hiyo yanayohimiza AMANI, bila kujali uwepo wa HAKI.

Ninapoandika kirefu hivi huwa sitaki kurudi nyuma na kusoma nilicho andika. Kama kuna makosa, basi yachukulie hivyo hivyo. La muhimu ni wasilisho la hoja iliyonuiwa kuwasilishwa. Kama hili nalo ni tatizo, basi nitarudi ninyooshe vizuri baadae nikitakiwa kufanya hivyo.
 
Hii ndiyo maana ya AMANI inayoimbwa na hao unaowaita "wahuni". Hawa siyo "wahuni", hawa ni watu 'serious' kabisa wanaojuwa wanachokifanya.
Ni watawala wasiotaka kuhojiwa na yeyote.
Kudai HAKI ni kupunguza hadhi yao ya kutawala.
 
Kimbesa uje upate shule hapa
 
Hawa mbwa wa MCC walichofanya hakina tofauti na mama wa kambo kumpiga na kumuumiza vibaya sana mtoto mdogo asiye na ubavu hata wa kurudisha kibao kisa tu alilalamika juu ya kusikia njaa na kiu ilihali anamuona mama wake wa kambo akijichana kwa chips, kuku na soda pamoja na marafiki zake. Kitendo hicho cha kikatili kimeshuhudiwa na ulimwengu mzima.

Kimsingi mtoto ana haki ya kulishwa na kunyweshwa ila badala ya kuulizia juu ya hio stahiki ameambulia kipigo cha mbwa koko na kuitwa hana adabu wala utii kwa wakubwa.

Mbaya zaidi mama wa kambo anajaribu kutengeneza maudhui kuwa mtoto hakuwa sahihi kusema ana njaa na kiu ila alitakiwa astahimili tu kwani kwa kukaa kimya asingepigwa. Hapo ndio tulipofikia kama taifa halafu mama wa kambo bado anakaza ubongo na kutaka kulifanya jambo hilo ni dogo.
 
Ukimsikia mtu au kiongozi anahubiri amani, mtu huyo ana matatizo makubwa katika ' faculty' ya kufikiri
Haki ikitendwa amani inajihubiri yenyewe, haihitaji microphone au kiongozi hata dakika moja

Natamani wangeiona hiyo picha katika bandiko#1.
Kiongozi anayezungumzia amani badala ya haki ni muflisi wa fikra na hoja. Ni kasuku tu.
 
Hata uisalam umekuwa ukijitanabaishi ni dini ya haki. Ila acha wajichimbie kaburi.
 
Amani haiwezi kusimama penye dhulma; na dhulma ni kukosekana kwa haki. Lakini tukimuuliza atatuambia "ni lazima kuwe na amani kwanza kabla sijawapa haki yenu". Na wapo watakaokubali na kukumbatia hili. Wengine bado watakataa.
Kwanza naunga mkono hoja, pili yule mtu wetu ni muumini wa haki kwa mawazo, maneno na matendo, tatizo sio yeye bali wasaidizi wake wamemdanganya, akadanganyika.
Mwanzo alianza vizuri Asante Rais Samia kwa kuwasisitiza watendaji wa vyombo vya haki kuwa haki sio hisani, bali ni stahiki. Watende haki, tubadili Katiba kurudisha haki

Wakupongeza, tukampongeza Asante Mungu kwa Rais Samia: Ni Msema Kweli na Mtenda Kweli, Ni Msema Haki na Mtenda Haki. Je, Ataruhusu Ubatili Huu Kuendelea Ndani ya Katiba Yetu?

Tukaendelea kufagilia Haki Huinua Taifa! Rais Samia kwa Kauli na Matendo ameonesha ni mtu wa Haki. Akitekeleza hili kama alivyosema, atabarikiwa, Tanzania itabarikiwa

Rais Samia ana nia njema Watanzania wapate haki, ila Watanzania hawajui Haki! Je, Tumsaidie kuelimisha umma Katiba, Sheria na Haki au? watu tukajitolea kusaidia.

Mara mambo yakaanza kubadilika, tukashauri ,Ombi kwa Rais Samia, tunakushukuru kwa mahubiri mazuri kuhusu haki, tunakuomba utende unachohubiri yasibaki kuwa maneno tuu lakini vitendo ni tofauti

Ndipo akadanganywa kuhusu uhaini Uhaini My God!. Kuna Uwezekano Anadanganywa na Kadanganyika? I Don't Believe This!. Sitatizwi na Uongo Wao, Natatizwa na The Motives Behind Such Lies!

Tukasaidia kuelimisha PreGE2025 - Wazalendo Wapenda Haki, Msiwe na Wasiwasi, Uhaini ni Matendo na Mipango Mkakati wa Kuutenda, Sio Maneno!, Maneno ni Sedition tuu na Sio Treason!

Tumsamehe bure, sio yeye, ni wasaidizi wake Inawezekana ni Kiburi na Jeuri or Real Busy? Wasaidizi wake hawajamwambia ukweli wa ubatili wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi?,Tufanye nini kupata Haki?

Ile October 29, wakamdanganya tena kuwa Gen Zii wanakuja kukuondoa Ikulu, mtoa amri akatoa amri ya zitumike za moto!. Ili Haki Itendeke, Sio Tuu Itendeke, Bali ni Lazima Ionekane Imetendeka!, Kama Tumewashitaki Waandamanaji, Pia Tuwashitaki na Wauaji!

Haki Huinua Taifa. Kilichotokea ni matokeo na sio chanzo. Kama matokeo yanapandishwa kizimbani na chanzo pia kipandishwe!

P
 
Watu wangu ehee.....
Wewe mzee acha shobo, lea watoto wako ambao ni kama unalea wajukuu kwa umri wako
Hilo jimbo ulikokuwa litakuwa ni redneck hasa mpaka ilichukua muda sana kujipata kwa vikazi vya deiwaka
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…