Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 2,813
- 11,991
Mbarawa amesema treni hiyo kwa kawaida itakuwa na mwendo kasi wa Kilometa 160 kwa Saa moja huku akieleza kuwa katika hatua za majaribio wanatumia mwendo wa chini ambao unazingatia usalama kama miongozo mbalimbali ya Kidunia inavyoelekeza kuhusu majaribio ya treni.
Akizungumzia suala hilo leo Machi 18, 2024 amesema baada ya majaribio ya mwisho yaliyofanyika wiki kadhaa zilizopita kuliibuka taarifa zisizo za kweli kwamba treni hiyo haina uwezo wa kutembea kwa mwendokasi ulioelezwa awali.
"Hatuwezi kufikia spidi hiyo 160 wakati tupo kwenye majaribio, majaribio kitu cha kwanza kabisa ni usalama, kwa vile hatuwezi kwenda spidi hiyo kwahiyo ni baada ya kumaliza majaribio yote tutaenda na spidi kati ya 150 km hadi 160 kwa saa," amesema Mbarawa.
"Hatuwezi kufikia spidi hiyo 160 wakati tupo bado kwenye majaribio, kwenye majaribio kitu cha kwanza kabisa ni usalama. Kwa vile hatuwezi kwenda spidi hiyo kwahiyo ni baada ya kumaliza majaribio yote tutaenda na spidi kati ya 150 km hadi 160 kwa saa," amesema Prof. Mbarawa.
Ameongeza "Kulikuwa na maneno mengi watu wanasema mbona aiendi spidi kubwa kama tunavyoona nje, naomba mnielewe kuna tofauti baina ya 'high speed train' na treni ya kawaida, 'high speed train' kama iliyopo Korea, China na Japan zile zinaenda spidi kati ya 200 na kuendelea."
Akiendelea kufafanua suala hilo, amesema treni zote Duniani zinazokwenda chini ya Kilometa 200 kwa Saa ni treni za kawaida na kwamba zile zinazoenda juu ya mwendo huo kwa saa ni treni za Mwendokasi wa juu zaidi (high speed train), ambapo amedai pia gharama za treni hizo ni utofautiana.
Ambapo ametolea mfano kwa kusema "Kwa mfano kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro cha ukubwa wa kilometa 300 Serikali imetumia dola za kimarekani Bilioni 1.2, ambapo gharama hizo kama ingekuwa treni ya 'high speed train' zingezidi zaidi."
Treini hiyo imeendelea na mwendelezo wa majaribio kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambapo imeshuhudiwa mabehewa yakiongezwa kwenye safari hiyo kutoka mabehewa manne kwenye safari ya mwisho hadi mabehewa 14 hali ambayo imetajwa kuwa itakuwa endelevu kwa kuongeza mabehewa zaidi kufikia kipindi rasmi ambacho safari hizo zitaanza.
Safari hiyo imeongozwa na Prof. Mbarawa akiambatana na wadau wengine akiwemo Mkurugenzi wa Bodi ya TRC, Mkurugenzi Mtendaji wa TRC, baadhi ya Madiwani kutoka Mkoa wa Dar es Salaam huku wakipokelewa na mwenyeji wao Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na watendaji mbalimbali wa Serikali.
Akizungumzia majaribio hayo Mbarawa amesema "Leo ni mwendelezo wa majaribio tulioanza muda murefu, kwanza tulifanya majaribio ya kichwa chenyewe, baadaye tukaunga mabehewa manne mpaka leo mabehewa 14, hayo yote tunayafanya kuhakikisha kwamba vichwa hivi vya treni vina uwezo wa kupeba mzigo kama ilivyokusudiwa. Huko mbeleni tutaenda kuongeza mabehewa zaidi."
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja kadogosa amesema kuwa zoezi la majaribio litakuwa endelevu na kwamba kuja kufikia mwishoni mwa Mwezi Aprili 2024 watakuwa wamefanya majaribio ya kwenda Mkoani Dodoma huku ikitajwa kuwa safari rasmi za treni hiyo zitaanza Mwezi Julai 2024.
Ameeleza kuwa mradi wa SGR unaendelea kwenye maeneo mengine kama ambavyo imekuwa ikibaishwa na Serikali ikiwemo vipande ambavyo Serikali tayari imeingia mikataba na wakandarasi.
Itakumbukwa kupitia mitandao ya kijamii kulikuwepo na mijadala mara baada ya safari ya awali iliyofanyika wiki kadhaa zilizopita, ambapo miongoni mwa mijadala hiyo ni kasi ya treni hiyo kudaiwa kuwa ndogo tofauti na ambavyo ilikuwa ikizungumzwa na viongozi mbalimbali, ambapo kati ya taarifa zilizoripotiwa ni kuwa treini hiyo ilitumia zaidi ya masaa mawili na nusu kufika Morogoro ikitokea Dar.