Stories of Change - 2023 Competition
Jun 25, 2023
23
21
Waraka kwa mtoto wa kike mwenzangu,
Tambua kuwa hapo Mwanzo Bwana Mungu hakuweka uadui kati ya mwanamume na nyoka yaani shetani, hivyo kinachoendelea kati yao Bwana ndiye anajua. Kwani wapo wanaume ambao ni marafiki wa Mungu lakini pia wapo wanaume ambao ni marafiki wa nyoka yaani shetani. (Mwanzo 3:15)

Hapo mwanzo Mungu aliweka uadui kati ya mwanamke na nyoka shetani hivyo adui wa shetani ni rafiki wa Mungu.

Tangu Mungu ameweka uadui kati ya mwanamke na shetani tafsiri yake ni kuwa mwanamke ni rafiki wa Mungu. (Mwanzo 3:15)

Kwa kulijua hili shetani hutumia wimbi la baadhi ya wanaume kuharibu adui zake wanawake ambao ni marafiki wa Mungu. Ndiyo maana katika ulimwengu leo hii video chafu za ngono zinapovuja walioshiriki tendo ni wawili lakini anayeonekana na kuchafuliwa ni mwanamke, mwanamume anakuwa nyuma au pembeni ya kamera na mbele ya kamera 'sterling' ni mwanamke.

Hii ndiyo sababu leo hii wazinzi ni wanawake kwa wanaume lakini wasioolewa na kuitwa makahaba ni wanawake, mwanaume hata awe mzinzi namna gani akitaka kuoa hata akiamka usingizini anaoa na anajitapa kabisa kumwambia mwanamke aliyelala naye jana 'atakuoa nani?' Kisa uzinzi na aliyezini nae ni yeye.

Hii ndiyo sababu baadhi ya wanaume ndiyo chanzo cha wanawake kukosa heshima kwenye jamii kisha wanaume huwageuka na kuanza kuwaponda.

Hii ndiyo sababu baadhi ya wanaume huwafanya wanawake chombo cha starehe na dampo la kuweka uchafu wa kila namna kwa kuwageuza wanawake bajaji; akishuka ya Kinondoni anapanda ya Ubungo, akishuka ya Ubungo anapanda ya kwenda Sinza akishuka ya Sinza anapanda ya kurudi Kinondoni.

Hii ndiyo sababu hadhi ya wanawake uharibiwa na baadhi ya wanaume ambao hawataki kuoa bali wanataka 'One Night' na 'Just For Fun' huku akilini akiwaza 'who's next'.

Mpendwa mtoto wa kike mwenzangu, siyo kila mwanamume anayekuja kwako kwa maneno ya kutaka kukuoa na mbwembwe za kila rangi ndiye mumeo huyo; wengine huja kukuharibu ili kukukosesha mumeo mzuri Mungu aliyekuandalia, kwa njia yoyote ile.

Ni kweli makosa hutokea, lakini hatupo hapa kuyahesabu makosa hayo, bali tunatakiwa tuyafute, tuyasahau, tuwasamehe na tuwasahau waliosababisha jamii ione kuwa wanawake ni viumbe dhaifu, visivyo na heshima, visivyofaa na vinavyoweza kupelekeshwa namna jamii itakavyo.

Bali kuanzia sasa watoto wa kike na wanawake tunatakiwa tufahamu kuwa sisi ni wa thamani kubwa haijalishi tumepitia nini, haijalishi wamesema nini kuhusu sisi, haijalishi jamii imesema nini kuhusu sisi, haijalishi wamegeuza watoto wa kike na wanawake kuwa bajaji au malori ya mizigo; wamepanda na kushuka, wamepandisha mizigo yao na kushusha watakavyo, haijalishi wame 'shoot' video ngapi za 'connection' ili kudhalilisha wanawake, haijalishi wamesambaza na bado wana mipango ya kuendelea kusambaza video chafu ngapi za wanawake mitandaoni, haijalishi wametukana wanawake kwa matusi mangapi ya kila rangi, haijalishi wametumia wanawake wachache kusaliti wanawake wenzao ili waangamie, haijalishi ni uongo gani wametumia kutulaghai, haijalishi! Nasema haijalishi!

Mwanamke ni mwenye thamani kubwa kwani fedha, noti ya shilingi elfu kumi (10,000/= TZS) hata iangushwe pale Sokoni Kariakoo wakapita maelfu ya watu juu yake wakaikanyaga itabaki kuwa shilingi elfu kumi (10,000/= TZS) na mtu mmoja ataiona ataiokota na kuisafisha kisha kuiweka kwenye 'wallet' yake na bado ikawa na THAMANI ileile ya shilingi elfu kumi, isiyopungua THAMANI yake eti iwe elfu moja au mia tano haiwezekani.

Mpendwa mtoto wa kike mwenzangu, mwanamume pekee anayetakiwa kufunguliwa mlango wa moyo kuanzia sasa kigezo pekee ni Upendo; tena upendo wa kweli na vitendo siyo maneno. Kwani hizi I love you, I love you nyingi vitendo 0 ndizo zilimponza binti mzuri Tamari ambaye kwa ushawishi wa Amnoni aliamua kushusha nguo yake ya ndani kwa ajili Amnoni akidhani ndiye mwanamume sahihi kwake kumbe siye mwishowe Tamari aliishia kubaki na majeraha makubwa na uchungu moyoni. (2 Samweli 13:1-19)

SIFA KUU ZA MWANAMUME MWENYE UPENDO WA KWELI

Ni msikivu, humpa na humfanyia chochote chema anachokitaka mwanamke wake kilicho ndani ya uwezo wake;
kama upendo wa Mfalme Ahasuero kwa Malkia Esther Abihaili.

Hapo awali, Mfalme Ahasuero alimwoa Vashti lakini kwa sababu Mungu kwa neema yake alimwandalia Mfalme Ahasuero mke mwema aitwaye Esther Abihaili, Vashti alijikuta anaibomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe na taji ya Umalkia akavalishwa Malkia Esther Abihaili.

Kwa kuwa Malkia Esther alipata neema ya kuandaliwa na Bwana kwa ajili ya kuwa mke wa Mfalme Ahasuero ili aingie kwenye Ufalme na kuwaokoa Wayahudi kutoka mikononi mwa adui yao Hamani; Malkia Esther akapendwa na Mfalme kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pa Mfalme kuliko mabikra wote hata akavikwa taji na kufanywa kuwa Malkia badala ya Vashti.

Kwa upendp wa Mfalme Ahasuero kwa Malkia Esther, kila alichokitaka Malkia Esther kutoka kwa Mfalme alipata Kibali cha kufanyiwa na kukubaliwa kwa sababu ulikuwa ni upendo wa kweli. (Esther 1:10-12) (Esther 2:1-4) (Esther 2:7, 15-18) (Esther 5:3-8)

Hupenda kuwa pekee na mwanamke wake muda mwingi kwa ajili ya kupeana furaha ya kweli, hata akijitahidi kuficha penzi lao lazima watu watajua; kama upendo wa Isaka kwa Rebeka.

Isaka alikuwa akiishi katika nchi ya Wafilisti. Watu wale wakamwona Rebeka, wakavutiwa na uzuri wake, hata wakamtamani. Wakamuuliza Isaka, ‘Ee bwana Ee, huyu msichana tunayemwona katika boma lako na wakati mwingine unaambatana naye, ni nani kwako? Isaka akaogopa kusema ni mke wake, kwa maana wangeweza kumwua ili wamchukue Rebeka, kwa jinsi alivyokuwa mzuri wa kuvutia, hivyo Isaka aliwajibu; ‘ni dada yangu’ nao wafilisti wakamwacha. Lakini kumbe wale watu walitumwa na Mfalme Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, ili kupeleleza na kujua uhusiano wao, kwasababu Mfalme alivutiwa sana na uzuri wa Rebeka hivyo akataka kumuoa.

"Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anacheza-cheza na Rebeka mkewe. Abimeleki akamwita Isaka, akasema, yakini huyu ni mkeo, mbona ulisema, ni ndugu yangu huyu? Isaka akamwambia, Kwa sababu nalisema, Nisife kwa ajili yake. Abimeleki akasema, ni nini hii uliyotutendea? Labda mtu mmojawapo angalilala na mkeo bila kufikiri, nawe ungalitutia hatiani. Basi Abimeleki akawaamuru watu wote, akisema, Amgusaye mtu huyu au mkewe lazima atauawa." (Mwanzo 26:8-11)

Yuko tayari kujitoa nafsi yake hata kufa; kwa ajili ya kumsafisha mkewe hasa pale anapochafuliwa au kumlinda na kumwokoa mkewe hasa pale anapokuwa hatarini lakini pia kumlisha na kumhudumia mkewe sawasawa na anavyojihudumia yeye mwenyewe; kama upendo wa Bwana Yesu Kristo kwa Kanisa.

"Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa." (Waefeso 5:25-29)

HITIMISHO

Upendo ni nini?

Upendo ni kutoa (Yohana 3:16) na kujitoa (Waefeso 5:25) kwa matendo na kweli wala si kwa maneno (1 Yohana 3:16-18); kwa ajili ya kuwaletea wengine baraka badala ya laana, utajiri badala ya umasikini, furaha badala ya huzuni, uhuru badala ya utumwa, raha badala ya karaha, vicheko badala ya vilio, kila lililo jema badala ya mabaya ya kila namna. (Isaya 61:1-7) (2 Wakorintho 9:8-15)

Upendo ndiyo amri kuu na ya pekee aliyotuachia Bwana Yesu Kristo kwani torati yote imetimilika katika upendo; yaani kumpenda Bwana Mungu wetu kwa kila kitu chetu na kupendana sisi kwa sisi kama kila mmoja anavyoipenda nafsi yake. (Yohana Mtakatifu 13:34) (Wagalatia 5:13-14) (Mathayo 22:37-40) (Marko 12:30-33)

Hii yote ni kwa sababu Mungu ni upendo hivyo tunapopendana Mungu hukaa ndani yetu nasi ndani yake. (1 Yohana 4:7-13)

Upendo una nguvu kama mauti (Wimbo Ulio Bora 8:6-7); hivyo mwanaume mwenye upendo wa kweli kwa mwanamke anao uwezo wa kumbadili Mwanamke hata kama ni kahaba akawa mke mwema. (Mithali 31:10-31), kwani;

Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauhusudu; yaani haumwonei mtu husda na wivu wa chuki, upendo hautakabari, upendo haujivuni, upendo haukosi kuwa na adabu, upendo hautafuti mambo yake, upendo hauoni uchungu, upendo hauhesabu mabaya, upendo haufurahii udhalimu bali hufurahi pamoja na kweli, upendo huvumilia yote, upendo huamini yote, upendo hutumaini yote, upendo hustahimili yote na neno la upendo lina nguvu ya kufanya mapinduzi na kuvunja sheria na taratibu zote; hata kupelekea kubadili na kuangusha utumwa na kupelekeshwa kwa kila namna kuwa Utawala Bora na Uwajibikaji wa kila mwanadamu ili kutimiza kusudi la Mungu hapa duniani. (1 Wakorintho 13:1-8)

Mwanamume mwenye upendo hawezi kuwa chanzo cha mwanamke kudhalilika iwe ni kwa 'video za connection' au kwa namna yoyote ile, bali atahakikisha ana - 'clear' kwa gharama yoyote ile kila kitu chenye kumchafua mwanamke wake. (Waefeso 5:25-26)

Wanaume jifunzeni upendo kutoka kwa Bwana Yesu Kristo ili na sisi tuwatii kama Kanisa limtiivyo Bwana Yesu Kristo. (Waefeso 5:22-24)
 
Back
Top Bottom